HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA MHESHIMIWA DKT. WILLIAM AUGUSTAO MGIMWA (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO ...
MHESHIMIWA DKT. WILLIAM AUGUSTAO
MGIMWA (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA
MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2013/2014
I.
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba
Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya
Serikali kwa mwaka 2013/14.Pamoja na hotuba hii, vimeandaliwa vitabu vinne vya
Bajeti vinavyoelezea takwimu mbalimbali za Bajeti. Kitabu cha Kwanza kinahusu makisio ya mapato;
Kitabu cha Pili kinaelezea makisio
ya matumizi ya kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa
Serikali; Kitabu cha Tatukinahusu
makisio ya matumizi ya kawaida kwa Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa; na
Kitabu cha Nne kinaainisha makadirio
ya matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala
za Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha,upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka
2013 ambao ni sehemu ya bajeti hii.
2.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote
ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kushiriki
mkutano wa nane wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha
namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete kwa uongozi wake thabiti. Vilevile, napenda kutumia fursa hii
kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wa vikao vya Bunge
kwa kuongoza majadiliano vizuri bungeni.
3.
Mheshimiwa Spika, kwa
kuzingatia mapendekezo ya Bunge ya mzunguko mpya wa bajeti, Serikali imeridhia
mapendekezo hayo ambayo yanatoa fursa ya kushirikisha wadau wengi zaidi na
kuwezesha utekelezaji wa bajeti kuanza tarehe 1 Julai kila mwaka. Serikali
imetekeleza mapendekezo hayo kwa kurekebisha muda na utaratibu wa hatua za uandaaji
wa bajeti ambazo zimezingatiwa wakati wa maandalizi ya bajeti ya mwaka 2013/14.
4.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko
hayo, Serikali itakuwa inatayarisha Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti mwezi
Agosti hadi Oktoba kila mwaka; kuidhinisha na kusambaza Mwongozo mwezi Novemba;
kuandaa rasimu za mipango na bajeti za mafungu mwezi Novemba hadi Januari;
kufanya uchambuzi wa rasimu za Bajeti na kuingiza takwimu kwenye mfumo wa IFMS
Mwezi Februari; kuwasilisha rasimu za Bajeti pamoja na randama kwenye Kamati za
Bunge za Kisekta mwezi Machi; kuchapisha na kuwasilisha Bungeni vitabu vya
bajeti mwezi Aprili; kuchambua na kuidhinisha bajeti Bungeni mwezi Aprili hadi
Juni; na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya shughuli zilizoidhinishwa muda wote
wa utekelezaji wa bajeti.
5.
Mheshimiwa Spika, kufuatia mabadiliko hayo, Wizara
zote zinatakiwa kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha na
kuhitimishwa na hotuba hii ya bajeti ya Serikali.
6.
Mheshimiwa Spika, Ninazishukuru Wizara,
Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali, Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa nawadau mbalimbaliwalioshiriki kufanikisha matayarisho ya
bajeti hii. Kwa namna ya pekee, ninaishukuru Kamati ya Bunge ya Bajeti
ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Andrew John Chenge,Mbunge wa Bariadi
Magharibi kwa kuchambua kwa kina bajeti za mafungu yote na kutoa mapendekezo.Aidha,
naishukuru Kamati Maalum yaMheshimiwaSpika kuhusu mapendekezo ya mapato ya
Serikali;Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara inayoongozwa na
Mhe. Mahmoud Hassan Mgimwa (Mb) na Waheshimiwa Wajumbe wengine wa Kamati hiyo pamoja
na Wenyeviti wa Kamati nyingine za kisekta kwa ushauri, mapendekezo na
maelekezo wakati wakichambua Bajeti hii. Vilevile, ninawashukuru Waheshimiwa
Wabunge wote kwa ushauri na mapendekezo yao ambayo yamesaidia kuboresha Bajeti
hii.
7.
Mheshimiwa Spika, ninampongezakwa dhati Waziri
Mkuu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb), kwa hotuba yake ambayo imefanya
majumuisho ya mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2012/13 na kutoa
mwelekeo wa shughuli za Serikali kwa mwaka 2013/14. Aidha, ninamshukuru Mhe.
Stephen Masatu Wasira (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu
kwa kuwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2012 na Mpango wa Maendeleo
wa mwaka 2013/14. Vilevile, ninawapongeza Mawaziri wenzangu kwakuwasilisha hotuba
za bajeti za wizara zao ambazo zimejumuishwa katika Bajeti hii.
8.
Mheshimiwa Spika, ninawashukuru Naibu
Mawaziri wa Fedha, Mhe. Janet Zebedayo Mbene (Mb) naMhe. Saada Mkuya Salum (Mb),
Katibu Mkuu; Naibu Makatibu Wakuu;Gavana wa Benki Kuu; Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato; Mkurugenzi Mkuu wa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu; Viongozi wakuuwataasisi zilizo chini ya Wizara;wakuu
wa idara na vitengo pamoja na watumishi wa Wizara ya Fedha na taasisi zake kwa michango
yao katika maandalizi ya Bajeti hii. Ninamshukuru
pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Fedha wa
mwaka 2013 na nyaraka mbalimbali za sheria ambazo ni sehemu ya Bajeti hii.
Aidha, ninamshukuru Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha nyaraka zote za
Bajeti kwa wakati.
vidokezo
Kodi juu:
Dizeli
Petroli
leseni za Magari
kodi ya barabara (fuel levy)
simu za kiganjani
simu za TTCL
Sigara
Bia
magari kukuu
vipodozi
samani kutokia nje
Ahueni:
Payee 1%
Mafuta ya taa
Maji ya chupa
kodi ya mafunzo (SDL)
ngano, mchele, sukari (kutoka nje)
Kodi mpya
M-pesa
Huduma ya ushauri
Tozo ya Petroli (petrol levy)
Misamaha iliyofutwa
Ukodishaji wa ndege
Bidhaa zisizo za mtaji kwa wawekezaji
Vipaumbele vya bajeti
Miundombinu
Kilimo
Viwanda
Raslimali watu
Utalii
Huduma za jamii
9.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2013/14
ni ya tatu katika utekelezaji wa Mpango wa kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano;
Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2010; naAwamu ya Pili ya Mkakati wa
Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II).Aidha, Bajeti hii inaendelea
kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015. Madhumuni ya mipango na mikakati hii ni kufikia
malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.Vilevile, Bajeti hii inalenga
kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa ajili ya maendeleo endelevu kupitia
mfumo mpya wa utekelezaji wa miradi ya kipaumbele ambayo italeta matokeo
makubwa kwa haraka.
10.
Mheshimiwa Spika, kama ilivyoelezwa katika
hotuba iliyowasilishwa na Mhe. Stephen Masatu Wasira (Mb), kuhusu utaratibu mpya
wa uibuaji wa vipaumbele vya Taifa ambavyo vitaleta matokeo makubwa na ya
haraka(Big Results Now –BRN),Bajeti
ya mwaka 2013/14, imedhamiria kutekeleza maeneo makuu sita yaliyobainishwa kama
vipaumbele vya kitaifa. Maeneo hayo ni maji, nishati, uchukuzi, kilimo, elimu
na kuongeza mapato.
11.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya
awali, naomba sasa kutoa taarifa kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya
mwaka 2012/13, na mwelekeo wa makadirio ya mapato na matumizi kwa kipindi cha
mwaka 2013/14.
II.
MAPITIO YA UTEKELEZAJIWA
SERA ZA BAJETI YA MWAKA 2012/13
12.
Mheshimiwa Spika, shabaha na malengo ya
Bajeti ya mwaka 2012/13 yalijikita katikakukuza Pato halisi la Taifa kwa
asilimia 6.8 mwaka 2012; kuongeza mapato ya ndani kufikia uwiano na Pato la
Taifa wa asilimia 18.0;kudhibiti mfumuko wa bei na hatimaye kuurudisha kwenye kiwango
cha tarakimu moja; kuimarisha kiwango cha ubadilishaji wa fedha kitakachotokana
na mwenendo wa soko la fedha pamoja na kuongeza mikopo kwa sekta binafsi kwa
asilimia 20 ya Pato la Taifa.
13.
Mheshimiwa Spika,maeneo mengine
yaliyozingatiwa katika misingi na shabaha ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka
2012/13 yalikuwa: kuwepo kwa nishati ya umeme wa uhakika na kuhamasisha
matumizi ya gesi asilia; kuimarika kwa utekelezajiwa Sera za Fedha na Bajeti;
kuimarika kwa mahusiano na Washirika wa Maendeleo; kutekeleza maboresho katika
sekta ya umma ikiwa ni pamoja na kuendelea kuimarika kwa usimamizi wa fedha za
umma; kuboresha mazingira ya biashara pamoja na kuongezeka kwa tija na fursa za
uwekezaji; kulinda na kudumisha mafanikio yaliyopatikana katika Sekta za huduma
za jamii; kuimarisha utawala bora na uwajibikaji; na kuimarisha utaratibu
wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi
(PPP).
Sera za
Mapato
14.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13,
Sera za mapato zilizotekelezwa na Serikali zililenga kuongeza mapato ya ndani
yatokanayo na kodi na yasiyo ya kodiili kuimarisha uwezo wa Serikali wa kutoa
huduma kwa umma na kupunguza utegemezi wa bajeti. Sera zilizotekelezwa zililengakatika
kuimarisha taratibu za kukadiria na kukusanya mapato; kuboresha sheria za kodi;
kuongeza matumizi ya kielektroniki katika kukusanya kodi; kupunguza misamaha ya
kodi; na kuwianisha viwango vya kodi na tozo.
15.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba katika
mwaka wa fedha 2012/13, Bunge lilipitisha sera mbalimbali za kodi ambazo
zimetekelezwa na Serikali. Azma ya sera hizo ilikuwa ni kuimarisha ukusanyaji
wa mapato ya ndani kwa kupanua wigo wa kodi, kuimarisha taratibu za kukusanya
mapato pamoja na kupunguza misamaha ya kodi ili kuweza kugharamia kwa kiwango
kikubwa matumizi ya Serikali kwa kutumia mapato ya ndani. Kwa kuzingatia azma
hiyo, Serikali imechukua hatua zifuatazo katika eneo la mapato:-
(i)
Kuboresha mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato
ya kodi na yasiyo ya kodi kwa kupitia upya mfumo wa ukadiriaji kodi, utoaji wa
stakabadhi na leseni, pamoja na kuboresha viwango vya kubakiza maduhuli kwa
Wizara, Idara na Taasisi za Serikali;
(ii)
Kupanua wigo wa kodi kwa kuendelea kurasimisha sekta
isiyo rasmi ili iingie kwenye mfumo wa kodi;
(iii)
Kufanya mapitio ya sheria za Wakala/Taasisi za Umma
zinazokusanya maduhuli ili ziweze kuchangia zaidi kwenye Mfuko Mkuu wa
Serikali;
(iv)
Kufanya mapitio ya sheria mbalimbali zinazotoa
misamaha ya kodi kwa lengo la kudhibiti na kupunguza misamaha hiyo;
(v)
Kupitia upya mfumo wa ukusanyaji wa kodi ya majengo
katika majiji, manispaa, miji, wilaya na miji midogo ili kuuboresha zaidi;
(vi)
Kufanya mapitio ya vyanzo vya mapato na mfumo wa
ukusanyaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuongeza mapato; na
(vii)
Kujenga uwezo wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na
Madini, Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania,
na Wakala wa Ukaguzi wa Madini ili kuweza kusimamia ukusanyaji wa mapato katika
maeneo ya madini, gesi na petroli.
Mwenendo
wa Ukusanyaji Mapato ya Ndani
16.
MheshimiwaSpika, hadi kufikia mwezi Aprili
2013, jumla ya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi yalifikia kiasi cha shilingi
bilioni 6,717.2, sawa na asilimia 93.2 ya makadirio ya kukusanya shilingi
bilioni 7,209.2 katika kipindi hicho na asilimia 77.1 ya makadirio ya mwaka ya
shilingi bilioni 8,714.7. Kati ya makusanyo hayo, mapato ya kodi yalikuwa
shilingi bilioni 6,371.3 ambayo ni sawa na asilimia 96 ya makadirio ya kipindi
hicho na asilimia 79.0 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 8,070.1 na mapato
yasiyotokana na kodi yalikuwa shilingi bilioni 357.8 ikiwa ni asilimia 55.5 ya
lengo la mwaka la shilingi bilioni 644.6.
17.
Mheshimiwa Spika, tathmini ya makusanyo ya
mapato ya kodi inaonesha mwenendo wa kuridhisha ambapo hadi kufikia mwezi
Aprili 2013, makusanyo ya ushuru wa forodha yalifikia shilingi bilioni 487.8,
sawa na asilimia 84.6 ya kukusanya shilingi bilioni 576.7; mapato kutokana na kodi
ya ongezeko la thamani yalifikia shilingi bilioni 1,965.5, sawa na asilimia 90.3
ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 2,176.4. Kwa upande wa ushuru wa bidhaa,
hadi kufikia mwezi Aprili 2013 jumla ya shilingi bilioni 1,050.7 zimekusanywa
ambazo ni sawa na asilimia 90.3 ya kukusanya shilingi bilioni 1,163.1. Kwa
upande wa kodi ya mapato kwa makampuni, makusanyo yalifikia shilingi bilioni
2,381.9 hadi mwezi Aprili 2013, ambayo ni sawa na asilimia 105.4 ya lengo la
kukusanya shilingi bilioni 2,260.7
18.
Mheshimiwa Spika, kuongezeka kwa makusanyo
ya kodi kulitokana, pamoja na sababu nyingine, na: kuongezeka kwa makusanyo ya
kodi ya mapato ya makampuni; kuongezeka kwa kodi ya zuio inayotokana na malipo
ya gawio katika makampuni ya madini; na ukusanyaji wa malimbikizo ya kodi.
Hatua zingine za kiutawala zilizosababisha kuongezeka kwa mapato zinajumuisha:
kuhakikisha mashine za kielektroniki zinatumika ipasavyo; kuendelea kuimarisha
mfumo wa kusimamia vitalu vya kodi; kuboresha mfumo wa uthamanishaji bidhaa;
kuimarisha ukaguzi wa hesabu za walipa kodi; mapato kutokana na mauzo ya hisa
za kampuni ya M/S BP Tanzania; kuongezeka kwa ushuru wa bidhaa wa muda wa
maongezi wa simu; na utozaji wa ushuru wa bidhaa katika bidhaa zote zisizo za
petroli zinazostahili kutozwa kodi hiyo.
19.
MheshimiwaSpika,licha ya mafanikio hayo, baadhi
ya kodi zimeonesha mwenendo usioridhisha tofauti na ilivyotarajiwa, hasa kwenye
kodi ya ongezeko la thamani, ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa zisizo za petroli
na kodi ya mapato inayotokana na ajira. Aidha, uzalishaji katika baadhi ya
viwanda ulipungua na hivyo kusababisha makusanyo ya ushuru wa bidhaa na kodi ya
ongezeko la thamani kuwa chini ya matarajio. Vilevile, kumekuwa na ongezeko la
uingizaji bidhaa kupitia njia zisizo rasmi bila kulipia ushuru na kodi.
