TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI: 09/06/2013 MAONI YA AWALI YA MWENYEKITI WA CUF KUHUSU RASIMU YA KATIBA MPYA UTANGULIZI; Kwan...
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:
09/06/2013
MAONI YA AWALI YA MWENYEKITI WA CUF
KUHUSU RASIMU YA KATIBA MPYA
UTANGULIZI;
Kwanza
naipongeza Tume ya Jaji Warioba kwa kazi kubwa waliofanya ya kuratibu maoni na
kuja na mapendekezo ya katiba mpya ambayo hayakushinikizwa na matakwa ya Chama
tawala cha CCM. Tume imeonyesha ujasiri mkubwa na hakika wahafidhina wa chama
hicho watachukia sana.
Mambo
mengi yaliyopendekezwa na Chama Cha Wananchi CUF yameingizwa katika Rasimu ya
Katiba. Mambo hayo ni pamoja na mfumo wa Muungano wa serikali tatu, kuruhusiwa
mgombea binafsi, Rais kutangazwa kushinda akipata zaidi ya asilimia 50 ya kura
zote zilizopigwa la sivyo uchaguzi urudiwe kwa wale wawili walio ongoza kwa
kura, Tume huru ya uchaguzi, Mawaziri kutokuwa wabunge, Spika kutokuwa mbunge,
haki za watu wenye ulemavu, haki za binadamu na mengine mengi.
Hata
hivyo mambo mengi muhimu kama vile umilikaji wa ardhi, maliasili na rasilimali
za nchi kutumiwa kwa manufaa ya wananchi wote, elimu, afya, mazingira ya kukuza
uchumi unaoleta neema kwa wananchi wote, wajibu, uwezo na uhuru wa serikali za
mitaa hayajaingizwa ndani ya katiba kikamilifu kwani rasimu ya katiba
imeshughulikia mambo ya muungano.
Mambo
ya Muungano ni saba: Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uraia na Uhamiaji, Sarafu
na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa na Ushuru wa bidhaa na
mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.
Mwongozo
wa Tume kuhusu utoaji wa maoni ulijikita katika maeneo
yafuatayo; Misingi na Maadili ya Kitaifa, Madaraka ya Wananchi, Muundo
wa Nchi na Taifa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Haki za Binadamu na
Wajibu wa Wananchi, Ardhi, Maliasili na Mazingira, Mihimili ya Nchi (Ardhi, Watu
na Utawala), Mihimili ya Utawala (Serikali, Bunge na Mahakama), Serikali za
Mitaa, Muundo na Mamlaka yake, Vyombo vya Ulinzi na Usalama. Mambo mengi muhimu kwa mwananchi wa kawaida ikiwa ni
pamoja na serikali za mitaa, umilikaji wa ardhi, haki za huduma za afya na
elimu, na matumizi ya maliasili hayajaingizwa katika katiba hii na yanatarajiwa
kuingizwa kwenye katiba ya Tanzania Bara. Rasimu ya katiba kwa wananchi wa
Tanzania Bara haijakamilika mpaka Rasimu ya katiba ya Tanzania Bara itakapokuwa
tayari. Hotuba ya uzinduzi wa katiba ya Jaji Warioba haikulifafanua suala hili.
Hakuna mantiki ya kupigia kura ya maoni katiba ya jamhuri ya muungano bila kuwa
na katiba ya Tanzania Bara kwa upande wa bara na marekebisho ya katiba ya Zanzibar
isikinzane na katiba ya jamhuri ya muungano kwa upande wa zanzibar. Katiba ya
Tanzania Bara na katiba ya Zanzibar iwe ni sehemu ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano.
Kuwepo
kwa rasimu ya katiba ya Tanzania Bara kutasaidi kuondoa kuweka asasi mbili au
tatu zinazofanya kazi moja. Kwa mfano Tume ya Uchaguzi, Jeshi la Polisi,
Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Taasisi ya kuzuia na kupambana na
rushwa ya serikali ya Muungano ikafanya kazi pia kwa serikali ya Tanzania Bara
ikiwa wananchi wa Tanzania Bara hawana tatizo na utaratibu huo.
MAPENDEKEZO YA JUMLA;
1.
