HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA MIZENGO PETER PINDA (MB), KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA ...
HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA
MIZENGO PETER PINDA (MB),
KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MATUMIZI
YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2013/2014
UTANGULIZI
Masuala ya Jumla
1.
Mheshimiwa Spika,
naomba kutoa Hoja kwamba kutokana na Taarifa zilizowasilishwa leo na Wenyeviti
wa Kamati za Katiba, Sheria na Utawala; Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa; na Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara na Kamati ya Masuala ya
UKIMWI na Dawa za Kulevya ndani ya Bunge lako Tukufu ambazo zimechambua Bajeti
ya Mafungu ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa
ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2012/2013 na Mwelekeo
kwa mwaka 2013/2014. Vilevile, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha
Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu -
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Taasisi zilizo chini yake pamoja na Ofisi
ya Bunge kwa mwaka 2013/2014.
2.
Mheshimiwa Spika,
awali ya yote napenda kumpongeza
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa kazi kubwa anayoifanya kwa maslahi ya Nchi yetu. Mheshimiwa Rais ameiletea
Tanzania sifa, heshima na kuiwezesha kutambulika zaidi Kimataifa katika Nyanja
mbalimbali. Ziara ya kihistoria ya Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya
Watu wa China aliyoifanya Nchini tarehe 24 hadi 25 Machi 2013 ni ushahidi tosha
wa kazi nzuri ya Mheshimiwa Rais ya kukuza ushirikiano wenye maslahi ya
kiuchumi kati ya Nchi yetu na Nchi nyingine. Katika ziara hiyo, Mikataba 16 ya
ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ilitiwa saini.
Utekelezaji wa Miradi hiyo utachochea uwekezaji na hivyo kuongeza kasi ya
ukuaji uchumi na kupunguza umaskini.
3.
Mheshimiwa Spika,
nawapongeza Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa kuwa Wenyeviti na Makamu
Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge. Vilevile, nawapongeza Waheshimiwa
Wabunge waliochaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika Taasisi mbalimbali za Kitaifa
na Kimataifa. Ni matumaini yangu kwamba wote walioteuliwa na kuchaguliwa
watatumia nafasi hizo kwa manufaa ya Bunge na kwa maendeleo ya Watanzania kwa
ujumla. Hongereni Sana!
4.
Mheshimiwa Spika,
niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na
Utawala inayoongozwa na Mheshimiwa Pindi
Hazara Chana, Mbunge wa Viti Maalum
na Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla, Mbunge
wa Nzega. Nawashukuru pia Wajumbe wa
Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara inayoongozwa na Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini na Kamati ya Masuala
ya UKIMWI na Dawa za Kulevya inayoongozwa na Mheshimiwa Lediana Mafuru Mng’ong’o Mbunge wa Viti Maalum. Kamati hizo zimetoa mchango mkubwa wakati wa
uchambuzi wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Mafungu ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na
Mfuko wa Bunge. Aidha, nawashukuru Wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge
lako Tukufu kwa ushauri waliotoa wakati wa kupitia Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali Zinazojitegemea na Mamlaka
za Serikali za Mitaa. Maoni na Ushauri wao utazingatiwa wakati wa kukamilisha mjadala
wa Bajeti ya Serikali na utekelezaji wake.
5.
Mheshimiwa
Spika,
katika kipindi cha mwaka 2012/2013, kumekuwa na majanga na matukio mbalimbali
yaliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali. Miongoni mwa matukio hayo
ni ajali mbaya ya Jahazi la Sunrise iliyotokea
Wangwi katika Bahari ya Hindi mwezi Januari 2013 na ajali mbalimbali za vyombo vingine
vya usafiri ambapo watu walipoteza maisha na wengine kupata majeraha. Hivi
karibuni pia tumeshuhudia ajali mbaya ya
kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 Jijini Dar es Salaam ambalo limesababisha vifo vya watu 34
na tukio linguine ni vifo 13 vilivyotokana
na kufukiwa na kifusi
cha ‘moram’ katika machimbo ya Mushono
Jijini Arusha. Aidha, tumempoteza ghafla Mbunge
mwenzetu, Mheshimiwa Salim Hemed Khamis,
Mbunge wa Chambani na baadhi yetu
tumepoteza Ndugu, wakiwemo wazazi na watoto kutokana na sababu mbalimbali. Wote nawapa Pole Sana!
Mzunguko Mpya wa Bajeti
6.
Mheshimiwa Spika, kuanzia
mwaka wa fedha 2013/2014, tumekubaliana kuanza Mzunguko Mpya wa Bajeti ambao
utatuwezesha kukamilisha mjadala wa Bajeti ya Serikali mapema. Lengo ni
kwamba ifikapo tarehe 30 Juni ya kila mwaka, taratibu zote za kuandaa,
kuchambua na kupitisha Bajeti ya
Serikali ziwe zimekamilika na utekelezaji wa Bajeti kuanza
ifikapo tarehe 1
Julai. Tofauti na miaka ya nyuma ambapo Bajeti ya Serikali ilikuwa ikijadiliwa na
kupitishwa kwanza na kufuatiwa na Bajeti za Kisekta, sasa makadirio na matumizi
ya Wizara yatajadilwa kwanza na hatimaye kuhitimishwa na majadiliano ya kina ya
Bajeti ya Serikali. Moja ya faida kubwa ya utaratibu huu mpya ni kwamba, mwaka
mpya wa fedha unapoanza utekelezaji wa
kazi za Serikali unaanza mara moja. Utaratibu huo utawawezesha Waheshimiwa
Mawaziri na Wabunge pamoja na Watendaji wa Serikali kurejea katika kazi zao na
kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Bajeti na Mpango wa Maendeleo. Kwa kuwa
tunaanza kwa mara ya kwanza kutumia utaratibu huo hazitakosekana dosari chache
ambazo zitafanyiwa kazi kadri tunavyoendelea
kuutumia.
Nawaomba Waheshimiwa Wabunge kutumia fursa hii kutoa
maoni na ushauri utakaosaidia kuboresha Bajeti ya Serikali ili iwe bora zaidi
na yenye maslahi makubwa kwa wananchi wetu.
7.
Mheshimiwa Spika,
maandalizi ya Bajeti yamezingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya
mwaka 2010; Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano; Malengo ya Maendeleo
ya Milenia na Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini.
Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali
chache tulizonazo ili kutekeleza Miradi ya Maendeleo ya Kipaumbele ambayo itachochea
ukuaji wa haraka wa uchumi.
8.
Mheshimiwa
Spika, nachukua
fursa hii kumpongeza sana Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bwana
Ludovick Utouh, pamoja na wafanyakazi wote wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa
kazi nzuri wanayoifanya ya kusimamia rasilimali za Serikali. Matunda ya kazi
hii yameonekana hadi nje ya Nchi na ndiyo maana Ofisi hii sasa imepandishwa
hadhi kutoka Daraja la Kwanza hadi la Tatu kwa vigezo vinavyotumiwa na Muungano
wa Ofisi za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali katika Bara la Afrika kwa Nchi
zinazotumia Lugha ya Kiingereza.
HALI YA SIASA
9.
Mheshimiwa
Spika,
Nchi yetu imepiga hatua ya kuridhisha katika kuimarisha Demokrasia ya Vyama
vingi. Kwa ujumla hali ya kisiasa Nchini ni tulivu na Vyama vya Siasa vinaendelea
kutekeleza majukumu yake. Idadi ya Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu
imefikia 20 baada ya Chama cha Alliance
for Democratic Change (ADC) kupata usajili wa kudumu. Chama cha Ukombozi wa
Umma (CHAUMA) kilipata usajili wa muda na zoezi la uhakiki wa wanachama
linaendelea. Chama cha Movement for
Democratic and Economic Change kilifutwa baada ya kukosa sifa za kupata
usajili wa kudumu.
10.
Mheshimiwa
Spika,
ili Demokrasia Nchini izidi kuimarika na Wananchi washiriki kikamilifu kwenye
siasa, Viongozi wote wa Vyama vya Siasa wana wajibu mkubwa wa kuendesha Siasa
za kistaarabu zinazozingatia maadili ya Kitanzania na kufuata Sheria, Kanuni na
Taratibu. Wito wangu kwa Vyama vyote ni kuendelea kuvumiliana na kutohamasisha
siasa za chuki au vurugu ambazo zitatugawa na kuhatarisha Amani, Utulivu na Umoja
wetu ambao umewekezwa kwa miaka mingi. Mwenye
Macho haambiwi Tazama. Wote ni mashahidi wa matatizo makubwa ambayo
yamezikumba Nchi zilizoingia katika siasa za chuki na vurugu.
11.
Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2013/2014, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itaandaa mapendekezo ya
kufanya mapitio ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama
za Uchaguzi ya mwaka 2010. Aidha, itaendelea na usajili wa Vyama vya Siasa,
kutoa elimu ya Demokrasia kwa Wananchi na kuboresha Baraza la Vyama vya Siasa.
Hatua hizo zitazidi kuimarisha Demokrasia ya Vyama Vingi Nchini.
ULINZI NA USALAMA
Hali ya Mipaka ya Nchi
12.
Mheshimiwa
Spika,
kwa ujumla hali ya mipaka ya Nchi yetu ni shwari na Wananchi wanafanya shughuli
zao bila vikwazo. Katika kuimarisha usalama wa mipaka yetu, Viongozi wa Mikoa ya
Kagera, Kigoma, Rukwa na Tanga wamefanya vikao vya ujirani mwema na
wenzao wa Mikoa
ya mipakani mwa Nchi za Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi, Zambia na Kenya. Pamoja na hali nzuri
ya usalama wa mipaka yetu, bado tunakabiliwa na changamoto ya Wahamiaji
haramu wanaotumia Nchi yetu
kama mapito ya kuelekea Nchi nyingine au kufanya makao Nchini. Ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali inaendesha
misako ya kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha kwenye Vyombo vya Sheria. Serikali pia, imeendelea kutoa elimu kwa
Wananchi wa Mikoa ya mipakani ili kutoa taarifa za Wahamiaji haramu. Natoa wito
kwa Wananchi wote kushirikiana na Serikali kuwabaini na kuwafichua wahamiaji
haramu na wale wanaowasafirisha ili wachukuliwe hatua stahiki za Kisheria.
Hali ya Uhalifu Nchini
13.
Mheshimiwa
Spika, Jeshi
la Polisi kwa kushirikiana na jamii kupitia dhana ya Ulinzi Shirikishi inafanya
kazi nzuri ya kudhibiti vitendo vya uhalifu Nchini. Jumla ya makosa makubwa ya
jinai yaliyotolewa taarifa katika Vituo vya Polisi Nchini yalipungua kutoka
69,678 mwaka 2011 hadi 66,255 mwaka 2012. Katika kipindi cha Januari hadi Februari
2013 makosa ya jinai yalikuwa 10,548 ikilinganishwa na makosa 10,989
yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Jeshi la Polisi pia
limedhibiti kwa kiasi kikubwa uingizaji wa silaha haramu ambapo jumla ya silaha
405 zilikamatwa katika operesheni mbalimbali kati ya Januari na Desemba 2012.
Natumia fursa hii kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri ya kutekeleza
kikamilifu dhana ya Ulinzi Shirikishi na kuwahamasisha Wananchi kuhusu Utii wa
Sheria bila Shuruti. Aidha, napenda kuwakumbusha Wananchi wote kwamba, suala la
Ulinzi na Usalama wa Nchi yetu ni jukumu letu sote. Ni wajibu wetu kutoa
taarifa za vitendo vya uhalifu kwa Jeshi letu ili hatua za kudhibiti vitendo
hivyo zichukuliwe.
Mauaji ya Kishirikina
14.
Mheshimiwa
Spika,
pamoja na juhudi za Serikali za kuwahudumia wazee na watu wenye ulemavu, siku
za karibuni kumeibuka tena dalili za vitendo vya ukatili dhidi ya wazee,
wanawake na walemavu wa ngozi katika baadhi ya Mikoa kwa sababu
za kishirikina. Ukatili huo siyo tu unyama uliopindukia kwa Binadamu wenzetu
bali pia unaondoa sifa kubwa ya jamii yetu ya
kupendana pasipo kujali rangi,
dini au kabila. Nitumie fursa hii kuwahakikishia
ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi, akina
mama na wazee kwamba, Serikali haitavumila kuona ukatili wowote unafanywa dhidi
yao.
Naziagiza
Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya zote Nchini kwa kushirikiana na
Jamii kuwabaini na kuwafikisha kwenye Vyombo vya Sheria wale wote
wanaojihusisha na vitendo hivyo viovu.
Migogoro ya Dini
15.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali imetoa uhuru kwa Wananchi wake kuabudu, kila mtu kwa Dini anayoitaka.
Hata hivyo, hivi karibuni kumejitokeza migongano na chokochoko za kidini ambazo
zimeanza kueneza chuki miongoni mwetu. Chokochoko zinazojitokeza si dalili
nzuri kwa mustakabali wa Nchi yetu inayopenda kudumisha Amani, Utulivu
na Umoja wa
Kitaifa.
Uzoefu
wa Mataifa mbalimbali umeonesha kwamba chokochoko za kidini zimesababisha machafuko
makubwa na kutoweka kwa amani katika Nchi hizo. Tukumbuke kwamba yakitokea
machafuko ya namna hiyo na kuvurugika kwa amani na utulivu, hakuna atakayesalimika.
Hivyo, natoa wito kwa Viongozi wa Madhehebu ya Dini kuelimisha Waumini wao
kuthamini na kuheshimu dini za wengine na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoamsha
hisia za chuki miongoni mwa wafuasi wa Dini mbalimbali.
Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa
16.
Mheshimiwa
Spika,
katika mwaka 2012/2013, Serikali iliahidi kukarabati na kujenga Makambi kwa
ajili ya kuchukua Vijana watakaojiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa
mujibu wa Sheria. Ninayo furaha kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa Serikali ya
Chama Cha Mapinduzi imetekeleza ahadi ilizotoa mwaka jana kwa ufanisi mkubwa.
Mafunzo ya JKT kwa mujibu wa Sheria yameanza mwaka huu kwa kuchukua Vijana
4,711 sambamba na Vijana 5,893 wa kujitolea wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa
Wabunge. Nitumie fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge vijana waliojiunga
na mafunzo ya JKT mwaka huu. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea
kuchukua vijana kwa ajili ya mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria.
SHUGHULI ZA UCHAGUZI, BUNGE, VITAMBULISHO VYA TAIFA, SENSA NA MUUNGANO
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
17.
