WAZIRI MKUU ATOA SAA 30, ATAKA KUPATA MAJIBU KUHUSU KIWANDA CHA NYAMA MBEYA * Asema malumbano ya viongozi hayawasaidii wananchi W...
WAZIRI MKUU ATOA SAA 30, ATAKA KUPATA MAJIBU
KUHUSU KIWANDA CHA NYAMA MBEYA
*Asema malumbano ya viongozi hayawasaidii
wananchi
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ametoa saa 30 na kutaka
kupatiwa majibu ni kwa nini maelekezo aliyotoa kuhusu kiwanda cha kusindika
nyama cha Mbeya hayajafanyiwa kazi.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Agosti Mosi,
2014) wakati akizindua Kongamano la siku tatu la Uwekezaji la Mikoa ya Iringa,
Njombe na Mbeya la mwaka 2014 ambalo limeanza leo kwenye ukumbi wa Benjamini
Mkapa jijini Mbeya.
“Mbeya inaweza kuwa na fursa kubwa ya viwanda vya
usindikaji nyama, unga wa mahindi ili kuongeza thamani ya mazao mnayozalisha
katika mkoa wenu. Nilipokuwa hapa ziara yangu ya mwisho 2012, niliagiza kiwanda
hiki kitafutiwe mwekezaji ili kianze uzalishaji. Jana nimeuliza kiwanda cha
nyama kimefikia wapi, naambiwa watu bado wanaongea. Wanaongea nini?,” alihoji.
“Mtu akija kusikia habari ya kiwanda hiki atatuona
ni wajinga tena ni wajinga wa kujitakia, kisa watu bado wanazungumza… hiki
kiwanda cha nyama ni cha Mbeya na manuafaa yake ni kwa ajili ya wana Mbeya.
Hivi wahusika ni kwani hamuioni hiyo fursa?” alisema.
“Dk. Mary Nagu watafute watu wa CHC waje hapa
kujieleza ni kwa nini suala hili limechukua muda mrefu. Kabla sijaondoka hapa
Mbeya kesho nataka nipate majibu kuhusu jambo hili,” aliagiza.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri Mkuu
alisisitiza suala la watendaji wa mikoa na wilaya kuchukulia kwa umakini suala
la uwekezaji kwani wasipofanya hivyo wao ndiyo watageuka kikwazo na kukwamisha
maendeleo ya wananchi wanaowaongoza.
“Ndugu zangu wa Serikali za mitaa msiwe vikwazo,
kuwezi wawezeshaji. Ninyi si watawala bali ni waleta maendeleo kwa jamii. Natoa
wito mshirikiane na wafanyabiashara kuharakisha maendeleo ya wananchi
mliokabidhiwa kuwaongoza. Acheni kudai hongo, kwani badala ya kuwasadia jamii,
mtajikuta ninyi ndo mnakuwa vikwazo vya maendeleo,” alionya.
Alisema Serikali za Mitaa zinapaswa kuwa
wawezeshaji na siyo wakwamishaji wa masuala ya maendeleo na ili kufanikisha
hilo aliwataka wakuu wa mikoa waanzishe one-stop centre katika ngazi
ya mkoa na Halmashauri ili wawekezaji wanapofika katika mikoa yao wasizungushwe
na kukatishwa tamaa kwa sababu ya mlolongo wa taasisi zilizopo.
“Uzoefu unaonyesha kuwa baada ya kufanya
makongamano kama haya, wawekezaji wengi wanajitokeza lakini katika ngazi ya
Mkoa na Halmashauri wanakosa mahali ambapo wanaweza kushughulikiwa na kupata
huduma bora kwa pamoja “One Stop Centre”. Hali hiyo huwafanya wakate tamaa.”
“Ninashauri kila Mkoa na kila Halmashauri iweke
mfumo mzuri wa kuwapokea wawekezaji hususan kuwa na Mratibu (Focal Point)
wa masuala ya uwekezaji ambaye ndiye atakuwa “One Stop Centre” wa
kushughulikia wawekezaji wanaojitokeza na kuwahudumia kwa ufanisi bila urasimu.
Ni imani yangu kuwa tukifanya hivyo, tutawezesha Kanda hii kuwa kitovu kikubwa
cha uwekezaji katika nchi yetu,” aliongeza.
Alisema kila mmoja hana budi kuendelea amani na
utulivu wa nchi ili uwekezaji uweze kufanikiwa na kushamiri. “Hakuna uwekezaji
endelevu na wenye tija katikati ya fujo na migogoro, na uwekezaji utashamiri
pale tu penye amani na utulivu,” alisisitiza.
Mapema, Waziri wa Nchi (OWM-Uwezeshaji na Uwekezaji),
Dk. Mary Nagu alisema ili uwekezaji uweze kuwanufaisha wananchi, ni lazima
rasilmali za nchi zigeuzwe kuwa bidhaa. “Ukiangalia chuma cha Liganga kipo pale
miaka mingi, bila kukigeuza kuwa bidhaa, bado hakiwezi kuwanufaisha wananchi
wetu,” alisema. Alisema bila uwekezaji hakuna uchumi, na bila uchumi hakuna
maendeleo na bila maendeleo hakuna maisha bora kwa kila Mtanzania.
Katika hatua nyingine, Wakuu wa mikoa ya Mbeya, Iringa
na Njombe walipewa nafasi ya kuzungumza na washiriki wa kongamano hilo ikiwa ni
pamoja na kuelezea fursa mahsusi zilizomo kwenye mikoa yao.
Mada zitakazowasilisha katika kongamano hilo
ambalo kaulimbiu yake ni “Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii katika Nyanda za
Juu Kusini” zinahusu fursa za uwekezaji katika sekta za uchumi na
miundombinu katika kanda hiyo, fursa za uwekezaji katika sekta za huduma za
jamii katika kanda hiyo, fursa za uwekezaji katika kilimo cha mazao ya bustani
(matunda, mboga, maua na viungo) na mchango wa taasisi za fedha katika
uwekezaji.
Nyingine ni mchango wa sekta binafsi katika
uwekezaji, na nafasi ya MKURABITA katika kukuza mitaji ya uwekezaji.
(mwisho)
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
IJUMAA,
AGOSTI MOSI, 2014
COMMENTS