20.
Mheshimiwa Spika, makusanyo ya mapato
yasiyo ya kodi yamekuwa hayaridhishi kutokana na: uwezo mdogo wa ukusanyaji na
kukosa utaalam, vifaa duni namifumo dhaifu ya ukusanyaji wa mapato ambayo
inachangia katika upotevu wa mapato. Baadhi ya wakala na Mashirika bado
hayachangii ipasavyo kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Aidha, baadhi ya Idara
ambazo zilikuwa vyanzo muhimuzimegeuzwa kuwa Wakala zilizoundwa chini ya Wizara
mbalimbali hivyo kupunguza michango yake kwenye mapato ya Mfuko Mkuu wa
Serikali.
21.
MheshimiwaSpika, hadi mwezi Aprili 2013,
mapato yanayokusanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa yalifikia shilingi
bilioni 177.4, sawa na asilimia 49 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi
bilioni 362.2.
Misaada
na Mikopo ya Nje yenye Masharti Nafuu
22.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13,
Serikali ilikadiria kupata shilingi bilioni 842.5 kama misaada na mikopo ya
kibajeti. Hadi kufikia Aprili, 2013 Serikali ilipata misaada na mikopo ya
kibajeti ya shilingi bilioni645.4 ambazo ni sawa na asilimia 77 ya makadirio ya
mwaka. Kwa upande mwingine, shilingi bilioni 443.4 zilipokelewa kupitia mifuko
ya kisekta, ikiwa ni sawa na asilimia 107 ya makadirio ya shilingi bilioni
415.1 kwa mwaka.
23.
Mheshimiwa Spika,misaada na mikopo nafuu
iliyopokelewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kipindi kilichoishia Aprili,
2013 ilifikia shilingi bilioni 1,235.7 ambayo ni asilimia 65 ya ahadi ya shilingi
bilioni 1,899.1 kwa mwaka. Kumekuwepo na changamoto inayotokana na Washirika wa
Maendeleo kuchelewa kutoa taarifa wanapotuma fedha moja kwa moja kwenyemiradi husika;
kasi ndogo ya utekelezaji wa baadhi ya miradi; ucheleweshwaji wa taarifa za
utekelezaji wa miradi kutoka Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa na Serikali za
mitaa; pamoja na mchakato mrefu wa ununuzi, hususan inapohusisha kupata idhini
ya mfadhili (no objection).
Mikopo ya Ndani
24.
Mheshimiwa Spika,katika kipindi cha Julai
hadi Aprili 2013, Serikali ilikopa shilingi bilioni 1,364.7 kutoka soko la
ndani la mitaji kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali zilizoiva pamoja na shilingi
bilioni 809.1 kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mikopo ya Nje yenye Masharti ya Kibiashara
25.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2012/13 Serikali
ilikadiria kupata mikopo yenye masharti ya kibiashara shilingi bilioni 1,254.1,
sawa na Dola za Kimarekani milioni 800 kwa ajili ya kugharamia miradi
mbalimbali ya maendeleo katika bajeti ya mwaka 2012/13 iliyopitishwa na Bunge
lako tukufu.Hadi kufikia Mei 2013, Serikali ilipokea shilingibilioni 947, sawa
na dola milioni 600 kutoka benki ya Stanbic, na shilingi bilioni 59.2, sawa na
dola milioni 37 kutoka benk ya Credit Suisse.
Sera za Matumizi
26.
Mheshimiwa Spika,Serikali ilitekeleza sera
za matumizi kwa kuzingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa
Maendeleo wa mwaka 2012/13,ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kupunguza
umaskini. Aidha, sera za matumizi zililenga kupunguza nakisi ya bajeti kwa
kuwianisha mapato na matumizi; kuzingatia Sheria ya Fedha za Umma na Sheria ya Ununuzi
wa Umma; kusimamia ulipaji wa mishahara; na kuendelea kuhakiki na kulipa madai
ya wakandarasi, wazabuni, watoa huduma na watumishi, pamoja na kufuatilia
utekelezaji wa bajeti.
27.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilikadiria kutumia shilingi bilioni 15,191.9
katika mwaka 2012/13. Mgawanyo wa matumizi ya Serikali katika kipindi hiki
ulikuwa kama ifuatavyo: shilingi bilioni 10,597.1 zilitengwa kwa matumizi ya
kawaida na shilingi bilioni 4,594.8 zilikadiriwa kutumika kwa ajili ya matumizi
ya maendeleo.
Mwenendo wa Matumizi
28.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili 2013, matumizi ya kawaida bila kujumuisha
malipo ya hatifungani zilizoiva (rollover)
yalifikia shilingi bilioni7,582.6, sawa na asilimia 82ya makadirio ya
mwaka. Kati ya kiasi hicho, malipo ya mishahara ya watumishi wa Serikali, katika
wizara, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka ya Serikali za
Mitaa na Taasisi zaUmma yalikuwa shilingi bilioni 3,209.2 sawa na asilimia 85 ya
makadirio ya mwaka ya shilingi bilioni 3,781.1.
29.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/13 Serikali
iliendelea na udhibiti wa ulipaji wa mishahara ya watumishi wa umma. Kwa mwaka
2012/13 Serikali imekamilisha uhakiki wa watumishi na malipo ya mishahara
kwenye Wizara pamoja na Sekretarieti za Mikoa. Kazi hii ilianza mwaka 2011/12
kwa kufanya uhakiki wa watumishi wa Serikali kwenyeMamlaka za Serikali za Mitaa
na Taasisi zote. Matokeo ya uhakiki wa watumishi yalisambazwa kwa waajiri kwa
ajili ya kuchukua hatua zinazostahili. Aidha, Serikali imechukua hatua ya
kusambaza mfumo wa malipo kwa waajiri wote ili marekebisho ya mishahara,
waajiriwa wapya, kuondoa watumishi wanaomaliza utumishi wao (wanaostaafu,
wanaofukuzwa, wanaofariki, wanaocha kazi) yaweze kufanyika mara moja baada ya
tukio hilo kutokea kwenye kituo cha kazi. Katika mwaka 2013/14 Serikali
itaendelea na hatua za kudhibiti mishahara ya watumishi, ikiwa ni pamoja na
Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali kuendelea kukagua eneo hilo.
30.
Mheshimiwa Spika,Serikali iliendelea kutoa
kipaumbele katika kulipa Deni la Taifa. Katika kipindi hicho, malipo ya riba kwa mikopo ya ndani na
nje yalikuwa shilingi bilioni 438.8,sawa na asilimia 79 ya makadirio ya shilingi bilioni 555.2 kwa mwaka. Malipo ya deni halisi lamikopo
ya nje yalikuwa shilingi bilioni 79.0, sawa na asilimia 34 ya makadirio ya
mwaka. Aidha, Serikali ilitumia shilingi bilioni 1,364 kwa ajili ya kulipia
dhamana za Serikali za muda mfupi na Hatifungani za Serikali zilizoiva. Vilevile,
matumizi mengineyo katika Wizara, Idara, Taasisi za Serikali, Mikoa na
Halmashauri yalifikia shilingi bilioni 3,000.8 ikiwa ni asilimia 74ya makadirio
ya shilingi bilioni4,070.9kwa mwaka.
31.
Mheshimiwa Spika,hadi Aprili 2013, jumla ya
shilingi bilioni 3,956.3zilitolewakatika miradi ya maendeleo ikilinganishwa na
makadirio ya mwaka ya kutumia shilingi bilioni 4,594.8.Kati ya hizo, fedha za ndani
zilikuwa shilingi bilioni 2,277.2ikilinganishwa na makadirio ya mwaka ya shilingi
bilioni 2,280.6,sawa na asilimia 99.9. Aidha, fedha za nje zilikuwa shilingi
bilioni 1,679.1ikilinganishwa na makadirio ya shilingi bilioni 2,314.2 sawa na
asilimia 73 ya makadirio ya mwaka.
Usimamizi wa Fedha za Umma
32.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2012/13, Serikali
ilianza kutekeleza mpangokazi wa miaka mitano wa kuiwezesha Serikali Kuu
kuandaa hesabu kwa viwango vipya vya uhasibu vya Kimataifa (IPSAS Accrual
Basis). Kwa mara ya kwanza hesabu za
Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea na Sekretarieti za Mikoa kwa mwaka wa
fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2013 zitaandaliwa kwa kutumia viwango hivyo.
Wizara imeandaa miongozo mbalimbali na kufanya mikutano elekezi ili kuwajengea
uwezo wa uelewa wahasibu na wadau mbalimbali.
33.
Mheshimiwa Spika,katikakudhibiti mapato na
matumizi,Serikali imeandaa na kutoa miongozo ya usimamizi wa vihatarishi katika
sekta ya umma pamoja na mwongozo wa uhakiki wa ubora wa ukaguzi wa ndani.
Serikali pia imetayarisha mwongozo wa ukaguzi wa ndani kwa kuzingatia viwango
vya kimataifa ambao unategemea kuanza kutumika rasmi Julai, 2013. Miongozo hiyo
ina lengo la kuboresha utendaji kazi wa ukaguzi wa ndani.
Maslahi ya
Watumishi
34.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2012/13, Serikali
iliendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa umma kulingana na uwezo wa mapato
yake kwa lengo la kuwawezesha kumudu gharama za maisha. Maeneo ambayo
yalitiliwa mkazo ni pamoja na ongezeko la mshahara hasa kima cha chini,
kupunguza kiwango cha kodi ya mapato kwenye mishahara, malipo ya mshahara kwa
wakati na kuhakikisha watumishi wanalipwa mafao yao mara baada ya kustaafu.
Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA
II)
35.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa MKUKUTA II
umeonesha mafanikio katika maeneo mengi ingawa bado kuna changamoto. Mafanikio
hayo ni pamoja na kuendelea kukua kwa pato la Taifa, kuongezeka kwa mapato ya
kodi, kukua kwa sekta ya fedha na mikopo kwa sekta binafsi, kuimarika kwa usimamizi
wa matumizi ya Serikali na kuimarika kwa utoaji na upatikanaji wa huduma za
jamii.
36.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kutathmini hali ya umaskini hapa
nchini, Serikali imefanikiwa kukamilisha zoezi la ukusanyaji wa takwimu za
Utafiti wa Hali ya Mapato na Matumizi katika kaya binafsi ya mwaka 2012. Uchambuzi
wa takwimu hizo unaendelea na unatarajia kukamilika kabla ya Desemba 2013.
Aidha, takwimu za Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika 2012, na Utafiti wa Hali
ya Ajira na Kipato wa mwaka 2012 vitafanyiwa uchambuzi wa kina ili kutuwezesha
kupata takwimu zitakazoonesha hali ya umaskini katika ngazi mbalimbali. Tafiti
hizi zitatoa matokeo ya utekelezaji wa MKUKUTA katika nguzo ya kwanza ya
Kupunguza Umaskini na Ukuaji wa Uchumi.
37.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa nguzo ya pili ya MKUKUTA ya kuboresha
hali ya maisha na ustawi wa jamii, viashiria vingi vilionesha mabadiliko
chanya. Viwango vya uandikishaji katika ngazi za elimu ya msingi na sekondari
vimeimarika. Aidha, uandikishaji katika ngazi ya vyuo vya ufundi na elimu ya
juu uko katika kiwango cha kuridhisha. Matokeo haya yanatokana na utekelezaji
wa juhudi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya shule, vyuo,
waalimu, upanuzi wa miundombinu ya ufundishaji na kuongezeka kwa mikopo ya
elimu ya juu. Changamoto iliyopo ni kuboresha mazingira ya kufundishia na
kujifunza katika ngazi zote.Katika mwaka 2012/13,
Serikali iliendelea pia kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha huduma za afya,
lishe, upatikanaji wa maji safi na salama na utoaji elimu kwa umma kuhusu kinga
ya malaria na athari za ugonjwa wa UKIMWI.
38.
Mheshimiwa Spika, ili
kuimarisha utawala bora na uwajibikaji, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo
kuimarisha mfumo wa usimamizi wa mali za umma, kuimarisha mfumo wa sheria na
haki za binadamu, hususan katika ngazi za chini kwa kuongeza idadi ya
mahakimu. Hatua hii imeboresha kasi ya
utoaji maamuzi ya mashauri katika mahakama zetu. Aidha, programu ya maboresho
ya sekta ya sheria nayo iliendelea kutekelezwa, lengo likiwa ni kuhakikisha
kuwa haki za raia zinaboreshwa na kulindwa, hususan wale walio katika mazingira
hatarishi.
Sensa ya
Watu na Makazi
39.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2012/13, Serikali ilifanya Sensa ya Watu na Makazi kama ilivyopangwa
ambapo jumla ya shilingi bilioni 127.3 zilitumika. Matokeo ya sensa hiyo,
yalibainisha kuwa Tanzania ina jumla ya watu milioni 44.9 sawa na ongezeko la
asilimia 2.6 kwa mwaka ikilinganishwa na matokeo ya Sensa ya mwaka 2002 ambapo
ongezeko lilikuwa asilimia 2.9.
40.
Mheshimiwa Spika, kasi
ya ongezeko la idadi ya watu ni kubwa kwa mikoa ya Dar es Salaam na Mjini
Magharibi ambapo kasi ya ongezeko la idadi ya watu kwa mkoa wa Dar es Salaam ni
asilimia 5.6 kwa mwaka, wakati Mjini Magharibi kasi hiyo ni asilimia
4.2. Aidha, mkoa wa Dar es salaam una idadi
kubwa ya watu ikilinganishwa na mikoa mingine ukiwa na asilimia 10 ya idadi ya
wakazi wote wa Tanzania Bara. Vilevile, wastani wa idadi ya watu kwa kaya kwa
mwaka 2012 umebakia karibu sawa na ule wa mwaka 2002. Wastani ulikuwa watu 4.9
kwa kaya mwaka 2012 ikilinganishwa na watu 4.8 mwaka 2002. Napenda niwajulishe waheshimiwa
wabunge kwamba Serikali inatumia takwimuza sensahii katika kuandaa sera,
mikakati,mipangona kufanya tathmini ya utekelezaji wa mikakati na mipango yake.
Nashauri wadau wengine wafanye hivyo pia wakati wa kuandaa mipango ya maendeleo
kwa ajili ya ujenzi wa Taifa letu.
41.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inaendelea na uchambuzi wa kina wa matokeo ya Sensa ambayo yatahusisha
viashiria vya kiuchumi na kijamii. Napenda nitumie nafasi hii kuwajulisha kuwa toleo
linalofuata ni la mgawanyo wa watu kwa umri na jinsia katika ngazi ya Taifa,
Mkoa na Wilaya ambalo litatolewa mwezi Julai, 2013. Matokeo yanayofuata ambayo
yanahusu viashiria vya kiuchumi na kijamii yataendelea kutolewa kama
yalivyoanishwa kwenye ratiba ya usambazaji napia katika tovuti ya Serikali.
Sekta ya Fedha
42.
