Wadau na wafanyabiashara wa mafuta wamedai kuwa kero ya kuchakachua mafuta imezungukwa na mazingira ya rushwa na kuitaka serikali kuchukulia...
Wadau na wafanyabiashara wa mafuta wamedai kuwa kero ya kuchakachua mafuta imezungukwa na mazingira ya rushwa na kuitaka serikali kuchukulia hatua za haraka ili kudhibiti hasara ya mabilioni inayosababishwa na uchakachuaji huo.
Wakitoa mapendekezo yao katika Kamati ya kudumu ya bunge ya Nishati na Madini jana wafanyabiashara hao kutoka Umoja wa Wasafirishaji wa Shehena kwa Njia za barabara nchini na nchi jirani ( (TATOA) na chama cha Waagizaji na wasambazaji wa mafuta (TAOMAC) walisisitiza kuwa njia pekee ya kudhibiti uchakachuaji wa mafuta ni kupandisha kodi ya mafuta ya taa.
Walisema yapo mazingira yanayoashiria kuwa fedha nyingi zinazotokana na uchakachuaji wa mafuta hayo zinatembea mikononi mwa watu wachake na kutumika kutoa rushwa kwa baadhi ya wanasiasa na watendaji katika mamlaka mbalimbali zinazohusika na nishati hiyo ya mafuta ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) na Mamlaka ya Mapato Tanzania na kampuni ya Global Fluids International (GFI).
Akielezea sababu na hasara inayotokana na uchakachuaji wa mafuta, Mkurugenzi Mtendaji wa TAOMAC Salum Biasarara alisema matufa ya diseli yanayotozwa kodi ya sh. 520. 80 wakati mafuta ya taa yanatozwa kodi ya 59.10 jambo ambalo linasababisha wafanyabiashara wasiowaaminifu kuchanyanga mafuta ya taa na diseli kwa lengo la kupata faida kubwa.
“Tofauti ya sh. 461.70 ni kubwa sana hivyo njia pekee ni kupandisha kodi ya mafuta ya taa ili kuepuka kuliingizia taifa hasara ya zaidi y ash. Bilioni 25 kila mwezi inayosababishwa na uchakachuaji,” alisema Biasarara.
Naye Mwenyekiti wa TATOA Seif Ally Seif alisema ingawa serikali iliamua kushusha bei ya mafuta ya taa kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wananchi wa kipato cha chini, hasara inayotokana na uchakachuzi wa mafuta inalisababishia Taifa hasara kubwa ambayo inawaathiri watu hao hao wa kipato cha chini.
Alisema badala ya serikali kuendelea kupoteza zaidi sh. Bilioni 25 sawa na bilioni 300 kwa mwaka kutokana na hasara ya uchakachuaji mafuta ni vyema kodi ya mafuta ipandishwe kisha fedha hizo zipelewe Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa lengo la kuboresha nishati kwa watu wa vijijini ambao ndio wateja wakubwa wa mafuta ya taa.
“Mtanzania wa leo sio wa kuendelea kutumia koroboi ambazo zina adhari kubwa kwa afya ya binadamu. Hatuoni ni kwa nini Serikali inasita kupandisha bei ya mafuta ya taa kisha kutumia fedha hizo kuwawezesha watanzania kutumia taa zinazotumia nishaji ya jua,” alisema Seif.
Alisema chama chake kinashindwa kuelewa ni kwa nini serikali inatumia fedha nyingi kuthibiti vitendo vya uchakachuaji mafuta wakati njia iko wazi na inaeleweka na kutaka kamati ya Bunge kufuatilia suala hilo kwa makini.
Alidai suala la udhibiti wa biashara haramu ya mafuta yaliyochakachuliwa imegubikwa na rushwa na kuingiliwa na masuala ya kisiasa na kutoa mfano wa madereva wa malori ya matufa waliokamatwa nchi jirani kutokana na shutuma za kushiriki katika biashara haramu ya uchakachuaji wa mafuta lakini walipoachiwa walipokelewa kama mashujaa.
“Madereva wanaondoka wakiwa na mafuta masafi na kuyabadilisha huko njiani lakini watu hawataki kukubali kuwa wanahusika katika biashara hiyo jambo ambalo linasababisha udhibiti kuwa mgumu,” alisema.
Alisema baadhi ya malori ya kampuni yake yaliwahi kukamatwa yakiwa yamebeba mafuta yaliyochakachuliwa lakini alipoitwa wadereva walimuambia akaye pembeni kwa kuwa jambo hilo halimhusu na baada ya muda akasikia kuwa malori hayo yameshavuka mpaka.
“Nilipouliza imekuwaje watu wa EWURA walinijibu kuwa yalikuwa yamekamatwa kwa makosa....jamani ni vigumu kudhibiti hizo bilioni 25 zinazozunguka hapa katikati kama serikali itaamua kuendelea kutotusikiliza,” alisema Seif.
Alisema sekta ya ushafirishaji wa Shehena kwa Njia za barabara nchini na nchi jirani ni ya tatu kwa kulipatia taifa fedha za kigeni na kwamba hivi sasa iko katika hatari ya kuporomoko kwa sababu wafanyabiashara wa nchi za jirani wanakosa imani na Watanzania hivyo kusita kutumia bandari ya Dar es Salaamu kwa sababu ya wafanyabiashara wachache wasiokuwa waaminifu.
Mjumbe mwingi alilalamika kwamba alipobaini kuwa magari yake yamebeba mafuta yaliyochakachuliwa alitoa taarifa kwa Mamlaka ya Mapato (TRA) ili idhibiti mafuta hayo lakini baadaye aliamuriwa kuyalipia kodi.
“Naomba kamati hii ya Bunge itusaidie...kama leo natoa taarifa juu ya magari yangu kushiriki katika biashara ya mafuta haramu kisha adhabu napewa mimi mtoa taarifa kesho nikiona nitatoa? Aliuliza mjumbe huo.
Pia walidai kuwa kampuni ya Global Fluids International (GFI) iliyopewa mamlaka ya kupima sampuli mafuta haifanyi kazi yake ipasavyo kwa kuwa baadhi ya watendaji wake wanauza vinasaba ya kupimia mafuta kwa njia ya magendo hivyo huweka kiasi kidogo cha vinasaba hivyo katika mafuta hivyo kusababisha mkakati mzima wa kuthibiti uchakachuaji wa mafuta kuwa mgumu zaidi.
Walisisitiza kuwa njia pekee ya kudhibiti mlolongo mrefu wa mianya ya rushwa katika sakata nzima la uchakachuaji wa matufa ni kupandisha kodi ya mafuta.
Pia wafanyabiashara hao walilalamikia utitiri wa kodi na vizuizi vingi barabarani ambayo vimekuwa kikazo kwa wawekezaji wa mafuta na kupunguza uwezo wa Tanzania kumudu ushindani katika soko la Afrika Mashariki.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba alisema kuwa alisema jumatano ijao kamati yake itaitisha kikao kitakachoshirikisha wadau wote ili kujadili suala hilo kwa upana na hatimaye kupata suluhisho kwa manufaa ya Taifa.
COMMENTS