Labda hizi zimenifurahisa: -Kupunguza matumizi ya magari kwa safari za mikoani kwa viongozi na watendaji wakuu serikalini yaani...
Labda hizi zimenifurahisa:
-Kupunguza matumizi ya magari kwa safari za mikoani kwa
viongozi na watendaji wakuu serikalini yaani dar -Bihalamuro au dar Tunduma- Dar Moshi au Dar Mbeya sasa
hamna tena
Watatumia usafiri wa umma na kukuta magari ya kazi hukohuko
Serikali itaanzisha
vituo vya kanda vya magari ya Serikali yatakayokuwa yakitumika mikoani katika
shughuli hizo za kikazi.
-Kuweka ukomo wa injini za magari yatakayonunuliwa na
Serikali Kuu, mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi zake ambapo sasa magari
yatakayonunuliwa hayatazidi ukubwa wa injini wa CC 3,000.
-Kupungua kwa bei ya matrekta na mfano wa trekta la Horse
power 50 limepunguzwa kutoka Sh milioni 25.6 hadi milioni 16.5 na la Horse
Power 70 limepunguzwa kutoka Sh milioni 45.8 hadi milioni 38.8.
-Watumishi
watakaobainika kuwa ni wabadhirifu wa fedha za
umma kuvuliwa madaraka waliyo nayo na kufikishwa mahakamani.
Lukwangule(kaka mkubwa)
Soma hotuba yenyewe
HOTUBA YA WAZIRI
MKUU,
MHESHIMIWA MIZENGO PETER
PINDA (MB), KUHUSU MAPITIO NA
MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA
WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2012/2013
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja kwamba kutokana na Taarifa zilizowasilishwa
leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na
Utawala na Kamati ya Fedha na Uchumi zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri
Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa
Kazi za Serikali kwa mwaka 2011/2012 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa mwaka
2012/2013. Vilevile, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya
Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa, Taasisi zilizo chini yake pamoja na Ofisi ya Bunge
kwa mwaka 2012/2013.
2.
Mheshimiwa
Spika, tangu tulipohaitimisha Mkutano wa Bajeti wa Bunge
hili mwaka jana, Nchi yetu imekumbwa na Majanga
na Matukio mbalimbali yaliyosababisha
vifo na uharibifu wa mali.
Nitumie fursa hii kutoa
pole kwa wote
waliofiwa na Ndugu, Jamaa na Marafiki. Mungu azilaze Roho za Marehemu mahali Pema Peponi. Kwa ndugu zetu
walioumia na bado wanajiuguza, tumwombe Mwenyezi Mungu awasaidie kupona haraka
na kurejea katika shughuli za ujenzi wa Taifa.
3.
Mheshimiwa Spika, nijiunge na wenzangu waliotangulia kuwapongeza Waheshimiwa
Wabunge wapya, Mawaziri na Naibu Mawaziri walioteuliwa na Mheshimiwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Mei 2012. Aidha, napenda kumpongeza Mheshimiwa
Mussa Zungu Azzan, Mbunge wa Ilala, kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge. Nawapongeza pia Wenyeviti
na Makamu Wenyeviti wa Kamati
za Kudumu za Bunge waliochaguliwa kuchukua nafasi zilizoachwa wazi. Vilevile, nawapongeza
Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa na Bunge lako Tukufu kuiwakilisha Tanzania
katika Bunge la Afrika Mashariki. Natarajia kwamba wote walioteuliwa na
kuchaguliwa watatumia nafasi hizo kwa manufaa ya Bunge na kwa maendeleo ya Watanzania
kwa ujumla.
4.
Mheshimiwa Spika, kwa takriban siku Tano Waheshimiwa Wabunge wamepata
fursa ya
kujadili Taarifa
Kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2011, Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti ya
Serikali kwa mwaka
2012/2013. Napenda kutoa Pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Stephen Masatu
Wasira (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu; na Mheshimiwa
Dkt. William Augustao Mgimwa (Mb.), Waziri wa Fedha kwa Hotuba nzuri na
ufafanuzi wa Hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Vilevile,
napenda kutoa shukrani zangu kwa Waheshimiwa Wabunge kwa kujadili kwa kina
Hotuba hizo na hatimaye kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/2013.
5.
Mheshimiwa Spika, kipekee, nitumie nafasi hii, kuwashukuru Wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala inayoongozwa na
Mheshimiwa Pindi Hazara Chana, Mbunge wa Viti Maalum. Nawashukuru pia Wajumbe
wa Kamati ya Fedha na Uchumi inayoongozwa na Mheshimiwa Andrew John Chenge,
Mbunge wa Bariadi Magharibi. Kamati hizo zimetoa mchango mkubwa wakati wa
uchambuzi wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Mafungu ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na
Mfuko wa Bunge. Aidha, nawashukuru Wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge
lako Tukufu kwa ushauri waliotoa wakati wa kupitia Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali Zinazojitegemea na Mamlaka
za Serikali za Mitaa. Maoni na Ushauri wao utazingatiwa wakati wa utekelezaji
wa Bajeti hii.
6.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge ni
mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka
2010. Vilevile, imezingatia Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa
kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Malengo ya Maendeleo ya Milenia na Awamu
ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini. Katika mwaka 2012/2013,
Serikali itaimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Mipango na Miradi ya Maendeleo,
matumizi ya fedha za Umma na uwajibikaji. Tutatumia rasilimali chache
tulizonazo kwa kazi ambazo zitajielekeza kwenye shughuli za uzalishaji mali na
kuongeza tija ili kuchochea ukuaji wa haraka wa uchumi.
HALI YA UCHUMI
7.
Mheshimiwa Spika, Pato la Taifa kwa mwaka 2011 lilikua kwa Asilimia 6.4 ikilinganishwa na Asilimia 7 mwaka 2010. Ukuaji huo wa Asilimia 6.4 ni mkubwa ikilinganishwa na kiwango cha ukuaji wa uchumi wa
Nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambacho kilikuwa wastani wa Asilimia
5.1. Kushuka kwa kiwango cha ukuaji
uchumi wetu kulichangiwa kwa kiasi kikubwa na ukame ambao uliathiri zaidi Sekta
ya Kilimo na uzalishaji wa Nishati ya Umeme Nchini. Tatizo la umeme, upungufu wa chakula katika
baadhi ya maeneo Nchini pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta katika Soko la
Dunia vilichangia pia kuongezeka kwa mfumuko wa bei. Hatua zinazoendelea
kuchukuliwa na Serikali kudhibiti Mfumuko wa Bei ni pamoja na kurejesha
upatikanaji wa umeme kwenye hali ya kawaida na kuimarisha ugavi wa chakula
Nchini. Hatua hizo, zimeanza kupunguza kiwango cha Mfumuko wa Bei. Ni vyema tukumbuke kwamba, hatua za kukabili
tatizo la kiuchumi kama vile Mfumuko wa Bei zinapochukuliwa leo, matokeo yake
hayawezi kuonekana siku hiyo hiyo. Wataalam wanaeleza kwamba mara nyingi inachukua
miezi 6 hadi 18 kuona dhahiri matokeo ya hatua zilizochukuliwa. Hivyo, siku za
usoni tutashuhudia Mfumuko wa Bei ukipungua zaidi.
Maboresho ya Sekta ya Fedha
8.
Mheshimiwa
Spika, Taasisi za Fedha zina mchango mkubwa katika
kuchochea kasi ya maendeleo na ukuaji wa Uchumi. Kwa kutambua mchango huo,
Serikali inatekeleza Programu ya Maboresho ya Sekta ya Fedha, ambayo imekuwa na
mafanikio ya kuridhisha. Mafanikio hayo
ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya Taasisi za Fedha ambazo hadi sasa
zimefikia 49 zikiwa na Matawi 519 Nchini kote. Aidha, baadhi ya
Taasisi hizo zimeonesha mafanikio makubwa katika eneo la huduma za Kibenki kwa
njia ya mtandao.
9.
Mheshimiwa
Spika, Serikali pia imetoa msukumo wa uanzishaji wa
huduma za Kifedha kupitia Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOs) ambavyo hadi sasa
vimefikia 5,346. Vyama hivyo vimetoa
mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 627.2.
Pamoja na mafanikio hayo, changamoto kubwa inayoikabili Sekta ya Fedha ni
viwango vikubwa vya riba kwenye Mikopo vinavyoendelea kutozwa na Benki za Biashara ikilinganishwa na riba
ndogo inayolipwa kwa amana. Changamoto nyingine ni kukosekana kwa Taasisi
nyingi za fedha zinazotoa Mikopo ya muda
mrefu yenye masharti
nafuu kwa Miradi ya Maendeleo hasa kwenye
Sekta ya Kilimo. Serikali inatambua Changamoto hizo na
tayari Mikakati inaandaliwa kukabiliana nazo hususan kuanzisha Dirisha la
Kilimo katika Benki ya Rasilimali Tanzania pamoja na kukamilisha mchakato wa
kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Aidha, Serikali inaendelea kuboresha
mazingira ya uwekezaji pamoja na kuanzisha Mfumo wa kuwatambua wakopaji (Credit Reference Bureau).
SENSA YA WATU NA MAKAZI 2012
10.
Mheshimiwa
Spika, katika hotuba zangu za Bajeti za miaka Miwili
iliyopita, nililijulisha Bunge lako Tukufu kuhusu maandalizi ya Sensa ya Watu
na Makazi ambayo itafanyika tarehe 26 Agosti 2012. Nilianza kutoa Taarifa ya
Sensa mapema kwa kuwa Sensa ni mchakato unaohitaji maandalizi ya muda mrefu
kabla na baada ya zoezi lenyewe la kuhesabu Watu. Kwa kutambua umuhimu wa Sensa
katika kuandaa na kutekeleza Mipango ya Maendeleo ya Nchi, zoezi hili limepewa
kipaumbele cha pekee katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/2013. Katika Awamu
ya Kwanza ya maandalizi ya Sensa, kazi zilizofanyika ni pamoja na kutenga
maeneo ya kuhesabia Watu, kutayarisha Madodoso na Miongozo mbalimbali, kufanya
Sensa ya Majaribio, kununua vitendea kazi, kuchapisha Nyaraka za Sensa na
kuunda Kamati za Sensa za Mikoa na Wilaya.
11.
Mheshimiwa
Spika, kazi za Sensa zinazoendelea ni uhamasishaji na
kutoa Elimu kwa Umma ili kila Mwananchi ashiriki kikamilifu katika zoezi hilo.
Shughuli nyingine ni utoaji wa mafunzo kwa watakaokuwa Makarani wa Kuhesabu
Watu na Wasimamizi, usambazaji wa Vifaa na Maandalizi ya kuingiza takwimu
kwenye Kompyuta. Katika utekelezaji wa zoezi hili, Serikali itawatumia Watumishi
mbalimbali wa Serikali wakiwemo Walimu. Kutokana na sababu hiyo, Serikali
imelazimika kubadili mihula ya Shule ili Walimu waweze kusaidia katika zoezi
hili la Sensa.
12.
Mheshimiwa Spika, nawaomba Viongozi
wote tusaidiane kuhamasisha na kusimamia utekelezaji wa zoezi la Sensa katika
maeneo yetu. Nawaomba Wananchi wote washiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na
Makazi kwa kutoa ushirikiano na taarifa sahihi kwa Makarani wa Sensa na
Wasimamizi ambao watatembelea Kaya zetu tarehe 26 Agosti 2012. Niwahakikishie Wananchi
wote, kuwa taarifa zote zinazokusanywa wakati wa Sensa ni Siri na zitatumika
kwa shughuli za Kitakwimu tu. Takwimu hizo hazina uhusiano na Dini, Kodi, Siasa
au mambo mengine kama hayo ambayo hayakukusudiwa.
KUIMARISHA
DEMOKRASIA NA MUUNGANO
Hali ya Siasa
13.
Mheshimiwa
Spika, kumekuwa na mwamko mkubwa wa Wananchi kushiriki
kwenye masuala ya Kisiasa hali inayoashiria kukua kwa Demokrasia Nchini. Vyama vipya
vya Siasa vimeendelea kusajiliwa na vilivyopo kujiimarisha zaidi. Katika mwaka
2011/2012, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imepokea maombi ya kusajili
Vyama vipya Viwili vya Siasa. Chama cha Kijamii (CCK) kimepata Usajili wa
Kudumu na kufanya idadi ya Vyama vyenye Usajili wa Kudumu kufikia 19. Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimepata Usajili wa muda na
Chama cha Movement for Democratic and
Economic Change kinaendelea kufanyiwa uhakiki.
14.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/2013, Ofisi ya Msajili wa Vyama
vya Siasa itaendelea kushughulikia maombi ya Usajili wa Vyama, kuendelea kutoa
elimu kwa Wananchi kuhusu mfumo wa Vyama vingi vya Siasa na Sheria ya Gharama
za Uchaguzi ya mwaka 2010. Aidha, itafuatilia uhai wa Vyama vya Siasa kwa
mujibu wa Sheria na kuanzisha Ofisi mbili za Kanda. Kanda hizo ni ile ya Kusini
inayojumuisha Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma na Kanda ya Magharibi
inayojumuisha Mikoa ya Tabora, Kigoma, Shinyanga na Katavi. Nitumie nafasi hii
kuwasihi Watanzania kutumia fursa ya kupanuka kwa Demokrasia kuendelea kushiriki
kwenye Siasa kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Nchi. Viongozi wa Vyama
vya Siasa waonyeshe mfano wa kuendesha Siasa za kistaarabu zenye lengo la kuunganisha Watanzania na siyo kuwachonganisha.
Hakuna Nchi au Kiongozi aliyewahi kupata sifa nzuri kwa kuwa chanzo cha
mifarakano. Tudumishe utulivu na amani pamoja na ustaarabu wetu wa Kitanzania.