Mheshimiwa Spika,
Serikali iliendelea kutekeleza progamu ya maboresho ya sekta ya fedha ili
kuhakikisha kwamba sekta hii inachangia kikamilifu katika shughuli za kiuchumi
na kukuza Pato la Taifa. Katika mwaka 2012, huduma ya sekta ya fedha ilichangia
asilimia 1.8 ya pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 1.7 mwaka 2011. Aidha,
katika kipindi hicho, sekta ya fedha ilikua kwa asilimia 13.2 ikilinganishwa na
ukuaji wa asilimia 10.7 mwaka 2011. Ongezeko hilo lilitokana na mafanikio ya utekelezaji
wa maboresho ya sekta ya fedha ambayo yaliwezesha kuongezeka kwa idadi ya benki
kutoka 49 Februari 2012 hadi 51 Februari 2013; kampuni za bima kutoka 26 mwaka
2011 hadi 28 mwaka 2012;na idadi yaSACCOS kutoka 5,424 Machi 2012 hadi 5,559
Machi 2013.
43.
Mheshimiwa Spika, Serikali
iliendelea kutekeleza sera ya fedha yenye lengo la kupunguza ukwasi nchini
ambapo Benki Kuu iliongeza mauzo ya fedha za kigeni katika soko la fedha za
kigeni pamoja na mauzo ya dhamana za Serikali. Aidha, Benki Kuu ilipandisha
kiwango cha chini cha fedha zinazotakiwa kuhifadhiwa Benki Kuu kwa ajili ya akiba
ya amana za serikali katika mabenki kutoka asilimia 30 hadi asilimia 40, pamoja
na kupunguza kiwango cha kuhodhi fedha za kigeni kulingana na mitaji yao kwa
mabenki kutoka asilimia 10 hadi asilimia 7.5 kuanzia Desemba, 2012. Hatua hizo
zilisaidia katika kupunguza kiwango cha mfumuko wa bei usiojumuisha chakula na
nishati(core inflation) kutoka asilimia 8.7Mei, 2012 hadi asilimia 7.1 Mei,
2013. Vilevile, hatua hizi zilisaidia kuimarika kwa kiwango cha ubadilishanaji
wa shilingi dhidi ya Dola ya Kimarekani.
44.
Mheshimiwa Spika,Serikali ilifanya utafiti
wa huduma ndogo ndogo za bimakwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za bima
kwa wananchi walio wengi. Utafiti umebaini kwamba kiwango cha matumizi ya
huduma za bima bado ni kidogo, ambapo ni asilimia 19 tu ya watu wazima
wanatumia huduma hizo (hii inajumuisha huduma za bima ya afya zinazotolewa na Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya). Utafiti umebaini pia kwamba uhitaji wa huduma ndogo
ndogo za bima ni mkubwa na upatikanaji wa huduma hizo utasaidia katika juhudi
za Serikali za kukuza uchumi na kuondoa umaskini. Serikali iliendelea
kuwahamasisha wananchi ili waone umuhimu wa kujiunga na huduma za bima.
45.
Mheshimiwa Spika,Serikali ilianzisha kampuni
ya Tanzania Mortgage Refinancing Company (TMRC) ili kuwezesha benki kutoa
mikopo ya nyumba. Ili benki ziweze kupata mikopo hiyo, zinapaswa ziwe na hisa
kwenye kampuni hiyo. Hadikufikia Desemba2012,benki 12 zimenunua hisa. Serikali
kupitia Kampuni ya TMRC ilitoa mikopo yenyethamani ya shilingi bilioni 4.2 kwa
benki 12 wanachama, ambazo zilitoa mikopo 1,799 yenye thamani ya shilingi bilioni
106.2.
46.
Mheshimiwa Spika, katika kutimiza azma ya
Serikali ya kuimarisha usimamizi na maendeleo ya Sekta ya Fedha, Serikali
inaendelea kuweka mazingira mazuri kwa kuanzisha Idara ya Maendeleo ya Sekta ya
Fedha ambayo ndani yake kutakuwa na kitengo cha kusimamia sekta ya huduma ndogo
ndogo za fedha na kitengo cha sera za sekta ya fedha. Muundo huu mpya kwa sasa
uko katika hatua ya kuridhiwa. Miongoni mwa majukumu ya idara hii ni kuandaa
sera ya sekta ya huduma ndogo ndogo za fedha.
47.
Mheshimiwa Spika, katika kuhamasisha
uanzishwaji wa benki za wananchi, Benki kuu imekuwa ikitoa masharti nafuu
yanayohusu mtaji wakati zinapoanza. Kwa mfano, wakati benki za biashara
zinatakiwa kuwa na mtaji wa shilingi bilioni 15, benki za wananchi zinatakiwa
kuwa na shilingi bilioni 2. Kwa upande mwingine, Serikali imekuwa ikihimiza
uanzishwaji wa SACCOS, VICOBA na benki za wananchi ili kuwawezesha wananchi
kupata mitaji kwa ajili ya biashara na uzalishaji.
Ununuzi wa
Umma
48.
Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu
limetunga Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 baada ya kubaini
upungufu uliokuwepo katika Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 21 ya mwaka 2004.
Aidha, Bunge lako pia limetunga Sheria ya Ubia Na. 19 ya mwaka 2010 ambayo
utekelezaji wake katika hatua ya kumpata Mbia unatumia Sheria ya Ununuzi wa
Umma. Hivyo kuna haja ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7
ya mwaka 2011 ili kuzingatia maboresho na mabadiliko yanayohitajika. Mbali na
kuleta uwiano wa Sheria ya Ununuzi na Sheria ya Ubia, maboresho yanalenga
kuweka misingi imara ya taratibu za kusimamia ununuzi wa umma; kufafanua
majukumu ya Mamlaka za usimamizi wa ununuzi wa umma; na kuongezea madaraka ya
kiutendaji Taasisi za ununuzi na zile zinazosimamia ununuzi wa umma. Aidha, maboresho
yanalenga kupunguza muda wa kushughulikia malalamiko ya wazabuni, na kupunguza
muda wa mchakato wa ununuzi. Serikali inakusudia kufuta Sheria ya Ununuzi wa
Umma na. 21 ya 2004 mara baada ya mabadiliko ya Sheria Na. 7 kukamilika na
Kanuni mpya kutangazwa katika gazeti la Serikali.
Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi
49.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea
kusimamamia sera yake ya kushirikisha sekta binafsi ili iweze kuongeza Pato la
Taifa. Katika mwaka 2012/13, Serikali ilifanya uchambuzi wa awali wa baadhi ya
miradi ya PPP katika sekta za ujenzi wa barabara na bandari. Miradi hiyo ni
pamoja na ujenzi wa barabara ya Dar es Salaam – Chalinze, bandari ya Katanga,
bandari ya Mwambani, na bandari ya Mtwara.
50.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Sheria ya
Ubia ya mwaka 2010, changamoto iliyojitokezani kuwepo kwa vitengo na ofisi
nyingi zinazoshughulikia masuala ya PPP.Kwa kutambua hili, Serikali katika
mwaka 2013/14 itaunganisha vitengo vya PPP na kufanya mapitio ya sheria na
kanuni za ubia kwa nia ya kufanya maboresho.Aidha, katika mwaka 2013/14,
Serikali imepanga kuanzisha mfuko maalumu utakaotumika kugharamia upembuzi
yakinifu ili kuendeleza miradi ya ubia hapa nchini.
Deni
la Taifa
51.
Mheshimiwa Spika, hadi mwishoni mwa Machi 2013, Deni la Taifa (likijumuisha deni la umma
na sekta binafsi) lilikuwa shilingi bilioni 23,673.53 ikilinganishwa na deni la
shilingi bilioni 20,276.6 Machi 2012 likiwa ni ongezeko la asilimia 17. Kati ya
kiasi hicho, shilingi bilioni 18,282.02 ni deni la nje na shilingi bilioni
5,397.50 ni deni la ndani. Deni la nje, linajumuisha deni la umma la shilingi
bilioni 15,203.34 na deni la sekta binafsi ni shilingi bilioni 3,078.69. Kiasi
hicho cha deni la nje kinajumuisha deni halisi shilingi bilioni 16,087.43 na
malimbikizo ya riba ya shilingi bilioni 2,194.59. Deni la ndani linajumuisha
hati fungani za muda mrefu kiasi cha shilingi bilioni 4,261.03 na dhamana za
Serikali za muda mfupi kiasi cha shilingi bilioni 1,136.48.Mikopo hiyoiligharamia miradi ya maendeleo hususan
miundombinu kwakuzingatia vipaumbele vilivyopitishwa na Bunge lako tukufu.
Uhimilivu
wa Deni la Taifa
52.
Mheshimiwa Spika, Serikali inasimamia deni
la taifa kwa kuzingatia Mkakati wa Taifa wa Kusimamia Deni la Taifa pamoja na
Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 kama ilivyorekebishwa mwaka
2004. Kwa kuzingatia Sheria hiyo, mwaka 2012 Serikali ilifanya tathmini ya
kuangalia uhimilivu wadeni la Taifa. Napenda kulijulisha bunge lako tukufu
kwamba, viashiria vyote vya kupima uhimilivu wa deni vilivyokubalika kimataifa
vinaonesha kuwa, deni la Taifa ni himilivu katika muda mfupi na muda wa kati.
Mathalani, uwiano wa thamani ya sasa ya deni la Taifa kwa Pato la Taifa ni
asilimia 18.9, ikilinganishwa na ukomo wake wa asilimia 50 na kiashiria cha
uwiano wa thamani ya sasa ya deni la Taifa kwa mapato yanayotokana na mauzo ya
bidhaa na huduma nje ya nchi ilikuwa asilimia 53.6 ikilinganishwa na ukomo wa
asilimia 200.
Tathmini
ya Uwezo wa Kukopa na Kulipa Madeni
53.
Mheshimiwa
Spika,Serikali imepiga hatua kubwa
katika kufanikisha zoezi la nchi kufanyiwa tathmini ya uwezo wa kukopa na
kulipa madeni na ipo kwenye hatua ya kupata kampuni za kufanya tathmini. Kazi
hii imepangwa kukamilika mwaka 2013/14 ambapo itawezesha nchi kukopa kwa
gharama nafuu katika masoko ya fedha ya kimataifa kwa ajili ya kugharamia
miradi mikubwa ya miundombinu. Aidha, kampuni za Tanzania nazo zitaweza kupata
mitaji kwa urahisi zaidi kutoka kwenye masoko ya mitaji ya kimataifa.
Ushirikiano wa Kiuchumi wa Kikanda
54.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea
kuimarisha ushiriki katika Jumuiyaya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya
Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Africa (SADC). Ushiriki wetu katika jumuiya
hizi ni mojawapo ya mkakati wa kuhakikisha tunaitumia jiografia ya nchi yetu
kwa kukuza uchumi.
55.
Mheshimiwa Spika, mtangamano wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki umefikia hatua ya kuanzisha Umoja wa Fedha na majadiliano ya
Itifaki hiyo yanaendelea na yanatarajiwa kukamilika mwezi Novemba 2013. Aidha,
hatua zinachukuliwa za kutekeleza Itifaki ya Soko la Pamoja ambapo yameainishwa
maeneo katika sheria zetu yanayotakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuwezesha
ushiriki wa nchi katika soko hili. Baadhi ya sheria zitakazo
rekebishwa ni zile zinazohusika na taratibu za kuwezesha watanzania kuwekeza
mitaji yao katika nchi za Jumuiya; lengo likiwa kurahisisha biashara ya mitaji
na huduma ili kuchochea uwekezaji.
56.
Mheshimiwa
Spika, mwaka 2012/13, Serikali iliendelea na
utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maendeleo wa SADC, ambapo taratibu za kuridhia
Itifaki ya Fedha na Uwekezaji ya SADC zimekamilika. Itifaki hii itarahisisha
taratibu za uwekezaji katika nchi za SADC, kuwezesha nchi za SADC kuwianisha
sera za kodi hasa eneo la vivutio vya uwekezaji. Kupitia Itifaki hii, nchi za
SADC zitaweza kubuni na kutekeleza sera za kuimarisha uchumi na fedha kwa
pamoja kwa lengo la kuwa na utulivu wa uchumi katika ukanda huu na hivyo
kuvutia uwekezaji. Ili kuhakikisha azma
hii inatekelezwa kwa vitendo, nchi za SADC zinakamilisha utaratibu wa kuanzisha
Mfuko wa Maendeleo.
III.
MAFANIKIONA CHANGAMOTO
KATIKA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2012/13
57.
Mheshimiwa Spika, mafanikio na changamoto
za utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2012/13 kwa kila sekta yameelezwa kwa kina
katika hotuba za bajeti za wizara husika ambazo bunge lako tukufu limepata
fursa ya kuzijadili na kuzipitisha. Kwa kuzingatia hilo, nitaeleza kwa kifupi
baadhi ya mafaniko na changamoto hizo.
Ukusanyaji wa Mapato
58.
Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwaka 2012/13
ilitekelezwa kwa mafanikio, hususan katika ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi; utoaji
wa huduma za jamii; kuimarisha ulinzi na usalama, pamoja na utengamano wa
kikanda na kimataifa. Aidha, Serikali imefanikiwa kuongeza ukusanyaji wa mapato
ya ndani, hususan mapato ya kodi kutoka wastani wa shilingi bilioni 540 kwa
mwezi kwa mwaka 2011/12 hadi shilingi bilioni 640 kwa mwezi kwa mwaka 2012/13.
Pamoja na wastani huo wa mwezi, kiwango cha juu cha makusanyo kilifikiwa mwezi
Desemba 2012, ambapo makusanyo ya kodi na yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi
bilioni 890.
Ukuaji wa Uchumi
59.
Mheshimiwa Spika,Pato la Taifa limeendelea kuimarika mwaka 2012 ambapo
ukuaji halisi ulikuwa asilimia 6.9 ikilinganishwa na asilimia 6.4 mwaka 2011.
Ongezeko hili la ukuaji lilitokana na kuboreshwa kwa miundombinu ya
usafirishaji na mawasiliano, pamoja na kuimarika kwa uzalishaji viwandani
kutokana na jitihada za serikali za kuhakisha upatikanaji wa umeme wa uhakika
sambamba na matumizi ya nishati mbadala katika uzalishaji viwandani.
60.
