HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA NANE WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA...
HOTUBA
YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO
WA NANE WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
TAREHE
16 AGOSTI 2012, DODOMA
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, tarehe 12 Juni, 2012 tulianza Kikao
cha Kwanza cha Mkutano wa Nane wa Bunge lako Tukufu na leo tunafikia tamati. Ni
jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuhitimisha shughuli zote
zilizopangwa kwa amani na salama. Mkutano huu ulikuwa mahsusi kwa ajili ya
kuwasilisha, kujadili na hatimaye kupitisha Bajeti ya Serikali ikiwa ni
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Wizara, Mikoa na Taasisi
mbalimbali.
2.
Mheshimiwa Spika, napenda niwashukuru Waheshimiwa
Wabunge kwa kutumia muda wote wa Mkutano huu kwa ufanisi mkubwa kuchangia hoja
zinazolenga katika kujenga na kusaidia Taifa letu. Napenda kuchukua nafasi hii
kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa mwamko huo mzuri ambao bila kujali
itikadi za Vyama umetoa changamoto kwa Serikali katika kutekeleza malengo
tuliyojiwekea ili kuleta maendeleo ya Nchi yetu. Ninawashukuru sana kwa
michango yenu.
3.
Mheshimiwa Spika, wakati wa Mkutano huu tukiwa hapa
Bungeni, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walipata Misiba kwa kupotelewa na
Wapendwa wao wakiwemo Wazazi, Ndugu, Jamaa na Marafiki. Nitumie nafasi hii
kuwapa pole wote waliofikwa na Misiba hiyo. Lakini kipekee kabisa niruhusu
nimtaje na kumpa pole Mheshimiwa Joseph Selasini, Mbunge wa Rombo kwa kumpoteza
Mama yake kutokana na ajali ambayo yeye mwenyewe alihusika na hivyo kupata
majeraha makubwa. Aidha, nimpe Pole kwa kumpoteza Baba yake akiwa bado ana
Majonzi ya kumpoteza Mama yake katika kipindi
kifupi. Tunampa Pole Sana. Pamoja na ajali aliyoipata
Mheshimiwa Selasini, katika siku chache zilizopita tumeshuhudia Ajali za
Barabarani zilizosababisha vifo, majeruhi kwa Abiria wa Magari hayo. Watu wengi
wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa. Niungane na Watanzania wote kuwapa
pole waliopoteza Ndugu, Jamaa na Marafiki katika Ajali hizo.
4.
Mheshimiwa Spika, vilevile, kama ambavyo wote
tunakumbuka kuwa mnamo tarehe 18 Julai 2012 tulipata taarifa ya tukio la
kusikitisha kuhusu ajali ya kuzama kwa Meli ya MV SKAGIT karibu na Kisiwa cha
Chumbe, Zanzibar. Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, Meli hiyo ambayo
inamilikiwa na Kampuni ya SEAGUL Transport ilikuwa imebeba Watu 290,
wakiwemo Watalii na Raia wa Kigeni 16. Katika ajali hiyo Watu 146
waliokolewa kwa msaada wa Vyombo vya uokoaji na waliobaki 144 wanahofiwa
kupoteza Maisha wakiwemo Raia Wawili wa Kigeni.
5.
Nitumie fursa hii ya mwanzo kabisa kuwapa pole Watanzania wote kwa msiba
huo mkubwa ambao ulikumba Taifa letu. Aidha, kwa uzito wa kipekee nawapa
pole Ndugu, Jamaa na Marafiki ambao wamepoteza Wapendwa wao katika ajali hiyo.
Kwa wale wote waliopoteza maisha, tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu ili azilaze
Roho zao mahala Pema Peponi. Amina! Vilevile, tunawaombea wote
walionusurika katika ajali hiyo kuweza kurejea katika afya zao za kawaida na
hivyo kuendelea na ujenzi wa Taifa.
6.
Aidha, napenda kuwashukuru wote walioshiriki katika uokoaji wa ndugu
zetu na hivyo kuokoa maisha yao. Nami niungane na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumpongeza Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein na
Viongozi wenzake wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kazi kubwa
walioifanya kuongoza juhudi za uokoaji, huduma zote walizozitoa kwa Majeruhi na
Wafiwa. Vilevile, ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wetu
kwa kukubali mapendekezo ya Baraza la Usalama la Taifa la kuunda Kikosi Maalum
cha Uokoaji na Usalama Majini, yaani Coastal Guards. Ni dhahiri
kuwa Kikosi hiki kitakuwa na faida kubwa katika Usafiri wa Majini na Usalama
wake.
7.
Mheshimiwa Spika, matarajio yetu ni kwamba Tume
iliyoundwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuchunguza ajali hiyo itatuwezesha
kujua mazingira yaliyosababisha ajali hiyo na kwamba tufanye nini ili
kuhakikisha Vyombo hivi vinasimamiwa vizuri katika kuzuia ajali hizo zisitokee
tena. Tayari Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imechukua hatua za kuzuia matumizi
ya Meli za Kampuni hii ambazo hazitakidhi viwango vya usafirishaji Abiria.
Aidha, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeanza taratibu za kununua Meli Mpya
ambayo itabeba Abiria 1,000 na kubeba Magari Mia Moja. Inatarajiwa kuwa
Ujenzi wa Meli hiyo utachukua takriban Mwaka Mmoja kuanzia sasa.
MJADALA
WA BAJETI YA SERIKALI 2012/2013
8.
Mheshimiwa Spika, mjadala wa Bajeti ya Serikali
tunaohitimisha leo, ulikuwa na hoja nyingi ambazo Waheshimiwa Wabunge walitaka
kupata majibu na ufafanuzi. Yapo maeneo ambayo Waheshimiwa Mawaziri walijibu na
kutoa maelezo ya ufafanuzi kwa ukamilifu. Napenda kuwashukuru Waheshimiwa
Mawaziri wote kwa kazi nzuri waliyoifanya hadi kupitishwa kwa Bajeti za Wizara
zao. Ninaelewa kwamba zipo Hoja kadhaa zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge
ambazo Mawaziri hawakupata muda wa kuzijibu na kutoa ufafanuzi wa kina kwa
sababu ya muda finyu. Aidha, najua kwamba kila Waziri aliahidi kujibu kwa
Maandishi hoja ambazo hazikupata nafasi ya kujibiwa wakati wa Majumuisho yake.
Napenda nami nitumie muda huu wa kujumuisha Hoja hii siku ya leo kwa kutoa
maelezo japo kwa kifupi kwa baadhi ya maeneo.
MPANGO
WA MAENDELEO NA BAJETI YA SERIKALI 2012/2013
9.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Serikali tuliyoipitisha
kwa mwaka 2012/2013 ni jumla ya Shilingi Trilioni 15.19. Kati ya
fedha hizo, Fedha za Matumizi ya Kawaida ni Shilingi Trilioni 10.60
na Fedha za Matumizi ya Maendeleo ni Shilingi Trilioni 4.59. Aidha, kati
ya Shilingi Trilioni 10.59 za Matumizi ya Kawaida, Shilingi Trilioni 2.74
ni za kulipa Deni la Taifa, Shilingi Trilioni 3.78 ni za malipo ya
Mishahara na Shilingi Trilioni 4.08, sawa na Asilimia 26.8 tu ya
Bajeti yote ni kwa Matumizi Mengineyo (Other Charges-OC). Bajeti hii
imeelekeza Rasilimali Fedha kidogo tulizo nazo katika maeneo machache ya
kipaumbele ambayo yatatuwezesha kufungulia fursa za Kukuza Uchumi na Kupunguza
Umaskini kwa kasi zaidi kwa kushirikiana na Sekta Binafsi.
10.
Kama mtakavyokumbuka, mwaka jana tarehe 8 Juni 2011 tukiwa hapa Dodoma,
Mheshimiwa Rais alizindua Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano
(2011/2012 – 2015/2016) wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo hadi 2025.
Mwaka wa Kwanza wa utekelezaji wa Mpango huo, (yaani 2011/2012) ulikuwa wa
Mpito (Transition) kabla ya kuanza utekelezaji halisi wa Mipango
inayofuata ya Miaka Mitano Mitano ya kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa hadi
2025. Aidha, Mheshimiwa Rais wakati wa uzinduzi alisisitiza kuwa, katika Mfumo
wa Upangaji Mipango, ni lazima Serikali ianze kuwekeza katika Vipaumbele
vichache vitakavyoleta matokeo (impact) makubwa katika Kukuza Uchumi na
Kuondoa Umaskini.