Mheshimiwa
Spika,
katika mwaka 2012/2013, Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliendesha Chaguzi Ndogo za
Madiwani katika Kata 29 Tanzania Bara ili kujaza nafasi wazi za Viti vya
Udiwani. Katika chaguzi hizo, Chama Cha Mapinduzi kilishinda Viti 22, CHADEMA
Viti 5 na CUF na TLP Kiti kimoja kimoja. Vilevile, Tume ilifanya teuzi 15 ili
kujaza nafasi zilizokuwa wazi za Udiwani wa Viti Maalum. Katika uteuzi huo, CCM
ilipata viti 10, CHADEMA viti vinne na TLP kiti kimoja. Katika mwaka 2013/2014,
Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaboresha Daftari la Wapiga Kura ambapo Awamu ya
Kwanza itakamilika mwezi Desemba, 2013. Uboreshaji huo utawezesha kuchapishwa
kwa Daftari la Wapiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka
2014 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
18.
Mheshimiwa
Spika, uchaguzi
wa Serikali za Mitaa ngazi ya Vitongoji, Vijiji na Mitaa unatarajiwa kufanyika mwezi
Oktoba 2014. Kazi za awali za uchaguzi huo zinaendelea kufanyika ikiwa ni
pamoja na kupitia upya Kanuni za Uchaguzi zitakazojumuisha maoni ya wadau
mbalimbali. Ili kufanikisha uchaguzi huo, Halmashauri zote Nchini zinatakiwa
kuanza maandalizi mapema kwa kupitia na kuhakiki orodha ya Vitongoji, Vijiji na
Mitaa. Baada ya kuhakiki orodha hiyo, maombi
mapya ya kugawa Vitongoji, Vijiji au Mitaa yawasilishwe katika ngazi husika kabla
ya tarehe 31 Desemba 2013 kwa kuzingatia Sheria na Taratibu zilizopo.
Shughuli za Bunge
19.
Mheshimiwa
Spika,
katika mwaka 2012/2013, Bunge limeendelea kutekeleza majukumu yake ya kuisimamia
na kuishauri Serikali katika nyanja mbalimbali. Aidha, Bunge limefanya Mikutano
mitatu, kupitisha Miswada minne ya Sheria
na kuridhia Maazimio nane. Katika kuboresha utendaji wa
Kamati za Kudumu za Bunge, Wajumbe wa Kamati hizo walipatiwa mafunzo ya
kuwajengea uwezo ili kumudu majukumu yao vizuri katika nyanja za utafiti, uchambuzi
wa Miswada, Sera na Bajeti, utunzaji wa kumbukumbu na taratibu za uendeshaji wa
Bunge. Vilevile, kuanzia tarehe 4 hadi 7 Desemba 2012 Bunge liliandaa kwa mafanikio
Mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani uliofanyika Dar es Salaam ukiwa na kauli
mbiu ya “Vita dhidi ya Ukatili wa Wanawake”.
20.
Mheshimiwa
Spika,
ili kuimarisha utendaji na kuongeza ufanisi, Kamati za Kudumu za Bunge
zimefanyiwa mabadiliko makubwa kwa kuunda Kamati mpya ya Bajeti na kugawanya
baadhi ya Kamati. Iliyokuwa Kamati ya
Nje, Ulinzi na Usalama imegawanywa mara mbili na kuwa Kamati ya Mambo ya Nje na
Kamati ya Ulinzi na Usalama. Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala
imegawanywa na kuwa Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala na Kamati ya Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa. Vilevile,
Kamati zilizokuwepo awali nazo zimeundwa upya na baadhi kuongezewa majukumu. Ni
imani yangu kwamba Kamati hizo, zitatekeleza wajibu wake kikamilifu kwa maslahi
ya Taifa.
Muungano
21.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2012/2013, Serikali imeendelea kuratibu masuala yote ya Muungano na
yasiyo ya Muungano kwa lengo la kudumisha Muungano na ushirikiano wa Serikali zote mbili. Katika kudumisha ushirikiano huo, Kikao
cha Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ cha kushughulikia Masuala ya Muungano kilifanyika
na kujadili Hoja zinazohusu utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia;
ushiriki wa Zanzibar katika Taasisi za Nje na katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki; Ongezeko la gharama za umeme wa TANESCO kwa ZECO; Usajili wa vyombo
vya moto, malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili na
mgawanyo wa mapato.
Mabadiliko ya Katiba
22.
Mheshimiwa Spika,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaendelea kuratibu, kukusanya na kuchambua maoni
ya Wananchi ili kupata Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inayotokana na ridhaa ya Wananchi wenyewe ifikapo mwaka 2014. Katika mwaka
2012/2013, Tume imekusanya maoni ya Wananchi kupitia njia mbalimbali na kuanza
uchambuzi wa maoni yaliyotolewa ili kuandaa Rasimu ya Katiba. Tume pia, imeanza
maandalizi ya kuunda Mabaraza ya Katiba katika Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za
Mitaa na Mabaraza ya Katiba yanayojumuisha Asasi, Taasisi na Makundi Maalum ya Watu.
Mabaraza hayo yatakuwa na jukumu la kupitia na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba
iliyoandaliwa na Tume. Mabaraza ya Katiba yatawashirikisha na kuwakutanisha
wawakilishi kutoka makundi mbalimbali ya wananchi katika jamii.
23.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2013/2014, Tume itaratibu, Mikutano ya Mabaraza ya Katiba Mpya, kuchambua
maoni ya Mabaraza ya Katiba
na kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya
itakayowasilishwa katika Bunge Maalum la Katiba. Vilevile, itachapisha Katiba
iliyotokana na maoni ya Bunge Maalum la Katiba kwa ajili ya kupigiwa Kura ya
Maoni. Naipongeza sana Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kazi nzuri waliyoifanya
hadi sasa. Nawasihi Watanzania wote kuendelea kutoa ushirikiano kwa Tume ili
iweze kukamilisha kazi hii muhimu kwa Taifa letu.
Sensa ya Watu na Makazi 2012
24.
Mheshimiwa
Spika,
mwaka 2012 ulikuwa ni mwaka wa Sensa ya Watu na Makazi ambayo ni ya tano
kufanyika tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Matokeo yanaonesha kuwa idadi ya watu Nchini
imeongezeka kutoka watu milioni 34.5 mwaka 2002 hadi milioni 44.9 mwaka 2012.
Hilo ni ongezeko la watu Milioni 10.4 kwa kipindi cha miaka kumi, sawa na
ukuaji wa wastani wa Asilimia 2.7 kwa mwaka. Kwa ujumla matokeo ya Sensa
yanaonesha kasi ya ongezeko la watu ni kubwa ikilinganishwa na kasi ya ukuaji
wa Pato la Taifa. Kwa kutambua changamoto hiyo, Serikali pamoja na mambo
mengine inaendelea kutekeleza Sera ya Idadi ya Watu ya mwaka 2006 kwa
kuelimisha Wananchi kuhusu umuhimu wa Uzazi wa Mpango. Nitumie fursa hii
kulikumbusha Bunge lako Tukufu na Watanzania kazi ya uchambuzi wa takwimu inaendelea
ili kupata mchanganuo wa kina zaidi utakaoiwezesha Serikali kupanga vizuri Mipango
yake ya Maendeleo. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itasambaza taarifa
mbalimbali za Sensa ya Watu na Makazi zenye mchanganuo wa kitakwimu na kuhamasisha
matumizi yake katika tafiti na kuandaa
Mipango ya Maendeleo katika ngazi zote.
Vitambulisho vya Taifa
25.
Mheshimiwa
Spika, Tarehe
07 Februari 2013, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania alizindua rasmi Mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Watu,
Jijini Dar es Salaam. Vilevile, tarehe 13 Februari 2013, Mheshimiwa Dkt. Ali
Mohamedi Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
alizindua Zoezi hilo kwa upande wa Zanzibar. Kuzinduliwa rasmi kwa mfumo huo ni
mwanzo wa utoaji wa Vitambulisho vya Taifa ambavyo vitasaidia kuwatambua na
kuwahudumia Wananchi ipasavyo. Zoezi la utoaji wa Vitambulisho vya Taifa
linaendelea kwa watumishi wa umma waliokuwa wamesajiliwa na kuhakikiwa. Zoezi
la kuingiza taarifa za Wananchi 220,000 kwa ajili ya kupatiwa Vitambulisho vya
Taifa katika Wilaya ya Kilombero iliyoteuliwa kuwa Wilaya ya mfano limekamilika
na uchambuzi wa taarifa za Wakazi wa Dar es Salaam 2,159,822 waliojiandikisha
zinaendelea. Aidha, Wakaazi wa Zanzibar 160,645 na Wageni 180 wameandikishwa.
Kazi ya Utambuzi na Usajili wa Watu katika Mikoa mbalimbali Nchini inaendelea
sambamba na utoaji wa Vitambulisho kwa wale walioandikishwa na kuhakikiwa.
MASUALA YA UCHUMI
Hali ya Uchumi
26.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012, Pato halisi la Taifa lilikua
kwa Asilimia 6.9 ikilinganishwa na ukuaji wa Asilimia 6.4 mwaka 2011. Sekta
zilizochangia zaidi katika ukuaji huo ni
pamoja na Mawasiliano, Fedha, Viwanda, Ujenzi, Madini, Biashara na Utalii.
Kutokana na ukuaji huo, Wastani wa Pato la Mtanzania umeongezeka kutoka Shilingi 869,436 mwaka 2011 hadi
Shilingi 995,298 mwaka 2012, sawa na ongezeko la Asilimia 12.6. Mfumuko wa Bei
umepungua kutoka Asilimia 19.4 mwezi Februari 2012 hadi Asilimia 9.8 mwezi Machi 2013.
Kupungua kwa Mfumuko wa Bei kumechangiwa na jitihada za Serikali za kuongeza usambazaji
wa vyakula kwenye masoko, kupunguza ujazi wa fedha kwenye soko, kudhibiti
upandaji wa bei ya mafuta ya petroli na kuimarika kwa upatikanaji wa umeme
viwandani ikilinganishwa na mwaka 2011/2012.
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
27.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao ulipitishwa na Bunge lako
Tukufu Mwaka 2011/2012. Katika
kutekeleza Mpango huo, Tume ya Mipango imeweka utaratibu wa kuchambua
kwa kina maandiko ya miradi yote ya kisekta ili kuhakikisha kwamba imezingatia vipaumbele
ambavyo sote tumekubaliana. Baada ya uchambuzi huo, ndipo fedha hutolewa kwa ajili
ya utekelezaji. Pamoja na utaratibu huo, Serikali imeona ni muhimu kuongeza
kasi ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa kuanzisha Mfumo imara zaidi wa
kupanga Vipaumbele, kufuatilia na kutathmini Utekelezaji wa Miradi ya Kimkakati
ya Maendeleo. Mfumo huo ambao utasimamiwa na Chombo Maalum (President’s Delivery Bureau) chini ya
Ofisi ya Rais, Ikulu, unazingatia uzoefu wa Nchi ya Malaysia. Chini ya Mfumo
huo, Miradi ya kipaumbele itakayotekelezwa itatengewa fedha za kutosha na usimamizi
wa kina utafanyika kuhakikisha kwamba malengo yaliyowekwa yanafikiwa.
28.
Mheshimiwa Spika, ili Mfumo huo ufanikiwe inabidi kwanza wadau wote
wakubaliane kimsingi vipaumbele ambavyo vitatoa matokeo makubwa na ya haraka na
kisha wataalamu kutoka Serikalini, Sekta Binafsi na Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali kukaa pamoja na kuchambua kwa undani vipaumbele hivyo, namna ya
kuvitekeleza, kubaini watekelezaji na kuibua viashiria vya kupima matokeo.
Tayari zoezi hilo la awali limefanyika ambapo maeneo sita ya kwanza ya
kipaumbele yamefanyiwa uchambuzi wa kina kwa utaratibu unaojulikana kama Maabara
(Labs). Utaratibu huo wa maabara
unatoa fursa kwa wataalam na watunga Sera kukaa pamoja, kufikiri na kuendesha
majadiliano ya wazi hadi pale wanapokubaliana kwamba ufumbuzi
wa tatizo umepatikana.Maeneo yaliyojadiliwa
katika awamu ya kwanza ni Nishati na Gesi Asilia, Uchukuzi, Kilimo, Elimu, Maji
na Kupanua wigo wa Mapato ya Serikali. Baada ya uchambuzi huo kukamilika,
matokeo yake ikiwemo miradi iliyoandaliwa pamoja na Bajeti ya utekelezaji itawekwa
hadharani ili kila Mtanzania ajue kitakachofanyika, kutoa maoni na kufuatilia
kwa kina utekelezaji.
29.
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kwamba kunakuwepo na uwajibikaji wa
kutosha katika kutekeleza vipaumbele vya Kitaifa, Chombo kitakachoanzishwa (President’s Delivery Bureau) kitakuwa na
jukumu la kuhakikisha kwamba kila Waziri wa Kisekta na Watendaji Wakuu wanawajibika
kusimamia utekelezaji wa miradi ya
kipaumbele na pia kufanya tathmini za mara kwa mara kupima matokeo. Napenda
kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Mawaziri wanaosimamia maeneo sita ambayo
tumeanza nayo walitoa ahadi kwamba watakuwa mstari wa mbele kusimamia kwa
weledi utekelezaji wa miradi ya Sekta
zao. Ahadi hizo walizitoa wakati wa uzinduzi wa awamu ya kwanza ya mfumo wa maabara
uliofanywa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania tarehe 22
Februari 2013. Ni matumani yangu kuwa,
utaratibu huo utasaidia sana kuimarisha uwajibikaji, ufuatiliaji na hatimaye
kupata matokeo ya haraka ambayo yatasaidia uchumi kukua kwa
kasi
zaidi na hivyo kupunguza umaskini miongoni mwa watu wetu. Ni vyema ieleweke wazi kwamba, maeneo ya
kipaumbele yaliyochaguliwa yatapata sehemu kubwa ya fedha za maendeleo. Hii
ndiyo maana ya dhana ya kupanga ni
kuchagua na haina maana kwamba kazi nyingine za uendeshaji wa Serikali zitasimama.
Katika Mwaka 2013/2014, kutafanyika uchambuzi wa kina wa maeneo mengine ya
kipaumbele ambayo yatasaidia Serikali kupanga Bajeti ya Maendeleo kwa mwaka
2014/2015.
Maendeleo ya Sekta Binafsi na Uwekezaji
30.