Mheshimiwa Spika, sekta ya mawasiliano ndiyo ilikuwa na kiwango kikubwa
cha ukuaji wa asilimia 20.6 mwaka 2012. Pamoja na kuwa na kiwango kikubwa cha
ukuaji, sekta ya mawasiliano ilichangia asilimia 2.3 tu katika Pato la Taifa
ikilinganishwa na sekta ya kilimo ambayo pamoja na kukua kwa kiwango kidogo
ilichangia asilimia 24.7 katika Pato la Taifa mwaka 2012. Zaidi ya asilimia 70
ya watanzania wamejikita katika shughuli za kilimo, hivyo hii ni sekta ambayo
serikali inaitilia mkazo ili kuhakikisha kuwa inaleta mafanikio yanayotarajiwa
na wengi, ikiwemo kupunguza umaskini. Serikali imefanya jitihada kubwa za
kuboresha sekta hii lakini bado imeendelea kukua kwa kiwango kisichozidi
asilimia 5 kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
61.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kuimarisha sekta
ya kilimo ili ikue kwa kasi zaidi na kuongeza kipato na hivyo kupunguza umaskini
kwa wananchi walio wengi. Juhudi hizo zinahusisha kuendeleza miundombinu ya
umwagiliaji ili kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua; kutoa ruzuku za
pembejeo za kilimo kwa wakati zikiwemo mbolea, madawa na mbegu bora; kuondoa
kodi katika zana mbalimbali za sekta ya kilimo ili kuongeza tija; kuimarisha
masoko ya mazao, kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi na
uhifadhi; na kuimarisha barabara vijijini. Aidha, Serikali itaendeleza juhudi
za upatikanaji wa umeme na maji vijijini. Vilevile, Serikali itaimarisha sekta
nyingine za kiuchumi zenye kutoa ajira kama vile sekta za ujenzi na uzalishaji
viwandani, pamoja na kupanua wigo wa kinga ya jamii ili kuongeza ushiriki wao
kwenye shughuli za uchumi na hivyo kuinua
Pato la wananchi na kuongeza kasi ya kupunguza umaskini wa kipato.
Mwenendo wa Bei
62.
Mheshimiwa Spika,wastani wa mfumuko wa bei kwa mwaka 2012 uliongezeka
kwa asilimia 16.0 ikilinganishwa na asilimia 12.7 mwaka 2011. Upandaji huu wa
bei ulitokana hasa na kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli katika soko la dunia
na kupanda kwa bei za chakula kulikotokana na mahitaji makubwa ya chakula
katika baadhi ya nchi jirani. Ikumbukwe
kwamba chakula peke yake huchangia asilimia 47.8 ya bidhaa na huduma
zinazotumika katika ukokotoaji wa fahirisi ya bei kwenye kapu la bidhaa za
walaji, ikifuatiwa na usafiri (asilimia 9.5) na nishati (asilimia 9.2). Makundi
haya ni muhimu sana katika kuchochea mwelekeo wa bei za bidhaa na huduma
mbalimbali. Katika kukabiliana na kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma,
Serikali ilichukua hatua kadhaa zikiwemo:
(i)
Kuhakikisha
kuwa kunakuwa na ugavi mzuri wa chakula unaoendana na mahitaji nchini;
(ii)
Kupanua
kilimo cha mazao ya chakula na kuongeza upatikanaji wa pembejeo za kilimo
zikiwemo mbolea, madawa na mbegu bora;
(iii)
Kuimarisha
miundombinu ya usafirishaji;
(iv)
Kuimarisha
upatikanaji wa umeme; na
(v)
Kupandisha
kiwango cha riba ya Benki Kuu inayotozwa kwa mikopo iendayo kwa taasisi za
fedha nchini kutoka asilimia 7.58 hadi asilimia 12.58.
63.
Mheshimiwa Spika, hatua hizi ziliwezesha
kupunguza kiwango cha mfumuko wa bei kutoka asilimia 18.2 mwezi Mei 2012 hadi asilimia 8.3 mwezi Mei 2013.
Mafanikio Katika
Sekta Mbalimbali
64.
Mheshimiwa Spika, Serikali
ilitoa jumla ya shilingi bilioni 826.1 kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa
umeme na kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati. Baadhi ya miradi
iliyotekelezwa ni pamoja na: kuanza ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi
Dar es Salaam ikijumuisha ujenzi wa kituo cha kupokelea gesi Kinyerezi; kukamilisha
ujenzi na kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta mazito katika vituo vya
Ubungo - Dar es Salaam (MW 105) na Nyakato - Mwanza (MW 60); kuendeleza miradi
ya umeme vijijini katika mikoa 16; na kuendeleza upembuzi yakinifu katika
miradi ya Makaa ya Mawe – Mchuchuma na Liganga. Aidha, hadi kufikia mwezi
Desemba 2012, kiasi cha umeme kilichoingizwa kwenye Grid ya Taifa kilikuwa MWh
5,759,756 ikilinganishwa na MWh 5,153,400 mwaka 2011, sawa na ongezeko la
asilimia 11.8.
65.
Mheshimiwa Spika, sekta
ya maji iliendelea kupewa kipaumbele katika mwaka 2012/13 kwa kuendeleza ujenzi
wa miradi ya maji katika vijiji 682 kupitia mpango wa vijiji kumi kwa kila
Halmashauri; uboreshaji wa mamlaka za maji mijini; na ujenzi wa miundombinu ya
maji, ikiwemo bomba la maji la Ruvu Chini hadi Dar es Salaam. Ili kutekeleza
miradi ya maji, Serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni 106.6 katika ngazi ya
Wizara na shilingi bilioni 98.4 katika ngazi ya Halmashauri.
66.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Serikali
ilitoa jumla ya shilingi bilioni 537.40 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya
tiba, kinga na ustawi wa jamii. Fedha hizo pia zilitumika katika kuendeleza
ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya afya; kuimarisha stadi na kujenga uwezo
wa rasilimali watu; na kuanza ujenzi wa Chuo Kikuu cha Afya, Mlonganzila - Dar
es Salaam.
67.
Mheshimiwa Spika, Serikali
ilitoa jumla ya shilingi bilioni 2,421.5 katika sekta ya elimu kwa ajili ya
kugharamia shughuli mbalimbali katika shule za msingi, sekondari, elimu ya watu
wazima, vyuo vya ufundi stadi, na vyuo vya elimu ya juu. Baadhi ya shughuli
zilizotekelezwa ni pamoja na: ulipaji wa mishahara kwa wakati; kuajiri walimu
wapya 27,773 (walimu 13,633 wa shule ya msingi, 14,060 wa sekondari na 80 wa
vyuo vya ualimu) na kuwalipa stahili zao; kugharamia uendeshaji mashuleni
(Capitation); kutoa mikopo kiasi cha shilingi bilioni 326.1 kwa wanafunzi
96,350 wa elimu ya juu; kuanza ujenzi wa maabara katika shule mbili kwa kila Halmashauri
132 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 102.3 kimetolewa; ununuzi wa vitabu vya
kiada na ziada 27,159,106 kwa ajili ya
shule za msingi; na kuendelea kuboresha miundombinu ya kutolea elimu katika
ngazi zote nchini.
68.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa
jumla ya shilingi bilioni 1,044.2 kwa ajili ya kujenga na kukarabati barabara
za lami; kufanya matengenezo maalumu na ya kawaida kwenye barabara za
changarawe; kuboresha barabara za wilaya pamoja na kujenga na kukarabati
madaraja. Aidha, fedha hizo zilitumika kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vivuko
vitatuna maegesho; kukarabati vivuko vitano; na kufanya upembuzi yakinifu wa
kujenga barabara na vivuko katika maeneo mengine nchini. Vilevile, Serikali
iliendelea na ujenzi na ukarabati wa barabara za Dar es Salaam na miji mingine
mikuu ili kupunguza msongamano wa magari.
69.
Mheshimiwa Spika, sekta ya uchukuzi
ilipewa jumla ya shilingi bilioni
181.8 kwa ajili ya shughuli mbalimbali
ikiwemo: kuanzisha usafiri wa treni ya abiria jijini Dar es
Salaam kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari na adha ya usafiri jijini
Dar es Salaam; kuboresha na kurejesha huduma za treni za abiria na mizigo
katika reli ya kati na TAZARA; na kuendeleza miradi ya ujenzi wa viwanja vya
ndege vya Songwe, Katavi, Mwanza, Kigoma na Tabora.
70.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuimarisha
utawala bora, Serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni 27.0 kwa
ajili ya mchakato wa marekebisho ya Katiba ikiwa ni pamoja na kukusanya kura za
maoni katika mikoa yote 30 ya Tanzania Bara na Zanzibar na shilingi bilioni 40
kutekeleza mradi wa vitambulisho vya Taifa.Aidha, shughuli zingine muhimu
zilizotekelezwa ni kukamilisha rasimu ya awali ya katiba mpya, kuchapisha
nakala za rasimu ya katiba mpya na kuzisambaza kwa wadau mbalimbali nchini
pamoja na kuendesha mikutano ya Mabaraza ya Katiba.
71.
Mheshimiwa Spika, katika
kukabiliana na upungufu wa chakula kwenye baadhi ya maeneo nchini, Serikali
ilitoa jumla ya shilingi bilioni 42.87 mwaka 2012/13 zilizotumika kununua tani
53,269.70 za nafaka kwa ajili ya kuongeza chakula cha hifadhi ya Taifa. Aidha,
Serikali ilisambaza chakula cha msaada kwa wananchi wenye mahitaji katika
Halmashauri 47 na kuuza jumla ya tani 16,653 kwa wasagishaji wa nafaka ili
kurahisisha usambazaji wa unga wa sembe
na hatimaye kupunguza mfumuko wa bei nchini. Vilevile, uzalishaji wa
chakula katika msimu wa mwaka 2012/13 ulifikia tani milioni 13.34 ikilinganishwa
na mahitaji ya chakula ya tani milioni 11.97.
72.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo,
changamoto bado ni nyingi, ambazo ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato
kutoka vyanzo vya ndani na upatikanaji wamikopo ya nje yenye masharti ya
kibiashara kwa wakati na hivyo kuchelewa kupeleka fedha kwenye sekta husika.
Changamoto nyingine ni: madai ya wakandarasi, wazabuni, watumishi na watoa
huduma wa ndani na nje; kuimarisha miundombinu; kupata thamani ya fedha katika
ununuzi wa umma; kuongeza ubora na tija katika uzalishaji; kutumia fursa za
kijiografia katika ukuzaji wa uchumi; upatikanaji wa nishati ya umeme wa
uhakika;riba za mikopo; kusimamia deni la Taifa; kudhibiti mfumuko wa bei na
mabadiliko ya tabianchi.
73.
Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine
ni:huduma za
jamii hususan elimu, afya, na maji bado hazijafikia viwango vinavyotarajiwa;
kuongeza fursa za ajira;kukuza ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi
(PPP);na upatikanaji wa huduma za mikopo ya kilimo. Changamoto hizo zitaendelea
kutafutiwa ufumbuzi hatua kwa hatua katika kipindi cha muda wa kati na muda
mrefu. Aidha, Serikali imejipanga kukabiliana na baadhi ya changamoto hizi
katika mwaka 2013/14.
IV. BAJETI YA MWAKA 2013/14
74.
Mheshimiwa Spika,bajeti ya mwaka 2013/14itazingatia
vipaumbele vilivyoainishwa kwenye: Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2013/14 namfumo
mpya wa utekelezaji wa vipaumbele vyenye matokeo makubwa na ya haraka (Big Results Now – BRN); Awamu ya Pili ya
Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II); Malengo ya
Maendeleo ya Milenia 2015; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010; na programu
za maboresho katika sekta ya umma. Lengo likiwa ni kufikia Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025.
Shabaha na Malengo ya Bajeti kwa
Mwaka 2013/14
75.
Mheshimiwa Spika,bajeti ya mwaka 2013/14,
imejielekeza katika kufikia shabaha na malengo ya uchumi jumla yafuatayo:
(i)
Pato
halisi la Taifa linatarajiwa kukua kwa asilimia 7.0 mwaka 2013, na asilimia 7.2
mwaka 2014;
(ii)
Kuendelea
kudhibiti kasi ya upandaji bei ili ibaki kwenye viwango vya tarakimu moja,
ambapo mfumuko wa bei unatarajiwa kushuka zaidi kufikia asilimia 6.0 Juni 2014;
(iii)
Kuongezeka
kwa mapato ya ndani yatakayofikia uwiano na Pato la Taifa wa asilimia 20.2 mwaka 2013/14 ikilinganishwa na
matarajio ya asilimia 17.7 kwa mwaka 2012/13;
(iv)
Kuwa
na nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) isiyozidi asilimia 5.0 ya Pato la
Taifa mwaka 2013/14;
(v)
Kudhibiti
ongezeko la ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) katika wigo wa asilimia
15.0 Juni 2014 utakaowiana na malengo ya
ukuaji wa uchumi na kasi ya upandaji bei;
(vi)
Kuwa
na akiba ya fedha za kigeni itakayoweza kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa
na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne mwaka 2013/14;
(vii)
Kupunguza
tofauti ya viwango vya riba vya kuweka na kukopa; na
(viii) Kuimarisha thamani ya Shilingi na kuwa na kiwango
imara cha ubadilishanaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha.
Misingi
ya Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha mwaka 2013/14
76.
Mheshimiwa Spika,
ili
kufikia malengo yaliyoainishwa hapo juu, misingi ya bajeti ya Serikali kwa
kipindi cha mwaka 2013/14 ni hii ifuatayo:-
(i)
Kuendelea
kuimarisha na kudumisha amani, usalama, utulivu na utengamano;
(ii)
Kuendelea
kuboresha viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii vikiwemo Pato
laTaifa, biashara ya nje, fedha, mapato na matumizi na viashiria vya huduma za
jamii;
(iii)
Kuongeza
mapato ya ndani kwa kuimarisha vyanzo vilivyopo na kubuni vyanzo vipya vya
mapato;
(iv)
Kuboresha
usimamizi wa fedha za umma;
(v)
Kuimarisha
mfumo wa IFMS na kuhakikisha unatumika kuweka mihadi ya huduma na bidhaa kabla
ya malipo;
(vi)
Kuzingatia
vipaumbele vilivyopo katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano hasa vipaumbele vyenye matokeo makubwa na ya haraka pamoja na MKUKUTA II;
(vii)
Kuboresha
mfumo wa utekelezaji wa vipaumbele na uwajibikaji;
(viii) Kuendelea kuimarisha sera za fedha ili ziendane na
sera za bajeti zitakazosaidia kupunguza mfumuko wa bei na tofauti ya riba za
amana na za mikopo;na
(ix)
Kuendelea
kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuvutia
ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi.
Sera za Mapato
77.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14,
Serikali inakusudia kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha mapato ya ndani
yanayotokana na kodi na yasiyo ya kodi. Sera za mapato zinajumuisha kupanua
wigo wa kodi kwa kubainisha vyanzo vipya na kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji
wa mapato kutoka vyanzo vilivyopo.Aidha, hatua zaidi zitachukuliwa kudhibiti na
kupunguza misamaha ya kodi. Kwa ujumla, sera na hatua zitakazotekelezwa katika
mwaka wa fedha 2013/14 zinalenga kuimarisha uwezo wa Serikali kukusanya mapato
ya ndani ili kupunguza utegemezi kutoka nje, na kupunguza kutegemea kodi
zinazotokana na biashara za kimataifa ambazo zimeanza kushuka kutokana na
kuongezeka kwa biashara za ushirikiano wa kikanda katika nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo
ya Kusini mwa Afrika.
78.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mikakati ya
pamoja ya kuongeza mapato ya Serikali, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe
binafsi kwa hatua uliyochukua ya kuunda Kamati ya Spikailikuishauri Serikali
kuhusu vyanzo vya mapato ambapo baadhi ya mapendekezo yakeyamezingatiwakatika Sera
za Mapato kwenye Bajeti ya mwaka 2013/14.