11.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi walipata
fursa ya kushiriki kwenye Uzinduzi wa Mpango huo wa Miaka Mitano uliofanyika
hapa Dodoma, St. Gaspar. Aidha, Serikali ilipata fursa ya kuwasilisha Mpango
huo Bungeni mwezi Juni 2011 katika Mkutano wa Bunge la Bajeti ya mwaka
2011/2012. Wakati wa mjadala Waheshimiwa Wabunge wengi pia walichangia mawazo
na kutoa maoni yao kwenye Mpango na Bajeti ya Serikali ya mwaka 2011/2012
ambayo Serikali imeanza kuyazingatia mwaka huu wa Bajeti ya 2012/2013.
12.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kurejea
Vipaumbele Vitano vilivyobainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
kama ifuatavyo:
·
Kipaumbele cha Kwanza ni kuwekeza kwenye Sekta za Miundombinu hasa
uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya Nishati, Usafirishaji, Maji Safi na
Maji Taka, Umwagiliaji na TEHAMA;
·
Kipaumbele cha Pili ni kuwekeza katika Sekta ya Kilimo kwa
tafsiri pana ambayo inajumuisha Sekta ya Kilimo cha mazao ya chakula na
biashara pamoja na Sekta ya Mifugo, Uvuvi, Ufugaji wa Nyuki na Rasilimali za
Misitu. Shabaha Kuu ya kuendeleza Kilimo ni kuleta Mapinduzi ya haraka ya
Kilimo yatakayotuwezesha kuongeza uzalishaji na tija ili kujitosheleza kwa
chakula na kuuza ziada nje;
·
Kipaumbele cha Tatu ni kukuza Maendeleo ya Viwanda, hasa
vile vinavyotumia malighafi zinazopatikana hapa Nchini ili kuwezesha kusindika
mazao ya Kilimo, Mifugo, Samaki, Misitu na Mazao ya Ufugaji Nyuki, pamoja na
kuongeza thamani ya Madini. Aidha, kuvutia uwekezaji kwenye viwanda vikubwa vya
mbolea, saruji na viwanda vya kieletroniki kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya
soko la ndani na kikanda hasa Afrika Mashariki;
·
Kipaumbele cha Nne ni Maendeleo ya Rasilimali Watu na
ujuzi, hasa kukuza Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na kuimarisha huduma za Jamii;
na
·
Kipaumbele cha Tano ni kuendeleza huduma za Utalii, Biashara na
Huduma za Fedha ambazo ni muhimu katika kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na
maendeleo ya jamii.
13.
Mheshimiwa Spika, Serikali inakubaliana na maoni na
ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge wengi na hasa Kamati ya Uchumi na
Fedha kwamba usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa Vipaumbele hivi na
nidhamu ya matumizi ya fedha zilizoelekezwa kwenye Vipaumbele vilivyowekwa,
itakuwa ndiyo nguzo kuu ya mafanikio ya Ukuaji wa Uchumi wetu, ikiwa ni
pamoja na kushirikisha Sekta Binafsi na Wananchi wote kwa ujumla.
14.
Mheshimiwa Spika, vilevile, wakati wa mjadala wa
Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/2013 baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walitoa
maoni na ushauri wao kuhusu uwiano wa Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa ambayo
imezingatia kutenga Asilimia 70 ya fedha za Bajeti kwa ajili ya Matumizi
ya Kawaida na Asilimia 30 kwa ajili ya Mpango wa Maendeleo, badala ya
mgawanyo wenye uwiano wa Asilimia 65 kwa Asilimia 35 katika
matumizi hayo. Pamoja na maoni hayo, tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge ambao
walielewa vizuri maelezo ya ufafanuzi yaliyotolewa tarehe 22 Juni 2012 na
Waziri wa Fedha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu kuhusu
Mgawanyo huo wa Bajeti. Kwa ujumla, mgawanyo huo umezingatia hali halisi ya
Mapato ya Serikali ikilinganishwa na mahitaji makubwa ya fedha kwa ajili ya Mishahara
ya Watumishi wa Serikali, Mfuko Mkuu wa Serikali na Matumizi Mengineyo ambayo
yanajumuisha matumizi kwa ajili ya shughuli zisizoweza kuepukika.
15.
Mheshimiwa Spika, matumizi yasiyoweza kuepukika ni
kama vile ununuzi wa Dawa na Vifaa vya Tiba; gharama za uendeshaji wa Shule na
Mitihani; uendeshaji wa Shughuli za Bunge; Mahakama na Vyombo vya Ulinzi na
Usalama pamoja na kutoa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo. Matumizi hayo yametengewa
jumla ya Shilingi Bilioni 2,032.2, sawa na Asilimia 19.2 ya
Matumizi ya Kawaida ya jumla ya Shilingi Trilioni 10.60. Kiasi
kinachobakia cha fedha za Matumizi ya Kawaida cha Shilingi Bilioni 1,959.5,
sawa na Asilimia 18.5 ndicho pekee kitatumika kwa ajili ya kugharamia
shughuli zote za uendeshaji wa Serikali nzima pamoja na kutekeleza kazi muhimu
zinazoendelea kama vile, kuendesha Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi,
Vitambulisho vya Taifa na kukidhi mahitaji ya Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba
Mpya na shughuli nyingine kama hizo.
16.
Aidha, ni muhimu Waheshimiwa Wabunge kutambua kuwa sehemu ya fedha za
Maendeleo ya Rasilimali Watu na huduma za Jamii ambacho ni Kipaumbele cha Nne
cha Mpango wa Maendeleo ya Taifa zimewekwa pia katika Matumizi ya Kawaida.
Kiasi kilichotengwa katika Bajeti kwa ajili ya matumizi hayo ni Shilingi Bilioni
841.4. Fedha hizo zikijumuishwa na Shilingi Trilioni 4.59
zilizotengwa kwa ajili ya Mpango wa Maendeleo, zinafikia jumla ya Shilingi Trilioni
5.4, sawa na Asilimia 35.7 ya Bajeti yote. Hivyo, uwiano
halisi wa Bajeti iliyotengwa kwa Miradi ya Maendeleo ni Asilimia 35.5. Serikali
itajitahidi kuzingatia ushauri wa kutenga Bajeti kubwa kwa ajili ya Miradi ya
Maendeleo kwa kadri Mapato ya Serikali yanavyoongezeka na kubana matumizi ya
Serikali yasiyo ya lazima.
17.
Mheshimiwa Spika, Serikali imejipanga vizuri
kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2012/2013. Serikali
itafanya ukaguzi na ufuatiliaji wa karibu wa Miradi ya Maendeleo na tathmini ya
mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa kazi zinazofanyika zinawiana na thamani ya
fedha zinazotolewa (Value for Money) kwa Miradi ya Maendeleo. Aidha,
Tume ya Mipango imepewa jukumu la kuchambua Mipango Kazi ya Miradi ya Maendeleo
na kushauri ipasavyo.
18.
Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuhakikisha
kwamba malengo ya ukusanyaji Mapato na Matumizi ya Fedha za Serikali
yanazingatia Bajeti iliyoidhishwa na Bunge. Ili kutekeleza azma hiyo, Serikali
imekubali kuwa kila baada ya robo ya mwaka, Baraza la Mawaziri la Kazi
litakutana na kujadili mwenendo wa ukusanyaji wa Mapato ya Serikali (ya Kodi na
yasiyo ya Kodi) pamoja na matumizi ya Serikali katika kipindi hicho. Baraza hilo
litajadili Mapato na Matumizi ya kila Wizara, kila Mkoa pamoja na Wakala na
Idara za Serikali zinazojitegemea na Taasisi zote za Serikali.
19.
Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Watendaji wote wa
Serikali katika ngazi zote kuwa na nidhamu katika matumizi kwa kuzingatia
Sheria, Kanuni na Taratibu za Matumizi ya Serikali pamoja na kuwajibika
ipasavyo katika matumizi ya Bajeti tuliyoipitisha.
KUIMARISHA
UTENDAJI SERIKALINI NA KUDHIBITI MATUMIZI
20.
Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuimarisha
Utendaji kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazoongoza Utendaji wa
Watumishi wa Serikalini. Ili kutekeleza azma hii kikamilifu, Serikali itatumia
uzoefu wa Nchi ya Malaysia ambayo imefanikiwa kuweka mfumo madhubuti wa kupima
ufanisi wa Utendaji Kazi wa Viongozi na Watendaji wake kwa kutumia Chombo
maalum kinachojulikana kwa jina la PEMANDU. Hatua hiyo, itawezesha Serikali
kuimarisha utoaji wa huduma nzuri kwa Wananchi pamoja na kuimarisha usimamizi
wa matumizi ya fedha za Serikali ikijumuisha Mipango ya Maendeleo.
