Huduma ya usafirishaji wa abiria kwa kutumia magari aina ya Toyota NOAH nchini Tanzania, ulianzia katika mikoa ya Kaskazini ya Kilimanj...
Huduma ya usafirishaji wa abiria kwa kutumia magari aina ya Toyota NOAH
nchini Tanzania, ulianzia katika mikoa ya Kaskazini ya Kilimanjaro,
Arusha na Manyara ambapo magari hayo yalipewa leseni za kutoa huduma ya
usafiri katika njia zote, leseni ambayo hutolewa kwa magari ya
kusafirisha watalii tu.
Hata hivyo wamiliki wa magari hayo hawakuzingatia masharti ya leseni ya
usafirishaji kwani badala ya kusafirisha watalii walijiingiza kwenye
biashara ya usafiri wa umma na hivyo kuzusha migogoro kati ya
wasafirishaji wa magari makubwa katika njia hizo na wamiliki wa Noah.
Migogoro hiyo ilitokana na magari hayo kutokuwa na leseni ya njia maalum
na hivyo kusababisha vurugu za mara kwa mara katika utoaji wa huduma ya
usafirishaji abiria katika maeneo husika.
Kwa kuzingatia kuwa tayari kulikuwa na mgogoro wa wasafirishaji,
Mamlaka ya SUMATRA iliona ni vyema kukutana na wadau wa usafiri katika
mikoani husika kwa lengo la kujua hali halisi ya usafiri katika mikoa
hiyo pamoja na kujua kero za wananchi kwa ujumla na kuzitafutia
ufumbuzi.
Katika mikutano hiyo, changamoto mbalimbali za masuala ya usafirishaji
zilijadiliwa zikiwemo, ajali za barabarani, upandishwaji holela wa nauli
pamoja na vurugu za mara kwa mara zinazosababishwa na waendeshaji wa
magari ya Noah ambayo hayakuwa na leseni za usafirishaji.
Baada ya kutathmini changamoto mbalimbali zilizojadiliwa kwenye mikutano
hiyo, Mamlaka ilifanya tathmini ya utendaji kazi wa aina hii ya magari
ya Noah na kubaini kuwa kulikuwa na malalamiko mengi kutoka kwa abiria
na wasafirishaji wa mabasi makubwa wanaotoa huduma ya usafiri katika
maeneo ambayo magari ya Noah yakitoa huduma.
Baadhi ya malalamiko yaliyotolewa na abiria waliotumia huduma ya magari
ya Noah ni pamoja na abiria kutozwa nauli kubwa zaidi ya viwango
vilivyoridhiwa na Mamlaka; abiria kuhoji umbali unaoruhusiwa kwenda
magari hayo pamoja na uimara wa bodi ya magari hayo kwa kubeba abiria;
mizigo ya abiria kuachwa kwenye vituo kutokana na kutokuwa na nafasi ya
kuhifadhia na magari hayo kutoa huduma bila kufuata njia maalum kama
ilivyoainishwa kwenye leseni zao. Malalamiko mengine yalihusisha magari
ya Noah kukwama mara kwa mara sehemu za vijijini hasa wakati wa mvua;
mwendo kasi ambao ni hatari kwa maisha ya abiria na madhara makubwa kwa
abiria na mali zao ajali zinapotokea kutokana na uhafifu wa bodi zake
Baadhi ya wasafirishaji wanaotoa huduma ya usafiri mijini na kati ya mji
na mji, wamelalamikia magari ya Noah kuwa magari hayo yemekuwa yakitoa
huduma ya usafirishaji bila ya kufuata utaratibu wa kupakia abiria wa
kufuata foleni kama ulivyo utaratibu wa watoa huduma kwa mikoa ya
Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Baadhi ya vyama vya wasafirishaji
viliwahi kuandika malalamiko yao na kuonyesha wasiwasi wa kuzorota au
kudidimia kwa sekta ya usafirishaji kutokana na wasafirishaji wenye
uwezo wa kuagiza mabasi makubwa kuacha kufanya hivyo na kununua magari
ya Noah ili kujipatia faida haraka pasipo kuangalia maslahi na usalama
wa wasafiri.
Baada ya Mamlaka ya SUMATRA kupokea malalamiko hayo Mamlaka ilifanya
tathmini iliyoshirikisha Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani
pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kubaini kuwa uwezo wa
magari hayo kutumika kama usafiri wa umma ni mdogo na hivyo kuifanya
biashara ya usafirishaji kwa kutumia magari hayo kutokuwa na tija;
magari ya aina hiyo madirisha yake ni madogo na hayana milango ya
dharura. Aidha, magari hayo hayakidhi matakwa ya kifungu namba 4.4.3 cha
Kiwango Na. 598:1999 pamoja na Kifungu Namba 5.2.1 - 5.3.5 Kiwango TZS
598 (Part 3): 2010 cha Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa magari ya
abiria. Vifungu hivyo vinaeleza viwango vya bodi, madirisha na urefu
katika gari la abiria.
Zaidi ya hiyo matumizi ya magari hayo yana hatari ya kudumaza au
kudidimiza sekta ya usafirishaji kwa waagizaji wa mabasi makubwa kuacha
kuagiza mabasi hayo yenye uwezo mkubwa (Economies of Scale) wa kubeba
abiria wengi kwa pamoja na kuagiza magari mengi ya Noah yenye uwezo wa
kubeba abiria wachache. Aidha ilibainika kuwepo kwa uwezekano mkubwa wa
msongamano wa magari kwenye miji ya mikoa hiyo pamoja na abiria kukosa
haki ya msingi ya kusafiri na mizigo usiozidi kilo 20 ambapo ni kinyume
na Kanuni Na. 23 (1) ya kanuni za leseni za usafirishaji magari ya
abiria mwaka 2007.