79.
Mheshimiwa Spika, Serikali itatekeleza baadhi
ya mapendekezo yaliyotolewa na Labs ya
kubuni vyanzo vya mapato. Baadhi ya mapendekezo hayo ni kuanza kuuza vitalu vya
misitu na uwindaji kwa njia ya mnada na kufanya tathmini ya mali na ardhi ili
kuimarisha makusanyo ya tozo ya mali na kodi ya ardhi. Hatua nyingine za
kumairisha makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi tayari zimeshatangazwa kupitia
bajeti za Wizara husika.
80.
Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka wa
fedha wa 2013/14 itatekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha ukusanyaji wa
mapato ili kupunguza utegemezi. Moja ya hatua muhimu itakayotekelezwa katika
mwaka 2013/14 ni kuangalia upya misamaha ya kodi kwa lengo la kuipunguza. Hatua
nyingine zitakazochukuliwa ni pamoja na:
(i)
Kupunguza misamaha ya kodi kwa
kufuta msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwenye huduma za utalii. Aidha, Sheria
ya Uwekezaji itafanyiwa marekebisho ili kupunguza misamaha ya kodi na kubakiza
misamaha yenye tija na yenye kuchochea uwekezaji mkubwa katika sekta za uchumi
za kimkakati;
(ii)
Kuendelea kuunga mkono
jitihada za kuanzishakituo kimoja cha kutoa huduma bandarini (one stop centre) katika bandari. Aidha,
Serikali itaendelea kutekeleza mpango wa kuanzisha One Stop Border Posts katika mipaka kwenye vituo vya Holili, Mutukula,
Sirari, Horohoro, Kabanga, Tunduma, Rusumo na Namanga;
(iii)
Kuendelea kuwajengea uwezo
watumishi wa Serikali wakiwemo wa Mamlaka ya Mapato ili kupata ujuzi wa
kuthibiti mbinu za kukwepa kodi zinazotumiwa na makampuni makubwa hasa katika
sekta za mawasiliano, madini na gesi ukiwemo ujuzi wa kukagua uhamishaji wa
gharama yaani “transfer pricing” hivyo kudhibiti mianya ya kupotea kwa mapato;
(iv)
Mamlaka ya Mapato Tanzania
inaendela kuimarisha matumizi ya mashine za kieletroniki za kutoarisiti (Electronic Fiscal Devices-EFDs) ambazo
zimeunganishwa moja kwa moja na Mamlaka kwa mtandao wa kompyuta ili kuhakikisha
kuwa Serikali inapata mapato yake stahiki.
Aidha, Mashine hizi zinasimamiwa kupitia mtandao wa kielektroniki ambapo
hupeleka moja kwa moja taarifa kwenye hifadhi kuu ya Mamlaka kila siku.
(v)
Kuwajengea uwezo watumishi kwa
kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu ndani na nje ya nchi, hususan katika sekta
ya gesi, mafuta na madini ili kusimamia ipasavyo mapato yatokanayo na rasimali
hizo; na
(vi)
Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania itaanzisha
mfumo mpya ujulikanao kama Revenue
Gatewayambao utaanza kutumika rasmi kuanzia tarehe 1 Julai 2013. Mfumo huo
unalenga kuboresha mifumo iliyopo ya ulipaji kodi na upatikanaji wa taarifa za
malipo ya kodi kwa njia ya mtandao. Aidha, mfumo huo utarahisisha uhamishaji wa
fedha kutoka kwenye benki za biashara hadi Mfuko Mkuu wa Serikali. Vilevile,
mlipakodi atalazimika kujisajili kwa ajili ya kufanya malipo kupitia tovuti ya Mamlaka
ya Mapato Tanzania kabla ya kulipa kupitia mfumo wa Tanzania Interbank Settlement System (TISS). Mtumiaji wa mfumo huuatanufaika kwa kupata taarifa kwa njia
ya barua pepe kuhusu malipo yake ya kodi aliyofanya.
81.
Mheshimiwa Spika,Sera za mapato katika
mwaka 2013/14, zinalenga kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya shilingi
bilioni 11,154.1 sawa na asilimia 20.2 ya Pato la Taifa. Kati ya kiasi hicho,
mapato ya kodi ni shilingi bilioni 10,412.9, na mapato yasiyo ya kodi ni
shilingi bilioni 741.1. Mapato yanayotokana na vyanzo vya Halmashauri ni
shilingi bilioni 383.5 sawa na asilimia 0.7 ya Pato la Taifa.
Mikopo
ya Ndani
82.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali bado ina changamoto ya kugharamia miradi ya maendeleo kwa kutegemea
mapato ya ndani. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali itakopa kutoka
soko la ndani shilingi bilioni 552.3, sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa
kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.Aidha,katika mwaka 2013/14,
Serikali itakopashilingi bilioni 1,147.6 kwa ajili ya kulipia hatifungani na
dhamana za Serikali za muda mfupi zinazoiva.
Misaada
na Mikopo ya Masharti Nafuu
83.
Mheshimiwa Spika,Washirika wa Maendeleo
wamekuwa wakichangia katika bajeti ya matumizi ya maendeleo. Katika mwaka
2013/14,Serikali inatarajia kupata misaada na mikopo yenye masharti nafuu kiasi
cha shilingi bilioni 3,855.2 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Kati ya fedha
hizo, misaada na mikopo ya kibajeti ni shilingi bilioni 1,163.1;misaada na
mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni shilingi bilioni 2,191.6; na mifuko
ya kisekta ni shilingi bilioni 500.Aidha, Serikali itaendelea kusimamia
matumizi ya fedha za Washirika wa Maendeleo na kuhakikisha zinaleta ufanisi na
tija.
84.
Mheshimiwa Spika,kutokana na juhudi zao za
kuchangia maendeleo yetu, naomba kuwatambua na kuwashukuru Washirika wa
Maendeleo yetu kama ifuatavyo: Nchi
za Canada, China, Denmark, Finland, Hispania, India, Ireland, Italia, Japani,
Korea ya Kusini, Marekani, Norway, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi,
Uingereza, Ujerumani, na Uswisi, pia taasisi mbalimbali za Kimataifa ikiwemo
Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, BADEA, Global Funds, OPEC Fund,Saudi
Fund, Umoja wa Ulaya, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Mashirika ya Umoja
wa Mataifa. Tunawashukuru sana na tunathamini michango yao.
Mikopo ya nje yenye Masharti ya Kibiashara
85.
Mheshimiwa Spika,kwa kuzingatia mahitaji
makubwa ya kuendeleza miradi ya maendeleo kwa mwaka 2013/14 na changamoto za
upatikanaji wa mapato ya ndani, Serikaliitakopa kutoka nje mikopo yenye
masharti nafuu ya kibiashara shilingi bilioni 1,156.4, sawa na Dola za Marekani
milioni 700. Mikopo hiyo itatumika kugharamia miradi ya maendeleo kama
ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2013/14. Uamuzi wa kuendelea
kukopa kwa masharti nafuu ya kibiashara unazingatia uhimilivu wa Deni la Taifa
uliopo.
Sera za Matumizi
86.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Serikali
itatekelezasera za matumizi zifuatazo:-
(i)
Kuwianisha
matumizi na mapato yanayotarajiwa;
(ii)
Nakisi
ya bajeti (ikijumuisha misaada) haitazidi asilimia 5.0 ya Pato la Taifa;
(iii)
Mafungu
yatazingatia viwango vya matumizi vitakavyoidhinishwa na Bunge;
(iv)
Kutenga
fedha za kutosha katika kutekeleza miradi ya vipaumbele vilivyoainishwa katika
Mpango wa Maendeleo;na
(v)
Kuzingatia
Sheria ya Fedha za Umma na Sheria ya Ununuzi wa Umma.
87.
Mheshimiwa Spika, matumizi ya kawaida kwa mwaka 2013/14 yanalenga katika kufanikisha maeneo
yafuatayo: kugharamia nyongeza
ya mishahara pamoja na kulipa mishahara kwa wakati; kuboresha huduma za
kiuchumi na maendeleo ya jamii; kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; kuendelea na utoaji wa vitambulisho vya Taifa;
kukamilisha uchambuzi wa takwimu za sensaya watu na makazi; maandalizi ya uchaguzi
mkuu wa mwaka 2015;na kuendelea kulipa madeni ya ndani na nje yaliyoiva pamoja
na madai mbalimbali ya watumishi na wazabuni yaliyohakikiwa.
88.
Mheshimiwa spika,katika bajeti ya mwaka 2012/13, Serikali ililenga kupunguza
matumizi yasiyo ya lazima katika maeneo mbalimbali kama vile semina, usafiri wa
ndani na nje, ununuzi wa samani, maonesho mbalimbali na katika magari.Matokeo
ya hatua hizi yameleta mafanikio kadhaa ikiwemo yafuatayo: semina na warsha
zimepunguzwa; manunuzi ya magari mapya yamepunguzwa na yananunuliwa kwa kibali
cha Waziri Mkuu tu na ukubwa wa injini umepunguzwa na kubaki zenye ukubwa
uliokubalika (cc 3,000 au chini ya hapo); maonyesho pia yamepunguzwa mfano maadhimisho
ya wiki ya utumishi wa umma hayakufanyika mwaka 2012/13; ununuzi wa samani
kutoka nje umepungua.
89.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Serikali itaendelea kudhibiti
matumizi yake katika maeneo mbalimbali ikiwemo kutumia malipo ya simu kabla ya
huduma; kutumia utaratibu wa ununuzi wa magari wa pamoja ambao utapunguza
gharama za ununuzi; kupunguza matumizi ya magari ya Serikali kwa kuanzisha
utaratibu wa kuwakopesha magari watumishi wa Serikali wanaostahili; kuoanisha
kanuni za ununuzi wa umma za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwa lengo la
kuimarisha ununuzi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa;na kuhimiza matumizi ya
samani zinazotengenezwa nchini.
90.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi ya maendeleo,bajeti itazingatia
kutekeleza vipaumbele vya Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao
mwaka 2013/14 unaingia mwaka wa tatu wa utekelezaji kama ifuatavyo:
(i)
Miundombinu: - miundombinu ya nishati;
usafirishaji (barabara, reli, viwanja vya ndege, usafiri wa majini ); TEHAMA;
maji safi na maji taka na umwagiliaji;
(ii)
Kilimo:– ikijumuisha mazao ya
chakula na biashara, malighafi ya viwandani, ufugaji, uvuvi na misitu;
(iii)
Viwanda: – vinavyotumia malighafi
hususan za ndani, na kuongeza thamani, viwanda vikubwa vya mbolea na saruji,
viwanda vya kanda maalum za kiuchumi, kielektroniki na TEHAMA;
(iv)
Maendeleo
ya rasilimali watu na Ujuzikwa kutilia mkazo sayansi, teknolojia na ubunifu;
(v)
Uendelezaji
wa huduma za utalii, biashara na fedha; na
(vi)
Huduma za jamii: kuimarisha upatikanaji na
ubora wa huduma za jamii.
91.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14,
Serikali itaendelea kuboresha mfumo wa ugawaji wa fedha kwenye Mamlaka za
Serikali za Mitaa kwa kuzingatia sera ya ugatuaji wa madaraka na rasilimali.
Aidha, Serikali itaimarisha mifumo ya ndani ya mapato na matumizi kwa kutoa
miongozo mahsusi ya ukaguzi wa ndani, kuimarisha utendaji wa kamati za ukaguzi,
kutoa mafunzo ya usimamizi na uimarishaji mifumo ya udhibiti wa ndani kwa
Wakurugenzi wa Halmashauri. Vile vile, Mamlaka za Serikali za Mitaa
zitawezeshwa kuainisha uwezo wa pato la kila Halmashauri na fursa zilizopo
katika ukusanyaji wa mapato ya ndani; na kujenga uwezo wa Halmashauri katika
matumizi ya mfumo wa IFMS; kuhuisha baadhi ya vyanzo vya mapato ya ndani ili
kuongeza mapato; kuboresha mfumo wa uthamini wa majengo kwa kutumia kanuni za
jumla; kuhamasisha Halmashauri kutumia teknolojia rahisi ya mitandao ya simu za
mkononi katika kufanya malipo.
92.
Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha Wizara,
Idara zinazojitegemea, Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kutekeleza
majukumu yao, Serikali itahakikisha kwamba mafungu yanapata fedha kama ilivyoidhinishwa
na Bunge lako tukufu.
93.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mashauriano
ya Kamati ya Bunge ya Bajeti na Serikali, pamoja na mahitaji mengine ya
Serikali jumla ya shilingi bilioni 538.6 zimeongezwa katika Bajeti hii kama
mchanganuo unavyoonesha.
MCHANGANUO WA FEDHA AMBAZO
ZIMETOLEWA NA SERIKALI KUPITIA
MASHAURIANO NA KAMATI YA BUNGE YA
BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 13/14
|
FUNGU
|
MAELEZO
YA FUNGU
|
BAJETI
KABLA YA NYONGEZA YA MWAKA 2013/14
|
FEDHA
ZILIZOTOLEWA NA SERIKALI
|
JUMLA
BAJETI YA FUNGU IKIJUMUISHA NYONGEZA
|
MAELEZO
|
|
15
|
Tume
ya Usuluhishi na Uamuzi
|
1,924,748,000
|
350,000,000
|
2,274,748,000
|
Fedha
kwa ajili ya shughuli za usuluhishi wa migogoro ya wafanyakazi
|
|
21
|
Hazina
|
1,416,332,728,000
|
5,600,000,000
|
1,421,932,728,000
|
Fedha
kwa ajili ya kugharamia uchambuzi wa mapato ya ziada
|
|
35
|
Idara ya Kurugenzi ya Mashtaka
|
13,011,796,000
|
10,000,000,000
|
23,011,796,000
|
Fedha
kwa ajili ya matumizi ya kawaida
|
|
40
|
Mfuko
wa Mahakama
|
141,696,825,000
|
20,000,000,000
|
161,696,825,000
|
Fedha
za maendeleo
|
|
43
|
Wizara ya
Kilimo, Chakula na Ushirika
|
328,134,608,000
|
21,150,000,000
|
349,284,608,000
|
Fedha
za ruzuku ya mbolea
|
|
44
|
Wizara
ya Viwanda na Biashara
|
78,492,632,000
|
30,000,000,000
|
108,492,632,000
|
Fedha
za maendeleo kwa ajili ya Kurasini Logistic Hub-EPZ Development
|
|
49
|
Wizara
ya Maji
|
398,395,874,000
|
184,500,000,000
|
582,895,874,000
|
Fedha
za matumizi ya kawaida na maendeleo kwa ajili ya miradi ya maji vijijini
|
|
53
|
Wizara
ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
|
21,870,448,700
|
2,000,000,000
|
23,870,448,700
|
Fedha
za maendeleo kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake
|
|
70-95
|
HALMASHAURI
MBALIMBALI
|
1,247,049,476,000
|
10,800,000,000
|
1,257,849,476,000
|
Matumizi
ya kawaida Kutokana na ongezeko la makusanyo ya mapato kwa Halmashauri
|
|
58
|
Wizara
ya Nishati na Madini (REA)
|
1,102,429,129,000
|
186,900,000,000
|
1,289,329,129,000
|
Fedha
za maendeleo kwa ajili ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA)
|
|
62
|
Wizara ya
Uchukuzi
|
491,105,994,000
|
38,300,000,000.0
|
529,405,994,000
|
Fedha
za maendeleo kwa ajili ya miundombinu ya Reli na Mtaji kwa TAZARA
|
|
96
|
Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
|
21,328,045,000
|
9,000,000,000
|
30,328,045,000
|
Fedha
za maendeleo kwa ajili ya kuongeza usikivu TBC shilingi bilioni 6 na Mfuko wa
Maendeleo wa Vijana shilingi bilioni 3
|
|
99
|
Wizara ya
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi
|
47,180,225,000
|
20,000,000,000
|
67,180,225,000
|
Fedha
za maendeleo kwa ajili ya maendeleo ya mifugo na uvuvi
|
|
JUMLA
|
5,308,952,528,700
|
538,600,000,000
|
5,847,552,528,700
|
|
|
94.
