TAARIFA KWA UMMA Natoa mwito kwa wananchi wa Jimbo la Ubungo kuhudhuria mkutano wa wadau, wananchi na watoa huduma ya maji kwa magari ...
TAARIFA
KWA UMMA
Natoa mwito kwa wananchi wa Jimbo
la Ubungo kuhudhuria mkutano wa wadau, wananchi na watoa huduma ya maji kwa
magari na visima binafsi katika Jiji la Dar es salaam ulioitishwa na Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) tarehe 27 Septemba 2012 katika
Ukumbi wa Land Mark Hotel River Side Ubungo kuanzia saa 3 asubuhi.
Aidha, katika kujadili ajenda za
mkutano huo zilizotolewa naitaka EWURA kuweka mkazo katika kupokea maoni ya
wananchi ili kuwezesha kuandaliwa kwa haraka kwa kanuni za usimamizi na bei
elekezi ya maji katika jiji la Dar es salaam ikiwemo katika visima na malori
binafsi kwa kuzingatia kuwa katika ziara yangu katika kata nane za Jimbo la
Ubungo katika kipindi cha mwezi Agosti na Septemba 2012 nimepokea malalamiko mengi
juu ya ongezeko la bei ya maji ambayo imefikia mpaka shilingi mia tano kwa dumu
moja la lita 20 bila udhibiti wowote.
Kwa mujibu wa Tangazo la EWURA
lililotolewa mwezi Septemba 2012 Mkutano huo ambao wadau wote wa maji ikiwemo
wananchi wanaalikwa kushiriki utajadili haki na wajibu wa watoa huduma ya maji
Jijini Dar es salaam; mwongozo wa watoa huduma ya maji kwa visima na magari
binafsi na utaratibu utakaotumiwa na DAWASCO kusajili watoa huduma wa maji ya
visima na wasambazaji wa maji kwa magari binafsi.
Izingatiwe kuwa katika mikutano
yangu na wananchi ya awamu ya pili katika kata nane za Jimbo la Ubungo kati ya
Agosti na Septemba 2012 nilisisitiza kuwa EWURA ina wajibu kama ilivyo kwenye
mafuta na umeme kusimamia sekta ya maji siyo ya umma tu hata binafsi, hata
hivyo kwa sasa inasimamia zaidi bei na ubora kwa upande wa mamlaka za umma.
Hivyo, nilitoa mwito kwa wananchi
kuungana kuitaka EWURA kueleza hatua iliyofikiwa katika kuandaa kanuni za
usimamizi wa sekta binafsi ya maji juu ya mfumo wa bei elekezi na viwango vya
ubora kama ambavyo mamlaka husika iliahidi kwenye Kongamano la Maji Ubungo
mwaka 2011 suala ambalo lipaswa kuzingatiwa na wadau watakaoshiriki kwenye
mkutano unaofanyika tarehe 27 Septemba 2012.
Itakumbukwa tarehe 2 Machi 2012
nilifanya mkutano na waandishi wa habari ambapo pamoja na mambo masuala mengine
niliitaka EWURA kutoa kauli ndani ya kipindi cha wiki moja kuhusu hatua
iliyofikiwa katika maandalizi ya kanuni husika pamoja na udhibiti wa bei ya
maji ikiwemo kwenye sekta binafsi katika jiji la Dar es salaam.
Katika mkutano wangu na
wanahabari tarehe 2 Machi 2012 nilieleza kuwa kupitia ziara ya kikazi katika
kata saba za Jimbo la Ubungo nilibaini kwamba
kubwa ya ubora na bei ya maji jijini Dar es salaam katika sekta binafsi;
bei ya maji iko juu sana hali ambayo inashawishi biashara haramu yenye
kuhusisha hujuma katika miundombinu ya maji na ufisadi wenye kuharibu ratiba ya
mgawo wa maji ili kupanua soko kinyemela.
Tarehe 8 Machi 2012 Mkuu wa Idara
ya Mawasiliano wa EWURA Titus Kaguo alinukuliwa vyombo vya habari akinijibu
kuwa mamlaka hiyo haiwezi kutoa bei elekezi kwenye maji kwa kuwa tayari
ilishafanya hivyo mwaka 2010 bila kuzingatia kuwa bei elekezi pekee iliyotolewa
na EWURA ni katika visima, maghati na mabombo ya umma yanayoendeshwa na DAWASA
na DAWASCO.
Kufuatia majibu hayo tarehe 8
Machi 2012 nilitoa taarifa kwa umma kuwa kauli ya Mamlaka ya Udhibiti wa
Nishati na Maji (EWURA) iliyonukuliwa na vyombo vya habari tarehe 8 Machi 2012
kuwa mamlaka hiyo haiwezi kutoa bei elekezi ya maji kwa kuwa imekwishatoa tayari
mwaka 2010 haipaswi kukubaliwa na wananchi na wadau wa sekta ya maji katika
Jiji la Dar es salaam.
Katika taarifa hiyo niliitaka
EWURA kutimiza kwa ukamilifu wake wajibu wake kwa mujibu wa Sheria mbili muhimu
za usimamizi wa sekta ya maji nchini (Water Supply and Sanitation Act of 2009
and The Energy and Water Utilities Regulatory Authority Act)
Katika taarifa hiyo nilitoa mwito
kwa EWURA kutoa maelezo ya kina kuhusu hatua iliyofikiwa katika kuandaa kanuni
za usimamizi wa sekta binafsi ya maji juu ya mfumo wa bei elekezi na viwango
vya ubora kama ambavyo mamlaka husika iliahidi kwenye Kongamano la Maji Ubungo
mwaka 2011.
Pamoja na kutoa taarifa hiyo kwa
umma niliiandikia barua EWURA itimize
wajibu wake wa kusimamia ubora na bei hata hivyo nilipokea majibu kuwa muongozo
bado haujaandaliwa, hivyo mkutano huu wa tarehe 27 Septemba 2012 ni fursa
muhimu ya kuharakisha maandalizi ya kanuni na utaratibu husika.
Ufumbuzi wa kudumu wa kushusha
bei ya maji ni DAWASA na DAWASCO kuongeza uzalishaji, usafirishaji na
usambazaji hata hivyo udhibiti wa EWURA kuhusu ubora na bei katika kipindi hiki
cha upungufu ni muhimu kuepusha madhara kwa umma ya kuuziwa maji yasiyo na
ubora na kwa bei ya kuruka hali ambayo inawathiri zaidi wananchi wa kipato cha
chini.
Imetolewa tarehe 26 Septemba 2012
na:
John Mnyika (Mb)
Jimbo la Ubungo
COMMENTS