HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA MHESHIMIWA BERNARD KAMILLIUS MEMBE (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO ...
HOTUBA
YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA
KIMATAIFA MHESHIMIWA BERNARD
KAMILLIUS MEMBE (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO
WA
KIMATAIFA KWA MWAKA
WA
FEDHA 2012/2013
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa
Spika, kufuatia
taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), naomba sasa kutoa hoja kwamba
Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mwaka wa
fedha 2012/2013.
2. Mheshimiwa
Spika, awali ya yote
napenda kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi kwa kuliongoza kwa umahiri
mkubwa Bunge hili la Bajeti la mwaka 2012/2013. Napenda pia kuwapongeza Mheshimiwa Job Ndugai
(Mb.), Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wanaokusaidia kuongoza Bunge hili
kwa kazi nzuri wanayoifanya.
3. Mheshimiwa
Spika, kwa namna ya
pekee nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri wa Serikali ya Awamu
ya Nne. Chini ya uongozi wake Taifa letu limeendeleza utamaduni wetu wa
kudumisha amani, utulivu na mshikamano. Nawaomba Watanzania wote tuendelee
kudumisha hali hiyo ili kuimarisha umoja wetu ambao ni tunu isiyopatikana kwa
bei yoyote.
4.
Mheshimiwa Spika, niruhusu
niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine wote walionitangulia kuwapongeza
kwa dhati kabisa Waheshimiwa Wabunge
wapya, Mawaziri na Naibu Mawaziri walioteuliwa na Mheshimiwa Rais mwezi Mei
2012. Nawapongeza Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge
waliochaguliwa kipindi hiki kutokana na mabadiliko yaliyotokea kwenye nafasi
mbalimbali humu Bungeni na ndani ya Serikali. Nampongeza pia Mheshimiwa Mussa
Zungu Azzan, Mbunge wa Ilala, kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge.
5.
Mheshimiwa Spika, kwa njia ya
kipekee kabisa, niruhusu niwapongeze Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa na
Bunge lako Tukufu kuiwakilisha Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki.
Wizara yangu kwa kuwa ndiyo inayosimamia masuala yote ya mambo ya nje,
nawaahidi Waheshimiwa Wabunge ushirikiano wangu binafsi na ule wa Wizara nzima
kwa kufanya kazi kwa karibu na kushirikiana na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki.
6.
Mheshimiwa
Spika, naomba
niwashukuru pia Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.), Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa William A. Mgimwa (Mb.), Waziri
wa Fedha; pamoja na Mheshimiwa Stephen Masatu Wasira (Mb.), Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu kwa hotuba zao za kina
ambazo zimetoa ufafanuzi na miongozo kwa masuala mbalimbali muhimu ya Taifa
letu kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Kwa ujumla wake, naomba kuwapongeza
Waheshimiwa Mawaziri wote waliotangulia kuwasilisha bajeti zao kwa kazi nzuri
walizozifanya. Hotuba zao zote zimefafanua kwa kina masuala ya uchumi, siasa na
jamii yanayohusu nchi yetu na hivyo kuigusa pia Wizara yangu kwa njia moja au
nyingine.
7.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie
fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati na za uongozi mzima wa Wizara kwa
Kamati ya Bunge ya kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), chini ya
uongozi madhubuti wa Mhe. Edward
Ngoyai Lowassa (Mb.), Mwenyekiti wa Kamati kwa ushauri wao mzuri
ambao wamekuwa wakiutoa mara kwa mara kwa Wizara yangu. Kamati hii imetoa
mchango mkubwa sana katika kuiwezesha Wizara kukabiliana na changamoto
zinazoikabili katika kutekeleza majukumu yake. Ninaamini ziara walizozifanya
kwenye nchi mbalimbali kutembelea Balozi zetu zimewapa fursa ya kujionea
wenyewe na kusikia kutoka kwa maafisa wetu changamoto mbalimbali zinazotukabili
kama Wizara. Aidha, kwa ujumla, napenda kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote
kwa michango yao wanayoitoa Bungeni katika kuishauri Serikali.
8.
Mheshimiwa Spika, natoa shukrani
na pongezi maalum kwa Mheshimiwa Mahadhi Juma Maalim (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa kwa ushirikiano anaonipa katika kutekeleza
majukumu ya Wizara. Vilevile, nawapongeza na kuwashukuru Bwana John M. Haule, Katibu
Mkuu, Mheshimiwa Balozi Rajabu H. Gamaha, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi,
Mabalozi na wafanyakazi wote kwa msaada mkubwa wanaonipa katika kuiongoza
Wizara hii. Pamoja na kukabiliwa na changamoto mbalimbali katika kutekeleza
majukumu yao, nawashukuru kwa kazi nzuri na ya kizalendo ya kutetea maslahi ya
Taifa letu.
9.
Mheshimiwa Spika, shukrani za
pekee ziwaendee wananchi na viongozi wa Mkoa wa Lindi, Wilaya ya Lindi na hasa
wana-Mtama wote. Napenda pia nimshukuru
mke wangu Mrs. Membe na watoto wangu kwa upendo na uvumilivu waliouonesha
kwangu.
10.
Mheshimiwa Spika,
kabla ya kuanza kueleza kwa kina kuhusu hotuba yangu, niruhusu niungane na
Viongozi wote, Wazanzibari na Watanzania kutoa pole kwa ndugu, jamaa na
marafiki wote waliopoteza ndugu zao kwenye ajali ya meli ya MV Skagit iliyotokea Zanzibar. Kwa wale
wote walioumia na wanaoendelea kujiuguza, namwomba Mwenyezi Mungu awape nguvu
waweze kupona haraka.
11.
Mheshimiwa Spika,
vilevile, natoa salamu za pole kwa wale Wabunge wote waliopatwa na misiba ya
wapendwa wao. Kwa wote, namwomba Mwenyezi Mungu awape faraja na azilaze Roho za
Marehemu mahali pema peponi. Amina.
TATHMINI YA HALI YA DUNIA KWA KIPINDI CHA 2011/2012
HALI YA DUNIA
ULAYA NA MAREKANI
12.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla,
hali ya dunia kiuchumi, kisiasa na kijamii katika mwaka wa fedha 2011/2012
imekuwa ya mashaka makubwa na hivyo kuathiri utulivu katika nchi nyingi
duniani. Hali hiyo imechochewa na mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na
mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali duniani.
13.
Mheshimiwa Spika, eneo la Ulaya
limeathirika sana kiuchumi kutokana na madeni pamoja na mdororo wa uchumi ulioikumba
dunia katika kipindi cha mwaka 2008. Hali hii pia iliathiri kwa kiasi kikubwa
sarafu ya Euro, uchumi wa nchi zilizo katika ukanda wa sarafu hiyo ujulikanao
kama “Eurozone” pamoja na nchi ambazo
zinafanya biashara na nchi za Umoja wa Ulaya. Hali hiyo imechangia kwa kiwango
kikubwa Viongozi katika baadhi ya nchi hizo kama vile; Ufaransa, Ugiriki,
Italia, Hispania na Ireland kushindwa katika Chaguzi Kuu au kushinikizwa
kujiuzulu. Kwa upande wa Marekani nayo ilikumbwa na misukosuko ya uchumi
iliyosababishwa pia na mdororo wa uchumi wa mwaka 2008. Hata hivyo, uchumi wake
umeanza kutengemaa baada ya mdororo huo.
14.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mdororo huo, nchi hizo zimelazimika
kuchukua hatua kadhaa kunusuru uchumi wao ikiwa ni pamoja na kubana matumizi,
kukopa zaidi ili kuwekeza katika sekta zenye kutoa ajira na kupunguza kutoa
misaada kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania kulingana na ahadi zao za
awali. Kuna kila kiashiria kuwa uchumi wa Ulaya na Marekani hautapata utulivu
kwa muda mrefu na hivyo uwezo wao wa kutoa misaada kupungua kadiri siku
zinavyokwenda. Wizara na Balozi zetu za nje zinaendelea kufuatilia kwa makini
hali ya uchumi inavyoendelea duniani na kuishauri Serikali kutekeleza mikakati
ya kukabiliana na changamoto zitokanazo na hali hiyo ili kuimarisha uchumi wa
Taifa letu na kuondokana na utegemezi.
ASIA
Mashariki ya Kati
15.
Mheshimiwa Spika, eneo la Mashariki ya Kati bado liko katika hali ya
tahadhari. Nchini Syria hali imeendelea kuwa tete kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo ambako
waasi wanapigana dhidi ya Serikali ya Rais Bashar al – Assad tangu Januari
mwaka 2011 na tayari wameshaingia kwenye Mji Mkuu wa Nchi hiyo. Umoja wa
Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) zikiongozwa na Msuluhishi
wa Mgogoro huo, Dkt. Kofi Annan wameshindwa hadi sasa kufanikisha kusitishwa
kwa mapigano. Aidha, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limegawanyika ambapo
wajumbe wa kudumu wenye kura ya turufu wametofautiana juu ya uamuzi wa kuchukua
hatua za kijeshi dhidi ya Serikali ya Syria. Tanzania inaunga mkono jitihada za
Msuluhishi Kofi Annan na kuwaomba wadau wote kutoingilia na kushinikiza matakwa
yao nchini Syria na badala yake kumuunga mkono Msuluhishi ili kumaliza mgogoro
huo kwa njia ya amani.
16.
Mheshimiwa Spika, aidha,
kuendelea kukua kwa uhasama baina ya Iran na nchi za Magharibi kunaleta
changamoto ya ustawi wa amani katika ukanda huo. Uhasama huo unaletwa na hofu
kuwa nchi ya Iran inarutubisha madini ya urani yanayotumika kutengeneza silaha
za nyuklia. Tayari, Iran imewekewa vikwazo vya kiuchumi na Marekani
ikishirikiana na nchi za Umoja wa Ulaya. Iran nayo imetishia kujibu mapigo kwa
kufunga mlango wa Bahari ya Hormuz ambao hupitisha asilimia ishirini 20 ya
mafuta yote ulimwenguni. Iwapo Iran itatekeleza uamuzi huo inaweza kuzusha vita
ambayo italeta madhara makubwa kwa uchumi wa dunia. Hali hii ya mtafaruku baina
ya Iran na nchi za Magharibi inaathiri pia mustakabali wa ukanda mzima wa
Mashariki ya Kati kwa kuwa Iran ina ushawishi mkubwa kwenye siasa za nchi
nyingine zenye machafuko kama vile Syria. Kuendelea kwa migogoro na machafuko
katika ukanda wa Mashariki ya Kati kunaathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa dunia
kwa sababu asilimia kubwa ya mafuta yanayotumika duniani hutoka katika ukanda
huo. Pamoja na changamoto hizo, habari njema ni kwamba tayari Irani, Marekani,
Nchi za Ulaya pamoja na wadau wengine wameshakubaliana kurejea kwenye meza ya
mazungumzo na tayari mzunguko wa kwanza wa mazungumzo haya umeshafanyika. Imani
yetu kama nchi ni kwamba wahusika wote kwenye mazungumzo hayo wataonesha utashi
wa kweli wa kumaliza tatizo hilo kwa njia ya mazungumzo na si vinginevyo.
Mashariki ya Mbali
17.
Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa Mashariki ya Mbali hali ni tulivu ukiachilia majanga ya asili
yaliyozikumba nchi za Japan, Ufilipino na Thailand na kusababisha athari za
kijamii na kiuchumi kwa baadhi ya sekta, hususan viwanda na makazi ya watu.
