Katibu Mkuu Chadema *TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI* KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod ...
| Katibu Mkuu Chadema |
*TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI*
KATIBU Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod
Slaa amehitimisha ziara
ya siku 10 ya kujenga chama na kukagua uhai wa
chama katika mikoa
mitano, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Geita na Mwanza,
ambako katika maeneo
mbalimbali alikopita amesimamia vikao vya kiutendaji
ambavyo vimelazimika
kuchukua maamuzi mazito na muhimu dhidi ya watu
waliobainika kuhujumu
maendeleo ya wananchi, kukihujumu chama, kuvunja
katiba, kanuni na
taratibu za CHADEMA.
Moja ya maamuzi hayo
mazito ni kuvuliwa kwa uanachama kwa aliyekuwa Diwani
wa Kata ya Katoro, Gervas
Daudi, kufutwa uongozi wa BAVICHA Geita, kuvuliwa
uanachama baadhi ya
viongozi na wanachama ambao baada ya kuhojiwa na vikao
walibainika pasi na shaka
kuwa wamekuwa wakihujumu chama hivyo kukwaza
matumaini ya wananchi kwa
CHADEMA, kuwa chama mbadala nchini. Watu hao
waliovuliwa uanachama
watalazimika kusubiri maamuzi zaidi ya Kamati Kuu
inayotarajiwa kuketi hivi
karibuni, ili kujua hatma yao ndani ya CHADEMA.
Akiwa katika vikao hivyo
vilivyofanya maamuzi hayo mazito, Katibu Mkuu Dkt.
Slaa alilazimika kutoa
kauli kali akisema kuwa chama hakitakubali kulea
viongozi wasiowajibika
kwa watu, akisisitiza kuwa kama kuna kiongozi yeyote
hawezi kuendana na kasi
ya mahitaji ya chama hicho katika kuwatumikia watu,
anapaswa kupisha mara
moja badala ya kukwaza juhudi hizo.
*“Viongozi wangu naomba
mtambue, chama hiki si mali ya mtu, wala si chama
cha viongozi, ni chama
cha wananchi, ni chama cha watu, ni chama cha
Watanzania. Hiki si chama
cha kukaa siku nzima kutatua migogoro, ni chama
cha kutafakari suluhisho
la matatizo mbalimbali yanayowakabili Watanzania.
Chadema ni tumaini pekee
la Watanzania kwa sasa.*
*“Hatutavumilia ufisadi,
hatutavumilia uzembe, hatutakubali viongozi
wanaojali maslahi yao
badala ya wananchi, katika hili CHADEMA tutakuwa
wakali kwa yeyote hata
kama angekuwa ni katibu mkuu, hatuwezi kujifungia
kuzungumzia migogoro
inayosababishwa na ubinafsi wa watu badala ya kutumia
muda huu kuzungumzia kero
na maendeleo ya watu,” amesisitiza Dkt. Slaa
katika ziara hiyo.*
Katika ziara hiyo
iliyoanzia Nzega, mkoani Tabora, Aprili 13 na kumalizikia
Jijini Mwanza Aprili 22,
2012, Katibu Mkuu Dkt. Slaa kupitia vikao hivyo
vya kimaamuzi amelazimika
pia kutoa kauli kali dhidi ya viongozi na
wanachama wanaoonekana
kukwaza jitihada za CHADEMA katika kuwatumikia watu,
akisema kuwa chama hiki
ndiyo tumaini pekee lililobaki kwa Watanzania
katika harakati za
ukombozi wa awamu ya pili, kutafuta mabadiliko ya
kimfumo na kiutawala
nchini kwa ajili ya maendeleo ya watu.