Mabadiliko ya Katiba
15.
Mheshimiwa
Spika, Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa katika
Mkutano wa Tano wa Bunge, mwezi Novemba 2011, Bunge lako Tukufu lilipitisha
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 8
ya Mwaka 2011 (Sura ya 83). Aidha,
Bunge lilifanya marekebisho ya Sheria hiyo katika Mkutano wa Sita, mwezi
Februari 2012. Hatua hiyo, ilimwezesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kuteua
Wajumbe wa Tume itakayoratibu na kukusanya Maoni ya Wananchi kuhusu Mabadiliko
ya Katiba. Tume hiyo yenye Wajumbe 32
inajumuisha Wawakilishi wa Makundi mbalimbali katika jamii kutoka pande mbili
za Muungano.
16.
Mheshimiwa
Spika, Tume imeanza kazi rasmi tarehe 1 Mei 2012, kama
ilivyopangwa. Serikali imefanya maandalizi muhimu kuiwezesha Tume kufanya kazi
yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuipatia Vifaa vya Kisasa vya kukusanya na
Kutunza Kumbukumbu na kufungua Tovuti rasmi. Aidha, Idara ya Mpigachapa Mkuu wa
Serikali imepewa jukumu la kuchapisha kwa wingi Katiba na Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba ili Wananchi waweze kuelewa na kutoa michango yao kwa uhakika zaidi
kwenye mchakato wa kutoa maoni.
17.
Mheshimiwa
Spika, napenda nichukue fursa hii tena kumpongeza Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba, Waziri
Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba na Mheshimiwa Augustino Ramadhani, Jaji Mkuu Mstaafu wa
Tanzania kwa kuteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti. Vilevile, napenda kuwapongeza
Wajumbe wote, wakiwemo Katibu na Naibu Katibu kwa kuteuliwa kuunda Tume hiyo.
Napenda kuwasihi Wananchi wajitokeze kwa wingi na kutoa maoni yao kwa utulivu
katika Mikutano itakayoitishwa na Tume na kuwapa Wajumbe ushirikiano wa kutosha
ili hatimaye tupate Katiba iliyoandikwa na Watanzania wenyewe.
Muungano
18.
Mheshimiwa Spika, tarehe 26 Aprili 2012, Muungano wetu ulitimiza Miaka 48 ya Watanzania kuishi pamoja, kwa
amani na utulivu. Katika mwaka
2011/2012, Vikao 14 vya Kisekta vya
Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT) na
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) vilifanyika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za Muungano.
Kikao cha Kamati ya Pamoja cha SMT na SMZ, chini ya Uenyekiti wa Makamu wa
Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, kilifanyika ambapo Hoja 13 zilijadiliwa na Hoja Mbili
zilipatiwa ufumbuzi. Hoja zilizopatiwa ufumbuzi ni kuhusu ongezeko kubwa la
Ankara za umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo.
Aidha, imekubalika kuwa marekebisho ya Sheria yafanyike mapema ili kupata
ufumbuzi katika hoja zinazohusu Usajili wa Vyombo vya Moto, Kodi ya Mapato na
Kodi ya Zuio (Withholding Tax).
19.
Mheshimiwa Spika, Hoja nyingine ambazo zipo katika hatua mbalimbali za
kutafutiwa ufumbuzi zitaendelea kujadiliwa katika Vikao
vya Kamati ya pamoja vya Kisekta na Kamati ya Pamoja. Serikali pia itaendelea
kuratibu masuala yasiyo ya Muungano kwa kuhakikisha kwamba Sekta, Wizara na
Asasi Zisizo za Muungano zinakutana na kujadili changamoto zilizopo. Ni ukweli
usiopingika kwamba, Muungano wowote Duniani unakutana na changamoto mbalimbali.
Jambo muhimu ni pande zote zinazounda Muungano kuzitatua changamoto hizo.
Hivyo, ni vyema tukaendelea kukaa pamoja na kujadiliana ili Muungano wetu huu
ambao msingi wake ni mahusiano ya kihistoria ya pande zote mbili uendelee
kudumu kwa faida ya watu wetu.
BUNGE
20.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Bunge limetekeleza kwa
ufanisi majukumu yake ya msingi ya kutunga Sheria na kuisimamia Serikali.
Kamati za Kudumu za Bunge pia zimetekeleza majukumu yake ipasavyo na Bunge zima
limefanya Mikutano Minne kwa mujibu wa Sheria. Katika Mikutano mitatu
iliyofanyika, Miswada ya Sheria Nane (8)
ilipitishwa na Maswali ya kawaida 373
na ya Nyongeza 894 ya Waheshimiwa
Wabunge yalijibiwa na Serikali. Aidha, Maswali ya Msingi 78 ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu yaliulizwa na kujibiwa. Hoja mbalimbali za Kamati za Kudumu za Bunge
ziliwasilishwa na kujadiliwa.
21.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Ofisi ya Bunge itakarabati
Ukumbi wa Bunge na kuboresha miundombinu mingine ya Ofisi zake ikiwa ni pamoja
na kuweka Vifaa vya Mawasiliano na kuendelea na ujenzi wa Ofisi za Wabunge
katika Majimbo. Aidha, huduma za Utafiti na Sheria zitaimarishwa sambamba na
shughuli za Kamati za Kudumu za Bunge.
MAENDELEO YA SEKTA BINAFSI, UWEKEZAJI NA UWEZESHAJI
Maendeleo ya Sekta Binafsi
22.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa
Sekta Binafsi ili iweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali
na kufanya biashara na hatimaye kuwa Injini
ya Ukuaji wa
Uchumi.
Katika kufanikisha lengo hilo, Serikali inasimamia utekelezaji wa Mpango Kazi wa
Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini wenye lengo la kurekebisha
mifumo iliyopo ili kupunguza gharama za kufanya biashara na kuwekeza Nchini.
Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na uanzishaji wa Kituo Kimoja cha Utoaji wa
Huduma kwenye Bandari ya Dar es Salaam, ambapo muda wa mizigo kukaa Bandarini
umepungua kutoka wastani wa Siku 25
mwaka 2009 hadi kufikia wastani wa Siku 9
mwezi Mei 2012.
23.
Mheshimiwa Spika, hatua nyingine ni kupunguza Vizuizi vya Kudumu katika Barabara
Kuu, kuunda Kamati za pamoja kwenye Vituo vya Mipakani mwa Nchi (Joint Border Post Committees), kuendelea
na taratibu za kuanzishwa kwa Vituo vya Utoaji Huduma kwa Pamoja Mipakani (One Stop Border Posts) na kuweka mkazo
kwenye matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki kwenye maeneo ya ulipaji Kodi, Mabenki, Usajili wa Makampuni na
utunzaji wa kumbukumbu kwenye Masjala
mbalimbali. Sambamba na hatua hizo, majadiliano na Sekta Binafsi yamefanyika
kwa lengo la kupata ufumbuzi wa changamoto za Kisera, Kisheria na Mifumo ya Kitaasisi
zinazoikabili Sekta hiyo. Katika mwaka 2012/2013, Serikali itafanya tafiti zinazohusiana na maendeleo ya Sekta Binafsi,
pamoja na kuendeleza mashauriano na Sekta Binafsi, Washirika wa Maendeleo na
Taasisi Zisizo za Serikali kwa lengo la kuiwezesha Sekta Binafsi kutekeleza
majukumu yake kwa ufanisi.
Uwekezaji
24.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imefanya juhudi
kubwa za kuhamasisha na kuvutia Wawekezaji wa Ndani na Nje. Kutokana na juhudi
hizo, Kituo cha Uwekezaji Nchini kilisajili jumla ya Miradi 681 yenye thamani ya Shilingi Trilioni 11.6 na fursa za Ajira 89,803. Kati ya Miradi iliyosajiliwa,
Miradi 356 sawa na Asilimia 52.3 ni ya Wawekezaji wa Ndani, Miradi 166, sawa na Asilimia 24.4 ni ya Ubia kati ya Wawekezaji wa
Ndani na Nje na Miradi 159, sawa na Asilimia
23.3 ni ya Wawekezaji wa Nje. Mitaji
ya moja kwa moja ya Wawekezaji wa Nje (FDI), iliyoingizwa Nchini imeongezeka
kutoka Shilingi Bilioni 681.2 mwaka
2010 hadi Trilioni 1.3 mwaka 2011.
25.
Mheshimiwa
Spika, katika jitihada za kuongeza kasi ya Uwekezaji
Nchini kupitia Sera ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Serikali imefanya maandalizi ya msingi ya
kuanzisha Kitengo cha Uratibu wa masuala ya Ubia kwenye Kituo cha Uwekezaji na
Kitengo cha Fedha (PPP – Finance Unit) kwenye Wizara ya Fedha. Jumla ya Miradi
125 iliyoainishwa na Wizara
mbalimbali itafanyiwa uchambuzi zaidi na Vitengo hivi ili kubaini kama inakidhi
vigezo vya kutekelezwa chini ya utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na
Sekta Binafsi. Miradi hiyo ni pamoja na ile ya kuzalisha umeme, ujenzi wa
barabara, reli, bandari, na ujenzi wa majengo kwa ajili ya Ofisi na biashara.
26.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imeweka umuhimu wa kipekee kuhamasisha
ushiriki wa Wawekezaji wa Kitanzania kuanzisha
Miradi ya Uwekezaji katika Mikoa na
Wilaya kwa kuandaa Makongamano na Mikutano ya Kuhamasisha Uwekezaji na kutoa elimu ya ujasiriamali kwa Wawekezaji
Wadogo. Hadi sasa, Mikutano ya kuhamasisha Uwekezaji imefanyika katika Mikoa ya
Ukanda wa Ziwa Tanganyika ya Rukwa, Katavi na Kigoma pamoja na Mikoa ya Mara,
Singida, Arusha na Mbeya. Aidha, Wilaya za Mbinga, Njombe, Mufindi, Mbozi na
Kahama nazo zimefanya Mikutano hiyo. Mikutano ya Kikanda ya Uwekezaji
itaendelea kufanyika katika mwaka 2012/2013. Nahimiza, Viongozi wa Mikoa na
Wilaya kuandaa Mikutano hiyo na kuondoa Vikwazo vinavyokwamisha uwekezaji
katika maeneo yao. Ofisi ya Waziri Mkuu
itasambaza Mwongozo kwa Mikoa ili ishirikiane ipasavyo na Mamlaka za Serikali
za Mitaa kuandaa Mikutano ya Uwekezaji.
27.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kushiriki katika Mikutano
mbalimbali inayohusu masuala ya uchumi, biashara na uwekezaji. Mwezi Mei 2012,
Tanzania ilishiriki katika Mkutano wa World Economic Forum – Addis Ababa na baadaye
katika Mkutano wa Nchi Nane Zilizoendelea katika Viwanda (G8) huko Washington, Marekani. Katika mikutano hiyo, Serikali ilielezea
Mipango yetu ya kuleta Mapinduzi ya Kilimo Nchini, hususan Mpango wa Kukuza
Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (Southern
Agricultural Growth Corridor of Tanzania – SAGCOT). Mipango hiyo ilipokelewa na
kukubalika ambapo Tanzania imeingizwa
katika Mpango wa G8 wa Kuendeleza Kilimo Barani Afrika. Nchi nyingine Barani
Afrika zilizokubalika kushiriki katika Mpango huo ujulikanao kama G8
The New Alliance for Food Security and Nutrition ni Ethiopia na Ghana. Chini
Mpango huu, Tanzania itanufaika na misaada ya Shilingi Trilioni 1.41 kwa ajili ya kuwekeza katika Sekta
ya Kilimo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
28.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uongozi wake Mahiri na
juhudi zake za
kuhakikisha kwamba Nchi yetu inakuwa
moja ya Nchi Tatu Barani Afrika zitakazonufaika na Mpango huo. Hii
inathibitisha kuwa ziara za Mheshimiwa Rais Nje ya Nchi mara nyingi zina
manufaa makubwa kwa uchumi na maendeleo ya Nchi yetu.
29.
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya kuainisha Miradi itakayotekelezwa na
Wawekezaji wa Ndani na Nje katika Ukanda wa SAGCOT yameanza. Kutokana na ukubwa
wa ukanda huo wa Kilimo, Miradi itakayoainishwa itatekelezwa kwa Mfumo wa Kongano
(Clusters) ambapo Wakulima Wadogo
watashirikiana na Wawekezaji Wakubwa kuendeleza Kilimo.
30.
Mheshimiwa Spika, tumeanza kuona matunda
mazuri yaliyotokana na ushirikiano kati ya Wawekezaji Wakubwa na Wakulima
Wadogo katika kuongeza uzalishaji na tija. Hali hii imejionesha dhahiri kwenye Kilimo cha Mpunga huko
Kilombero ambapo Kampuni ya Kilombero
Plantations Limited iliyowekeza
kwenye Shamba la Mngeta Wilayani Kilombero imewasaidia Wakulima Wadogo
kupata Teknolojia rahisi ya kupanda na kupalilia mpunga. Wakulima hao wamewezeshwa kuanzisha vikundi vya
uzalishaji na kukopeshwa mbegu bora. Kutokana na ushirikiano huo, uzalishaji wa
mpunga kwa Wakulima Wadogo umeongezeka kutoka wastani wa Tani Mbili hadi Tani Saba
kwa Hekta moja. Utaratibu wa namna hiyo pia unatumiwa na Mwekezaji wa Kampuni
ya Sukari Kilombero na umewanufaisha Wakulima Wadogo wa Miwa Wilayani Kilombero kupitia vikundi vyao vya
uzalishaji. Ushirikiano wa aina hiyo
unatoa fursa za Masoko na Usindikaji wa Mazao yanayozalishwa na Wakulima Wadogo
wanaozunguka mashamba ya Wawekezaji Wakubwa. Hii ni dalili njema kabisa na
mfano wa kuigwa na Wawekezaji Wakubwa na Wakulima Wadogo Nchini.