Hali ya kiusalama katika Peninsula ya Korea nayo imeonekana kutulia kidogo
kufuatia mabadiliko ya uongozi nchini Korea Kaskazini baada ya kifo cha Rais
Kim Jong-il aliyekuwa Rais wa Korea Kaskazini. Aidha, kwa upande wa Japan, hali
ya kiuchumi imeanza kuimarika hasa baada ya kukumbwa na tukio la Tsunami la
mwaka 2011 lililoathiri kwa kiasi kikubwa kinu cha nyuklia cha Fukushima.
AFRIKA
18.
Mheshimiwa Spika, kama
ilivyo kwenye maeneo mengine duniani, Bara la Afrika nalo limeathiriwa na hali
ya mitikisiko ya aina mbalimbali duniani, ikiwemo ya kiuchumi, kisiasa na
kijamii. Maendeleo ya Bara hili yameendelea kukabiliwa na changamoto za
kiusalama, kisiasa, kiuchumi, kijamii, mabadiliko ya tabianchi, vitisho vya
ugaidi, uharamia wa baharini, kupanda kwa gharama za bidhaa muhimu kama vile
chakula, matatizo ya nishati ya umeme na kukosekana kwa ajira. Pamoja na masuala
hayo ya jumla, yapo baadhi ya masuala ambayo yanaweza yakaipambanua hali ya
Barani Afrika kwa sasa, hasa katika kipindi hiki cha miezi sita iliyopita. Aidha,
kuna masuala yanayozigusa baadhi ya nchi kama inavyoelezwa hapa chini:
Uchaguzi wa Uongozi wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika
19.
Mheshimiwa Spika, suala kubwa
lililotawala hali ya kidiplomasia Barani Afrika ndani ya mwaka wa fedha 2011/2012
ni uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika. Kama
itakavyokumbukwa, uchaguzi huo ulipangwa kufanyika mwezi Januari, 2012 wakati
wa Mkutano wa 18 wa Umoja wa Afrika wa
Wakuu wa Nchi na Serikali. Ushindani mkali ulizuka kati ya wagombea wawili
waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ambao ni Bw. Jean Ping wa Gabon, Mwenyekiti
wa Kamisheni aliyemaliza muda wake na Bibi Nkosazana Dlamini-Zuma, Waziri wa
Mambo ya Ndani wa Afrika Kusini. Mvutano huo ulisababisha Wakuu wa Nchi
kushindwa kumchagua Mwenyekiti mpya wa Kamisheni hiyo baada ya wagombea wote
wawili kushindwa kufikia theluthi mbili za kura zinazohitajika kisheria.
20.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kukosekana
mshindi, Wakuu wa Nchi na Serikali waliamua kuahirisha uchaguzi huo hadi kwenye
mkutano wao wa 19 uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia, mwezi Julai 2012. Katika
uchaguzi huo, Bibi Nkosazana Dlamini-Zuma, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afrika
Kusini, alifanikiwa kuibuka mshindi. Hivyo, Mama Zuma anakuwa mwanamke wa
kwanza kuongoza Kamisheni hiyo. Ushindi wa Bi. Nkosazana Zuma ni ushindi wetu
pia kwa kuwa alikuwa ni mgombea wa SADC na Tanzania ilishiriki kikamilifu
katika kampeni zake.
Misri
21.
Mheshimiwa Spika, hali
ya kisiasa nchini Misri ilishuhudiwa na matokeo ya machafuko yaliyopelekea
kuangushwa kwa utawala wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Mheshimiwa Hosni
Mubarak. Baada ya utawala wa Mpito ulioongozwa na Jeshi la nchi hiyo, hatimaye
Chama chenye mlengo wa kushoto cha Udugu wa Kiislam (Muslim Brotherhood)
kimefanikiwa kushinda uchaguzi huru uliofanyika Juni, 2012 kupitia mgombea wake
Mheshmiwa Dkt. Mohammed Mursi. Wizara yangu itashirikiana na
Serikali mpya na kuendeleza mahusiano mazuri baina ya nchi zetu mbili
ikizingatiwa kuwa Misri ni mdau muhimu katika kufanikisha matumizi ya
rasilimali za Bonde la Mto Nile kwa maslahi ya pande zote husika.
22.
Mheshimiwa
Spika,
ni vyema kutambua kuwa ingawa uchaguzi umefanyika bado hali ya kisiasa ni tete. Hii ni kwa sababu licha ya kuwa Muslim
Brotherhood wameshinda kwa kuwa na Wabunge wengi Bungeni na kushika Ikulu, bado
Jeshi la Misri linaendelea kushika hatamu za uongozi. Jeshi limevunja Bunge na ndilo linalofanya
maamuzi makubwa.
23.
Mheshimiwa
Spika, ni
matumaini yetu kwamba hali hiyo tete ya kisiasa itatengemaa na hali kuwa nzuri.
Tanzania itashirikiana na Serikali mpya ya Misri ili kuendeleza na kudumisha
mahusiano yetu ya kirafiki na ya kihistoria.
Libya
24.
Mheshimiwa Spika, baada
ya aliyekuwa Kiongozi wa Libya Kanali Muammar Qaddafi kuuawa na Serikali yake
kupinduliwa na wapinzani wa NTC, Libya ilikumbwa na matatizo ya usalama. Mauaji ya Walibya weusi yaliendelea. Hakukuwa na Serikali madhubuti, hakukuwa na
Bunge na wala hakukuwa na taasisi za Kidemokrasia.
25.
Mheshimiwa
Spika, Tanzania
tulilaani mauaji ya Kiongozi huyo na tulisema kuwa tungalitambua Serikali ya
NTC tu iwapo ingalikuwa na viongozi wa kuchaguliwa, Bunge, Mahakama na uundwaji
wa Serikali ya mpito ambayo itajumuisha wadau kutoka vyama vyote vya siasa.
26.
Mheshimiwa Spika, uchaguzi wa
kwanza wa Kidemokrasia ulifanyika Libya mwezi Julai, 2012 kuchagua Wabunge
200. Waombaji 3,000 walijitokeza
kugombea nafasi hizo. Pamoja na matatizo
yote ya kiusalama, wananchi milioni moja na laki nane waliweza kuchagua Wabunge
wao 200 na Bunge linategemewa kumchagua Rais na Waziri Mkuu katika kipindi cha
siku 30 baada ya uchaguzi. Zoezi hilo
limekamilika. Aidha, Bunge limechagua kutoka miongoni mwao Wabunge 60 wa kuunda
Baraza la kuandika Katiba mpya, na Baraza hilo limepewa siku 120 kuwakilisha
mapendekezo ya Katiba kwenye Bunge lao. Mchakato huo umeanza.
27.
Mheshimiwa Spika, uongozi wa
Serikali ya Libya umekutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Kikwete mjini Addis Ababa tarehe 15 Julai, 2012 na ukaeleza nia yake ya kutuma
ujumbe Tanzania kuja kutoa taarifa ya hali ya usalama na kisiasa na kufufua
rasmi mahusiano ya Kibalozi na Tanzania.
Tunausubiri ujumbe huo na sisi sasa tumeridhika na mchakato wa kujenga
demokrasia unaoendelea nchini Libya.
Tanategemea kuletewa hati za Balozi mpya hivi karibuni na tutazipokea
ili tuweze kurejesha huduma za Kibalozi kama ilivyokuwa mwanzo.
Somalia
28.
Mheshimiwa Spika, hali ya kisiasa na kiusalama nchini Somalia kwa sasa inatia matumaini
ya kupatikana kwa amani kutokana na juhudi za Umoja wa Afrika pamoja na
washirika wake katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa muda mrefu wa nchi hiyo.
Serikali ya Mpito ya Somalia inatarajiwa kumaliza muda wake mwezi huu Agosti,
2012 na tayari rasimu ya Katiba kwa ajili ya Serikali mpya imeandaliwa na
inatarajiwa kupitiwa na Baraza la Katiba linalojumuisha Wazee kutoka Koo zote
tarehe 20 Agosti 2012. Kupatikana kwa Serikali mpya ambayo uhalali wake
utatokana na wananchi wenyewe inatazamiwa kutoa fursa kwa Wasomali kujenga
mustakabali mpya wa taifa lao.
29.
Mheshimiwa Spika, hali ya usalama katika mji wa Mogadishu sasa
ni ya kuridhisha kutokana na jitihada za majeshi ya AMISOM na yale ya Kenya
kudhibiti maeneo na miji muhimu iliyokuwa ngome ya Al-Shabaab.
Pamoja na kuwa wamedhibitiwa, Al-Shabaab wameendelea kufanya matukio machache
nchini Kenya ikiwa ni njia ya kulipiza kisasi. Hali hiyo imeleta hofu kwa
watalii na wageni kutoka nje wanaotembelea ukanda wa Afrika Mashariki. Serikali
zetu zinashirikiana kwa karibu katika kuimarisha usalama dhidi ya vitendo vya
uharamia vya Al-Shabaab. Vivyo hivyo, hali ya usalama katika pwani ya Bahari ya
Hindi na Ghuba ya Aden nayo inazidi kuimarika na matukio ya uharamia kupungua
kutokana na operesheni inayoendelea kati ya nchi za pwani ya Afrika Mashariki
kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya. Katika mwaka 2011/12 peke yake, Jeshi la
Wananchi liliweza kudhibiti matukio 27 ya uharamia. Tuungane kulipongeza jeshi
letu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kulinda mipaka ya nchi yetu. Tunachukua
jitihada za makusudi kulisaidia jeshi letu kupata vifaa madhubuti kwa ajili ya
ulinzi wa pwani yetu ambayo ina utajiri mkubwa wa gesi asilia dhidi ya
maharamia hawa.
Ukanda wa Maziwa Makuu
30.
Mheshimiwa Spika, hali
ya usalama mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Ukanda wa Maziwa
Makuu kwa ujumla nayo iko tete hata baada ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
ulimalizika na Rais Joseph Kabila kutangazwa mshindi dhidi ya mpinzani wake
mkuu Bw. Etienne Tshisekedi. Mapigano
yameripotiwa kutokea hivi karibuni tarehe 6 Julai, 2012 Kaskazini Mashariki mwa
DRC. Kikundi cha waasi kijulikanacho kama M23 kinachosemekana kinaongozwa na Jenerali
Bosco Ntaganda anayesakwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa tuhuma za uhalifu wa
kivita kujibu tuhuma mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC)
kinadaiwa kuhusika na mapigano hayo. Kikundi hicho kinasadikiwa kuyateka na
kuyadhibiti baadhi ya maeneo ya Mashariki ya DRC yakiwemo Rutshuru, Bunagana na
Kivu. Majeshi ya Umoja wa Mataifa yameingilia kati kwa kutoa ulinzi katika mji
wa Goma, na tarehe 25 Julai, 2012 yalilazimika kutumia silaha kuwasambaratisha
M23 kutoka kwenye maeneo wanayoyashikilia.
31.
Mheshimiwa Spika, Wakuu
wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, katika kikao chao tarehe 14 Julai, 2012
waliuomba Umoja wa Mataifa kuongeza wanajeshi wa kulinda amani kwa lengo la
kudhibiti usalama wa mpaka kati ya DRC na Rwanda ili kurejesha hali ya
kuaminiana baina ya nchi hizi mbili. Vilevile, walikubaliana kufufua mpango wa
usuluhishi uliokuwa chini ya Mheshimiwa Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Tanzania
na Mheshimiwa Olesegum Obasanjo, Rais Mstaafu wa Nigeria. Serikali ya Tanzania
inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya kisiasa na kiusalama nchini DRC kwa
kuwa machafuko hayo yanatuathiri kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiusalama. Ni
kutokana na hali hiyo, Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete anahudhuria
Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu utakaofanyika Kampala nchini
Uganda kesho tarehe 7 Agosti, 2012.
