Kiranja mkuu ataka 'displin' katika matumizi

HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO PETER PINDA (MB), WAZIRI MKUU, KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA...

HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO PETER PINDA (MB), WAZIRI MKUU, KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU NA
OFISI YA BUNGE YA MWAKA 2009/2010


UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na Taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, iliyochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2008/2009 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2009/2010. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Taasisi zilizo chini yake pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2009/2010.

2. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Bunge lako Tukufu lilipata Msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Marehemu Chacha Zakayo Wangwe; Marehemu Richard Nyaulawa, aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Vijijini; Marehemu Faustine Kabuzi Rwilomba aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Busanda na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Biharamulo, Marehemu Phares Kabuye. Vilevile, katika kipindi hiki, kumetokea matukio mbalimbali yaliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali za Wananchi wengi. Nitumie fursa hii kuwapa pole wote waliopatwa na Misiba hii na Maafa mbalimbali. Tunamwomba Mwenyezi Mungu awaponye haraka Majeruhi wote na Aziweke Roho za Marehemu Mahali Pema Peponi. Amina.

3. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla wamepata fursa ya kujadili Taarifa kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2008 na Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2009/2010. Nitumie nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Mustafa Haidi Mkulo (Mb.), Waziri wa Fedha na Uchumi kwa Hotuba nzuri na ufafanuzi fasaha wa hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango mizuri waliyoitoa wakati wa mjadala wa Hotuba hizo na hatimaye kupitisha Bajeti ya Serikali. Serikali itazingatia ushauri uliotolewa katika utekelezaji wa Mpango na Bajeti hiyo.

4. Mheshimiwa Spika, nawashukuru Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge lako Tukufu kwa michango na ushauri waliotoa wakati wa kupitia Makadirio ya Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali Zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kipekee, nitumie nafasi hii pia, kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala chini ya Uongozi wa Mwenyekiti wake Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kwa mchango wao mkubwa wakati wa uchambuzi wa Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Bunge. Maoni na Ushauri wao umesaidia sana kuboresha Makadirio ya Bajeti ya Ofisi hizi.

5. Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu limepitisha Bajeti ya Serikali ambayo ndiyo itatuongoza kuelekea mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005. Katika Ilani hiyo, Chama kiliahidi mambo mbalimbali ambayo yamezingatiwa katika Bajeti hii. Vilevile, Bajeti hii, imezingatia yaliyomo katika Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini (MKUKUTA), Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Malengo ya Maendeleo ya Milenia. Serikali katika ngazi zote itaendelea kutekeleza kwa makini ahadi zilizoahidiwa kwa kuimarisha usimamizi na matumizi mazuri ya Bajeti ya Serikali iliyopitishwa.

HALI YA SIASA NCHINI

Kuimarika kwa Demokrasia
6. Mheshimiwa Spika, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayotekeleza Demokrasia ya Vyama Vingi. Ili kudumisha Demokrasia, kumekuwepo na maboresho mbalimbali yanayofanyika kila mara kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu. Kwa mfano, kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Vyama Vingi uliofanyika Mwaka 2005, kulianzishwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kutumika wakati wa Uchaguzi huo. Maboresho hayo pia yalihusu Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya Mwaka 1985 na Na. 4 ya Mwaka 1979. Masuala mengine yanayodumisha Demokrasia ya Nchi yetu ni kukubalika kwa Maadili ya Uchaguzi, kuimarika kwa mahusiano baina ya Tume ya Uchaguzi na Wadau, Vyama vyote vya Siasa kupewa fursa sawa ya kunadi na kushindanisha Sera zao kwa Wananchi, kuboreka kwa Mchakato wa Kupiga na Kuhesabu Kura pamoja na Kutangaza Matokeo.

Vyama vya Siasa
7. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeendelea na majukumu yake ya Kusajili Vyama vya Siasa, Kuratibu shughuli za Vyama vya Siasa na Kukuza Demokrasia ya Vyama Vingi hapa Nchini. Hadi sasa idadi ya Vyama vyenye Usajili wa Kudumu hapa Nchini ni 17. Katika mwaka 2008/2009, Vyama vitatu vya Peoples Democratic Movement (PDM), Democratic National Congress (DNC) na Alliance for Tanzania Farmers Party (ATFP) vimepatiwa Usajili wa muda. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeendelea kutoa Elimu kwa Umma ili kudumisha na kuendeleza Mfumo wa Demokrasia ya Vyama Vingi Nchini na kufungua Ofisi ya Kanda Dodoma. Ofisi hiyo itahudumia Mikoa ya Dodoma, Iringa, Singida na Tabora. Aidha, Bunge lilipitisha Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa Namba 5 ya mwaka 1992 ili kutoa fursa sawa ya kukuza na kuendeleza Demokrasia Nchini.

8. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itaandaa Kanuni za Sheria zitakazoelekeza jinsi marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa yatakavyotekelezwa. Vilevile, itafungua Ofisi ya Kanda ya Mwanza itakayohudumia Mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga na Kigoma.

Chaguzi Ndogo
9. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2008/2009, kulifanyika Chaguzi Ndogo tatu za Wabunge katika Majimbo ya Tarime, Mbeya Vijijini na Busanda. Vilevile, zilifanyika Chaguzi Ndogo za Madiwani katika Kata 45. Nichukue fursa hii kuwapongeza Wananchi wote na Vyama vya Siasa vilivyoshiriki katika chaguzi hizo ambazo zilifanyika kwa Amani na Utulivu. Aidha, nawapongeza wale wote walioshinda katika chaguzi hizo. Kipekee, napenda nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Charles Nyanguru Mwera (Mb.), kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime; Mheshimiwa Mchungaji Luckson Mwanjale (Mb.), kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini na Mheshimiwa Lolensia Bukwimba (Mb.), kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Busanda. Wote nawatakia mafanikio katika kuwatumikia Wananchi wa Majimbo yao na Vyama vyao katika muda uliobaki kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
10. Mheshimiwa Spika, uchaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wa Viongozi wa ngazi ya Kijiji, Kitongoji na Mtaa utafanyika mwezi Oktoba, 2009. Maandalizi muhimu ya kufanikisha uchaguzi huo yanaendelea ikiwemo kuandaa Orodha ya Vijiji, Vitongoji na Mitaa kwa ajili ya Uchaguzi huo. Natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wa Kisiasa kuendelea kuwahamasisha Wananchi watambue umuhimu wa Uchaguzi kama nguzo muhimu ya kuimarisha Utawala Bora na Demokrasia Nchini, na wawe tayari kushiriki kikamilifu katika kuwachagua Viongozi wanaowataka kwa hiari yao wenyewe. Aidha, Vyama vya Siasa na Wanachama wao wanahimizwa kufanya shughuli zao za Siasa kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu ili kudumisha Amani na Utulivu uliopo Nchini.

Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010
11. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Uchaguzi imekamilisha Awamu ya Kwanza ya Uboreshaji Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Hatua hii ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2010. Serikali pia, inakusudia kuwasilisha Bungeni mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya Mwaka 1985 na Sheria Na. 4 ya mwaka 1979. Mapendekezo hayo ni pamoja na Tume kupewa Mamlaka ya kuandikisha Wapiga Kura wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa na Kipindi Maalum cha kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura walau mara mbili kati ya chaguzi na kubadilisha kipindi cha kufanya uteuzi wa mgombea endapo Mgombea Urais au Makamu atafariki. Mapendekezo mengine ni kuondoa Vifungu vya Sheria vinavyoruhusu takrima, muda wa kufungua Kesi za Kupinga Matokeo kuongezwa, kuwekwa kikomo cha mgombea kujitoa katika Uchaguzi na Tume kupewa Mamlaka ya kufanya Chaguzi Ndogo za Madiwani walau mara mbili kwa mwaka badala ya kila wakati wa ukomo wa muda wa kusikiliza Kesi za Madiwani katika Mahakama. Pia, Tume ya Uchaguzi itaandaa vigezo na utaratibu utakaotumika kugawa Majimbo ya Uchaguzi. Nawasihi Wananchi kushirikiana na Tume ya Uchaguzi katika zoezi la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili wasikose haki yao ya msingi ya kuwachagua Viongozi wao ifikapo mwaka 2010.

Muungano
12. Mheshimiwa Spika, Muungano wetu unaendelea kuimarika mwaka hadi mwaka. Hata hivyo, bado zipo kero chache ambazo pande zote mbili zinaendelea kuzifanyia kazi. Ili kuhakikisha kwamba kasi ya kushughulikia kero hizo inaongezeka, Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayojadili na kutoa ufumbuzi wa kero mbalimbali za Muungano imeandaa ratiba maalum kwa lengo la kuharakisha mchakato wa kutatua kero hizo. Tangu mwezi Februari, 2008 Mheshimiwa Makamu wa Rais alipoteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Vikao vya Pamoja vya kushughulikia Kero za Muungano hadi kufikia mwezi Mei 2009, jumla ya Vikao Saba vimeshafanyika katika ngazi za Makatibu Wakuu, Mawaziri na Kamati ya Pamoja yenye Wajumbe kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

13. Mheshimiwa Spika, mazungumzo katika Vikao vya kutatua maeneo yenye Kero za Muungano yanakwenda vizuri ambapo baadhi ya maeneo hayo yamemalizika baada ya maamuzi yenye muafaka wa pamoja kutolewa. Maeneo hayo yanahusu utekelezaji wa:-
(i) Sheria ya Haki za Binadamu Zanzibar;
(ii) Sheria ya Uvuvi katika Ukanda wa Bahari Kuu; na
(iii) Sheria ya Biashara ya Meli katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Napenda kutumia fursa hii, kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein, Makamu wa Rais, kwa kuongoza kwa makini Vikao vya pamoja vya kushughulikia Kero za Muungano hadi kupata mafanikio hayo.

14. Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi hizo, Serikali imechukua hatua za makusudi kuelimisha umma kuhusu masuala ya Muungano kupitia vipindi vya Redio, Luninga na Vipeperushi. Aidha, Miradi ya pamoja ya kijamii na kiuchumi kama vile TASAF, PADEP na SELF inaendelea kutekelezwa katika pande zote mbili. Katika mwaka 2009/2010, Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kuratibu Vikao vya pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa lengo la kudumisha Muungano wetu. Aidha, itaendelea na jukumu la kuimarisha ushirikiano kati ya pande mbili za Muungano kwa masuala yasiyo ya Muungano.

Bunge
15. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Bunge lilitekeleza majukumu yake ya msingi kwa mujibu wa Ibara 63(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bunge lilifanya Mikutano minne kama ilivyopangwa ambapo jumla ya Maswali 1,028 yaliulizwa na kujibiwa na Serikali. Aidha, Waziri Mkuu aliulizwa jumla ya maswali ya msingi 95 katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo. Bunge pia, lilipitisha Miswada 24 na kuridhia Maazimio 10. Vilevile, Bunge lilizindua rasmi Mpango Mkakati wa Bunge wa miaka mitano kuanzia mwaka 2009 hadi 2013. Malengo Makuu ya Mpango Mkakati huo ni kuimarisha utendaji na uwajibikaji, kuboresha huduma itolewayo kwa Waheshimiwa Wabunge na matumizi ya TEKNOHAMA. Aidha, unalenga kutoa mafunzo kwa Watumishi na Wabunge ili kuwaongezea uwezo wa kuhudumia Wananchi vizuri.

16. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, Bunge letu lilishiriki Mikutano mbalimbali ya Kibunge katika Kanda na ile ya Kimataifa. Miongoni mwa Mikutano hiyo ni pamoja na Mkutano wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola uliofanyika Malaysia tarehe 1 - 10 Agosti, 2008. Katika Mkutano huo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samwel Sitta (Mb.), alichaguliwa kuwa Rais wa Taasisi ya Mabunge ya Jumuiya ya Madola. Aidha, mwezi Mei 2009, Bunge letu lilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa Chama cha Wabunge wa Kamati za Hesabu za Serikali kwa Nchi za Mashariki mwa Afrika (Eastern Africa Association of Public Accounts Committes). Mkutano huo ulijadili na kubadilishana uzoefu kuhusu uwajibikaji wa Serikali kwa Bunge katika kufuatilia Hesabu za Serikali. Nichukue fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge walioshiriki na kutuwakilisha vizuri katika Mikutano hiyo. Nampongeza Mheshimiwa Spika kwa nafasi hiyo aliyopewa ambayo imetuletea heshima katika Nchi yetu.

17. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Bunge litaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi na kuanza utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Bunge. Aidha, Bunge letu litakuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola utakaofanyika mwezi Septemba, 2009 Jijini Arusha. Nawasihi tutumie fursa hiyo kujifunza na kubadilishana uzoefu na wenzetu kuhusu Kauli Mbiu ya Mkutano huo ambayo ni “Kukabiliana na Changamoto Zinazoikabili Dunia”. Aidha, hii ni fursa nzuri ya kuitangaza Nchi yetu hasa katika Sekta ya Utalii na Biashara.

USIMAMIZI WA Uchumi
18. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005 katika eneo la kusimamia Uchumi Jumla. Takwimu zinaonyesha kwamba Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 7.4 mwaka 2008 ikilinganishwa na asilimia 7.1 mwaka 2007. Hata hivyo, Uchumi umeendelea kukabiliwa na Mfumuko wa Bei uliotokana hasa na athari za kupanda kwa bei za bidhaa katika Soko la Dunia na upungufu wa chakula. Hali hii ilisababisha Mfumuko wa Bei kufikia asilimia 13.5 mwezi Desemba 2008. Kufuatia kushuka kwa bei ya bidhaa, kama vile vyakula na mafuta, Mfumuko wa Bei umeshuka na kufika asilimia 12.0 mwezi Aprili 2009. Serikali itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Sera za Uchumi Jumla ili kuleta hali ya utulivu na ukuaji mzuri wa Uchumi Nchini. Wito wangu ni kwamba, sote tufanye kazi kwa bidii kujenga Uchumi imara, wa kisasa na endelevu ili tuweze kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ambayo ni kuwa Nchi ya Pato la Kati ifikapo mwaka 2025.

19. Mheshimiwa Spika, ili kuutoa Uchumi wetu kutoka kwenye Uchumi uliyo nyuma na tegemezi na kuuingiza kwenye Uchumi imara, wa kisasa na endelevu tunahitaji kufanya Mapinduzi katika Sekta ya Kilimo na Viwanda. Mapinduzi haya yataongeza uzalishaji na tija na hivyo kuongeza ukuaji wa Uchumi. Uzalishaji wa mazao ya Kilimo ukiongezeka, mavuno yataongezeka na hivyo ongezeko hilo litawawezesha Wakulima kunufaika kupata kipato kutokana na kuuza mazao mengi zaidi nje. Hii pia, inavutia Wawekezaji kujenga Viwanda vya Usindikaji na utengenezaji wa bidhaa za Viwandani kutokana na mazao ya kilimo. Tukifanya mapinduzi hayo, tutakuwa tumetekeleza ahadi yetu ya Maisha Bora kwa kila Mtanzania. Hivyo, Viongozi na Watendaji wa Serikali wanao wajibu mkubwa wa kusimamia mapinduzi haya ili kukuza Uchumi kwa kiwango kikubwa na Kuutokomeza Umasikini.

20. Mheshimiwa Spika, kama alivyoelezea Mheshimiwa Rais katika Hotuba yake ya tarehe 10 Juni, 2009 mjini Dodoma, Dunia inakabiliwa na Msukosuko wa Masoko ya Fedha ulioanzia huko Marekani na Nchi za Ulaya, Asia na kuenea sehemu nyingine Duniani. Msukosuko huu umesababisha Uchumi wa Dunia kuporomoka. Athari kubwa ya Msukosuko huo kwa Nchi Zinazoendelea inatarajiwa kujitokeza zaidi katika mwaka 2009. Athari za Msukosuko huo kwa Tanzania zinaweza kutazamwa katika Sekta ya Fedha na Uchumi wa Nchi. Kwa upande wa Sekta ya Fedha, Soko letu la fedha halitegemewi kuathirika sana kwa sababu ya kuwa na kiwango kidogo cha muunganiko na Masoko ya Fedha Duniani. Athari za kiuchumi ni pamoja na ukuaji mdogo wa Uchumi, kushuka kwa bei za mazao na bidhaa tunazozalisha Viwandani, kushuka kwa mapato kutokana na utalii na kupungua kwa uwekezaji kutoka nje. Ili kukabiliana na hali hiyo, Serikali imeandaa Mpango wa Kunusuru Uchumi wa Tanzania na Athari za Msukosuko wa Fedha na Uchumi Duniani. Napenda kusisitiza kuwa, ni vyema tuhakikishe kuwa kuna nidhamu katika matumizi ya Serikali kutokana na hofu ya kupungua misaada kutoka nje. Vilevile, tuongeze juhudi katika kukusanya mapato ya ndani na kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuendeleza uwekezaji kwenye maeneo yatakayosaidia ukuaji wa Uchumi.