Mheshimiwa Spika,
Serikali inaratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya
Biashara na Uwekezaji Nchini. Lengo ni kuimarisha ushiriki wa Sekta Binafsi
katika shughuli za uwekezaji na Biashara Nchini. Katika utekelezaji wa Mpango
Kazi huo, Serikali imeazimia kupunguza muda unaotumika kupitisha mizigo
Bandarini na Mipakani kwa kuanzisha utaratibu wa kubadilishana taarifa
zinazohusu mizigo kwa njia za kielektroniki kabla mizigo haijafika kwenye Vituo
vya Forodha. Vilevile, Kamati za Pamoja (Joint
Border Post Committees) zimeundwa kwenye Vituo vya Mipakani vya Tunduma,
Kabanga, Mutukula, Holili, Sirari na Namanga. Kupitia Kamati hizo wadau wote
wanaoshughulika na utoaji huduma mipakani hufanya kazi kwa pamoja.
31.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imekamilisha Mkakati na Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Sera ya Ubia
baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP). Vilevile, Mwongozo wa Utendaji
kwa ajili ya kutekeleza Sera, Sheria na Kanuni za Ubia baina ya Sekta ya Umma
na Sekta Binafsi umekamilika. Aidha, Serikali imefanya tathmini ya Sera
zinazohusu Uwekezaji kwa kutumia Mfumo wa Tathmini unaotumiwa na Shirika la
Kimataifa la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD). Taarifa ya tathmini
ya Sera hizo itachangia katika kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya
mwaka 1996 pamoja na Sheria yake ya mwaka 1997. Nazihimiza Wizara na Taasisi za
Serikali kuongeza juhudi katika kuainisha miradi inayokidhi vigezo vya
kutekelezwa kwa utaratibu wa PPP ili Nchi iweze kunufaika na fursa zinazotokana
na utaratibu huo.
32.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kuratibu majadiliano baina ya Sekta ya Umma na Sekta
Binafsi ili kuibua fursa zilizopo na kupata ufumbuzi wa changamoto za kisera, kisheria
na kitaasisi zinazokwamisha biashara na uwekezaji. Kutokana na umuhimu wa
majadiliano hayo, Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa “Majadiliano ya Ushirikiano kwa
Manufaa ya Wote wa mwaka 2013” (Global 2013 Smart Partnership Dialogue) utakaofanyika mwezi Julai 2013, Jijini
Dar es Salaam. Maandalizi ya Mkutano huo yanaendelea ambapo Mkutano maalum kwa
Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Makatibu Tawala wa Mikoa ulifanyika mjini Dodoma
mwezi Novemba 2012. Katika Mkutano huo, washiriki walipata uelewa wa pamoja wa
dhana ya majadiliano ya ushirikiano kwa manufaa ya wote yatakayowasaidia
kusimamia majadiliano katika maeneo yao.
33.
Mheshimwa Spika,
Serikali imetoa mwongozo kwa Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya kuendesha
majadiliano katika maeneo yao ili matokeo ya majadiliano hayo yatumike
kikamilifu wakati wa majadiliano ya Kimataifa mwezi Julai 2013. Uzoefu wa Nchi
ambazo zimeandaa majadiliano kama hayo umeonesha kwamba kuna manufaa makubwa
yakiwemo kubaini wagunduzi na wabunifu, kuibua fursa mpya za teknolojia na uwekezaji
na pia kupata uzoefu wa Mataifa mengine katika masuala mbalimbali. Natoa wito
kwa Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya kuendesha majadiliano katika maeneo
yao na kujiandaa kikamilifu kushiriki katika Mkutano huo.
34.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha Januari 2012 hadi Desemba 2012, Kituo cha
Uwekezaji Tanzania kilisajili Miradi 869 yenye thamani inayokadiriwa kufikia
Shilingi Bilioni 30,866. Kati ya miradi hiyo, Miradi 469 sawa na Asilimia 54 ni
miradi ya wawekezaji wa ndani, Miradi 195 sawa na Asilimia 22 ni ya ubia kati
ya wawekezaji wa ndani na Nje na Miradi 205, sawa na Asilimia 24 ni ya wawekezaji
kutoka Nje. Usajili
wa miradi hiyo umeongeza ajira Nchini ambapo zaidi ya Watanzania 174,412
walipata ajira kwenye miradi hiyo. Tathmini ya thamani ya uwekezaji kisekta inaonesha kwamba katika mwaka 2012 miradi ya
Sekta ya Kilimo inaongoza ikiwa imechangia Shilingi Bilioni 14,226 ikifuatiwa
na Sekta ya Uzalishaji Viwandani iliyochangia
Shilingi Bilioni
4,672. Sekta hizo zinafuatiwa na Sekta ya Mawasiliano iliyochangia Shilingi Bilioni
4,663 na Sekta ya Nishati iliyochangia Shilingi Bilioni 2,110. Pamoja na
mafanikio hayo, bado kuna changamoto kubwa ya kufanya kazi kama Timu moja
katika kuvutia wawekezaji. Ili kuweza kuvutia wawekezaji katika hali endelevu,
ni muhimu sana Sera na Sheria za Uwekezaji zikatoa Mwongozo ambao unatabirika
kwa muda mrefu.
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
35.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeratibu na kufanya tathmini ya Mifuko mbalimbali ya Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi. Mifuko hiyo ni pamoja na Mfuko wa Uwezeshaji wa Mwananchi,
Mpango wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira, SIDO, SELF, Agriculture Input Trust Fund na Presidential Trust Fund. Mifuko mingine ni Mfuko wa Maendeleo ya
Vijana, Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Mauzo
ya Nje na Mfuko wa Kudhamini Taasisi za Fedha Kutoa Mikopo kwa Miradi Midogo na
ya Kati. Katika Makubaliano yaliyofikiwa baina ya Serikali na
Taasisi za Fedha zilizoteuliwa kutoa mikopo kwa wajasiriamali ni kwamba Taasisi
hizo zikopeshe mara tatu zaidi ya dhamana iliyotolewa na Serikali. Katika
kutekeleza makubaliano hayo, hadi Desemba 2012 Mpango wa Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi na Kuongeza Ajira ulitoa mikopo kwa Wajasiriamali 76,546 yenye thamani
ya Shilingi Bilioni 50.06. Urejeshaji wa
mikopo hiyo umefikia wastani wa Asilimia
82. Aidha, katika kipindi hicho, Mfuko
wa Uwezeshaji wa Mwananchi umetoa mikopo ya Shillingi Bilioni 8.6 kwa Mikoa 11,
Wilaya 27, Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOs) 49 na Wajasiriamali 8,497.
Ufuatiliaji wa maendeleo ya Mifuko mbalimbali ya Uwezeshaji unaonesha kuwa
Wananchi waliopata mikopo wameweza kupiga hatua za kimaendeleo kwa kuongeza
tija na uzalishaji katika shughuli zao na hatimaye kuongeza kipato na kuboresha
hali zao za maisha.
36.
Mheshimiwa Spika,
utekelezaji wa awamu ya pili ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulikamilika
mwaka 2012. Tathmini ya utekelezaji imeonesha kwamba TASAF imetoa mchango
mkubwa katika kuwezesha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo Vijijini
iliyoibuliwa na Wananchi. Katika utekelezaji wa awamu hiyo, jumla ya Miradi
1,010 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 20 iliibuliwa na kuwezeshwa katika Wilaya za Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha, mafunzo ya ujasiriamali yalitolewa kwa Vikundi 1,778 vyenye wanachama
22,712 katika Halmashauri 44 kwa lengo la kuviimarisha ili kuongeza ufanisi
zaidi katika shughuli zao.
37.
Mheshimiwa Spika,
kutokana na mafanikio hayo, tarehe 15 Agosti 2012, awamu ya tatu ya TASAF ilizinduliwa
Mjini Dodoma na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Awamu hiyo itakayogharimu jumla ya Shilingi Bilioni 440
inatekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
Zilizo Katika Mazingira Hatarishi. Mpango
huo unalenga kuziwezesha kaya maskini kupata chakula na kujiongezea fursa
za kipato kwa kuzipatia fedha ili kumudu mahitaji ya msingi kama vile lishe bora,
huduma za afya na elimu. Mpango huo utakaotekelezwa kwa awamu katika
Halmashauri zote Tanzania Bara na Zanzibar, umeanza kwa utambuzi wa Kaya
maskini katika Vijiji 20 vya Halmashauri ya Bagamoyo ambapo jumla ya Kaya 3,056
zimetambuliwa. Zoezi hilo linaendelea kwenye Halmashauri nyingine 13 na ifikapo
Juni 2014, Halmashauri zote Nchini zitafikiwa.
UZALISHAJI MALI
Kilimo cha Mazao ya Chakula na Biashara
38.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inatekeleza mipango na mikakati
mbalimbali ya kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. Hatua
hizo ni pamoja na kutekeleza Azma ya KILIMO KWANZA, Programu ya Kuendeleza
Sekta ya Kilimo (ASDP), Mpango wa Utoaji wa Ruzuku ya Pembejeo na Dawa za
Kilimo, Programu ya Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Programu Kabambe ya Kuendeleza
Kilimo Barani Afrika (Comprehensive
Africa Agriculture Development Programme – CAADP) na kuboresha huduma za
ugani na utafiti katika Sekta ya Kilimo. Hatua nyingine ni pamoja na kuvutia
Wawekezaji katika Sekta ya Kilimo, kuhimiza Kilimo cha Umwagiliaji, kuongeza
fursa za upatikanaji wa zana bora za kilimo hasa matrekta, kuimarisha masoko na
kurahisisha upatikanaji wa mitaji kutoka Vyombo vya Fedha, hususan kupitia
Dirisha la Kilimo katika Benki ya Maendeleo Tanzania.
39.
Mheshimiwa
Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa
jitihada za kuendeleza Kilimo zimeanza kuleta matumaini hasa katika kuongeza
upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo na kuongeza tija na uzalishaji. Kwa mfano,
katika mwaka 2012/2013, Tani 226,092 za mbolea zilifikishwa
kwa Wakulima 3,792,000 Nchini na upatikanaji wa
mbegu bora ulifikia Tani 30,443 ikilinganishwa na Tani 28,612 zilizozalishwa
mwaka 2011/2012. Kutokana na ongezeko la
matumizi ya mbolea na Wakulima kuzingatia Kanuni za Kilimo Bora, tija anayopata
mkulima katika zao la mahindi chotara kwa sasa ni Wastani wa Tani 3.9 kwa hekta
na tija ya uzalishaji wa zao la mpunga ni Tani 3.8 kwa hekta katika maeneo ya
umwagiliaji.
40.
Mheshimiwa
Spika, Serikali ilianza kutekeleza Mpango wa utoaji
ruzuku ya mbolea na mbegu bora kwa kutumia utaratibu wa Vocha mwaka 2008/2009.
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana kutokana na utaratibu huo, hasa kuongezeka
kwa upatikanaji na matumizi ya mbolea na
mbegu bora pamoja na tija katika
uzalishaji wa mazao ya kilimo, mpango huo umekuwa na changamoto kadhaa. Changamoto
zilizojitokeza ni pamoja na mbolea na Vocha kuchelewa kufika kwa walengwa;
uteuzi wa Mawakala usiozingatia vigezo na udanganyifu uliofanywa na baadhi ya Mawakala
kwa kushirikiana na Watumishi wasio waaminifu pamoja na Wajumbe wa Kamati za
Pembejeo katika ngazi mbalimbali za utekelezaji. Serikali imechukua hatua kwa
kufanya ukaguzi maalum kwenye maeneo yaliyokuwa na upungufu huo na waliobainika
kuhusika na udanganyifu wamefikishwa kwenye Vyombo vya Sheria.
41.
Mheshimiwa
Spika, mwaka jana Serikali iliahidi kufanya mapitio ya
Mfumo wa utoaji wa mbolea ya ruzuku na mbegu bora kwa kutumia utaratibu wa Vocha
ili kuondoa upungufu uliojitokeza. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa,
Serikali imeboresha mfumo huo na kuanzia mwaka 2013/2014 ruzuku ya pembejeo za
kilimo itatolewa kwa Mikopo kupitia Vikundi vya Wakulima.
Umwagiliaji
42.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali imepanua eneo la
Kilimo cha Umwagiliaji Nchini. Miongoni mwa kazi zilizotekelezwa ni pamoja na
ujenzi wa miundombinu katika skimu 21 za umwagiliaji zenye eneo la hekta
19,567. Kazi nyingine zinazoendelea ni kukamilisha ujenzi wa Mabwawa matano ya Umwagiliaji
ya Mahiga (Kwimba); Inala (Tabora); Lwanyo (Mbarali); Mesaga (Serengeti) na
Dongobesh (Mbulu). Miradi mingine iliyotekelezwa ni Skimu 34 zenye eneo la
Hekta 17,824 kwa kutumia Mfuko wa Wilaya wa Kuendeleza Umwagiliaji. Katika
mwaka 2013/2014, Serikali itaanza ujenzi wa mabwawa matatu ya Idodi (Iringa);
Manyoni (Singida) na Masengwa (Shinyanga Vijijini).
Kilimo cha Matunda na Mboga
43.
Mheshimiwa
Spika, Kilimo cha matunda na mboga kina mchango mkubwa
katika ukuaji uchumi, fursa za ajira, lishe na kupunguza umaskini. Kwa
kuzingatia umuhimu huo, Serikali
inatekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kuendeleza Mazao ya Bustani wa mwaka
2010/2011 – 2020/2021. Utekelezaji wa Mkakati huo unaolenga kukuza uwekezaji
katika mnyororo wa thamani wa mazao ya bustani; ujenzi wa miundombinu; uhifadhi
bora wa Mazao ya Bustani; ujenzi na utafutaji
wa masoko; na ukuzaji rasilimali watu umeanza kuonesha matokeo mazuri.
Uzalishaji wa mazao ya bustani umeongezeka kutoka Tani milioni 4.1 mwaka
2009/2010 hadi Tani milioni 5.1 mwaka 2012/2013 na mauzo ya mazao hayo nje ya
Nchi yameongezeka kutoka Shilingi Bilioni 159.8 mwaka 2009 hadi Bilioni 602.1
mwaka 2012. Mafanikio haya ni ya kuridhisha ingawa bado kuna fursa kubwa ya
kuongeza tija na ufanisi katika sekta hii. Tayari tunao Mwongozo wa Kilimo cha
Embe ambao utatuwezesha kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo. Miongozo ya
Uzalishaji bora wenye tija kwa mazao mengine ya bustani itaandaliwa. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itatoa
mafunzo ya teknolojia za uzalishaji wa miche bora ya mazao ya bustani hususan
kwa vikundi vya Vijana.
Mwenendo Wa Bei Za Mazao Makuu
44.