MASUALA YA USHIRIKIANO WA KIKANDA
32.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/2012, Wizara imetekeleza jukumu la
uratibu wa masuala ya ushirikiano wa kikanda kwa kuendelea kushiriki kikamilifu
katika shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Ushirikiano ya
Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (IOR-ARC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za
Kusini mwa Afrika (SADC). Kwa kuwa eneo la Jumuiya ya Afrika Mashariki
limeelezewa vizuri na Waziri husika kwenye hotuba ya bajeti yake, niruhusu
nidurusu masuala machache yafuatayo:
Uenyekiti wa Tanzania katika Kamati ya Utatu ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC
33.
Mheshimiwa Spika, mnamo mwezi Agosti, 2011 Tanzania iliteuliwa kuwa Makamu
Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC. Kutokana na uteuzi huo, Tanzania imeingia
katika Kamati hiyo ya Utatu (Troika) ambayo kwa sasa inaongozwa na nchi ya Afrika
Kusini. Ifikapo tarehe 17 Agosti, 2012 Tanzania itatwaa rasmi Uenyekiti wa Asasi hiyo muhimu ya SADC ambayo
itaipa jukumu la kusimamia, kufuatilia na kushiriki kwa kina katika masuala
yote ya siasa, ulinzi na usalama ya Nchi za SADC, hususan katika nchi za Madagascar
na Zimbabwe ambazo ziko kwenye agenda ya SADC Troika kwa sasa.
UTEKELEZAJI WA SERA YA DIPLOMASIA YA UCHUMI NA MPANGO WA MAENDELEO WA MIAKA MITANO 2011/2012 – 2015/2016
34.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kupata mgao kidogo sana wa bajeti
isiyokidhi mahitaji katika mwaka wa fedha 2011/2012. Katika kipindi tajwa,
Wizara yangu ilipata asilimia 44 tu ya Bajeti iliyoombwa. Bajeti ndogo tunayopewa imekuwa changamoto
kubwa katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi
kwa kiwango kinachostahiki. Hata hivyo, pamoja na mapungufu hayo, Wizara yangu
kwa nafasi yake kama kiungo muhimu cha nchi yetu na nchi za nje imeendelea kushirikiana
kwa karibu na Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na sekta
binafsi kuhakikisha kwamba nchi yetu inafaidika kwa kadri iwezekanavyo na fursa
mbalimbali zenye manufaa kwa nchi yetu katika sekta za uchumi na jamii. Juhudi
zetu katika kutafuta fursa hizo zilizingatia vipaumbele katika Mpango wa Taifa
wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/12 - 2015/16.
Niruhusu nitumie fursa hii kueleza kwa uchache mchango wa Wizara
yangu kwenye sekta mbalimbali katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango huo wa
Maendeleo wa Miaka Mitano.
Sekta ya Nishati na Madini
35.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta ya nishati, Wizara yangu
kupitia Ubalozi wetu nchini China imeshirikiana bega kwa bega na Wizara ya
Nishati na Madini pamoja na Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba nchi yetu
inapata mkopo wa Dola za Marekani bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa bomba la
kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es salaam. Kama ilivyokwishaelezwa
na Waziri wa Fedha hapa Bungeni, tayari mkataba wa kupata fedha hizo
umekwisainiwa na Mheshimiwa Philip Marmo, Balozi wetu nchini China kwa niaba ya
Serikali. Uzinduzi wa ujenzi wa Bomba hilo ulifanyika tarehe 21 Julai, 2012 Mkoani
Mtwara. Ujenzi wa bomba hilo utaleta mapinduzi makubwa sana katika uzalishaji
wa umeme kwa kutumia gesi. Bomba la zamani lilikuwa dogo na lisilokidhi
mahitaji ya kusafirisha kiasi kikubwa cha gesi kwenda Dar es Salaam. Pindi
ujenzi wa bomba hilo utakapokamilika fursa nyingi za uchumi zitafunguka na
kuimarika hasa zile zote zinazotumia gesi.
36.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu pia ilikuwa mstari wa mbele katika
kuishawishi Tume ya Uhifadhi Duniani (World Heritage Commission-WHC) na jumuiya
ya kimataifa kukubali kurekebisha mpaka wa Hifadhi ya Selous ili kuruhusu
uchimbaji wa madini ya urani kufanyika kusini mwa hifadhi hiyo. Juhudi
zetu zimezaa matunda ambapo mwezi Juni, 2012 WHC wameridhia hoja zetu, jambo
ambalo huwa si rahisi kufanywa na Tume hiyo. Ushindi huu ni kielelezo cha nguvu
ya ushawishi wetu na kuaminika kwetu duniani. Matarajio yetu ni kwamba Kampuni
ya Uranium One kutoka Urusi itaanza kazi ya utafiti na hatimaye uchimbaji muda
si mrefu mara baada ya kukamilisha taratibu zingine na Wizara husika za Maliasili
na Utalii na Wizara ya Nishati na Madini.
37.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua hofu za msingi juu ya usalama wa
uchimbaji wa madini hayo, Wizara yangu imetoa pia msukumo katika upatikanaji wa
wataalam na mafunzo na hivi karibuni Timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Nishati
na Madini imekwenda Nchini Australia na Namibia kujifunza namna ya kuendesha
miradi ya urani. Tanzania itatumia nafasi yake ya Ujumbe wa Bodi ya Shirika la
Atomiki Duniani (IAEA) kupata kila aina ya utaalamu na uzoefu kuhakikisha kuwa
uchimbaji wa madini hayo unafuata taratibu na viwango vya kiusalama
vinavyotolewa na IAEA.
38.
Mheshimiwa Spika, jitihada za Wizara yangu kuufufua mradi wa umeme wa
Stieglers Gorge nazo zinaanza kuzaa matumaini. Kufuatia jitihada za Wizara
yangu, Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu walifanya Ziara nchini Brazil
ambapo agenda ya mradi wa Stieglers Gorge
ilipewa kipaumbele kikuu. Kutokana na ziara hizo, Kampuni ya Brazil ya ODEBRECHT na Shirika la RUBADA kwa
upande wa Tanzania wameshasaini Makubaliano ya Awali (MoU) kwa ajili ya kuanza
kutekeleza mradi wa uzalishaji wa umeme ambao unakadiriwa utazalisha zaidi ya megawati
2,100 za umeme wa uhakika na wa bei nafuu. Wizara yangu itaendelea kufuatilia
ili kuhakikisha Wataalam wanaotakiwa kuja tena nchini kwa ajili kufanya mapitio
ya taarifa ya environmental impact
assessment (EIA) na upembuzi yakinifu wanafanya hivyo ili mradi huo uweze
kuanza mara moja.
Sekta ya Kilimo
39.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa
sekta ya kilimo, Wizara yangu imeshirikiana kwa karibu na Wizara ya Kilimo, Chakula
na Ushirika katika kufanikisha upatikanaji wa teknolojia ya umwagiliaji kutoka
nchini India chini ya makubaliano ya Mpango wa Maendeleo wa India-Afrika. Makubaliano
mahsusi haya ya ushirikiano baina ya nchi zetu mbili yanayotokana na ziara ya
Rais wa India hapa nchini mapema mwezi Februari 2012. Vilevile, Wizara yangu
ilishiriki na kushuhudia utiaji saini wa Makubaliano ya Awali kati ya Serikali
ya Tanzania na Kampuni ya Jain Irrigation
ya India mbele ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ajili ya kutekeleza kwa pamoja
miradi ya umwagiliaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa. Wizara yangu pia imeendelea
kuishawishi Serikali ya India kutupatia mkopo kwa ajili ya awamu ya pili ya
mradi wa Matrekta. Matumaini yetu ni kwamba juhudi hizo zitazaa matunda katika
mwaka huu wa fedha.
40.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeshiriki katika kufanikisha ushiriki
wa nchi yetu katika Mkutano wa nchi Tajiri na zenye Viwanda vikubwa
duniani zinazojulikana kama G8 uliyofanyika nchini Marekani. Mkutano huo ulikuwa
na mafanikio makubwa kwa sekta ya kilimo nchini baada ya mataifa hayo kutoa
ahadi ya Dola za Marekani milioni 890.
Aidha, makampuni binafsi ya nchi hizo yaliahidi kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani
bilioni 3 katika sekta ya kilimo.
Katika mwaka huu wa fedha, Wizara yangu itaelekeza nguvu zake kuvutia
wawekezaji kutoka nchi za Japan, Korea Kusini na China kuwekeza katika Ukanda
wa Kusini wa SAGCOT na vilevile kuanzisha kanda nyinginezo za kilimo magharibi,
kaskazini na mashariki mwa nchi yetu.
Sekta ya Miundombinu
41.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sekta ya Miundombinu, Wizara yangu
imeendelea kushirikiana na Wizara ya Ujenzi katika kutafuta misaada na mikopo
kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu. Katika mwaka wa fedha 2011/2012, Wizara
yangu kupitia Ubalozi wetu Japan, iliweza kuishawishi Serikali ya Japan kugharamia
upanuzi wa barabara ya Gerezani na Mwenge-Morocco. Hivi sasa tunaendelea
na juhudi za kuwashawishi ndugu zetu wa Japan watusaidie kujenga barabara za
juu (Flyovers) maeneo ya Tazara. Wameonesha utayari wao kutusaidia. Vilevile,
Wizara yangu inaendelea kushirikiana na Wizara ya Ujenzi kupata wawekezaji wa
ujenzi wa barabara ya njia sita ya kutoka Ubungo hadi Chalinze chini ya mpango
wa ushirikiano wa sekta binafsi na sekta ya umma (PPP). Matumaini yetu ni
kwamba ujenzi wa barabara hizi utasaidia kupunguza tatizo sugu la msongamano wa
magari jijini, Dar es Salaam na yale yanayokwenda mikoani na nje ya nchi
na hatimaye kupunguza madhara ya kiuchumi yatokanayo na msongamano mkubwa wa
magari.
Sekta ya Maji
42.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta ya maji, Wizara yangu kwa
kushirikiana na Wizara ya Maji na Wizara ya Fedha tumeweza kuishawishi Serikali
ya India kutupatia mkopo wa Dola za Marekani milioni 178.25 kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji katika miji
ya Dar es salaam na Pwani. Hivi sasa mchakato wa kupata fedha hizo umefikia hatua
za mwisho na bila shaka inatarajiwa mapema mwezi ujao Mkataba utasainiwa na
utekelezaji wa mradi huo kuanza. Vilevile, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara
ya Fedha, Ujenzi, Nishati na Maji za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanikisha
upatikanaji wa mkopo wa masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 50 kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Uchumi ya Korea kwa ajili
ya mradi wa kilimo cha umwagiliaji Zanzibar.
Sekta ya Viwanda
43.
Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea na juhudi za kuchangia katika sekta ya ukuaji wa viwanda. Kilicho
dhahiri ni kuwa, kwa hali ya uchumi wetu kwa sasa, viwanda vinavyohitajika
haraka ni vile vya msingi ambavyo vinatumia rasilimali za ndani, vinaongeza
thamani na vinatoa ajira nyingi. Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba
katika mwaka huu wa fedha tutapata wawekezaji wa viwanda vya kutengeneza nyuzi
za nguo kutoka Japan na China. Uwekezaji huu mkubwa sio tu utatengeneza ajira
kwa wananchi wengi, bali pia utawahakikishia wakulima wetu wa pamba soko la
uhakika kwani viwanda vyote hivi vikianza kufanya kazi, vitahitaji kiasi cha
tani laki mbili za pamba. Hivi sasa nchi yetu inazalisha tani laki moja tu.
Hivyo basi, ipo fursa kwa nchi yetu kuzalisha pamba kwa wingi zaidi kutokana na
kuwepo kwa soko la uhakika nchini. Aidha, uko uwezekano mkubwa kwa Serikali ya
Marekani kuendelea na Mpango wake wa AGOA ambapo bidhaa za nguo kutoka Afrika
ikiwemo Tanzania, zitaendelea kupewa upendeleo maalum.
Sekta ya Ajira
44.
Mheshimiwa
Spika, katika
kuwatafutia ajira Watanzania nje, Wizara ikishirikiana na
mamlaka husika za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imekamilisha mchakato wa makubaliano ya kusaini mkataba wa ajira na
nchi ya Qatar. Kwa sasa, Wizara yangu inatarajia kupokea ujumbe kutoka Qatar
kuja hapa nchini kusaini mkataba huo ili Watanzania waweze kuchangamkia fursa
hizo nyingi za ajira wakati Qatar ikijiandaa kuandaa Kombe la Dunia la mwaka
2022. Halikadhalika, jitihada za Wizara yangu katika kuvutia misaada na
uwekezaji katika sekta za miundominu, zimechangia kuchochea uzalishaji wa ajira
nyingi nchini. Tunatambua changamoto ya ajira bado ni kubwa lakini tunaendelea na
jitihada hizi kwa kushirikiana na Sekta nyingine kadiri uwezo wetu wa kibajeti
utakavyoruhusu.
Sekta ya Elimu
45.
Mheshimiwa Spika, mbali na
kuendelea kutafuta fursa za mafunzo nje ya nchi, Wizara yangu kwa kushirikiana
na Bunge lako Tukufu ilisimama kidete kupigania urejeshwaji wa fedha za ziada
kiasi cha pauni za Uingereza milioni
29.5, zilizojumuisha kiasi tulicholanguliwa na kile kilichotolewa mlungula
wakati wa ununuzi wa rada kutoka kampuni ya Kiingereza inayojihusisha na uuzaji
wa silaha (BAE). Kama nilivyoahidi katika Bunge lako wakati wa kuwasilisha
Kauli ya Serikali na baadae wakati nikiwasilisha Bajeti ya Wizara yangu kwa
mwaka 2011/2012, fedha hizo zote zimerejeshwa Serikalini na sio kwenye Asasi za
Kijamii. Kwa pamoja, jitihada zetu zimewezesha kuipatia sekta ya elimu shilingi
bilioni 90 kama ambavyo Bunge hili
limejulishwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu.
46.
Mheshimiwa Spika, sitakuwa nimetenda haki nisipomshukuru kwa dhati
Mheshimiwa Rais kwa msimamo wake thabiti na Mheshimiwa Spika kwa kuiunga mkono
Serikali na kuteua Kamati ya Wabunge ambayo imefanya kazi ya kutukuka
kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa Serikalini. Naomba nitambue mchango mahsusi
wa Waheshimiwa Wabunge wote. Aidha, niwashukuru pia Mhe. Balozi Peter Kalaghe,
timu yake na watumishi wa Wizara waliosimama kidete pamoja nasi kwenye suala
hili lenye maslahi kwa taifa. Nimejifunza kuwa imo ndani yetu nguvu kubwa ya
umoja pale tunapoweka kando maslahi yetu finyu ya vyama na itikadi na kusimamia
maslahi mapana ya Taifa. Hii ndio Tanzania ninayoijua na kujivunia, Tanzania
yenye umoja na Tanzania yenye kuthubutu. Tumeonesha uzalendo wa hali ya juu kwa
nchi yetu na historia itatupa tuzo njema na kulikumbuka Bunge hili kwa kazi
hiyo nzuri.
MASUALA MTAMBUKA YALIYOTEKELEZWA NA WIZARA
Mradi wa Kiswahili kwenye Umoja wa Afrika
47.
Mheshimiwa Spika, lugha ya
Kiswahili imekuwa ikitumika tangu mwaka 2004 katika shughuli za Umoja wa Afrika
na Serikali yetu imekuwa ikigharamia wakalimani wa Kiswahili hadi mwaka 2008
ambapo Kamisheni ya Umoja wa Afrika ilichukua jukumu hilo. Serikali yetu
inaendelea kushawishi nchi wanachama walau thelathini na sita ambayo ni
theluthi mbili kuridhia Itifaki ya Marekebisho ya Mkataba wa Kuanzisha Umoja wa
Afrika (Protocol on the Amendments to the Constitutive Act of the African
Union). Kuanza kutumika kwa Itifaki hiyo
kutawezesha lugha ya Kiswahili kutumika katika shughuli za kila siku za Umoja
wa Afrika.
48.
Mheshimiwa Spika, sambamba na
juhudi hizo, mwezi Januari, 2012 Umoja wa Afrika umeanza kufundisha lugha ya
Kiswahili katika Kituo cha kufundishia Lugha cha Kamisheni ya Umoja wa Afrika.
Tayari wamekwishajisajili wanafunzi 15 chini ya Wakufunzi wawili wa kujitolea kutoka
Tanzania. Naomba nitambue mchango wao wa dhati na kuwapongeza kwa uzalendo wao.
Mimi binafsi nilipata fursa ya kuwatembelea na kuwatia moyo mwezi Januari, 2012
wakati nikihudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Umoja wa Afrika mjini
Addis Ababa. Changamoto kubwa inayotukabili ni upatikanaji wa fedha za
kuendesha Kituo hicho na walimu wa kutosha wa kufundisha. Mpango wa Serikali ni
kutafuta fedha kwa ajili ya kuanzisha Kituo cha Utamaduni cha Kitanzania jijini
Addis Ababa kwa lengo la kukuza utamaduni wetu na Lugha ya Kiswahili miongoni
mwa jamii ya Wanadiplomasia na Watumishi wa Umoja wa Afrika. Tukifanikiwa
katika hili tutakuwa tumetengeneza fursa za ajira kwa Wakufunzi wa Kiswahili
pamoja na kupanua wigo wa fursa kwa Watanzania kufanya kazi katika Taasisi za
Umoja wa Afrika.
Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC)
49.
Mheshimiwa Spika, napenda
kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa ujenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha
Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, umekamilika kwa Asilimia 95 na
tunategemea kukabidhiwa mwezi Septemba 2012. Kituo hiki cha kisasa kinaweza
kuhodhi Mikutano minne kwa mara moja, yenye idadi ya watu 1,600. Kituo hiki
kitakuwa na huduma nyingine muhimu kama vile huduma za benki, afya, ukalimani
na migahawa. Kituo kimejengwa kwa msaada
wa Serikali ya Jamhuri wa Watu wa China. Sanjari na Kituo hiki, pia Serikali
hiyo imetoa msaada wa magari madogo na mabasi yapatayo 75 ambayo tayari yapo
nchini kwa ajili ya kutoa huduma katika Kituo hicho. Kuanza kufanya kazi kwa
Kituo hicho, kutachochea ajira nyingi zaidi za moja kwa moja na nyingine
zinatarajiwa kutengenezwa katika sekta za huduma.
Kusimamia Mikataba na Makubaliano ya Kimataifa
50.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia
wajibu huu, Wizara imeshiriki kwenye majadiliano mbalimbali yaliyopelekea
uwekaji saini Makubaliano ya Mikataba mbalimbali katika kipindi cha mwaka 2011/2012
kama ifuatavyo:
1.
Mkataba wa mpaka wa Bahari kati ya Tanzania na
Comoro, ambao uliosainiwa tarehe 05 Desemba, 2011 jijini Maputo – Msumbiji.
Mkataba huu utahakikisha kuimarika kwa usalama wa mpaka wa Bahari baina ya nchi
hizi mbili;
2.
Mkataba wa mpaka wa Bahari kati ya Tanzania na
Msumbiji ambao ulisainiwa tarehe 05 Desemba, 2011 jijini Maputo –
Msumbiji. Kama ilivyo kwa Mkataba baina
ya Tanzania na Visiwa vya Comoro, Mkataba huu utahakikisha usalama wa mpaka wa
bahari baina ya nchi hizi mbili unaimarika;
3.
Muhtasari wa Makubaliano ya Mkutano wa Pili juu ya
Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari (EEZ) kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Serikali ya Visiwa vya Comoro
na Serikali ya Ushelisheli, uliosainiwa tarehe 07 Septemba, 2011 huko
Port Louis, Mauritius. Utekelezaji wa makubaliano haya ni muhimu ili kuwezesha
nchi zote husika kunufaika na ukanda wa kiuchumi wa Bahari ya Hindi;
4.
Makubaliano kati ya Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano cha Arusha (AICC) na Beijing
Construction Engineering Group Co. Ltd (BCEG) kuhusu ujenzi wa Mount Kilimanjaro International Convention
Centre ambayo yalisainiwa mwezi Agosti, 2011 mjini Arusha. Mkataba huu
unatoa fursa ya kujengwa kwa Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Jijini Arusha ambao utaiingizia Serikali mapato na
pia kuendelea kuitangaza Arusha na Tanzania kwa ujumla kupitia Diplomasia ya
Mikutano; na mwisho
5.
Makubaliano ya Pamoja (MoU) kati ya Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na China
Petroleum Technology and Development Corporation (CPTDC) mwezi Machi, 2012
kufuatia ziara ya Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa
Li Jinzao hapa nchini ili kuendeleza eneo hilo.
Mradi wa kuongeza Eneo la Bahari Nje ya Ukanda wa Kiuchumi (Exclusive Economic Zone - EEZ)
51.
Mheshimiwa Spika, Wizara
yangu kupitia Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa - New York,
imekuwa ikiratibu na kushiriki katika utekelezaji wa Mradi wa kuongeza eneo la
Tanzania la Bahari nje ya Ukanda wa Kiuchumi. Wizara ikishirikiana na Kamati
ilioundwa kushughulikia suala hilo, imeendelea kufanya mawasiliano na Taasisi
za Umoja wa Mataifa zenye jukumu la kupitia Maandiko ya Miradi kama hii ya nchi
zote zilizofanikiwa kuongeza eneo la Bahari. Andiko la Mradi la Tanzania
liliwasilishwa Umoja wa Mataifa mwezi Januari, 2012 na Mheshimiwa Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Aidha, mwezi Agosti, 2012 Timu ya
wataalamu inatarajiwa kwenda kutetea Andiko hilo mbele ya “Commission on the Limits of the Continental Shelf” (CLCS),
inayoendelea na mkutano wake ulioanza tarehe 30 Julai, 2012 na unaotarajiwa
kumalizika tarehe 10 Agosti, 2012 huko New York. Wizara imeendelea kushiriki
katika maandalizi ili kufanikisha utetezi unaotarajiwa.
Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano
52.