Mheshimiwa Spika,kwa hali hiyo, Serikali itaongeza
juhudi za kukusanya mapato ya ndani, kuharakisha majadiliano na Washirika wa
Maendeleo na wakopeshaji mbalimbali katika kutafuta mikopo na misaada kwa
wakati. Ninatoa wito kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa kuhakikisha kwamba wanatimiza masharti na taratibu za kupata
fedha zilizoidhinishwa na Bunge.
Mfumo Mpya wa Uandaaji na Utekelezaji wa Vipaumbele
vya Miradi ya Maendeleo
95.
Mheshimiwa spika,kama ilivyoelezwa hapo awali kwenye hotuba ya Waziri
wa Nchi katika Ofisi ya Rais – Mahusiano na Uratibu, Mh. Stephen Masatu Wassira
(Mb), Serikali imeainisha maeneo ya kimkakati ambayo yatafungua fursa ya
mapinduzi ya kiuchumi na kuleta matokeo makubwa kiuchumi na kijamii kwa muda
mfupi. Maeneo hayo ni utafutaji wa mapato, kilimo, maji, elimu, nishati na
miundombinu ya uchukuzi. Serikali imedhamiria kutekeleza miradi kwenye maeneo
hayo katika kipindi cha muda wa kati.Utekelezaji
madhubuti wa vipaumbele hivi utafanikisha kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025 ya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati.
96.
Mheshimiwa spika,ili kuongeza ufanisi
katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Serikaliimeweka mikakati ya kuongeza
nidhamu ya kupanga na kutekeleza miradi ya mendeleo ili kupata matokeo
yanayowiana na thamani halisi ya fedha. Kwa kuzingatia hilo, Serikali
imeainisha maeneo makuu sita kama nilivyoeleza hapo awali ambayo yatazingatiwa
katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Aidha, kama mnavyofahamu, Serikali
imeunda chombo (Presidential Delivery Bureau) kitakachoratibu, kufuatilia na
kutathmini utekelezaji wa miradi katika sekta zilizobainishwa.
97.
Mheshimiwa spika,katika mwaka 2013/14,
Serikali imeweka kipaumbele katika kutatua kero ya maji kwa wananchi ambapo shilingi
bilioni 747.6zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya maji mijini na
vijijini. Katika kipindi cha muda wa kati, Serikali itaendelea na juhudi
zakuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama.
98.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha miundombinu
ya uchukuzi ambayo inajumuisha barabara, reli, madaraja, bandari na viwanja vya
ndege, Serikali imetenga shilingi bilioni 2,169.0 katika mwaka 2013/14
ikilinganishwa na shilingi bilioni 1,940.0 mwaka 2012/13. Kati ya fedha hizo
zilizotengwa mwaka 2013/14, shilingi bilioni 196.8ni kwa ajili ya kuimarisha
miundombinu ya reli ikilinganishwa na shilingi bilioni134.2 zilizotengwa mwaka
2012/13, sawa na ongezeko la asilimia 46.6.
Aidha, Serikali imedhamiria kuongeza bajeti na kuchukua hatua za
kuishirikisha sekta binafsi katika kuimarisha miuondombinu ya reli.
99.
Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza sekta ya
nishati na madini, juhudi zitaelekezwa katika kuongeza uzalishaji, usafirishaji
na usambazaji wa umeme ambapo jumla ya shilingi bilioni 1,426.9 zimetengwa kwa
ajili hiyo ikilinganishwa na shilingi bilioni 731.8 mwaka 2012/13.
Sekta ya Fedha
100.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Serikali itachukua hatua zifuatazo
katika kuboresha sekta ya fedha:-
(i)
Kutunga sheria ya Mfumo wa Malipo nchini kwa ajili ya
kuwa na utaratibu wa usimamizi wa mifumo ya malipo nchini ili kuboresha
matumizi ya kielektroniki katika kufanya malipo, hususan kwa kutumia simu za
mikononi, huduma za benki kwa njia ya mtandao, vituo vya mauzo na mashine za
kutolea fedha (ATM);
(ii)
Kuandaa Sera ya Bima ya Taifa; na
(iii)
Kufanyamapitio ya Sera ya Taifa ya Taasisi ndogo za
Fedha, 2002.
101.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha
2013/14 Serikali itaendelea na hatua za kuboresha sekta ya hifadhi ya jamii kwa
kutekeleza kazi zifuatazo:-
(i)
Kuandaa kanuni na miongozo ambayo itajikita katika
kuboresha sekta ya hifadhi ya jamii na kuifanya kuwa endelevu na yenye mchango
katika maendeleo ya wanachama wa mifuko na nchi kwa ujumla;
(ii)
Kusajili mifuko, mameneja uwekezaji (Fund Managers) na watunza mali (Custodians) kwa ajili ya kutenganisha
majukumu kwenye uendeshaji wa Mifuko ili kuleta ufanisi zaidi; na
(iii)
Kutoa elimu kwa umma kuhusu sekta ya hifadhi ya jamii.
Mikakati ya Kukabiliana na Changamoto
102.
Mheshimiwa Spika,kutokana na changamoto
nilizozieleza awali, serikali imeandaa mikakati ya kukabiliana nazo katika
mwaka 2013/14 kama ifuatavyo:kuhusu suala la tija katika kilimo, Serikali itaboresha
mfumo wa kilimo, mifugo na uvuvi uwe wa kibiashara badala ya ule wa kujikimu;
kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji; kuongeza upatikanaji na utumiaji wa
pembejeo za kilimo; kuimarisha huduma za ugani; upatikanaji wa mikopo kwa
wakulima, kusimamia upatikanaji wa masoko; na kuboresha mazingira ya uwekezaji
katika sekta ya kilimo.
103.
Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi ya fedha
za umma, Serikali itaendelea kuwajengea uwezo watumishi wa kada za uhasibu,
ununuzi, uhakiki mali na ukaguzi wa ndani. Aidha, Serikali itaimarisha,
usimamizi wa mali za Serikali na kufanya uhakiki wa mali za Serikali katika
Wizara, Mikoa na Halmashauri ili kuboresha daftari la mali za Serikali na
kubaini mali zisizokuwa na tija kwa ajili ya kuzifuta.
104.
Mheshimiwa Spika, katika hatua za kudhibiti
matumizi, Serikali itapunguza matumizi kwenye maeneombayo hayataathiri utoaji
wa huduma za msingi. Aidha, Serikali itapitia kanuni za ununuzi ili kuhakikisha
kuwa huduma na vifaa vinavyonunuliwa vinaendana na thamani ya fedha. Serikali
itaendelea kuhamasisha matumizi ya TEHAMA katika kupunguza gharama za
uendeshaji.
105.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Sheria
ya ununuzi wa umma, kumekuwepo na kanuni za ununuzi tofauti kati ya zinazotumika
katika Serikali Kuu na zile zinazotumika katika Serikali za Mitaa. Uzoefu
uliopo unaonesha kuwa kanuni hizo zimekuwa na changamoto nyingi za
kiutekelezaji. Ili kutatua tatizo hilo, Serikali imepanga kuoanisha kanuni za
ununuzi wa umma zinazotumika katika Serikali Kuu na zile zinazotumika katika
Serikali za Mitaa. Hatua hii itaboresha usimamizi na udhibiti wa ununuzi wa
umma. Ili kuhakikisha ununuzi wa umma unatekelezwa kulingana na Sera na Sheria
husika, Wizara ya Fedha itasimamia shughuli hiyo.
106.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha
usimamizi wa Deni la Taifa, Serikali inakamilisha taratibu za kuanzisha Idara
ya Usimamizi wa Deni la Taifa ndani ya Wizara ya Fedha ambayo itaanza kazi
mwaka 2013/14. Aidha, Serikali inapitia upya Mkakati wa Kusimamia Deni laTaifa
wa mwaka 2002 pamoja na kuifanyia marekebisho Sheria ya Mikopo, Dhamana na
Misaada ya mwaka 1974 iliyorekebishwa mwaka 2004, ili kutambua uanzishwaji wa
Idara ya Kusimamia Deni la Taifa kwa mujibu wa Sheria na kuiboresha ili kwenda
na wakati.
107.
Mheshimiwa Spika,katika kuhakikisha kwamba
Bajeti ya Serikali inatekelezwa kama ilivyokusudiwa, Serikali itawajengea uwezo
watumiaji wa Mfumo wa Malipo (IFMS) kuhusu maeneo yaliyoboreshwa katika toleo
la Epicor 9.02; kuhakikisha mihadi na malipo yote yanafanyika kwa kutumia mfumo
wa IFMS; na kufanya ukaguzi wa ununuzi kwenye Wizara, Idara zinazojitegemea,
Taasisi na wakala wa Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, Serikali
itaweka utaratibu wa kuibua miradi, kuifanyia upembuzi yakinifu na kuichambua
kabla haijatengewa fedha katika bajeti ya mwaka husikaili kuhakikisha kuwa
miradi inatekelezwa kwa wakati na Serikali inapata thamani halisi ya fedha.
108.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kutumia fursa za
kijiografia katika ukuzaji wa uchumi, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu
ya usafirishaji hususan barabara, reli, bandari, na viwanja vya ndege; kuongeza
upatikanaji wa nishati ya umeme; kuboresha huduma za utalii;kupunguza gharama
za kufanya biashara nchini ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje; na kuimarisha
ulinzi na usalama katika ngazi zote.
109.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14,
Serikali itaendelea kudhibiti mfumuko wa bei kwa kuhamasisha uzalishaji na
usambazaji sawia wa mahitaji muhimu kama vile chakula, mafuta ya nishati,
sukari, vifaa vya ujenzi na huduma za usafiri. Aidha, Serikali itatumia hifadhi
ya taifa ya chakula kusambaza chakula katika masoko kwa ajili ya kudhibiti bei.
110.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na
changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, Serikali itaimarisha kamati za kisekta
za kuratibu mifumo ya kuhimili na kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Mabadiliko ya Tabianchi;
kuhimiza wananchi kutumia nishati mbadala; kuhamasisha wananchi kupanda mazao
yanayostahimili ukame; kutumia chakula kilichopo kwa tija na uangalifu ili
kukidhi mahitaji ya msingi; kuchukua tahadhari ya upatikanaji wa umeme wa
uhakika; na kuelimisha wananchi wachukue tahadhari za mabadiliko ya tabianchi
pamoja na kuepuka uhaba wa chakula.
V.
MABORESHO YAMFUMO WA KODI,
ADA, TOZO NA HATUA NYINGINE ZA MAPATO
111.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendeleakuchukua
hatua za makusudi ili kuongeza mapato na kupanua wigo wa kodi hususan kubuni
vyanzo vipya vya mapato. Aidha, itaendelea pia kupunguza misamaha ya kodi katika
muda wa kati kutoka asilimia 4.3 ya Pato la Taifa katika mwaka 2011 hadi
kufikia walau asilimia 1. Hivi karibuni uchambuzi wa misamaha ya kodi umeonesha
kwamba, misamaha mingi ya kodi imetokana na kuongezeka kwa uwekezaji kwenye
maeneo ya kimkakati kupitia Kituo cha Uwekezaji. Aidha, Serikali ilisamehe kodi
na ushuru kwenye mafuta ya kuendeshea mitambo ya umeme wa dharura na pia
kusamehe kodi na ushuru kwenye uagizaji wa sukari na mchele ili kuziba pengo la
upungufu wa bidhaa hizo hapa nchini. Vile vile misamaha pia imekuwa ikitolewa
kwa wawekezaji katika Maeneo Maalum ambao wanazalisha bidhaa zinazouzwa nje
(EPZ na SEZ), ujenzi wa miundombinu na baadhi ya miradi inayofadhiliwa na
wahisani ili kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo yenye gharama kubwa kwa
ukamilifu.
112.
Mheshimiwa Spika, juhudi
zakupunguzamisamahazitaelekezwa zaidi katika kupunguza misamaha isiyo na tija
na yenye uwezekano wa kutumika vibaya. Kwa sasa Serikali inakamilisha mapitio
ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kupunguza misamaha. Aidha,
Serikali inakamilisha kazi ya utafiti wa kuchambua misamaha yote ya kodi ili
kuleta mapendekezo ya kupunguza misamaha isiyo na tija.
113.
Mheshimiwa Spika, kufuatia kuendelea kufanya
vibaya katika ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, Serikali iko katika hatua
nzuri ya kukamilisha utafiti wa kuangalia vyanzo vya mapato na kuwianisha
mifumo inayotumika katika ukusanyaji wa mapato hayo. Mapendekezo ya utafiti huo
yatazingatiwa kwenye kipindi cha mwaka 2014/15.
114.
Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo ya kiuchumina
mapato katika mwaka 2013/14, ninapendekeza kufanya maboresho ya sheria
mbalimbali za kodi kama ifuatavyo:
a.
Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;
b.
Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;
c.
Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
d.
Sheria ya Ushuru wa Mafuta, SURA, 220;
e.
Sheria ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82
f.
Sheria ya Usalama Barabarani, SURA, 168;
g.
Sheria ya Petroli (Petroleum Act) SURA, 392;
h.
Sheria ya Uwekezaji
Tanzania, SURA, 38;
i.
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka
2004;
j.
Marekebisho mengine madogo madogo katika baadhi ya sheria
za kodi na Sheria nyingine mbalimbali; na
k.
Marekebisho ya Ada na Tozo Mbalimbali za Wizara, Mikoa na
Idara zinazojitegemea.
(a)
Sheria ya Kodi ya Ongezeko la
Thamani, SURA 148
115.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho yafuatayo katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148
kama ifuatavyo: -
(i)
Kufuta msamaha wa VAT unaotolewa kwenye huduma za utalii chini ya Jedwali
la Pili la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Kipengele cha 14. Aidha,
hatua hii itahusisha huduma zifuatazo: (i)
Tourist Guiding (ii) Game driving (iii) Water Safaris (iv) Animal or bed
watching (v) Park fees (vi) Tourist Charter Services (vii) Ground Transport.