Mheshimiwa
Spika, mwenendo wa bei za mazao makuu ya biashara Nchini
ambayo ni Pamba, Kahawa, Chai, Tumbaku, Korosho, Katani na Pareto umekuwa
ukibadilika mara kwa mara kwa kutegemea bei za Soko la Dunia. Mabadiliko hayo
yanawaathiri sana wakulima wetu pale bei zinaposhuka. Kutokana na hali hiyo,
Serikali ilikutana na Wadau wa mazao makuu asilia ya biashara Nchini ili kuangalia
uwezekano wa kuanzisha Mfuko Maalum wa kufidia bei za Mazao kwa wakulima pale
zinaposhuka (Price Stabilization Fund).
Lengo ni kuwawezesha wakulima kupata bei nzuri ya mazao na kuwaepusha na hasara
inayotokana na kushuka kwa bei hizo katika masoko ya kimataifa na pia
kuwahamasisha wakulima kuendelea kulima mazao husika. Serikali kwa kushirikiana
na Wataalam kutoka Bodi Sita za mazao inayafanyia kazi maoni ya wadau kuhusu
kuanzisha Mfuko Maalum wa Kufidia Bei za mazao.
45.
Mheshimiwa
Spika, mwezi Septemba na Novemba 2012, niliongoza Mikutano
mikubwa iliyolenga kuwaleta pamoja Watunga Sera, Washirika wa Maendeleo na
Wawekezaji ili kujadili fursa na changamoto mbalimbali za Sekta ya Kilimo.
Katika Mikutano hiyo, wadau waliandaa na kukubaliana Mpango Kazi ulioainisha
majukumu yatakayotekelezwa na kila mdau ili kuongeza uwekezaji katika Ukanda wa
SAGCOT. Majukumu ya Serikali ni pamoja
na upimaji ardhi kwa ajili ya kilimo, ujenzi wa miundombinu ya msingi na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha
uwekezaji katika Sekta ya Kilimo. Serikali imechukua hatua kwa kuainisha na
kuweka mipaka ya ardhi kwa kuanzia na Wilaya za Kilombero, Ulanga na Rufiji.
Zoezi hilo la kuanisha ardhi limelenga kutoa kipaumbele cha kwanza katika
upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya wakulima wadogo. Hadi sasa ardhi ya Vijiji
100 katika Wilaya ya Kilombero imepimwa.
46.
Mheshimiwa
Spika, wawekezaji wengi wa ndani na nje ya Nchi wameonesha
mwamko mkubwa wa kuwekeza katika ukanda wa SAGCOT. Msisitizo wa Serikali ni
kwamba kila mwekezaji mkubwa atakayewekeza atalazimika kuwa na Mpango wa
kuendeleza na kushirikiana na wakulima wadogo. Hatua hiyo itamsaidia mkulima
mdogo kupata teknolojia mpya, uhakika wa pembejeo, miundombinu ya umwagiliaji
pamoja na soko la uhakika. Tayari utaratibu wa namna hiyo umeanza kuonesha
matokeo mazuri Wilayani Kilombero.
47.
Mheshimiwa
Spika, katika hatua nyingine, Washirika wa Maendeleo ambao ni Shirika la Maendeleo la Marekani,
Umoja wa Ulaya na Shirika la Maendeleo la Uingereza wamekubali kusaidia ujenzi
wa barabara yenye urefu wa Kilometa 103 kwa kiwango cha lami ambayo itaunganisha
Mikumi na Ifakara katika Bonde la Kilombero. Hatua za awali za ujenzi wa
barabara hiyo zimeanza. Kukamilika kwa barabara hiyo muhimu kutafungua fursa
zaidi za uwekezaji na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao ya wakulima.
Nitumie fursa hii kuwashukuru kwa dhati Washirika wetu hao wa Maendeleo kwa
kukubali kusaidia utekelezaji wa mradi huo.
Miundombinu ya Masoko ya Mazao
48.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuendeleza
miundombinu ya masoko ya mazao kama moja ya mkakati madhubuti wa kumrahisishia mkulima kufikisha mazao yake sokoni
na kuongeza bei ya mazao hayo. Chini ya
Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha
Vijijini, Serikali, imekamilisha usanifu na kutangaza zabuni za ujenzi wa
barabara zenye
jumla ya Kilometa 210.8 katika Halmashauri za Mbulu, Njombe, Iringa
Vijijini, Kahama, Lushoto, Rufiji, Songea Vijijini na Singida Vijijini. Aidha,
zabuni kwa ajili ya ujenzi wa maghala mawili katika Halmashauri za Wilaya ya
Iringa Vijijini na Njombe zimetangazwa na taratibu za ujenzi wa ghala katika
Halmashauri ya Mbulu zinakamilishwa. Katika mwaka 2013/2014, Serikali
itaendelea na ujenzi wa barabara na miundombinu mingine ya masoko Tanzania Bara
na Zanzibar.
Maendeleo ya Sekta ya Mifugo
49.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/2013 Serikali imeanza
kutekeleza Programu ya Miaka Mitano ya Kuendeleza Sekta ya Mifugo (2011/2012 –
2015/2016). Programu hiyo inalenga kuwa na Sekta ya Mifugo ya kisasa itakayoongeza
ukuaji wa Sekta kutoka Asilimia 2.3 hadi 4.5 kwa mwaka ifikapo mwaka 2016. Ili
kufikia malengo hayo, Serikali pamoja na mambo mengine, imezielekeza
Halmashauri zote Nchini kufanya tathmini ya uwezo wa ardhi katika maeneo yao
ili kufuga kulingana na uwezo wa eneo lililopo.
50.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali pia imeboresha huduma za uhamilishaji pamoja na
kutoa Ruzuku ya Dawa za Kuogesha Mifugo Lita 92,323 zenye thamani
ya Shilingi Bilioni 1.5 ambazo zimesambazwa katika Mikoa yote ya Tanzania Bara.
Hatua hiyo imekwenda sambamba na kujenga
Majosho Mapya 14 na kukarabati Majosho 20 katika Mikoa ya Arusha, Iringa, Kagera, Lindi, Mara,
Mbeya, Mwanza, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Simiyu, Singida, Geita na Tanga. Vilevile,
Serikali imetoa mafunzo ya unenepeshaji mifugo kwa Wafugaji wanaozunguka Ranchi
za Taifa. Pia, Miradi 13 ya unenepeshaji mifugo imeibuliwa kupitia Mipango ya Maendeleo
ya Kilimo ya Wilaya katika Mikoa ya Arusha, Dodoma, Manyara, Mwanza, Shinyanga
na Singida. Hatua hiyo imeongeza idadi ya Ng’ombe walionenepeshwa kutoka
132,246 mwaka 2011 hadi Ng’ombe 150,000 mwaka 2012. Aidha, Vijiji 781 vya Halmashauri za Wilaya
80 katika Mikoa ya Iringa, Mbeya, Morogoro, Pwani, Katavi, Rukwa, Ruvuma na
Singida vimepimwa ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara kati ya wafugaji na
watumiaji wengine wa ardhi.
51.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2013/2014, Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Mifugo
ili itoe mchango mkubwa zaidi katika uchumi. Aidha, itakamilisha ujenzi wa
Mfumo wa Utambuzi na Ufuatiliaji Mifugo ambao unatarajiwa kuanza kazi mwezi
Agosti 2013. Vilevile, itaimarisha uhamilishaji Nchini kwa kuzalisha Dozi za
mbegu bora za uhamilishaji.
Maendeleo ya Sekta ya Uvuvi
52.
Mheshimiwa
Spika,
katika mwaka 2012/2013, Serikali imeanza kupitia Sera ya Taifa ya Uvuvi ya
mwaka 1997 na kuandaa Mkakati wa utekelezaji. Lengo ni kuihuisha Sera hiyo ili
iendane na mabadiliko ya Kiuchumi na Kijamii yaliyojitokeza pamoja na
kuzingatia maendeleo ya Sayansi na Teknolojia katika Sekta ya Uvuvi. Katika
mwaka 2013/2014, Serikali itakamilisha kupitia Sera ya Taifa ya Uvuvi ya mwaka
1997 na kuendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali za uvuvi. Aidha, Vikundi
vya Ulinzi Shirikishi vya Kudhibiti Uvuvi Haramu na Vituo vya Doria
vitaimarishwa. Serikali pia itaendelea kusimamia shughuli za ukuzaji wa viumbe
kwenye maji ikiwa ni pamoja na kuanzisha vituo vipya vya kuzalisha vifaranga
vya samaki.
Ufugaji Nyuki
53.
Mheshimiwa
Spika, Uzalishaji wa Asali na Nta kwa miaka ya hivi karibuni
unatupa moyo kwamba, Ufugaji wa Nyuki unaweza kuwa ni shughuli ya kiuchumi
inayoweza kuwaongezea Wananchi wetu kipato na kuwaondolea umaskini. Katika kipindi
cha miaka minne iliyopita 2009 - 2012,
uzalishaji wa Asali ulifikia Wastani wa Tani 8,747 na Nta Tani 583. Katika
juhudi za kuongeza uzalishaji, Serikali imetoa elimu ya ufugaji nyuki katika Wilaya za Kahama (Vijiji 7), Chunya (Vijiji 4),
Same (Vijiji 2), Manyoni (Vijiji 3), Singida (Vijiji 2) na Kibondo (Vijiji 13).
Aidha, Mizinga 500 imesambazwa katika Wilaya za Ruangwa, Mtwara, Newala,
Tunduru na Namtumbo ambapo kila Wilaya ilipata Mizinga 100. Pamoja na juhudi
hizo, Hekta 56,290 zimepimwa kwa ajili ya kutenga hifadhi za nyuki katika
Vijiji mbalimbali Nchini.
54.
Mheshimiwa
Spika,
kwa kuzingatia umuhimu wa Sekta ndogo ya Ufugaji Nyuki kwa maendeleo ya
Wananchi, niliahidi kwamba yatafanyika Maonesho Maalum ya Ufugaji Nyuki.
Maonesho hayo yamefanyika Kitaifa Jijini
Dar es Salaam, tarehe 4 - 7 Oktoba 2012 katika Viwanja vya Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere ambapo yalitanguliwa na Kongamano lililofanyika tarehe 3
Oktoba 2012. Kauli Mbiu ya Maonesho
ilikuwa ni “ASALI KWA AFYA NA USTAWI”. Maonesho hayo yameleta chachu na
matumaini makubwa ya kukua kwa biashara ya mazao ya Nyuki kwani tangu
kumalizika, Wafugaji Nyuki wa Tanzania wamepata soko la kuuza zaidi ya Tani 100
za Asali Nchini Ujerumani. Aidha, Wajasiriamali wengi wamepata Alama ya
Utambulisho wa Biashara (Barcode) kwa
ajili ya kutambulisha Asali yao. Vilevile, kutokana na wananchi kuhamasika
kufuga nyuki, Serikali imeanza kutengeneza mizinga bora ipatayo 70,000,
kuiwekea chambo na kuisambaza kwa wananchi kwa gharama nafuu.
55.
Mheshimiwa
Spika,
kutokana na umuhimu wa Sekta ya Nyuki, kwa
mara ya kwanza Tanzania iliadhimisha siku ya Kitaifa ya Kutundika Mizinga,
tarehe 4 Machi 2013 katika Hifadhi ya Aghondi iliyopo Wilayani Manyoni Mkoa wa Singida.
Katika uzinduzi huo, Wadau
walipata nafasi ya kutambua fursa kubwa zilizopo katika Sekta hiyo na kujenga
mahusiano ya karibu ya kibiashara. Katika mwaka 2013/2014, Serikali
itafanya mapitio ya Sera ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998 ili iendane na
mabadiliko yanayotokea. Aidha, mafunzo na vifaa kwa ajili ya ufugaji nyuki yatatolewa
kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa Asali na Nta.
Maendeleo ya Viwanda
56.
Mheshimiwa
Spika,
mchango wa Sekta ya Viwanda kwenye Pato la Taifa uliongezeka na kufikia Asilimia
9.7 mwaka 2012 ikilinganishwa na Asilimia 9.0 mwaka 2011. Viwanda vinavyoendelea
vizuri katika uzalishaji na kutoa mchango mkubwa ni
pamoja na viwanda vya saruji, bia, unga
wa ngano, vinywaji baridi, sukari, rangi,
nyaya za umeme na usindikaji wa ngozi. Kwa upande
wa SIDO, jumla ya Wajasiriamali 4,766 wamepatiwa
mafunzo mbalimbali ya kukuza ujuzi wao
hususan katika usindikaji
wa mafuta ya kupikia, ngozi, ubanguaji
wa korosho pamoja na kuhifadhi na kusindika
vyakula vya aina
mbalimbali. Aidha,
SIDO
ilitoa huduma za ugani kwa Wajasiriamali 6,779 ili kuboresha shughuli za
uzalishaji. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kubuni mikakati mipya
yenye lengo la kuendeleza na kuviwezesha viwanda vidogo na vya kati vya
wajasiriamali wa ndani pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya ukuaji wa viwanda
Nchini.
57.
Mheshimiwa Spika,
ili kuhamasisha Usindikaji wa Ngozi hapa Nchini na kuongeza thamani ya zao la
ngozi, mwezi Julai 2012, Serikali iliongeza Ushuru wa Ngozi Ghafi zinazouzwa
nje ya Nchi kutoka Asilimia 40 hadi 90 kwa kilo. Kutokana na hatua hiyo, ngozi
zinazosindikwa Nchini zimeongezeka kutoka vipande vya ngozi za Ng’ombe 166,773
na vipande vya ngozi za Mbuzi na Kondoo 778,023 kipindi cha Januari - Juni,
2012 hadi vipande vya ngozi za Ng’ombe 343,860 na vipande vya ngozi za Mbuzi na
Kondoo 1,173,875 kipindi cha Julai - Desemba, 2012. Ongezeko hilo linathibitisha
kwamba hatua zilizochukuliwa na Serikali zimeongeza usindikaji wa ngozi na
kupanua wigo wa uzalishaji wa mazao ya ngozi Nchini. Serikali itaendelea
kusimamia mafanikio hayo na kuchukua hatua zaidi zitakazoongeza usindikaji wa
ngozi hapa Nchini.
Sekta ya Utalii
58.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa Mpango Mkakati wa kuifanya Mikoa ya Dar
es Salaam, Lindi, Mtwara na Tanga kuwa vituo vya utalii wa fukwe. Mikoa hiyo
ina fukwe za kipekee zinazovutia watalii na pia zinafaa kwa uwekezaji wa
kitalii. Vilevile, Serikali imevitangaza vivutio vya utalii katika soko la ndani
na nje ya nchi kupitia Vyombo vya Habari na maonesho ya ndani na Kimataifa. Kutokana na
hatua hiyo, idadi ya Watalii walioingia nchini mwaka 2012 imeongezeka na
kufikia watalii 930,753 ikilinganishwa na watalii 867,994 mwaka 2011. Aidha,
mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka Shilingi Bilioni 2,119 mwaka
2011 hadi Shilingi Bilioni 2,183 mwaka 2012.