21.
Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kwamba,
Utendaji Kazi mzuri ni pamoja na matumizi bora ya rasilimali chache tulizonazo,
kutoa huduma inayotarajiwa na Watanzania. Sote tunaelewa kwamba, mahitaji ya
fedha ni makubwa sana kulinganisha na uwezo wetu wa sasa. Hata hivyo, kila
mmoja wetu akiwajibika ipasavyo na kutumia kwa uangalifu rasilimali hizo bado
tunaweza kufanya mambo makubwa sana. Ni kwa sababu hiyo Serikali imeendelea
kusisitiza kwamba Bajeti tuliyoipitisha hapa inalenga matumizi yatakayotupatia
matokeo makubwa na ya haraka. Tutaendelea kubana matumizi yasiyo na tija kama
vile Warsha, Semina na Makongamano, Safari zisizo na lazima Ndani na Nje ya
Nchi, ununuzi na matumizi ya magari ya kifahari pamoja na matumizi mengine
yasiyo ya lazima.
MAANDALIZI YA MSIMU WA
KILIMO 2012/2013 NA UPATIKANAJI WA PEMBEJEO NA ZANA ZA KILIMO
Mbolea
Mheshimiwa
Spika, moja ya maeneo ambayo yalikuwa na hoja nyingi
katika Mjadala wa Bunge hili la Bajeti ni suala la Kilimo, hususan maandalizi
ya Msimu wa Kilimo, upatikanaji wa Pembejeo na Zana za Kilimo. Programu ya
kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) inalenga kuleta mageuzi ya Sekta ya Kilimo,
mkazo wake mkuu ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa pembejeo na Zana za
Kilimo. Napenda kuwahakikishia Watanzania kwamba, katika msimu wa Kilimo
2012/2013, Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea na mbegu kwa mazao
mbalimbali kwa utaratibu wa Vocha. Lengo ni kuongeza upatikanaji wa pembejeo na
uelewa wa Wakulima kuhusu matumizi ya mbolea na mbegu bora. Kwenye maeneo ya
Nchi yenye ukame, ambayo imethibitishwa na Wataalam kwamba matumizi ya Mbolea
ya Minjingu Mazao (NPS) inafaa kwa uzalishaji wa Mazao ya Alizeti na
Mtama, Vocha za Ruzuku zitatolewa kwa ajili ya mazao hayo. Lengo ni kubadilisha
mtazamo hasi kuwa mazao haya hayahitaji mbolea pamoja na kuwapunguzia Wakulima
gharama kwa sababu bei ya mbolea ya Minjingu Mazao (NPS) ni nafuu
ikilinganishwa na mbolea ya DAP. Vilevile, lengo lingine la Serikali ni
kuongeza uzalishaji wa mazao hayo ili kupunguza uagizaji wa Mafuta ya Kula
kutoka nje pamoja na kukabiliana na upungufu wa chakula katika maeneo hayo. Kwa
hiyo, nawasihi Wakulima kutumia Mbolea ya Minjingu Mazao (NPS) kwa
sababu bei yake ni nafuu, inatengenezwa hapa Nchini na pia ni rafiki wa
mazingira.
Mbegu
22.
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya mbegu kwa mwaka ni
Tani 60,000, lakini mwaka 2011/2012 Tani 28,770 tu zilizalishwa
kutoka katika mashamba ya Wakala wa Mbegu wa Taifa, Mashamba ya Magereza na JKT
na Sekta Binafsi. Ili kupunguza tatizo hili, Sekta Binafsi imeruhusiwa kupata
Mbegu Mama (Breeder Seeds) kutoka Vituo vya Utafiti ili wazalishe Mbegu
za Msingi (Foundation Seeds) zitakazotumika kuzalisha Mbegu
zilizothibitishwa (Certified Seeds). Serikali itahakikisha kwamba Mbegu
bora zinapatikana kwa wakati ili ziweze kuwafikia Wakulima kabla ya kuanza kwa
Msimu wa Kilimo.
Zana
za Kilimo
23.
Mheshimiwa Spika, Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya
Kilimo, Chakula na Ushirika ilielezea kwa kina jitihada za Serikali katika
kuhamasisha matumizi ya Zana Bora za Kilimo ili kuongeza tija na kupunguza
Sulubu ya kazi za kutumia Jembe la Mkono. Matumizi ya Matrekta Makubwa na
Madogo yaliyoingizwa Nchini na SUMA JKT yameongezeka na hivyo kuongeza eneo
linalolimwa kutoka Asilimia 12 mwaka 2010 hadi Asilimia 14 mwaka 2011. Nitumie
nafasi hii kuwahimiza Wananchi kwamba Matrekta ya SUMA JKT aina ya Farmtrac
2; Wheel Drive yapatayo 547 bado yapo. Ninazo taarifa kwamba Matrekta
ya New Holland na Farmtrac 4 Wheel Drive yameisha, lakini
bado mahitaji ni makubwa. Serikali inafanya Mpango wa kuagiza Matrekta hayo na
tayari kuna Mpango wa kupata Mkopo wa Matrekta 3,000 kupitia Makubaliano kati
ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya India. Aidha, bei za Matrekta ya SUMA
JKT zimepunguzwa na muda wa marejesho ya Mkopo wa Matrekta hayo kwa Wananchi
umeongezwa. Nawasihi Wananchi kujiunga katika Vikundi vya kuwawezesha kukopa
Matrekta hayo.
24.
Mheshimiwa Spika, ni hivi karibuni tu nilifanya
Uzinduzi wa Matrekta 50 ili yakopeshwe kwa Wakulima wa Mkoa wa Ruvuma.
Alichokifanya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ni kuchukua jukumu la kuratibu zoezi zima
la ukopeshaji wa Matrekta hayo kwa Wakulima katika Mkoa wake. Yeye akawa kama Focal
Person wa kukusanya fedha zinazohitajika na kuhakikisha upatikanaji wa
Matrekta hayo kwa Wakulima wake. Nitumie mfano huu mzuri kuwaomba Viongozi wote
katika ngazi za Mikoa na Wilaya kuweka nguvu za ziada wasaidie katika
kufanikisha upatikanaji wa Matrekta hayo katika maeneo yao. Halmashauri
zijipange kuhakikisha kwamba fursa iliyotolewa ya kupunguza bei ya Matrekta ya
SUMA JKT na fursa ya Asilimia 10 ya malipo ya awali inatumika vizuri.
Kipaumbele kiwe kwenye SACCOS, hasa za Vijana.
Hali
ya Chakula Nchini
25.
Mheshimiwa Spika, hali ya chakula Nchini ni ya
kuridhisha. Takwimu za tathmini ya awali za mwezi Juni 2012 kuhusu hali ya
uzalishaji wa mazao ya chakula na utabiri wa hali ya chakula kwa 2012/2013
zinaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula utafikia Tani 13,572,804
ikilinganishwa na mahitaji ya chakula yanayokadiriwa kuwa Tani Milioni 11.99.
Taifa linatarajia kujitosheleza kwa chakula kwa Asilimia 113 na hivyo
kuwa na ziada ya Tani Milioni 1.58. Matarajio ni kwamba kwa maeneo yenye
kuonesha upungufu wa chakula utaratibu utafanywa wa kupata mahindi toka katika
Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA).
26.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hali hiyo ya kuridhisha,
tathmini ya mwezi Juni 2012 inaonesha kuwa bado kutakuwepo na uhaba wa chakula
katika Mikoa Sita (6) ya Arusha, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Manyara,
Shinyanga na Tabora. Kutokana na hali hiyo, katika mwaka 2012/2013 Serikali
itawezesha Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kununua Tani 200,000 za
nafaka kutoka kwa Wakulima wa Mikoa iliyozalisha ziada ya Iringa, Mbeya, Rukwa
na Ruvuma. Aidha, Serikali itahamisha Tani 100,000 za akiba ya Nafaka
iliyopo katika Maghala yenye ziada ya chakula kwenda kwenye Maghala ya Mikoa
yenye upungufu wa chakula. Zoezi la kuhamisha Mahindi hayo kwenda Dar es Salaam
limeanza. Hatua hii pia itatoa nafasi ya kuhifadhi nafaka zitakazonunuliwa
Msimu wa Ununuzi wa 2012/2013.