31.
Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Watanzania
wenzangu kuona uwekezaji mkubwa katika Kilimo
kama fursa muhimu ya kuongeza uzalishaji na tija. Jambo la msingi ni
kuhakikisha kwamba maslahi ya Wakulima Wadogo yanalindwa kwa kuwekeana mikataba
mizuri na kufuatilia utekelezaji wake. Ni imani yangu kwamba, tukiitumia vizuri
ardhi yenye rutuba tuliyonayo tutaweza kuongeza ukuaji kwenye Sekta ya Kilimo
ambayo ni tegemeo kwa Watanzania wengi na hatimaye kupunguza Umaskini wa Kipato.
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
32.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia
Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi imeendelea kusimamia na kuratibu
utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004
kupitia Programu na Mifuko mbalimbali.
Hadi kufikia mwezi Aprili 2012, Mfuko wa
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (Mwananchi
Empowerment Fund), umetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 7.3 kwa Wajasiriamali 7,187 katika Mikoa ya Dodoma, Lindi,
Manyara, Mtwara, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Singida na Tanga. Sehemu kubwa ya Mikopo
iliyotolewa ilitumika kugharamia shughuli za Kilimo ikijumuisha ununuzi wa Pembejeo
na Zana za Kisasa za Kilimo na Umwagiliaji.
33.
Mheshimiwa Spika, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), katika
mwaka 2011/2012, Miradi 878 yenye
thamani ya Shilingi Bilioni 18.6
iliyoibuliwa na Wananchi kwenye Halmashauri zote Tanzania Bara na Zanzibar
ilitekelezwa. Vilevile, hadi kufikia Desemba 2011, Mfuko huo umetoa Shilingi Bilioni 1.14 kwa Walengwa 14,000 kupitia Utaratibu wa Uhawilishaji Fedha katika
Kaya Maskini. Aidha, Mafunzo ya Ujasiriamali yametolewa kwa Vikundi 500 Nchini katika Wilaya za Tanzania
Bara na Zanzibar. Vilevile, Wajumbe 8,780
wa Kamati za Usimamizi wa Mradi na 13,500
wa Kamati za Serikali za Vijiji na Mitaa walipata mafunzo.
34.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2012/2013, Serikali itaanza utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya TASAF. Benki ya Dunia
imepitisha Shilingi Bilioni 345.4
kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango huo utakaotekelezwa kwa kipindi cha Miaka
Mitatu. Serikali pia itasimamia Mifuko
ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ili Wajasiriamali wengi zaidi wanufaike.
Aidha, Serikali itawahamasisha Wananchi kuweka akiba, kuwekeza na kutambua na
kutumia fursa za kiuchumi zilizopo ili kuongeza kipato na ajira.
SEKTA ZA UZALISHAJI
Kilimo
35.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa mkakati wa kuhimiza Kilimo
cha Kisasa kinachotumia Kanuni Bora za Kilimo, Zana za Kisasa na msukumo kwenye
Kilimo cha Umwagiliaji ndiyo njia ya uhakika ya kuongeza uzalishaji na tija
katika kilimo. Aidha, ushirikiano baina ya Serikali na Sekta Binafsi ni nguzo
muhimu ya kuleta Mapinduzi ya Kilimo. Jitihada za Serikali katika mwaka
2011/2012 zilielekezwa katika vipaumbele hivyo pamoja na kuongeza upatikanaji
na matumizi ya Pembejeo na Zana Bora za Kilimo.
Pembejeo na Zana za Kilimo
36.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2011/2012, Serikali iliimarisha
upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo hasa Mbolea, Mbegu Bora na Madawa ya Mimea. Jumla
ya Vocha Milioni 5.3 za Ruzuku ya Pembejeo
za Kilimo zilisambazwa kwa Kaya Milioni 2 Nchini. Lengo la Serikali ni kuongeza upatikanaji wa
Pembejeo ili kuwanufaisha Wakulima wengi waweze kuongeza tija, uzalishaji na
kipato. Kama nilivyoahidi kwenye Hotuba yangu ya mwaka 2011/2012, tayari
Serikali imefanya ukaguzi maalum kuhusu utoaji wa Ruzuku za Pembejeo kwenye Kilimo
kwa utaratibu wa Vocha. Kutokana na matokeo ya awali ya ukaguzi huo, TAKUKURU
imefungua Kesi 19 kwa wale waliobainika
kufanya Ubadhirifu na Udanganyifu katika utoaji wa Vocha za Pembejeo za Kilimo.
Pamoja na hatua hiyo, Serikali itaboresha mfumo wa sasa wa utoaji wa Vocha za Pembejeo kwa
kubuni Mfumo mwingine ambao utaondoa upungufu uliojitokeza katika mfumo unaotumika
hivi sasa. Lengo ni kuhakikisha kwamba Vocha zinawafikia walengwa kwa wakati na
zinatumika kwa madhumuni yaliyopangwa.
37.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba, Serikali kupitia SUMA JKT iliingiza
Nchini Matrekta Makubwa 1,860 na Zana
zake; Matrekta Madogo ya Mkono 400 na Pampu za Umwagiliaji 1,100 kupitia Mkopo wenye Masharti
Nafuu kutoka Serikali ya India. Ili kuwawezesha Wakulima wengi zaidi kumudu bei
ya Matrekta hayo, Serikali imeamua kupunguza bei ya Matrekta hayo kwa kiasi
kikubwa. Kwa mfano, bei ya Trekta Moja la Horse
Power 50 imepunguzwa kutoka
Shilingi Milioni 25.6 hadi Milioni 16.5 na Trekta la
Horse Power 70 imepunguzwa kutoka Shilingi Milioni 45.8 hadi Milioni 38.8. Natoa wito kwa Halmashauri, Vyama vya
Ushirika, Vikundi vya Wakulima na Wananchi kutumia fursa hii kununua Matrekta
hayo. Aidha, jana baada ya kushauriana na Halmashauri husika tuliafikiana
kuwa Halmashauri ziangalie uwezekano wa kuwapunguzia zaidi Wakulima kiwango cha
Asilimia 30 wanachotakiwa kuchangia katika ununuzi wa Matrekta ya SUMA JKT ili waweze
kupata Matrekta hayo kwa bei nafuu zaidi. Lengo ni kuhakikisha kuwa Matrekta hayo
yanawafikia Wakulima wengi.
Umwagiliaji
38.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imekarabati Miundombinu
ya Skimu 32 za umwagiliaji zenye ukubwa wa
Hekta 17,824.
Aidha, kazi ya ujenzi
wa Mabwawa 8 ya Maji inaendelea na Upembuzi Yakinifu wa Miradi 25 ya Umwagiliaji yenye eneo la Hekta 17,113 umefanyika. Kutokana na juhudi hizo, eneo la umwagiliaji
Nchini limeongezeka kutoka Hekta 331,490 mwaka 2010/2011, hadi Hekta 345,690
mwaka 2011/2012. Katika mwaka 2012/2013, Serikali itashirikiana na Wadau
wa Maendeleo kuwawezesha Wakulima 33,108
katika Skimu 20 za Umwagiliaji zenye
Hekta 15,431 kulima zao la Mpunga
kibiashara kwa kutumia Teknolojia za Kisasa.
Mifugo
39.
Mheshimiwa
Spika, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka
2010 ilielekeza Serikali iandae Programu Kabambe ya Kuendeleza Sekta ya Mifugo
ambayo itajumuisha uendelezaji wa Malisho, kuchimba na kujenga Malambo, Mabwawa na Majosho na huduma za Ugani ili hatimaye Wafugaji waondokane na
ufugaji wa kuhamahama. Katika kutekeleza maelekezo hayo, Serikali kwa
kushirikiana na Wadau wa Sekta ya Mifugo imeandaa Programu ya Kuendeleza Sekta
ya Mifugo. Kukamilika kwa Programu hii kutaiwezesha Sekta
ya Mifugo kutoa mchango zaidi kwenye Pato la Taifa na kuwanufaisha Wafugaji.
Mafanikio ya Programu hii yatategemea sana Wadau wa Sekta ya Mifugo kuzingatia
Sheria Na. 13 ya Mwaka 2011
iliyopitishwa na Bunge lako inayohusu Maeneo ya Malisho na Rasilimali ya Vyakula
vya Mifugo. Nawahakikishia Wananchi kwamba Serikali itasimamia kikamilifu
utekelezaji wa Sheria hii pamoja na Programu ya Kuendeleza Sekta ya Mifugo, ili
kuleta mabadiliko kutoka kwenye Uchungaji kwenda kwenye Ufugaji wa Kisasa.
40.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imetoa Ruzuku ya
Shilingi Bilioni 1.6 zilizotumika
kununua na kusambaza lita 62,500 za Dawa
za Kuogesha Mifugo na Dozi Milioni 3.5 za Chanjo ya Ugonjwa wa Homa ya Mapafu ya Ng’ombe katika Halmashauri zote
Nchini. Serikali pia imeendelea
kushirikiana na Wadau mbalimbali kujenga na kukarabati Majosho 108 na Malambo 98.
Aidha, Kituo cha Taifa cha Uhamilishaji kilichopo Usa River, Arusha pamoja na Vituo
Vitano vya Kanda vya Afya ya Mifugo vimeimarishwa. Serikali
itaendelea kutoa Ruzuku ya Dawa za Mifugo na kuhamasisha Wafugaji na Wafanyabiashara kuwekeza zaidi
kwenye Ufugaji wa Kisasa na unenepeshaji Mifugo.
Uvuvi
41.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali ilianza kutekeleza
Mkakati wa Uendelezaji Ukuzaji Viumbe kwenye Maji kwa kuimarisha Ufugaji Samaki
na ukuzaji wa Viumbe vingine. Utekelezaji wa Mkakati huo, umeongeza idadi ya Mabwawa
ya Kufugia Samaki kutoka 19,039
mwaka 2010/2011 hadi 19,443 mwaka 2011/2012, na Vituo vya Kuzalisha Vifaranga vimeongezeka kutoka 8 hadi 10 ambapo jumla ya Vifaranga Milioni 1.9 vya Samaki vimezalishwa na kusambazwa kwa Wadau. Aidha, elimu ya
usimamizi na matumizi endelevu ya Rasilimali za Uvuvi imetolewa katika maeneo
ya Wavuvi. Vikundi 188
vilihamasishwa kufanya shughuli mbadala kwa kupatiwa elimu ya ujasiriamali
ambapo Miradi Midogo 459 ya kiuchumi
imeanzishwa. Katika mwaka 2012/2013,
Serikali itafanya Mapitio ya Sera ya Taifa ya Uvuvi ya mwaka 1997 na kuandaa
Mkakati wa utekelezaji.
Ufugaji Nyuki
42.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Ufugaji Nyuki ina mchango mkubwa katika
kuondoa Umaskini na kuhifadhi mazingira. Kwa kuzingatia fursa kubwa tuliyonayo
ya Rasilimali za Ufugaji Nyuki, Serikali imeziagiza Mamlaka za Serikali za
Mitaa zote Nchini kuanzisha Mashamba Darasa ya kutoa Elimu ya Ufugaji Nyuki.
Katika mwaka 2011/2012, jumla ya Wafugaji Nyuki 4,573 kutoka Wilaya 33
walipewa mafunzo ya Ufugaji Bora wa Nyuki. Aidha, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa
Wilaya wamepewa mafunzo kuhusu Ufugaji Bora wa Nyuki ili waweze kuwa chachu ya
uhamasishaji katika Mikoa na Wilaya kuhusu manufaa ya Ufugaji Nyuki. Kutokana
na jitihada hizo, katika mwaka 2011/2012,
uzalishaji wa Asali ulifikia Tani 9,000
zenye thamani ya Shilingi Bilioni 27
na Nta iliyozalishwa ilikuwa Tani 600
zenye thamani ya Shilingi Bilioni 3.
Aidha, tarehe 9 Juni, 2012 nilipata fursa ya kufungua Kiwanda kipya na cha Kisasa
cha Kuchakata Asali kilichojengwa na Kampuni ya Honey King Limited katika Kijiji cha Visiga Mkoani Pwani na hivyo
kufanya jumla ya Viwanda vya kuchakata na kufungasha Asali Nchini kufikia Vinane. Napenda kuwapongeza Wawekezaji hao kwa kujenga Kiwanda
chenye uwezo wa Kuchakata Tani 10,000
za Asali kwa mwaka. Nawaomba Wafugaji Nyuki kuitumia vizuri fursa hii kwa
kuzalisha Mazao ya Nyuki kwa wingi na yenye ubora ili kunufaika na Soko la
kuaminika la Kiwanda hicho na vingine vilivyopo hapa Nchini.
43.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali itaendelea kutoa elimu ya Ufugaji
Nyuki kwa Wadau mbalimbali. Aidha, ili kutangaza Ubora wa Asali na Nta ya Nchi
yetu, yatafanyika Maonyesho Maalum ya
Mazao ya Ufugaji Nyuki mwezi Oktoba 2012. Maonyesho hayo yataandaliwa kwa
ushirikiano baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Viwanda na
Biashara, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania na Wadau wengine.
Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani Mazao na Huduma za Kifedha Vijijini
44.