Hatua hii inalenga katika kutekeleza azma ya Serikali ya kupunguza misamaha ya
kodi. Hata hivyo, msamaha wa ushuru wa forodha utaendelea kutolewa kwenye vifaa
mbalimbali vinavyotumika katika kutoa huduma za utalii;
(ii)
Kutoa msamaha wa VAT kwa wazalishaji wa nguo nchini
zinazozalishwa kwa pamba ya ndani kwa bidhaa na huduma zitakazotumika tu kwenye
uzalishaji wa nguo hizo kupitia jedwali la tatu la Sheria ya kodi ya Ongezeko
la Thamani badala ya utaratibu wa sasa wa kutoza VAT kwa wazalishaji kwa
kiwango cha asilimia sifuri chini ya Jedwali la kwanza la Sheria ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani “VAT”. Kwa hatua hii mzalishaji wa nguo zinazotumia pamba
ya hapa nchini hatalipa VAT kwenye manunuzi ya pamba, umemr na malighafi za
uzalishaji wa nguo hizo;
Hatua hizi katika Kodi ya
Ongezeko la Thamani kwa pamoja zitaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha
shilingi milioni 48,977.60
(b)
Sheria ya Kodi ya Mapato,
SURA 332
116.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 kama ifuatavyo: -
(i)
Kupunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato ya
ajira kutoka asilimia 14 hadi asilimia 13. Hatua hii inalenga katika kutoa
nafuu ya kodi kwa mfanyakazi;
Viwango vya sasa na vile
vinavyopendekezwa ni kama ifuatavyo: -
Viwango vya sasa
|
Jumla ya Mapato
|
Kiwango cha Kodi
|
|
Mapato ya jumla yasiyozidi Shilingi 2,040,000/=
|
Asilimia sifuri (0%)
|
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 2,040,000 lakini
hayazidi shilingi 4,320,000/=
|
14% ya kiasi kinachozidi Shilingi 2,040,000/=
|
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 4,320,000/= lakini
hayazidi shilingi 6,480,000/=
|
Shilingi 319,200/= + 20% ya kiasi kinachozidi Shilingi
4,320,000/=
|
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 6,480,000/= lakini
hayazidi shilingi 8,640,000/=
|
Shilingi 751,200/= + 25% ya kiasi kinachozidi Shilingi
6,480,000/=
|
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi 8,640,000/=
|
Shilingi 1,291,200/= + 30% ya kiasi kinachozidi
Shilingi 8,640,000/=
|
Viwango vinavyopendekezwa
|
Jumla ya Mapato
|
Kiwango cha Kodi
|
|
Mapato ya jumla yasiyozidi
Shilingi 2,040,000/=
|
Asilimia sifuri (0%)
|
|
Mapato ya jumla yanayozidi Shilingi
2,040,000 lakini hayazidi shilingi 4,320,000/=
|
13% ya kiasi kinachozidi Shilingi 2,040,000/=
|
|
Mapato ya jumla yanayozidi
Shilingi 4,320,000/= lakini hayazidi shilingi 6,480,000/=
|
Shilingi 296,400/= + 20% ya
kiasi kinachozidi Shilingi 4,320,000/=
|
|
Mapato ya jumla yanayozidi
Shilingi 6,480,000/= lakini hayazidi shilingi 8,640,000/=
|
Shilingi 728,400/= + 25% ya
kiasi kinachozidi Shilingi 6,480,000/=
|
|
Mapato ya jumla yanayozidi
Shilingi 8,640,000/=
|
Shilingi 1,268,400/= + 30%
ya kiasi kinachozidi Shilingi 8,640,000/=
|
(i)
Kuanzisha kodi ya zuio
ya asilimia 10 ya kamisheni (commission) ya usafirishaji wa fedha kwa njia ya
simu za mkononi. Kodi hiyo itakusanywa na kampuni za simu kutoka kwa wakala
wanaotoa huduma za kusafirisha fedha kupitia simu za mkononi;
(ii)
Kutoza kodi ya zuio
kwa kiwango cha asilimia 5 kwenye malipo yatokanayo na huduma mbali mbali kama
vile huduma za ushauri wa kitaalamu na nyinginezo (Consultancy services and
other services). Kodi hii itatozwa bila kujali kama kuna Namba ya Utambulisho wa
Mlipa kodi (TIN) au la. Lengo la hatua hii ni kudhibiti na kulinda mapato ya
Serikali;
(ii)
Kutoza kodi ya zuio
kwenye bidhaa zinazonunuliwa na Serikali na Taasisi zake kwa kiwango cha
asilimia 2 bila kujali kama kuna Namba ya Utambulisho wa Mlipa kodi (TIN) au
la. Lengo la hatua hii ni kudhibiti na kulinda mapato ya Serikali;
(iii)
Kufuta msamaha wa kodi
ya zuio kwenye ukodishaji wa ndege kwa walipa kodi wasio wakazi (non-resident).
Hatua hii inalenga katika kupunguza misamaha ya kodi na kuhuisha mapato ya
Serikali;
Hatua hizi za Kodi ya Mapato
kwa pamoja zitaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 131,686.
(c)
Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147
117.
Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147 kama ifuatavyo:-
(i)
Kuongeza kiwango cha
Ushuru wa Bidhaa kwenye magari yasiyo ya uzalishaji (Non-Utility Motor
Vehicles) ya umri wa zaidi ya miaka 10 kutoka asilimia 20 hadi asilimia 25.
Hatua hii inalenga katika kupunguza uagizaji wa magari chakavu, kulinda mazingira
na kupunguza ajali;
(ii)
Kuanzisha kiwango
kipya cha Ushuru wa Bidhaa cha asilimia 5 kwenye magari ya uzalishaji (Utility
Motor Vehicles) yenye umri wa zaidi ya miaka 10 yanayotambuliwa katika HS Code
87.01, 87.02 na 87.04. Hatua hii haitahusisha magari chini ya HS Code 8701.10.00; na HS Code 8701.90.00 ambayo
kimsingi ni matrekta yaliyounganishwa; na magari yasiyounganishwa chini ya HS
Code 8702.10.11; 8702.10.21, 8702.10.91; 9702.90.11, 8702.90.21; 8702.90.91; HS
Code 87.04; 8704.10.10; 8704.21.10; 8704.22.10; 8704.23.10; 8704.31.10, na
8704.32.10, 8704.90.10. Lengo la kuanzisha kiwango kipya cha ushuru ni
kupunguza uagizaji wa magari chakavu, kulinda mazingira na kupunguza ajali.
Aidha, matrekta na magari yasiyounganishwa hayatatozwa ushuru huu kwa nia ya
kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta ya uunganishaji wa magari na hivyo kuongeza
ajira na mapato ya serikali;
(iii)
Kurekebisha viwango
vya Ushuru wa bidhaa kwenye mafuta ya Petroli kama ifuatavyo: -
a.
Mafuta ya Dizeli
kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 215 kwa lita hadi shilingi 217 kwa lita
ikiwa ni ongezeko la shilingi 2 tu;
b.
mafuta ya Petroli
kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 339 kwa lita hadi shilingi 400 kwa lita;
na,
c.
mafuta ya Taa kutoka
kiwango cha sasa cha shilingi 400.30 kwa lita kwa mafuta ya taa hakitabadilika;
(iv)
Kutoza ushuru wa
bidhaa wa asilimia kati ya 10 hadi asilimia 25 kwenye bidhaa mbalimbali
zinazozalishwa au kuingizwa nchini kama
vile; Mazulia, vipodozi, mafuta ya kujipaka, bidhaa na mifuko ya ngozi, bunduki
na risasi, boti za kifahari, ndege na helikopta;
(v)
Kuanzisha kiwango cha
Ushuru wa bidhaa wa asilimia 15 kwenye samani zinazoagizwa kutoka nje ya nchi,
zinazotambulika katika HS Code 94.03. Hatua hii inalenga katika kulinda na
kuhamasisha uzalishaji wa samani kwa kutumia mbao zinazozalishwa hapa nchini.
Aidha hatua hii itachochea ukuaji wa ajira na kuongeza mapato ya Serikali;
(vi)
Kutoza Ushuru wa
bidhaa wa asilimia 14.5 kwenye huduma zote (all
mobile phone services) za simu za kiganjani/mkononi badala ya muda wa
maongezi tu (airtime alone). Katika ushuru huu asilimia 2.5 zitatumika
kugharamia elimu hapa nchini.
(vii)
Kuongeza wigo wa
kutoza Ushuru wa bidhaa kwenye huduma za simu za mezani (zinazojulikana kama simu za TTCL) na zisizokuwa na waya;
(viii)
Kurekebisha viwango
maalum (specific rates) vya Ushuru wa bidhaa zisizokuwa za mafuta kama vile vinywaji baridi, mvinyo,
pombe, vinywaji vikali, sigara n.k. kwa
asilimia 10 kama ifuatavyo:-
(a) Vinywaji baridi, kutoka
shilingi 83 kwa lita hadi shilingi 91 kwa lita; Hilo ni ongezeko la shilingi 8
tu kwa lita;
(b) Ushuru wa bidhaa kwenye
maji ya matunda (Juisi) iliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa hapa nchini
kutoka shilingi 8 kwa lita hadi shilingi 9 kwa lita, sawa na ongezeko la
shilingi 1 tu kwa lita;
(c) Ushuru wa bidhaa kwenye
Juisi iliyotengenezwa kwa matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini kutoka
shilingi 100 kwa lita hadi shilingi 110 kwa lita, sawa na ongezeko la shilingi
10 kwa lita;
(d) Bia inayotengenezwa kwa
nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa, kutoka shilingi 310 kwa lita hadi
shilingi 341 kwa lita, sawa na ongezeko la shilingi 31 kwa lita;
(e) Bia nyingine zote, kutoka shilingi 525 kwa lita
hadi shilingi 578 kwa lita; yaani ongezeko la shillingi 51 kwa lita;
(f) Mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa
ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, kutoka shilingi 145 kwa lita
hadi shilingi 160 kwa lita, sawa na ongezeko
la shilingi 15 kwa lita moja;
(g) Mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje
ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, kutoka shilingi 1,614 kwa lita
hadi shilingi 1,775 kwa lita. sawa na ongezeko
la shilingi 161 kwa lita;
(h) Vinywaji vikali, kutoka shilingi 2,392 kwa lita
hadi shilingi 2,631 kwa lita; sawa na ongezeko la shilingi 239 kwa lita moja;
(i) Ushuru wa bidhaa kwenye
maji yanayozalishwa viwandani hautaongezeka;
(ix)
Kurekebisha viwango
vya ushuru wa bidhaa kwenye sigara kama ifuatavyo:-
(a)
Sigara zisizo na
kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa
kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 8,210 hadi shilingi 9,031 kwa
sigara elfu moja; sawa na ongezeko la senti 82 tu kwa sigara 1;
(b)
Sigara zenye kichungi
na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango
cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 19,410 hadi shilingi 21,351 kwa sigara
elfu moja; ikiiwa ni ongezeko la shilingi 1 na senti 94 kwa sigara moja;
(c)
Sigara nyingine zenye
sifa tofauti na (a) na (b) kutoka shilingi 35,117 hadi shilingi 38,628 kwa
sigara elfu moja; ikiwa ni ongezeko la shilingi 3 na senti 50 tu kwa sigara
moja;
(d)
Tumbaku ambayo iko
tayari kutengeneza sigara (“cut filler’) kutoka shilingi 17,736 hadi shilingi
19,510 kwa kilo; na
(e)
Ushuru wa Bidhaa kwa
“Cigar” unabaki kuwa asilimia 30.
Hatua hizi katika Ushuru wa Bidhaa kwa pamoja
zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni
510,017.50.
(d)
Sheria ya Ushuru wa Mafuta,
SURA, 220;
118.
Mheshimiwa Spika, ili kuongeza uwezo wa
Serikali katika kugharamia ukarabati wa miundo mbinu ya barabara ambayo ni
muhimu katika kuleta maendeleo na kujenga uchumi hapa nchini, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Mafuta ya
Petroli, SURA, 220 kama ifuatavyo: -
(i)
Kuongeza kiwango cha
Ushuru wa mafuta (fuel levy) kutoka shilingi 200 kwa lita hadi shilingi 263 kwa
lita, sawa na ongezeko la shilingi 63 kwa lita.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali
kwa kiasi cha shilingi milioni
155,893.50
(e)
Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA
82
119.
Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho katika Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82
kama ifuatavyo:-
(iv)
Kupunguza tozo ya
kuendeleza mafunzo ya ufundi stadi (Skills
Development Levy “SDL”)kutoka kwenye kiwango cha sasa cha asilimia 6 hadi
kiwango cha asilimia 5. Aidha, sambamba na kupunguza kiwango cha sasa cha SDL,
Taasisi za Serikali zisizotegemea bajeti ya Serikali kwa kiwango kikubwa katika
kujiendesha pia zitalipa tozo hii.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali
kwa kiasi cha shilingi milioni
28,213.90
(f)
Sheria ya Usalama Barabarani,
SURA, 168;
120.
Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho katika Sheria ya Usalama Barabarani, SURA, 168 ili kuongeza viwango vya Ada ya mwaka ya leseni
za Magari (Annual
Motor vehicle Licence Fee) kama ifuatavyo: -
(i) Gari lenye ujazo wa Injini
501.cc – 1500.cc kutoka kiwango cha sasa
cha shilingi 100,000 hadi shilingi 150,000;
(ii) Gari lenye ujazo wa Injini
1501.cc – 2500.cc kutoka kiwango cha
sasa cha shilingi 150,000 hadi shilingi 200,000;
(iii) Gari lenye ujazo wa Injini
zaidi ya 2501.cc kutoka kiwango cha sasa
cha shilingi 200,000 hadi shilingi 250,000.
(iv) Magari yenye ujazo wa Injini
chini ya 501cc hayatatozwa Ada ya leseni
za magari.
Hatua hii itatekelezwa kupitia tangazo
litakalochapishwa kwenye Gazeti la Serikali.
Hatua hizi kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato
ya Serikali kwa kiasi cha shilingi
milioni 19,710.90
(g)
Sheria ya Petroli (Petroleum
Act), SURA, 392;
(ii)
Ili kutekeleza dhamira
ya Serikali ya kusambaza umeme vijijini, napendekeza kuanzisha Tozo ya mafuta
ya petroli (petroleum levy) ya shilingi 50 kwa lita ambayo itakusanywa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Mapato yatakayokusanywa kutoka kwenye tozo
hiyo yatatumika kugharamia mahitaji ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) katika
kusambaza umeme vijijini. Hatua hii itatekelezwa kupitia tangazo
litakalochapishwa kwenye Gazeti la Serikali.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali
kwa kiasi cha shilingi milioni
123,725.