Pendekezo
langu la msingi ni kwamba, kura ya maoni isubiri kukamilishwa kwa rasimu ya
katiba ya Tanzania Bara na zote zikajadiliwa na wananchi kwa pamoja. Sina
pingamizi kuwa Wajumbe wa Tume wa Tanzania Bara waandae rasimu ya Katiba ya
Tanzania Bara, na wajumbe wa Zanzibar waandae mapendekezo ya marekebisho ya
katiba ya Zanzibari ili isikinzane na katiba ya Jamhuri ya Muungano. Muda wa
kuyatekeleza haya na kubadilisha sheria zifuate matakwa ya katiba mpya kabla ya
uchaguzi mkuu wa 2015 haupo. Serikali imeeleza kuwa haina nia na Rais Kikwete
hataki kabisa kujiongezea muda kwa kisingizio cha kukamilisha utaratibu wa
katiba mpya. Wananchi pia wamechoka wanataka mabadiliko.
2.
Katika
masuala ya haki za binadamu ningependa Katiba itamke wazi kuwa mwanamke
mjamzito ana haki ya kupata lishe bora na huduma za afya wakati wa ujauzito na
kujifungua. Vile vile watoto bila kujali uwezo wa wazazi wao wana haki ya lishe
bora, huduma za msingi za afya na elimu inayomuandaa mtoto kukabiliana na changamoto
za maisha.
3.
Pendekezo la
Rasimu ya Katiba ya kuwepo Tume Huru ya Uchaguzi ni la msingi. Pendekezo hili
lianze kufanyiwa kazi mara moja ili kufanya mabadiliko ya sheria ya uchaguzi na
Tume ya uchaguzi ili uchaguzi wa 2015 uendeshwe na Tume iliyo Huru kweli.
Mchakato wa mabadiliko ya katiba utaendelea baada ya uchaguzi mpaka ukamilike
na sheria husika kufanyiwa mabadiliko.
4.
Siyo lazima
Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wawe watu waliyewahi
kushika wadhifa wa Jaji wa Makakama ya Juu, Mahakama ya Rufani au Mahakama Kuu
na ameshika wadhifa huo kwa kipindi kisichopungua miaka mitano kama Rasimu ya
Katiba inavyoelekeza katika kifungu 181
(4). Masuala ya kusimamia uchaguzi ni ya utawala na uendeshaji
kuliko ya kutafsiri sheria. Majaji siyo wasimamizi na mameneja wazuri wa
utawala na logistics. Nchini Ghana mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ambaye
kafanya vizuri siyo Jaji bali ni Profesa wa sayansi ya siasa – Jaji Lewis
Makame kwa miaka zaidi ya 15 na hakufanikiwa kujenga Tume ya Uchaguzi yenye uwezo
na kuaminika. Ni vyema wigo wanaoweza kuomba kuwa wenyeviti wa Tume ukapanuliwa
na kuingiza wenye uzoefu wa utawala na logistics. Tume ina mwanasheria wake
ambaye ataelekeza na kushauri masuala yahusiyo sheria.
5.
Kasoro kubwa
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ni kwamba haina nyenzo za kutimiza malengo
muhimu ya katiba yenyewe. Ibara ya 6(b) imeeleza kuwa “lengo kuu la Serikali litakuwa ni maendeleo na ustawi wa wananchi.”
Mambo ya uchumi yote isipokuwa Benki Kuu na sarafu hayamo katika orodha ya
mambo ya Muungano. Hata suala la uratibu wa sera za uchumi halimo. Ibara ya 7(2)
inaeleza “mamlaka ya nchi na vyombo vyake
vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote kwa lengo la kuhakikisha
kwamba: (c)Serikali itahakikisha kuwa shughuli zinazofanywa zinatekelezwa kwa
njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na
unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya
mtu mwingine; (d)ardhi ikiwa rasilimali kuu na msingi wa Taifa, inalindwa, inatunzwa
na kutumiwa na wananchi wa Tanzania kwa manufaa, maslahi na ustawi wa kizazi
cha sasa na vizazi vijavyo; (e)maendeleo ya uchumi wa Taifa yanapangwa na
kukuzwa kwa ulinganifu na kwa pamoja na kwa namna ambayo inawanufaisha wananchi
wote; (f)kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi, na kazi maana
yake ni shughuli yoyote ya halali inayompatia mtu kipato chake; (j)utajiri wa
rasilimali na maliasili za Taifa unaelekezwa katika kuleta maendeleo, kuondoa
umaskini, ujinga na maradhi”. Serikali
ya Muungano haina nyenzo ya kusimamia mambo hayo.
6.