Bajeti
ya Kilimo kuwa Asilimia 10
27.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa Nchi za Umoja wa
Afrika (AU) uliofanyika Maputo, Msumbiji mwezi Julai 2003, moja ya makubaliano
ya Kikao hicho ni agizo la Nchi zote za Umoja huo kuhakikisha kuwa Bajeti zao
za Kilimo zinafikia Asilimia 10 ya Bajeti ya Taifa baada ya kipindi cha
miaka Mitano. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, makubaliano hayo
tunayatekeleza kwa kadri ya uwezo wetu na fedha zinazotengwa kwa ajili ya
Kilimo zimeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 233.3 mwaka 2005/2006, sawa
na Asilimia 5.6 hadi kufikia Shilingi Bilioni 926.2 mwaka
2011/2012, sawa na Asilimia 8. Katika mwaka huu wa fedha 2012/2013,
fedha zilizotengwa ni Shilingi Bilioni 1,103.6, sawa na Asilimia
9.0. Ni matumaini yangu kwamba kwa mwelekeo huu tutaweza kufikia Asilimia 10
kama tulivyokubaliana katika Nchi za Umoja wa Afrika muda wowote kuanzia mwaka
ujao wa fedha.
MAENDELEO
YA MIFUGO NA UVUVI
Kuboresha Ufugaji wa
Kuku ili Kuondoa Umaskini
28.
Mheshimiwa Spika, ufugaji wa Kuku wa Asili unayo
nafasi kubwa ya kukuza uchumi wa Wananchi waishio Vijijini, kuboresha lishe na
kipato chao. Takwimu zinaonesha kuwa Ufugaji wa Kuku wa Asili huchangia
Asilimia 94 ya Kuku wote Nchini. Aidha, unachangia Asilimia 80 ya
nyama na mayai yanayoliwa Vijijini na Asilimia 20 ya Mijini. Hata hivyo,
Sekta hii bado inakabiliwa na changamoto nyingi hususan, vifo vya Kuku
vinavyosababishwa na magonjwa hasa ya mdondo (Newcastle Disease).
Changamoto nyingine ni uhaba wa Maafisa Ugani, ukosefu wa taarifa za masoko na
ukosefu wa mitaji ya kuanzisha Miradi endelevu ya Ufugaji Kuku.
29.
Serikali imekuwa na mikakati mbalimbali ya kuboresha ufugaji wa Kuku wa
Asili ikiwa ni pamoja na kutengenezwa kwa Chanjo ya Kupunguza Vifo vya Kuku
kutokana na Ugonjwa wa Mdondo. Chanjo ya kuzuia Mdondo wa Kuku (Newcastle
Disease Vaccine) iligunduliwa Nchini Australia na kufanyiwa majaribio hapa
Nchini. Serikali inaagiza mbegu kutoka Australia na kutumia teknolojia hiyo
kutengeneza Chanjo hiyo hapa Nchini kupitia Maabara Kuu ya Temeke. Chanjo hii
imefanya vizuri sana na katika baadhi ya Vijiji katika Mkoa wa Singida na
imepunguza vifo dhidi ya Mdondo wa Kuku kwa Asilimia 96 hadi Asilimia 100.
30.
Mheshimiwa Spika, Shirika la Research Into Use
(RIU) linaloongozwa na Timu ya Wataalam ambao ni Vijana wetu waliosoma
Chuo Kikuu cha Sokoine, Morogoro wameanzisha Mradi wa Kuendeleza Kuku wa Asili.
Mradi huu ulizinduliwa Mwezi Machi mwaka huu 2012. Mradi wa RIU,
umeonesha kuwa Kuku wa Asili wanaweza kufugwa kibiashara. Mradi huo ambao
unatekelezwa katika Mikoa ya Singida, Dodoma, Morogoro na Pwani umewezesha
Wafugaji wa Kuku wa Asili wapatao 3,500 kuongeza idadi ya Kuku
wanaofugwa katika Kaya kutoka 5 hadi 10 na kufikia kati ya 100
hadi 300. Mafanikio haya yametokana na Wafugaji kuwezeshwa kupata
mafunzo, mitaji, masoko na kuwaunganisha na Wadau wengine hususan wauzaji wa
Dawa za Tiba ya Kuku.
31.
Kutokana na mafanikio yaliyoonekana katika Mradi huo, Serikali
itaendelea kuwasaidia Wananchi na Wafugaji wa Kuku hapa Nchini kuendeleza
Ufugaji wa Kuku wa Asili ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo na kuajiri Maafisa
Ugani wa kutosha wa Kuku Asili. Vilevile, Serikali itahimiza Mpango wa
kuanzisha Mashamba Darasa ya Ufugaji Bora wa Kuku ambao utawezesha kutoa elimu
kwa Wafugaji wengi zaidi. Natoa wito kwa Halmashauri za Wilaya kutoa kipaumbele
katika kuhamasisha Wananchi kuanza Ufugaji wa Kuku wa Asili ambao umeonesha
kuwa na mafanikio na manufaa makubwa ya kuondoa umaskini.
Maendeleo
ya Ufugaji Nyuki
32.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo mtakumbuka katika
Mikutano kadhaa ndani ya Bunge lako Tukufu nimekuwa nikisisitiza fursa ya
kipekee tuliyonayo ya kufanya Ufugaji Nyuki ambao una faida kubwa
kiuchumi na katika kuondoa umaskini. Gharama za Ufugaji Nyuki ni nafuu
sana ikilinganishwa na aina nyingine yoyote ya Ufugaji. Kutokana
na ukweli huo Wananchi wameanza kuhamasika katika maeneo mengi Nchini kuhusu
Ufugaji Nyuki. Aidha, Wawekezaji wameanza kuwekeza baada ya kujiridhisha kwamba
Ufugaji wa Nyuki katika Nchi yetu una faida na manufaa makubwa.
33.
Mheshimiwa Spika, mwanzoni mwa mwezi Juni 2012
niliweza kufungua Kiwanda kipya cha kisasa cha kuchakata Asali pale Visiga,
Kibaha. Kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata Tani 10,000 za Asali kwa
mwaka. Aidha, vipo pia Viwanda vingine Saba (7) Nchini. Takwimu za mwaka
2011/2012 zinaonesha Uzalishaji wa Asali ulifikia Tani 9,000 zenye
thamani ya Shilingi Bilioni 27 na Nta Tani 600 zenye thamani ya Shilingi
Bilioni tatu (3). Hii ni ishara nzuri ya kwamba Soko la Asali lipo na
Asali ni zao muhimu la kuongeza Kipato cha Wananchi. Napenda kutumia nafasi hii
tena kuwahimiza Wananchi kutumia fursa hii kwa kuzalisha mazao ya Nyuki kwa
wingi, kwani Soko la Asali na Nta lipo tayari.
UPATIKANAJI
WA MAJI NCHINI
34.
Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala wa Hotuba ya
Bajeti ya Wizara ya Maji, Waheshimiwa Wabunge wengi walionesha kutoridhishwa na
hali ya upatikanaji wa Maji katika maeneo mbalimbali Nchini. Maeneo mengi ya
Nchini yameendelea kuwa na uhaba wa maji kutokana na uharibifu wa vyanzo vya
maji, ongezeko la watu, ukame unaotokana na athari za mabadiliko ya Tabianchi
na matumizi ya maji yasiyozingatia tija na ufanisi. Aidha, tatizo la Maji
limechangiwa na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii zisizowiana na
uwekezaji katika miundombinu ya maji.
35.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na Tatizo la
Maji Nchini, Serikali inatekeleza Miradi mbalimbali kwa kutumia fedha za ndani
na fedha za nje kupitia kwa Wafadhili na Wadau wa Maendeleo. Iko Miradi ya Maji
inayoendelea kutekelezwa katika Halmalshauri mbalimbali Nchini kwenye Mikoa ya
Arusha, Dar es Salaam, Lindi, Kagera, Katavi, Kigoma na Kilimanjaro. Miradi
hiyo iko pia katika Mikoa ya Manyara, Mtwara, Mwanza, Shinyanga na Tabora.
36.