Mheshimiwa
Spika, Serikali ilianza utekelezaji wa Programu ya
Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani Mazao na Huduma za Kifedha Vijijini (Marketing Infrastructure Value Addition and
Rural Finance Program - MIVARF) mwezi Julai, 2011. Kazi zilizotekelezwa ni
pamoja na kuandaa mfumo wa utekelezaji ikiwemo uundaji wa Kamati za Usimamizi,
ununuzi wa Vitendea Kazi, kuajiri wafanyakazi na kuitambulisha Programu katika
Mikoa yote. Aidha, uchambuzi wa Maandiko ya Miradi iliyopokelewa kutoka
Halmashauri mbalimbali umefanyika na Halmashauri zitakazoanza kushiriki katika
utekekezaji wa Programu zimechaguliwa.
45.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/2013, Kilometa 250 za barabara za vjijini
zitakarabatiwa, maghala mawili yatajengwa na manne yatakarabatiwa. Vilevile,
vituo vinne vya mafunzo ya uongezaji thamani mazao vitakarabatiwa; Wakulima
watapatiwa mafunzo kuhusu hifadhi ya mazao, mbinu za kuyafikia masoko na Mfumo
wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani. Kazi nyingine zitakazofanyika ni kuviendeleza Vikundi
864 vya Kifedha vikiwemo VICOBA,
kuzijengea uwezo SACCOS 108 pamoja
na Asasi nyingine ndogo za Kifedha ili ziweze kutoa Huduma za Kifedha Vijijini
kwa ufanisi zaidi.
Viwanda
46.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mchango na umuhimu wa Sekta ya
Viwanda katika kuleta maendeleo endelevu, kuongeza ajira, kuongeza thamani ya
Mazao, Kukuza Masoko, kuongeza Mapato ya Serikali na fedha za kigeni. Kwa
kuzingatia umuhimu huo, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na uhamasishaji wa
Uwekezaji wa Viwanda Vipya katika Maeneo Maalum ya Uzalishaji (EPZ) na Maeneo
Maalum ya Uchumi (SEZ). Idadi ya Makampuni yaliyosajiliwa katika maeneo hayo
imeongezeka kutoka 44 mwaka 2010/2011 hadi 54 mwaka
2011/2012. Uwekezaji wa Mitaji umeongezeka kutoka Shilingi Trilioni 1.02 hadi Trilioni 1.1. Pia, mauzo ya Nje yameongezeka kutoka Shilingi Bilioni 560.5 hadi Bilioni 706.5 na Ajira zimeongezeka kutoka 13,500 hadi 15,100.
47.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali
itaimarisha Sekta ya Viwanda kwa kuhimiza uwekezaji katika Viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na bidhaa
za kilimo na kuwaunganisha Wakulima na wenye Viwanda ili kuwawezesha kupata
Soko la uhakika. Aidha, itaendelea
kuweka umuhimu katika utekelezaji wa miradi ya Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na Chuma
cha Liganga.
Madini
48.
Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua mbalimbali zenye lengo la
kuboresha Sekta ya Madini ili Taifa linufaike zaidi na Rasilimali hiyo. Hatua
hizo ni pamoja na kuimarisha Shirika la Madini la Taifa - STAMICO ili liweze
kuchukua Hisa kwa niaba ya Serikali katika Migodi Mipya inayotarajiwa
kuanzishwa. Kupitia utaratibu huo, STAMICO inamiliki Asilimia 45
ya hisa katika Mgodi wa Backreef na
Asilimia 55 zinamilikiwa na
Mwekezaji. Hatua nyingine ni kuwawezesha
Wachimbaji Wadogo kuanzisha Vituo
vya kuwasaidia kukopeshwa na kununua Vifaa vya Kisasa vya kuchimbia Madini
katika maeneo ya Rwamgasa - Geita, Londoni – Manyoni na Pongwe – Bagamoyo.
Aidha, kupitia
Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini, shughuli za Ukaguzi katika Migodi mikubwa
zimeimarishwa na sasa Migodi mingi imeanza kulipa Kodi ya Mapato.
49.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imechukua hatua madhubuti kuhakikisha kwamba
Makampuni yote Makubwa ya Madini
yanalipa mrabaha wa Asilimia Nne (4) kwa kuzingatia matakwa ya Sheria Mpya
ya Madini Na. 14 ya mwaka 2010. Makampuni ya madini ambayo hayajazingatia
matakwa haya ya Kisheria yametakiwa kulipa malimbikizo yote tangu Sheria hiyo
ilipopitishwa mwaka 2010. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, hakuna Kampuni ya Madini ambayo itakwepa
kulipa Mrabaha kwa Kiwango kipya na Kodi zote kama inavyotakiwa. Tutakuwa
makini kuhakikisha kwamba Sheria na Taratibu za Biashara ya Madini na Hifadhi
ya Mazingira zinafuatwa na kila Mmiliki wa Mgodi. Napenda
kutoa wito kwa Wachimbaji Wadogo, jamii
inayozunguka Migodi Mikubwa pamoja na wamiliki wa Migodi mikubwa kushirikiana
kwa karibu na kila mmoja atimize wajibu wake ili kuleta mahusiano mazuri na
kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima.
Utalii
50.
Mheshimiwa Spika, kutokana na juhudi zinazoendelea za kutangaza Vivutio
mbalimbali vya Utalii, idadi ya Watalii imeongezeka kutoka 782,699 mwaka
2010 hadi 867,994 mwaka 2011, sawa
na ongezeko la Asilimia 11. Mapato yatokanayo na Utalii yameliingizia
Taifa Shilingi Trilioni 2.14 mwaka
2011 ikilinganishwa na Shilingi Trilioni
1.96 mwaka 2010. Serikali pia, imeandaa
Programu ya Kutunza na Kuweka Kumbukumbu za Urithi wa Malikale ili kupanua wigo wa Vivutio vya Utalii. Hatua hii itaiwezesha Tanzania kutangaza zaidi
maeneo ya urithi wa Utamaduni wetu pamoja na Maeneo 22 ya Wapigania Uhuru kwa ajili ya Ukombozi wa Bara la Afrika. Katika mwaka 2012/2013, Serikali
itaongeza kasi zaidi ya kutangaza Vivutio vya Utalii wetu nje ya Nchi, kwa
kutumia Balozi zetu pamoja na Tovuti; kuwavutia Wawekezaji wa Nje na Ndani
katika Sekta ya Utalii na kuhamasisha Utalii wa Ndani.
AJIRA
51.
Mheshimiwa Spika, Vijana ndiyo sehemu kubwa ya nguvu kazi katika Nchi
yetu. Inakadiriwa kuwa Asilimia 35 ya
Watanzania wote ni Vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35. Aidha,
Vijana ni Asilimia 68 ya Watanzania
wote wenye nguvu na uwezo wa kufanya kazi. Jitihada kubwa za Serikali
zinaendelea kuwekwa katika kutoa msukumo kwenye uwekezaji katika sekta zenye
fursa kubwa ya kutoa ajira nyingi kama vile
kilimo, mifugo, uvuvi, ufugaji nyuki, ujenzi, mawasiliano, uchukuzi, utalii
na viwanda. Aidha, ili kuwawezesha Vijana kupata mitaji, Serikali imeongeza
mtaji kwa Benki ya Rasilimali, Benki ya Wanawake, Benki ya Posta pamoja na
Mifuko mbalimbali ya Uwezeshaji wananchi Kiuchumi. Vilevile, Mafunzo ya
Ujasiriamali na Elimu ya Ufundi Stadi
kwa Vijana waishio Mijini na Vijijini yataimarishwa kwa lengo la kuwaongezea
sifa katika Soko la Ajira, hasa Sekta Binafsi.
52.
Mheshimiwa
Spika, ufumbuzi wa
uhakika wa tatizo la Ajira hususan kwa Vijana utatokana na jitihada za makusudi
za kuongeza uwekezaji katika sekta zote. Napenda kutoa rai kwa Viongozi na
Watendaji wote kwenye ngazi ya Taifa, Mikoa, Wilaya na Mamlaka za Serikali za
Mitaa; kuhakikisha kwamba wanaongeza jitihada za kuboresha mazingira ya
uwekezaji ili kuvutia wawekezaji na kuongeza kasi ya ukuaji wa Sekta Binafsi.
HUDUMA ZA KIUCHUMI
Ardhi
53.
Mheshimiwa
Spika, Ardhi
ni Rasilimali muhimu katika Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini. Hata hivyo, ili
kunufaika na Rasilimali hiyo, ni muhimu Ardhi ipimwe na kuwa na Mpango endelevu
wa matumizi bora ya Ardhi. Kwa kuzingatia umuhimu huo, hadi kufikia Aprili 2012, mipaka ya Vijiji 11,261 ilipimwa. Vyeti vya Ardhi ya Vijiji 3,283 vilitolewa, upimaji wa Viwanja 26,788 na Mashamba 706
ulifanyika na Hati za Hakimiliki za Kimila 46,063
zilitolewa na kufanya jumla ya Hati za Hakimiliki za Kimila zilizokwishatolewa Nchini
kote kufikia 157,968.
54.
Mheshimiwa Spika, ili kuwawezesha Wananchi kunufaika na Rasilimali
Ardhi wanayomiliki, Serikali
itakamilisha Mradi wa Kuweka Kituo cha
Kupokea Picha za Satellite (Direct Satellite Imagery Receiving Station). Kituo hicho
kitawawezesha Wananchi kupimiwa ardhi yao na kupatiwa hati kwa vile upimaji na
utayarishaji wa ramani kwa ardhi yote Nchini utakuwa umerahisishwa kwa kiasi
kikubwa. Huu utakuwa ukombozi wa kiuchumi kwa Watanzania.
55.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha kujenga Mtandao Mpya wa Alama
za Msingi za Upimaji Ardhi Nchini (National
Geodetic Control Unit). Alama hizo zinatarajiwa kuanza kutumika mwezi
Julai, 2012. Mtandao wa Alama hizo,
utarahisisha Upimaji wa Ardhi kwa matumizi mbalimbali na kupunguza gharama za
upimaji Nchini.
Nishati
56.
Mheshimiwa
Spika,
mwezi Agosti 2011, Serikali iliwasilisha Bungeni Mpango wa Dharura wa Kuondoa
Mgao wa Umeme uliokuwepo Nchini. Mgao huo ulisababishwa kwa kiasi kikubwa na
kupungua kwa uzalishaji hasa kwenye Vyanzo vya Umeme vya Maji. Kutokana na utekelezaji wa Mpango wa Dharura
wa Umeme hadi kufikia mwezi Aprili 2012, jumla ya Megawati 342 zimezalishwa na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa. Uzalishaji huo
umeimarisha hali ya upatikanaji Umeme na hivyo Makali ya Mgao kupungua. Hata
hivyo, uzalishaji wa Umeme wa Dharura ni wa gharama kubwa kutokana na Mitambo
mingi kuendeshwa kwa kutumia Mafuta ya Dizeli.
57.
Mheshimiwa
Spika, hatuwezi kuendelea na hali hii ya uzalishaji
umeme kwa gharama kubwa huku tukiwa na Rasilimali zinazoweza kubadili kabisa
hali hiyo. Kwa hiyo, Serikali imeanza kutekeleza Mradi mkubwa wa ujenzi wa
Bomba la Gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa lengo la kuongeza kiasi cha
Gesi itakayotumika kuendesha Mitambo ya Uzalishaji Umeme. Tayari fedha za
kutekeleza mradi huu zimepatikana na ujenzi unatarajiwa kuanza mwaka 2012/2013.
Serikali pia katika mwaka 2011/2012 imetoa Shilingi Bilioni 39 ikiwa ni sehemu ya mchango wake
katika ujenzi wa Mradi huo. Fedha nyingine kiasi cha Shilingi Bilioni 110 zimewekwa katika Bajeti ya
2012/2013.
58.
Mheshimiwa
Spika, hatua nyingine ambayo Serikali imechukua kutatua
tatizo la Umeme Nchini ni kuongeza ushiriki wa Sekta Binafsi katika uzalishaji
na usafirishaji wa umeme. Kwa kuanzia, Serikali inashirikiana na Serikali ya
Marekani kubaini vikwazo vinavyozuia Sekta Binafsi kuwekeza kwenye Miradi
mikubwa ya Umeme. Kazi hiyo itafuatiwa na utekelezaji wa Mpango Maalum wa
Pamoja wa Miaka Mitano utakaoanza kutekelezwa mwaka 2012/2013. Lengo ni
Kuzalisha Umeme wa MW 2,700 ifikapo
mwaka 2016.
59.
Mheshimiwa
Spika, Wakala wa Umeme Vijijini unatekeleza Programu
Kabambe ya Kusambaza Umeme Vijijini katika Mikoa 16. Mikoa hiyo ni Kigoma, Kagera, Mwanza, Mara, Shinyanga, Arusha,
Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Mbeya, Rukwa na
Tabora. Chini ya Programu hiyo, Miradi Midogo 41 inatekelezwa ambapo Wateja 22,000
watalipiwa gharama za kuunganisha Umeme kupitia Mfuko wa Nishati Vijijini.
Programu hiyo itawawezesha Wananchi wengi zaidi Vijijini kupata Nishati ya
Umeme ili kuharakisha maendeleo katika maeneo hayo.