Ibara ya 11
inazungumzia utekelezaji wa malengo ya taifa. Kifungu (2) kinaeleza “Serikali itatoa taarifa Bungeni si chini ya
mara moja katika kila mwaka, kuhusu hatua zilizochukuliwa na mamlaka ya nchi
ili kuhakikisha utekelezaji wa malengo ya Taifa yaliyoainishwa katika Katiba
hii. (c) kiuchumi, Serikali inachukua hatua zinazofaa ili: (i) kuwaletea
wananchi maisha bora kwa kuondoa umaskini; (ii) kuhakikisha kwamba shughuli za
Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kuwa utajiri wa Taifa
unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla
na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine; (iii) kuweka mazingira bora kwa ajili
ya kuanzisha na kuendeleza vyombo vya uwakilishi wa wakulima, wafugaji na
wavuvi; (iv) kuweka mazingira bora ya kufanya biashara na kukuza fursa za
uwekezaji; (v) kuweka mazingira bora kwa ajili ya kukuza kilimo, ufugaji na
uvuvi kwa kuhakikisha kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi wanakuwa na ardhi na
nyenzo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao; (vi) kuweka mazingira bora ya
uzalishaji wa mazao kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, utafutaji na uendelezaji
wa masoko ya mazao yao; (vii) kuweka utaratibu mzuri wa upangaji na usimamiaji
wa mizania ya bei za mazao na pembejeo; (viii) kuimarisha na kuendeleza
uwekezaji wa ndani, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, maeneo ya ufugaji na
vifaa vya uvuvi; (ix) kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa fursa na nafasi za
wazi kwa watu wote na kuanzisha shughuli za kiuchumi na kukuza mazingira yaliyo
bora kwa ajili ya kuhamasisha sekta binafsi katika uchumi; (x) kuhakikisha kuwa
kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anapata fursa ya kufanya kazi, kwa maana
ya kufanya shughuli yoyote halali inayompatia kipato; (xi) kuweka utaratibu unaofaa
kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa haki ya mtu kujipatia elimu na kuwa
huru kupata fursa sawa ya kutafuta elimu katika fani anayoipenda hadi kufikia
upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake. Mambo yote haya siyo ya
muungano”. Serikali ya Muungano
itawezaje kutoa taarifa Bungeni kwa mambo ambayo haiyasimamii.
7.
Ukizingatia
mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa na Rasimu, Serikali ya Muungano haina vyanzo
vya mapato ya kodi. Ibara ya 215
imeeleza Vyanzo vya mapato ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano vitakuwa:
“(a) ushuru wa bidhaa; (b) maduhuli
yatokanayo na taasisi za Muungano; (c) mchango kutoka kwa Washirika wa
Muungano; na (d) mikopo kutoka ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano”. Katiba haizungumzii taasisi yeyote ya
kukusanya kodi. Jambo la saba la muungano ni Ushuru wa bidhaa na mapato
yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano. Mambo sita ya Muungano hayalipi
ushuru wa bidhaa. Biashara siyo jambo la
Muungano kwa hiyo ushuru wa forodha, kodi za ongezeko la thamani (VAT), excise duty,
kodi ya mauzo haziwezi kuwa suala la Muungano. Mwaka wa fedha wa 2010/11
Mapato ya serikali Asilimia 34.3 ushuru wa forodha na VAT katika bidhaa
zinazoagizwa toka nje, Asilimia 18.6 kodi (VAT na Excise duty) za bidhaa
zinazozalishwa ndani ya nchi. Asilimia 29 kodi ya mapato. Kodi na tozo nyingine
asilimia 10.5, Mapato ya halmashauri asilimia 2.8. Kodi ni chanzo cha mapato ya
serikali lakini pia ni sera ya uchumi. Viwango gani vya kodi havina athari
kubwa kwa wananchi maskini na kupunguza motisha ya uzalishaji na uwekezaji?
Serikali za washirika wa Muungano hawatakubali Serikali ya Muungano kutoza kodi
katika maeneo ambayo siyo ya muungano. Katiba
haina muongozo wowote wa michango toka washirika wa Muungano. Rasimu hii ilivyo
ikipitishwa kutakuwa na mgogoro mkubwa wa fedha za kuendeshea serikali ya
Muungano na hatma yake itakuwa Muungano kuvunjika.
8.