Mheshimiwa Spika, niruhusu nitumie muda mfupi
kuelezea Miradi michache inayotekelezwa na Serikali kama njia ya kukabiliana na
tatizo hili. Kwa mfano, tarehe 21 Julai 2012 Serikali ya Tanzania imesaini
Mkataba na Umoja wa Nchi za Ulaya wenye thamani ya Euro Milioni 51.51
kwa ajili ya Miradi ya Majisafi na Mazingira katika Mikoa ya Lindi, Kigoma,
Babati, Mtwara na Rukwa. Aidha, Serikali ya Ujerumani imetenga Euro Milioni
20 kwa ajili ya Mikoa ya Lindi, Kigoma na Rukwa. Majadiliano ya kusaini
Mkataba huu na Wafadhili yanaendelea. Halmashauri zimeendelea kutekeleza Miradi
ya Maji katika Vijiji 10 ambapo hadi Julai 2012, Halmashauri 67
zimepata vibali vya kuanza Ujenzi wa Miundombinu ya Maji. Miradi hii
inafadhiliwa chini ya Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini
inayotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, Benki ya
Maendeleo ya Afrika, Benki ya Kiarabu, Serikali za Uholanzi, Ufaransa, Korea
Kusini na Ubelgiji. Tayari fedha zimekwishatolewa kwa ajili ya Vijiji ambapo
utekelezaji utafanyika kufikia Wastani wa Vijiji Vitano (5) kwa kila
Halmashauri.
37.
Mheshimiwa Spika, katika Awamu ya Kwanza ya Mradi wa
Maji kutoka Ziwa Victoria, Serikali ililenga kufikisha maji katika Miji ya
Kahama na Shinyanga pamoja na Vijiji vyote vilivyopo kandokando ya Bomba Kuu la
kusafirishia Maji umbali usiozidi Km 5. Jumla ya Vijiji 54
vilihusika na kati ya hivyo 39 vilianza kupata huduma ya maji tangu
uendeshaji wa Mradi ulipoanza mwezi Februari 2009. Vijiji hivyo vyote vipo
katika Mikoa ya Shinyanga na Mwanza. Katika Awamu ya Pili ya Mradi, Vijiji
vyote vilivyopo umbali wa Km 12 kutoka kwenye Bomba Kuu katika Wilaya za
Misungwi, Kwimba, Shinyanga na Kahama vitaunganishwa, Vijiji hivyo tayari
vimetambuliwa. Tayari Serikali imepeleka kiasi cha Shilingi Milioni 304.5
katika Mradi huu.
38.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kawa,
katika Wilaya ya Nkasi unaendelea kukamilishwa. Mradi huu unahusu Usanifu wa
miundombinu ya usambazaji maji kutoka kwenye Bwawa la Kawa kwenda kwenye Vijiji
vya Nkundi, Fyengerezya na Kalundi. Uandaaji wa Makabrasha ya Zabuni kwa ajili
ya kupata Mkandarasi wa kujenga miundombinu ya maji umeanza na ujenzi utaanza
mara baada ya kupata Mkandarasi. Kiasi cha Shilingi Milioni 300 kimetengwa
katika mwaka 2012/2013 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji.
39.
Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2007/2008 hadi
2011/2012, Serikali ilifanya maamuzi ya kutumia Shilingi Milioni 95.9
kwa ajili ya ukarabati wa Bwawa la Mfili na Bomba Kuu la kutoka Mfili hadi
kwenye matanki pamoja na upanuzi wa Mtandao wa Maji Safi kwa Mji wa Namanyere.
Mwaka 2012/2013 Serikali imetenga Shilingi Bilioni 2.1 ili
kutekeleza hatua za dharura kuupatia Mji huo maji kwa kuboresha huduma ya maji.
Aidha, tarehe 23 Septemba 2011 Serikali ilisaini Mkataba na BADEA
kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Majisafi kwa Mji wa Orkesumet katika
Wilaya ya Simanjiro. Hadi sasa, majina ya Wahandisi Washauri watakaofanya
mapitio ya usanifu na kusimamia ujenzi yamepitishwa na Wizara; na BADEA
imekwisha idhinisha majina hayo kwa hatua zaidi. Mtaalamu Mshauri anatarajiwa
kuanza kazi mwaka 2012/2013.
40.
Mheshimiwa Spika, ni hivi karibuni tu tarehe 22
Julai 2012 Mheshimiwa Rais, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alizindua Mradi Mkubwa
wa Maji Safi katika Jiji la Mbeya uliotekelezwa chini ya Programu ya Regional
Centres uliofadhiliwa na Mfuko wa pamoja wa Programu ya Maendeleo ya Sekta
ya Maji, Jumuiya ya Ulaya, na Serikali ya Ujerumani. Kukamilika kwa Mradi huu
ambao uligharimu takriban Shilingi Bilioni 80 umeongeza huduma za Maji
kutoka Mita za Ujazo 32,000 kwa siku hadi Mita za Ujazo 49,000 kwa
siku kwa Wakazi wa Jiji la Mbeya. Lengo ni kufikia Mahitaji ya Jiji hili kwa
Asilimia 100 ifikapo mwaka 2017.
41.
Mheshimiwa Spika, napenda nitumie fursa hii
kuwaahidi Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwa ujumla kwamba Miradi yote ambayo
ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji Nchini itaendelea kupewa Kipaumbele
na Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi hadi yote ikamilike.
Mradi wa Maji wa
Ntomoko Wilayani Kondoa
42.
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 12 Agosti, 2012
nilipata fursa ya kutembelea mradi wa maji wa Ntomoko uliopo
Wilayani Kondoa. Mradi huu ulibuniwa na Serikali chini ya Uongozi
wa Hayati Baba wa Taifa, Mwl. Julius K. Nyerere ili kutoa huduma kwa watu
wapatao 23,400 katika Vijiji 17 vilivyoko katika Uwanda kame wa
Goima (The Goima Difficult Zone) ambao una tatizo kubwa la kupata maji.
Vijiji hivyo haviwezi kupata maji kupitia visima virefu kutokana na asili
ya Tabaka la miamba iliyopo katika Ukanda huo.
43.
Mheshimiwa Spika, Changamoto kubwa zilizopo katika
mradi huo, ni pamoja na uchakavu wa Miundombinu na huduma ya maji na ongezeko
la mahitaji ya maji linatokana na ongezeko kubwa la Watu ambalo sasa linafikia
watu wapatao 55,397. Chanzo cha Maji katika Mradi huu ni Chemchem
ya Ntomoko ambayo ina uwezo wa kuzalisha maji wastani wa lita 689,000
kwa siku. Hata hivyo, kwa sasa mahitaji halisi ya Maji katika Vijiji 17
ni Lita za Ujazo zipatazo 1,464,000 siku. Uchakavu wa Miundombinu ya
Mradi umesababisha Vijiji vinavyopata maji kupungua kutoka 17 mwaka 1973
hadi Vijiji Vitano (5) kwa sasa.
44.
Mheshimiwa Spika, ili kuondoa changamoto mbalimbali
za Mradi huu, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Serikali itaongeza kiasi cha
Shilingi Bilioni 2.3 katika Fedha iliyotengwa kwa Mradi huo na
Halmashauri za Wilaya ya Kondoa na Chemba ambazo zimetenga Shilingi Milioni
90. Lengo ni kuhakikisha kuwa Mradi huo unafufuliwa na kurudisha
huduma ya maji kwa Wananchi. Aidha, Serikali itaendelea na Juhudi za
kufufua Miradi ya namna hii ya maji ili kuhakikisha kuwa Wananchi wanapata
huduma ya maji. Aidha, katika kuhakikisha kuwa chanzo hiki kinalindwa,
niliwaelekeza Viongozi wa Wilaya ya Kondoa na Mkoa wa Dodoma kuhakikisha kuwa
Wanakijiji cha Mafai ambako ndiko iliko Chemchem ya Ntomoko, wanapata maji
kutoka kwenye Chanzo hicho.
USAFIRI WA BARABARA NA
KUKABILIANA NA MSONGAMANO WA MAGARI MIJINI
45.
Mheshimiwa Spika, wakati wa kujadili Bajeti za Ofisi
ya Waziri Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi, masuala mengi
yaliyojitokeza katika mijadala hiyo yalihusu namna ya kukabiliana na changamoto
zinazoikabili Sekta Ndogo ya Usafiri wa Barabara. Changamoto hizo ni
pamoja na kutounganika kwa Mtandao wa Barabara na maeneo ya uzalishaji Vijijini
pamoja na masoko, msongamano wa magari Mijini na mpangilio usio mzuri wa Miji
yetu, uhaba wa fedha za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara, uchakavu
na uchache wa mitaro ya kuondoa maji ya mvua katika barabara zetu, uhaba wa
Watalam na uwezo mdogo wa Makandarasi wa barabara na mfumo dhaifu wa kitaasisi
wa kuhudumia barabara za Wilaya na Vijiji.