Mheshimiwa Spika, Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano (JPCs) ni
nyenzo muhimu sana katika ufanikishaji wa utekelezaji wa diplomasia ya uchumi. Ni katika Tume hizi
mikataba ya msingi husainiwa ambayo huweka mazingira kwa sekta binafsi kuweza
kupata unafuu na fursa katika nchi ambazo tuna Mikataba nazo. Kwa mfano, soko
la tumbaku nchini China ni kubwa zaidi kuliko lile la Marekani lakini wakulima
wa Tanzania wanashindwa kupenya katika soko hilo kutokana na kukosekana kwa
mikataba ya aina hii baina ya nchi zetu mbili. Kutokana na ufinyu wa bajeti,
tumeshindwa kutumia nyenzo hii vizuri kufungua na kufufua fursa za ushirikiano.
Kwa kutambua umuhimu huo na kuzingatia ufinyu wa bajeti uliopo, tumedhamiria
katika mwaka wa fedha 2012/2013 kufanya mikutano ya JPC walau na nchi tatu kwa
kuzingatia vipaumbele vya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/2012
- 2015/2016.
53.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa,
asili ya miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa katika sekta nyingi
nchini kwa kushirikiana na washirika wetu wa maendeleo inatokana na Tume za
Pamoja za Kudumu za Ushirikiano. Katika mwaka wa fedha 2011/2012 Wizara
ilifanikisha makubaliano kuhusu uanzishwaji wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya
Ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya
Jamhuri ya Afrika Kusini. Makubaliano hayo yalifikiwa mwezi Julai, 2011 jijini Pretoria – Afrika Kusini. Lengo la
Makubaliano haya ni kuzidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi
hizi mbili katika nyanja mbalimbali hasa za uchumi.
54.
Mheshimiwa Spika, haya niliyoyataja ni maeneo machache tu ambayo
Wizara yangu imeyafanya katika kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa
Maendeleo wa Miaka Mitano katika sekta za uchumi. Yako mengine mengi ambayo
tumewezesha kufanyika katika kila sekta nchini lakini kwa ufinyu wa muda siwezi
kuyasema yote kwa muda nilionao. Itoshe
tu kuongelea haya machache kwa leo. Ninaliahidi Bunge lako Tukufu kwamba
tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa
Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ya kwanza. Zipo fursa nyingi za ushirikiano
huko nje ya nchi ambazo nchi yetu inaweza kunufaika nazo. Tumejidhatiti
kunufaika na fursa zitokanazo na China-Afrika Forum (FOCAC), TICAD V,
EU-Africa, EBA, AGOA, Turkey-Africa, SADC, NEPAD, Tume za Kudumu za Ushirikiano
baina ya nchi yetu na mataifa mengine.
Tunachohitaji ni kuwezeshwa zaidi ili tufanye kazi hiyo kwa ufanisi
zaidi.
NAFASI YA TANZANIA KATIKA JUMUIYA ZA KIMATAIFA NA KIKANDA
55.
Mheshimiwa Spika,
bendera ya Tanzania
imeendelea kupepea vyema katika medani za Kimataifa kutokana na uongozi mahiri wa Waasisi wa
Taifa hili na uongozi uliopo kufuatia kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na inayoendelea
kufanywa na Watanzania katika Mashirika ya Kimataifa na Kikanda. Wizara yangu imeendelea kufanya jitihada za
makusudi kuhakikisha Watanzania wengi wanajiunga na kufanya kazi kwenye
Mashirika ya Kimataifa. Aidha, Tanzania imeendelea pia kugombania na kuchukuwa
nafasi za uongozi kwenye mashirika mbalimbali ya Kimataifa.
56.
Mheshimiwa
Spika, wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Jumuiya ya Madola (CHOGM) uliofanyika Perth, Australia mwezi Oktoba 2011.
Tanzania ilichaguliwa kuingia kwenye Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Mambo ya Nje
wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth Ministerial Action Group - CMAG) kwa kipindi
cha kuanzia mwaka 2011 hadi 2013. CMAG ndiyo chombo chenye jukumu la kusimamia
misingi, sheria, kanuni na taratibu za Jumuiya ya Madola. Kikundi Kazi hicho
kinaundwa na jumla ya nchi tisa kati ya
nchi 54 za Jumuiya hiyo. Kuchaguliwa kwa Tanzania kuingia kwenye Kikundi Kazi
hicho kumezidi kudhihirisha imani ya Jumuiya ya Kimataifa kwa nchi yetu. Mbali
na kuleta sifa kubwa kwa Taifa letu, nafasi hii inaipa
nchi yetu nguvu kubwa ya ushawishi ndani ya Jumuiya ya Madola na pia nafasi ya
kuingiza na kusimamia maslahi yake kwenye Jumuiya hiyo.
57.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kumpongeza Dkt. Agness L. Kijazi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza
Kuu la Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuanzia mwezi Juni, 2012 hadi
mwaka 2015. Nafasi hii ni muhimu kwani kati ya nchi 189 ambazo ni wanachama wa
Shirika la Hali ya Hewa Duniani, nchi 37 tu ndio wanaingia kwenye Baraza Kuu la
Shirika hilo. Dkt. Kijazi anakuwa ni mwanamke wa kwanza kutoka Afrika Mashariki
kuteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Shirika hilo.
58.
Mheshimiwa
Spika,
Tanzania kupitia raia wake Prof. Chris Maina Peter, ilichaguliwa kwa kishindo
kuwa Mjumbe kwa kipindi cha miaka mitano kwenye Kamisheni ya Sheria za
Kimataifa ya Umoja wa Mataifa katika uchaguzi wa wajumbe wa Kamisheni hiyo
uliofanyika mwezi Novemba, 2011 Mjini New York, Marekani. Prof. Maina ni
Mtanzania wa pili kuiwakilisha Tanzania kwenye Kamisheni hiyo, baada ya Mheshimiwa
Balozi James L. Kateka ambaye alikuwa Mjumbe kwenye Kamisheni hiyo kwa vipindi
viwili vya miaka mitano mitano (1997 - 2006). Balozi Kateka sasa ni Jaji katika
Mahakama ya Kimataifa ya Sheria za Bahari.
59.
Mheshimiwa
Spika, Majaji wawili Watanzania
– Jaji William Hussein Sekule na
Jaji Joseph E. Chiondo Masanche nao walichaguliwa kuwa Majaji wa Mahakama
inayorithi shughuli za iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya
Rwanda (ICTR) katika uchaguzi uliofanyika New York, Marekani mwezi Desemba
2011.
60.
Mheshimiwa
Spika,
kupitia azimio namba 66/408 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la mwezi Novemba,
2011 lilimthibitisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa
Tanzania, Bw. Ludovic Utouh pamoja na Ofisi yake kuwa kwenye Bodi ya Wakaguzi
ya Umoja wa Mataifa kuanzia Julai, 2012 kwa kipindi cha miaka sita. Mafanikio
haya yanatokana na umakini wa Wizara yangu kwa kufanya kampeni za uhakika hadi
kufanikisha kuchaguliwa.
61.
Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi
Septemba, 2011 Tanzania imekuwa mjumbe katika Bodi ya Magavana ya Shirika la
Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) kwa kipindi cha 2011/2012. Kuwemo kwenye Bodi hiyo, kunaipa nchi fursa ya kushiriki
kwenye masuala nyeti na muhimu kama vile kwenye majadiliano kuhusu mipango ya
nyuklia ya baadhi ya nchi. Bodi hiyo ina jukumu la kutathmini maombi ya nchi
zinazoomba uanachama na kuthibitisha viwango vya usalama. Aidha, Bodi ndiyo
inayomteua Mkurugenzi Mkuu wa IAEA ambaye huthibitishwa na Mkutano Mkuu wa
IAEA. Hii ni fursa nzuri kwa nchi yetu hasa ikizingatiwa kwamba Tanzania inayo
malighafi ya urani.
62.
Mheshimiwa
Spika, niruhusu nilitaarifu rasmi Bunge lako Tukufu kwamba Mtanzania mwenzetu,
Dkt. Asha-Rose Migiro, amemaliza kipindi chake kama Naibu Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa. Kwa hakika Dkt. Migiro
amefanya kazi nzuri na kubwa iliyotukuka katika Umoja wa Mataifa. Ameiletea
sifa nchi yetu na Bara la Afrika kwa ujumla kutokana na kumsaidia Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban ki Moon. Kwa niaba ya Watanzania wote,
ninamshukuru kwa kutuwakilisha vizuri na ninampongeza sana na kumkaribisha tena
nyumbani ili aendelee kushirikiana na wananchi wenzake katika ujenzi wa Taifa
letu. Aidha, napenda pia, kupitia Bunge lako Tukufu kumpongeza Dkt. Migiro kwa
kuteuliwa tena kuwa Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya
Ugonjwa wa UKIMWI Barani Afrika.
63.
Mheshimiwa
Spika, vile vile, nchi
yetu ilijipatia sifa kutokana na kazi nzuri aliyoifanya Mheshimiwa Balozi
Liberata Mulamula akiwa Katibu Mtendaji wa kwanza wa Jumuiya ya Nchi Wanachama
wa Ukanda wa Maziwa Mkuu. Balozi Mulamula aliratibu, aliisimamia na kuongoza
Jumuiya hiyo kwa mafanikio makubwa pamoja na changamoto nyingi zilizokuwepo
katika Ukanda wa Maziwa Makuu. Kutokana na kazi yake nzuri, ndio maana
Mheshimiwa Rais amemteua sasa kuwa Msaidizi wake Mwandamizi wa Masuala ya
Kidiplomasia.
MSIMAMO WA TANZANIA KATIKA MASUALA MBALIMBALI
64.
Mheshimiwa
Spika,
tumekuwa tukishuhudia mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii
duniani kote ambayo wakati mwingine yanahitaji nchi kuonesha msimamo wake kwa
baadhi ya masuala hayo. Moja ya sifa kubwa ambayo Mwasisi wa Taifa hili Hayati
Mwalimu Nyerere aliyotuachia ni kuweka misimamo kwenye misingi tunayoiamini
kama Taifa. Kutokana na hali hiyo, Tanzania
kama nchi huru imeweza kuwa na misimamo yake kuhusiana na masuala hayo kama
yanavyoelezewa hapa chini.
Suala la Mpaka Kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa
65.
Mheshimiwa Spika, lipo tatizo la
muda mrefu kati yetu na nchi jirani ya Malawi linalohusiana na mpaka kwenye
Ziwa Nyasa. Tatizo lenyewe ni kwamba
Malawi wanadai kuwa Ziwa lote Kaskazini ya Msumbiji kuelekea Ruvuma na Mbeya ni
mali yao kwa mujibu wa Mkataba wa Heligoland uliowekwa saini tarehe 1 Julai 1890.
66.
Mheshimiwa Spika, Tanzania kwa
upande wetu tunasema kuwa mpaka wa kweli kati yetu na Malawi unapita katikati
ya Ziwa hivyo kufanya eneo lote la kaskazini mashariki ya Ziwa kati ya Latitude
digree 9° na digree 11° kuwa mali ya Tanzania kwa mujibu wa Mkataba huo huo wa
Heligoland (Ango-German Agreement) wa mwaka 1890 ambao ulikubali kuwa kwa vile
kuna maeneo ya mpaka ambayo hayana mantiki, pande zinazohusika zikutane na
kurekebisha kwa kuunda “Border Commissions”.
Aidha, tunazo ramani ambazo Waingereza wenyewe (ambao wakati huo
walikuwa wakitawala Nyasaland na Tanganyika) walikubaliana kurekebisha na hivyo
kusogeza mpaka katikati kama ulivyo mpaka kati ya Malawi na Msumbiji.