UKUZAJI WA SEKTA BINAFSI NA UWEKEZAJI

Uwekezaji na Maendeleo ya Sekta Binafsi
21. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua nafasi ya kimkakati ya Sekta Binafsi katika kukuza Uchumi na kuleta maendeleo. Kwa kuzingatia umuhimu huo, Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya kuimarisha Sekta Binafsi. Ili kutekeleza azma hiyo, katika mwaka 2008/2009, Serikali ilihamishia Ofisi ya Waziri Mkuu jukumu la kuratibu, kusimamia na kufuatilia masuala yote yanayohusu Maendeleo ya Sekta Binafsi na Uwekezaji ili iweze kupata msukumo unaostahili. Kwa kuzingatia hali hii, Ofisi yangu imesambaza Taarifa ya Hali ya Kufanya Biashara Nchini (Report on Doing Business 2009) kwa Watendaji Wakuu wote katika Wizara, Mikoa na Halmashauri. Taarifa hiyo ambayo imeainisha maeneo kumi yanayokwamisha Wawekezaji na Wafanyabiashara hapa Nchini, ilisambazwa kwa Watendaji Wakuu ili wachukue hatua zinazostahili kuondoa vikwazo hivyo. Nawaagiza Watendaji Wakuu wote kuwasilisha Taarifa za Utekelezaji kuhusu hatua zinazochukuliwa kuondoa vikwazo hivyo Ofisi ya Waziri Mkuu kila baada ya miezi mitatu.

Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara Tanzania (MKUMBITA)
22. Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi inaendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara Tanzania - MKUMBITA (Business Environment Strengthening Programme - BEST). Lengo la Mpango huu ni kupunguza gharama za kuanzisha na kuendesha Biashara kwa kuondoa vikwazo vya Sera, Sheria pamoja na udhibiti katika Sekta mbalimbali. Ili kuondoa vikwazo hivyo, MKUMBITA umejikita katika maeneo manne ambayo ni Usajili wa Miliki ya Ardhi, Maboresho ya Sheria na Soko la Ajira, Ufumbuzi wa Migogoro ya Kibiashara na Usajili, Udhibiti na Ufilisi wa Biashara.

23. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, MKUMBITA umewezesha maandalizi ya utoaji Hati Miliki za Kimila kwa Vijiji na kuendeleza Makazi yaliyojengwa kiholela katika Jiji la Mwanza na Dar es Salaam. Mchakato wa kutoa Hati Miliki katika Wilaya za Babati na Bariadi umeanza mwezi Mei, 2009. Aidha, Mpango umewezesha kuanzishwa kwa Mahakama ya Biashara, Mkoani Mwanza ambayo imezinduliwa na kuanza kazi na sasa inaendelea kusikiliza kesi zinazohusu migogoro ya biashara. Vilevile, Mpango wa Utekelezaji wa Mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Mahakama umeandaliwa na umeanza kutekelezwa na Ripoti ya awali ya marekebisho ya Sheria zinazohusu Mfumo wa Haki na Madai imekamilika.

24. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali itaendelea kujenga mazingira mazuri ya kukuza Sekta Binafsi na kuvutia Uwekezaji Nchini. Aidha, itaendelea na maboresho yenye lengo la kupunguza gharama za kufanya biashara na uwekezaji Nchini kama zilivyoainishwa katika Taarifa ya Hali ya Kufanya Biashara Nchini ya mwaka 2009. Serikali pia, itakamilisha Sera ya Ubia baina ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma (Public Private Partnership Policy) Nchini. Uzoefu wa Mataifa mbalimbali yakiwemo ya Marekani, India, Afrika Kusini, Misri, Ufaransa na Uingereza unaonyesha kuwa Sekta Binafsi ikishirikishwa ipasavyo katika kuendeleza miundombinu na kutoa huduma muhimu, mzigo katika Bajeti ya Serikali utapungua na kuiwezesha Serikali kugharamia majukumu mengine ya maendeleo.

Kituo cha Uwekezaji Tanzania
25. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania imeendelea na juhudi za kuhamasisha Uwekezaji wa Ndani na Nje ya Nchi kwa lengo la kuongeza ubia, kujenga uwezo wa ushindani, kukuza Sekta Binafsi na hatimaye kukuza Uchumi wa Taifa. Kutokana na juhudi hizo, idadi ya Makampuni ya Kitanzania yameongezeka kujiandikisha ili kunufaika na vivutio vya Uwekezaji vinavyotolewa na Kituo hiki. Katika mwaka 2008/2009, Kituo cha Uwekezaji Nchini kilisajili jumla ya Miradi 797 yenye thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 3.6 ambayo inakadiriwa kutoa nafasi za Ajira 109,328. Kati ya miradi hiyo, Miradi 454 au asilimia 57 inamilikiwa na Watanzania, Miradi 128 au asilimia 16 ni ya Wageni na Miradi 215 au asilimia 27 ni ya ubia. Sekta ya Utalii ndiyo iliyopata miradi mingi zaidi, kwa Kusajili Miradi 241. Sekta nyingine zilizovutia Wawekezaji wengi ni pamoja na Sekta ya Viwanda Miradi 215 na Sekta ya Nyumba za Biashara Miradi 124. Takwimu za Kimkoa zinaonyesha kuwa, Mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Kilimanjaro na Pwani iliongoza kwa kusajili miradi mingi.

26. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania imeendelea kubuni na kutekeleza Mipango mbalimbali ya kuongeza ushiriki wa Wananchi katika kuwekeza Nchini. Kituo kimebuni mpango wa kuwahamasisha Watanzania kujiunga katika Vikundi vya Kiuchumi na kuunda Makampuni endelevu ambayo yanaweza kusajiliwa na kujiendesha kibiashara. Aidha, Kituo kwa kushirikiana na Uongozi wa Mikoa mbalimbali kimeanzisha mpango wa kutoa mafunzo kwa Wajasiriamali Mikoani ili waweze kutayarisha Taarifa za Miradi inayokopesheka. Tayari kazi hii imeanza katika Mikoa ya Mara na Ruvuma. Kituo pia, kimeanzisha Mpango Maalum wa kuhakikisha kuwa Mikoa ambayo ipo nyuma katika uwekezaji inapanga maeneo ya Uwekezaji na kuyanadi kwa pamoja kupitia Kituo hiki. Mpango huu unajulikana kama Regional Partnership Program na umeanza katika Mikoa Mitano ambayo ni Rukwa, Kagera, Tabora, Tanga na Singida.

Baraza la Taifa la Biashara
27. Mheshimiwa Spika, Baraza la Taifa la Biashara limeendelea kukuza mashauriano baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kwa madhumuni ya kuboresha mazingira ya Biashara na Uwekezaji. Katika mwaka 2008/2009, Baraza lilifanya Mikutano ya Wawekezaji wa Nje na Ndani. Katika Mikutano hiyo, majadiliano yalilenga kutathmini uelewa wa dhana nzima ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, kuanzisha majadiliano katika ngazi ya Wilaya kwa kushirikisha Wadau mbalimbali na kuboresha mazingira ya biashara na fursa za uwekezaji Nchini kwa kuzingatia hali ya Uchumi Duniani. Aidha, Mheshimiwa Rais alizindua Mabaraza ya Biashara ya Wilaya zote Tanzania Bara ambayo yatashirikisha Wananchi kwenye mijadala ya maendeleo ngazi ya chini.

28. Mheshimiwa Spika, tarehe 2 hadi 3 Juni 2009, Baraza la Taifa la Biashara liliandaa Mkutano Maalum na wa Kihistoria kuhusu Kilimo uliohudhuriwa na Wadau kutoka Sekta ya Umma na Binafsi kwa lengo la kujadili mikakati thabiti itakayoleta Mapinduzi ya Kijani ambayo yatafanya Kilimo chetu kiwe cha kisasa, chenye tija na cha kibiashara. Mkutano huo ambao ulifunguliwa na kuongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara, Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete ulihudhuriwa pia na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge, Watendaji Wakuu Serikalini, Wakulima na Wawekezaji. Aidha, nilipata fursa ya kushiriki katika Mkutano huo ambao Kauli Mbiu yake ni “KILIMO KWANZA” ikiwa na maana kuwa mambo mengine yote yanaweza kusubiri isipokuwa Kilimo.

29. Mheshimiwa Spika, Mkutano huo ulikuwa na mafanikio makubwa, kwa sababu tuliweza kufikia muafaka kuhusu hatua za kuleta Mapinduzi ya Kilimo Nchini, ikiwa ni pamoja na:-
(i) Viongozi na Watendaji wote kuwa na utashi wa kuendeleza Kilimo;
(ii) Kuwekeza zaidi katika Kilimo;
(iii) Kuanzisha Benki ya Kilimo; na
(iv) Kila Sekta kutayarisha Mpango Kazi wa kutekeleza “KILIMO KWANZA”.

Wadau wote walikubaliana kuwa wakati umefika kukipa Kilimo kipaumbele kwani ndiyo nguzo kuu ya Uchumi wetu na pia Kilimo ndicho kitawezesha Wakulima wengi na Wananchi waishio Vijijini kutoka katika maisha duni na kufikia maisha bora tunayoyataka. Serikali inakamilisha Mpango Kazi wa kutekeleza mapendekezo ya Mkutano huo na utakapokamilika utasambazwa kwa Wadau mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge ili uwe Mwongozo wa kuhamasisha Wananchi katika jitihada za kuleta Mapinduzi ya Kilimo Nchini.

Programu ya Huduma za Kifedha Vijijini
30. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Programu ya Huduma za Kifedha Vijijini imewezesha Asasi 276 za Kifedha kuwa na mifumo Bora ya Usimamizi na Uongozi. Wakufunzi kumi wa Asasi za kutoa Huduma za Mafunzo walihitimu na kupata Vyeti vya Utambuzi kama Wakufunzi wa Masuala ya Kifedha (Accredited Trainers in Microfinance Best Practices). Aidha, Asasi ndogo za Kifedha 140 zimeunganishwa na Mabenki na Asasi kubwa za Kifedha. Asilimia 40 ya Wanachama wa Asasi hizo ndogo ni Wanawake. Programu pia, ilikabidhi shughuli zake pamoja na nyenzo za kufanyia kazi kwa Halmashauri za Wilaya 12 ambazo ni Same, Mwanga, Rombo, Moshi (V), Dodoma (V), Mpwapwa, Kondoa, Njombe, Mufindi, Mbeya (V), Mbarali na Rungwe, kati ya Wilaya 22 ambazo ilikuwa inafanya kazi. Programu inaendelea kutekeleza shughuli zake katika Wilaya 10 zilizobaki.

31. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Programu itaendelea kuboresha usimamizi na uendeshaji wa Asasi ndogo za fedha, kuimarisha mifumo ya fedha Vijijini na kuwajengea uwezo Wananchi Vijijini ili waweze kujiunga na kushiriki katika shughuli za SACCOS. Aidha, Programu itaendelea kuimarisha Benki za Wananchi, mitandao ya Asasi za Kifedha na kuendelea kusaidia mchakato wa uanzishwaji wa Benki za Wananchi. Natoa wito kwa Wananchi wajiunge kwa wingi katika Vyama vya Kuweka na Kukopa ili waweze kutumia fursa mbalimbali za Mikopo zinazojitokeza ambazo zitawasaidia kuinua kipato chao.

Programu ya Uendelezaji wa Mifumo ya Masoko ya Mazao ya Kilimo
32. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Programu ya Uendelezaji wa Mifumo ya Masoko ya Mazao ya Kilimo iliendelea kutekeleza shughuli zake kwenye maeneo mbalimbali katika Mikoa Nane ya Tanzania Bara. Mojawapo ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kutungwa kwa Sera ya Masoko ya Bidhaa za Kilimo. Sera hii imetoa mwelekeo na Mwongozo katika kuimarisha na kuendeleza mifumo ya Masoko ya mazao na bidhaa za Kilimo kwa kuondoa vikwazo vinavyokabili ushiriki, uendeshaji na unufaikaji wa Mfumo wa haki na usawa kwa Wadau wote wanaoshiriki katika Soko huru la Mazao na Bidhaa za Kilimo. Mafanikio mengine ni pamoja na uwezeshaji wa Wazalishaji Wadogo katika ushiriki wa Masoko ya Bidhaa wanazozalisha, na ongezeko la idadi ya Washiriki katika Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani. Vilevile, Programu imejenga na kukarabati miundombinu ya Masoko kwenye Wilaya Nane za Awamu ya Mwisho ambazo ni Korogwe, Mwanga, Moshi Vijijini, Simanjiro, Kyela, Nkasi, Njombe na Makete. Pia, shughuli kama hizi ziliendelezwa katika Wilaya nyingine chache za Awamu ya Pili ambazo ni Mbozi, Same na Mbulu. Kwa ujumla shughuli hizi zimeleta mafanikio makubwa kulingana na makusudio ya Programu ambayo ni kuongeza kipato kwa Wananchi na kuwa na uhakika wa Chakula.

33. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Programu itasimamia na kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba shughuli zake zinakuwa endelevu hata baada ya Programu kumaliza muda wake kwa kuziwezesha Halmashauri husika kuingiza shughuli za Programu katika Mipango yao ya Maendeleo. Aidha, Programu kwa ushirikiano na Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko itakamilisha Mchakato wa uandaaji wa Mkakati wa utekelezaji na Sera ya Masoko ya Bidhaa za Kilimo. Programu pia, itakamilisha ukarabati wa Barabara za Vijijini na ujenzi wa Masoko katika Wilaya za Awamu ya Mwisho.

KILIMO, MIFUGO NA UVUVI

Kilimo
34. Mheshimiwa Spika, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, inatamka bayana umuhimu wa Maendeleo ya Kilimo chenye Tija kama njia ya kuharakisha Maendeleo Vijijini kwa kuongeza mapato na pia kujitosheleza kwa chakula. Aidha, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005, inatambua umuhimu wa Kilimo cha Kisasa kama sharti muhimu katika kujenga msingi wa Uchumi wa kisasa. Ili kuboresha Kilimo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za Kisera na Kibajeti ikiwemo kushirikiana na Wananchi kuandaa Miradi ya Pamoja ya Kilimo. Mwezi Oktoba 2008, Serikali iliitisha Mkutano wa Wadau wa Kilimo kutoka Mikoa ya Morogoro, Iringa, Mbeya, Kigoma, Rukwa na Ruvuma ambayo inazalisha chakula kwa wingi ili kujiwekea mikakati ya kuendesha Kilimo cha Kisasa zaidi kwenye Mikoa hiyo. Lengo ni kuhimiza Mikoa hiyo yenye ardhi nzuri na mvua za kutosha kati ya Milimita 800 hadi 1,500 kuwa kichocheo cha kuongoza Mapinduzi ya Kilimo katika kuzalisha na kujitosheleza kwa chakula. Katika Mkutano huo, tuliwekeana maazimio na tukakubaliana namna ya kuyatekeleza.