60.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na jitihada za Serikali za kuvutia
uwekezaji katika Sekta ya Nishati, kasi ya utafutaji na ugunduzi wa hazina mpya
ya Gesi Asili Nchini imeongezeka. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba,
hivi karibuni Makampuni yanayofanya utafiti wa Gesi Asili Nchini yamegundua
kiasi kikubwa cha Gesi Asili yenye futi za ujazo Trilioni 3. Gesi hiyo imegundulika kwenye kina cha maji marefu
baharini takriban Kilometa 80 kutoka
Nchi kavu Mashariki mwa Mkoa wa Lindi. Ugunduzi huo unafanya kiasi cha Gesi
kilichogundulika hadi sasa kwenye kina cha maji marefu baharini kufikia futi za
ujazo Trilioni 20.97. Kwa kuzingatia
fursa zinazotokana na kasi kubwa ya ukuaji wa Sekta ya Gesi Nchini, Serikali
imejipanga kuhakikisha kwamba Taifa linanufaika kikamilifu na ugunduzi wa
rasilimali hiyo. Serikali inaandaa Sera na Sheria Mahsusi ya Gesi Asili pamoja
na Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi kwa lengo la kuimarisha usimamizi na
uendelezaji wa sekta hiyo. Aidha, Serikali itawawezesha Vijana wetu kupata
Mafunzo Maalum (Specialized Training)
yanayohusiana na masuala ya Gesi Asili kwa lengo la kupata Wataalam Wazalendo
waliobobea kwenye sekta hii kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa Miaka Mitano.
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
61.
Mheshimiwa
Spika, Nchi zote Duniani zimeazimia kubadili Teknolojia
ya Utangazaji kutoka Analojia kwenda Dijitali ambayo imeonekana kuwa na tija na
yenye kutumiwa na Vifaa vingi zaidi vya Mawasiliano. Kwa kuzingatia azimio hilo, Nchi za Jumuiya
ya Afrika Mashariki nazo zimekubaliana kutekeleza mabadiliko hayo na kuanza Kurusha
Matangazo katika Mfumo wa Dijitali pekee ifikapo tarehe 31 Desemba 2012. Ili Watanzania wawe tayari kuyapokea mabadiliko
hayo, Serikali imeandaa mpango wa kuelimisha Umma unaojulikana
kwa jina la “Digital Tanzania” ambao
ulizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, mwezi Agosti 2011. Wananchi wote watambue
kwamba mabadiliko ya Teknolojia za Utangazaji
kutoka Analojia kwenda Dijitali ni matokeo ya ukuaji
wa kasi wa Teknolojia ya Mawasiliano ambao hatuwezi kuuepuka.
62.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2011/2012, Awamu ya Pili ya Ujenzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa wenye
urefu wa Kilomita 3,000 umekamilika
na kuanza kutumika. Kukamilika kwa Awamu hii kunafanya Nchi yetu kuwa na Mkongo
uliojengwa wenye jumla ya Kilometa 7,300 na kumeiwezesha
Mikoa yote ya Tanzania Bara kuunganishwa kwenye Mkongo huo. Aidha, Mkongo wa
Mawasiliano wa Taifa umeunganishwa na Kisiwa cha Pemba kupitia Tanga. Katika mwaka 2012/2013, Kisiwa cha Unguja
kitaunganishwa na Mkongo huo kupitia Dar es Salaam, baada ya kukamilika kwa
ujenzi wa Mkongo wa Majini.
Barabara na Madaraja
63.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imeendelea kujenga,
kukarabati na kuzifanyia matengenezo Barabara Kuu, za Mikoa na Wilaya ili
ziweze kupitika wakati wote. Hadi mwezi Mei
2012, Serikali imejenga jumla ya Kilometa 305.6
za Barabara Kuu na Kilometa 29.5 za Barabara
za Mikoa kwa kiwango cha Lami. Pia,
imefanya ukarabati mkubwa wa Kilometa 78.4
za Barabara Kuu kwa kiwango cha Lami na Kilometa 463.2 kwa kiwango cha Changarawe katika Barabara za Mikoa. Aidha, jumla ya Kilometa 7,209 za Barabara za Mamlaka ya Serikali za Mitaa zimefanyiwa
matengenezo ya kawaida. Vilevile, ujenzi wa Daraja la Nangoo lililopo Mtwara na
Daraja la Malagarasi Mkoani Kigoma umeanza.
64.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali imepanga kujenga
Kilometa 414 na kukarabati Kilometa 135 kwa kiwango cha Lami pamoja na
kujenga Madaraja 11 katika Barabara
Kuu. Vilevile, itajenga Kilometa 573
kwa kiwango cha Changarawe na Kilometa 32
kiwango cha Lami katika Barabara za Mikoa pamoja na Madaraja 27.
Katika kipindi hicho, Mfuko wa Barabara unatarajiwa kuingiza zaidi ya
Shilingi Bilioni 400 ambazo
zitatumika kwa ajili ya matengenezo, ujenzi na usimamizi wa Miradi mbalimbali
ya Barabara, zinazosimamiwa na TANROADS na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Bandari
65.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imeendelea kuboresha
miundombinu na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma katika Bandari Kuu za Dar es
Salaam, Tanga na Mtwara pamoja na kukarabati Bandari za Kigoma na Mwanza.
Aidha, imekamilisha Upembuzi Yakinifu wa ujenzi wa Bandari Mpya ya Mbegani
(Bagamoyo) na Mwambani Tanga.
Reli
66.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali iliweka Menejimenti
Mpya ya Shirika la Reli (TRL) inayoongozwa na Wazalendo. Serikali pia ilitoa fedha
za kukarabati Miundombinu chakavu ya Reli ya Kati ikiwa ni pamoja na ukarabati
wa Injini za Treni na Mabehewa ya Abiria. Aidha,
kazi ya usanifu wa kina kwa ajili ya kuijenga Reli ya Kati kwa kiwango cha
Kimataifa (Standard Gauge) na
kuiunganisha na Nchi za Rwanda na Burundi imeanza mwezi Februari 2012 na
inatarajiwa kukamilika Mwaka 2013.
67.
Mheshimiwa Spika, Serikali za Tanzania, Zambia na Jamhuri ya Watu wa
China mwezi Machi 2012, zimesaini Mikataba yenye Thamani ya Shilingi Bilioni 66.67 kwa ajili ya kuboresha
Miundombinu na huduma za TAZARA. Mikataba
hiyo itatekelezwa kuanzia mwaka 2012/2013. Jitihada hizo zitawezesha huduma
za Reli kuimarika na hivyo kutoa mchango mkubwa katika uchumi wetu.
HUDUMA ZA JAMII
Elimu
Elimu ya Msingi
68.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imeanza kufanya Mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka
1995 kwa lengo la kuiboresha ili kuendana na Mazingira ya sasa. Kazi hiyo inatarajiwa kukamilika Mwaka
2012/2013. Aidha, Serikali iliendelea na Utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango
wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi ambapo jumla ya Madarasa 485 na Nyumba za Walimu 344
zilijengwa na Madawati 61,363
yalinunuliwa. Katika kipindi hicho, jumla ya Walimu 11,243 waliajiriwa
na 2,259 walipewa mafunzo kazini ili
kuongeza ubora wa ufundishaji wa Masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza.
Lengo ni kuwajengea Walimu uwezo wa kufundisha na hatimaye kuongeza kiwango cha
Ufaulu wa Wanafunzi katika masomo hayo.
Elimu ya Sekondari
69.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2011/2012, utekelezaji wa Awamu ya Pili
ya Mpango wa Elimu ya Sekondari (MMES II) umekuwa na mafanikio ya kuridhisha. Jumla
ya Madarasa 1,316, Maabara 127 na Nyumba za Walimu 270 zilijengwa na Madawati 123,855 yalinunuliwa. Katika kipindi
hicho, jumla ya Walimu wa Sekondari 13,900
wameajiriwa na Vitabu Milioni 1.5 vilinunuliwa na kusambazwa katika
Shule mbalimbali za Sekondari. Wanafunzi waliojiunga na Kidato cha Kwanza
waliongezeka kutoka 456,350 Mwaka
2011 hadi 517,993 Mwaka 2012. Hili
ni ongezeko la Wanafunzi 61,643.
70.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali itaendelea kuimarisha Miundombinu ya Shule za Sekondari ili kuboresha mazingira ya
kufundishia na kujifunzia. Jitihada zitaongezwa katika kuhamasisha ujenzi wa
Madarasa zaidi kwa ajili ya Wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Tano na Sita
kukidhi mahitaji makubwa yaliyojitokeza baada ya kupanuliwa kwa Elimu ya
Sekondari Nchini.
Mafunzo ya Ufundi Stadi
71.
Mheshimiwa Spika, Mafunzo ya Ufundi Stadi yana mchango mkubwa katika
kuwapatia ujuzi na kuwajengea uwezo Wanafunzi wanaohitimu Elimu ya Msingi na
Sekondari. Katika mwaka 2011/2012, Serikali imekamilisha ujenzi wa Vyuo
vya Mafunzo ya Ufundi Stadi
katika Mikoa ya Lindi, Pwani, Manyara, Arusha na Dar es Salaam.
Kukamilika kwa Vyuo hivyo kumeongeza idadi ya Wanafunzi wanaojiunga na Vyuo vya
Ufundi kutoka 72,938 mwaka 2010 hadi
102,217 mwaka 2011. Katika Mwaka
2012/2013, Serikali itapanua zaidi
Mafunzo ya Ufundi Stadi Nchini.
Elimu ya Juu
72.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali ilitekeleza Mpango
wake wa kuimarisha Miundombinu ya Vyuo Vikuu na Vyuo vya Elimu ya Juu
Nchini. Kutokana na hatua hiyo, Udahili
wa Wanachuo katika Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki uliongezeka kutoka Wanachuo 40,993 mwaka 2005/2006 hadi 139,638
mwaka 2010/2011. Idadi ya Wanachuo waliopewa mikopo ya elimu ya juu ikijumuisha
Wanachuo wa Vyuo Vikuu na Vyuo vingine iliongezeka kutoka 42,729 mwaka 2005/2006 hadi 93,784
mwezi Aprili 2012. Aidha, katika kipindi hicho, fedha zilizokopeshwa Wanachuo hao
ziliongezeka kutoka Shilingi Bilioni 56.1 hadi Bilioni 291. Katika
Mwaka 2012/2013, Serikali itatoa kipaumbele katika kuongeza ubora wa Elimu ya
Juu ili kuendana na mahitaji ya Soko la Ajira Nchini na katika Jumuiya ya
Afrika Mshariki.
Afya
73.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imetekeleza Mpango wa
kugawa Vyandarua vyenye Dawa ili kupunguza Maambukizi ya Ugonjwa wa
Malaria. Hadi Desemba 2011 jumla ya
Vyandarua Milioni 17.6 viligawanywa
bila malipo kwa kila Kaya yenye Watoto wenye umri chini ya Miaka Mitano Nchi
nzima. Sambamba na hatua hiyo, Mpango wa Kunyunyizia Dawa ya Ukoko aina ya ICON
kwenye kuta za Nyumba ili kuua mbu ulitekelezwa katika Wilaya 18 za Mikoa ya Kagera, Mwanza na Mara
ambayo imeonekana kuwa na Maambukizi makubwa ya Malaria. Aidha, jitihada za
kuongeza upatikanaji wa Dawa Mseto za kutibu Malaria kwa bei yenye punguzo
zinaendelea. Jitihada za udhibiti wa malaria zimechangia kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka vifo 99 kwa kila watoto 1,000
mwaka 1999 hadi vifo 51 kwa kila
watoto 1,000 mwaka 2010. Vilevile, vifo vya watoto wa umri chini ya miaka mitano
vimepungua kutoka vifo 147 kwa
kila watoto 1,000 mwaka 1999 hadi
vifo 81 kwa kila Watoto 1,000 mwaka 2010.
74.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali itaendelea na
utekelezaji wa Mpango wa Kuangamiza Viluwiluwi vya Mbu kwa kutumia njia za
Kibaiolojia kwa ushirikiano na Serikali ya Cuba. Mpango huo ulianza mwaka 2011
kwa majaribio katika Jiji la Dar es Salaam. Aidha, Serikali itaandaa Mkakati
Maalum wa kugawa Vyandarua kupitia Shuleni ili kuhakikisha kuwa matumizi ya
Vyandarua yanakuwa endelevu. Natoa wito kwa Wananchi wote kutumia Vyandarua
vinavyotolewa na Serikali kwa lengo lililokusudiwa badala ya matumizi mengine. Vilevile, nawahimiza kutokomeza Mazalia ya
Mbu na kuweka Mazingira katika hali ya Usafi ili tufanikiwe kuondoa Ugonjwa wa
Malaria Nchini.
75.
Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kupunguza idadi kubwa ya Wagonjwa wa Moyo wanaopoteza maisha kwa
kukosa Tiba Stahiki na gharama kubwa inayotumika kupata Tiba hiyo nje ya Nchi.
Ili kutekeleza dhamira hiyo, katika mwaka 2011/2012, Serikali kwa kushirikiana
na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imekamilisha ujenzi wa Kituo cha Kisasa
cha Upasuaji, Tiba na Mafunzo ya Ugonjwa wa Moyo katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili. Pamoja na mafanikio hayo, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili iliendelea
kutoa huduma za Upasuaji Mkubwa wa Moyo ambapo hadi mwezi Aprili, 2012 jumla ya
Wagonjwa 300 walipata huduma hiyo na
hivyo kuokoa zaidi ya Shilingi Bilioni Sita (6) ambazo zingetumika kuwapeleka Wagonjwa hao Nje ya Nchi. Napenda
kuwapongeza Madaktari na Wahudumu wote wa Afya kwa huduma nzuri wanayotoa kwa wagonjwa. Nawasihi
kuendelea na moyo huo, kwani wamepewa dhamana kubwa ya kuwahudumia wananchi kutokana
na ujuzi na weledi walionao.