Kutokana na hali hiyo SUMATRA ilifikia uamuzi wa kusitisha utoaji wa
leseni hizo, baada ya ya kutathminini malalamiko na hoja mbalimbali
zilizotolewa na wadau wa usafiri.
maamuzi hayo yanazingatia jukumu la SUAMTRA katika kusimamia sekta ya
usafirishaji abiria kwa njia ya barabara kama yalivyoainishwa katika
Kifungu Namba 5(b)(c)(d) cha Sheria ya SUMATRA, ambapo Mamlaka ilitoa
maamuzi kuwa kuanzia tarehe 10/01/2012 hakutakuwa na utoaji wa leseni za
usafiri wa umma kwa msafirishaji mpya anayemiliki gari la Noah. Aidha
magari ya aina hiyo ambayo yatahitaji kufanya biashara ya usafirishaji
abiria yataruhusiwa kwa kupewa leseni ya kutoa huduma ya usafiri kwa
watalii tu.
Kwa mmiliki wa Noah mwenye leseni ya usafirishaji, ataruhusiwa
kuendeleza leseni hiyo na mwisho tarehe 30/06/2012 ambapo matumizi ya
leseni itakayo endelezwa kuanzia tarehe hiyo mwisho wake wa kutumika
utakuwa tarehe 29/06/2013.
Pia iliamuliwa kuwa wasafirishaji wote wa leseni za Noah, watakao
endeleza leseni zao kila moja itaishia kwa utaratibu wake kwa kipindi
cha mwaka mmoja kwa leseni hizo kama kanuni inavyoelekeza. Mfano leseni
iliyotolewa tarehe 1/4/2012 itaishishia tarehe 30/03/2013, leseni
iliyotolewa tarehe 10/08/2011 itaishia tarehe 09/08/2012 na
haitaendelezwa tena. Utaratibu huo utafuatwa mpaka leseni ya mwisho
itakapoishia tarehe 29/06/2013.
Misingi ya Uamuzi wa SUMATRA imezingatia kifungu Namba 5 cha Sheria ya
SUMATRA, Sura ya 314, Mamlaka inalo jukumu la kisheria la kulinda
maslahi ya watumiaji pamoja na watoa huduma wa sekta inazozidhibiti.
Aidha, kifungu Namba 6 cha Sheria hii, kinaipa Mamlaka wajibu wa
kuhakikisha kwamba huduma zinazotolewa na sekta inazozidhibiti,
zinatolewa katika ubora (quality) unaokubalika, gharama zinazostahili
(cost effective) na zinakidhi viwango (Standards) vilivyowekwa na
Mamlaka husika.
Kwa kuzingatia jukumu na kazi za Mmalaka katika udhibiti wa usafiri wa
nchi kavu, Mamlaka ilifikia uamuzi wa kusitisha leseni za Noah kwa
kuzingatia hasa mambo makuu yafuatayo:
(a). Sababu za Kiuchumi
Uwezo mdogo wa mabasi yaliyotajwa hapo juu katika kubeba abiria na hivyo
kuifanya biashara ya usafirishaji kwa kutumia mabasi hayo kutokuwa na
tija. Noah inabeba abiria saba tu wa kulipa kwa nauli ya Sh 300/= kwa
abiria kwa umbali wa chini ya kilomita 10 haiwezi kukidhi gharama za
uendeshaji.
(b). Sababu za Kiusalama
Magari ya Noah hayakidhi viwango vya usalama kwa magari ya umma
(commuter buses). Aidha, magari hayo hayakidhi matakwa ya kifungu namba
4.4.3 cha Kiwango Na. 598:1999 cha Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa
magari ya abiria. Magari hayo yameundwa kwa shughuli za kifamilia na
burudani.
(c) Umuhimu wa kusimamisha magari ya Noah kwa awamu (Gradual
phasing out)
Utaratibu wa kusimamisha leseni kwa gari mojamoja kadiri
muda wa leseni husika unapoisha linaondoa uwezekano wa kutokea
msongamano wa wamiliki wa magari ya Noah siku ya mwisho wa huduma endapo
wote wataruhusiwa kuendesha biashara zao mpaka tarehe ya mwisho.
Msongamano wa wamiliki wengi ambao wote leseni zao zinaisha muda wake
kwa siku moja utachochea mgogoro mkubwa utakaoathiri utulivu kwenye
shughuli za usafirishaji nchini.
(d) Wakati SUMATRA inaendelea kuondoa mabasi madogo yaani vipanya
(mini buses) na kuhamasisha matumizi ya mabasi makubwa yenye faida
kiuchumi (economies of scale) kwa mtoa huduma na mtumia huduma, matumizi
ya magari madogo zaidi ya vipanya (micro bus) ni jambo lisilokubalika.
Kwa maelezo hayo, Mamlaka ya SUMATRA inapenda kuuhakikishia Umma kwamba
nia ya Mamlaka katika kutekeleza hatua hii ni kuepusha madhara
yanayolikumba na yanayoweza kulikumba Taifa kutokana na utumiaji wa aina
hii ya usafiri ambayo si salama kwa maisha ya abiria lakini vile vile
hauleti tija katika kuboresha sekta hii ya usafirishaji wa umma kwa njia
ya barabara.
David Mziray
Public Affairs Manager
SUMATRA
P.O.Box 3093
Dar es Salaam
Tel: +255 22 2197521
Mob: 0767 250 550
Website: www.sumatra.or.tz <http://www.sumatra.or.tz>
Email: davymzy@yahoo.com <mailto:davymzy@yahoo.com>
COMMENTS