59.
Mheshimiwa
Spika, matunda ya juhudi za kutangaza vivutio vya utalii
na pia kuhamasisha utalii wa ndani yamedhihirika baada ya Taasisi ya The Seven Natural Wonders yenye Makao yake Nchini Marekani kuijumuisha Tanzania
katika zoezi la kutafuta Maajabu Saba ya Asili katika Bara la Afrika. Zoezi
hilo lilishirikisha wataalam wengi Duniani na kupigiwa kura na watu kutoka
sehemu mbalimbali, wakiwemo Watanzania kwa
kutumia Tovuti. Matokeo ya zoezi hilo yalitangazwa
tarehe 11 Februari 2013, Jijini Arusha, ambapo Tanzania iliibuka mshindi kwa vivutio
vitatu vya Maajabu
Saba ya Asili ya Afrika yakijumuisha Mlima Kilimanjaro, Ngorongoro Crater na Hifadhi
ya Taifa ya Serengeti. Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Watanzania wote wa
ndani na nje ya Nchi walioshiriki kupiga kura na hatimaye
kutuwezesha kupata ushindi huo. Aidha, namshukuru
Dkt. Philip Imler ambaye ni mwanzilishi wa Taasisi ya The Seven Natural Wonders aliyesimamia
zoezi hilo. Pia, nayashukuru Makampuni yote yaliyofadhili mashindano hayo na
kutangaza vivutio vya Tanzania Barani Afrika na Duniani kote. Natoa wito kwa
Watanzania wote kuhakikisha kwamba tunavilinda, tunavitunza na kuviendeleza
vivutio hivyo kwa manufaa ya Taifa letu. Tutumie pia ushindi huo kutangaza
zaidi utalii wetu ili rasilimali hizi nzuri tulizo nazo ziendelee kuvutia
watalii wengi na kuongeza mapato yetu.
Sekta ya Madini
60.
Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo wa madini wana mchango mkubwa katika
kukuza uchumi wa Nchi yetu. Ili kuwaendeleza wachimbaji hao, Serikali
imekamilisha Mkakati, Mpango Kazi na Programu ya Mafunzo pamoja na kuwatengea
maeneo wachimbaji wadogo kwa
mujibu wa Sheria. Maeneo hayo ni Mpambaa (Singida),
Kilindi (Tanga), Dete na Melela (Morogoro), Winza (Dodoma), Songwe (Mbeya),
Nyakunguru (Mara), Nyamilonge na Ilagala (Kigoma), Mihama (Katavi), Mwajanga
(Manyara), Makanya (Kilimanjaro) na Mbesa (Ruvuma). Aidha, Serikali imekusanya
takwimu na taarifa muhimu za wachimbaji wadogo kote Nchini kwa lengo la
kuwatambua, kufahamu changamoto walizonazo na kujenga kanzidata
(database).
61.
Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa Mwanachama kamili wa Mpango wa Kimataifa
Unaohimiza Uwazi katika Sekta ya Madini (Extractive
Industries Transparency Initiatives- EITI) baada ya kutimiza vigezo
vilivyowekwa kimataifa katika Sekta ya Madini. Hatua hiyo imeiwezesha Tanzania
kuwa na mfumo thabiti wa utoaji taarifa za malipo na mapato kutoka katika
kampuni zinazojishughulisha na uchimbaji wa Madini, Gesi Asilia na Mafuta ambao
unamwezesha mwananchi kufahamu na kujadili mchango wa Kampuni hizo katika Pato
la Taifa. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaimarisha ukaguzi kwenye
uzalishaji na biashara ya madini pamoja na kuimarisha STAMICO ili itekeleze
majukumu yake kikamilifu.
HALI YA AJIRA NCHINI
62.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuongeza fursa za
ajira kwa vijana wengi wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka.
Kwa mujibu wa matokeo ya Utafiti wa Ajira na Kipato Nchini wa mwaka 2010/2011,
Ajira ziliongezeka kutoka 1,276,982 mwaka 2010 hadi Ajira 1,362,559 mwaka 2011,
sawa na ongezeko la Asilimia 6.7. Ili kuongeza kasi ya ukuaji
wa ajira, Serikali inakamilisha Programu
ya Kitaifa ya Kukuza Ajira kwa Vijana.
Programu hiyo ya miaka mitatu itaongeza fursa za Vijana 301,100 kuweza
kujiajiri au kuajiriwa. Msukumo zaidi utawekwa katika Miradi ya Kilimo,
Viwanda Vidogo, Maeneo Maalum ya Kiuchumi (EPZ na SEZ), Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano. Sambamba na hatua hiyo,
Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa Vyuo vya Ufundi
na vya Elimu ya Juu ili kuwawezesha kujiajiri baada ya kuhitimu mafunzo yao.
HUDUMA ZA KIUCHUMI
Ardhi
63.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na Nchi yetu kuwa na ardhi ya kutosha na
inayofaa kwa Kilimo na uwekezaji mwingine, bado hatujakamilisha zoezi la
uwekaji mipaka, kupima na kutoa Hati kwa matumizi mbalimbali. Hali hiyo
inachangia migogoro ya ardhi na kukwamisha uwekezaji kwa kiasi kikubwa.
Serikali imechukua hatua muhimu kwa kutumia teknolojia ya kisasa
itakayoharakisha zoezi la upimaji ardhi. Katika kutekeleza kazi hiyo, Awamu ya Kwanza
ya usimikaji wa Mtandao wa Alama za Msingi za Upimaji Ardhi Nchini (Geodetic Control Network) imekamilika.
Mikoa iliyohusika ni Pwani, Morogoro, Mara, Mwanza, Kagera, Shinyanga, Lindi,
Tabora na Dodoma. Tayari majaribio ya matumizi ya Alama hizo yamefanyika katika
Wilaya za Ngorongoro na Kilombero na kudhihirisha kuwa gharama na muda wa
kupima ardhi zimepungua. Awamu ya Pili ya usimikaji wa Alama hizo utaendelea
katika Mikoa iliyobaki na kuanza upimaji wa viwanja na mashamba kwa kutumia utaratibu
mpya wa upimaji wa ardhi.
64.
Mheshimiwa
Spika, ili kuwa na mfumo endelevu wa utunzaji wa
kumbukumbu za ardhi, Serikali imeanza ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi
Kumbukumbu za Ardhi. Mfumo huo utakaounganisha Ofisi za Ardhi Nchini
unategemewa kukamilika mwaka 2014 na utaiwezesha Tanzania kuwa na kumbukumbu
sahihi za ardhi. Vilevile, utaharakisha na kurahisisha utoaji wa maamuzi,
upimaji na utoaji wa Hati Miliki na hivyo kupunguza migogoro ya ardhi. Katika
mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi
Kumbukumbu za ardhi na kurahisisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji.
Nishati
65.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusogeza huduma ya nishati ya umeme
karibu na Wananchi ili kuharakisha maendeleo
yao. Katika kutekeleza azma hiyo,
gharama za kuunganisha umeme wa
njia moja kwa
wateja
wadogo Vijijini na Mijini zimepunguzwa kwa wastani wa kati ya Shilingi Milioni 1,311,000 na Shilingi 114,000.
Hatua hiyo imewezesha wananchi wengi kumudu gharama ya kuunganisha umeme na
kuongeza kasi ya usambazaji umeme Nchini. Serikali pia, imefikisha umeme katika
Makao Makuu ya Wilaya za Nkasi na Namtumbo, hivyo kufanya idadi ya Makao Makuu ya
Wilaya zenye umeme kuwa 117, sawa na Asilimia 88 ya Wilaya zote Nchini.
Vilevile, Serikali inatekeleza Programu Kabambe ya Kusambaza Umeme Vijijini
ambapo wateja 8,046 wamelipiwa gharama za kuunganishiwa umeme kupitia Mfuko wa
Nishati Vijijini. Aidha, kazi ya kusambaza na kuboresha miundombinu ya umeme
katika Mikoa ya Mtwara na Lindi inaendelea kufanyika.
66.
Mheshimiwa Spika, Sekta ndogo ya Gesi Asilia inakua kwa kasi ambapo hadi
kufikia Januari 2013, kiasi cha futi za ujazo Trilioni 35 zimegundulika Nchini.
Ili kusimamia rasilimali hiyo muhimu, Serikali imeandaa rasimu ya Sera ya Gesi
Asilia na kupata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali. Aidha, tarehe 8 Novemba
2012, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania alizindua mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Gesi Asilia kutoka Mtwara
hadi Dar es Salaam. Mradi huo utaongeza uzalishaji wa umeme na kupunguza
gharama za umeme Nchini.
67.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na ujenzi
wa Mradi wa bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na ujenzi wa Mitambo
ya kuzalisha umeme wa Kinyerezi (MW 200). Vilevile, itaanza kutekeleza Awamu ya
Pili ya Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini na kufikisha umeme wa gridi kwenye
Makao Makuu ya Wilaya zisizokuwa na umeme.
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
68.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inatekeleza
Mradi wa ujenzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa
wenye Awamu Tano. Awamu ya Kwanza na
ya Pili ya Ujenzi wa Mkongo huo wenye urefu wa Kilomita 7,560 imekamilika na
kuunganisha Makao Makuu ya Mikoa
24 ya Tanzania Bara. Kazi
ya kuunganisha Kisiwa cha
Unguja na Mkongo
huo kupitia Dar es Salaam itakamilika mwaka 2013. Tayari Makampuni ya Simu na Mawasiliano
ya hapa Nchini yameunganishwa kwenye Mkongo hatua ambayo imewezesha upatikanaji
wa huduma bora za mawasiliano katika eneo kubwa zaidi na kwa gharama nafuu.
Sambamba na hatua hiyo, Serikali imeanza ujenzi wa Mfumo wa Kuratibu Huduma za
Mawasiliano Nchini (Traffic Monitoring
System). Mfumo huo utasaidia kuhakikisha mapato yanayotokana na huduma
katika Sekta ya Mawasiliano yanajulikana ili Makampuni ya Mawasiliano Nchini yalipe
kodi stahiki kwa Serikali.
69.
Mheshimiwa
Spika, Tanzania pamoja na Nchi zote Duniani kupitia
Umoja wa Mawasiliano Duniani (ITU) zimekubaliana kusitisha matumizi ya
teknolojia ya utangazaji kutoka Mfumo wa Analojia na kuanza Matumizi ya
Teknolojia ya Dijitali ifikapo Juni 2015. Hapa Nchini, usitishaji wa matumizi ya mfumo wa
mitambo ya analojia umeanza kutekelezwa tarehe 31 Desemba 2012 kwa awamu kwa kuanzia
na Jiji la
Dar es Salaam na kufuatiwa
na Mikoa ya Dodoma, Tanga na Mwanza. Matangazo ya
analojia yataendelea kusitishwa katika Mikoa mingine Nchini kulingana na
ratiba iliyowekwa. Natambua kwamba kuna changamoto zilizojitokeza katika
utekelezaji wa zoezi hilo la mabadiliko. Hata hivyo, mabadiliko hayo yanalenga
kuimarisha mawasiliano na kuiwezesha Nchi yetu kuendana
na hali halisi ya mabadiliko ya teknolojia Duniani. Katika mazingira ya sasa, sisi kama
Taifa siyo vyema kubaki kama kisiwa
wakati tumeunganishwa na mifumo
ya teknolojia ya kidunia.
Hivyo, ni busara tuendelee
na mabadiliko hayo sasa kuliko kusubiri na hatimaye tukajikuta tuko nyuma na nje
ya mstari. Natoa wito kwa Watanzania wote kuyaona mabadiliko hayo kwa mtazamo
chanya na kuyakubali kama hatua kubwa sana ya maendeleo ya teknolojia Nchini.
Sayansi na Teknolojia
70.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inafanya jitihada kubwa za kuendeleza
Sayansi na Teknolojia kama njia ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi. Jitihada
hizo ni pamoja na kutenga fedha za kutosha kila mwaka kwa ajili ya utafiti na
maendeleo ya kisayansi. Serikali pia, imekamilisha ujenzi wa Taasisi ya Sayansi
na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyopo Mkoani Arusha ambayo ilizinduliwa rasmi
tarehe 2 Novemba 2012. Kukamilika kwa ujenzi
wa Taasisi hiyo kumeongeza udahili wa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili na Uzamivu
kutoka wanafunzi 83 mwaka 2011/2012 hadi wanafunzi 135 mwaka 2012/2013.
71.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea
kueneza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kupanua matumizi yake katika maeneo
mbalimbali Nchini na Nchi jirani. Vilevile, Serikali itaendelea na zoezi la
kuhama kutoka katika mfumo wa analojia kwenda dijitali na kupanua na kuboresha Mtandao
wa Huduma za Mawasiliano ya simu na intaneti Nchini.
Barabara na Madaraja
72.
Mheshimiwa Spika, Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika kujenga,
kukarabati na kuboresha mtandao wa Barabara Kuu, za Mikoa, Wilaya pamoja na za
Vijijini ili zipitike wakati wote wa mwaka. Lengo ni kuwa na mtandao bora wa
barabara utakaowezesha Wananchi, hasa Wakulima kusafirisha mazao yao
hadi kwenye Masoko
ya ndani na nje ya Nchi. Katika mwaka 2012/2013, Serikali imejenga jumla ya Kilometa 294.4 za kiwango
cha lami katika
Barabara Kuu na za Mikoa na kukarabati
kwa kiwango cha lami jumla ya Kilometa 111.8 katika barabara hizo. Aidha, kazi za ujenzi na ukarabati wa
Barabara Kuu na za Mikoa zenye urefu wa Kilometa 179 kwa kiwango cha lami
unaendelea katika maeneo mbalimbali Nchini.
73.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne imedhamiria kujenga na
kukamilisha ujenzi wa Madaraja makubwa na ya kisasa mawili ambayo ni Daraja la
Mto Malagarasi na Daraja la Kigamboni.
Ujenzi wa Daraja la Mto Malagarasi unaojumuisha
ujenzi wa Daraja kubwa lenye urefu wa Meta 200 na Madaraja mengine madogo
katika Bonde la Mto Malagarasi unaendelea
vizuri. Hadi mwezi Machi 2013, Mkandarasi amekamilisha ujenzi kwa Asilimia 85. Sambamba na hatua hiyo, taratibu zimekamilika
za kupata mkopo wa nyongeza kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya
Kiuchumi wa Korea kwa ajili ya ujenzi wa barabara kiungo za Daraja hilo zenye
urefu wa Kilometa 37 kwa kiwango cha lami.