Huduma kwa Watu wenye Ulemavu
76.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imekamilisha zoezi la
kuandaa Kanuni za utekelezaji wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu iliyopitishwa na
Bunge mwaka 2010. Utekelezaji wa Sheria
hiyo umeanza ambapo Watu wenye Ulemavu wanapatiwa haki na huduma za msingi
ikiwemo elimu, afya, ajira na kulindwa Kisheria. Kwa Watu wenye Ulemavu wa
Ngozi, Serikali kwa kiasi kikubwa imedhibiti Vitendo vya Ukatili
walivyokuwa wanafanyiwa. Napenda kutumia fursa hii kutoa
Wito kwa Wananchi wote kuwapenda na kuwahudumia Walemavu wakiwemo Watu wenye
Ulemavu wa Ngozi.
Lishe
77.
Mheshimiwa Spika, katika Hotuba yangu ya Bajeti ya mwaka 2011/2012,
nililitaarifu Bunge kuhusu hali isiyoridhisha ya Lishe hapa Nchini na hatua
ambazo Serikali imeanza kuzichukua kukabiliana na hali hiyo. Napenda
kulifahamisha Bunge lako kuwa, Mkakati
wa Kitaifa wa Lishe ulizinduliwa
rasmi tarehe 20 Septemba,
2011. Mkakati huo umeainisha maeneo ya kipaumbele ambayo yatatekelezwa katika
kipindi cha Miaka Mitano ili kupunguza idadi ya Watoto wenye Uzito Pungufu,
Udumavu, pamoja na idadi ya Wanawake Wajawazito wenye Upungufu wa Damu.
78.
Mheshimiwa Spika, ili kuliongezea uzito
suala la Lishe, Kamati zitakazohakikisha kwamba Mkakati wa Lishe unatekelezeka kikamilifu zimeanzishwa katika ngazi ya Taifa na
Halmashauri. Napenda kutoa msisitizo wa kipekee kwamba Lishe Bora ni muhimu kwa
maendeleo ya Watu na
Taifa kwa ujumla.
Lishe Duni ina Madhara makubwa
hasa kwa Watoto wadogo; Mtoto mdogo anapokosa Lishe Bora, maendeleo yake katika
masomo yana walakini mkubwa na hali hiyo haiwezi kurejeshwa tena. Hivyo, Watendaji katika ngazi zote watoe
umuhimu mkubwa kwenye suala la Lishe Bora kwa kuendelea kutoa elimu ya Lishe
Bora ili Wananchi walielewe na wale chakula chenye Virutubisho muhimu ambavyo
vipo kwenye maeneo mengi Nchini.
Maji
79.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeboresha huduma ya maji Vijijini kwa kujenga Miradi
mipya, kupanua na kukarabati iliyopo kwa kushirikisha Wananchi. Katika mwaka
2011/2012, Serikali kwa kushirikiana na
Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) iliendelea na utekelezaji wa mradi wa
maji katika Wilaya za Moshi Vijijini na Hai. Vilevile, kwa kushirikiana na
Serikali ya Japan iliendelea kutekeleza mradi wa maji Vijijini katika Mikoa ya
Mwanza, Mara na Tabora. Aidha, Serikali
imeendelea na juhudi zake za kujenga mabwawa ya maji katika maeneo kame Nchini.
Mabwawa yanayoendelea kujengwa ni Kawa (Nkasi), Sasajila (Chamwino), Matwiga
(Chunya), Nyambori (Rorya), Wegero (Musoma), Habiya (Bariadi), Iguluba
(Iringa), Mwanjoro (Meatu) na Seke Ididi (Kishapu).
80.
Mheshimwa Spika, Serikali pia, imeimarisha usimamizi na uendelezaji wa Rasilimali
za Maji katika Mabonde yote Tisa (9)
ya Maji Nchini na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa Kutunza Vyanzo vya Maji katika
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, Serikali imejenga Visima 946 katika Halmashauri 84.
81.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mijini, Serikali imejenga na kukarabati Mifumo ya Maji katika Miji Mikuu ya Mikoa
19. Kutokana na jitihada hizo,
kiwango cha upatikanaji wa Maji kwa wakazi wa Miji hiyo kimeongezeka kutoka Asilimia
84 mwaka 2010 hadi kufikia Asilimia 86 mwaka 2011. Katika mwaka 2012/2013,
Serikali itaendelea kuboresha upatikanaji wa Maji Mijini kwa kuimarisha
utendaji wa Mamlaka za Maji za Miji Nchini. Kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam,
Serikali itakamilisha upanuzi wa Mtambo
wa Ruvu Chini na kuanza ujenzi wa Bomba Jipya la Maji kutoka Ruvu Chini hadi
kwenye Matenki ya Maji yaliyopo maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Aidha, itakamilisha Usanifu wa Mradi wa Kuchimba
Visima Virefu katika maeneo ya Kimbiji na Mpera na kuanza ujenzi wa Visima
hivyo.
ULINZI NA USALAMA
82.
Mheshimiwa
Spika, Majeshi yetu ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
yanafanya kazi nzuri kuhakikisha kwamba hali ya Usalama wa Nchi na Mipaka yetu
ni shwari. Aidha, Majeshi yetu yameshiriki kikamilifu katika shughuli za kiraia
kusaidia Wananchi wakati wa Majanga hususan mafuriko, ajali na milipuko ya magonjwa.
Pamoja na kazi hizo, katika
mwaka wa 2011/2012, Jeshi la Kujenga
Taifa limekamilisha ukarabati wa Makambi 10
ya Jeshi la Kujenga Taifa yenye uwezo wa kuchukua Vijana 20,000 kwa wakati mmoja. Kwa mwaka 2012/2013, jumla ya Vijana 5,000 wataanza tena kujiunga na JKT
kwa Mujibu wa Sheria.
83.
Mheshimiwa
Spika, katika kuitikia Wito wa kutekeleza Azma ya KILIMO KWANZA, mwaka 2011/2012, Jeshi
la Kujenga Taifa limezalisha Tani 731.5
za mbegu bora zenye thamani ya Shilingi Milioni 544.4. Katika
mwaka 2012/2013, Serikali itaendelea
kuyawezesha Majeshi yetu kwa Vifaa na Zana za Kivita na upatikanaji wa mahitaji
muhimu. Serikali pia itaendelea kukarabati Makambi ya Jeshi la Kujenga
Taifa kwa ajili ya kuchukua Vijana wengi zaidi na pia kujenga maghala salama ya
kuhifadhia silaha, mabomu na milipuko.
84.
Mheshimiwa
Spika, Waheshimiwa Wabunge watakubaliana na mimi kwamba
Jeshi la Polisi linafanya kazi kubwa ya kudhibiti Matukio ya Uhalifu hapa Nchini.
Mafanikio hayo yamepatikana kutokana na ushirikiano mzuri kati ya Polisi na
Wananchi kupitia Mkakati wa Ulinzi Shirikishi. Moja ya Mbinu zinazotumika na
Jeshi hilo ni kuwashirikisha Wadau, hasa Viongozi wa Kijamii kama vile Wazee wa
Kimila, Madhehebu ya Dini, Vyama vya Hiari katika kuhamasisha Wananchi kuzuia
na kudhibiti Uhalifu Nchini. Mbinu nyingine ni kudhibiti tatizo la kuzagaa kwa
Silaha Ndogo Nchini kwa Kusajili na kuhamasisha Wananchi kujitokeza kuwekewa Alama
Maalum kwenye Silaha wanazomiliki. Hadi kufikia mwezi Februari 2012, jumla ya Silaha
Ndogo 1,250 zilisajiliwa. Natumia
fursa hii kuvipongeza Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama kwa kazi nzuri wanayofanya
kuhakikisha Nchi yetu inakuwa salama.
85.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na mafanikio hayo, tunayo changamoto ya Ajali nyingi za Barabarani. Ajali hizo
zimeendelea kupoteza maisha ya Watu wengi na kusababisha Ulemavu wa Kudumu kwa
wengine. Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Wadau wengine lijipange
kukabiliana na Ajali hizo kwa umakini ili kuokoa maisha ya Watanzania
yanayopotea kutokana na Ajali ambazo zinazuilika. Hii ni pamoja na kuendelea kutoa elimu ya Usalama Barabarani; kufanya
ukaguzi wa mara kwa mara; kuwachukulia hatua za Kisheria Madereva Wazembe na
kuweka Mfumo madhubuti wa kudhibiti Mwendo Kasi wa Magari.
USHIRIKIANO WA KIMATAIFA NA KIKANDA
86.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inatekeleza Sera ya Diplomasia ya
Uchumi inayoweka umuhimu katika ushirikiano wenye maslahi ya kiuchumi kwa Nchi
yetu na Nchi nyingine pamoja na Mashirika ya Kimataifa. Tayari tumeanza kushuhudia
mafanikio ya Sera hii kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Balozi zetu kwa
kudumisha mahusiano mema na kuitangaza Tanzania katika medani za Kimataifa. Jitihada
hizo, zimewezesha kuvutia Wawekezaji wengi, kuongeza idadi ya Watalii, fursa za
kibiashara na ajira.
87.
Mheshimiwa
Spika, katika kuimarisha Mtangamano wa Jumuiya ya
Afrika ya Mashariki Nchi Wanachama zinatekeleza makubaliano ya kuanzisha Vituo
vya Utoaji Huduma kwa Pamoja Mipakani (One
Stop Boarder Posts). Hadi sasa ujenzi wa Vituo Vinne vya Mpakani vya Horohoro, Holili, Sirari na
Mtukula uko katika hatua
za kukamilika.
Pamoja
na hatua hizo, mwenendo wa biashara baina ya Tanzania na Jumuiya Afrika ya
Mashariki umezidi kuimarika ambapo mauzo nje yameongezeka kwa Asilimia 12.8 kutoka Shilingi Bilioni 512.76 mwaka 2010 hadi Shilingi Bilioni
578.39 mwaka 2011. Serikali inaendelea na maandalizi ya Sera
ya Mtangamano ambayo itakuwa mwongozo wa utekelezaji wa shughuli za Kitaifa za
Mtangamano wa Kikanda na Mkakati wa Utekelezaji wa Soko la Pamoja.
TAWALA ZA MIKOA NA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA
88.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2010/2011, Serikali ilitangaza nia ya kuanzisha
maeneo Mapya ya Utawala ya Mikoa minne ya Simiyu, Katavi, Njombe na Geita
pamoja na Wilaya Mpya 19 na Tarafa 34 kwa lengo la kusogeza na kurahisisha
utoaji wa huduma kwa Wananchi. Tayari Serikali imeyaanzisha rasmi Maeneo hayo
na Uteuzi wa Viongozi wa kusimamia Mikoa na Wilaya hizo umefanywa.
89.
Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha Viongozi wa Mikoa na Wilaya kutekeleza
majukumu yao ipasavyo, Serikali imetoa Mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa
Wilaya zote Nchini mwezi Mei, 2012. Aidha, Serikali imetekeleza ahadi yake ya
kutoa Mafunzo kwa Madiwani 4,451
Nchini. Ni imani yangu kwamba baada ya mafunzo hayo, utendaji kazi wa Viongozi
hao utakuwa ni wa ufanisi zaidi.
90.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusogeza huduma kwa Wananchi kwa
kuzipandisha hadhi Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mamlaka za Miji
Midogo ya Geita, Bariadi na Tarime
zimepandishwa hadhi na kuwa Halmashauri za Miji. Vilevile, Tangazo la kuanzishwa kwa
Halmashauri za Manispaa za Lindi na Ilemela limetolewa kwenye Gazeti la
Serikali Na.182 na 256, na Tangazo la Kupandishwa Hadhi kwa
Halmashauri ya Manispaa ya Arusha kuwa Halmashauri ya Jiji limetolewa katika
Gazeti la Serikali Na. 341. Serikali
inaendelea na taratibu za kuanzisha Halmashauri za Wilaya 25 Mpya zikiwemo 19
kwenye Wilaya Mpya zilizoanzishwa na sita kutokana na kugawa baadhi ya
Halmashauri.
91.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa wakati nahitimisha mjadala wa Hotuba ya
Bajeti ya Ofisi yangu mwaka jana, niliahidi kuwa Serikali itaangalia upya viwango vya Posho za Waheshimiwa Madiwani
kwa lengo la kuviongeza. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba zoezi hilo
limekamilika na kuanzia mwaka 2012/2013
Waheshimiwa Madiwani watalipwa Viwango Vipya vya Posho vilivyoboreshwa.
MASUALA MTAMBUKA
Jinsia
92.
Mheshimiwa
Spika, Ibara ya 176
ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010, inahimiza kutambua uwezo na nguvu kubwa ya
Wanawake katika kusukuma kasi ya maendeleo na kuleta mageuzi ya Kiuchumi, Kijamii
na Kisiasa. Katika mwaka 2011/2012, Serikali
imeandaa Mkakati na Mwongozo wa Kitaifa wa Kuzuia Ukatili wa Kijinsia Nchini.
Aidha, imeunda na kuzindua Kamati ya Kitaifa ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake
na Watoto. Katika
mwaka 2012/2013, Serikali itaendelea kutoa fursa zaidi za kuwawezesha Wanawake
katika Nyanja mbalimbali pamoja na kuratibu Utekelezaji wa Mikataba ya Kikanda
na Kimataifa kuhusu Haki za Wanawake na Watoto.
Vita Dhidi ya Rushwa
93.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imeendelea na Mapambano
Dhidi ya Vitendo vya Rushwa Nchini. Jumla ya Tuhuma zilizopokelewa hadi Mei
2012 ni 4,498. Kati ya hizo, Tuhuma 884 uchunguzi wake umekamilika na
majalada yamefunguliwa. Aidha, Kesi 612
ziliendeshwa Mahakamani; na Kati ya hizo, Kesi 478 zinaendelea na 134
zilitolewa uamuzi ambapo Kesi 46 watuhumiwa walipatikana na hatia na
kuadhibiwa, Kesi 32 ziliondolewa Mahakamani
kutokana na sababu mbalimbali na Kesi 56 watuhumiwa wake waliachiwa huru. Vilevile, Mafunzo kuhusu Vita
Dhidi ya Rushwa yametolewa kwa Wanajamii 328,947
na Watumishi 439 wa Serikali. Katika
mwaka 2012/2013, Serikali itaendelea kuchunguza Tuhuma 2,729 zilizopo na Tuhuma mpya zitakazopokelewa pamoja na kuendelea
na Uchunguzi Maalum wa Tuhuma zilizobainishwa kwenye Taarifa za Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Ubadhirifu katika Taasisi mbalimbali
za Serikali.