67.
Mheshimiwa Spika, kutokana na
tatizo hili, mwaka 2005 Marehemu Rais Bingu wa Mutharika, alimwandikia Rais wa
awamu ya tatu Mheshimiwa Mkapa akimtaka waunde Kamati ya kuliangalia tatizo
hilo na kulipatia ufumbuzi. Awamu ya Nne
ikaendeleza kwa kuunda Kamati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje kuliangalia tatizo na
kulitolea mapendekezo. Kama zilivyokutana
mwaka 2010, mwaka 2012 zilikutana tena ili kuendeleza mazungumzo ya mwaka 2010
na pia kujadili matukio ya kuonekana kwa ndege ndogo ndogo za utafiti wa mafuta
na gesi kwenye Ziwa Nyasa zikitafiti hadi pwani ya Ziwa hilo upande wa
Tanzania.
68.
Mheshimiwa Spika, baada ya
majadiliano makubwa kati yetu na Malawi, Serikali yetu iliwataka wenzetu wa
Serikali ya Malawi pamoja na kampuni za utafiti au uchimbaji kusitisha mara
moja shughuli zote za utafiti hadi majadiliano yatakapokamilika. Ni matumaini yetu kuwa wenzetu wa Malawi
wametuelewa. Hata hivyo, kuna uwezekano
mkubwa wa mgogoro huu mbele ya safari kutatuliwa na Msuluhishi badala ya sisi
wenyewe.
69.
Mheshimiwa Spika, sehemu ya pili
ya mgogoro bado iko mezani kwa majadiliano. Kufuatia maelekezo ya Marais wa pande mbili, Mawaziri wa Mambo ya Nje na
wataalamu wetu wa masuala ya mipaka, ulinzi na usalama tulikutana Dar es Salaam
tarehe 27 Julai, 2012 kujadili kwa kina
mgogoro na kuupatia suluhu ya kudumu. Majadiliano yanaendelea vizuri na tumekubaliana
kuwa wakati tukiendelea na mazungumzo, nchi zote zijiepushe na shughuli zozote
kwenye Ziwa Nyasa ambazo zinaweza kutafsiriwa kuathiri maslahi ya nchi
mojawapo. Kwa makubaliano haya, naomba niwatoe hofu wananchi wa mikoa ya Mbeya
na Ruvuma kuhusu hali ya usalama mpakani mwa nchi yetu na Malawi. Chini ya
uongozi wa Serikali ya CCM, wananchi wa Tanzania daima watakuwa salama dhidi ya
tishio lolote la dhahiri au la kificho la kiusalama. Tumefanya hivyo tokea
uhuru na hatutachelea kufanya vinginevyo wakati wote tukiwa madarakani. Hili
limeelezewa katika Ibara ya Nane, aya ya 191 na 192 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM
ya mwaka 2010 - 2015.
Mgogoro wa Morocco na Sahara Magharibi
70.
Mheshimiwa Spika, Tanzania ina uhusiano mkubwa na wa kihistoria na
Jamhuri ya Sahara Magharibi. Itakumbukwa
kuwa nchi ya Sahara Magharibi inapakana na Morocco, Mauritania na Algeria
ilikuwa ni koloni la Hispania. Wakoloni
hao waliondoka Sahara Magharibi mwaka 1975 na wakati wananchi wanajiandaa
kujitawala, ghafla nchi yao ikavamiwa na nchi jirani za Mauritania na Morocco.
Mauritania iliondoka na Morocco ikaendelea kuikalia Sahara Magharibi tangu wakati
huo yaani 1975 hadi sasa. Wananchi wa Sahara Magharibi walianza kazi upya ya
kudai uhuru wao kutoka kwa jirani yao na Mwanachama wa OAU, Morocco. Mwaka 1976
Umoja wa Afrika uliamua kuitambua Sahara Magharibi kama mwanachama wa OAU. Morocco ikajitoa kwenye Umoja huo. Kwa kuwa Tanzania ilikuwa ndiyo Makao Makuu
ya vyama vya Ukombozi Barani Afrika, kuanzia mwaka 1963, ukombozi wa Sahara
Magharibi ulikuwa ni moja ya agenda yetu kuanzia wakati huo hadi sasa.
71.
Mheshimiwa Spika, msimamo wa
Tanzania kuhusu Sahara ya Magharibi, haujabadilika na upo pale pale. Tunataka wananchi wa Sahara Magharibi waachwe
waamue kupitia kura ya maoni (referundum) iwapo wanataka kujitawala
(independence) wenyewe au wanataka kuwa chini ya Himaya ya utawala wa Morocco. Huo pia ndio msimamo wa AU na Umoja wa
Mataifa tangu mwaka 1992. Serikali ya
Morocco imekataa kura ya maoni (referendum) na badala yake wanataka Sahara
Magharibi iwe sehemu ya Himaya ya Morocco.
Wamekataa kwa sababu wanajua kuwa wakikubali kura ya maoni kufanyika,
wananchi wa Sahara Magharibi watataka kujitawala.
72.
Mheshimiwa Spika, Tanzania inauomba Umoja wa Mataifa kuendelea na
jitihada zake za usuluhishi na tunaitaka Serikali ya Morocco kubadilika. Tupo tayari kuwa na mahusiano na Morocco bila
ya kuathiri msimamo wetu na Sahara Magharibi.
Tunafanya hivyo kwa Israel na Palestina.
Ziara za Viongozi
73.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kuratibu ziara za Viongozi
wa Kitaifa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar nje ya nchi. Ziara hizo zimekuwa na mafanikio na faida
kubwa kwa nchi yetu, hasa
katika kulinda na kuendeleza maslahi ya kitaifa ya kiuchumi na kijamii, kukuza
mahusiano ya kidiplomasia na nchi mbali mbali, Mashirika ya Kimataifa na
Kikanda, Kampuni za Kimataifa na hata watu binafsi.
74.
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kwamba ziara hizo zinaendelea kuwa
na tija pamoja na kupunguza gharama katika mazingira ya kiuchumi tuliyonayo,
kama alivyoelekeza Mheshimiwa Rais, Wizara yangu imeanza kuchukua hatua mbalimbali kupunguza utegemezi
wa ziara hizo pekee katika kupata mafanikio mbalimbali, hususan ya kiuchumi.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni:
1.
Kupunguza ukubwa wa ujumbe katika misafara ya
Viongozi Wakuu;
2.
Kuwatumia Wawakilishi, hususan Mawaziri katika
safari mbalimbali hatua ambayo inapunguza gharama kwani anaposafiri Waziri
huongozana na wajumbe wachache sana;
3.
Kuelekeza nguvu katika kuziimarisha Balozi zetu
ikiwa ni pamoja na kufungua Balozi Ndogo katika maeneo yenye maslahi ya
kiuchumi kwa Taifa; na
4.
Kutoa kipaumbele katika kufungua Ofisi za
Wawakilishi wa Heshima katika maeneo muhimu
ambayo Tanzania haina Uwakilishi.
75.
Mheshimiwa Spika, katika kudumisha mahusiano na nchi nyingine, nchi
yetu imeendelea kutembelewa na wageni mbalimbali katika ngazi ya Wakuu wa Nchi
na Serikali, Mawaziri na Viongozi wengine wa Kimataifa. Katika diplomasia,
kutembelewa na wageni ni daraja muhimu la kukuza mahusiano na pia ni kielelezo
cha sera za nchi yako kukubalika na Mataifa mengine yakiwemo Mashirika ya Kimataifa.
76.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
wa fedha uliopita wa 2011/2012 tulitembelewa na Marais kutoka Ivory Coast,
Somalia, Uganda, Liberia na Malawi. Vilevile, tulitembelewa na Makamu wa Rais
kutoka Burundi, Kenya, Zambia, Iran na Afrika ya Kusini. Wageni wengine
mashuhuri waliotembelea nchini ni pamoja na Prince Charles wa Uingereza na
mkewe Duchess of Cornwall Camilla Parker, Mwana wa Mfalme wa Saudi Arabia na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt.
Donald Kaberuka na wengineo.
77.
Mheshimiwa Spika, Tanzania imepokea idadi kubwa ya mawaziri kutoka
nchi mbalimbali duniani kama vile China, Uingereza, Japan, Sweden, Finland,
Afrika ya Kusini, Korea ya Kusini, Korea ya Kaskazini, Marekani na Umoja wa
Falme za Kiarabu. Wizara
inaendelea kutekeleza mwongozo unaowataka viongozi wanaofanya ziara nchini
Tanzania pia kutembelea Zanzibar.
78.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka fedha wa 2011/2012, Viongozi
wafuatao walitembelea Zanzibar: Mwana wa Malkia wa
Uingereza, Prince Charles na Mkewe Camilla; Mfalme wa Ashanti wa Ghana; Waziri
wa Uingereza wa Maendeleo ya Afrika; Waziri wa Finland wa Maendeleo ya Afrika; Waziri
wa Afya wa Finland; Waziri wa Afya wa Marekani; na Waziri wa Afya wa Norway.
CHANGAMOTO MBALIMBALI ZINAZOIKABILI WIZARA NA HATUA ZILIZOCHUKULIWA
79.
Mheshimiwa Spika, kama ilivyo kwa Wizara, Idara na Taasisi nyingine
za Serikali, Wizara yangu imekumbwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji
wa majukumu yake, hususan kwa mwaka wa fedha 2011/2012. Changamoto hizo kwa
kiasi kikubwa zinasababishwa na kuendelea kupungua kwa bajeti ya Wizara kila
mwaka. Aidha, kuendelea kushuka kwa
thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Marekani
ambayo hutumiwa na Balozi zetu nje nako kunasababisha bajeti kuendelea
kutokukidhi mahitaji. Ufinyu wa bajeti umesababisha Wizara na Balozi zetu kushindwa
kutekeleza kwa vitendo diplomasia ya uchumi. Kuendelea kupewa bajeti ndogo
kumesababisha, pamoja na matatizo mengine, madeni makubwa, wafanyakazi
kutolipwa stahili zao na uchakavu wa magari na majengo. Aidha, ufinyu wa bajeti
umechangia kwa kiasi kikubwa kwa Wizara kushindwa kuwarejesha nyumbani
watumishi waliomaliza muda wao Balozini na kuwapeleka wengine kutoka Makao Makuu.
Kama nilivyosema hapo awali, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi
na Usalam (NUU) imetembelea Balozi zetu mbalimbali na kujionea hali halisi.
Ninaamini Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati hiyo watakuwa wasemaji wazuri wa
matatizo yanayozikabili Balozi zetu kutokana na ufinyu wa bajeti.
80.
Mheshimiwa Spika, katika
kuhakikisha changamoto hizo zinapungua, Wizara yangu imepanga kuwa na majengo
ya vitega uchumi katika baadhi ya Balozi zetu ili kusaidia kuongeza mapato na
kuokoa fedha ambazo zingetumika kulipia pango katika maeneo hayo. Katika hatua
nyingine, Wizara inaendelea
kushirikiana na Wizara ya Fedha kuhusu uwezekano wa kutumia utaratibu wa mikopo
ya nyumba (Mortgage Financing) katika Balozi zetu badala ya
utaratibu wa sasa ambao una gharama kubwa kwa Serikali. Vile vile, Wizara yangu
katika mwaka huu wa fedha imepanga kuwasiliana na Mamlaka ya Udhibiti wa
Manunuzi ya Umma (PPRA) ili kuwaomba waruhusu Balozi zetu zitumie utaratibu wa
“hire and purchase” kununua vifaa
mbalimbali kama vile magari ya uwakilishi na hivyo, kupunguza gharama.