Katika mambo
ya uchumi Tume haikufanya uchambuzi wa kina wa kuwa na katiba inayojenga
mazingira mazuri ya kukuza uchumi unaoleta maendeleo kwa wote. Katiba haiibani
serikali iwe na utaratibu mzuri wa bajeti. Katika mambo ya usimamizi wa
matumizi ya serikali na kazi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali rasimu hii ime –“copy” na ku-“paste” katiba
ya sasa bila kutathmini kama mfumo wa hivi sasa unafanya kazi. Eneo hili
linahitaji kufanyiwa uchambuzi zaidi.
9.
Ibara za 213
na 214 zinawapa uwezo Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mshirika
wa Muungano “zitakuwa na mamlaka ya
kukopa fedha ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kugharamia
shughuli zilizo chini ya mamlaka yake.” Katika utaratibu huu nchi inaweza
kughubikwa na madeni ikiwa serikali tatu zitashindana kukopa ndani na nje ya
nchi. Lazima pawe na mwongozo wa
kudhibiti mikopo na kuongezeka kwa deni la taifa. Nchi inaweza kuingizwa
katika mgogoro wa madeni. Uhuru wa
serikali zote tatu kukopa ndani na nje ya nchi inaweza kusababisha kukua kwa
madeni kupita kiasi. Serikali za washirika zina vyanzo vya mapato serikali
ya muungano haina. Kwa Rasimu ya Katiba hii serikali za washirika ndizo
zinazokopesheka na siyo serikali ya muungano.
10.
Rasimu ya
Katiba bila kusema hivyo inapendekeza kuwepo na Benki Kuu tatu. Ibara ya 217
inaeleza “Kutakuwa na Benki Kuu ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayojulikana kuwa “Benki Kuu” ambayo itakuwa
na majukumu yafuatayo: (a) kutoa sarafu, kudhibiti na kusimamia mzunguko wa
sarafu; (b) kuandaa na kusimamia Sera na Mipango inayohusiana na sarafu; (c)
kudhibiti na kusimamia masuala ya fedha za kigeni; na (d) kusimamia Benki za
Washirika wa Muungano.” Ibara ya 218 inaeleza “Serikali za Washirika zitakuwa na Benki zitakazokuwa najukumu la
kutunza akaunti ya fedha za Serikali husika, kusimamia Sera za Kifedha na benki
za biashara katika mamlaka zao.” Kazi ya Benki Kuu ni kusimamia Benki za
Biashara, sera za fedha na hasa riba, na mfumo wa malipo. Kazi hizi zitafanywa
na Benki za Washirika wa Muungano. Moja
ya chanzo cha mgogoro wa Euro ni kutokuwepo usimamizi wa pamoja wa Benki za
biashara. Hivi sasa Ukanda wa Euro unajaribu kuandaa utaratibu wa pamoja wa
kuifanya Benki Kuu ya Ulaya (ECB) kusimamia Benki za Biashara. Kama tuna sarafu moja tuwe na Benki Kuu
moja. Benki Kuu isiposimamia benki za biashara haitaweza kudhibiti na kusimamia
ujazi wa fedha (money supply)
11.
Ibara ya 105
inaeleza “(2) Wajumbe wa Bunge watakuwa
wa aina zifuatazo: (a) Wabunge waliochaguliwa kuwakilisha majimbo ya uchaguzi;
(3) Kwa madhumuni ya Ibara ya ndogo (2)(a), kila mkoa kwa upande wa Tanzania
Bara na wilaya kwa upande wa Zanzibar, itakuwa ni jimbo la uchaguzi”.
Nini vigezo vya kufanya
mikoa na wilaya kuwa majimbo ya uchaguzi? Utaratibu wa kuanzisha mikoa na
wilaya ni wa serikali washirika au wa Serikali ya Muungano? Hata hivyo ibara ya
180 (a) inaeleza “mamlaka zinazosimamia
uchaguzi kutangaza majimbo kwa madhumuni ya uchaguzi wa wabunge.” Majimbo ya uchaguzi yataundwa na Tume au
tayari yameishatajwa na katiba?
12.
Mamlaka ya
Bunge katika kuisimamia serikali katika masuala ya bajeti ni madogo. Ibara ya
107 (2) inaeleza, “katika kutekeleza
majukumu yake, Bunge litakuwa na madaraka yafuatayo: (c) kujadili mgawanyo na
kuidhinisha matumizi ya fedha kwa Wizara, taasisi na mashirika ya Serikali; (d)
kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa
bajeti; (e) kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda
mfupi unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika Jamhuri ya Muungano; (f)
kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango wowote wa muda mrefu au muda
mfupi”. Hata hivyo Mambo ya Muungano
hayahusishi Mpango wa Maendeleo wa taifa.