35. Mheshimiwa Spika, mwezi Machi na Mei 2009, nilitembelea Mikoa hiyo kujionea mwenyewe utekelezaji wa yale tuliyokubaliana. Baada ya ziara yangu katika Mikoa hiyo Sita, nimeona kazi inayofanyika na kujifunza mambo mengi. Kwa ujumla tumeanza vizuri utekelezaji wa Maazimio na Malengo tuliyojiwekea. Katika maeneo mengi niliyotembelea nimefarijika sana kuona mabadiliko ya tija yanaanza kujitokeza, hasa maeneo yale ambayo yanatumia Skimu za Umwagiliaji. Kwa mfano, uzalishaji wa Mpunga umeongezeka kutoka wastani wa Magunia 15 hadi 50 kwa Hekta katika Skimu za Umwagiliaji za Igomelo (Mbarali) na Iganjo (Uyole). Uzalishaji wa mahindi nao umeongezeka na kufikia Magunia 50 kutoka wastani wa Magunia 30 kwa Hekta, maharage nayo yameongezeka kutoka wastani wa Magunia 10 hadi kufikia 20 kwa Hekta. Vilevile, kwenye Skimu hizi Wakulima wanaweza kuvuna mazao mara mbili. Hii inaonyesha kwamba kuna umuhimu wa kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji ili kuongeza tija na uzalishaji.

36. Mheshimiwa Spika, Kilimo tunachokitaka ni lazima kiwe chenye tija, cha kisasa na kibiashara. Hata hivyo, ili kuongeza tija na uzalishaji, ni lazima kutumia mbegu bora, mbolea na utaalam. Serikali imekuwa ikitoa mbolea ya ruzuku kwa miaka kadhaa sasa ili imsaidie Mkulima kupunguza ukali wa bei za mbolea. Kwa mara ya kwanza, katika mwaka 2008/2009, Serikali ilianza kutoa mbolea ya ruzuku kwa kutumia Mfumo wa Vocha. Hadi kufikia mwezi Aprili 2009, Mbolea ya Ruzuku kiasi cha Tani 141,050 sawa na Vocha 1,496,000 zilisambazwa Nchini. Tathmini ya awali ya Mfumo wa Vocha imeonyesha kwamba ni mfumo mzuri kwani tofauti na Mfumo tuliokuwa tunatumia awali, unamnufaisha Mkulima moja kwa moja na siyo Mtu wa Kati. Kwa kuwa ni Mfumo mpya, zimejitokeza changamoto mbalimbali katika utekelezaji. Serikali inazifanyia kazi changamoto hizo ili Mfumo huo uzidi kuwa bora zaidi na kuwafikia walengwa wengi zaidi. Ni vyema sote tufahamu kwamba, mbolea inayotolewa inalenga kukuza uzalishaji katika Kilimo, hivyo Wakulima watumie nafuu hiyo ya bei ya mbolea kuzalisha zaidi na si kuiuza tena kwa Mawakala. Kufanya hivyo ni kosa na wale watakaofanya hivyo watakuwa wanahujumu maendeleo yao wenyewe.

37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali pia ilitoa ruzuku ya Mbegu Bora zenye jumla ya Tani 7,180, sawa na Vocha 624,500. Vilevile, Mfuko wa Pembejeo umetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 5.8 kwa ajili ya kununua Matrekta Makubwa 66 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.3, Matrekta Madogo 29 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.0 na Pembejeo nyingine zenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.5. Wakati huo huo, tathmini ya matumizi sahihi ya Matrekta 200 yaliyokopeshwa kwa Wakulima kupitia Mfuko wa Pembejeo imefanyika katika Kanda Saba za Kilimo ili kuweza kutoa ushauri wa kiufundi kuhusu Kilimo cha kibiashara na faida za kutumia zana bora za Kilimo.

38. Mheshimiwa Spika, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 imeelekeza Serikali kuwaandaa Maafisa Ugani wa fani mbalimbali za Kilimo na kuwapeleka katika maeneo wanakohitajika. Katika mwaka 2008/2009, jumla ya Wataalam wa Ugani 544 waliajiriwa na kupangiwa kazi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Pamoja na Serikali kuajiri Wataalam wa Ugani kila mwaka, bado mahitaji yao ni makubwa na hivyo kuhitaji ubunifu zaidi ili kufanya Mapinduzi ya Kilimo kwa kasi inayostahili. Kwa mfano, Mkoa wa Kigoma umewakusanya Vijana kutoka Vijiji mbalimbali na kuwapa mafunzo ya muda mfupi ya vitendo kuhusu Kanuni Bora za Kilimo ambazo watazitumia Vijijini kwao mara wanapomaliza mafunzo hayo na kusaidia Wanavijiji wengine. Vijana hawa wanaitwa Waganikazi. Hii ni hatua ya kupongezwa na kuungwa mkono na kila mpenda Kilimo. Naupongeza sana Uongozi wa Mkoa wa Kigoma kwa Ubunifu huu na Vijana walioitikia wito huo. Natoa wito kwa Mikoa mingine kuiga mbinu za Mafunzo ya Waganikazi hao na kuzitekeleza katika Mikoa yao.

39. Mheshimiwa Spika, Utafiti umeendelea kupewa umuhimu mkubwa katika kuendeleza Kilimo katika nyakati hizi ambazo Dunia inashuhudia mabadiliko makubwa ya Tabianchi. Vituo vyetu vya utafiti vya mazao ya Kilimo viliendesha tafiti mbalimbali na kugundua aina mpya za mbegu bora zikiwemo nyanya, maharage, pamba na mahindi. Vilevile, Miradi 55 ya Utafiti iliendelea kutekelezwa chini ya Mfuko wa Utafiti ambao unatekelezwa Kikanda. Tafiti hizo zinawahusisha Wakulima, Wagani, Wasambazaji Pembejeo, Mashirika yasiyo ya Kiserikali na Watafiti wenyewe kwa lengo la kutoa na kusambaza teknolojia zenye ubora. Natoa wito kwa Watafiti na Vituo vya Utafiti kujizatiti kutafiti mbegu bora na kusambaza matokeo ya tafiti zao kwa Wakulima, Wafugaji na Maafisa Ugani. Aidha, Viongozi wawe na mashamba ya mfano ili kuongeza kasi ya usambazaji wa teknolojia zinazogunduliwa.

40. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali itaongeza usambazaji wa aina mbalimbali za Pembejeo za Kilimo ili Wakulima waweze kuongeza tija zaidi. Aidha, itahimiza matumizi ya Zana Bora za Kilimo ambapo Halmashauri za Wilaya Nchini zitanunua jumla ya Matrekta ya Mkono 1,628 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 10.6 na Matrekta Makubwa 55 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 2.2. Fedha hizi zimetengwa kwenye Bajeti za Halmashauri zetu. Vilevile, Mikoa ya Iringa, Kigoma, Mbeya, Morogoro, Rukwa na Ruvuma imepangiwa kupewa ruzuku ya Shilingi Bilioni 29.2 za Mpango wa Maendeleo ya Kilimo wa Wilaya (DADP’s) kama chachu ya kuongeza uzalishaji wa chakula katika Mikoa hiyo. Kama tulivyokubaliana katika Mkutano wa “KILIMO KWANZA”, kazi ya kusukuma Kilimo siyo ya Wizara ya Kilimo peke yake. Hili ni jukumu la Viongozi na Watendaji wote katika ngazi zote wakishirikiana na Wananchi wote. Kwa hiyo, sote tushikamane kuleta Mapinduzi ya Kilimo haraka iwezekanavyo.

Umwagiliaji
41. Mheshimiwa Spika, moja ya maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2005 ni kuweka kipaumbele zaidi katika Kilimo cha Umwagiliaji Maji, msisitizo ukiwa kwenye Miradi Midogo na ya Kati. Ili kutekeleza maelekezo hayo, katika mwaka 2008/2009, Serikali iliongeza kiasi cha Hekta 27,500 za Umwagiliaji na kuwezesha eneo lote lililoendelezwa kwa umwagiliaji hapa Nchini kufikia hekta 318,745. Aidha, kupitia DADP’s, Miradi ya Umwagiliaji 167 imejengwa, 94 imekarabatiwa, Visima vifupi 18 vimejengwa na jumla ya Pampu 84 zimenunuliwa na kugawanywa kwa Wakulima kwa ajili ya Umwagiliaji wa Mazao ya Bustani. Vilevile, jumla ya Miradi 141 ya Umwagiliaji imefanyiwa tafiti za maandalizi. Hali hii imefanya maeneo mengi ya Kilimo cha Umwagiliaji yaliyoboreshwa kuongeza uzalishaji na hivyo kuwa kichocheo cha kupiga vita umasikini na kuwaongezea Wananchi kipato. Katika maeneo ambayo Miundombinu ya Umwagiliaji imeboreshwa kumekuwepo na ongezeko la uzalishaji na kuweza kuvuna mara 2 hadi 3 ikilinganishwa na uzalishaji wa Kilimo cha kutegemea Mvua. Natoa wito kwa Maafisa Kilimo wa Halmashauri zote kuwasaidia Wakulima kuibua Miradi Midogo ya Umwagiliaji katika Wilaya zao kwani wanahitaji msaada katika kuibua Miradi mizuri na yenye matokeo ya haraka.

Mifugo
42. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kufanya jitihada za kutenga ardhi kwa ajili ya Mifugo ili kupunguza na hatimaye kumaliza migogoro inayotokea mara kwa mara kati ya Wakulima na Wafugaji. Hata hivyo, kumeendelea kuwepo kwa migogoro ya matumizi ya rasilimali mbalimbali hasa Ardhi, Maji na Malisho katika baadhi ya Wilaya. Serikali haipendi kuona migogoro hii ikiendelea kwani inapotokea huambatana na madhara makubwa ambayo wakati mwingine husababisha kupotea kwa mali za Wananchi, kupoteza maisha na kusababisha Majeraha kwa Watu. Ili kukabiliana na tatizo hilo, kuanzia mwaka 2006/2007 hadi 2008/2009, jumla ya Hekta 1,391,109.4 za Ardhi zimetengwa katika Vijiji 240 vya Wilaya 31 katika Mikoa 13 kwa ajili ya Mifugo. Natoa wito kwa Viongozi wote wa Mikoa na Wilaya kuongeza kasi ya kutenga maeneo kwa ajili ya Malisho ya Mifugo na kuhakikisha kwamba utengaji huo hauna madhara kwa mazingira. Aidha, Wakulima na Wafugaji wote Nchini waheshimu Haki na Mipaka ya kila mmoja ili waendelee kuishi kwa amani na kufanya shughuli zao za uzalishaji mali kwa uhakika. Serikali inathamini mchango wa Wakulima na Wafugaji na inaheshimu Haki zao za kufanya kazi za ujenzi wa Taifa.

Uvuvi
43. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Uvuvi imeendelea kuchangia ukuaji wa Uchumi wetu na kupunguza umasikini. Hata hivyo, Sekta hiyo inakabiliwa na tatizo kubwa la nyenzo duni na Uvuvi Haramu. Katika mwaka 2008/2009, Serikali imechukua hatua za kudhibiti na kupambana na Uvuvi Haramu kwa kufanya doria na kutoa elimu kuhusu athari za Uvuvi Haramu. Aidha, Zana Haramu nyingi zilikamatwa zikiwemo Nyavu zisizoruhusiwa, Makokoro, Mitumbwi na Boti. Vilevile, Meli kubwa ya Uvuvi (Tawariq 1) iliyokuwa ikivua kinyume cha Sheria katika Bahari Kuu ya Tanzania ilikamatwa na kukutwa na jumla ya Tani 294 za Samaki. Serikali imedhamiria kuona kwamba Rasilimali za Tanzania tulizopewa na Mwenyezi Mungu zinawanufaisha Wananchi wote na siyo wajanja wachache wanaotumia Uvuvi Haramu kuhujumu rasilimali tulizonazo. Napenda tena nichukue fursa hii kuwaonya wale wote wanaoendesha Uvuvi Haramu kwa njia yoyote ile, wawe wa Ndani au wa Nje waache. Doria zitaendelea kuimarishwa katika maeneo yote ya Nchi na wale watakaokamatwa watachukuliwa hatua kali za Kisheria.

44. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali itaendelea kuboresha Miundombinu muhimu ya Mifugo kama Maabara ya Mifugo, Majosho, Malambo na Minada. Aidha, itapima maeneo ya Wafugaji, kufanya Sensa ya Mifugo na kuimarisha Vituo vya Utafiti vya Mifugo. Vilevile, itaimarisha Miundombinu ya kupokelea, kuhifadhi, kusafirisha Samaki na Mazao ya Uvuvi, kudhibiti Uvuvi Haramu na kuhifadhi mazingira na kuimarisha shughuli za utoaji wa huduma za Ufugaji wa Samaki na ukuzaji wa Viumbe wengine kwenye Maji.

VIWANDA NA BIASHARA
45. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Viwanda na Biashara Nchini inaendelea kuimarika kutokana na juhudi za Serikali kuwajengea uwezo Wajasiriamali Wadogo kuanzisha Viwanda Vidogo na vya Kati na kuhimiza wenye Viwanda vikubwa kuongeza tija katika uzalishaji wa bidhaa. Katika mwaka 2008/2009, uzalishaji wa baadhi ya bidhaa umeongezeka kama vile saruji, chuma, nguo, vyandarua, sigara na vifaa vya plastiki. Pamoja na mafanikio hayo, Serikali imetoa mafunzo kwa Wajasiriamali 1,989 wa Viwanda Vidogo vya Usindikaji wa Vyakula na Wajasiriamali 6,224 wa bidhaa nyingine mbalimbali ili kuwapa ujuzi maalum wa kiufundi na Teknolojia mpya. Aidha, Serikali imekamilisha maandalizi ya Mkakati Unganishi wa Biashara (Tanzania Trade Integration Strategy) ambao unalenga kukuza Sekta ya Biashara na kujenga uwezo wa kiushindani wa Wafanyabiashara wa ndani. Utekelezaji wa Mkakati huo unatarajiwa kuongeza mauzo nje kwa kutumia rasilimali zilizopo na kutumia vizuri fursa kubwa za Biashara za Kikanda na Kimataifa tulizo nazo.

46. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008 thamani ya mauzo ya bidhaa nje yaliongezeka hadi kufikia Dola za Kimarekani Milioni 3,036.7 ikilinganishwa na Dola za Kimarekani Milioni 2,226.6 mwaka 2007, sawa na ongezeko la asilimia 36.4. Mwenendo huu wenye matumaini unatokana na jitihada zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi kutafuta Masoko ya Nje. Hata hivyo, bado ipo changamoto kubwa ya kutafuta Masoko zaidi, hasa katika Nchi za Ukanda wa Afrika ambapo kuna mahitaji makubwa ya bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania. Ni wazi Nchi hizo zina masharti rahisi ya kibiashara ikilinganishwa na Nchi Zilizoendelea. Hivyo, tuelekeze nguvu zetu kwenye Masoko ambayo yana viwango vya ubora tunavyovimudu, kwa kuwa Nchi Zilizoendelea wakati mwingine zinaweka vikwazo visivyo vya lazima kwa lengo la kupunguza bidhaa zetu hasa kutoka Nchi changa. Nina imani kuwa tukitumia vizuri mtaji wa Mahusiano mazuri ya Kidiplomasia tuliyonayo na Nchi nyingi za Afrika na kwingineko, tutakuwa na uwezo wa kufikia Masoko mengi na kuuza bidhaa nyingi zaidi.

47. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhamasisha uanzishwaji wa Maeneo Maalum ya uzalishaji kwa ajili ya uuzaji nje na Uwekezaji katika viwanda ndani ya maeneo hayo. Hadi sasa Mikoa 14 imeainisha maeneo maalum ya kuzalisha na kuuza bidhaa nje (Export Processing Zones and Special Economic Zones). Maeneo hayo yapo katika Mikoa ya Kigoma, Tanga, Pwani, Arusha, Mwanza, Kilimanjaro, Mara, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Morogoro, Kagera, Mbeya na Manyara. Mpango Mkakati wa miaka mitano wa kuendeleza maeneo hayo umeandaliwa kwa kushirikiana na Benki ya Dunia. Aidha, ujenzi wa miundombinu katika eneo maalum la uwekezaji la Benjamin William Mkapa Special Economic Zone lililoko Mabibo Jijini Dar es Salaam umekamilika. Eneo hili limewekewa miundombinu na huduma zote muhimu na Serikali. Natoa rai kwa Wafanyabiashara na Sekta Binafsi kwa ujumla wake kutumia kikamilifu fursa hizi ili kukuza Sekta ya Viwanda Nchini.

48. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali itapitia upya Sheria za Maeneo Maalum ya Kukuza Mauzo Nje ili kuandaa Sheria Unganishi itakayoboresha zaidi Mfumo wa usimamizi wa maeneo hayo na kuwawezesha Wawekezaji wa Sekta mbalimbali wanaolenga Soko la Ndani na Nje kuwekeza katika eneo moja. Vilevile, Serikali itaimarisha Mafunzo ya Ujasiriamali pamoja na kuhimiza kuanzishwa kwa Viwanda vya Usindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini ili kuongeza thamani ya bidhaa.

Utalii
49. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Utalii ina umuhimu mkubwa katika Uchumi wetu hasa katika kuiletea Nchi yetu Fedha za Kigeni. Utalii unachangia asilimia 28 ya Mapato ya Fedha za Kigeni yatokanayo na huduma zitolewazo nje ya Nchi. Katika mwaka 2008/2009, Serikali imeanza zoezi la kupanga Hoteli katika Madaraja na kuhakikisha zinakuwa katika hali ya unadhifu kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005. Zoezi hilo limeanzia Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na kazi itaendelea kwa Mikoa ya Arusha, Manyara na sehemu nyingine. Vilevile, maeneo ya Fukwe kwa ajili ya Uwekezaji yalibainishwa katika Wilaya za Pangani, Tanga, Mkinga, Muheza, Lindi na Kilwa. Serikali pia, iliendelea kupanua wigo wa Utalii kwa kuainisha aina nyingine za Utalii kama vile Utalii wa Mikutano, Fukwe za Bahari, Ekolojia na Malikale.

50. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali itaweka mkazo katika kutangaza zaidi vivutio vyetu na kutafuta masoko mapya. Aidha, itaendelea kutangaza Utalii wa Ndani, Utalii wa Mikutano na kuboresha viwango vya huduma zitolewazo kwa Watalii. Serikali pia, itaongeza juhudi zaidi katika kutangaza Utalii wa Utamaduni na mambo ya Kale kama vile, Miji Mikongwe ya Kilwa na Mikindani ili iweze kuvutia Watalii wengi zaidi.

NISHATI NA MADINI

Nishati
51. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Nishati bado ina changamoto kubwa katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa Umeme katika Gridi ya Taifa. Hali hii inasababishwa na Miundombinu chakavu inayohitaji ukarabati wa mara kwa mara. Pamoja na hali hiyo, mahitaji ya umeme ni makubwa kuliko uzalishaji na yanaendelea kukua. Ili kuendana na kasi ya ukuaji huo, Serikali imeandaa Mpango wa muda mrefu, kati na mfupi wa kuimarisha Sekta ya Nishati hapa Nchini. Miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na kukarabati na kununua mitambo mipya na kukamilisha mradi wa umeme wa Tegeta/Salasala wa MW 45. Katika mwaka 2009/2010, Serikali itaimarisha Gridi ya Taifa, itaendelea na ukarabati wa Mitambo iliyopo na kununua Jenereta mpya kwa ajili ya maeneo yasiyokuwa na umeme wa Gridi. Aidha, Serikali itaandaa Programu ya Kupunguza Matumizi ya Umeme, hususan, Viwandani na Majumbani ili kupata umeme wa ziada kwa watumiaji wengine.

Madini
52. Mheshimiwa Spika, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005 imeelekeza kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuimarisha usalama migodini. Katika kutekeleza maelekezo hayo, Serikali imetenga maeneo katika sehemu mbalimbali Nchini likiwemo eneo lenye Hekta 4,000 huko Winza Wilayani Mpwapwa. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Wachimbaji Wadogo imeanza kuweka Utaratibu wa Uchimbaji Salama unaozingatia Sheria, Kanuni, uhifadhi wa mazingira na Uchimbaji unaotumia Teknolojia ya Kisasa. Mafunzo maalum kuhusu masuala hayo yameanza kutolewa kwa awamu. Awamu ya Kwanza ya mafunzo hayo yalifanyika mwezi Mei 2009, kwa Wachimbaji Wadogo wa Wilaya ya Geita. Serikali pia, imeanza mchakato wa kuaandaa mapendekezo ya Sheria ya Usonara na Uongezaji Thamani ya Madini ambayo itaweka mazingira ya kuwezesha kuongeza thamani ya Madini yetu kabla ya kuuza nje kwa bei kubwa zaidi. Utaratibu huu utaongeza Pato la Taifa na Ajira kwa Wananchi.

53. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali itapitia upya Sera na Sheria ya Madini ambayo itatilia maanani mapendekezo yaliyotolewa na Wadau mbalimbali ikiwemo Kamati ya Jaji Mark Bomani. Serikali pia, itaendelea kuboresha uchimbaji mdogo kwa lengo la kuinua kipato cha Wachimbaji Wadogo na Uchumi kwa ujumla. Aidha, itatoa mafunzo yanayohusu njia salama za uchimbaji na kuwashawishi wajiunge katika Vikundi ili waweze kupata mitaji kwa urahisi. Nichukue tena fursa hii kutoa wito kwa Wachimbaji Wadogo kufanya shughuli zao kwa makini na uangalifu na washirikiane na Serikali katika jitihada inazofanya za kuimarisha na kuboresha usalama katika migodi.

UJENZI NA MAWASILIANO

Barabara
54. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kujenga na kuboresha mtandao wa barabara nchini kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005. Lengo ni kuunganisha Nchi nzima na mtandao mzuri wa barabara zinazopitika wakati wote. Pamoja na mahitaji makubwa ya Barabara nzuri, ujenzi wake ni wa gharama kubwa na una mchakato mrefu kuanzia upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na ujenzi wenyewe. Katika mwaka 2008/2009, ujenzi wa baadhi ya Barabara Kuu na za Mikoa ulikamilika na ujenzi wa Barabara nyingine nyingi upo katika hatua mbalimbali. Serikali itaendelea kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na kutangaza zabuni za ujenzi pamoja na ukarabati wa Barabara Kuu na za Mikoa. Nina uhakika kwamba ujenzi wa barabara hizo utakapokamilika, utafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa Wananchi wa maeneo hayo na Watanzania kwa ujumla.

55. Mheshimiwa Spika, tuna kazi kubwa ya ujenzi wa Barabara lakini pia namna ya kuzitunza. Barabara zetu zikiwa nzuri zitarahisisha mazao mengi ya Wakulima kupelekwa kwenye masoko ya Ndani na Nje na wao kupata bei nzuri na ari ya kuzalisha zaidi. Hivyo, ni jukumu letu sote kujenga na kutunza vizuri Barabara hizo. Matatizo ya kukarabati Barabara mara kwa mara yatapungua kama Teknolojia sahihi na Viwango vya Kitaalamu vitafuatwa katika hatua zote za ujenzi wa Barabara zetu. Natoa wito kwa Makandarasi kuzingatia Viwango vya Ubora katika ujenzi wa Barabara na kuzikamilisha kwa wakati. Aidha, Mamlaka husika kwa kushirikiana na Wananchi zisimamie kikamilifu utunzaji wa Barabara hizo.

Vivuko
56. Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuboresha Vivuko mbalimbali hapa Nchini kwa kuvifanyia ukarabati vilivyochakaa na kununua vipya. Katika mwaka 2008/2009, Kivuko kikubwa cha MV Magogoni (Dar es Salaam) kilianza kufanya kazi. Kivuko hiki kilizinduliwa na Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 4 Juni 2009. Vivuko vya MV Kigamboni (Dar es Salaam) na MV Sengerema (Mwanza) vinaendelea kufanyiwa ukarabati mkubwa. Katika mwaka 2009/2010, Serikali itakamilisha kutengeneza Vivuko vinne vya Musoma - Kinesi, Rugezi - Kisorya, Utete na Mto Pangani. Aidha, Vivuko vipya vya Kilambo (Mtwara), Msanga Mkuu (Mtwara) na Rusoma (Ngara) vitanunuliwa.

Viwanja vya Ndege
57. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na juhudi za kuboresha Sekta ya Uchukuzi ili kuongeza ufanisi na kuondoa kero mbalimbali zinazowakabili Wananchi. Moja ya kazi zilizofanyika ni uboreshaji, upanuzi na matengenezo ya Viwanja vya Ndege. Katika mwaka 2008/2009, Serikali iliendelea na Awamu ya Pili ya ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Mwanza umekamilika na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe unaendelea. Katika mwaka 2009/2010, Serikali itaboresha Viwanja vya Ndege vya Ziwa Manyara, Arusha, Tabora, Shinyanga na Musoma. Aidha, Mitambo mbalimbali ya kisasa kwa ajili ya ukaguzi wa abiria na mizigo na ya kutoa taarifa za safari za ndege itafungwa katika Viwanja vya Ndege vya Mwanza na Julius Nyerere.

Mawasiliano
58. Mheshimiwa Spika, kutokana na kasi ya kukua kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na umuhimu wa kuwa na miundombinu ya uhakika ya mawasiliano na yenye gharama nafuu, mradi wa ujenzi wa Mkongo wa Taifa ulianza rasmi mwezi Februari 2009. Mkongo huo wa Taifa unatarajiwa kuunganisha Makao Makuu ya Mikoa na Wilaya zote Tanzania Bara na Zanzibar. Mradi huo utakapokamilika utaifanya Tanzania kuwa kitovu cha mawasiliano ya Kikanda na Kimataifa kutokana na fursa yake ya kijiografia ya kuzungukwa na Nchi nyingi ambazo hazijapakana na Bahari. Sambamba na hatua hiyo, Serikali imekamilisha taratibu za kuanzisha Mfuko wa Huduma za Mawasiliano ambao unalenga kusaidia kufikisha huduma za Mawasiliano ya Simu na Internet hadi Vijijini, hasa sehemu ambazo hazina mvuto kibiashara. Nitumie fursa hii kuyapongeza Makampuni yote ya Simu kwa jitihada kubwa za kupanua kwa kasi huduma za mawasiliano ya simu Mijini na Vijijini.

59. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali itaendelea kuimarisha huduma za Mawasiliano Nchini ikiwemo huduma za Posta. Aidha, itafanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

ARDHI NA MAENDELEO YA MAKAZI

Ardhi
60. Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 ili kuwawezesha Watanzania wengi kutumia ardhi kama dhamana ya kupata mikopo. Ardhi pia ni Rasilimali muhimu kwa maendeleo ya Sekta nyingine. Katika mwaka 2008/2009, Serikali iliendelea kutoa Hati za Kumiliki Ardhi na Vyeti vya Ardhi ya Vijiji kwa Wananchi. Utoaji wa Hatimiliki umerahisishwa kwa kuanzisha Ofisi za Makamishna wa Ardhi Wasaidizi katika Kanda sita ambazo zitatoa huduma kwa Mikoa yote. Majukumu ya Ofisi hizo za Kanda ni pamoja na utoaji wa hati za Ardhi hasa zilizokuwa zinawasilishwa kwa Kamishna wa Ardhi kwa ajili ya kusainiwa. Utaratibu huu umeongeza kasi ya utayarishaji na Usajili wa Hatimiliki. Katika mwaka 2009/2010, Serikali itaziboresha Ofisi za Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Kanda kwa kuongeza Watumishi na vitendea kazi.

Upimaji wa Vijiji na Viwanja Mijini
61. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kupima Viwanja Mijini na mipaka ya Vijiji. Tangu zoezi la Upimaji wa Vijiji lianze kutekelezwa, jumla ya Vijiji 9,500 vimepimwa kati ya Vijiji vipatavyo 11,000 Nchini kote. Katika kipindi cha mwaka 2008/2009, Serikali ilipima Vijiji 450 na Ardhi za Wananchi sehemu mbalimbali Nchini. Aidha, kutokana na kufunguliwa Ofisi za Ardhi za Kanda, kasi ya kuandaa na kutoa Vyeti vya Ardhi ya Vijiji imeongezeka ambapo jumla ya Vyeti vya Ardhi ya Vijiji 910 vilitolewa katika Wilaya 25 Nchini. Vilevile, Serikali imeendelea kupunguza uhaba wa Viwanja kwenye Miji Mikubwa inayopanuka kwa kasi kama Jiji la Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya kwa kupima Viwanja vingi kwa mtindo wa kurejesha gharama za upimaji. Halmashauri za Miji na Wilaya zinahimizwa kutekeleza Miradi ya Upimaji wa Viwanja kwa kuzingatia dhana ya kuchangia gharama kama ilivyofanyika katika Jiji la Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya, na Manispaa ya Dodoma na Morogoro.

MAENDELEO YA ELIMU

Elimu ya Msingi
62. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali iliendelea na utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM-II) ambao utamalizika mwaka 2011. Mpango huu unaendeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Awamu ya Kwanza pamoja na kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza hususan upungufu wa Walimu, Vitabu vya Shule pamoja na uhaba wa Nyumba za Walimu. Chini ya Mpango huu, idadi ya Shule za Msingi za Serikali imeongezeka kutoka 15,122 mwaka 2007 hadi Shule 15,257 mwaka 2008. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Wananchi na Wadau mbalimbali wa Elimu imeboresha kwa kiasi kikubwa mazingira na miundombinu mbalimbali ya Shule za Awali na Msingi. Ili kuinua zaidi ubora wa Elimu ya Msingi Nchini, napenda kuzikumbusha Halmashauri zote kuendelea kuimarisha usimamizi na kuelimisha Jamii na Kamati za Shule ili watambue kuwa Mpango wa kuboresha Shule za Awali na Msingi ni endelevu na hivyo ni lazima wajihusishe nao kikamilifu.

Chakula cha Mchana kwa Wanafunzi
63. Mheshimiwa Spika, Shule zetu za Awali na Msingi zinakabiliwa na changamoto ya kuwawezesha Watoto kupata chakula cha mchana Mashuleni. Tafiti zilizofanyika katika Mikoa ya Dodoma, Manyara, Singida na Arusha zimeonyesha kuwa Shule zinazotoa chakula cha mchana kwa Wanafunzi zimepata mafanikio ya kupunguza utoro Mashuleni na kuongeza kiwango cha ufaulu. Hata hivyo, fedha za kununua chakula hicho zimekuwa zinapatikana kwa kufanya matembezi ya hisani ambayo yalianzishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani. Lengo la matembezi hayo ni kutunisha Mfuko wa Kuondoa Njaa Mashuleni unaochangiwa na Wahisani mbalimbali.

64. Mheshimiwa Spika, jambo linalosikitisha ni kwamba kutokana na matembezi hayo, inaonekana baadhi ya Wazazi wamesahau wajibu wao wa kuhakikisha Watoto wetu wanapata mlo wa mchana wawapo Shuleni. Kama Mzazi, ninaamini kuwa Wajibu wa kwanza ni kuwalea na kuwakuza Watoto katika Maadili na Tabia njema pamoja na kuwapatia chakula bora. Siamini kuwa kama Mzazi anaweza kumpa Mtoto chakula cha asubuhi au jioni atashindwa kuchangia chakula cha Mtoto wake mchana pale Shuleni. Ninawasihi Wazazi wote wasikwepe wajibu wao wa kuhakikisha Watoto wao wanapata mlo wa mchana wawapo Mashuleni. Hivyo, natoa wito kwa Viongozi wa Shule kukaa pamoja na Wazazi ili kuona njia bora zaidi ya kuhakikisha Wanafunzi wanapata chakula cha mchana wawapo Mashuleni.

Elimu ya Sekondari
65. Mheshimiwa Spika, Wananchi wameitikia kwa ari kubwa wito wa Serikali wa kujenga Shule za Sekondari chini ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES). Hatua hii imeongeza nafasi kwa Wanafunzi wengi wanaohitimu Elimu ya Msingi kuendelea na Elimu ya Sekondari. Idadi ya Shule za Sekondari za Serikali imeongezeka kutoka Shule 2,806 mwaka 2007 hadi 3,039 mwaka 2008. Idadi ya Wanafunzi waliojiunga na Kidato cha Kwanza katika Shule za Serikali imeongezeka kutoka Wanafunzi 401,011 mwaka 2007 hadi 528,149 mwaka 2008. Vilevile, idadi ya Wanafunzi waliojiunga Kidato cha 5 imeongezeka kutoka Wanafunzi 21,789 mwaka 2007 hadi 25,240 mwaka 2008. Ongezeko hili limefanya idadi ya Wanafunzi wote wa Shule za Sekondari Nchini kuanzia Kidato 1 – 6 kuongezeka kutoka Wanafunzi 1,205,510 mwaka 2007 hadi kufikia 1,222,403 mwaka 2008.

66. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali itaendelea kuongeza ubora katika utoaji wa Elimu ya Msingi, Sekondari, Vyuo vya Ualimu na Mafunzo ya Ufundi. Juhudi zitaelekezwa katika kuongeza na kuimarisha Miundombinu muhimu ya Shule za Msingi na Sekondari kama vile ujenzi wa Madarasa, Maabara, Nyumba za Walimu, Maktaba na ununuzi wa Madawati na Vitabu vya kujifunzia na kufundishia. Serikali pia, itaongeza idadi ya Walimu Tarajali ili kukidhi mahitaji yanayotokana na ongezeko la Wanafunzi katika ngazi zote za Elimu na kuimarisha matumizi ya Vituo vya Walimu ili kuboresha ufundishaji hasa katika Masomo ya Sayansi, Lugha na Hisabati.

Elimu ya Juu
67. Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Wadau imeendelea kupanua Elimu ya Juu kwa kujenga na kukarabati Vyuo vya Elimu ya Juu. Kazi nyingine ni kuongeza ubora wa miundombinu ya Vyuo vilivyopo ili kukidhi mahitaji ya Elimu ya Juu ambayo yanaongezeka mwaka hadi mwaka. Idadi ya Vyuo Vikuu vya Serikali imeongezeka kutoka Vyuo 8 mwaka 2005 hadi 11 mwaka 2008. Aidha, Vyuo Vikuu Binafsi vimeongezeka kutoka Vyuo 18 mwaka 2005 hadi 21 mwaka 2008.

68. Mheshimiwa Spika, Vyuo Vikuu vya Serikali na Binafsi vinavyoendelea kujengwa vimeongeza fursa kwa Wanafunzi kujiunga na Elimu ya Juu. Idadi ya Wanafunzi katika Vyuo vya Elimu ya Juu imeongezeka kutoka Wanafunzi 49,967 mwaka 2007 hadi kufikia 82,529 mwaka 2008. Vilevile, Serikali imeendelea kutoa mikopo ya kugharamia Wanafunzi wa Elimu ya Juu ambapo katika mwaka 2008 Wanafunzi 56,071 walipewa mikopo ikilinganishwa na 47,554 mwaka 2007. Sehemu kubwa ya mikopo hiyo imetolewa kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu wanaosoma Masomo ya Ualimu, Uhandisi, Sayansi, Kilimo, Tiba ya Binadamu na Tiba ya Wanyama.

69. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali itaendelea kukarabati na kupanua Vyuo vya Elimu ya Juu vya Umma ili Wanafunzi wengi zaidi waweze kujiunga na Vyuo hivyo. Vilevile, Serikali itaongeza kasi ya ujenzi wa Maabara ya Sayansi, Kumbi za Mihadhara, Hosteli, ukarabati wa Miundombinu, upanuzi wa Maktaba na kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya Kisasa (TEKNOHAMA) kwa ajili ya kujifunzia na kufundishia. Serikali pia, itaandaa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Juu na Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi ambayo utekelezaji wake utaanza mwaka 2010. Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Wananchi na Wadau wetu wote wa Maendeleo kwa kushirikiana kikamilifu na Serikali katika kuendeleza Sekta ya Elimu Nchini.

HUDUMA ZA AFYA NA MAJI

Mpango wa Taifa wa Chanjo
70. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali imepata mafanikio makubwa katika kutoa huduma za Chanjo Nchini. Viwango vya Chanjo vimeongezeka na kufikia zaidi ya asilimia 80 kwa Chanjo zote. Katika kipindi hicho, Serikali iliendesha Kampeni ya kutokomeza Ugonjwa wa Surua Nchini kwa Kuchanja Watoto 10,567,104 wenye umri kati ya miezi 9 hadi miaka 10. Aidha, Chanjo ya Polio ilitolewa katika Wilaya 18 za Mipakani na zenye Viashiria vya kuambukiza Polio na Watoto 1,459,162 walipata chanjo hiyo. Hatua hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza Vifo vya Watoto wenye umri chini ya miaka mitano kutoka Vifo 112 kwa kila Watoto 1,000 waliozaliwa hai mwaka 2005 hadi Vifo 91 mwaka 2008. Lengo la Milenia ni kupunguza Vifo vya Watoto hadi kufikia Watoto 54 kwa kila Watoto 1,000 ifikapo mwaka 2015. Nina hakika kwa jitihada zinazofanywa na Serikali tutafikia malengo hayo.

71. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali itaimarisha huduma za Chanjo kwenye Kliniki zote za huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto, huduma za Mkoba na Kliniki Tembezi. Aidha, itatekeleza Mpango Maalum wa Kumfikia kila Mtoto katika Wilaya 48 ambazo zimeonekana kuwa na kiwango cha chini cha Chanjo.

Malaria
72. Mheshimiwa Spika, Ugonjwa wa Malaria bado unasababisha Vifo vingi kwa Wananchi wetu. Ili kukabiliana na Ugonjwa huo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali. Katika mwaka 2008/2009, Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia kwa ajili ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria ulitoa fedha kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 90.5 kwa ajili ya ununuzi wa Dawa Mseto na kuelimisha watoa huduma wote Nchini. Dawa hizo zinatolewa katika Vituo 4,921 vya Tiba Nchini vikiwemo vya Serikali na Binafsi. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi walitoa Vyandarua vyenye Viuatilifu kwa bei nafuu kwa Wanawake Wajawazito na Watoto chini ya umri wa miaka mitano waliohudhuria Kliniki ya Mama na Mtoto kupitia Mpango wa Hati Punguzo. Serikali pia, ilipata kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 113 kupitia Mfuko huo kwa ajili ya kuwezesha kila Kaya yenye Watoto chini ya umri wa miaka mitano kupata Vyandarua Viwili vyenye Viuatilifu kwa ajili ya Kinga dhidi ya Malaria. Katika mwaka 2009/2010, Serikali itaendelea na ugawaji wa Vyandarua vyenye Viuatilifu bila malipo kwa Watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Zaidi ya Vyandarua Milioni 14 vitagawanywa kwa kila Kaya yenye Walengwa na kila Kaya itapata Vyandarua Viwili.

Maji
73. Mheshimiwa Spika, Dira ya Taifa ya Maendeleo, imeweka lengo la kuwapatia Wananchi wote waishio Vijijini na Mijini huduma ya Maji Safi na Salama ifikapo mwaka 2025. Katika mwaka 2008/2009, utoaji wa huduma za Majisafi Mijini umeboreshwa kwa kukarabati na kupanua Miundombinu ya Mifumo ya Majisafi katika sehemu mbalimbali Nchini. Moja ya Miradi iliyokamilika ni ujenzi wa Mradi wa kutoa Maji Ziwa Viktoria kwenda Miji ya Kahama na Shinyanga pamoja na Vijiji 54 vilivyo kando ya Mabomba Makuu. Mradi huu ulizinduliwa na Mheshimwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 30 Mei, 2009. Huu ndiyo Mradi Mkubwa wa maji katika Historia ya Nchi yetu ambao umegharamiwa na Serikali yetu kwa kutumia fedha zetu wenyewe. Hili siyo jambo dogo, kwa kuwa linaonyesha tukidhamiria na kuweka kipaumbele tunaweza kufanya mambo makubwa na ya manufaa kwa Nchi yetu.

74. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma za Maji Vijijini kwa kujenga, kupanua na kukarabati Miradi ya Maji Vijijini na kuchimba Visima. Mafanikio yaliyopatikana katika uboreshaji wa huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ni pamoja na ujenzi wa Vituo vya Kuchotea Maji 1,657 vyenye uwezo wa kuhudumia Wananchi 394,250; jumla ya Visima 407 vilichimbwa na Wananchi 379,609 walihamasishwa kuhusu Usafi wa Mazingira na Elimu ya Afya. Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa kutekeleza Programu Ndogo ya Uboreshaji wa Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira katika Vijiji Kumi vilivyoainishwa kwa kila Wilaya.

Habari NA Michezo
Habari
75. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Habari Nchini imeendelea kukua na kutoa mchango mkubwa katika kuelimisha Jamii kuhusu mambo mbalimbali katika nyanja za Siasa, Demokrasia, Utawala Bora, Uchumi, Maendeleo ya Jamii, Burudani na kutoa habari za matukio mbalimbali. Hadi sasa Vituo 52 vya Redio na 27 vya Televisheni vimesajiliwa. Aidha, idadi ya magazeti na majarida yaliyosajiliwa imefikia 683. Hata hivyo, bado kuna changamoto ya kuimarisha usimamizi wa Vyombo vya Habari na upatikanaji wa habari usioridhisha hasa Vijijini. Ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali inapitia upya Sera ya Habari ya mwaka 2003 na kukamilisha Muswada wa Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari. Natoa wito kwa Wawekezaji katika Sekta ya Habari kujitokeza kutoa huduma hii katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa.

Michezo
76. Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza Sekta ya Michezo, Serikali imekamilisha Awamu ya Kwanza ya ujenzi wa Eneo Changamani la Michezo (Sports Complex) Jijini Dar es Salaam ambapo Viwanja vya Mpira wa Miguu na Riadha vyenye hadhi ya Olimpiki vimekamilika. Uwanja huo ulizinduliwa rasmi tarehe 15 Februari 2009 na Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Hu Jin Tao, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China. Ili kuendeleza taaluma ya michezo katika ngazi ya kati, Chuo cha Maendeleo ya Michezo cha Malya kitaimarishwa kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

ULINZI NA USALAMA
77. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali imeendelea kuliwezesha Jeshi la Ulinzi kuimarisha uwezo wake wa kulinda mipaka ya Nchi yetu pamoja na kuimarisha Amani na Utulivu baina ya Tanzania na Nchi nyingine Duniani na hasa Nchi jirani. Hali katika mipaka ya Nchi yetu ni shwari na Wananchi wako huru kutekeleza shughuli zao za kujiletea maendeleo. Watendaji wa Jeshi la Wananchi wamepatiwa mafunzo mbalimbali ya kuendeleza taaluma zao Ndani na Nje ya Nchi. Aidha, Jeshi limepatiwa Vitendea Kazi mbalimbali ili liweze kutekeleza wajibu wake kikamilifu, hususan kufanya Doria Mipakani, Baharini, kwenye Maziwa na kutoa misaada ya kukabiliana na Maafa au Majanga pindi yanapotokea.

78. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili liwe na taswira ya uzalishaji mali na kutoa mchango kwa Ulinzi wa Taifa. Vijana wa Kitanzania 6,500 wameendelea kupatiwa mafunzo mbalimbali katika Makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa. Lengo ni kufikisha Vijana 10,000 katika mwaka 2010/2011, ambapo Wahitimu wa Kidato cha Sita wataanza kuchukuliwa tena kwa mujibu wa Sheria. Vijana hao, zaidi ya kupata mafunzo ya awali ya Ulinzi na Usalama, watapewa mafunzo katika Stadi mbalimbali zikiwemo za Kilimo, Ufugaji na Ufundi wa aina mbalimbali kwa lengo la kuwafanya wawe na uwezo wa kujitegemea. Tunatarajia kuwa Vijana hao watakapomaliza mafunzo yao watakuwa chachu kwa Vijana wenzao katika kushiriki shughuli mbalimbali za uzalishaji mali Vijijini na Mijini na Ulinzi wa Taifa letu.

79. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2009/2010, Serikali itaendelea kulinda mipaka ya Nchi yetu pamoja na kuimarisha Amani na Utulivu Nchini. Serikali pia, itaimarisha na kuliongezea uwezo Jeshi la Wananchi kwa kulipatia Vifaa na Zana Bora za Kisasa; kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na Makazi; na kuimarisha upatikanaji wa huduma, mahitaji na Stahili kwa Wanajeshi. Aidha, itaimarisha jukumu la kulea Vijana wa Kitanzania katika Makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa na kuimarisha Ushirikiano wa Kijeshi na Kiulinzi na Nchi nyingine Duniani kupitia Jumuiya za Kimataifa, Kikanda na ushirikiano na Nchi moja moja.

80. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limeendelea kulinda Usalama wa Raia na Mali zao. Katika mwaka 2008/2009, jitihada kubwa ziliwekwa katika kuendesha Operesheni za Kudhibiti ongezeko la Ujambazi na vitendo vya uhalifu kwa kushirikiana na Wananchi. Kutokana na jitihada hizo Majambazi Sugu na Wahalifu wengi wamekamatwa. Hii imewezekana kutokana na ushirikiano wa karibu baina ya Vyombo mbalimbali vya Ulinzi na Usalama na Raia Wema kupitia dhana ya Ulinzi Shirikishi wa Jamii.

81. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali imeongeza Bajeti ya Jeshi la Polisi ili kuliwezesha kukabiliana na matukio mbalimbali ya uhalifu Nchini. Dhana ya Ulinzi Shirikishi wa Jamii kupitia Polisi Jamii itaimarishwa; kinachotakiwa ni kuimarisha ushirikiano na Wananchi katika kuwafichua Wahalifu tunaoishi nao, ili mafanikio tuliyoyapata yawe makubwa zaidi. Hivyo, natoa wito kwa Watanzania wote kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuimarisha Usalama, Utulivu na Amani katika maeneo tunayoishi. Sote tujivunie kuwa Walinzi imara wa Nchi yetu.

KAZI NA AJIRA

Ajira
82. Mheshimiwa Spika, Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2005 pamoja na masuala mengine, iliahidi kupatikana kwa ajira mpya zaidi ya Milioni Moja katika kipindi cha miaka mitano. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi na Umma zinatekeleza Mpango wa Taifa wa Kukuza Ajira pamoja na Programu mbalimbali za Kukuza Ajira na kuwezesha Wananchi Kiuchumi. Hatua hizi zimewezesha kuongeza Ajira Nchini. Hadi kufikia Mwezi Mei 2009, Ajira mpya zaidi ya Milioni 1.3 zilipatikana Nchini. Ajira hizi ni mbali ya zile zinazotokana na Ajira Binafsi katika Kilimo, Ufugaji na Uvuvi. Aidha, ili kuendelea kuongeza Ajira zaidi, Ofisi za Mikoa na Wilaya zimeelekezwa kuunda Kamati za Kukuza Ajira na kuteua Maafisa Waratibu wa Ajira katika ngazi za Mikoa, Wilaya na Kata. Naipongeza Mikoa ya Mtwara, Lindi na Morogoro kwa kuunda Kamati hizo. Natoa wito kwa Mikoa ambayo bado haijaunda Kamati hizo iongeze kasi ili iweze kukuza na kuratibu Ajira katika maeneo yao.

Kazi
83. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza wajibu wake wa kudumisha mahusiano mema mahali pa kazi, ili kuongeza tija. Ili kutekeleza wajibu huo, Bunge limepitisha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi mwezi Novemba 2008. Sheria hii inatoa utaratibu wa ulipwaji wa fidia kwa Wafanyakazi wanaoumia kazini pamoja na kuanzishwa kwa Mfuko wa Fidia. Aidha, Serikali imefanya kaguzi za kazi 277 katika maeneo mbalimbali ya kazi Nchini. Pia, imefanya utatuzi wa migogoro ya kikazi chini ya Sheria za Kazi Na. 6 na 7 za mwaka 2004, kwa mafanikio kwa kupunguza au kuondoa kero ya kulundikana kwa migogoro ya kikazi.

84. Mheshimiwa Spika, kati ya migogoro 7,303 iliyopokelewa katika kipindi cha Julai 2008 mpaka Mei 2009, migogoro 5,220 sawa na asilimia 72 imepatiwa ufumbuzi. Tume ya Usuluhishi na Uamuzi imesimamia uanzishwaji wa vyombo vya Ushirikishwaji wa Wafanyakazi kwa kuunda Mabaraza ya Wafanyakazi 170 katika Taasisi za Umma na za Binafsi. Tume imeendesha mafunzo ya kujenga uelewa juu ya matumizi sahihi ya Sheria mpya ya Kazi na Kanuni zake za mwaka 2007 ikiwa ni pamoja na kutafsiri Kanuni hizo kwa Lugha ya Kiswahili. Mafunzo haya yamefanyika katika Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya Tanzania Bara.