Mazingira
94.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imeendelea kutekeleza Sera, Mikakati,
Sheria, Kanuni na Miongozo ya Kuhifadhi Mazingira. Miongoni mwa kazi
zilizotekelezwa ni pamoja na kuandaa Kanuni 14 za Usimamizi wa Mazingira ikiwemo Udhibiti wa Taka, Matumizi ya Bioteknolojia
ya Kisasa na tathmini na ukaguzi wa athari za Mazingira. Pamoja na miongozo
hiyo, Miradi 130 imefanyiwa tathmini
na kupatiwa Hati za Tathmini ya Athari kwa Mazingira, Kampeni ya Upandaji Miti imeendeshwa na
mafunzo kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi yametolewa. Serikali
itaendelea kuzijengea uwezo Mamlaka za
Serikali za Mitaa kutekeleza Mikakati ya Kuhifadhi Mazingira kwa kushirikiana na Wadau wengine. Serikali
pia itaendelea kutekeleza Mpango
wa Kitaifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi, kutoa Elimu ya Hifadhi ya Mazingira kwa Umma na
kuhamasisha utekelezaji wa Kampeni ya Upandaji Miti Nchini.
Maafa
95.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imeshughulikia matukio
ya Maafa katika maeneo mbalimbali Nchini. Maafa hayo yalisababishwa na mafuriko,
magonjwa ya mlipuko, upepo mkali
na ukame uliosababisha
baadhi ya maeneo kupata
upungufu wa chakula. Ukame ulizikumba Wilaya 55 na kuathiri Watu 2,186,990 ambao walihitaji msaada wa chakula.
Hadi mwezi Mei 2012, Serikali imetoa Tani 69,688
zenye thamani ya Shilingi Bilioni 24.4
kwa waathirika ikiwa ni chakula cha msaada. Vilevile, imetoa Shilingi Bilioni 5.5 kwa ajili ya kusafirishia chakula hicho hadi kwa walengwa.
96.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia iliendelea kushughulikia Waathirika wa
Milipuko ya Mabomu iliyotokea tarehe 16 Februari 2011, katika Kambi ya
Jeshi ya Gongo la Mboto, Dar-es-Salaam.
Serikali inakamilisha ujenzi wa Nyumba 36
za Waathirika wa Mabomu zilizobomoka kabisa ambazo zinajengwa na SUMA JKT
katika eneo la Msongola, Manispaa ya Ilala.
97.
Mheshimiwa Spika, Mafuriko yaliyotokea Jijini
Dar es Salaam mwezi Desemba 2011, yalikuwa na athari kubwa. Mafuriko hayo,
yalisababisha Watu 41 kupoteza
maisha, mali nyingi za Wananchi kupotea
na miundombinu ya barabara, madaraja, umeme na maji kuharibika. Serikali kwa
kushirikiana na Wadau mbalimbali ilichukua hatua za kuwasaidia waathirika wa mafuriko
kwa kuwapatia misaada ya kibinadamu kama vile, makazi ya muda, chakula, mavazi,
malazi na huduma za matibabu. Serikali pia imewapatia waathirika waliokuwa
wamejenga nyumba zao mabondeni viwanja katika eneo la Ekari 360 lililopo Mabwepande, Wilayani Kinondoni
ili waweze kujenga makazi mapya.
Hadi mwezi Mei 2012, Kaya 1,010 zilizoainishwa kuwa katika
maeneo hatarishi zaidi zimetengewa viwanja. Vilevile, miundombinu muhimu
katika eneo hilo ikiwemo maji, barabara na umeme pamoja na huduma za afya,
elimu na Kituo cha Polisi imejengwa.
98.
Mheshimiwa Spika, ili kuondoa tatizo la Wananchi kujenga katika maeneo Hatarishi,
Serikali imeziagiza Mamlaka za Serikali
za Mitaa Nchini ziandae Mipango endelevu ya kuwaondoa Watu wanaoishi mabondeni
na kuwahamishia katika maeneo salama. Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam tayari
zimeandaa Mpango ambao utaanza kutekelezwa katika Bajeti ya mwaka 2012/2013.
99.
Mheshimiwa Spika, mwaka jana, wakati nahitimisha Hotuba ya Makadirio ya
Ofisi yangu, niliahidi kuwa Serikali itatoa Kifuta Machozi kwa Wafugaji ambao Mifugo
yao ilikufa kutokana na Ukame Mkali uliotokea mwaka 2008/2009. Athari za Ukame
huo, ni pamoja na Vifo vingi vya Mifugo, zikiwemo Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo katika
Wilaya za Monduli, Longido na Ngorongoro. Kutokana na hali hiyo, mfumo wa
maisha wa Wafugaji wengi ulivurugika kwa kuwa Uchumi wao unategemea zaidi Ufugaji.
Baada ya tathmini kufanyika,
Serikali iliamua kutoa mifugo ya kianzio (seed
stock) ili kuziwezesha Kaya zilizopoteza
Mifugo yote kuendeleza ufugaji.
Utekelezaji wa zoezi hilo umeanza na
utaendelea katika kipindi
cha mwaka ujao wa
fedha. Napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wake wa busara wa kuwawezesha
Wafugaji hao na kushiriki yeye binafsi katika uzinduzi wa Mpango huo
uliofanyika tarehe 19 Februari 2012, Wilayani Longido.
100.
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2012/2013,
Serikali itajenga uwezo zaidi wa Nchi yetu wa Kuzuia, Kujiandaa na Kukabiliana
na Maafa na kurejesha hali ya kawaida kwa Waathirika. Aidha, Serikali itakamilisha
maandalizi ya Sheria Mpya ya Menejimenti ya Maafa, mapitio ya Sera ya
Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 na Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Sera
hiyo.
Udhibiti wa UKIMWI
101.
Mheshimiwa Spika, Tanzania ni moja
kati ya Nchi 32 Duniani ambazo
zimethibitishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa
kuweka jitihada kubwa za kupunguza kiwango cha maambukizi mapya ya UKIMWI
kwa Asilimia 25. Mafanikio hayo
yanatia moyo kwamba mkazo unaotiliwa na Serikali na Wadau wengine umeanza kuzaa
Matunda. Hata hivyo, jitihada zaidi zitahitajika kutoka kila Sekta, Asasi Zisizo
za Serikali, Wananchi na Watu Binafsi katika Mapambano Dhidi ya VVU na UKIMWI.
102.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imeweka jitihada kubwa
za kuendelea kupunguza Maambukizi Mapya, Vifo vitokanavyo na UKIMWI na Unyanyapaa. Hadi Desemba 2011,
jumla ya watu 1,125,211 wamepata
huduma na Ushauri Nasaha na Upimaji wa
VVU kwa hiari. Aidha, Watu wanaoishi na VVU wapatao 412,108 wanapata Dawa za ARV’s chini ya Mpango wa Taifa wa Matunzo
na Matibabu. Katika mwaka 2012/2013, Serikali itaimarisha Uratibu
wa shughuli za UKIMWI hasa katika Asasi za Kiraia na kuongeza juhudi za
uraghibishaji na uhamasishaji kwa Umma. Serikali pia itaandaa Mkakati wa Tatu
wa Kitaifa wa Mapambano dhidi ya UKIMWI na kufanya mapitio ya Mkakati wa Kinga
Nchini.
Dawa za Kulevya
103.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imejizatiti kukabiliana na tatizo la
usafirishaji na matumizi ya Dawa za Kulevya nchini. Katika kipindi cha Julai
2011 hadi Februari 2012, Kilo 349
za Dawa za Kulevya za Viwandani, Kilo 48,227
za Bangi
na Kilo 10,680
za Mirungi zilikamatwa. Hali hii si nzuri na
ni dalili tosha kuwa nguvu zaidi zinahitajika ili
kukabiliana na janga hili kubwa kwa Jamii yetu. Serikali itaendelea kutoa Elimu
kwa Umma juu ya madhara ya Dawa za Kulevya, kufanya misako na operesheni katika
maeneo mbalimbali na kuendelea kuteketeza mashamba ya bangi. Aidha, Serikali
itaimarisha na kuboresha Huduma za Tiba na Utengemao kwa Waathirika wa Dawa za
Kulevya. Napenda kuwatahadharisha wale wote wanaojihusisha na biashara hiyo
haramu kwamba Tanzania siyo Kituo cha Kupitisha au sehemu ya kufanyia Biashara
ya Dawa za Kulevya. Vyombo vya Usalama vimeimarishwa ili kudhibiti Biashara
hiyo. Nachukua fursa hii kukishukuru na
kukipongeza Kikosi Maalum cha Serikali cha Kupambana na Dawa za Kulevya ambacho
kimefanya kazi kubwa ya kukamata dawa nyingi zilizoingizwa Nchini.
Nawasihi waendelee kufanya kazi hiyo kwa
moyo zaidi ili kuepusha Nchi yetu na athari kubwa zitokanazo na matumizi ya Dawa
za Kulevya.
Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma
104.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2011/2012, Mamlaka ya Ustawishaji
Makao Makuu Dodoma imefanya Mapitio ya Mpango Kabambe wa Kuendeleza Mji Mkuu
Dodoma ili kuzingatia kasi ya ukuaji wa Mji huo. Aidha, mapitio ya Ikama na Muundo
wa Utumishi umefanyika kwa lengo la kuongeza
ufanisi wa kiutendaji wa Mamlaka. Kazi
nyingine zilizofanyika ni ujenzi wa Barabara zenye urefu wa Kilomita 27 katika maeneo ya Ipagala, Area E,
Chang’ombe Extension, Mwangaza,
Chidachi na inaendelea na ujenzi wa Barabara zenye urefu wa Kilomita 15 kwa kiwango cha Lami katika maeneo
ya Kisasa na Chang’ombe. Aidha, Mamlaka imepata Mkopo kutoka Benki ya CRDB wa
jumla ya Shilingi Bilioni 16 kwa
ajili ya uwekaji wa miundombinu ya maji, umeme na barabara zenye jumla ya urefu
wa Kilomita 20.6 kwa kiwango cha
Lami katika eneo la Uwekezaji la Njedengwa.
105.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/2013, Mamlaka ya Ustawishaji
Makao Makuu itafanya kazi ya kusanifu Mipango ya Makazi ya Uendelezaji wa Miji
(Satellite Towns) katika maeneo ya
Ihumwa na Hombolo. Mamlaka pia itaendelea kupima Viwanja 7,850 katika maeneo ya Iyumbu, Nzuguni na Miganga na kukamilisha
upimaji wa viwanja vya zamani 1,938
katika maeneo ya Ipagala, Nkuhungu na Kisasa. Hali kadhalika, Mamlaka itajenga
barabara zenye urefu wa Kilomita 11.3
kwa kiwango cha Lami katika maeneo ya Area ‘A’ na Kikuyu na kuendelea na ujenzi
wa miundombinu ya maji, umeme na barabara kwa kiwango cha Lami katika eneo la
Uwekezaji la Njedengwa. Serikali pia itafanyia kazi mapendekezo ya Mshauri
Mwelekezi aliyefanya mapitio ya Muundo wa CDA hasa kutatua mwingiliano wa
utendaji uliopo kati ya CDA na Manispaa ya Dodoma.
Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi
106.
Mheshimiwa Spika, mwezi Novemba 2011, nililiarifu Bunge lako Tukufu
kwamba Tanzania imejiunga na Mpango wa Kimataifa wa Uendeshaji wa Shughuli za
Serikali kwa Uwazi (Open Government
Partnership – OGP). Mpango huo unahimiza uendeshaji wa shughuli za Serikali
kwa Uwazi, Utawala Bora, Uadilifu, Mapambano Dhidi ya Rushwa na Ushirikishwaji
mpana wa Wananchi katika Mipango ya maendeleo na usimamizi bora wa Rasilimali
za Taifa. Chini ya makubaliano ya Mpango huo, kila Nchi inaandaa Mpango Kazi wa
Utekelezaji ambao ni shirikishi na unaotekelezeka kulingana na mazingira yake.
Napenda kuliarifu Bunge lako kuwa Serikali imeandaa Mpango Kazi wa utekelezaji
ambapo Sekta za Afya, Elimu na Maji zimepewa kipaumbele. Mpango Kazi huo
uliwasilishwa katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wanaohusika na Mpango
huo uliofanyika tarehe 17-18 Aprili 2012, Nchini Brazil. Utekelezaji wa Mpango
huo utaanza katika mwaka 2012/2013.
UDHIBITI WA MATUMIZI YA SERIKALI
107.
Mheshimiwa
Spika, katika Mkutano wa Saba wa Bunge mwezi Aprili
2012, niliahidi kuwa Serikali itayafanyia kazi maoni, ushauri na mapendekezo
yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wakijadili Taarifa mbalimbali za Kamati
za Kudumu za Bunge. Taarifa hizo ni pamoja na zile
za Kamati zinazoshughulikia Hesabu za Serikali
Kuu, Mashirika ya Umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo ziliainisha
Hoja mbalimbali za Ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2009/2010.
Aidha, nilieleza kuwa Serikali itawawajibisha wote waliotajwa kuhusika na ubadhirifu
wa Mali ya Umma ulioainishwa katika Taarifa hizo pale itakapothibitika kuwa
Watumishi hao wametenda makosa.