13.
Ibara ya 177
inaeleza “Bila ya kuathiri masharti ya
Katiba hii, utumishi wa umma na uongozi katika Jamhuri ya Muungano utazingatia
misingi kwamba utoaji wa ajira na uteuzi wa viongozi utakuwa kwa uwiano baina
ya Washirika wa Muungano, kwa kuzingatia weledi na taaluma katika eneo au
nyanja husika.” Nini maana ya
uwiano? Je maana yake nusu ya wafanyakazi watoke Zanzibar na nusu watoke
Tanzania Bara?
14.
Taasisi ya
kuzuia na kupambana na rushwa ni muhimu iwemo ndani ya Katiba. Rasimu haina
asasi hii muhimu ya usimamizi na uwajibikaji. Tunarudia pendekezo letu kuwa
Katiba ieleze kuwepo kwa Tume ya Kupambana na Kuzuia Rushwa na kueleza kazi
zake. Tume hii iwe na uhuru wa kupeleka kesi mahakamani bila idhini ya
Mkurungezi wa Mashtaka ya Umma (DPP).
15.
Katiba
imejaa imani kuwa vyeti vya shule na vyuo ndiyo elimu na hekima na kwa kutumia
sifa za vyeti vya elimu inawanyima haki wananchi wengi kushiriki na kuwania
uongozi katika ngazi mbalimbali. Ibara ya 75(f) inaeleza sifa moja ya Rais kuwa
“anayo angalau shahada ya kwanza ya chuo
kikuu kinachotambuliwa kwa mujibu wa sheria za nchi.” Cheti cha shahada
siyo kipimo kizuri cha elimu, hekima na uwezo wa kuongoza. Bill Gates
hakumaliza masomo yake ya shahada ya kwanza Chuo Kikuu cha Harvard. Aliona
anapoteza muda akaanzisha kampuni ya Microsoft. Kama Bill Gates angekuwa
Mtanzania, Rasimu ya Katiba ingemzuia kugombea Urais kwa kuwa hana cheti cha
shahada. Steve Jobs pia hakumaliza na kupata shahada badala yake alifanya
masomo aliyoyaona muhimu na kuanzisha kampuni ya Apple. Hapa Tanzania sidhani
kama Said Salim Bakhresa ana shahada yeyote. Taarifa iliyoko Wikipedia na
gazeti la Forbes inaeleza aliacha shule akiwa na miaka 14 na akaanza biashara
ya kuuza potato mix. Kama taarifa hii ni kweli basi huenda hata darasa la 8
hakumaliza. Lakini uwezo, uzoefu na elimu itokanayo na uzoefu wa kazi ni kubwa
kuliko hata mtu mwenye PhD ya biashara. Mzee Bakhresa hana sifa ya kugombea
Urais kwa kuwa hana shahada ya kwanza. Sina uhakika kama Freeman Mbowe ana
shahada. Ikiwa hana siyo haki kumzuia kugombea Urais kwa sababu hiyo. Mwache
agombee na wengine wajenge hoja hana maadili na uwezo wa kuongoza nchi. John
Major alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza mwaka 1991 – 97 hana shahada ya Chuo
Kikuu. Kuna watu wengi wenye shahada nyingi lakini hawana hekima wala busara.
Vyeti vingi vys siku hizi ni vya kughushi na inawezakana kabisa usiweze
kugundua kuwa vimeghushiwa. Sifa ibakie kusoma na kuandika kiswahili. Wache
wapiga kura waamue kuwa elimu ya mgombea haitoshi kumfanya kuwa Rais. Sifa ya
elimu ya mgombea ubunge ni kidato cha nne. Rasimu itamzuia Mzee Bakhresa hata kugombea
ubunge kwa sababu hana cheti cha kidato cha nne. Kuna Watanzania wengi
waliomaliza darasa la nane au la saba la zamani wenye elimu bora kuliko
aliyemaliza kidato cha nne hivi karibuni. Kuna watu wengi wamemaliza darasa la
7 wana uzoefu mzuri na wana uwezo wa kuwawakilisha wananchi katika Bunge.
Vigezo vya vyeti vya elimu visitumiwe kuwanyima wananch haki zao za kisiasa.