81.
Mheshimiwa Spika, ninayo kila sababu ya kuwapongeza wafanyakazi wa
Wizara yangu walioko Wizarani na Ubalozini kwa uvumilivu na kujitolea kwa moyo
wao wote katika mazingira haya magumu. Wafanyakazi wameendelea kutekeleza
wajibu wao kwa uaminifu na uadilifu mkubwa sana. Kamati ya Bunge ya Kudumu ya
Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama tumekuwa tukiihusisha kwa karibu kuhusu
changamoto hizi na wameshuhudia hali hii kila walipopata fursa ya kutembelea
Balozi zetu. Tunawashukuru kwa kuielewa hali yetu halisi na kushirikiana nasi katika
kushauri namna bora ya kuondokana na changamoto hizo. Nasi tunauchukulia
ushauri wao na ule wa Kambi ya Upinzani kwa umakini mkubwa sana.
UTAWALA NA MAENDELEO YA WATUMISHI WIZARANI NA KWENYE BALOZI ZETU
82.
Mheshimiwa Spika, napenda
kulifahamisha Bunge lako tukufu kuwa, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliteua Mabalozi – kuiwakilisha nchi yetu huko
Kenya, Misri, Msumbiji, Uganda, Oman, Zambia, Italia, Ubelgiji na China. Vile vile,
aliwateua Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa na Naibu wake pamoja na
Wakurugenzi tisa katika Wizara yangu ambao wana hadhi ya Balozi.
83.
Mheshimiwa Spika, hadi
sasa Wizara yangu ina jumla ya watumishi 430 ambapo kati yao 249 wapo Makao
Makuu ya Wizara, 18 wapo ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar na 163 wapo kwenye
Balozi zetu. Kwa kipindi cha Julai, 2011
hadi Juni, 2012 jumla ya watumishi 50 walihudhuria mafunzo ndani na nje ya
nchi. Kati ya hao, 17 walihudhuria mafunzo ya muda mrefu na watumishi 33
wamehudhuria mafunzo ya muda mfupi.
84.
Mheshimiwa Spika, kwa
kipindi hicho hicho, jumla ya watumishi 58 walipandishwa cheo baada ya
kutekeleza majukumu yao vizuri pamoja na kutimiza masharti ya Miundo ya Utumishi
inayosimamia kada zao. Vile vile,
watumishi 51 walithibitishwa kazini baada ya kumaliza muda wa mwaka mmoja wa
majaribio baada ya kuajiriwa, na watumishi wanne walibadilishwa vyeo baada ya
kujiendeleza na kupata sifa za kada husika.
85.
Mheshimiwa Spika, Wizara
yangu imeweka mkakati wa kuongeza idadi ya watumishi kutoka Zanzibar katika
kada ya Maafisa Mambo ya Nje kwa kuwapatia fursa Wanafunzi 18 kutoka Tanzania
Visiwani kuingia kwenye Chuo chetu cha Diplomasia. Dhamira ya Wizara ni kuona
kwamba, pindi watakapomaliza na kufaulu masomo hayo waweze kuajiriwa kwenye
Wizara yangu kulingana na nafasi za ajira mpya tutakazokuwa nazo.
TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA
Chuo Cha Diplomasia
86.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kukisaidia Chuo ili kiweze
kutekeleza majukumu yake kama yalivyo kwenye nia na madhumuni ya uanzishwaji
wake. Lengo ni kukiwezesha Chuo kuendelea kutoa mafunzo na kufanya utafiti
katika masuala ya diplomasia, uhusiano wa kimataifa, stratejia, usuluhishi wa
migogoro, ujenzi wa amani, kutoa ushauri na kuendesha mafunzo ya muda mfupi.
Lengo tarajiwa ni kukifanya Chuo kuwa taasisi bingwa ya elimu ya juu na ushauri
katika nyanja hizo pamoja na kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa katika masuala ya utekelezaji wa shughuli zake.
87.
Mheshimiwa Spika, tatizo
la umiliki wa ardhi limemalizika baada ya Chuo kupatiwa Hati ya Umiliki wa eneo
lake. Kwa kuwa Chuo kinaendelea kupanuka ni wazi kuwa eneo la sasa kwa Chuo
haliwezi kukidhi mahitaji hayo. Hivyo, Serikali kupitia Wizara yangu imeendelea
kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo. Hadi sasa eneo la ekari 1,000
limeshapatikana. Vile vile, tathmini ya kulipa fidia ya ardhi imekwishafanyika
ambapo Serikali inapaswa kulipa shilingi bilioni
2.5 kwa wananchi wa eneo la Buma lililopo Wilayani Bagamoyo na Wizara inaendelea
kufuatilia upatikanaji wa fedha hizo kutoka kwa mamlaka husika.
Kituo Cha Kimataifa Cha Mikutano Cha Arusha (AICC)
88.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitatu
iliyopita, Kituo kimeweza kukaribisha wastani wa mikutano 64 kwa mwaka. Kati ya mikutano hii asilimia 30 ya mikutano
ni ya kimataifa na asilimia 70 ni ya kitaifa. Idadi hiyo ya mikutano imeweza
kuleta Arusha wageni wanaokadiriwa kufikia 44,578 kila mwaka. Kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2011 Kituo
kiliweza kuwa mwenyeji wa mikutano ya kimataifa 15 na ya kitaifa 47 iliyoingiza
nchini wageni wanaokadiriwa kufikia 35,000.
89.
Mheshimiwa Spika, naomba
kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa kwa mara nyingine tena, Kituo kimeendelea
kupata hati safi ya hesabu zake zilizoandaliwa na kukaguliwa kwa wakati kwa
kipindi kilichoishia tarehe 30 Juni 2011. Kituo kilipata faida ghafi ya
shilingi milioni mia tano thelathini na moja,
elfu mia sita na tano mia tatu na ishirini (531,605,320/=) na kinaendelea kufanya shughuli zake kwa ufanisi na
bila kuwa tegemezi kwa Serikali Kuu.
Katika kipindi cha mwaka 2012/2013, Kituo kimepanga kuingiza mapato ya
shilingi bilioni tisa, milioni mia sita arobaini na tano, elfu mia tatu hamsini
na tisa na mia saba (9,645,359,700/=) kutokana na vyanzo vyake
mbalimbali vya mapato na baada ya kutoa gharama za uendeshaji, Kituo
kinategemea kupata ziada ghafi ya shilingi
milioni miatano ishirini na tano, elfu mia moja hamsini na tisa, mia sita
sitini na nne (525,159,664./=).
90.
Mheshimiwa Spika, Wizara
yangu inaendelea kufuatilia kuhusiana na kujengwa kwa Kituo kipya cha mikutano
mjini Arusha kitakachoitwa Mt.
Kilimanjaro International Convention Centre (MK-ICC). Mradi huu ni moja ya miradi itakayofadhiliwa
na Serikali ya Watu wa China kupitia benki yao ya Exim. Napenda kuipongeza Bodi
ya Wakurugenzi wa Kituo, Menejimenti na wafanyakazi wote wa AICC na pia
kuwatakia mafanikio mema katika kazi zilizo mbele yao.
Mpango wa Kujitathmini kwa Utawala Bora
Barani Afrika (APRM)
91.
Mheshimiwa Spika, kazi
ya tathmini ya utawala bora hapa nchini imeendelea kufanyika kwa ufanisi mkubwa. Kwa kuwa Taarifa ya tathmini
iliyokuwa imetayarishwa mwaka 2009 haikufanyiwa uhakiki kama ilivyotarajiwa. taarifa
hiyo ilihuishwa ili kurekebisha takwimu mbalimbali zilizokuwa zimepitwa na
wakati lakini pia kuakisi mabadiliko ya kisiasa yaliyokuwa yametokea baada ya
uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. APRM Tanzania kwa kushauriana na Sekretarieti ya
Afrika Kusini na Wizara, iliandaa pia Taarifa mahsusi ya Zanzibar. Hatua hii
ilitokana na maoni ya mara kwa mara ya wadau wa Zanzibar hasa Makatibu Wakuu na
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa ingawa suala la APRM ni la Muungano,
ingekuwa ni busara ikaandaliwa taarifa mahsusi ya Zanzibar kwa nia ya
kurahisisha utekelezaji wa changamoto zitakazobainishwa. Taarifa hiyo nayo ilikamilishwa
na kuwa sehemu ya Taarifa ya nchi iliyokuja kufanyiwa tathmini na uhakiki na
Timu ya Wataalamu wa kutoka nchi za Afrika tarehe 2 hadi 23 Machi 2012.
92.
Mheshimiwa Spika, wataalam
wa Country Review Mission wapatao 20
waliwasili nchini mwezi Machi 2012. Wakiwa nchini walikutana na Mheshimiwa
Rais, Makamu wa Rais, Serikali ya Muungano, Makamu wa Kwanza wa Rais (SMZ), Makamu wa Pili
wa Rais (SMZ), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri wa
Katiba na Sheria Zanzibar, Makatibu Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Wawakilishi wa Serikali, Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa,
Wabunge, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Jumuiya ya Wafanya Biashara, Washirika wa
Maendeleo pamoja na Asasi zisizo za Kiserikali ili kupata maoni yao. Aidha, Wataalam
hao, waligawanyika katika makundi mawili tofauti walitembelea mikoa ya Mjini
Magharibi, Kusini Pemba, Mtwara, Mbeya, Dodoma, Arusha, Kagera, Ruvuma na
Kigoma.
93.
Mheshimiwa Spika, katika
mikutano mbalimbali iliyofanyika masuala yafuatayo yalijitokeza ambapo pamoja
na kuwepo kwa amani na utulivu, maeneo mengine yaliyoonekana kuwa ni tunu na yanayopaswa
kuenziwa ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, utaratibu wa kurithishana
madaraka kwa amani kila baada ya uchaguzi mkuu, Muafaka wa kisiasa Zanzibar na
kazi nzuri inayofanywa kwa uhuru na uwazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Serikali.
94.
Mheshimiwa Spika, Tanzania inatarajia kufanyiwa
tahmini kwenye Kikao cha nchi wenza zinazoshiriki katika mchakato Januari, 2013
badala ya Julai, 2012 kutokana na Timu hiyo ya APRM kutokuweza kukamilisha taarifa
yao katika muda ambao ungetoa nafasi kwa Serikali yetu kutoa majibu na
kuyawasilisha kwenye Kikao cha APRM cha Tathmini cha Wakuu wa Nchi
kilichofanyika Julai, 2012 mjini Addis Ababa. Ninaipongeza Bodi ya Uendeshaji ya
APRM kwa kazi nzuri walioifanyia nchi yetu.
MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012
95.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2011/2012 Wizara yangu
ilipangiwa kutumia kiasi cha
shilingi bilioni mia moja ishirini na tano, mia moja na mbili milioni na mia
nane sabini na tano elfu (125,102,875,000/=). Kati ya fedha hizo shilingi bilioni themanini, mia
sita na mbili milioni na mia nane sabini na tano elfu (80,602,875,000/=) ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi
bilioni arobaini na nne na milioni mia tano (44,500,000,000/=) ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo. Aidha,
katika bajeti ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara (Recurrent Budget), shilingi
bilioni sabini na sita, mia tatu themanini na saba milioni na mia moja
themanini na saba elfu (76,387,187,000/=) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida (OC) na bilioni
nne, mia mbili kumi na tano milioni na mia sita themanini na nane elfu (4,215,688,000/=) ni kwa ajili ya mishahara.