85. Mheshimiwa Spika, suala la migomo ya Wafanyakazi limekuwa likijitokeza mara kwa mara katika Makampuni, Viwanda na Mashirika humu Nchini. Pamoja na kwamba Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini imetoa haki kwa Wafanyakazi kugoma, migomo inapotokea sehemu za kazi hasa zile zinazohusika na utoaji wa huduma muhimu kwa jamii, inaleta athari nyingi kwa Wananchi, kusababisha hasara kubwa kwa Taasisi husika na Uchumi wa Nchi kwa ujumla. Vyanzo vya migomo hii ni mawasiliano duni kati ya Waajiri na Waajiriwa na wakati mwingine Wafanyakazi kutofuata taratibu za Kisheria za kudai haki zao. Serikali imekuwa ikishirikiana na Waajiri na Vyama vya Wafanyakazi kutafuta suluhisho la migogoro mbalimbali ili kuepusha migomo ambayo hatimaye huathiri huduma za kibiashara na kijamii. Nawasihi Wafanyakazi kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za kazi pamoja na kujadiliana na Waajiri pale wanapoona haki haitendeki. Aidha, Vyama vya Wafanyakazi, pamoja na wajibu wao wa kutetea maslahi ya Wafanyakazi, vinao wajibu mkubwa wa kuepusha migomo isiyo ya lazima. Nina imani tukikaa pamoja, tukizungumza na kujadiliana hatutafikia hatua ya kugoma kwa kuwa mijadala huleta suluhisho.

86. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali itaendeleza juhudi za kudumisha mahusiano mema mahali pa kazi ikiwa ni pamoja na kutatua mapema iwezekanavyo migogoro inayoibuka sehemu za kazi. Aidha, itaendelea kuhakikisha kuwa juhudi zilizoanzishwa za kuongeza ajira nchini zinaendelezwa.

Ushirikiano wa Kimataifa
87. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, uhusiano wa Nchi yetu na Mataifa mengine Duniani pamoja na Mashirika ya Kimataifa na Kikanda umeimarika kwa kiwango kikubwa. Katika kipindi hicho, tumeshuhudia Viongozi Mashuhuri na Wakuu wa Nchi mbalimbali, wakiambatana na Wawekezaji na Wafanyabiashara kutembelea Tanzania kwa malengo mbalimbali ya kiuchumi na kuimarisha ushirikiano wetu. Maeneo ya Kipaumbele ambayo Viongozi na Wawekezaji hao wameonyesha nia na dhamira ya kukuza ushirikiano ni katika Nyanja za kilimo, elimu, utalii, viwanda, miundombinu na kukuza mauzo nje. Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa Tanzania ina mahusiano mazuri na Mataifa yote Duniani na Mashirika ya Kimataifa na Kikanda, ikiwemo Umoja wa Afrika.

88. Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii, kutambua juhudi kubwa zilizofanywa na Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika. Ni dhahiri alipokuwa Mwenyekiti wa Umoja huo, Mheshimiwa Rais aliwezesha Nchi yetu kung’ara katika medani za Siasa za Bara la Afrika na Mataifa mengine Duniani. Vilevile, katika kipindi chake cha Uongozi, Umoja wa Afrika ulipata mafaniko makubwa ya kushughulikia changamoto nyingi za Kisiasa, Kiuchumi na Kijamii zinazolikabili Bara la Afrika katika nyanja mbalimbali, zikiwemo za Ulinzi, Usalama, Ushirikiano na Kanda nyingine pamoja na kutafuta ufumbuzi wa migogoro iliyopo katika Bara hili.

89. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali itaendelea kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje ambayo inasisitiza zaidi Diplomasia ya Uchumi. Aidha, uimarishaji wa Ofisi za Balozi za Tanzania zilizopo utapewa kipaumbele. Sambamba na hatua hiyo, Serikali itaangalia namna bora ya kuwawezesha Watanzania wanaoishi Ughaibuni (Diaspora) kushiriki kikamilifu katika kuchangia shughuli za Kiuchumi na Kijamii hapa Nchini.

Ushirikiano wa Afrika Mashariki

90. Mheshimiwa Spika, kutokana na mikakati ambayo Serikali ilijiwekea katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005, Tanzania imeendelea kunufaika kutokana na kuanzishwa kwa Umoja wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Biashara baina ya Nchi Wanachama imeshamiri na inaongezeka mwaka hadi mwaka. Mfano, mauzo ya bidhaa za Tanzania katika Soko la Afrika Mashariki yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani Milioni 173.1 mwaka 2007, hadi kufikia Dola za Kimarekani Milioni 315.5 mwaka 2008, sawa na ongezeko la asilimia 82.3. Inatarajiwa kuwa mauzo ya bidhaa za Tanzania ndani ya Soko hili la Afrika Mashariki yataongezeka zaidi kuanzia mwezi Julai 2009 ambapo Nchi za Burundi na Rwanda zitaanza kutekeleza Itifaki ya Umoja wa Forodha.

91. Mheshimiwa Spika, Nchi hizi tayari zimekubali kupunguza Ushuru wa Forodha kwa asilimia 80 kwa bidhaa kutoka Tanzania ikiwa ni hatua za utekelezaji wa Itifaki hiyo. Vilevile, ikumbukwe kuwa Nchi za Rwanda na Burundi ni Soko kubwa na muhimu kwa bidhaa nyingi kutoka Tanzania kama vile saruji, chumvi, samaki wabichi na wakavu, mpunga na mchele, kahawa, mahindi, mtama, mafuta ya mawese na nguo zitokanazo na pamba. Hivyo, natoa wito kwa Wafanyabiashara wa Tanzania kujiandaa na kuchangamkia fursa za kibiashara zinazopatikana katika Nchi hizo bila kuchelewa.

92. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali itaendelea kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya uundaji wa Soko la Pamoja la Afrika Mashariki ambalo litafungua fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Aidha, itashirikiana na Wadau mbalimbali kukamilisha maandalizi ya Mkakati wa Kitaifa na Mikakati ya kisekta ili kuhakikisha kuwa Tanzania imejipanga vizuri kunufaika ipasavyo na fursa za Soko la Pamoja.

MAMLAKA YA USTAWISHAJI MAKAO MAKUU

93. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Mamlaka ilikamilisha Mradi Mkubwa wa Upigaji Picha za Anga kwa eneo la Hekta 276,910 la Mji Mkuu linalojumuisha eneo lote la Kiutawala la Wilaya ya Dodoma Mjini. Aidha, imekamilisha Mpango wa ujenzi wa Mji Mpya wa kisasa wa Iyumbu utakaohuisha maendeleo yote ya Kimji yanayotosheleza kasi ya kukua kwa mahitaji ya makazi na shughuli za kiuchumi na huduma za kijamii. Mamlaka pia, ilipima Viwanja 4,000 na kukamilisha uandaaji wa mipango ya uendelezaji yenye jumla ya Viwanja vya Makazi na shughuli nyingine vipatavyo 20,000. Viwanja hivyo vitapimwa katika maeneo ya Ntyuka, Mkonze, Nzuguni, Ndachi, Msalato na Kiterera.

94. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu itaanza mapitio ya Mpango Kabambe wa Mji wa Dodoma ili kuurekebisha na kuufanya uendane na mabadiliko makubwa yaliyopo pamoja na mahitaji ya ukuaji wa Mji. Aidha, itapima Viwanja katika maeneo mbalimbali ambayo yamekwisha tayarishiwa Michoro ya Viwanja, kujenga Miundombinu katika maeneo ya Ipagala, Area E, Chang’ombe, Mwangaza na Ilazo. Pia, itaanza ujenzi wa Awamu ya Kwanza ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Mjini Dodoma.

MPIGACHAPA MKUU WA SERIKALI

95. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Idara ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali ilichapisha kwa wakati Nyaraka na Hotuba za Bunge la Bajeti za mwaka 2008/2009, Chaguzi Ndogo za Wabunge na Madiwani na Nyaraka nyingine za uendeshaji wa shughuli za Serikali. Ili kuongeza ufanisi, Serikali imenunua mtambo mpya wa kisasa utakaosaidia katika kuboresha kazi za uchapaji wa Nyaraka za Serikali. Lengo ni kuhakikisha kwamba Nyaraka zote za Serikali zinachapishwa na Mpigachapa Mkuu wa Serikali. Katika mwaka 2009/2010, Idara itakuwa na jukumu kubwa la kuchapisha Nyaraka za Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Ninapenda kuwahimiza Watendaji Wakuu wote Serikalini kuhakikisha kuwa wanatumia ipasavyo Idara hiyo katika uchapishaji wa Nyaraka za Serikali ili kudhibiti uvujaji siri wa Nyaraka na maamuzi mbalimbali ya Serikali.

MASUALA MTAMBUKA

Ushiriki wa Wanawake katika Uongozi
96. Mheshimiwa Spika, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, imeweka malengo ya kuondolewa kwa ubaguzi wa aina yoyote wa jinsia katika uongozi na utoaji maamuzi. Ili kufikia malengo hayo, Serikali imeandaa mkakati wa kuwajengea uwezo na kuwapatia fursa Wanawake kushiriki katika ngazi mbalimbali za uongozi. Aidha, Serikali imeendelea kuingiza masuala ya jinsia kwenye Sera, Mipango na Bajeti. Vilevile, imetoa mafunzo ya uelewa wa masuala ya Jinsia kwa Viongozi na Watendaji Wakuu wa Serikali wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge. Katika mwaka 2009/2010, Serikali itaendelea kukamilisha Mkakati wa kuongeza ushiriki wa Wanawake kufikia asilimia 50 katika Uongozi na maamuzi, pamoja na kuendelea kutoa mafunzo ya uingizwaji wa masuala ya jinsia katika Sera, Mipango na Bajeti.

Udhibiti wa UKIMWI
97. Mheshimiwa Spika, UKIMWI umeendelea kuwa tishio la Taifa na madhara yake yataendelea kuathiri Uchumi wa Nchi. Jitihada za kupunguza maambukizi mapya na kuwepo kwa mpango wa matunzo na matibabu kwa Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI yamechangia katika kupunguza kasi ya madhara ya UKIMWI Nchini. Hata hivyo, Watanzania takriban Milioni 2 wanaishi na Virusi vya UKIMWI na bado maambukizi mapya yanaongezeka. Idadi hii bado ni kubwa na ni changamoto kwetu sote; hivyo jitihada za dhati zinahitajika kutoka katika Sekta zote na Wananchi wote ili kudhibiti maambukizi mapya na kuhakikisha kwamba huduma zaidi zinapatikana kwa wanaoishi na Virusi vya UKIMWI.

98. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali iliendelea kuwezesha Sekta mbalimbali kifedha na kitaalamu katika kupanga na kutekeleza afua za kuthibiti UKIMWI sehemu za kazi. Aidha, ilifanya mapitio ya Mkakati wa kwanza wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI na kuandaa Mkakati wa Pili wa mwaka 2008 – 2012. Mkakati huo umetoa mwongozo wa maeneo ya kipaumbele katika kudhibiti UKIMWI. Eneo mojawapo ni kuongeza juhudi za kupunguza maambukizi mapya hasa kwa kuwalenga Vijana wa miaka 15 – 24. Eneo lingine ni kuhakikisha Watanzania wote wanapata elimu kuhusu kuzuia maambukizi mapya, matunzo na matibabu. Katika mwaka 2009/2010, Serikali itapitia upya Sera ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI ya mwaka 2001, kusambaza kwa Wadau mbalimbali Mkakati Mpya wa Kudhibiti UKIMWI, na Matokeo ya Utafiti wa Viashiria vya UKIMWI.

Mapambano Dhidi ya Rushwa
99. Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa imeendelea kupambana na Rushwa kubwa na ndogo hapa Nchini. Katika kutimiza azma hiyo, Taasisi imeendesha tafiti 10 ndogo za kubaini mianya ya rushwa katika ngazi za Mikoa na kutoa mapendekezo Serikalini. Vilevile, imefanya uchunguzi kuhusu Rushwa Kubwa zilizoripotiwa na kuwasilisha mapendekezo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kwa hatua zaidi. Aidha, Taarifa 1,338 za Rushwa kutoka kwa Wananchi zimepokelewa na kufanyiwa kazi ambapo jumla ya kesi 321 ziliendeshwa Mahakamani. Katika mwaka 2009/2010, Taasisi itaendelea kufanya utafiti na uchunguzi ili kubaini Mianya ya Rushwa Kubwa na Ndogo na kutoa elimu juu ya Mapambano Dhidi ya Rushwa. Aidha, itawafungulia mashtaka wote wanaobainika kujihusisha na vitendo vya Rushwa.

Mazingira
100. Mheshimiwa Spika, Tafiti na Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na kasi ya ongezeko la Joto Duniani. Kutokana na hali hii, katika kipindi cha mwaka 2008/2009, Serikali imeendelea kutekeleza Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi kwa kuelimisha na kuhamasisha Wananchi kuhusu athari za mabadiliko ya Tabianchi na changamoto za kukabiliana nazo. Mafunzo kwa Wananchi na Watendaji yameendeshwa katika Mikoa ya Iringa, Tanga na Pwani kuhusu mabadiliko ya Tabianchi pamoja na nafasi ya Ushiriki wa Wananchi katika shughuli za Upandaji Miti ambazo zinaweza kuwaongezea kipato kupitia biashara ya hewa mkaa. Maeneo ya Kipaumbele yamebainishwa kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya kupunguza utoaji wa Gesijoto utokanao na Ukataji na Uharibifu wa Misitu. Katika mwaka 2009/2010, Serikali itaendelea kuratibu shughuli zote zinazohusu mabadiliko ya Tabianchi.

Maafa
101. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Serikali iliendelea kuelimisha Jamii kuhusu mbinu za kukabili Maafa, kutathmini maeneo ya Maafa Nchini na kuijengea uwezo Idara ya Maafa. Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali ilifanya tathmini ya kina ya Hali ya Chakula Nchini na kubaini kuwa, baadhi ya maeneo yameathirika kwa ukame na hivyo kusababisha upungufu wa chakula. Jumla ya Wilaya 36 katika Mikoa 12 zimeathirika kwa ukame. Mikoa hiyo ni Arusha, Kilimanjaro, Pwani, Mwanza, Dodoma, Lindi, Tanga, Manyara, Morogoro, Mara, Mtwara na Iringa. Katika kukabiliana na hali hii, Serikali ilitoa jumla ya Tani 28,684 za mahindi kwa Walengwa. Aidha, ilitoa jumla Shilingi Bilioni 1.8 kwa ajili ya kununua mbegu za mahindi na mtama kwa Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mwanza Dodoma, Lindi, Tanga, Manyara, Morogoro, Mara, Mtwara, Shinyanga na Tabora.

102. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwezi Oktoba 2008 hadi Mei 2009, Nchi yetu imekumbwa na Maafa mengine yakiwemo kuporomoka kwa Machimbo ya Madini katika Kijiji cha Mugusu (Geita), ambapo zaidi ya Watu Sita wanahofiwa Kufa. Maafa mengine ni Ajali ya Treni Dodoma iliyosababisha Vifo vya Watu Saba na yale yaliyotokea katika Ukumbi wa Starehe tarehe 1 Oktoba, 2008 Mjini Tabora ambapo Watoto 19 walipoteza maisha na wengine 16 walinusurika katika tukio hilo. Aidha, hivi karibuni kulitokea Ajali za kuzama kwa Boti huko Tanga na Meli Zanzibar.

103. Mheshimiwa Spika, vilevile, Ajali za Barabarani zimeendelea kupoteza nguvu kazi kutokana na Vifo na kuongeza idadi ya Walemavu. Kwa mfano, kati ya kipindi cha Januari hadi Aprili 2009, jumla ya ajali 6,647 ziliripotiwa Nchini kote ikilinganishwa na 5,111 kipindi kama hicho mwaka 2008. Kati ya Ajali hizo, Ajali 880 zilisababisha Vifo vya Watu 1,190. Hizi ni Ajali na Vifo vingi ambavyo vingeweza kuepukika kama Madereva, Abiria, Watembea kwa miguu na Askari wa Usalama Barabarani wangetimiza wajibu wao kikamilifu.