Kigezo cha shahada pia kimeingizwa katika uteuzi wa Mawaziri. Watu wenye uzoefu
na uwezo wa uongozi lakini hawana vyeti vya shahada hawawezi kuteuliwa kuwa
mawaziri. Nastaajabu hii obsession na vyeti imetoka wapi?
16.
Ibara ya 31
inazungumzia Dini. “(1) Kila mtu anao uhuru wa mawazo, imani na
uchaguzi katika mambo ya imani ya dini na anao uhuru pia wa kubadilisha dini,
imani yake au kutokuwa na imani na dini. Kifungu cha (5) Ni marufuku kwa mtu,
kikundi au taasisi ya dini kutumia uhuru wa kutangaza dini kwa kukashifu imani
na dini nyingine, kujenga chuki au kuchochea vurugu na ghasia kwa madai ya
kutetea imani au dini”. Tatizo ya ibara hii ni tafsiri ya kukashifu. Imani
za dini zina tofauti. Imani ya msingi ya dhehebu moja inaweza kuwa kufuru kwa
dhehebu lingine na ikatafsiriwa kuwa ni kukashifu. Kuna masuala ambayo jamii
inapaswa kujenga maelewano ya kuvumiliana na kuheshimiana na kukubali tofauti
za imani bila kugombana. Kuliweka katika katiba inaweza kujenga chuki na
ikatafsiriwa kuwa inalenga kundi fulani. Ibara
na 5 imelenga kikundi au taasisi ya dini. Je vikundi ambavyo siyo vya dini
vinaruhusiwa kukashifu imani na dini?
17.
Serikali ya
Muungano itakuwa na Jeshi la ulinzi, Polisi na Usalama wa Taifa. Serikali za
washirika zinaruhusiwa kuwa na polisi na usalama wa taifa. Inawezekana serikali
ya Muungano ikaongozwa na Chama A, Serikali ya Zanzibar ikaongozwa na chama B
na serikali ya Tanzania Bara ikaongozwa na chama C. Serikali zote zina polisi
na usalama wa taifa wake, haitakuwa kasheshe ndani ya nchi? Sina uhakika katiba
imeweka bayana utaratibu wa kuzuia migongano kati ya vyombo vya Muungano na
vyombo vya Washirika.
Haya
ni mapendekezo ya awali tu, mapendekezo mengine yataendelea kutolewa kwa kadri
ambavyo tutazidi kuichambua rasimu hii ya katiba. Natoa wito kwa Watanzania
wote kuhakikisha kuwa wanaitafuta rasimu hii bila kuchoka, kuisoma na kuielewa
na kuendelea kutoa mapendekezo yao kwa tume ya mabadiliko ya katiba iwe ndiyo
lengo kuu.
Kwa
sababu tume imetangaza kuwa itachapisha rasimu katika magazeti ya serikali kwa
maana ya HABARI LEO na ZANZIBAR LEO, tunaona kama huku ni kuififisha rasimu
isiwafikie watanzania wengi zaidi.
Kuna
haja ya dhati, tume ikaitangaza rasimu katika magazeti mbalimbali ya kila wiki
na ya kila siku ili kuhakikisha kuwa rasimu imefikiwa na imesomwa na watanzania
wengi. Na nakala zitakazobakia “returns” baada ya mauzo ya magazeti husika tume
izinunue nakala hizo na izisambaze kwa utaratibu maalum mikoani na vijijini.
Ni
ushauri wetu kwa Tume pia kwamba baada ya kazi kubwa waliyoifanya, wasikubali
kuyumbishwa na wahafidhina wasiopenda mabadiliko wanaotokana na CCM. Tume iwe
na msimamo na iangalie wananchi wanataka nini na itetee masuala ya msingi na ya
maslahi ya wananchi ambayo inaona ni muhimu yakatetewa kwa maslahi ya taifa na
hasa kwa kuzingatia matakwa ya wananchi.
Na
mwisho, Tume ihakikishe kuwa masuala haya tunayoyashauri kwa awamu yanapewa
uzito na tafakuri pana ili kuipata katiba itakayokuza uchumi imara, kuongeza
ajira kwa vijana na kuinua maisha ya wananchi wa kipato cha chini.
“Mungu
Ibariki Tanzania”
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba.
Mwenyekiti,
09 Juni 2013, Dar Es
Salaam.

COMMENTS