46.
Mheshimiwa Spika, vilevile, wakati wa kuhitimisha
Hoja za Bajeti kuhusu Sekta Ndogo ya Usafiri wa Barabara, Mawaziri wa Sekta
hizo walieleza mikakati ya kupunguza changamoto hizo kwa Awamu kwa kuanzia na
Bajeti ya mwaka 2012/2013. Barabara zilizopewa kipaumbele katika Bajeti hizo ni
zile zenye kufungua fursa za kiuchumi katika maeneo ya uzalishaji, kupunguza
msongamano katika Miji hasa Jiji la Dar es Salaam, kuunganisha Nchi yetu na
Nchi jirani na kuendelea kutekeleza Programu kuhusu Uwekezaji katika
Miundombinu ya Uchukuzi kwa mwaka 2007 hadi 2017. Katika Programu hii, Miradi
16 ya ujenzi wa barabara kuu za lami iliyoanza kutekelezwa na Serikali ya
Awamu ya Tatu na kuendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Nne, ilikamilika
kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2005 na 2010. Barabara zilizokamilika katika
kipindi hicho zina urefu wa jumla ya Kilometa 1,236.
47.
Mheshimiwa Spika, kati ya mwaka 2005 hadi 2012,
Serikali ya Awamu ya Nne ilianzisha Miradi Mipya 78 ya Ujenzi na Ukarabati
wa Barabara zenye urefu wa jumla ya Kilometa 4,176. Kati ya Miradi hiyo,
Miradi 17 yenye urefu wa jumla ya Kilometa 662.2 imekamilika kwa
Asilimia 100 kufikia mwezi Juni 2012 na mingine 61 ipo katika
hatua mbalimbali za ujenzi. Sambamba na ujenzi unaoendelea katika Miradi hiyo,
kuna Miradi mingine 43 iliyobuniwa katika Awamu ya Nne yenye urefu wa
jumla ya Kilometa 5,739 ambayo inaandaliwa kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Kati ya Miradi hiyo, Miradi 16 yenye urefu wa jumla ya Kilometa 3,817,
ipo katika hatua mbalimbali za kukamilishwa Usanifu, na Miradi 27 yenye urefu
wa jumla ya Kilometa 1,921 usanifu wake umekamilika na inatafutiwa Makandarasi.
Lengo ni kuunganisha kwa awamu Miji Mikuu ya Mikoa yote Nchini kwa barabara za
lami ifikapo mwaka 2017/2018.
Kuondoa
Msongamano wa Magari katika Jiji la Dar es Salaam
48.
Mheshimiwa Spika, tatizo la msongamano wa magari
katika Jiji la Dar es Salaam linaathiri Wananchi wengi. Waheshimiwa Wabunge
wengi, hasa wale wa Mkoa wa Dar es Salaam walielezea kwa uchungu tatizo hili.
Serikali kupitia Wizara husika imeeleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa ili
kukabiliana na Msongamano kuwa ni pamoja na kuanzisha Mradi wa Mabasi yaendayo
Haraka, ujenzi wa Barabara za Mzunguko (ring roads), Barabara za Mlisho
(feeder roads), Barabara za Juu (flyovers) na kuanzisha huduma za
Usafiri wa Reli na vivuko Jijini Dar es Salaam.
Mradi
wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART)
49.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mradi wa
Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART). Lengo ni kuliwezesha Jiji la Dar
es Salaam kuwa na Mtandao wa Usafiri wa Mabasi makubwa yatakayopita katika njia
Maalum na hivyo kuwahakikishia Wananchi huduma bora za usafiri Jijini. Mradi
huo pia utasaidia kupunguza msongamano unaotokana na wingi wa mabasi madogo ya
Daladala katika barabara za Jiji.
50.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Mwaka 2012/2013
itatumika zaidi katika utekelezaji wa Miradi ya Awamu ya Kwanza na kuanza
maandalizi ya Miradi itakayotekelezwa katika Awamu ya Pili na ya Tatu. Awamu ya
Kwanza ina Miradi Saba (7) ambayo Mikataba ya Ujenzi ilisainiwa katika vipindi
tofauti kuanzia mwezi Mei 2010 hadi mwezi Machi 2012. Miradi yote hii
itakamilika katika vipindi tofauti, kuanzia mwaka 2012 hadi 2015.
Ujenzi wa Barabara
Mbalimbali, Madaraja na Barabara za Juu (flyovers)
51.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Mradi wa Mabasi yaendayo
Kasi, katika Bajeti Wizara ya ujenzi ya mwaka 2012/2013, Wakala wa Barabara
Nchini (TANROADS) unatekeleza Miradi 14 itakayogharimu Shilingi Bilioni
580 kwa ajili ya ujenzi wa barabara zitakazopunguza msongamano wa magari
katika Jiji la Dar es Salaam. Miradi hiyo inahusu ujenzi wa Barabara Kuu za
njia nne, Barabara za Mzunguko (ring roads), Barabara za Mlisho (feeder
roads) barabara ya kupita juu (flyover) kwenye Makutano ya TAZARA,
Daraja la Kigamboni na Gati za Vivuko. Miradi hii itakapokamilika itatoa
mchango mkubwa katika kupunguza msongamano uliopo hivi sasa.
Mradi
wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania
52.
Mheshimiwa Spika, tarehe 29 Julai 2012 nilikagua
utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu na Utoaji wa Huduma za
Jamii (Tanzania Strategic Cities Project) unaotekelezwa na Mamlaka
ya Uendelezaji Makao Makuu (CDA) na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma. Mradi
huu unatekelezwa pia katika Halmashauri nyingine saba Nchini kwa ufadhili
wa Benki ya Dunia na Serikali ya Denmark.
53.
Mheshimiwa Spika, katika ziara hiyo nilibaini kwamba
ili Miradi hii itekelezwe kwa kasi iliyokusudiwa, kuna umuhimu mkubwa kwa Wadau
wanaoguswa na utekelezaji wakiwemo TANESCO na Mamlaka za Maji, kukutana mara
kwa mara ili kuondoa vikwazo mbalimbali vinavyoathiri utekelezaji wa Mradi.
Halmashauri nyingine ambako Mradi huu unatekelezwa ni Majiji ya Mwanza, Tanga
na Mbeya na Arusha na Manispaa za Kigoma Ujiji na Mtwara Mikindani. Kazi
zitakazofanyika ni ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa Kilometa 141,
ujenzi wa Madampo ya Taka Ngumu, Vituo vya Mabasi na Mitaro ya Maji Machafu.
Mradi huu pia unajumuisha kipengele cha kujenga uwezo wa Halmashauri hizo
katika usimamizi na uendelezaji Miji, usimamizi na utunzaji mali za Miji,
usimamizi wa taka ngumu Mijini na uboreshaji wa Mfumo wa kukusanya mapato ya
ndani na upangaji Miji kimkakati. Nitumie fursa hii kuagiza Vikao vya Kamati za
Mashauriano za Mikoa husika kujadili taarifa za utekelezaji wa Miradi hii kila
vinapokaa ili matatizo yatakayobainika ya kiutekelezaji yaweze kupatiwa
ufumbuzi wa pamoja haraka.
54.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia inaendelea na
maandalizi ya Mradi mwingine utakaogharimu Dola za Marekani Milioni 255,
utakaoanza kutekelezwa mwaka 2013/2014. Mradi huu utahusu uimarishaji
wa Serikali za Mitaa zikiwemo Manispaa tatu za Jiji la Dar es Salaam
pamoja na Manispaa 11 za Morogoro, Tabora, Moshi, Sumbawanga, Shinyanga,
Songea, Singida, Musoma, Iringa, Bukoba na Lindi na Miji ya Mpanda,
Njombe, Babati, Geita, Korogwe, Bariadi na Kibaha. Kutekelezwa kwa Miradi
hii kutaboresha hali ya Miji yetu pamoja na huduma zitolewazo na hivyo
kuondokana na vikwazo vya usafiri na usafirishaji vilivyopo katika Miji hiyo
likiwemo suala la kuondoa misongamano ya magari kwa baadhi ya Miji.
UKUSANYAJI WA MAONI
KUHUSU KATIBA MPYA
55.
Mheshimiwa Spika, wakati nikiwasilisha Bajeti yangu
nilielezea hatua iliyofikiwa katika Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba na kwamba
Mheshimiwa Rais alikwishateua Tume na tayari Tume hiyo ilianza kazi tarehe 1
Mei, 2012. Aidha, Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria wakati akiwasilisha
Bajeti yake alifafanua kwa kina Muundo na Majukumu ya Tume na utaratibu wa
jinsi kazi ya kukusanya Maoni itakavyofanyika.