104. Mheshimiwa Spika, Maafa mengine ni yale ya Mlipuko wa Mabomu yaliyotokea tarehe 29 Aprili, 2009, katika Kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) iliyopo Mbagala, Dar-es-Salaam. Katika tukio hilo madhara makubwa yalitokea na kusababisha Watu 26 kupoteza Maisha, ambapo Raia walikuwa 20 na Askari wa JWTZ ni Sita. Watu 338 walijeruhiwa. Serikali iliunda Kamati Maalum ya Wataalam kufanya tathmini ya nyumba zilizoharibika. Taarifa ya tathmini inaonyesha kuwa jumla ya nyumba 9,049 zimeharibika. Kati ya hizo, nyumba zipatazo 286 zilibomoka kabisa na zilizobaki 8,763 zimeezuliwa paa, kuvunjika au kupata nyufa. Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali imechukua hatua za kuwapatia Waathirika Misaada ya Chakula, Mahema na Vifaa vya Nyumbani. Aidha, Serikali inaandaa utaratibu wa kuwalipa fidia Waathirika wa maafa hayo. Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wote waliotoa Misaada ya Hali na Mali katika kuwasaidia Walioathirika. Aidha, nawapa pole wale wote waliopoteza Ndugu na Jamaa zao katika Matukio hayo na Mwenyezi Mungu Azilaze Roho za Marehemu Mahali Pema Peponi. Amina.

105. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali itaendelea kuijengea uwezo Idara ya Maafa ili iweze Kuratibu na Kujenga uwezo wa Wadau mbalimbali katika kukabili Maafa Nchini. Hatua hizo ni pamoja na kuiwezesha Idara hiyo kutoa Elimu kwa Jamii juu ya Mbinu za Kujikinga na Maafa kupitia Vyombo vya Habari na kutoa mafunzo kwa Kamati za Maafa za Wilaya na Mikoa.

Mauaji ya Walemavu wa Ngozi
106. Mheshimiwa Spika, kwa takriban miaka miwili kuanzia mwezi Juni 2007, Nchi yetu imeshuhudia kuibuka kwa wimbi kubwa na kushamiri kwa Mauaji ya kutisha ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi, yaani Albino. Tatizo hili kwa kiasi kikubwa linachochewa na Imani za Kishirikina na udanganyifu kwamba Viungo vya Mlemavu wa Ngozi ni Dawa ya kusaidia kuleta Utajiri wa haraka haraka, hasa kwa Watu wachache wenye tamaa ya fedha wanaojishughulisha na biashara na Uchimbaji wa Madini na Uvuvi wa Samaki. Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali imechukua hatua mbalimbali ili kwa pamoja kuweza kupata njia sahihi ya kukabiliana na Ukatili dhidi ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi. Serikali imefanya Sensa ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi Nchini ili kuwatambua pamoja na kuendesha zoezi la Upigaji Kura dhidi ya Wahalifu na Wanaojishughulisha na Mauaji hayo. Uchambuzi na uhakiki wa waliotajwa katika zoezi hilo unafanywa na Vyombo vya Ulinzi na Usalama. Watuhumiwa katika baadhi ya Mikoa wamepelekwa Mahakamani na kesi zimeanza kusikilizwa.

Dawa za Kulevya
107. Mheshimiwa Spika, Nchi yetu bado inakabiliwa na tatizo la matumizi na biashara haramu ya Dawa za Kulevya. Hali hii inatishia Ustawi na Usalama wa Taifa letu. Tatizo hili linadhihirishwa na takwimu za watumiaji wa Dawa za Kulevya waliojitokeza kwenye Hospitali na Vituo vya Tiba pamoja na zile za ukamataji wa Dawa za Kulevya na uteketezaji wa Mashamba ya Bangi. Kwa mfano, mwaka 2007/2008 Waathirika wa Dawa hizo wapatao 4,723 walipata tiba. Halikadhalika, mwaka 2008 Tani 76 za Bangi zilikamatwa ikilinganishwa na Tani 59 zilizokamatwa mwaka 2007. Katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka 2008, jumla ya Ekari 72 za Mashamba ya Bangi ziliteketezwa. Ukamataji wa Dawa za Kulevya aina ya Heroin na Cocaine ulipungua kwa mwaka 2008 ambapo jumla ya Kilo 7 zilikamatwa ikilinganishwa na jumla ya Kilo 22.8 za Dawa hizo zilizokamatwa mwaka 2007. Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2006 hadi 2008 Watanzania wapatao 103 walikamatwa Nje ya Nchi kwa kujihusisha na Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya, jambo ambalo linaleta taswira mbaya ya Nchi yetu kwa Jamii na Kimataifa.

108. Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kupambana na tatizo hili la Dawa za Kulevya. Hatua hizo ni pamoja na uelimishaji kwenye Maonyesho na katika Matukio mbalimbali ya Kitaifa na Vyombo vya Habari kama vile Redio, Televisheni, Magazeti pamoja na Machapisho mbalimbali. Aidha, Serikali imeandaa Sera ya Taifa ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya ambayo inatoa Mwongozo wa namna ya Kudhibiti Matumizi na Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya.

109. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2009/2010, Serikali itaendelea kuelimisha Umma kuhusu madhara ya Dawa za Kulevya. Aidha, itaongeza uwezo wa Idara na Wakala wa Serikali katika kusimamia Mipaka, Bandari na Viwanja vya Ndege ili visitumike kupitishia Dawa Haramu za Kulevya. Pia, Serikali itaendelea kusimamia na kuendesha Operesheni Maalum za kuwabaini na kuwakamata Wafanyabiashara wa Dawa za Kulevya Nchini pamoja na kuteketeza Mashamba ya Bangi. Kutokana na matumizi ya Dawa za Kulevya kuchochea Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI, Serikali itaendelea kutekeleza Mikakati ya Kudhibiti Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI miongoni mwa Watumiaji wa Dawa za Kulevya. Hata hivyo, ningependa kusisitiza kuwa, wajibu mkubwa wa kupambana na utumiaji wa Dawa za Kulevya upo kwa Wazazi na Walezi ambao wanawajibika kuwaelimisha na kufuatilia kwa karibu tabia za Watoto kabla hawajaingia katika mtego wa kutumia Dawa hizo. Wazazi na Walezi wawe karibu na Watoto wao. Tusiwaache Watoto walelewe na Televisheni na Internet.

HITIMISHO

110. Mheshimiwa Spika, nimeelezea kwa muhtasari shughuli mbalimbali ambazo Serikali imetekeleza kwa kipindi cha mwaka 2008/2009, na pia nimetoa mwelekeo wa kazi zitakazofanyika katika mwaka 2009/2010. Katika kuhitimisha Hotuba hii ningependa kusisitiza mambo muhimu yafuatayo:
(a) Sote tunatambua kuwa mwaka wa fedha ujao ni wa mwisho kabla ya kuelekea kwenye kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Hivyo, tunahitaji ushirikiano mkubwa na Wadau wote wa Maendeleo na Wananchi kwa ujumla ili kutekeleza kwa dhati na kwa makini Kazi za Serikali zilizopangwa na hatimaye tuweze kuhitimisha utekelezaji wa malengo yaliyokusudiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala na yale ya MKUKUTA. Nawaombeni tudumishe Utulivu, Amani na Mshikamano wetu. Demokrasia pana na Uhuru wa kuzungumza uliopo usitumike vibaya na wachache wetu. Tuendelee kudumisha Umoja wetu kama Taifa wakati huu wa kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na kujiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

(b) Serikali imedhamiria kuleta mapinduzi ya kweli katika Sekta ya Kilimo. Hivyo, tunayo kazi kubwa mbele yetu ya kuwahamasisha Wananchi kuzingatia Kanuni bora za Kilimo na kutumia zana bora na mbolea ili wazalishe kwa tija na kuongeza uzalishaji kuwezesha Taifa letu kujitosheleza kwa chakula na kupata ziada. Natoa rai kwamba ni wajibu wa kila mmoja wetu kuchangia kwa nguvu zote jitihada hizi ili kufanikisha azma yetu ya kuleta Mapinduzi katika Kilimo. Kauli Mbiu yetu na Wimbo wetu sasa uwe ni “KILIMO KWANZA”. Kipaumbele chetu cha kwanza kiwe ni Kilimo. Kipaumbele chetu cha Pili ni Kilimo na Kipaumbele chetu cha Tatu kiwe ni Kilimo. Kwa kufanya hivyo, tutaweza kufikia lengo la Maisha Bora kwa kila Mtanzania.

(c) Serikali itaendelea kudhibiti matumizi ya fedha yasiyo ya lazima katika baadhi ya maeneo ili kuweka nguvu zetu katika Kilimo, hususan cha Umwagiliaji. Makongamano, Warsha na Semina zisizo na tija zitaendelea kusitishwa pamoja na ununuzi wa magari ya kifahari ili fedha hizo zielekezwe kwenye Kilimo. Natoa wito kwa Viongozi katika ngazi zote, Wadau wetu wa Maendeleo na Wananchi wote tushirikiane kuisaidia Serikali kutoa msukumo katika Kilimo. Napenda kusisitiza kuwa Viongozi wa Mikoa na Halmashauri wana wajibu mkubwa kuwasaidia Wananchi kuibua Miradi bora ya Kilimo, na kutafuta vyanzo zaidi vya fedha za kununulia pembejeo hasa Matrekta na Vitendea kazi kwa Maafisa Ugani ili kuongeza tija na uzalishaji katika Kilimo.

(d) Serikali inathamini na kuheshimu mchango wa Wakulima na Wafugaji na inaheshimu haki zao. Tushirikiane na Serikali katika juhudi zinazofanywa za kutenga maeneo kwa ajili ya Malisho ya Mifugo na ya Wakulima. Wakulima na Wafugaji wote Nchini waheshimu Haki na Mipaka ya kila mmoja ili waendelee kuishi kwa amani na kufanya shughuli zao za uzalishaji mali kwa uhakika.

(e) Ili kufanikisha utekelezaji wa Majukumu na Kazi za Serikali zilizopangwa kwa mwaka 2009/2010 na kutoa huduma bora kwa Wananchi ni muhimu Watumishi wote wa Serikali wawajibike ipasavyo katika kuwatumikia Wananchi na kuondoa Kero zinazowakabili. Nahimiza Watumishi wote kuzingatia Maadili ya Kazi, Kanuni na Sheria pamoja na kufanya Kazi kwa Bidii na Ubunifu na kuepuka vitendo vya Rushwa. Watumishi wa Umma wasio Waaminifu na Wababaishaji wabanwe na kuchukuliwa hatua za Kinidhamu.

(f) Pamoja na Msukosuko wa Masoko ya Kifedha na kuyumba kwa Uchumi Duniani, bado tunazo fursa nyingi za kukuza Uchumi wetu kwa kuongeza uzalishaji na pia zipo fursa za kufanya hivyo kupitia Medani ya Ushirikiano wa Kimataifa. Tunazo bidhaa nyingi zinazoweza kupenya na kushindanishwa katika Masoko ya Kimataifa, Masoko ya Kikanda na Soko la Pamoja la Afrika Mashariki. Nawasihi Wananchi wetu tutumie fursa hizi vizuri kwa kujiandaa vyema na kushiriki katika biashara za Kimataifa na kuhamasisha Utalii na fursa nyingine za Kiuchumi ili tuiingizie Nchi yetu Pato kubwa zaidi na kuondoa Umaskini kwa kasi zaidi.

111. Mheshimiwa Spika, kabla ya kumaliza Hotuba yangu, nimwombe Mheshimiwa Celina Ompeshi Kombani (Mb.), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa atoe maelezo ya Mapitio ya Kazi Zilizofanyika katika mwaka 2008/2009 na Mwelekeo wa Kazi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2009/2010. Ni matumaini yangu kwamba maelezo hayo yatawezesha Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kufahamu kwa upana shughuli zinazotekelezwa na Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

SHUKRANI

112. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Mawaziri wote na Naibu Mawaziri wote kwa ushauri wao ambao umewawezesha Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kutekeleza majukumu yao ya Kitaifa kwa ufanisi. Aidha, nawashukuru Wafanyakazi wote wa Serikali na Taasisi zake chini ya uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi, Bwana Phillemon Luhanjo pamoja na Vyombo vyote vya Dola kwa kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kuiwezesha kukamilisha maandalizi yote ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2009/2010, pamoja na Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya kila Wizara, Mikoa, Wakala na Taasisi za Serikali Zinazojitegemea. Nawashukuru Watanzania wote na Washirika wetu wa Maendeleo kwa michango yao ambayo imewezesha kufanikisha Serikali kutoa huduma mbalimbali kwa Wananchi.

113. Mheshimiwa Spika, vilevile, napenda kuwashukuru Mheshimiwa Phillip Sanka Marmo, Mbunge wa Mbulu, Waziri wa Nchi (Sera, Uratibu na Bunge), Mheshimiwa Celina Ompeshi Kombani, Mbunge wa Ulanga Mashariki, Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Aggrey Joshua Mwanri, Mbunge wa Siha, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa msaada mkubwa na ushirikiano walionipa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Shukrani za pekee kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa jitihada walizoonyesha katika kipindi hiki. Nawashukuru vilevile Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya uongozi wa Makatibu Wakuu, Bwana Peniel Michael Lyimo na Bibi Maimuna Kibenga Tarishi na Naibu Katibu Mkuu, Bwana Fanuel Eusebius Mbonde kwa ushauri wao wa Kitaalam ambao wamenipa mimi na Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi katika kipindi hiki. Nawashukuru kwa kukamilisha maandalizi yote ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2009/2010.

114. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/2009, Nchi yetu imepata misaada na mikopo kutoka kwa Wahisani wetu mbalimbali. Misaada na mikopo hiyo imetoka kwa Nchi rafiki, Nchi fadhili, Taasisi za Fedha Duniani, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Mifuko Mbalimbali ya Fedha Duniani, Madhehebu ya Dini na Mashirika Yasiyo ya Serikali. Misaada na mikopo hiyo imechangia sana katika kutekeleza miradi ya mbalimbali ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa Wananchi. Napenda kuwashukuru wote kwa dhati na kuwahakikishia kuwa Watanzania tunathamini misaada na mikopo waliyotupatia na tutaendelea kushirikiana nao katika harakati za kuleta maendeleo ya Taifa letu.

MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU, OFISI YA WAZIRI MKUU - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA NA OFISI YA BUNGE YA MWAKA 2009/2010

115. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2009/2010, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake inaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi 143,268,010,000. Kati ya fedha hizo, Shilingi 67,979,095,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 75,288,915,000 ni kwa ajili ya Mpango wa Maendeleo.

116. Mheshimiwa Spika, vilevile, kwa mwaka 2009/2010 Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Asasi zake inaombewa jumla ya Shilingi 197,886,256,000. Kati ya hizo, Shilingi 124,368,171,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 73,518,085,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.

117. Mheshimiwa Spika, Ofisi za Wakuu wa Mikoa zinaombewa jumla ya Shilingi 168,135,049,000. Kati ya hizo Shilingi 123,013,358,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 45,121,691,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo. Aidha, Halmashauri zote zinaombewa jumla ya Shilingi 2,044,567,344,000 kati ya hizo Shilingi 1,565,973,955,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 478,593,389,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.

118. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano inaombewa jumla ya Shilingi 68,257,038,000 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo Shilingi 62,109,293,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 6,147,745,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
MUHTASARI

119. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya kwa muhtasari, naomba sasa Bunge lako Tukufu likubali kuidhinisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2009/2010 ya jumla ya Shilingi 68,257,038,000 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge, na jumla ya Shilingi 2,553,856,659,000 kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ikiwa ni Matumizi ya Kawaida na Fedha za Maendeleo za Ndani na Nje kwa ujumla wake. Mchanganuo wake ni kama ifuatavyo:


A. MAFUNGU YA OFISI YA WAZIRI MKUU

(i) Ofisi ya Waziri Mkuu
Sh. 143,268,010,000
· Matumizi ya Kawaida
Sh. 67,979,095,000
· Matumizi ya Maendeleo
Sh. 75,288,915,000

B. MAFUNGU YA OFISI YA WAZIRI MKUU – TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

(i) Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa
Sh. 197,886,256,000
· Matumizi ya Kawaida
Sh. 124,368,171,000
· Matumizi ya Maendeleo
Sh. 73,518,085,000

(ii) Ofisi za Wakuu wa Mikoa
Sh. 168,135,049,000
· Matumizi ya Kawaida
Sh. 123,013,358,000
· Matumizi ya Maendeleo
Sh. 45,121,691,000




(iii) Ruzuku kwa Halmashauri
Sh. 2,044,567,344,000
· Matumizi ya Kawaida
Sh. 1,565,973,955,000
· Matumizi ya Maendeleo
Sh. 478,593,389,000

C. MFUKO WA BUNGE
Sh. 68,257,038,000
· Matumizi ya Kawaida
Sh. 62,109,293,000
· Matumizi ya Maendeleo
Sh. 6,147,745,000

Jumla Kuu Sh. 2,622,113,697,000

120. Mheshimiwa Spika, pamoja na Hotuba hii yapo Majedwali ambayo yanafafanua kwa kina Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Bunge.

121. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

COMMENTS

Name

Anga,11,Arusha,27,Burudani,302,burundani,1,come rain,1,come sun,1,Crazy in Love kama wimbo kama wao wenyewe,1,dahh sijui kweli mbona shida,1,Dar utakuja je tumejiandaa,1,daraja sahau nini,1,demokrasia ya upanga,1,Dodoma,77,Dole tupu vijana wa zamani,1,Duhh bibie endeleza libeneke,1,Duhh kaisikie Walibana,1,duhh kwa mbagala mama lazima awe supa,1,Fedha za maiti haziliwi bure,1,Fedha za watu kwa maendeleo ya watu,1,Fikira,14,filamu,238,Filamu ndio kielelezo cha ukuzi wa taifa,1,flamu,7,Gandamiza Kibara baba ake,1,Habari,4810,habari. dodoma,24,hadithi,19,hakika tumeweka historia,1,hakuna noma jongwe,1,hapa kwetu inakuwaje vile,1,hasira hasara,1,hata maji,1,hataki masikhara na maisha yake,1,hatubonyezi kizenji,1,haya ndiyo mambo ya Ulaya,1,haya si yangu ni ya mdau mwenye hasira,1,haya wabongo na mambo kutoka nje,1,He he he wananikumbusha upishi wa shaba,1,Headline,1,Hii hurejesha uhai,1,Hii iko sawa kweli?,1,Hii imekaa vizuri,1,Hii inakaaje vile,1,Hii kweli noma,1,Hii maana yake Moro kuna uhaba wa chakula,1,Hii mexico,1,Hii mihasira mingine bwana,1,Hii ndio moro sio mpaka dar,1,hii ni hatari,1,Hii ni kiboko anayetaka kubisha ajibishie tu,1,Hii ni moja ya staili za kunyoa nywele,1,Hii si lukwangule,1,hii staili mpya,1,hili ni jengo pacha la malaysia ghorofa 88,1,Hivi ni ngoma tu,1,hivi nini siri za serikali,1,hivi sisi tunajua kama kuna vitu vya aina hii,1,hivi vitu bwana,1,Hiyo ndiyo gharama ya demokrasia,1,Hizi imani nyingine ni hatari,1,Hizi takwimu hizi mhh,1,Hongera bibie,1,Hongera dada etu kwa kutuletea kaka etu (shemeji) kwani mwenye dada hakosi shemeji,1,Hongera sana,1,huhitaji mifedha kuwa msafi,1,Huko Ulaya,1,Huu ndio ustaarabu,1,huu ujiko utakuwa mkubwa,1,imetosha,1,Inahitaji nidhamu fulani,1,inakuuma au...,1,Inakuwaje kama filamu yenyewe itahitaji busu la nguvu,1,Inaonekana watanzania hatukuwepo,1,Ipo kazi Maximo,1,Iringa,22,Isiwe mijineno tu manake mihela hubadili watu kweli,1,Itakuwa laki moja ya halali,1,jamani huu kama si ushamba kumbe nini,1,Jamani mbona Mungu anatupigania,1,Jamani watoto wanatakiwa kupendwa,1,jamani.. jamani ukiikosa Diamond usijutie,1,Je nyumbani hakuna vitu vya aina hii?Tuambie,1,je walikuwepo watu wa huduma ya kwanza,1,Je watanzania wanalipa kodi,1,jela kwa raha,1,Jolie,1,juhudi za lazima kuinua filamu,1,kama si kiwanda cha chumvi nani atawajua hawa,1,Kama kweli ndio kweli basi kila heri,1,Kama Mkristo naamini hilo hiyo si sahihi,1,kama unajua kuyarudi nenda Malta,1,kama wao wanaweza sisi je,1,Kamua baba waache wakanyagane,1,karibu nyumbani dada yote maisha tu,1,karibu Tatiii,1,KARIBUNI,1,Katavi,5,kaza buti hakuna kukata tamaa inalipa,1,kazi kwako mheshimiwa waziri wa madini,1,kazi na burudani,1,keep it up bloggers,1,kero ya usafiri sasa kwisha,1,Kila chenye roho na mwili kitaonja umauti,1,kila kitu kina vitu,1,Kila la Heri jamila,1,kila la heri kwani ni changamoto,1,Kipya,51,Kiuno bila mfupa,1,Kolelo mzimu ambao bado hai,1,KUBWA,1,Kudumisha urafiki wa dunia,1,Kuna dalili za wasomi kukubali Uafrika,1,kuna makala humu humu ndani ya blogu sijui mnasemaje,1,Kuu,113,kwa mara nyingine tena Tigo imewezesha,1,Kwa mchanganyiko huu muungano lazima udumu,1,Kwa mihasira hajambo,1,kweli,1,Kweli ina mkono mrefu tuone,1,Kweli duniani tunatofautiana,1,la maana ni kuwa na jiko au vipi,1,labda halitabadilika tena,1,lakini mwafaka lazima,1,lengo ni kutafakari,1,leteni vitu tuvione,1,lets us,1,Lucy wanakuelewa hawa...,1,Lukwangule nyumbani kwetu,2,M ungu bariki mikono ya madaktari wafanikiwe,1,MAARUFU,1,maendeleo ya soka siku zote yanahitaji fedha ili yapatikane,1,maisha ni vyema kuyaangalia,1,MAJIBU,1,makala,51,mama ni mama tu anapendeza,1,mambo mengine we angalia tu,1,mambo msimamo,1,mambo sasa mchanganyiko,1,Mara nyingine huona tunakotoka kwa kuona wenzetu,1,Mashabiki wa rhumba mpooooooooo,1,Masitaa,12,Maskani,1,MASOKO,3,Masupa staa mnaoinukia mpoo,1,Matamasha,6,mavazi ya kuogelea yanaposhindaniwa,1,Mbeya,11,Mchakamchaka anti Asmah,1,Mchanganyiko,81,MCHANYATO,1,mchezo,5,mengi wanayoyaita siri ni public information,1,mfumuko wa bei mpaka noma,1,Mhh sijui watu wa Sua ambao wako huko wanasemaje,1,Mhh ugua pole dada watu wanataka burudani,1,Michezo,501,Michezo maalum inatakiwa kupigiwa debe,1,miguu,1,miguu babu,1,Mikataba mingine ama hakika tuiangalie hata wakopeshaji nao wanatugeuza sakala,1,MIMI NI KISURA NAJITAMBUA,1,Mimi sijajua hasa kumetokea nini kwani ninavyojua hawa huwa na ungalizi wa hali ya juu,1,Mimi simo,1,mimi sisemi,1,mkiwa chumvi basi mkoze,1,Mkiwa taa mulikeni,1,Mnaonaje je hii imekaa vyema,1,Mnaweza wakwetu hapa,1,Morogoro,51,mrithi wa mwanadada Whitney Houston,1,Mtwara,4,Mungu aiweke mahali pema roho yake,4,Mungu amrehemu,1,Mungu amweke pema peponi,1,Mungu awabariki sana,1,Mungu awe nao,1,Mungu ibariki Tanzania,1,Mungu tuepushe na imani hizi za kishirikina,1,mungu tufanye tuwe na upendo,1,Mungu twaomba utuhurumie,1,Muziki,350,muziki na fasheni,5,Mwanahabari,33,Mwanza,6,Mwendo mdundo dada,1,Mwenge huo utakimbizwa duniani kwa siku 130,1,Mwenge wa olimpiki ni ishara ya urafiki,1,Mzee wa Farasi nakupa saluti,1,Mzimbabwe huyu kutoka kwa mama mkali,1,N i dar mpaka Moro au bao tatu bila,1,Na sisi je,1,Naam kama haiwezekani hapa,1,Nairobi waanzisha tena utalii,1,namna bora ya kusaidia jamii,1,nani abebe hukumu na lawama,1,nani asiyejua utamu wa pipi,1,Nani kama baba,1,naona inafaa kuchangia mimi sitoi hoja,1,ndoa za mastaa huwa na mgogoro,1,nenda mwaya nenda,1,New Zanzibar Modern Taarab na wapenzi big up,1,news,5,Ni bikini kwa kwenda mbele,1,Ni Dar mpaka Moro au.. tatu bila,1,ni furaha za muungano,1,Ni kazi ngumu yenye kuhifadhi utamaduni,1,Ni kuchakarika kuonyesha urafiki na biashara pia,1,ni mfumuko wa bei au mfumuko wa nchi,1,Ni muhimu kutazama afya yako,1,ni muziki kwa kwenda mbele,1,Ni muziki mpaka China,1,Ni raha tupu,1,Ni Serengeti Premium Lager,1,Ni Tigo na mawasiliano ya kisasa,1,Ni wakati wa kuujadili utamaduni,1,Ni zaidi ya jazz,1,Nitasubiri and welcome home,1,nje je?,1,NUKUU YA LEO,1,nyie mnasemaje kuhusu hili,1,Ona Kolelo na sindikizwa na Wazee wa Gwasuma,1,ona vya dunia,1,One step ahead,1,patna mwingine mjamzito,1,Pengine anamuogopa Jada Pinkett manake kwa wivu..,1,picha,494,Pole Jamila hayo ndiyo mashindano,1,poleni sana,1,poleni sana wanyalukolo,1,Powa sana,1,Profesa jamaa wanakumaindi,1,Roho za marehemu zipate pumziko la milele,1,Ruvuma,9,sakata dansi mpaka kwenye kilele cha dunia,1,sasa kumebakia ugonjwa mmoja polisi kuendesha mashtaka,1,sasa mifedha kila mahali hongereni,1,Sasa ni mavuno,1,Sasa ni wakati wa kutafuta upenyo ndani ya IDOLS,1,SAYANSI,1,SAYANSI ANGA,1,See Uluguru Montains,1,serikali inataka kujihami kwanini,1,Show of support Big Up Madame,1,Si kitu kidogo hata kidogo,1,si unajua tena namie naimwaga hivyo hivyo,1,Siasa,346,siasa habari,2,Sijui kama City wanajua Mbagala noma,1,Sijui tunaishi karne gani yailahi,1,Sinema,9,sio advencha....kaaa ...niko kibaruani,1,Sisi ndio tunaanza vitongoji,1,Sisi yetu macho na masikio,1,Slow slow jamani,1,sto,1,tabasamu kali la mwenge wa olimpiki,1,Tabora,1,Tazama Waziri Mkuu Pinda wasije wakapindisha maamuzi yako,1,TEKNOLOJIA,1,Thats big man game,1,This is crazy Africa,1,This is Mgeta,1,Tibet wamegeuza Olimpiki jukwaa la siasa,1,Titbits collection,1,Tubadili tamaduni,1,Tuchangie mambo yaive,1,tuendeleze sanaa,1,tuienzi na sisi mbona wizara haituambii,1,Tuipeleke kaskazini,1,Tuisaidie serikali shida ya Mererani,1,tujue namna ya kupumzika,1,Tulienda kustarehe au kufanya fujo,1,Tumsaidie mtototo huyu kurejea katika hali ya kawaida,1,tunahitaji haya,1,Tunajifunza kweli kutoka kwao,1,Tunapandisha chati tu,1,Tunasubiri,1,tunazidi kuhesabu siku,1,TUNAZISUBIRI ZA VINARA ADAR,1,Tuombe nafuu kwa wagonjwa,1,Tuombe rehema kwa mungu,1,Tuone yatufae,1,Tusingoje wengine watusemee,1,tutampa tafu kubwa Prof,1,tuuenzi utamaduni au vipi,1,Tuukuze na kuulinda,1,tuvipende,1,tuwalinde maalbino,1,Tuwe kweli wakweli,1,ubunifu siku zote hulipa,1,uchumi huzunguka kwa kuwawezesha wasukaji,1,udumu muungano,1,Ugonjwa huu wa sasa ni kitendawili,1,Ukiiona kolelo utaipenda,1,Ukirejea salama kila mtu anafurahi,1,Umelenga Mkuchika utamaduni unakufa,1,unaposaka uwakilishi wa dunia,1,urafiki,1,Usisahau wazee wa Ngwasuma,1,UTAMADUNI,1,Video,2,Vionjo vipya ndani ya Gwasuma,1,Vita dhidi ya ufisadi,1,vitongoji Miss Tanzania navyo vimeanza,1,Vitu vikali vyazidi kuingia Dar,1,Vituko,77,Vituo vya polisi Tanga vyatelekezwa,1,VIVALO,1,Wacha tujifue,2,Wadau ilitolewa kiingereza,1,wakali wa ubunifu,1,wala usibabaike mwakwetu hii noma,1,wanadamu wanapotaka kujua zaidi,1,wanasema mpaka kieleweke,1,Wanataka kujua mali za JK na wengine,1,Wanawake wenye mvuto: Monroe,1,Wapo mabinti wa matawi ya juu,1,watu wanapofanya weli kwenye sanaa,1,waweza kurejea enzi ya Moro jazz na Cuban malimba,1,Wazee tupo kusindikiza,1,waziri,1,welcome dar baby,1,Wenzetu wameona sisi tunangoja nini kuangalia,1,wewe unasemaje,1,wigo mpana wa utamaduni,1,wilaya ya 'Mbagala' mlie tu,1,Yaaani sijui itawezekana,1,Yaani wakati mwingine hata huelewi prioty over priority,1,yeye mbele sisi nyuma,1,Yote maisha dada,1,ZA MOTOMOTO,1,Zanzibar,79,zawadi zinatakiwa ziende shule,1,ZILIZOTIA FORA,1,zitachangia kupunguza makali ya bei za umeme,1,
ltr
item
Lukwangule Entertainment: Kiranja mkuu ataka 'displin' katika matumizi
Kiranja mkuu ataka 'displin' katika matumizi
Lukwangule Entertainment
http://lukwangule.blogspot.com/2009/06/kiranja-mkuu-ataka-displin-katika.html
http://lukwangule.blogspot.com/
http://lukwangule.blogspot.com/
http://lukwangule.blogspot.com/2009/06/kiranja-mkuu-ataka-displin-katika.html
true
934549962738256429
UTF-8
Loaded All Posts Not found any posts VIEW ALL Readmore Reply Cancel reply Delete By Home PAGES POSTS View All RECOMMENDED FOR YOU LABEL ARCHIVE SEARCH ALL POSTS Not found any post match with your request Back Home Sunday Monday Tuesday Wednesday Thursday Friday Saturday Sun Mon Tue Wed Thu Fri Sat January February March April May June July August September October November December Jan Feb Mar Apr May Jun Jul Aug Sep Oct Nov Dec just now 1 minute ago $$1$$ minutes ago 1 hour ago $$1$$ hours ago Yesterday $$1$$ days ago $$1$$ weeks ago more than 5 weeks ago Followers Follow THIS CONTENT IS PREMIUM Please share to unlock Copy All Code Select All Code All codes were copied to your clipboard Can not copy the codes / texts, please press [CTRL]+[C] (or CMD+C with Mac) to copy