Wilayani Nzega, kikao cha
kiutendaji kiliwavua uongozi aliyekuwa Mwenyekiti
wa Jimbo, Tito Onesmo
kutokana na kupata nafasi hiyo kinyume cha utaratibu
na Katibu Mwenezi,
Shaaban Mohamed kwa kosa la kughushi barua. Wote
walipewa karipio kali na
kutakiwa kuandika barua ya maelezo kwa nini
wasichukuliwe hatua kali
zaidi. Mohamed baada ya kubanwa na kukosa utetezi
wa makosa yake, aliamua
kurejesha kadi ya uanachama mbele ya kikao hicho.
Katika Wilaya ya Bariadi,
Katibu Mkuu alifutilia mbali kile kilichoitwa
uongozi wa Mkoa wa Simiyu
kwani kwa taratibu za chama mkoa huo bado haupo,
hivyo uchaguzi ulikuwa
batili tangu mwanzo.
Viongozi wa Wilaya ya
Bariadi waliohusika katika kuitisha uchaguzi huo,
akiwemo Mwenyekiti
Mwenyekiti wa Wilaya Limbu Ntalima, Katibu wake Elias
Maduka Kaselabantu na
Mwenyekiti wa Vijana wa Wilaya, Khamis Rajab, na
Bwana Kube Kube
aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mkoa, walipewa onyo kali,
kuwekwa chini ya
uangalizi maalum kwa kipindi cha miezi 12, kuangalia
mwenendo wao ndani ya
chama, huku pia Kube akitakiwa kuandika barua ndani
ya siku 30 kueleza kwa
nini alikuwa nyuma ya suala hilo.
Mbali ya kufutilia mbali
uongozi huo, kikao hicho kiliwaondoa madarakani
viongozi wa wilaya
waliochukua madaraka isivyohalali aliyekuwa Mwenyekiti
wa Wilaya Limbu Ntalima,
Katibu wake Elias Maduka Kaselabantu na Mwenyekiti
wa Vijana wa Wilaya,
Khamis Rajab kwa kukiuka katiba ya chama na kukihujumu
katika uchaguzi mdogo wa
kutafuta Diwani wa Kata ya Legangabilili, ambapo
CHADEMA ilikuwa ikipewa
asilimia kubwa ya kuibuka mshindi.
Viongozi hao waliomba
radhi na kuahidi mbele ya kikao kuwa mara moja
watakwenda kufuta kesi
waliyofungua mahakamani kuhoji uhalali wa Kamati
Maalum (task force)
iliyoundwa kwa ajili ya kuongoza chama wilayani Bariadi
kwa muda.
Katika Wilaya ya Kahama,
Baraza la Mashauriano lilikubaliana kwa kauli moja
Charles Dotto Lubala,
Anastazia Kanyanda na Justine Mganga wavuliwe
uanachama, huku wenzao 12
wakiwekwa chini ya uangalizi maalum kwa kosa la
kusababisha mgogoro ndani
ya chama wilayani humo, hali iliyosababisha chama
kushindwa kufanya kazi ya
kuwatumikia wananchi katika maeneo mbalimbali
kama vile ngazi ya
vitongoji, vijiji na kata ambako wananchi waliichagua
CHADEMA kuwatumikia.
Katika Jimbo la Busanda,
Mkutano Mkuu wa Jimbo uliamua kwa sauti moja,
baada ya kupiga kura,
kumuachisha uanachama aliyekuwa Diwani wa Kata ya
Katoro, Gervas Daudi,
akikabiliwa na tuhuma kadhaa ikiwemo kukihujumu chama
hicho. Ngazi husika za
chama zitawasilisha taarifa ya maamuzi husika kwa
ajili ya uamuzi wa mwisho
kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama.
Mbele ya kikao hicho,
Daudi alituhumiwa kukihujumu chama hicho kwa kuzuia
uongozi wa Serikali ya Kijiji
cha Katoro ambayo inaongozwa na Chadema
kutekeleza ilani ya chama
hicho katika kuwaletea maendeleo wananchi wa eneo
hilo, hasa katika
kusimamia rasilimali za wanakijiji, huku akishiriki vikao
vya kuizushia tuhuma za
kutengeneza.
