ASKARI Polisi wawili waliokuwa katika msafara wa Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal mkoani Tanga, wamekufa baada gari lao kupinduka na kutumbukia kwenye korongo.
Msafara wa Dk. Bilal aliyekuwa akihitimisha ziara ya wilaya nne kati ya nane za mkoa wa Tanga, alikuwa njiani kwenda Hale katika wilaya ya Korogwe akitokea Lushoto.
Ajali hiyo imethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe aliyewataja waliokufa kuwa ni Koplo Jegi na askari mwingine, Henry, katika eneo la ajali, kona ya Nduru eneo la Mombo, Lushoto.
Alisema gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili PT 2000 ambalo lilikuwa linaendeshwa na Denanta Abdallah, breki zake zilishindwa kufanya kazi na hivyo kutokana na mwendo kasi, gari lilipinduka na kutumbukia kwenye korongo. Kufikia saa 2 mbili usiku, lilikuwa halijatolewa korongoni.
Mbali ya dereva, askari wengine waliojeruhiwa wametajwa kuwa ni Majesta Mlaka, Nyamsanga Bitulo na Justine Kangulu. Majeruhi wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Korogwe ya Magunga ambako pia miili ya marehemu imehifadhiwa.
0 comments:
Post a Comment