108.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeziagiza
Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia Taarifa na Hoja zote za Ukaguzi za mwaka
2009/2010, zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na
kuzitafutia majibu fasaha katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi Aprili
2012. Baada ya zoezi hilo kukamilika, Taarifa hizo zitawasilishwa Ngazi ya Mkoa
ambapo watapitia majibu ya Hoja hizo na kuziwasilisha katika Kamati ya Ushauri
ya Mkoa (RCC). Taarifa za Mikoa na Halmashauri zote zitawasilishwa Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kabla ya mwezi Novemba 2012
ili hatimaye kuandaa majibu ya pamoja na kuyawasilisha Bungeni.
109.
Mheshimiwa
Spika, vilevile, Wizara, Wakala, Mashirika ya Umma na Idara
za Serikali Zinazojitegemea zimeagizwa kupitia
Hoja zote zilizotolewa
na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
na kuzifanyia kazi. Wakala wa Serikali na Mashirika ya Umma yametakiwa
kupitisha majibu ya Hoja kwenye Bodi za Wakurugenzi kabla ya kuwasilishwa
Wizarani. Utaratibu huo utakuwa endelevu na utafanyika
kila mwaka. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Usimamizi
wa Fedha za Umma unaimarishwa katika Ngazi zote. Majibu ya Hoja zote yatawasilishwa Bungeni ili kuongeza Uwazi na
Uwajibikaji wa Fedha za Umma.
110.
Mheshimiwa
Spika, sambamba na hatua hiyo, Watumishi wa Umma
watakaotuhumiwa kufanya ubadhirifu wa fedha za
Umma watachunguzwa na tuhuma zikibainika
ni za kweli watavuliwa madaraka waliyo
nayo na kufikishwa katika Vyombo vya Sheria. Napenda kusisitiza kwamba, Serikali haitawahamisha Watumishi wa aina
hiyo, bali hatua za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa wakiwa kwenye vituo
vyao vya kazi. Natoa wito kwa Watendaji Wakuu wa Serikali, Bodi za Wakurugenzi
wa Mashirika ya Umma na Madiwani kuhakikisha wanashiriki ipasavyo katika
kusimamia fedha za Umma kwa mujibu wa Sheria, Taratibu, Miongozo na Kanuni
zilizopo. Nawaagiza Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kubandika kwenye mbao za matangazo za Makao
Makuu ya Halmashauri na katika vituo vyote vya utoaji huduma kiasi cha fedha
kinachopokelewa kila mwezi na matumizi yake. Hii itawezesha Wananchi
kufuatilia matumizi ya fedha zilizopelekwa kwa ajili ya utoaji huduma kwenye
maeneo yao.
111.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za
kupunguza matumizi yasiyo na tija, hususan ununuzi wa magari makubwa na ya
kifahari ambayo gharama za ununuzi na
uendeshaji ni kubwa sana. Kuanzia mwaka
2012/2013, hatua zaidi zitachukuliwa kwa kuweka ukomo wa ukubwa wa injini wa
magari ambayo yanaweza kununuliwa na Serikali Kuu na Taasisi zake pamoja na Mamlaka
za Serikali za Mitaa. Chini ya utaratibu huo, magari yatakayonunuliwa
yatakuwa ni yale yasiyozidi ukubwa wa injini wa CC 3,000 kwa Viongozi na Watendaji Wakuu na yasiyozidi CC 2,000 kwa Watumishi
wengine ambao wana stahili ya kutumia magari ya Serikali. Vilevile, ili
kupunguza matumizi ya magari kwa Viongozi na Watendaji Wakuu kwa safari za
Mikoani, Serikali itaanzisha vituo vya
Kanda vya magari ya Serikali au kila Ofisi itatenga magari machache yatakayotumika
Mikoani kwa shughuli za kikazi. Mwongozo
wa utekelezaji utatolewa. Inategemewa kuwa utaratibu huu utapunguza matumizi ya
fedha za Serikali kwa kiwango kikubwa.
HITIMISHO
112.
Mheshimiwa Spika, nimeelezea kwa muhtasari baadhi ya shughuli ambazo
Serikali imetekeleza kwa kipindi kilichopita. Aidha, nimetoa Mwelekeo wa Kazi zitakazofanyika
mwaka 2012/2013. Kwa kuhitimisha, napenda kusisitiza mambo muhimu yafuatayo:
a)
Wote tunatambua kuwa tumeanza kutekeleza
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa Tume ya Kuratibu maoni kuanza kazi.
Tuendelee kuwaelimisha Wananchi kuhusu Mambo ya Msingi wakati wa kuchangia
Maoni, na kwamba kila mmoja anao wajibu na Uhuru wa kutoa Maoni yake kwenye
Tume bila shinikizo lolote.
b)
Tumepitisha
Bajeti ya Serikali ambayo changamoto yake kubwa ni Rasilimali Fedha kidogo
tuliyonayo kukidhi mahitaji makubwa ya kutoa huduma bora kwa Wananchi
tunaowaongoza. Kutokana na hali hiyo, ni muhimu kujipanga vizuri kudhibiti na kusimamia
matumizi ya fedha za Umma
kwa ufanisi na tija
zaidi. Serikali itaimarisha Mifumo yake
ya usimamizi na ufuatiliaji na kuhakikisha kwamba fedha za umma zinatumika
kulingana na Sheria na Kanuni za Matumizi ya Fedha za Serikali.
c)
Katika muda usiozidi miezi miwili ijayo,
tarehe 26 Agosti 2012 itakuwa ni Siku ya Sensa ya Watu na Makazi Nchini. Napenda
kusisitiza kwamba uandikishaji hautakuwa
wa siku moja tu, bali siku hiyo ndiyo itakayokuwa msingi wa kuhesabu watu
waliolala katika Kaya husika. Kazi hiyo itaendelea kwa siku saba
hadi tarehe 2 Septemba 2012. Natoa wito kwa Wananchi kutoa ushirikiano kwa
Makarani wa Sensa na kujitokeza kuhesabiwa na kuhakikisha kwamba kila mtu anahesabiwa
mara moja tu. Aidha, Viongozi katika Ngazi zote wana wajibu mkubwa wa
kuwahamasisha Wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki kwenye Sensa.
113.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kumaliza
Hotuba yangu, nimwombe Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia (Mb.), Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa atoe maelezo
ya Mapitio ya Kazi zilizofanyika katika mwaka 2011/2012
na Mwelekeo wa Kazi za Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2012/2013. Ni
matumaini yangu kwamba maelezo hayo yatawezesha Waheshimiwa Wabunge na Wananchi
kufahamu kwa upana shughuli zinazotekelezwa na Mikoa na Mamlaka za Serikali za
Mitaa.
SHUKRANI
114.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii sasa kuwashukuru Mawaziri na Naibu
Mawaziri kwa ushirikiano walionipa katika kipindi hiki. Aidha, nawashukuru
Watumishi wote wa Serikali na Taasisi zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Yohana Sefue kwa
kukamilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/2013. Nawashukuru Watanzania wote
na Washirika wetu wa Maendeleo kwa Michango yao ambayo imewezesha Serikali
kutoa huduma mbalimbali kwa Wananchi.
115.
Mheshimiwa
Spika, vilevile, napenda kuwashukuru Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi,
Mbunge wa Ismani, Waziri wa Nchi (Sera, Uratibu na Bunge); Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang,
Waziri wa Nchi (Uwekezaji na Uwezeshaji); Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia,
Mbunge wa Mtwara Vijijini, Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa; Mheshimiwa Aggrey Joshua Mwanry,
Mbunge wa Siha, Naibu Waziri, Ofisi
ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa; na Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa,
Mbunge wa Ruangwa, Naibu Waziri,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu) kwa
ushirikiano walionipa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Shukrani za pekee kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa jitihada walizoonesha katika
kipindi hiki. Nawashukuru vilevile Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu,
chini ya Uongozi wa Makatibu Wakuu, Bwana Peniel Moses Lyimo na Bwana Hussein
Athuman Kattanga na Naibu Makatibu Wakuu, Bwana Charles Amos Pallangyo, Jumanne
Abdallah Sagini na Alphayo Japan Kidata kwa ushauri wao wa Kitaalam ambao
wamenipa mimi na Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi katika kipindi hiki. Nawashukuru
kwa kukamilisha maandalizi yote ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya
Waziri Mkuu kwa mwaka 2012/2013.
116.
Mheshimiwa Spika, kipekee napenda nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kwangu na kuendelea
kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu ipasavyo. Pia, ninamshukuru Mheshimiwa Dkt.
Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed
Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi kwa ushirikiano
mkubwa wanaonipa katika kuwatumikia Watanzania. Vilevile, ninawashukuru
Waheshimiwa Wabunge, Viongozi wote wa Kitaifa na wa ngazi nyingine zote kwa
ushirikiano wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Kwa umuhimu wa kipekee,
napenda kuwashukuru Wapiga Kura wangu kwa imani na ushirikiano wanaoendelea
kunipa katika kuleta maendeleo ya Jimbo la Katavi. Naomba pia nitumie fursa hii
kumshukuru sana sana Mama Tunu Pinda kwa uvumilivu wake na msaada mkubwa anaonipa
katika kutekeleza majukumu yangu mazito. Vilevile, nawashukuru sana Watoto
wangu ambao mara nyingi wamekuwa wakinitia moyo na wamekuwa na uvumilivu mkubwa
wanaponikosa kwa sababu ya kazi. Wote nasema, Asanteni sana kwa kunipa nguvu ya
kutekeleza majukumu yangu. Nyote nawashukuru
sana!
MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU, OFISI YA WAZIRI MKUU - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA NA OFISI YA BUNGE YA MWAKA 2012/2013
117.
Mheshimiwa Spika,
kwa mwaka 2012/2013, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake inaliomba Bunge lako
Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi
Bilioni Mia Moja Sabini na Sita, Milioni Mia Saba Tisini na Nne, Laki Nane
Thelathini na Nane Elfu (176,794,838,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Sitini na Nane, Milioni Mia Tano Ishirini na Mbili, Laki Nane
Sitini na Sita Elfu (68,522,866,000)
ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi
Bilioni Mia Moja na Nane, Milioni Mia Mbili Sabini na Moja, Laki Tisa Sabini na
Mbili Elfu (108,271,972,000) ni kwa
ajili ya Mpango wa Maendeleo.
118.
Mheshimiwa
Spika, vilevile, kwa mwaka 2012/2013, Ofisi ya Waziri
Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Asasi zake inaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Themanini na
Sita, Milioni Mia Nane Tisini na Moja, Laki Tano Tisini na Nane Elfu (186,891,598,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Moja Sitini na Nne,
Milioni Mia Sita Kumi na Nne, Laki Saba Ishirini na Sita Elfu
(164,614,726,000) ni kwa
ajili ya Matumizi ya Kawaida
na Shilingi Bilioni Ishirini na Mbili, Milioni
Mia Mbili Sabini na Sita, Laki Nane Sabini na Mbili Elfu (22,276,872,000) ni
kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
119.
Mheshimiwa Spika,
Ofisi za Wakuu wa Mikoa zinaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Sabini na Tatu, Milioni Mia Mbili Sabini na
Sita, Laki Saba Sitini na Moja Elfu (173,276,761,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Moja Arobaini na Sita,
Milioni Mia Tano Hamsini na Mbili, Laki Mbili Sitini na Mbili Elfu
(146,552,262,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Ishirini na Sita, Milioni
Mia Saba Ishirini na Nne, Laki Nne Tisini na Tisa Elfu (26,724,499,000) ni
kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo. Aidha, Halmashauri
zote zinaombewa jumla ya Shilingi
Trilioni Tatu, Bilioni Mia Mbili Sabini na Tisa, Milioni Mia Nane; na Sabini na
Tano Elfu (3,279,800,075,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Trilioni Mbili, Bilioni Mia Saba Thelathini na Tano, Milioni
Mia Sita Arobaini na Sita, Laki Moja Kumi na Saba Elfu (2,735,646,117,000)
ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi
Bilioni Mia Tano Arobaini na Nne, Milioni Mia Moja Hamsini na Tatu, Laki Tisa
Hamsini na Nane Elfu (544,153,958,000)
ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
120.
Mheshimiwa Spika,
Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano inaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Kumi na Tatu, Milioni Mia Mbili Ishirini,
Laki Sita Hamsini na Tatu Elfu (113,220,653,000) kwa ajili ya Mfuko wa
Bunge ambapo Shilingi
Bilioni Mia Moja Kumi na Moja, Milioni Mia Tano Themanini na Tano, Laki Sita
Hamsini na Tatu Elfu (111,585,653,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida
na Shilingi Bilioni Moja na Milioni Mia
Sita Thelathini na Tano (1,635,000,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya
Maendeleo.
MUHTASARI
121.
Mheshimiwa
Spika, baada ya maelezo haya kwa
muhtasari, naomba sasa Bunge lako Tukufu likubali kuidhinisha Makadirio ya
Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2012/2013 ya jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Kumi na Tatu, Milioni Mia Mbili Ishirini, Laki
Sita Hamsini na Tatu Elfu (113,220,653,000) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge, na
jumla ya Shilingi Trilioni Tatu, Bilioni
Mia Nane Kumi na Sita, Milioni Mia Saba Sitini na Tatu, Laki Mbili Sabini na
Mbili Elfu (3,816,763,272,000) kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi
ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ikiwa ni Matumizi ya
Kawaida na Fedha za Maendeleo za Ndani na Nje kwa ujumla wake.
122.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Hotuba hii, yapo Majedwali ambayo
yanafafanua kwa kina Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na
Taasisi zake, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na
Ofisi ya Bunge.
123.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja.
COMMENTS