56.
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako
Tukufu kwamba, kazi ya kukusanya Maoni inaendelea vizuri. Hadi sasa Wajumbe wa
Tume wamekwisha kamilisha kukusanya maoni katika Mikoa minane, ambayo ni Tanga,
Pwani, Dodoma, Shinyanga, Kagera, Manyara, Kusini Unguja na Kusini Pemba.
Awamu ya Pili inaendelea na Wajumbe hivi sasa wanakusanya maoni katika Mikoa ya
Lindi, Morogoro, Mbeya, Ruvuma, Katavi, Kigoma na Mwanza. Nachukua fursa
hii kuwapongeza Wananchi kwa kutoa Maoni yao kwa amani na utulivu na bila woga.
57.
Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilisha kazi za
Awamu ya Kwanza, katika Awamu ya Pili, Tume itaandaa utaratibu wa kukusanya
maoni ya Wananchi kupitia Mabaraza ya Katiba katika ngazi mbalimbali. Mabaraza
hayo yatawashirikisha Wawakilishi kutoka makundi mbalimbali katika Jamii.
58.
Mheshimiwa Spika, ninaelewa zipo changamoto
zilizojitokeza kutokana na Jiografia ya Nchi yetu, hususan ukubwa wake hivyo
kuwa na uwezekano wa baadhi ya Wananchi wasifikiwe na Tume kwa karibu. Kutokana
na changamoto hizo, Tume imeweka taratibu nyingine zitakazowezesha Wananchi
kutoa maoni kwa njia ya barua, tovuti na mitandao ya kijamii. Nawashauri
Wananchi watumie njia hizo bila kusita ili kuwasilisha maoni yao kwenye Tume.
Aidha, tatizo la usambazaji wa Nyaraka kwa wakati nalo linafanyiwa kazi ili
nyaraka hizo zisambazwe kwa kasi zaidi.
59.
Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Wananchi wote
kuendelea kutoa ushirikiano kwa Tume pindi watakapofika katika maeneo yao kwa
lengo la kupata maoni. Suala la kutoa maoni ni wajibu wetu sote. Katiba nzuri
itatokana na maoni ya Wananchi wenyewe. Hii ni fursa pekee kwa Watanzania,
hivyo hatuna budi kuitumia kikamilifu.
UTAMADUNI
WA KUPIMA AFYA
60.
Mheshimiwa Spika, tarehe 16 Aprili, 2011 wakati
nikihitimisha Mkutano wa Tatu wa Bunge lako Tukufu nilizungumzia hali ya
Magonjwa Makuu Nchini. Nilibainisha maradhi makubwa ambayo yamepewa msukumo
mkubwa na Serikali katika kuyatokomeza. Magonjwa hayo ni Malaria, Kifua Kikuu,
Shinikizo la Damu, Kisukari, Saratani na UKIMWI. Hata hivyo, ilibainika kwamba
Magonjwa ya Shinikizo la Damu, Kisukari na Saratani hayajapata msukumo mkubwa
unaostahili pamoja na kwamba yamekuwa yakisababisha vifo vingi Nchini. Niruhusu
nieleze kwa mara nyingine kwa ufupi kuhusu Ugonjwa wa Saratani, hususan
Saratani ya Tezi ya Kibofu cha Mkojo (Prostate Cancer) ambao unawapata
Wanaume zaidi.
61.
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Saratani Duniani (The
World Cancer Report) za miaka mbalimbali zinaonesha kuwa Wanaume wawili
Duniani wanahitaji kupata matibabu ya Saratani ya Tezi la Kibofu cha Mkojo kila
dakika tano. Aidha, ukubwa wa tatizo la Ugonjwa huu umekuwa ukiongezeka kwa
kasi na sasa unawapata Wanaume wenye umri wa kuanzia Miaka 45 na
kuendelea badala ya Miaka 50 ya Awali hivyo, kupanua wigo wa uwezekano
wa Watu wengi zaidi kupata ugonjwa huo. Dalili za Ugonjwa huu katika
hatua za mwanzo kabisa ni pamoja na kushindwa kupata haja ndogo vizuri,
kupata haja ndogo mara nyingi kuliko kawaida, na kuanza kukojoa damu, au haja
ndogo kushindwa kutoka kabisa. Aidha, Vimelea vinapoanza kusambaa, mgonjwa
anaanza kupata maumivu ya mgongo, kuvimba miguu, na baadaye figo kushindwa
kufanya kazi. Kutokana na hali hiyo, upo umuhimu wa kuongeza nguvu katika
kutoa elimu kuhusu ugonjwa huu na kuhamasisha Wananchi waweze kupima afya zao
mapema.
62.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwaomba
Wanaume wote wenye umri unaofika miaka 45 na kuendelea kujenga utamaduni
wa kupima afya zao mapema ili kubaini hali ilivyo kuhusu ugonjwa huu wa
Saratani ya Tezi la Kibofu cha Mkojo kwa sababu ugonjwa huu unatibika kama
ukibainika mapema. Kwa misingi hiyo, napenda kuiagiza Wizara ya Afya kuweka
utaratibu maalum wa kuelimisha Wananchi kuhusu ugonjwa huu wa Tezi la Kibofu
cha Mkojo.
Bajeti
ya Afya kuwa Asilimia 15
63.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano kati ya Mawaziri wa
Fedha na Mawaziri wa Afya wa Afrika ulioandaliwa na Benki ya Maendeleo ya
Afrika kwa kushirikiana na Shirika la Harmonization for Health in Africa
(HHA) uliofanyika Nchini Tunisia tarehe 03 hadi 06 Julai 2012, suala kubwa
lililojadiliwa lilikuwa ni kuendelea kusisitiza Serikali za Nchi za Afrika
kutenga fedha zaidi kwenye Sekta ya Afya. Lengo likiwa ni kuhakikisha
kuwa, Wananchi wanakuwa na Afya nzuri kwa ukuaji wa uchumi wa Nchi zetu.
Mkutano huo ulipendekeza angalau Asilimia 15 ya Bajeti ya Serikali za Nchi
za Afrika iende kwenye Sekta ya Afya. Michango mingi iliyotolewa katika
Mkutano huo ilithibitisha kwamba, Uchumi wa Nchi za Afrika hauwezi kukua na kuwa
endelevu kama Nchi hizi hazina Wananchi wanaopata huduma nzuri za Afya.
64.
Mheshimiwa Spika, licha ya ufinyu wa Bajeti,
Serikali imedhamiria kadri ya uwezo wetu kufikia lengo hilo kama
ilivyopendekezwa. Fedha zinazotengwa kwa ajili ya Afya zimekuwa zikiongezeka
mwaka hadi mwaka. Kwa maana hiyo, kiasi kilichotengwa kimeongezeka kutoka
Shilingi Bilioni 365.8 sawa na Asilimia 8.8 mwaka 2005/2006 hadi
Shilingi Bilioni 1,288.8 sawa na Asilimia 10.0 mwaka
2012/2013. Ni matumaini yangu kwamba, kwa mwelekeo huo Serikali inaamini
tutaweza kufikia Asilimia 15 kama tulivyokubaliana katika Mkutano huo.
Aidha, ongezeko hilo linaonesha jinsi Serikali ilivyoamua kuwekeza katika Sekta
hii muhimu ya Afya kwa manufaa ya Wananchi wake.
AJIRA KWA VIJANA
65.
Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto zinazokabili
Taifa letu ni kiwango cha juu cha ukosefu wa Ajira hasa kwa Vijana. Kwa mujibu
wa takwimu zilizopo, jumla ya Vijana wasio na Ajira hapa Nchini ni Milioni
1.4, sawa na Asilimia 13.4 ya nguvu kazi yote ya Vijana.
Kuongezeka kwa kasi kwa ukosefu wa Ajira kwa Vijana kunachangiwa na mambo
kadhaa, ikiwemo uwekezaji mdogo wa ndani na nje, kasi ndogo ya ukuaji wa Sekta
Binafsi Nchini na ukosefu wa elimu ya ujasiriamali kwa Vijana wengi. Aidha, ukosefu
wa Ajira pia unasababishwa na baadhi ya Vijana kuchagua kazi za kuajiriwa,
badala ya kujiajiri wenyewe hasa kwenye Sekta zenye fursa kubwa kama vile
Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Ufugaji Nyuki.