96.
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Balozi zake ilitegemea kukusanya kiasi cha shilingi bilioni kumi na nne,
mia nane sabini na mbili milioni na mia nne tisini na mbili elfu (14,872,492,000/=). Hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2012 kiasi cha
shilingi bilioni kumi na tatu, mia nane hamsini na tatu milioni, mia nne
arobaini na tisa elfu na mia tano hamsini na tisa (13,853,449,559/=) ikiwa ni makusanyo ya maduhuli balozini na Makao
Makuu. Kiasi hiki cha fedha ni sawa na asilimia 93 ya makusanyo ya fedha zote
za maduhuli zilizokadiriwa kukusanywa balozini na Makao Makuu kwa mwaka wa
fedha 2011/2012.
97.
Mheshimiwa Spika, hadi
kufikia tarehe 30 Juni, 2012 Wizara ilikuwa imepokea kutoka HAZINA jumla ya
shilingi bilioni mia moja na ishirini na tatu, milioni mia nane themanini na
nne elfu mia saba sabini na nane na mia saba themanini na saba (123,884,778,787/=) ikiwa ni pungufu ya
asilimia 0.97 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, Mishahara, pamoja na bajeti ya
Maendeleo. Kiasi cha shilingi bilioni tisini na saba, milioni mia mbili
arobaini na moja elfu mia mbili thelathini na tisa, mia saba themanini na saba (97,241,239,787/=) ni kwa ajili ya Matumizi
ya Kawaida pamoja na Mishahara ikionyesha
ongezeko la asilimia 20.64 ya
bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
98.
Mheshimiwa Spika,
ongezeko hili limechangiwa na kuibuka kwa majukumu mbalimbali ya kitaifa ambayo
awali hayakupangiwa fedha kutokana na ufinyu wa bajeti kama vile; Ujio wa Timu
ya Ukaguzi kuhusu Mpango wa Kujitathmini Wenyewe kuhusu Utawala Bora (APRM)
kutoka Makao Makuu ya Taasisi hiyo, Mchakato wa maandalizi pamoja na uzinduzi
wa Majadiliano ya Ubia Nadhifu (Smart
Partnership Dialogue), Ujumbe na ushiriki wa Tanzania katika Kikosi Kazi
cha Kamati ya Mawaziri ya Jumuiya ya Madola (CommonWealth Ministerial Action Group – CMAG), Mchakato wa ujumbe wa
Tanzania katika Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za
kusini mwa Afrika pamoja na Ujumbe wa Tanzania katika Baraza la Amani na
Usalama la Umoja wa Afrika.
99.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa bajeti ya
Maendeleo, Wizara hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2012 imepokea kutoka Hazina
shilingi bilioni ishirini na sita, mia sita arobaini na tatu milioni na mia
tano thelathini na tisa elfu (26,643,539,000/=). Kiasi hiki ni sawa na
asilimia 59.87 ya bajeti yote ya Maendeleo iliyotengwa kwa Wizara kwa mwaka wa
fedha 2011/2012. Ikumbukwe kuwa Bajeti
ya Maendeleo ya Wizara ilipunguzwa kwa kiasi cha shilingi 16,898,098,757/= kutokana
na hali ya mapato ilivyodhihirika.
MALENGO YA WIZARA KATIKA MWAKA WA FEDHA WA 2012/2013
100.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013,
Wizara itaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi kama yalivyoainishwa
katika hotuba hii. Aidha,
Wizara itaendelea kutekeleza malengo yake iliyojiwekea kulingana na Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015. Msisitizo
utakuwa ushiriki wa Wizara katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka
Mitano 2011/2012 – 2015/2016. Naomba kusisitiza na kukumbusha Wizara nyingne
kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ni Wizara mtambuka na
hivyo inahusika na ufanikishaji wa miradi mingi inayotekelezwa na Wizara, Idara
na Taasisi nyingine mbalimbali za Serikali. Kama nilivyoeleza hapo awali,
Wizara yangu ina nafasi kubwa katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya
Taifa.
101.
Mheshimiwa Spika, kama sehemu ya kuendeleza na kuhimiza njia mbadala za
kukabiliana na changamoto zinazotokana na bajeti inayoendelea kupungua kila
mwaka, pamoja na mambo mengine, Wizara inatarajia kufaya
mambo yafuatayo:
i.
Kufungua Balozi Ndogo katika miji ya Uturuki, Loss Angeles (LA), California, Lubumbashi
na Guangzhou; ambazo sanjari na kuendeshwa kwa gharama nafuu zinaweza kukusanya
maduhuli mengi kupitia utoaji wa viza na tozo, hivyo kuongeza idadi ya watalii
na kukuza biashara nje ya zile nchi tulizozoea (traditional allies) zilizoko
Ulaya ambazo uchumi wake unayumba kwa sasa;
ii.
Tume za Kudumu za Pamoja za Ushirikiano (JPC) -Wizara inatarajia kuitisha mikutano ya Tume za
Kudumu za Pamoja za Ushirikiano angalau kwenye nchi tatu kwa lengo la kuzifufua
tume hizo na kupanua fursa za ushirikiano, hususan masoko ya bidhaa
zinazozalishwa nchini;
iii.
Watanzania Waishio Ughaibuni (Diaspora) - Nafurahi kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa
kufuatia Mheshimiwa Rais kuteua Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora mapema Mei,
2012 Wizara yangu sasa ipo katika mchakato wa kuandaa Sera na Mpango wa Kitaifa
kuhusu masuala ya Diaspora ili kuweka mazingira mazuri zaidi ya kuwahusisha
Watanzania hao katika kuchangia maendeleo ya nchi yao. Hatua hii muhimu
itasaidia kuainisha wigo wa kisera, ushiriki wa wadau na majukumu ya Wizara, Idara
na Taasisi nyingine katika kufanikisha ushirikishwaji wa Watanzania waishio
ughaibuni kuchangia katika maendeleo ya taifa. Ni azma ya Wizara yangu kuona
kuwa mchakato huu unakamilika mapema ili kutoa mwongozo kwa wadau na
kurahisisha uelewa wa pamoja kuhusu mikakati bora ya kuwatambua na
kuwashirikisha diaspora katika kuchangia maendeleo ya nchi yao;
iv.
Majukumu ya Kimataifa - Wizara imejipanga kutumia kikamilifu nafasi za Tanzania
kimataifa katika kipindi hiki zikiwemo uenyekiti wa asasi ya SADC organ Troika na ujumbe wa Baraza la
Usalama la Umoja wa Afrika kukuza taswira ya nchi yetu nje na kukuza
ushirikiano wa Tanzania na nchi
zilizoendelea ambazo ndizo zinafanya vizuri kiuchumi kwa sasa;
v.
Utatuzi wa Migogoro na Uimarishaji wa Amani - Tanzania imeendelea kuwa nchi ya kutumainiwa katika
ulinzi na ujenzi amani Barani Afrika. Kumejitokeza haja kubwa ya uzoefu wetu
kutakiwa na nchi nyingine katika utatuzi wa migogoro na ujenzi wa amani katika
nchi zinazotoka katika migogoro. Serikali imeamua kujikita katika kutumia
uzoefu wetu na sifa hii katika kupanua maslahi ya nchi yetu kwa kuitikia fursa
hizo. Tunajipanga kutumia Wanadiplomasia wetu wastaafu na waliopo katika
kutafuta suluhu ya migogoro. Lengo ni baadae kuanzisha taasisi ya usuluhishi wa
migogoro katika Chuo chetu cha Diplomasia. Uwepo wa Taasisi hiyo nchini
Tanzania itavuna mikutano mingi na hivyo kuingizia nchi fedha za kigeni,
kupanua sekta ya utalii na kutoa fursa ya kujenga urafiki na kupanua maslahi
yetu kwa nchi nyingi zaidi. Tutatumia fursa zetu za kuwa Mjumbe wa Baraza la
Usalama la Umoja wa Afrika na Uenyekiti wa Asasi ya SADC kufanikisha azma hiyo;
na
vi.
Ulinzi wa Amani - sambamba na mkakati huo, eneo la ulinzi wa amani (peacekeeping
operations) ni eneo jipya tunalotaka kulipa kipaumbele. Azma hiyo inakwenda
sambamba na uanzishwaji wa Chuo cha Ulinzi wa Amani (Peacekeeping School)
nchini kwa ushirikiano wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Canada.
Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa tayari Hati ya Awali ya
Makubaliano (MoU) imesainiwa mwaka huu. Kuanza kwa Chuo hicho kutatoa fursa kwa
vijana wetu kujenga uwezo wa kushiriki katika operesheni za Ulinzi wa Amani,
vijana wetu wa jeshi kupata uzoefu na mbinu mpya za kivita nje ya nchi,
kuwezesha Watanzania wa fani mbalimbali kupata ujuzi na utaalamu na kuweza
kushiriki kwenye operesheni za AU na UN (Civilian Peacekeeping Mission) ambako
kwa sasa ushiriki wetu ni mdogo kutokana na kukosa stadi za aina hii.
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2012/2013
102.
Mheshimiwa Spika, ili kuweza kutekeleza kikamilifu kazi zilizotajwa hapo
juu, Wizara yangu imepangiwa kiasi cha shilingi bilioni tisini na nane, mia
tatu thelathini na tisa milioni na mia saba na saba elfu (98,339,707,000/=) kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Kati ya fedha hizo,
shilingi bilioni themanini na moja, milioni mia sita themanini na sita, mia tano na tatu elfu (81,686,503,000/=) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, shilingi
bilioni kumi na sita, mia sita hamsini na tatu milioni na mia mbili na nne elfu
(16,653,204,000/) ni kwa ajili ya bajeti ya Maendeleo. Aidha, jumla
ya shilingi bilioni sabini na sita, mia tano arobaini milioni na mia tano
ishirini na moja elfu (76,540,521,000/=) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na bilioni
tano, mia moja arobaini na tano milioni na mia tisa themanini na mbili elfu (5,145,982,000/=) ni kwa ajili ya Mishahara.
103.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara; shilingi
bilioni moja, mia tano arobaini na tisa milioni na mia tisa ishirini na tano
elfu (1,549,925,000/=) ni kwa ajili ya mchakato wa APRM, shilingi
bilioni moja, mia tano na nne milioni, mia tano sabini na nne elfu na mia nne
sabini na nane (1,504,574,478/=) ni
kwa ajili ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na shilingi bilioni
mbili, mia tano ishirini na sita milioni, mia tisa sabini na tatu elfu na mia
nne sitini na mbili (2,526,973,462/=)
ni kwa ajili ya fedha za Mshahara na Matumizi ya Kawaida ya Chuo cha
Diplomasia.
104.
Mheshimiwa Spika, aidha, Wizara yangu, kupitia Balozi zake, inatarajia
kukusanya kiasi cha shilingi bilioni kumi na sita, milioni mia nane themanini
na mbili elfu mia mbili thelathini na moja, mia tatu na thelathini (16,882,231,330/=) kama maduhuli ya
Serikali. Kwa maana ya utekelezaji wa Bajeti, kiasi hiki cha maduhuli tayari
kimehesabiwa kama sehemu ya Matumizi ya Kawaida ya Bajeti ya Wizara yangu.
105.
Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja.
COMMENTS