(h)
Sheria ya Uwekezaji Tanzania, SURA, 38
Kutoza asilimia 25 ya ushuru wa forodha unaopaswa kutozwa kwenye bidhaa
zinazotambulika kama “Deemed Capital
Goods” (yaani kutoa msamaha wa kodi wa asilimia 75 kwenye bidhaa hizo
badala ya asilimia 90 za sasa), na kuziondoa baadhi ya bidhaa kwenye orodha ya
kupata msamaha. Bidhaa hizo ni zile ambazo hazina uasilia wa kuwa bidhaa za
mtaji (capital goods) kama vile vifaa vya ofisi, samani, sukari, vinywaji
(viburudisho), bidhaa za mafuta ya petroli, magari madogo (Non Utility Motor
Vehicles), viyoyozi, majokofu, na vifaa vya kielektroniki, mashuka, vijiko,
vikombe nk.
(i)
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,
ya mwaka 2004
121.
Mheshimiwa Spika,
Mawaziri wa Fedha kutoka katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya Kikao
cha mashauriano kuhusu masuala ya Bajeti
(Pre-Budget Consultations of EAC Ministers for Finance) tarehe 07 Juni 2013
mjini Arusha. Kikao hicho kilipendekeza marekebisho ya viwango vya Ushuru wa
Pamoja wa Forodha (EAC-Common External Tariff “CET”) na Sheria ya Forodha ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-Customs
Management Act, 2004) kwa mwaka wa fedha wa 2013/14.
122.
Mheshimiwa Spika,maeneo yaliyopendekezwa
kufanyiwa marekebisho kwenye viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha ni:-
(i) Kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia
10 badala ya asilimia 35 kwenye ngano inayotambuliwa katika HS Code 1001.99.20
na HS Code 1001.99.90. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa viwanda na
wazalishaji wa bidhaa na vyakula vinavyotumia ngano hiyo;
(ii) Kutoza ushuru wa
asilimia 25 kwenye bidhaa za mchele na sukari wakati bidhaa hizo zinapoingizwa
nchini kwa msamaha maalumu wa Serikali baada ya kupata ridhaa ya Baraza la
Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Bidhaa hizo kwa sasa zinatozwa Ushuru
wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa asilimia 100 kwa sukari na asilimia
75 kwa mchele.
123.
Mheshimiwa Spika,Mawaziri wa Fedha wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki walifanya marekebisho kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC-Customs Management
Act, 2004) kama ifuatavyo:-
(i)
Kurekebisha Jedwali la
Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ili kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwa
mashine na vipuli vya reli vinavyoagizwa na Shirika la Reli Tanzania. Hatua hii inalenga katika kutoa unafuu
kwenye gharama za kuboresha reli na kuimarisha usafirishaji wa reli;
(ii)
Kufuta utaratibu wa kutokukagua mizigo inayoingizwa na wafanyabishara
ujulikanao kama “Compliant Trader Scheme”
ambao uzoefu umeonesha kwamba unatumiwa vibaya na baadhi ya wafanyabiashara
wasio waaminifu kukwepa kulipa kodi sahihi na hivyo kuipotezea Serikali mapato
yake halali;
(iii) Kuimarisha mfumo wa
uthamini (valuation) wa bidhaa kutoka nje ya nchi ili kuondoa tatizo la upotevu
wa mapato kutokana na uthamini usio sahihi. Hatua zitakazochukuliwa ni pamoja
na kuboresha mfumo wa Import Export
Commodity Database (IECDB);
(iv)
Kuendelea kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha (duty remission) kwa
malighafi ya kutengeneza sabuni inayojulikana kama LABSA inayotambuliwa katika
HS Code 3402.11.00; HS Code 3402.12.00 na HS Code 3402.19.00 kwa kipindi
kingine cha mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika kuimarisha uzalishaji na
kukuza viwanda vidogo na vya kati vya sabuni hapa nchini;
(v)
Kutoa msamaha wa
ushuru wa forodha kwenye mifuko ya plastiki inayotumika katika uzalishaji wa
nishati ya gesi (plastic bag biogas
digesters). Lengo la hatua hii ni kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala
na kutunza mazingira;
(vi)
Kuongeza ushuru wa forodha kwenye mawe
yanayotumika katika mashine za kusaga bidhaa mbalimbali kutoka asilimia sifuri
hadi asilimia 25. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani vya Jumuiya
ya Afrika Mashariki;
(vii)
Kutoa msamaha wa
ushuru wa forodha kwenye mitambo ya kusafisha uchafu katika maji (Water
treatment effluent plant) unaotoka viwandani kutoka asilimia 10 hadi asilimia
sifuri. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha viwanda vya ndani kutumia mitambo hii
ili kupunguza uchafuzi wa mazingira na kupunguza gharama za uzalishaji
viwandani;
(viii)
Kuendelea kutoa
msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye migahawa ya Majeshi ya Ulinzi kwa kipindi
cha mwaka mmoja;
(ix)
Kufanya marekebisho
kwenye Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili
kutoa msamaha kwa Idara ya Usalama wa Taifa.
Hatua hizi kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato
ya Serikali kwa kiasi cha shilingi
milioni 135,526.90
(j) Marekebisho
mengine madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na sheria nyingine
mbalimbali.
124.
Mheshimiwa Spika,napendekeza kufanya
marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika Sheria mbalimbali za
kodi ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha utekelezaji wake.
(i) Kwa
kutambua kwamba Sekta binafsi ndiyo yenye msukumo mkubwa katika maendeleo ya
uchumi duniani kote, napendekeza kufanya marekebisho katika sheria ya Public
Procurement Act, 2011 na Public Private Partnership Act 2010 ili kuwezesha “unsolicited PPP Proposals” kutohusika na
utaratibu wa ushindani ikiwa ni njia mojawapo ya kuvutia wawekezaji katika miradi
ya maendeleo kwa manufaa ya kiuchumi ya nchi yetu;
(ii) Kurekebisha
Sheria ya Fedha Za Umma SURA 348, Sheria ya Msajili wa Hazina SURA 418, na
Sheria ya Wakala za Serikali, SURA 245, ili kuweka sharti kwa wakala na taasisi
za serikali kuwasilisha kiasi cha asilimia 10 ya mapato ghafi (badala ya mapato
ya ziada) ya taasisi na wakala hizo kwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
(k)
Marekebisho ya Ada na Tozo
Mbalimbali za Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea
125.
Mheshimiwa Spika,napendekeza kufanya
marekebisho ya viwango vya ada na tozo mbali mbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa
na Idara zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana na hali halisi ya ukuaji wa
uchumi.
(l)
Tarehe ya Kuanza Kutekeleza
Hatua Mpya za Kodi
126.
Mheshimiwa Spika,hatua hizi za kodi
zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2013, isipokuwa pale
ilipoelezwa vinginevyo.
VI.
SURA YA BAJETI KWA MWAKA
2013/14
127.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sera za
uchumi jumla pamoja na misingi na shabaha ya bajeti, sura ya bajeti itakuwa
kama ifuatavyo; Serikali imepanga kukusanya jumla ya shilingi bilioni 18,249
kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje. Mapato
ya kodi na mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufikia shilingi bilioni 11,154.1
sawa na asilimia 20.2 ya Pato la Taifa. Aidha, mapato kutokana na vyanzo vya
Halmashauri yanatarajiwa kufikia shilingi bilioni 383.5 sawa na asilimia 0.7 ya
Pato la Taifa.
128.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14 Washirika
wa Maendeleo wanatarajiwa kuendelea kutupatia misaada na mikopo ya jumla ya
shilingi bilioni 3,855.2. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni1,163.1 ni
misaada na mikopo ya kibajeti na shilingi bilioni 2,692.1ni mikopo na misaada
kwa ajili ya miradi ya maendeleo, na Mifuko ya Pamoja ya Kisekta shilingi
bilioni 500.4.
129.
Mheshimiwa Spika, ili kuziba nakisi ya
bajeti, Serikali inatarajia kukopa kutoka katika vyanzo vya ndani na nje shilingi
bilioni 2,856.3. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 1,147.6 ni kwa ajili ya
kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na mkopo wa ndani shilingi
bilioni 552.3 ambao ni asilimia moja ya Pato la Taifa na shilingi bilioni 1,156.4ambazo
ni mikopo yenye masharti ya kibiashara zitatumika kwa ajili ya miradi ya
maendeleo.
130.
Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi, jumla ya
shilingi bilioni 18,249 zimekadiriwa kutumika katika mwaka 2013/14, kwa ajili
ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo. Kati ya hizo matumizi ya kawaida ni
shilingi bilioni 12,574.9 ambayo yanajumuisha shilingi bilioni 4,763 kwa ajili
ya mishahara ya watumishi wa Serikali,Taasisi na Wakala za Serikali; Mfuko Mkuu
wa Serikali shilingi bilioni 3,319.2, na Matumizi Mengineyoshilingi bilioni 4,492.6.
131.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2013/14 jumla ya
shilingi bilioni 5,674 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, ambapo
kiasi cha shilingi bilioni 2,982 kitagharamiwa kwa fedha za ndani. Kati ya
kiasi hicho, shilingi bilioni 552.3 zinatokana na mkopo kutoka vyanzo vya
ndani, shilingi bilioni 1,156.4 ni mikopo ya masharti ya kibiashara, shilingi
bilioni 386.2 ni mikopo ya kibajeti, na shilingi bilioni 887.1 zitatokana na
asilimia 8 ya mapato ya kawaida. Kiasi cha shilingi bilioni 2,692.6
kitagharamiwa kwa fedha za nje, misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo ikijumuisha
Mifuko ya Pamoja ya Kisekta.
132.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa
bajeti kama ulivyoelezwa hapo juu, mfumo wa bajeti kwa mwaka 2013/14 unakuwa
kama ifuatavyo:
|
|
Mapato
|
Shilingi Milioni
|
|
|
A.
|
Mapato ya Ndani
|
|
11,154,071
|
|
(i) Mapato
ya Kodi (TRA)
|
10,412,937
|
|
|
|
(ii) Mapato
yasiyo ya Kodi
|
741,134
|
|
|
|
|
|
||
|
B.
|
Mapato ya Halmashauri
|
|
383,452
|
|
C.
|
Mikopo na Misaada ya Kibajeti
|
|
1,163,131
|
|
D.
|
Mikopo na Misaada ya Miradi ya Maendeleo ikijumuisha
MCA (T)
|
|
2,692,069
|
|
E.
|
Mikopo ya Ndani
|
|
1,699,860
|
|
F.
|
Mikopo yenye Masharti ya Kibiashara
|
|
1,156,400
|
|
|
|
|
|
|
|
JUMLA YA MAPATO YOTE
|
|
18,248,983
|
|
|
|
|
|
|
|
Matumizi
|
|
|
|
G.
|
Matumizi ya Kawaida
|
|
2,574,949
|
|
|
(i) Deni la
Taifa
|
3,319,156
|
|
|
|
(ii)
Mishahara
|
4,763,196
|
|
|
|
(iii)
Matumizi Mengineyo
|
4,492,566
|
|
|
|
Wizara3,738,316
|
|
|
|
|
Mikoa
49,701
|
|
|
|
|
Halmashauri 04,549
|
|
|
|
H.
|
Matumizi ya Maendeleo
|
|
5,674,034
|
|
|
(i) Fedha za
Ndani
|
2,981,965
|
|
|
|
(ii) Fedha za
Nje
|
2,692,069
|
|
|
|
JUMLA YA MATUMIZI YOTE
|
|
18,248,983
|
VII. HITIMISHO
133.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo
awali, bajeti ya mwaka 2013/14imelenga kutekeleza Mpango wa Kwanza wa Maendeleo
wa miaka mitano; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010; Awamu ya Pili ya
Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II);Malengo ya
Maendeleo ya Milenia 2015; na kuanza kutekeleza maeneo ya vipaumbele
yaliyoainishwa katika Labs. Madhumuni
ya mipango namikakati hii ni kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo
2025.
134.
Mheshimiwa Spika, suala ambalo ningependa
kulisisitiza ni sote kwa pamoja kuongeza ushirikiano katika kusimamia majukumu
na matumizi ya fedha na rasilimali zetu vizuri ili kuongeza ufanisi. Masuala
yote tuliyoyajadili katika bunge hili ni ya msingi sana,hivyo kama yakifanyiwa
kazi kwa ufanisi tutafikia matarajio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambayo
yanalenga kuitoa Tanzania katika kundi la nchi maskini na kuingia katika kundi
la nchi zenye viwango vya kati vya mapato na hali bora ya maisha.
135.
Mhesimiwa Spika,bajeti hii imelenga pia
kuongeza makusanyo ya mapato, hasa ya ndani kwa kuanzisha vyanzo vipya na
kuboresha vilivyopo. Lengo likiwa ni kujitosheleza kwa mapato yatakayowezesha
kutekelezwa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha huduma kwa
wananchi. Katika kikao hiki cha Bunge la bajeti, waheshimiwa wabunge
walipendekeza kuongeza fedha kwa baadhi ya mafungu ili kuyawezesha kutekeleza
majukumu yao kikamilifu. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Serikali
sikivu ya Chama cha Mapinduzi imezingatia kwa kiasi kikubwa mapendekezo hayo. Ili
kutekeleza mapendekezo hayo, imelazimu kufanya maboresho zaidi katika kodi na
tozo mbalimbali kwani isingewezekana kugharamia mapendekezo hayo bila kuathiri
upande wa kodi. Hivyo, waheshimiwa wabunge naomba mnielewe katika hili na
kuniunga mkono ili mafungu yaweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kufikia
malengo tuliojiwekea.
136.
Mhesimiwa Spika,Serikali kwa upande wake
inaendelea kuboresha miundombinu ya kiuchumi, kifedha na kijamii ili kuongeza
fursa za ushiriki wa wananchi katika uzalishaji na kuboresha hali zao za maisha.
Bajeti, inalenga pia kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika, kuendeleza
ardhi na kuunganisha nchi yetu kwa njia ya miuondombinu ya barabara, reli na
viwanja vya ndege na mawasiliano. Hii itasaidia pia kutumia vyema fursa za
kijiografia zinazotokana na kupakana na nchi zisizokuwa na bahari.Aidha, bajeti
hii inalenga kufungua fursa za kuchumi na kijamii kwa ajili ya maendeleo
endelevu kupitia mfumo mpya wa utekelezaji wa miradi ya kipaumbele ambapo
italeta matokeo makubwa kwa haraka.
137.
Mheshimiwa Spika, bajeti ya Serikali kwa
mwaka 2013/14 imezingatia mapendekezo ya Kamati ya Bajeti na Kamati za Kisekta
za Bunge kadiri hali ya fedha ilivyoruhusu. Ushauri uliotolewa na Kamati hizo
na hoja mbalimbali zilizotolewa na waheshimiwa wabunge zilifanyiwa kazi kadiri
ilivyowezekana. Aidha, kwa utaratibu huu mpya wa mzunguko wa bajeti ambao ulipitisha
bajeti za mafungu mbalimbali, maelelezo yangu haya ni kuhitimisha mjadala wa
bajeti ya Serikali kwa mwaka 2013/14.
138.
Mheshimiwa Spika, yote niliyoyasema
yanawezekana iwapo kila mmoja wetu na wananchi kwa ujumla tutatimiza wajibu
wetu, kila mmoja kwa nafasi yake, kwa kushiriki na kuwajibika kikamilifu katika
kutekeleza sera na mipango tuliyojiwekea.
COMMENTS