TAMKO LA MAASKOFU WA KANISA ANGLIKANA
TANZANIA KUHUSU KUNDI LA WAUMINI WA KANISA LA WATAKATIFU WOTE LA MJINI
SUMBAWANGA AMBALO LIMEKATAA KUMRUHUSU ASKOFU MATHAYO KASAGRA KUTOA HUDUMA
KWENYE MTAA HUO
Kikao cha Maaskofu kilichokutana tarehe
26 Septemba 2012 huko Mtumba, Dodoma kilitafakari kwa pamoja juu ya fujo
zilizojitokeza katika kanisa la Watakatifu Wote huko Sumbawanga tarehe 23
Septemba 2012 zilizosababishwa na kundi lisilotaka kumtambua Askofu Mathayo
Kasagara kwamba ni Askofu wa Kanuni wa Dayosisi ya Lake Rukwa na kutoa tamko
lifuatalo:
KWAKUWA kundi la waumini
wanaowakilishwa na Fulgence Rusunzu na Rojas Bendera wanaojitambulisha kuwa ni
viongozi wa Kamati ya Usimamizi wa Kanisa la Watakatifu Wote katika mji wa
Sumbawanga iliyo ndani ya Dayosisi ya Lake Rukwa ya Kanisa Anglikana
Tanzania inayowakilishwa na John M. Mahinya ambaye amekuwa akiandika barua kwa
niaba ya Kamati wamekataa kumtambua Askofu Mathayo Kasagara kuwa ni Askofu wa
Kanuni wa Dayosisi ya Ziwa Rukwa.
NA KWAKUWA viongozi hawa wa kundi hili
la waumini walifikisha suala hili kwenye Mahakama ya serikali ya Wilaya ya
Sumbawanga kupinga uhalali wa Uaskofu wa Askofu Kasagara na kuomba azuiliwe
kutoa kuhudumu yake ya kiaskofu
NA KWAKUWA Mahakama hii ya Wilaya
ilikwishatoa uamuzi wake uliomo kwenye Deed of Settlement uliokubaliwa
na pande zote mbili mbele ya Hakimu Mkazi Mheshimiwa M. W. Goroba tarehe 17
Januari 2012. Makubaliano ambayo yalitiwa saini na
Fulgence Rusunzu na Rojas Bendera kwa upande wa walalamikaji na Askofu Mathayo
Kasagara kwa upande wa walalamikiwa. Upande wa malalamikaji ukiwakilishwa na
kampuni ya uwakili ya S. Mawalla Law Consultants wa Sumbawanga na upande wa
walalamikiwa ukiwakilishwa na kampuni ya uwakili ya Albert Msando Legal
Consultants ya Arusha ambao wote walitia saini zao,
NA KWAKUWA uamuzi huo wa Mahakama kwa
kuzingatia kwamba Kanisa la Watakatifu Wote la mjini Sumbawanga ni mali ya
Wadhamini wa Kanisa Anglikana Tanzania (Maaskofu) na uliitaka Nyumba ya
Maaskofu wa Kanisa Anglikana Tanzania itoe uamuzi utakaohitimisha suala hili,
NA KWAKUWA Nyumba la Maaskofu wa Kanisa
Anglikana Tanzania linaheshimu maamuzi ya Mahakama za Serikali ingawa viongozi
wa kundi hili la waumini walivunja Katiba ya Kanisa kwa kukimbilia mahakamani
kabla ya kupitia hatua mbali mbali zilizomo kwenye Katiba ya Kanisa Anglikana
Tanzania, Maaskofu waliona vyema wasikilize kwanza hoja za waumini hao kabla ya
kutoa uamuzi wao na hivyo kutuma tume iliyokwenda Sumbawanga tarehe 23 Machi
2012 na kuwasikiliza
NA KWAKUWA kundi hilo lilishindwa kutoa
vielelezo vya kuthibitisha kwamba Askofu Mathayo Kasagara alitoa rushwa ili
achaguliwe kuwa Askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Lake Rukwa na hivyo kuifanya
Nyumba ya Maaskofu itoe uamuzi wa kuendelea kumtambua Askofu Kasagara kwamba ni
Askofu wa Kanuni wa Dayosisi ya Lake Rukwa,
NA KWAKUWA tarehe 23 Septemba 2012
kundi hili la waumini lilipinga uamuzi wa Nyumba ya Maaskofu wa kumtambua
Askofu Kasagara kuwa ni Askofu wa Kanuni wa Dayosisi ya Lake Rukwa uliosomwa
kwao na Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Rev Canon Dr Dickson
Chilongani, mbele ya Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, The Most Rev Dr
Valentino Mokiwa na Askofu wa Dayosisi ya Ruaha The Rt Rev Dr Joseph Mgomi,
ndani ya Kanisa la Watakatifu Wote,
KWA HIYO BASI NYUMBA YA MAASKOFU WA
KANISA ANGLIKANA TANZANIA INATOA TAMKO KUWA:
- Kulingana na Katiba ya Kanisa Anglikana Tanzania ya mwaka 1970 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004, kifungu cha 14 (8) Nyumba Ya Maaskofu imeridhika kabisa kwamba Askofu Kasagara ni Askofu halali wa Dayosisi ya Lake Rukwa. Kifungu hicho kinasomeka hivi: “Matokeo ya uchaguzi huo ni ya mwisho, hayatapingwa popote na taratibu za kumweka wakfu na kumsimika Askofu Mteule zitafuata.”Kifungu kinamaanisha kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Kanisa Anglikana Tanzania hakuna pingamizi lolote linalokubaliwa baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa. Kwa hiyo pingamizi la kundi hili la Watakatifu wote linakiuka Kifungu hiki cha Katiba kwavile liliibuka baada ya matokeo kutangazwa na tena halina uthibitisho wowote kwahiyo halina nguvu yoyote ya kisheria. Pia kifungu hiki kinazuia matokeo hayo kupingwa mahali popote. Hivyo basi masuala ya uchaguzi wa Askofu hayawezi kupelekwa katika mahakama za kidunia. Anayefanya hivyo au anayekusudia kufanya hivyo, kama ni Mkristo au Mhudumu anavunja Katiba ya Kanisa Anglikana Tanzania.
- Viongozi wa kundi hili la Waumini wanatakiwa wawasiliane na Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania ili wafanye utaratibu wa kukabidhi mali zote za Dayosisi ya Lake Rukwa kwa Wadhamini wa Kanisa Anglikana Tanzania kama zilivyoorodheshwa kwenye makubaliano yao na Mahakama (deed of settlement) ambayo walitia saini. Mali hizo ni pamoja na Kanisa la Watakatifu Wote, Ofisi ya Mchungaji, Nyumba mbili za Wachungaji, uwanja wa Kantalamba ulio na Nyumba ya Askofu na Chapel ya Askofu, jengo la ofisi ambalo halijakamilika, viwanja 14 vya kanisa vilivyopo eneo la Majumba Sita pamoja na St. Matthias English Medium School. Kukaidi kukabidhi mali hizi ni kukiuka maamuzi ya Mahakama, na Kanisa Anglikana Tanzania halitasita kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wa kundi hili.
- Nyumba ya Maaskofu inalitaka kundi hili la Wakristo wanaompinga Askofu Kasagara waelewe kwamba muumuni kuwa Mwanglikana ni suala la hiari na kama hakubaliani na mafundisho ya kanisa na maamuzi ya Maaskofu amejitenga yeye mwenyewe na kanisa na hivyo ni vyema akajitoa maana machoni mwa Kanisa yeye ni mwasi na si muumini tena wa Kanisa Anglikana.








0 comments:
Post a Comment