74.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa
Daraja la Kigamboni lenye urefu wa Meta 680 linalojengwa kuunganisha eneo la Kurasini
na Kigamboni katika Bahari ya Hindi, tayari Mkandarasi amekamilisha kazi za maandalizi kwa Asilimia 90. Kazi ya
ujenzi wa Daraja la Kudumu na Barabara zake inatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia
sasa. Daraja hili
linajengwa kwa Ubia kati ya Serikali na Mfuko wa Hifadhi ya
Jamii (NSSF). Lengo ni kukamilisha ujenzi wa Daraja hilo mwanzoni mwa mwaka
2015.
75.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014 Serikali itajenga Barabara Kuu
kwa kiwango cha lami zenye urefu wa Kilometa 495 na kukarabati Barabara zenye
urefu wa Kilometa 190 na Madaraja 11. Serikali pia, itajenga barabara za Mikoa
za lami zenye urefu wa Kilometa 54.3 na kukarabati Kilometa 855 kwa kiwango cha
changarawe na Madaraja 36. Aidha, matengenezo ya kawaida na matengenezo ya muda
maalum ya Barabara Kuu na za Mikoa yataendelea kufanyika katika kipindi kijacho.
Usafiri wa Barabara katika Jiji la Dar es Salaam
76.
Mheshimiwa Spika, msongamano wa magari katika barabara za Jiji la Dar es
Salaam ni moja ya changamoto ambayo Serikali inaendelea kuifanyia kazi.
Jitihada zinazofanyika kupunguza msongamano wa magari barabarani ni pamoja na
kujenga miundombinu zaidi ya barabara mpya za kuingia na kutoka katikati ya
Jiji; kuanzisha usafiri wa Treni ya Abiria; kuharakisha utekelezaji wa Mradi wa
Mabasi Yaendayo Haraka (DART); na kuimarisha usimamizi wa Sheria za Usalama
Barabarani.
77.
Mheshimiwa
Spika, kuhusu ujenzi wa barabara mpya za kupunguza
msongamano katika Jiji la Dar es Salaam, hadi Machi, 2013 ujenzi wa Barabara ya
kiwango cha lami yenye urefu wa Kilometa 6.4 kutoka Kituo Kikuu cha Mabasi
Ubungo - Kigogo hadi mzunguko wa barabara ya Kawawa imekamilika na barabara
yenye urefu wa Kilometa 2.7 kutoka barabara ya Kawawa – Bonde la Msimbazi hadi Makutano
ya Jangwani na Twiga imekamilika kwa Asilimia 70. Aidha, ujenzi wa Barabara
yenye urefu wa Kilometa 10.3 kutoka Jet
Corner - Vituka hadi Davis Corner
imekamilika kwa Asilimia 90. Vilevile, utekelezaji
wa Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka unaendelea ambapo kazi
zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa barabara za DART na za magari mchanganyiko
na baiskeli katika Barabara ya Morogoro, na ujenzi wa Miundombinu ya Mifumo ya Maji, Vituo
vya Mabasi na Madaraja. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na ujenzi
wa barabara nyingine za kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam
pamoja na ujenzi wa miundombinu ya DART.
HALI YA UCHUKUZI
Huduma za Usafiri wa Reli Jijini Dar es Salaam
78.
Mheshimiwa Spika, mwezi Oktoba 2012, Serikali ilianzisha huduma ya usafiri
wa treni ya abiria Jijini Dar es Salaam kupitia Kampuni ya Reli (TRL) na TAZARA
kwa lengo la kukabiliana na tatizo la msongamano wa magari na abiria. Wastani
wa idadi ya Abiria wanaosafiri kwa Treni ya TAZARA ni 4,500 kwa siku na TRL ni Abiria
5,000. Takwimu zinaonesha kuwa, Abiria 9,500 wanaosafiri kila siku kwa njia ya
treni wangehitaji kutumia mabasi zaidi ya 380 yenye uwezo wa kubeba Abiria 25
kila moja. Kwa ujumla mwitikio wa wananchi wa kutumia huduma ya treni ya abiria ni mkubwa
ikilinganishwa na uwezo wa kutoa huduma hiyo. Kwa kuzingatia mahitaji hayo
makubwa, Serikali imeunda Kamati maalum ya wadau wa usafiri Jijini Dar es Salaam
kwa lengo la kuchambua, kuanisha na kushauri mipango na mikakati ya baadaye ya
kuboresha huduma hiyo ili iwe endelevu na salama. Ni mategemeo yangu kwamba
Kamati hiyo itaandaa Mpango mzuri zaidi wa kupanua huduma hiyo muhimu kwa Jiji
la Dar es Salaam ambalo kwa mujibu wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya
mwaka 2012 lina idadi ya watu Milioni 4.36, sawa na Asilimia 10 ya Wakazi wote wa
Tanzania Bara. Ongezeko hilo ni kubwa na hivyo linahitaji Mpango Kabambe wa
usafiri na usafirishaji.
Usafiri wa Reli ya Kati na TAZARA
79.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka
2012/2013, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya reli ya kati kwa kujenga
na kukarabati maeneo mbalimbali ili kuiwezesha kupitika wakati wote. Pamoja na
ukarabati huo, usanifu wa
kina wa Mradi wa Uendelezaji na Ujenzi wa Reli kutoka Dar es Salaam - Isaka -
Keza - Kigali na Keza - Musongati kwa kiwango cha Kimataifa
umekamilika mwezi Februari
2013. Serikali pia, imekamilisha
mchakato wa kumpata Mshauri mwelekezi atakayefanya upembuzi yakinifu wa kuinua
kiwango cha reli kuwa katika kiwango cha kimataifa kutoka Tabora hadi Kigoma,
Kaliua hadi Mpanda na Isaka hadi Mwanza. Lengo ni kuwezesha reli hiyo ifanane
na inayotarajiwa kujengwa kutoka Dar es Salaam-Isaka-Kigali/Musongati. Upembuzi
Yakinifu wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Rwanda na Burundi na kutoka
Arusha hadi Musoma unatarajiwa kuanza mwaka 2013/2014.
80.
Mheshimiwa
Spika, itakumbukwa kwamba mwezi Machi
2012, Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China zilitia saini Itifaki ya 15 ya kuboresha Reli ya TAZARA.
Tayari Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imetoa jumla ya Shilingi Bilioni
38.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi iliyo chini ya Itifaki hiyo ambayo
inajumuisha kufanya upembuzi yakinifu wa kuboresha reli hiyo, kukarabati njia ya reli, kununua vichwa vipya
vya treni na kukarabati mabehewa ya abiria. Hatua hizi zikikamilika
zitaboresha kwa kiwango kikubwa usafiri wa Reli ya TAZARA.
Bandari
81.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inachukua hatua
mbalimbali za kuongeza uwezo na ufanisi wa bandari zake kwa kutekeleza Mpango Kabambe
wa Mamlaka ya Bandari. Baadhi ya Miradi inayotekelezwa chini ya Mpango huo ni Upembuzi
Yakinifu kwa ajili ya kuimarisha na kuongeza kina cha maji katika Gati Namba 1
hadi 7 katika Bandari ya Dar es Salaam na
kuanza awamu ya pili ya mradi wa
ujenzi wa matanki ya kuhifadhia mafuta. Mradi mwingine ni kufanya Upembuzi
Yakinifu wa ujenzi wa kituo kikubwa cha kuhifadhia mizigo ya kwenda Nchi jirani
katika eneo la Kisarawe.
82.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na nafasi ya Nchi yetu kijiografia na
ongezeko kubwa la biashara na uingizaji wa mizigo ya hapa Nchini na Nchi jirani
ambazo hazina bandari, uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhimili ongezeko hilo
unapungua. Pamoja na jitihada zinazoendelea za kupanua miundombinu ya bandari
hiyo, Serikali imeona umuhimu wa kuwa na Bandari mpya ya Bagamoyo ili isaidiane
na Bandari zilizopo kukabiliana na ongezeko hilo. Tarehe 24 Machi 2013, Serikali
ya Tanzania na China zimetia saini makubaliano ya kujenga Bandari mpya ya
Bagamoyo ambayo itakuwa kubwa kuliko zote katika Ukanda wa Nchi za Afrika
Mashariki na Kati. Makubaliano hayo yanajumuisha pia ujenzi wa eneo huru la
biashara na miundombinu mingine muhimu ikiwemo reli itakayounganisha Bandari ya
Bagamoyo na Reli ya Kati na ya TAZARA pamoja na barabara ya lami kutoka Bagamoyo
hadi Mlandizi. Huu ni mradi mkubwa na wa kimkakati ambao utabadili kabisa mfumo
wa uendeshaji wa Bandari na usafirishaji Nchini.
Usafiri wa Anga
83.
Mheshimiwa Spika, Serikali imetekeleza kwa mafanikio Awamu ya Kwanza ya Uboreshaji na Upanuzi wa Viwanja vya Ndege vya
Tabora, Kigoma na Bukoba. Ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege kwa
kiwango cha lami katika kiwanja cha Ndege cha Tabora umekamilika na kazi za
ujenzi zinazoendelea katika kiwanja cha Kigoma zinatarajiwa kumalizika mwezi
Juni 2013. Kwa upande wa Kiwanja cha Ndege cha Bukoba, ukarabati wa njia ya
kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami unaendelea. Aidha, Kiwanja kipya cha
Kimataifa cha Songwe, Mbeya kilianza kutoa huduma tarehe 13 Desemba, 2012.
Kiwanja hicho ambacho kijiografia kipo karibu na Nchi za Zambia, Malawi, Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo na Nchi nyingine za Kusini mwa Afrika ni kichocheo
muhimu cha shughuli za uchumi na kijamii zikiwemo utalii na kilimo hasa cha
matunda, mbogamboga na maua kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Ni muhimu sana
wananchi wa maeneo hayo na mengine wahamasishwe na kujipanga kutumia fursa za
kiuchumi zitakazoambatana na kukamilika kwa kiwanja hicho.
84.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na utekelezaji wa Mradi
wa Upanuzi na Uboreshaji wa Viwanja vya Ndege. Kazi zitakazofanyika ni pamoja
na Upembuzi Yakinifu na usanifu wa kina wa ukarabati kwa kiwango cha lami wa
njia za kuruka na kutua ndege kwa viwanja vya Iringa, Kilwa Masoko, Ziwa
Manyara, Musoma, Mtwara, Njombe, Songea, Singida na Tanga.
MAENDELEO YA SEKTA YA ELIMU
Elimu ya Msingi
85.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilianza kutekeleza Programu kubwa za
kuendeleza elimu Nchini mwaka 2001 kwa lengo la kuongeza idadi ya Wanafunzi wa
rika lengwa wanaojiunga na shule na kuboresha elimu. Utekelezaji wa Awamu ya
Kwanza na ya Pili ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM I & II)
umeleta mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu ya elimu, kuandikisha
Wanafunzi wa rika lengwa na kupunguza pengo la uandikishaji kati ya Wanafunzi
wa Kike na wa Kiume. Mafanikio hayo yaliambatana na changamoto za upungufu wa Walimu, Vifaa vya
kujifunzia na kufundishia pamoja na madawati. Kwa kutambua
changamoto hizo, Ilani ya Uchaguzi ya
CCM ya mwaka 2010 inaelekeza Serikali kulinda mafanikio yaliyopatikana pamoja
na kuweka msisitizo mkubwa katika ubora wa elimu.
86.
Mheshimiwa Spika, ili kuendeleza kasi tuliyoanza nayo, Serikali
inatekeleza Awamu ya Tatu ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM III)
unaolenga kuboresha elimu kwa kuongeza idadi ya Walimu, vitabu vya ziada na
kiada na vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Jitihada za Serikali za kuajiri walimu
zinaendelea ambapo Walimu wapya 13,568 wameajiriwa katika Shule za Msingi mwaka
2012/2013. Serikali itaendelea kuweka msisitizo katika kuboresha Elimu ya
Msingi Nchini kwa kuzingatia manufaa makubwa yanayopatikana katika ngazi hiyo
muhimu ya elimu.
Elimu ya Sekondari
87.
Mheshimiwa Spika, mafanikio ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya
Elimu ya Msingi Nchini ambayo ni pamoja na kuongezeka kwa idadi
ya wahitimu wanaofaulu ngazi hiyo,
yameongeza mahitaji ya nafasi zaidi katika Shule za Sekondari. Kutokana na hali hiyo, Serikali ilianza
kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES) mwaka 2006. Mpango
huo umesaidia sana kukabiliana na changamoto ya nafasi zaidi katika Shule za Sekondari kwa kujenga Shule
nyingi za Sekondari na hivyo kuwa na wanafunzi wengi zaidi. Ni dhahiri kuwa ongezeko
hilo la Wanafunzi
lilihitaji Walimu wengi zaidi, Maabara,
Vitabu na Vifaa vingine muhimu. Aidha, Serikali iligatua usimamizi wa Shule za
Sekondari kutoka Serikali Kuu kwenda katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuboresha usimamizi wa
shule hizo pamoja na kuanzisha programu kabambe ya kufundisha walimu zaidi ili
wafundishe katika shule zinazoongezeka. Katika mwaka 2012/2013, Serikali
imeajiri jumla ya Walimu 12,969 ambao watafundisha katika Shule mbalimbali za Sekondari
Nchini. Hatua hizo zote ni uwekezaji mkubwa ambao matokeo yake yatawezesha
kuboresha elimu Nchini hatua kwa hatua.
88.
Mheshimiwa Spika, sote tumehuzunishwa sana na matokeo yasiyoridhisha
ya mtihani wa Kidato cha Nne kwa mwaka 2012.
Matokeo hayo siyo tu kwamba yamewahuzunisha wazazi ambao wamewekeza
rasilimali kwa Watoto wao bali pia Serikali ambayo imetumia rasilimali nyingi
kwenye Sekta ya Elimu. Huu siyo wakati
wa kulaumiana ama kutafuta mchawi wa matokeo hayo yasiyoridhisha. Ni lazima
tutafute suluhisho, kusonga mbele na
kubuni mikakati na hatua za haraka za kusaidia Watoto hao ambao wamepata
matokeo mabaya. Tumeanza kwa kuunda Tume yenye Watu makini ambayo itachunguza
chanzo cha matokeo hayo mabaya na kutoa mapendekezo ya namna ya kutatua tatizo
hilo katika muda mfupi, kati na mrefu na
pia kupendekeza suluhisho la haraka kwa wale waliopata daraja la IV na sifuri.
Napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba, matokeo
ya Tume hiyo yatawekwa bayana na hatua zitakazopendekezwa zenye lengo la
kuimarisha elimu Nchini zitachukuliwa. Hata hivyo, ni vyema tukumbuke kwamba, sote
tuna wajibu wa kutoa mwongozo na mapendekezo yatakayosaidia kutoka hapa tulipo.
Wazazi, Wanafunzi na Jamii nzima wana nafasi yao pia katika kuboresha elimu ya
Nchi hii. Hili siyo suala la Serikali pekee.
Elimu Maalum
89.
Mheshimiwa Spika,
Serikali inaendelea kuweka
msukumo wa kipekee katika kutoa Elimu
Maalum kwa watu wenye Ulemavu wakiwemo wenye Ulemavu
wa Ngozi, Uoni Hafifu na Usikivu.
Katika mwaka 2012/2013, Serikali imeandaa Mwongozo wa kufundishia Wanafunzi
wenye Ulemavu wa Ngozi na Uoni Hafifu. Aidha, Serikali imenunua na kusambaza vifaa
maalum na visaidizi vya kufundishia na kujifunzia kuanzia ngazi ya Elimu ya
Awali hadi Chuo Kikuu. Kazi nyingine zilizofanyika ni kukarabati na kujenga
majengo rafiki kwa walemavu katika Chuo cha Ualimu Patandi. Katika mwaka
2013/2014, Serikali itaendelea kuboresha utoaji wa Elimu Maalum hususan baada
ya kupata takwimu sahihi za walemavu kutokana na Sensa ya Watu na Makazi ya
mwaka 2012.
Elimu ya Juu
90.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya
Juu kwa kupanua na kuongeza Taasisi za Elimu ya Juu za Serikali na Binafsi. Katika kipindi takribani cha miaka 8 idadi ya wanafunzi wanaosoma Vyuo vya
Elimu ya Juu Nchini imeongezeka kutoka 40,993 mwaka 2005/2006 hadi 166,484
mwaka 2012/2013, sawa na ongezeko la Asilimia 306. Serikali pia, inatoa mikopo kwa wanafunzi wa
Vyuo vya Elimu ya Juu vya Umma na vile vya Mashirika ya Dini na vya Sekta
Binafsi. Katika mwaka 2012/2013, Serikali
imetoa mikopo ya Shilingi Bilioni 345 kwa wanafunzi 98,772 ikilinganishwa na
mikopo ya Shilingi Bilioni 291 kwa wanafunzi 93,784 mwaka 2011/2012.
91.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kuongeza
kiasi cha fedha kwa ajili ya Mikopo ya Elimu ya Juu na kuimarisha usimamizi
wa urejeshaji wa mikopo ili wanafunzi
wengi zaidi waweze kunufaika. Nitumie fursa hii kuwakumbusha wale wote
walionufaika na mikopo ya elimu ya juu kulipa mikopo hiyo yenye masharti nafuu
sana ili wanafunzi zaidi waweze kunufaika nayo.
Aidha, waajiri watimize wajibu wao kwa kuwataka waajiriwa walionufaika kulipa
mikopo hiyo. Vilevile, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu iongeze kasi ya kukusanya
madeni na kuchukua hatua stahiki kwa wale wasiolipa kwa mujibu wa Sheria.
MAENDELEO YA SEKTA YA AFYA
Vituo vya Utoaji wa Huduma za Afya Nchini
92.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imeweka jitihada kubwa za kuhakikisha
kwamba Vituo vya Utoaji wa Huduma za Afya katika ngazi zote Nchini vinapatiwa
dawa muhimu na vifaa vya Teknolojia ya kisasa vya kuchunguza na kutibu
magonjwa. Katika mwaka 2012/2013, Serikali imenunua Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba na
vitendanishi na kuvisambaza kwenye Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali zote
za Serikali Nchini. Serikali pia, imeongeza uwezo wa ndani wa kutibu maradhi
mbalimbali. Mathalan, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imewezeshwa kutoa huduma
za Afya za ubingwa wa juu ikiwa ni pamoja na upasuaji wa moyo ambapo hadi sasa
zaidi ya Wagonjwa 450 wamepatiwa
huduma hiyo. Vilevile, huduma ya usafishaji damu kwa Wagonjwa wa figo na Upasuaji
kupitia tundu dogo pamoja na uchunguzi wa magonjwa kwa kutumia mashine za
kisasa unafanyika hapa Nchini. Hatua hiyo imewezesha Serikali na Wananchi kuokoa
fedha nyingi zinazotumika kupeleka wagonjwa kutibiwa nje ya Nchi. Napenda
kutumia fursa hii kuwapongeza Madaktari, Wauguzi na Wataalam wengine wa Afya kwa
kuliwezesha Taifa letu kupiga hatua kubwa katika kutibu magonjwa hayo na
mengine yanayohitaji utaalam na ubingwa wa hali ya juu.
93.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imeimarisha huduma ya tiba ya saratani Nchini
kwa kukamilisha ujenzi wa Jengo la kulaza wagonjwa katika Hospitali ya Saratani
ya Ocean Road na hivyo kuongeza uwezo
wake kutoka vitanda 120 hadi 270. Aidha, Serikali imesogeza huduma ya tiba ya
saratani karibu na Wananchi kwa kukamilisha ujenzi wa Jengo Maalum la kutoa
huduma hiyo katika Hospitali ya Bugando. Hatua hiyo itapanua wigo wa kutoa
huduma ya tiba ya saratani na kupunguza msongamano wa Wagonjwa wa saratani kutoka
Mikoa mbalimbali waliokuwa wanalazimika kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya
Saratani ya Ocean Road Jijini Dar es
Salaam.
Udhibiti wa Maambukizi ya Malaria na UKIMWI
94.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012, Serikali ilifanya Utafiti
kuhusu Viashiria vya UKIMWI na Malaria. Taarifa ya matokeo ya utafiti huo inaonesha
kuwa kiwango cha Malaria Nchini kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano kimepungua
kutoka Asilimia 18 mwaka 2007 hadi Asilimia Tisa mwaka 2012. Hali hii
imechangiwa zaidi na ongezeko kubwa la matumizi ya Vyandarua vilivyowekwa
Viuatilifu vya muda mrefu ambapo zaidi ya Vyandarua milioni 34 vimesambazwa
katika Kaya zenye Watoto walio na umri chini ya miaka mitano na Wanawake
Wajawazito. Kutokana na usambazaji huo, matumizi ya Vyandarua yameongezeka
kutoka Asilimia 26 mwaka 2007 hadi Asilimia 72 mwaka 2012 kwa Watoto wenye umri
chini ya miaka Mitano. Kwa Wanawake Wajawazito, matumizi ya Vyandarua
yameongezeka kutoka Asilimia 27 mwaka 2007 hadi Asilimia 75 mwaka 2012. Ni
dhahiri kupungua kwa kiwango cha Malaria Nchini ni jitihada za kipekee za
Serikali ya Awamu ya Nne kwa kushirikiana na Wananchi na Washirika wa Maendeleo
kupitia Kampeni mbalimbali za Kudhibiti Malaria.
95.
Mheshimiwa
Spika, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru na
kuwapongeza Wananchi na Wadau wote walioshirikiana na Serikali katika kupata
mafanikio haya ambayo yanatokana na utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti
Malaria Nchini na Mpango wa Hati Punguzo kwa Wanawake Wajawazito ulioanza kutekelezwa mwaka 2008 hadi 2012. Natoa wito
kwa Wananchi wote kuendeleza juhudi za Kujikinga na Malaria, hususan kwa
kutumia Vyandarua vyenye Viuatilifu vya muda mrefu na kutokomeza Mazalia ya
Mbu.
96.
Mheshimiwa Spika, juhudi za Serikali za kupambana na ugonjwa wa UKIMWI Nchini pia zimeanza
kuzaa matunda. Kwa mujibu wa Utafiti wa mwaka 2011 - 2012 wa Viashiria vya Malaria
na UKIMWI, maambukizi ya Virusi vya UKIMWI yamepungua kutoka Asilimia 5.7 mwaka
2007/2008 hadi Asilimia 5.1 mwaka 2011/2012 kwa wanawake na wanaume wa umri wa
miaka 15 - 49. Ili kuendelea kupunguza kasi ya maambukizi ya UKIMWI Nchini,
Serikali inaendelea kutoa elimu ya UKIMWI;
kutoa ushauri nasaha na kuhamasisha upimaji wa
hiari. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaanza kutekeleza Mkakati Mpya
wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2013 hadi 2017 unaolenga kuwa na Sifuri tatu, yaani Kutokuwa
na Maambukizi Mapya; Kukomesha Vifo Vitokanavyo na UKIMWI na Kuondoa Kabisa
Unyanyapaa na Ubaguzi. Lengo hilo
litatimia iwapo sote tutabadili tabia zinazosababisha maambukizi mapya.
Lishe
97.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inachukua hatua thabiti za kupambana na
utapiamlo hususan udumavu unaoathiri watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Katika hotuba yangu ya mwaka 2012/2013 nilieleza kwamba Serikali imezindua
Mkakati wa Kitaifa wa Lishe wa mwaka 2010/2011 hadi 2014/2015. Mkakati huo
umeanza kutekelezwa kwa kuandaliwa Mpango wa Utekelezaji ulioainisha gharama na
majukumu ya kila mdau katika kupunguza Utapiamlo Nchini. Pamoja na mambo
mengine, Mpango huo umesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa umma kuhusu lishe
bora hasa kwa mama wajawazito na watoto wachanga, kuongeza viini lishe kwenye
vyakula pamoja na kuingiza masuala ya lishe kwenye Sera na Mipango mbalimbali
ya Serikali. Tayari hatua zimechukuliwa ambapo masuala ya lishe yameingizwa
kwenye Mpango wa Taifa wa Uwekezaji katika Kilimo na Chakula (Tanzania
Agriculture and Food Security Investment Plan - TAFSIP). Vilevile, Serikali inaendelea
na zoezi la kuhuisha Sera ya Usalama wa Chakula na Lishe ya mwaka 1992 ili
iendane na Mkakati wa Taifa wa Lishe wa mwaka 2010/2011 hadi 2014/2015.
98.
Mheshimiwa
Spika, tunayo kazi kubwa mbele yetu ya kupambana na
tatizo la lishe duni katika maeneo yote Nchini. Takwimu zinabainisha kwamba,
hakuna tofauti kubwa ya kiwango cha udumavu katika Mikoa inayozalisha chakula
kwa wingi na ile yenye uhaba wa chakula.
Napenda kusisitiza tena kwamba hali ya udumavu humtokea mtoto katika
siku elfu moja za kwanza za uhai wake, yaani tangu kutungwa mimba hadi umri wa
miaka miwili. Hivyo, tunahitaji kuimarisha utoaji elimu ya lishe kwa Wajawazito
na Mama wanaonyonyesha ili wapate mlo kamili na kunyonyesha watoto wao
kikamilifu hususan miezi sita ya mwanzo tangu kuzaliwa. Natoa wito kwa
Waheshimiwa Wabunge zaidi kujiunga na Kikundi cha Wabunge kinachohamasisha
umuhimu wa Lishe Bora ili kuongeza kasi na chachu ya kutoa elimu ya lishe
katika maeneo yetu ya uwakilishi.
HALI YA UPATIKANAJI MAJI NCHINI
Huduma ya Maji Vijijini
99.
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa maji ya uhakika na ya kutosha kwa
wananchi Vijijini bado ni changamoto inayohitaji nguvu zaidi na mbinu mpya kwa
kuzingatia ongezeko kubwa la watu pamoja na mabadiliko ya Tabianchi. Katika
kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imetenga na kupima
maeneo ya vyanzo vya maji na kuyawekea mipaka ili kuzuia uchafuzi na uharibifu
wa vyanzo hivyo. Aidha, Vituo mbalimbali
vya kuchotea maji vimeainishwa katika Halmashauri 122 na kuwekwa kwenye ramani
ili vifahamike. Ujenzi wa miradi mipya, upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya
maji Vijijini pia umefanyika katika maeneo mbalimbali ili kusogeza huduma ya
maji karibu na wananchi. Kutokana na juhudi hizo, idadi ya Wananchi wanaoishi
Vijijini ambao wanapata huduma ya majisafi, salama na ya kutosha karibu na
makazi imeongezeka kutoka watu Milioni 16.3 mwaka 2006 hadi Milioni 20.6 mwaka
2012.
Huduma ya Maji Mijini
100.
Mheshimiwa
Spika, huduma ya Maji Mijini inasimamiwa na kutekelezwa
na Mamlaka 19 za Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Miji Mikuu ya Mikoa,
Mamlaka 109 katika ngazi za Wilaya, Miji Midogo
na Miradi ya
Maji ya Kitaifa. Serikali kupitia Mamlaka hizo
imeongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Miji hiyo kutoka Asilimia
84 mwaka 2010/2011 hadi Asilimia 86 mwaka 2011/2012. Katika Jiji la Dar es
Salaam, Serikali inaboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa kupanua uwezo wa
mtambo wa maji wa Ruvu Chini ambapo ujenzi umefikia Asilimia 85. Kazi ya kulaza bomba kuu la pili lenye kipenyo cha Meta 1.8 na urefu wa
km 55.5, kutoka Ruvu Chini hadi kwenye matanki ya kuhifadhia
maji yaliyopo eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam inatarajiwa kukamilika mwezi Februari 2014. Aidha, kazi ya usanifu wa Mradi wa Kuchimba Visima Virefu 12 katika maeneo ya Kimbiji na Visima
8 katika eneo la Mpera imekamilika na Wananchi waliohamishwa wamelipwa fidia.
Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea
kukarabati na kujenga miradi ya maji Mijini na Vijijini pamoja na kujenga
mabwawa kwa ajili ya matumizi ya majumbani na mifugo hususan katika maeneo
kame.
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
Uanzishaji wa Maeneo Mapya ya Utawala
101.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imekamilisha taratibu za kuanzisha
Halmashauri Mpya 31 ili kusogeza huduma karibu na Wananchi. Halmashauri hizo ni
Jiji la Arusha, Manispaa ya Ilemela, Manispaa ya Lindi na Halmashauri za Miji ya
Kahama, Masasi, Makambako, Geita na Bariadi. Vilevile, imeanzisha Halmashauri za
Wilaya ya Kalambo, Busega, Nsimbo, Bumbuli, Mlele, Ushetu, Msalala, Momba,
Mbogwe, Kyerwa, Busokelo na Buhigwe. Halmashauri nyingine zilizoanzishwa ni Nyangh’wale,
Wanging’ombe, Chemba, Mkalama, Gairo, Nyasa, Kakonko, Itilima, Uvinza, Ikungi na
Kaliua. Serikali itaendelea kuzipatia Halmashauri mpya vitendea kazi, Watumishi
pamoja na kujenga miundombinu muhimu hatua kwa hatua.