66.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Waheshimiwa
Wabunge mbalimbali walipata fursa ya kutoa michango mizuri ya mawazo
inayoelezea ukubwa wa tatizo la Ajira Nchini, na namna ya kulipatia ufumbuzi.
Aidha, Waheshimiwa Wabunge wengi waliafikiana na Serikali kwamba changamoto ya
upatikanaji wa Ajira nyingi kwa Vijana inahitaji ushirikiano wa Wadau wengi. Ni
dhahiri kuwa, juhudi za pamoja zinahitajika baina ya Serikali, Sekta Binafsi,
Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri, Taasisi Zisizo za Kiserikali na Jamii kwa
ujumla kukabiliana na changamoto hii. Kwa upande wake, Serikali ina wajibu
mkubwa wa kuweka mazingira wezeshi ya kuongeza Uwekezaji na ukuaji wa Sekta
Binafsi ili kuongeza fursa nyingi za upatikanaji wa Ajira. Hii ni pamoja na
kubuni na kuandaa Sera na Sheria Wezeshi za Uwekezaji, uzalishaji na kufanya
biashara. Vilevile, kuhakikisha kwamba kuna miundombinu muhimu ya usafirishaji,
umeme wa kutosha, maeneo ya kuwekeza na kuzalisha pamoja na Mfumo bora wa elimu
utakaowezesha wahitimu wengi kujiajiri na kushindana katika Soko la Ajira.
67.
Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada za kuvutia
uwekezaji, Serikali inaimarisha Mifuko mbalimbali ya kuwawezesha Vijana ili
waweze kujiajiri wenyewe. Kwa mfano, Mfuko wa Dhamana chini ya Programu ya
Taifa ya Kuwezesha Wananchi Kiuchumi, (Maarufu kama Fedha za JK); Mfuko wa
Maendeleo ya Vijana unaosimamiwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo; Mfuko wa Wajasiliamali Wadogo unaosimamiwa na SIDO; na Vyama vya Akiba
na Mikopo (SACCOS) vimeimarishwa na kuwekewa mazingira mazuri ya kuviwezesha
kufanya kazi kibiashara na kwa ufanisi. Ni matumaini yangu kwamba tukitumia
Mifuko hii vizuri tutaweza kuongeza Ajira kwa Vijana kwa kasi zaidi.
Nasisitiza pia kuwa, ni muhimu kwa vijana wetu na wale wote wanaopata ajira au
kujiajiri wenyewe wawe na nidhamu kazini, wafanye kazi kwa weledi na kutumia
utaalam wao vizuri. Tusiwe wepesi kulalamika wakati hatutimizi wajibu
wetu kama Waajiriwa.
SENSA YA WATU NA MAKAZI
68.
Mheshimiwa Spika, takriban siku kumi zijazo tutakuwa
na Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika kuanzia saa Sita Usiku wa kuamkia
tarehe 26 Agosti, 2012 Nchini kote. Umuhimu wa Sensa hii nimeuelezea
katika hotuba zangu za ndani na nje ya Bunge lako Tukufu zikiwemo hotuba za
Bajeti kwa miaka mitatu mfululizo. Kwa kutambua umuhimu wake maandalizi
yaliyoanza mapema mwaka huu sasa yamekamilika. Kwa vile, Mkutano huu
unamalizika siku chache kabla ya kufanyika kwa Sensa hiyo, napenda kutumia
fursa hii kuwashukuru kwa dhati Watanzania wote waliojitolea kwa hali na mali
wakati wa kipindi chote cha maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi. Tumejitahidi
kwa kadri ya uwezo wetu kujiandaa vizuri na sasa siku imewadia. Wito wangu kwa
Wananchi wote ni kuendelea kutoa ushirikiano kwa Makarani wa Sensa na
kujitokeza kuhesabiwa kuanzia tarehe 26 Agosti, 2012 hadi zoezi hilo
litakapokamilika.
69.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee niwashukuru
Viongozi wa Taasisi za Dini ambao kwa pamoja waliona umuhimu wa Sensa na
hatimaye kuwahamasisha Waumini wao kushiriki katika zoezi zima la Sensa ya Watu
na Makazi. Niwashukuru kwa kuwasaidia Waumini hao kwa kuwapa maelezo
yaliyo sahihi kuhusu zoezi zima la Sensa. Madhumuni ya Zoezi la Sensa ni
kuliwezesha Taifa kupata Takwimu sahihi na za uhakika kuhusu idadi ya Watu ili
ziweze kutumika kutunga Sera za Kiuchumi na Kijamii, pamoja na kuwezesha
kupanga kwa usahihi, kutekeleza na kutathmini Mipango ya Maendeleo ya muda
mfupi na muda mrefu.
70.
Aidha, napenda kusisitiza tena kwamba Zoezi la Sensa halitakuwa la siku
moja tu, bali siku hiyo ya tarehe 26 Agosti, 2012 itakuwa ndiyo siku ya
msingi wa kuhesabu Watu waliolala siku hiyo katika Kaya husika. Kazi
yenyewe ya kuhesabu Watu itaendelea kwa siku saba hadi tarehe 2 Septemba, 2012.
Hivyo, Nawasihi Waheshimiwa
Wabunge na Viongozi wote katika ngazi zote kusimamia zoezi hili na kuendelea
kuwahamasisha Wananchi kushiriki kuhesabiwa siku ya Sensa tarehe 26 Agosti
2012.
HITIMISHO
71.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha hotuba yangu
napenda kusisitiza kuwa tumetekeleza wajibu wetu kama Wabunge kwa kutoa
michango yetu ndani ya Bunge lako Tukufu. Ni kweli kwamba, tumefanya kazi kubwa
inayostahili pongezi. Lakini pia Bunge kama Chombo cha Uwakilishi, linayo
majukumu mengine na moja ni kuisimamia Serikali iliyoko Madarakani itimize
Wajibu wake. Ni wajibu wetu kama Wabunge kuikosoa Serikali ili kuhakikisha
kwamba matatizo na kero mbalimbali za Wananchi yanatatuliwa. Lakini siyo
kuikosoa na kuishia hapo tu, bali tuna wajibu wa kuishauri na kuielekeza kwa
lengo la kuwaletea maendeleo Wananchi walio tuchagua.
72.
Mheshimiwa Spika, ili yote hayo yafanyike, ni lazima
sisi kama Wabunge tuwe Wasafi na wenye Maadili mbele za Wananchi wetu. Tuhuma
za Rushwa zilizojitokeza dhidi ya baadhi ya Wabunge na hivyo kupelekwa kwenye
Kamati ya Maadili, haileti picha nzuri kwa Bunge letu. Ninachowaomba
Waheshimiwa Wabunge ni kwamba tutambue dhamana kubwa tuliyonayo kwa Wananchi
wetu. Ni vizuri tuienzi dhamana hiyo na kuiheshimu. Hivyo, nawasihi tutumie
fursa ya kipindi hiki kilichobaki cha takribani miaka mitatu kuendelea
kuimarisha utamaduni wa kushirikiana na kuhakikisha kwamba tunawatumikia
Wananchi waliotuchagua kwa bidii zetu zote.
73.
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuwashukuru tena
wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Shukrani za pekee ni kwako wewe
Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri. Nawashukuru
vilevile Wenyeviti wa Bunge wote kwa msaada mkubwa walioutoa katika kuliongoza Bunge
kwenye Mkutano huu. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango
yao pamoja na Watumishi wote wa Serikali walioisaidia Serikali kujibu maswali
na kuwasilisha Hoja za Serikali hapa Bungeni.
Kipekee namshukuru Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilillah pamoja na Watumishi
wote wa Ofisi ya Bunge kwa kufanikisha Mkutano huu. Nawashukuru wale wote
waliokuwa na jukumu la Ulinzi na Usalama ili kuhakikisha Mkutano huu unafanyika
na kumalizika salama. Napenda pia niwashukuru Madereva wote kwa kutekeleza
wajibu wao kwa ufanisi mkubwa. Nawashukuru pia Waandishi wa Habari kwa
kuhakikisha kuwa Habari za hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Mwisho,
niwashukuru Wananchi wa Dodoma kwa ukarimu wao wa kutupatia huduma zote muhimu
na hivyo kukamilisha Mkutano huu wa mafanikio makubwa.
74.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa
hoja kuwa Bunge lako Tukufu sasa liahirishwe hadi Jumanne, tarehe 30 Oktoba,
2012, litakapokutana saa 3.00 Asubuhi hapa Mjini Dodoma.
75.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
4
COMMENTS