Maulid Dilunga, mwanaspoti ambaye alikuwa gumzo enzi zake kiasi cha kuwa akina Etoo wa nyakati hizo amefariki dunia na kuzikwa nyumbani kwao...
Maulid Dilunga, mwanaspoti ambaye alikuwa gumzo enzi zake kiasi cha kuwa akina Etoo wa nyakati hizo amefariki dunia na kuzikwa nyumbani kwao Kisarawe. Makala haya yanamzungumzia mwanasoka huyu ambaye ama hakika hatasahaulika katika timu ya Afrika na Tanzania.
JINA Maulid Dilunga si geni kwa wapenda soka wa hapa nchini na hata nje ya Tanzania kutokana na umahiri aliokuwa nao mchezaji huyo katika kusakata kabumbu katika miaka ya 1960 na 1970.
Kutokana na umahiri huo, Dilunga alipachikwa majina mbalimbali, likiwamo la ‘dangerous man.’ Hata hivyo, mwanasoka huyo wa zamani hayupo nasi tena, ingawa kutokana na mchango wake katika maendeleo ya soka nchini atabaki kuwa simulizi vizazi na vizazi.
Mchezaji huyo wa zamani wa timu za Yanga, Simba na timu ya taifa (Taifa Stars), alifariki dunia juzi usiku nyumbani kwake Vingunguti, Dar es Salaam na kuzikwa Juni 11,2008 kijijini kwake Kisarawe, mkoani Pwani.
Waliomwona enzi zake na wachezaji wenzake wa zamani wanasema Dilunga alikuwa mchezaji aliyekuwa na kipaji cha hali ya juu aliyetumia akili, madoido na majonjo katika kumiliki mpira. Wanasema uwezo wake wa kufunga mabao akiwa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars, ulikuwa wa hali ya juu.
Dilunga alizichezea kwa muda mrefu timu za Yanga, Simba, Pan African, Cargo na Taifa Stars aliyoichezea kwa zaidi ya miaka 10, tangu mwaka 1960 hadi 1974.
Mwaka 1969, Dilunga aliiongoza Yanga kufikia hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa akiwa na wachezaji wenzake kama Kitwana Manara, Awadh Gessan na Salehe Zimbwe.
Yanga ilitolewa na Asante Kotoko ya Ghana kwa kurusha shilingi baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1, mjini Accra na kufungana mabao 2-2 jijini Dar es Salaam.
Mwaka 1972, Dilunga alikuwa miongoni mwa wachezaji wanne waliochaguliwa kuunda kombaini ya Afrika Mashariki akiwa na wachezaji Arthur Mwambeta na Kitwana Manara.
Mwaka 1974, alichaguliwa kuwa namba 10 wa timu ya Afrika akiwa na Mtanzania mwenzake kipa Omar Mahadhi ambaye sasa ni marehemu pia. Akiwa na timu hiyo ya Afrika aliteuliwa kuwa nahodha.
Mwaka huo huo, Dilunga akiwa na kikosi cha Yanga kilichokuwa kikinolewa na Kocha Tambwe Leya alikwenda kwenye mafunzo nchini Romania akiwa na wachezaji kama Elias Michael, Kapera, Hassan Gobos, Emmanuel Chitete, Sunday na Kitwana Manara, Gibson Sembuli ambaye pia ni marehemu na mchezaji kinda wakati huo aliyekuwa timu ya vijana, Mohamed "Adolf" Rishard.
Mashabiki wa soka wa enzi hizo wanasema kama ilivyokuwa kwa Sunday Manara, Maulid Dilunga alikuwa akicheza soka ya ladha na ya kuvutia.
Kumbukumbu mojawapo ya kilele cha uanasoka wake ni mechi ya mwaka 1968 Yanga ilipoitandika Simba, wakati ikifahamika kama Sunderland, mabao 5-0. Rekodi zilizopo zinaonyesha kwamba Dilunga alifunga mabao mawili katika mechi hiyo, moja katika dakika ya 18 kwa penalti na jingine katika dk 43, huku Saleh Zimbwe akifunga katika dakika za 54 na 89 na Kitwana Manara aliyepachika bao jingine katika dakika ya 86.
Omar Gumbo ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Simba anamkumbuka kwa kusema: “ Dilunga nimecheza naye timu ya taifa na tulikuwa tunakaa chumba kimoja.
“Alikuwa mchezaji mwenye kipaji na uwezo mkubwa. Siku zote alikuwa mpole na mkimya na kusema kweli alikuwa ni mchezaji wa mfano hapa nchini kutokana na uwezo wake.”
Gumbo anasema: “Nakumbuka mechi moja tuliyocheza akiwa timu ya taifa ambayo ilikuwa ngumu na nzito ni ile iliyotukutanisha na Uganda kwenye michuano ya Chalenji. Katika mchezo huo tulitoka sare ya bao 1-1 na Dilunga alikuwa mchezaji bora kwenye mechi hiyo.”
Mdau wa soka Feruzi Maganga anasema: “Ni mmoja wa wachezaji bora ambao taifa hili limewahi kuwapata ambaye anafahamika zaidi kutokana na umahiri na kipaji chake katika kumiliki mpira na kufungia timu yake ya Yanga na Taifa Stars.
Kipindi ambacho Maulid Dilunga alivuma ni ambacho kiwango cha soka cha Tanzania, kama timu na mchezaji mmoja mmoja kilikuwa juu na ndio maana inaaminika kuwa aliweza kuchaguliwa kuchezea namba 10 ya Afrika.
Kutokana na kutokuwapo na wachezaji wengine wa aina ya Maulid Dilunga nchini kwa sasa, namba hiyo na nyinginezo zimechukuliwa na nchi za Magharibi na Tanzania haionekani vizuri katika ramani ya soka Afrika kwa sasa.
Mara baada ya kutundika daluga, Dilunga anakumbukwa kwa kuchangia kuibua vipaji vya wachezaji wachanga kwa kutumia muda wake kufundisha taasisi ya kuinua vipaji ya Elite na kuifundisha timu ya Kilosa, mkoani Morogoro.
Katika kumuenzi mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Florian Kaijage amesema kuwa wakati wa mechi ya kuwania kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika na Kombe la Dunia 2010 kati ya Taifa Stars na Cameroon keshokutwa, wachezaji na watazamaji watasimama dakika moja kuomboleza.
Dilunga(pichani) aliyefariki akiwa na umri wa miaka 62, ameacha mjane na watoto sita. Mungu amlaze mahali pema peponi. Amina. Makala haya ni ya Anastazia Anyimike wa TSN
Makala haya ni ya Anastazia Anyimike wa TSN.
COMMENTS