TAMKO LA BARAZA LA WANAWAKE WA CHADEMA ( BAWACHA) KWA VYOMBO VYA HABARI Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA), tunalaani...
TAMKO LA BARAZA LA WANAWAKE WA CHADEMA ( BAWACHA) KWA VYOMBO VYA HABARI
Baraza la Wanawake wa
CHADEMA (BAWACHA), tunalaani
kwa nguvu zote mauaji yanayoendelea nchini
yakifanywa au
kusababishwa na Jeshi la Polisi ambao tuliamini kuwa ni walinzi wetu na mali zetu, lakini wamegeukaa kuwa
ndio wauaji wakubwa wa wananchi wasiokuwa na hatia.
Aidha, BAWACHA tumeshangazwa na kauli ya Msajili
wa Vyama vya Siasa John Tendwa ya kufuta vyama vya siasa ambavyo mauaji
yatatokea katika mikutano yao, wakati anajua kuweli kuwa mauaji hayo yanafanywa
na Jeshi la Polisi.
BAWACHA tunatambua kuwa kauli hiyo inailenga
CHADEMA ili kutekeleza dhamira ovu ya Tendwa aliyotumwa na Serikali
inayooongozwa na CCM. Tunamtaka Tendwa awaeleze Watanzania iwapo kauli yake
hiyo haitatumiwa na polisi na CCM kuua tena ili kukoleza sababu za kutaka
kuifuta CHADEMA.
Tunashangazwa na utendaji kazi wa Jeshi la Polisi
ambalo limefikia mahali linatumia nguvu kubwa na kuua wananchi ambao mbali ya
kuwa hawana hatia yoyote, pia hawana silaha yoyote
lakini ndio wanaopigwa na mabomu na risasi za moto.
Baraza la Wanawake wa CHADEMA,
tunalaani vitendo hivi vya kinyama vinavyoendelea nchini.
Kumekuwa na matukio mfululizo wa Jeshi la Polisi kutumia
nguvu kubwa sana katika mikutano ya CHADEMA, mauaji ya Januari 5, 2011
Jijini Arusha, ambapo polisi waliua kwa risasi za moto watu watatu ambao
hawakuwa na hatia wala silaha yoyote.
Hata katika matukio mengine yasiyohusiana na
shughuli za kisiasa zinazofanywa na wananchi, polisi wamekuwa wakitumia nguvu
kubwa kudhibiti mitafaruku inayotokea hali ambayo badala ya kutatua imekuwa
ikiongeza ukubwa na ugumu wa tatizo. Tulishuhudia katika Jiji la Mbeya
Watanzania wanaofanya shughuli za biashara ndogondogo (Wamachinga) walipigwa mabomu na risasi
za moto kusababisha hasara kubwa, ambapo
pia katika tukio hilo waandishi wa habari ambao hawakuwa na silaha yoyote zaidi
ya kalamu zao, waliathiriwa na matumizi hayo nguvu kubwa kutoka kwa askari bila
sababu za msingi.
Tukio la karibuni kabisa ni lile lililotokea mjini
Morogoro ambapo kijana mmoja, Ali Zona aliyekuwa akiendelea na shughuli
zake pembeni mwa barabara, aliuawa na Jeshi la Polisi kwa
kitu kinachoonekana kuwa ni risasi au bomu, lakini polisi wakatoa taarifa
isiyokidhi kiu ya kutaka kujua, wakisema kijana huyo hakupigwa
risasi bali alipigwa na kitu kizito.
Aidha BAWACHA inalaani
vikali mauaji ya Mwandishi wa Habari wa Channel Ten, Hayati Daudi Mwangosi aliyeuawa kwa
kushambuliwa kinyama na hatimaye kulipuliwa kwa bomu na polisi mbele ya mashuhuda walioshuhudia jinsi mwandishi huyo
akisambaratishwa mithili ya mnyama wakati akitimiza wajibu wake wa kuitumikia jamii.
Mwangosi hakuwa na silaha yoyote zaidi ya vitendea kazi vyake vya uandishi wa
habari, lakini bado askari walitumia nguvu kubwa kumshambulia na kumuua.
Mfululizo huu wa mauaji katika maeneo tofauti ya
mikoa mbalimbali nchini yanayofanywa na
Jeshi la Polisi unathibitisha kuwa
hayafanyiki katika mikutano ya CHADEMA pekee, bali pia katika matukio mengine
ya wananchi katika maeneo mengi nchini.
Hivyo BAWACHA inataka Watanzania kupuuza kauli
iliyotolewa na CCM kupitia kwa Nape Nnauye ya kuwataka CHADEMA na viongozi kuwajibika
kwa mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi mkoani Iringa na maeneo mengine
nchini.