Alituhumiwa kuzuia
utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa
sekondari, kituo cha
magari na urekebishaji wa mikataba mibovu ya upangaji
wa vibanda vya biashara
mali ya kijiji hicho ambayo iliingiwa wakati wa
uongozi wa CCM katika Serikali ya Kijiji cha Katoro
kabla ya uchaguzi
uliokiondoa madarakani
chama hicho katika eneo hilo.
Tuhuma zingine ni
kuwachangisha fedha wananchi 9 kiasi cha shilingi laki 5
kinyume na taratibu,
akiwaahidi kuwatoa waume zao ambao wanashikiliwa
mahabusu wakituhumiwa kwa
kosa la mauaji, pia alituhumiwa kushiriki vikao
na wafanyabiashara,
viongozi na wanachama wa CCM wakipanga kuipindua
serikali ya kijiji hicho
na pia kuwapindua viongozi wengine wa vitongoji
wanaotokana na CHADEMA.
Daudi pia amesimamishwa
nafasi zake zingine ndani ya chama hicho, ikiwemo
Uenezi Jimbo la Busanda,
Uenyekiti Wilaya ya Geita, ambapo Kamati Tendaji
ya Wilaya ya Geita
imeagizwa kukaa haraka kuteua mtu atakayeziba nafasi ya
Daudi kisha jina hilo
litumwe na kujadiliwa Kamati Kuu ya chama hicho
inayotarajiwa kuketi hivi
karibuni.
Halikadhalika katika
Wilaya ya Geita, Baraza la Mashauriano kwa kauli moja,
baada ya kupiga kura
lilifikia uamuzi wa kuvuliwa uanachama kwa viongozi wa
Baraza la Vijana
(BAVICHA); aliyekuwa Mwenyekiti wa BAVICHA Jimbo la Geita,
Emmanuel Otto, Katibu
wake, Vincent Paul na Mratibu wa Uhamasishaji
Philibert Msiba. Pia
uongozi mzima wa baraza hilo ngazi ya jimbo
uliondolewa. Diwani wa
Marceline Simbasana aliandikiwa barua ya karipio
kali kwa mwenendo wake
kinyume na taratibu za chama.
Baraza la Mashauriano
katika Wilaya ya Sengerema liliamua kwa kauli moja
kuvunja Baraza la Uongozi
la Wilaya, pia uongozi wa Mabaraza yote, yaani
BAVICHA, BAWACHA na
Baraza la Wazee katika majimbo mawili ya Buchosa na
Sengerema ulivunjwa baada
ya kuonekana haukidhi mahitaji ya kikatiba,
kanuni na taratibu za
chama.
Halikadhalika uongozi wa
CHADEMA Jimbo la Sengerema wote ulivunjwa, ambapo
ilikubaliwa kuwa viongozi
wote waliohusika katika kuvunja katiba, kanuni na
taratibu katika kusimamia
shughuli za chama ikiwemo kuwafukuza wenzao
uanachama wasihusike
katika mchakato wa kujaza nafasi za uongozi wakati
uchaguzi wa kukaimisha na
pia katika uchaguzi wa ndani unaotarajiwa kuanza
hivi karibuni na
kukamilika mwaka 2013.
Katibu Mkuu, Dkt. Slaa
amesema kuwa hatarudi nyuma katika kuendesha
‘safisha safisha’ hiyo
kwani akiwa Mtendaji Mkuu wa chama anatekeleza
azimio la Kamati Kuu
iliyoazimia kuwa ofisi yake ifanye uhakiki wa uongozi
na utendaji wa chama ili
kujenga chama na kukagua uhai wa chama kuanzia
ngazi ya chini, Msingi
mpaka juu.
*Imetolewa leo Aprili 26,
2012, Dar es Salaam na; *
*Tumaini Makene*
*Afisa Habari wa CHADEMA*
COMMENTS