MASUALA MTAMBUKA
Vita Dhidi ya Rushwa
102.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na tatizo la rushwa kwa
kuelimisha Umma kuhusu athari za Rushwa,
kuziba mianya ya rushwa na kuwasihi
Wananchi
kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Aidha, Vyombo vya Dola vimechunguza tuhuma za makosa ya
Rushwa na kuwafikisha watuhumiwa mbele ya Vyombo vya Kisheria. Hadi kufikia Desemba 2012, tuhuma 2,911 zilichunguzwa
ambapo uchunguzi wa tuhuma 390 umekamilika na Kesi 121 zimefunguliwa Mahakamani. Katika mwaka 2013/2014, TAKUKURU itaendelea na uchunguzi wa tuhuma zilizopo na
mpya zitakazojitokeza, kuendesha Kesi nyingine zilizopo Mahakamani na
zitakazoendelea kufunguliwa kutokana na kukamilika kwa chunguzi mbalimbali.
Serikali pia itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za rushwa.
Maafa
103.
Mheshimiwa
Spika,
changamoto kubwa iliyoikumba Nchi yetu kwa mwaka 2012/2013 ni ukame uliosababisha
upungufu mkubwa wa Chakula
katika
baadhi ya maeneo
Nchini. Kutokana na hali hiyo, Serikali ilifanyaTathmini za kina za Hali ya
Chakula na Lishe Nchini na kubaini kwamba Watu 1,615,440 katika Halmashauri 47
Nchini wanahitaji msaada wa chakula. Katika kukabiliana na hali hiyo, kuanzia mwezi
Julai 2012 hadi Machi 2013, Serikali imetoa Tani 69,452 za chakula cha msaada chenye
thamani ya Shilingi Bilioni 26.39 kwa walengwa katika maeneo yenye upungufu.
Serikali pia imetoa Shilingi Bilioni 4.6 kwa ajili ya usafirishaji wa chakula
hicho.
104.
Mheshimiwa
Spika,
katika kurejesha hali ya kawaida kwa waathirika wa Mabomu eneo la Gongolamboto,
Serikali imekamilisha ujenzi wa Nyumba 36 eneo la Msongola Wilayani Ilala na Nyumba
moja eneo la
Mbweni Wilayani Kinondoni. Zoezi hilo kwa ujumla
limegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 1.75. Nyumba hizo ambazo zimewekewa
huduma za msingi za maji na umeme zilikabidhiwa kwa walengwa na Mheshimiwa Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 11 Desemba
2012.
105.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa
kwamba mafuriko yaliyotokea Dar es Salaam mwezi Desemba 2011 yalisababisha Kaya 1,007 za waathirika
waliokuwa wanaishi katika maeneo hatarishi zaidi kuhamishiwa katika eneo la
Mabwepande Wilayani Kinondoni. Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuwapatia huduma mbalimbali za kijamii na kuwajengea miundombinu muhimu ikiwemo barabara, maji,
umeme, shule, zahanati na Kituo cha
Polisi. Aidha, hivi karibuni Serikali
imetoa Mifuko 100 ya Saruji kwa kila Kaya ili kuziwezesha kujenga nyumba bora
na za kudumu. Napenda kutoa wito kwa Wananchi ambao bado wanaishi mabondeni
kuhama ili kuepuka athari zinazoweza kuwapata. Aidha, Mamlaka za Serikali za Mitaa Nchini ziendelee
kutenga maeneo yenye usalama kwa ajili ya kuwahamisha wananchi wanaokaa katika
maeneo hatarishi.
Dawa za Kulevya
106.
Mheshimiwa
Spika, biashara
na matumizi ya Dawa haramu za Kulevya bado ni tatizo Nchini. Hali hii inadhihirishwa na idadi kubwa ya
watumiaji walio mitaani na wale wanaojitokeza kupata tiba. Hata hivyo, kutokana
na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kwa kutumia Kikosi Kazi Maalum cha Kitaifa
cha Udhibiti wa Dawa za Kulevya, jumla ya Kilo 255 za Heroin na Kilo 151 za
Cocaine zilikamatwa mwaka 2012 na Watuhumiwa 45 walikamatwa. Vilevile,
jumla ya Ekari
184 za Mashamba ya Bangi na Kilo 3,200 za Bangi kavu ziliteketezwa na Kilo
4,840 za mirungi zilikamatwa. Katika
kipindi hicho, Waathirika wa Dawa za Kulevya wapatao 20,426 walijitokeza katika Vituo mbalimbali vya tiba. Hospitali ya
Taifa ya Magonjwa ya Akili ya Mirembe imekuwa ikipokea wastani wa Waathirika 400 kila mwaka.
107.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali
itakamilisha Sera ya Taifa ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya Nchini na kuandaa
Mkakati wake wa Utekelezaji. Serikali pia itaendelea kutoa elimu kwa umma juu
ya madhara ya Dawa za Kulevya na kupanua huduma za matibabu kwa waathirika wa
Dawa za Kulevya. Wito wangu kwa jamii nzima ni
kuendelea kupambana kwa nguvu zote na tatizo la biashara na matumizi ya dawa za
kulevya ili kunusuru vijana wetu. Wasafirishaji na watumiaji wa dawa hizo
tunaishi nao mitaani na ni wajibu wa kila mmoja wetu kuwabaini na kutoa taarifa
katika Vyombo vya Dola.
Ustawishaji Makao Makuu Dodoma
108.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali imeendelea
kuimarisha miundombinu ya Manispaa ya Dodoma kwa kujenga barabara zenye jumla
ya Kilometa 20.6 kwa kiwango cha lami katika maeneo ya Kisasa, Chang'ombe,
Kikuyu na Area A. Aidha, imekarabati mtandao wa maji wenye urefu wa Kilometa
17.5 na kusambaza umeme wa msongo mkubwa wenye urefu wa Kilometa 13.5 katika
eneo la uwekezaji la Njedengwa. Vilevile, Viwanja 1,098 vimepimwa katika maeneo
ya Ndachi, Ilazo C-centre, Nala Mizani, Mwangaza, Ipagala, Kizota Relini pamoja
na lyumbu New Town Centre.
109. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali
imepanga kukamilisha ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami katika maeneo ya
Kisasa, Chang'ombe, Kikuyu na Area A. Vilevile, itaendelea na ujenzi wa
Barabara kwa kiwango cha lami, usambazaji wa umeme wa msongo mkubwa pamoja na
usambazaji wa mabomba ya maji safi katika eneo la Uwekezaji la
Njedengwa. Pia, itapima Viwanja vipya 4,476 katika maeneo ya
Nzuguni, Mkonze, Ndachi na maeneo ya Viwanda. Pamoja na kazi hizo, kazi
iliyoanza ya kuimarisha utendaji wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma
itaendelea.
HITIMISHO
110.
Mheshimiwa Spika, nimeelezea kwa muhtasari baadhi ya shughuli ambazo
Serikali imetekeleza kwa kipindi kilichopita. Aidha, nimetoa Mwelekeo wa Kazi zitakazofanyika
mwaka 2013/2014. Kwa kuhitimisha, napenda kusisitiza mambo machache yafuatayo:
a)
Matokeo
ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 yameonesha kuna ongezeko la watu
Milioni 10.1 kutoka watu Milioni 34.4 mwaka 2002 hadi Milioni 44.5 mwaka 2012,
sawa na ongezeko la Asilimia 30. Ni dhahiri ongezeko hilo kubwa linahitaji
juhudi za pamoja kati ya Serikali, Sekta Binafsi, Wadau wa Maendeleo na
Wananchi kwa ujumla kuongeza uwekezaji katika huduma mbalimbali za kiuchumi na
kijamii. Rai yangu kwenu ni kuzitumia takwimu hizo kikamilifu katika kupanga
mipango ya maendeleo kwa ajili ya watu wetu.
b)
Tumebakiza
miaka takribani 12 kabla ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025,
miaka miwili kufikia malengo ya Maendeleo ya Milenia na miaka miwili ya
kukamilisha utekelezaji wa Mpango wa Kwanza wa Miaka Mitano. Mfumo mpya ulioanzishwa
na Serikali wa kufuatilia na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya
kipaumbele na kufanya tathmini ya mara kwa mara ya kupima matokeo utasaidia
kuharakisha kufikiwa kwa malengo hayo mapema. Serikali itahakikisha kwamba
Mfumo huo unaimarisha uwajibikaji na kuleta matokeo makubwa na ya haraka katika
kipindi kifupi.
c)
Jitihada
za Serikali ya Awamu ya Nne katika kuvutia uwekezaji katika kilimo hususan
katika Ukanda wa Kilimo wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) zimeleta mwamko na
matumaini makubwa. Azma ya Serikali ni kuona kwamba Wawekezaji wakubwa
wanashirikiana kwa karibu na wakulima wadogo ili waweze kuondoka kwenye kilimo
cha kujikimu na kuingia katika kilimo cha kisasa chenye tija na cha kibiashara.
Nawahakikishia Watanzania wote kwamba upatikanaji wa ardhi iliyopimwa kwa ajili
ya Mkulima mdogo ndicho kipaumbele cha Serikali.
d)
Mchakato
wa kuandaa Katiba Mpya umeingia katika
hatua ya kuunda Mabaraza ya Katiba katika ngazi mbalimbali yatakayopitia
Rasimu ya Katiba Mpya na kutoa maoni. Tume baada ya kuzingatia maoni ya
Mabaraza itaandaa Rasimu ya Katiba Mpya itakayowasilishwa katika Bunge Maalum
la Katiba. Natoa wito kwa wananchi watoe ushirikiano kwa Tume iweze kukamilisha
zoezi hilo muhimu kwa ufanisi na kwa wakati.
e)
Amani
iliyopo Nchini imetujengea heshima kubwa katika Bara la Afrika na Duniani kote.
Sote tuna wajibu wa kuienzi na kuisimamia isitoweke. Serikali ya awamu ya Nne
itahakikisha kwamba Amani na umoja wa Kitaifa vinadumishwa ili kuwawezesha Wananchi
kuendelea kufanya shughuli zao za maendeleo bila hofu. Serikali haitavumilia
kuona mtu au kikundi cha watu wenye dhamira mbaya wakivuruga Amani, Umoja na
Mshikamano uliopo Nchini kwa kisingizio chochote. Sote tuna wajibu wa kuheshimu
utawala wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.
111.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kumaliza Hotuba yangu, nimwombe Mheshimiwa Hawa
Abdulrahman Ghasia (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa atoe maelezo ya Mapitio ya Kazi zilizofanyika katika
mwaka 2012/2013 na Mwelekeo wa Kazi za
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2013/2014.
SHUKRANI
112.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii sasa kuwashukuru Mawaziri na Naibu
Mawaziri kwa ushirikiano walionipa katika kipindi hiki. Aidha, nawashukuru
Watumishi wote wa Serikali na Taasisi zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Yohana Sefue kwa
kusimamia Shughuli za Serikali vizuri. Nawashukuru Watanzania wote na Washirika
wetu wa Maendeleo kwa michango yao ambayo imewezesha Serikali kutoa huduma
mbalimbali kwa Wananchi.
113.
Mheshimiwa
Spika, vilevile, napenda kuwashukuru Mheshimiwa Dkt. Mary
Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, Waziri wa Nchi
(Uwezeshaji na Uwekezaji); Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, Mbunge wa
Ismani, Waziri wa Nchi (Sera, Uratibu na Bunge); Mheshimiwa Hawa Abdulrahman
Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa; Mheshimiwa Aggrey Joshua
Mwanry, Mbunge wa Siha, Naibu Waziri, Ofisi
ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa; na Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, Mbunge wa
Ruangwa, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Elimu) kwa ushirikiano
walionipa katika utekelezaji wa
majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nawashukuru
pia Wakuu wa
Mikoa na Wilaya kwa jitihada walizoonesha katika kipindi hiki. Nawashukuru vilevile Wafanyakazi wote wa
Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu, Bwana Peniel Moses Lyimo
na Kaimu Katibu Mkuu, Bwana Jumanne Abdallah Sagini kwa kazi nzuri
wanayoifanya. Niwashukuru Naibu Makatibu Wakuu, Bwana Charles Amos Pallangyo,
na Bwana Alphayo Japan Kidata kwa ushauri wao wa Kitaalam ambao wamenipa mimi
na Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi katika kipindi hiki. Nawashukuru kwa kukamilisha
maandalizi yote ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa
mwaka 2013/2014.
114.
Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri na maelekezo anayonipatia
katika kutekeleza majukumu yangu. Pia ninamshukuru
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi kwa ushirikiano wao mkubwa. Vilevile, ninawashukuru
Waheshimiwa Wabunge, Viongozi wote wa Kitaifa na wa ngazi nyingine zote kwa
ushirikiano wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Niwashukuru sana Wapiga
Kura wangu wa Jimbo la Katavi kwa ushirikiano wanaonipa katika kuleta maendeleo
ya Jimbo letu. Nawashukuru sana!
115.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee, naomba uniruhusu kutumia fursa hii
kumshukuru sana Mama Tunu Pinda na Familia yangu yote kwa kunitia moyo,
kunivumilia kwa kila hali na kunipa nguvu katika utekelezaji wa majukumu yangu
ya Kitaifa. Nawashukuru sana!!
MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU, OFISI YA WAZIRI MKUU - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA NA OFISI YA BUNGE YA MWAKA 2013/2014
MUHTASARI
116.
Mheshimiwa Spika, kwa muhtasari, naomba
sasa Bunge lako Tukufu likubali kuidhinisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa
mwaka 2013/2014 ya jumla ya Shilingi Bilioni
Mia Moja Ishirini na Tatu, Milioni Mia Nne na Moja, na Hamsini na Tisa Elfu (123,401,059,000);
kwa ajili ya Mfuko wa Bunge, na jumla ya Shilingi Trilioni Nne, Bilioni Mia Mbili Ishirini na Sita, Milioni Mia Moja
Ishirini na Tatu, Mia Tisa Hamsini na Nne Elfu na Mia Nane na Mbili (4,226,123,954,802) kwa ajili ya Ofisi
ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
ikiwa ni Matumizi ya Kawaida na Fedha za Maendeleo za Ndani na Nje kwa ujumla
wake.
117.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Hotuba hii, yapo Majedwali ambayo
yanafafanua kwa kina Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na
Taasisi zake, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na
Ofisi ya Bunge.
118.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja.
COMMENTS