BAWACHA inatambua kuwa kauli hiyo ni ishara ya CCM
kushiundwa kuongoza na kulinda mauaji yanayoendelea nchini. Ikiwa CCM ingekuwa
inakerwa na mauaji hayo, badala ya kutaka CHADEMA iwajibike ingewawajibisha
viongozi wake wa CCM na serikali, ambao wameongoza vikao vya Kamati za Ulinzi
na Usalama kushawishi Jeshi la Polisi kuvuruga operesheni halali za CHADEMA na
kufanya mauaji.
Tunapenda polisi wajue kuwa haya ni makosa makubwa kutumia vibaya madaraka waliyodhaminiwa na wananchi, ambao pia ndiyo
waliowasomesha, wanawalipa mishahara na kutimiza mahitaji yao muhimu ikiwemo
vitendea kazi vyao kutokana na kodi wanazolipa lakini badala ya kuwatumikia,
wanawaua kwa ukatili mkubwa.
Izingatiwe kwamba
CHADEMA walikuwa hawaandamani wala kufanya mikutano ya hadhara bali
walikuwa wanafungua matawi ya chama chao
na kufanya vikao vya ndani.
Wamesababisha usumbufu
mkubwa kwa Taifa, familia zao kuwakosa wapendwa wao, na si hivyo tu BAWACHA
kama wanawake na wazazi tumeumia sana na vitendo vya kinyama vinavyofanywa na
Jeshi la Polisi kote nchini.
Tunasema tukiwa kama wazazi wenye uchungu na uzazi, tumechoka kusikia na kuona
mauaji haya ya kinyama ya watu wasiokuwa na hatia.
BAWACHA tunasema kwa
kuwa Jeshi la Polisi limelifedhehesha
Taifa na kutia doa nchi yetu inayojulikana dunia nzima kwamba ni kisima
cha amani.
BAWACHA tunamtaka
Waziri Emmanuel
Nchimbi, IGP Said Mwema, Kamishna Paul Chagonja na RPC Michael Kamuhanda
wajiuzuru haraka sana, ili wakati tume huru ya uchunguzi itakapoundwa kwa
mujibu wa sheria kuchunguza tukio hilo na mengine, wao wahojiwe wakiwa hawako
madarakani ili wasiharibu ushahidi.
Aidha BAWACHA kwa ujumla tunasikitishwa kuona kwamba CCM na
serikali yake, kwa kutumia Jeshi la Polisi sasa wameamua kutumia silaha kujibu
nguvu za hoja za CHADEMA zinazochochea fikra na kuamusha ari ya mabadiliko
makubwa ya kimfumo na kiutawala miongoni mwa Watanzania makini, ndani na nje ya
bunge.
Lengo kubwa la
Serikali ya CCM ni kuwafanya wananchi
washindwe kutambua haki zao ili
waweze kuwatala kwa urahisi, na kuifanya nchi kama mali yao binafsi wakiwa na
hati miliki ya kutawala watakavyo.
Aidha BAWACHA
tunalitaka Jeshi la Polisi Mkoani Iringa liwaambie wananchi ni
nani aliyewashinikiza kwenda kuvuruga mikutano halali ya CHADEMA na kufanya mauaji.
Hizo ni mbinu za Chama
Tawala cha CCM kuanzisha vurugu ili kuuhadaa umma na kutaka kuuaminisha kuwa CHADEMA ni
chama cha vurugu. Tunawataka wajue katika mbinu hiyo pia hawatafanikiwa kama
ambavyo hawajawahi kufanikiwa katika mbinu zao zingine.
BAWACHA tunawasihi Watanzania wote waendelee kuiunga mkono
CHADEMA katika kupaza sauti kutaka uwajibikaji wa Waziri
Nchimbi, Said Mwema, RPC
Michael Kamuhanda na Paul Chagonja wajiuzuru kwa maana
wamelitia fedheha Taifa letu.
Aidha BAWACHA
tunawaomba wanawake wote watuunge mkono kwani athari za mauaji haya
yanayoendelea sasa ambayo yanafanywa na Jeshi la Polisi ni kubwa sana.
Watanzania tuungane
kwa pamoja kuhakikisha
haki inapatikana kwa kila mmoja wetu ili kudumisha na kulinda amani na
utulivu katika nchi yetu.
Mungu ibariki Tanzania,
Mungu ibariki Afrika
Subira Waziri
Naibu Katibu Mkuu
BAWACHA - Taifa
COMMENTS