Mtathmini kiongozi wa mradi wa PREPARE Mrema Kilonzo akizungumza na waandishi wa habari.Mwingine ni mtafiti kiongozi Lusajo Kajula ...
Mtathmini kiongozi wa mradi wa PREPARE Mrema Kilonzo akizungumza na waandishi wa habari.Mwingine ni mtafiti kiongozi Lusajo Kajula |
SAMPULI tathmini ya
matokeo ya mradi wa PREPARE uliokuwa na lengo la kuangalia uwezekano wa vijana
kupunguza ngono, imebainisha haja ya elimu ya afya ya uzazi kukabili hali ya
sasa ya tabia hatarishi zinazowakabili vijana wadogo.
Matokeo ya awali ya mradi yalionesha kuwa
asilimia 10 ya vijana wenye umri wa miaka 12 mpaka 14 ambao ni darasa la tano
na sita waliofanyiwa utafiti walikuwa wameshawahi kufanya ngono na asilimia
kubwa ikiwa ni kwa kutumia njia ya haja kubwa.
Kauli hiyo imetolewa na
mmoja wa watafiti wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi shirikishi cha
Muhimbili,Kitengo cha magonjwa na afya ya akili, Lusajo Kajula.
“Vijana wengi walionekana wakifanya ngono ya uke
na ya mdomo ikifuatiwa na ngono ya njia ya haja kubwa Kwa wale ambao
wameshawahi kufanya ngono, asilimia 6.3 wamefanya ngono ya njia ya haja kubwa
wakati asilimia 93.7 hawajawahi.”
Aidha alisema utumiaji wa kondomu ulionekana
kuwa mdogo kwa vijana wadogo ambao wameanza kufanya ngono.
“Asilimia 68 ya wale walioanza kufanya ngono
hawajawai kutumia kondomu kabisa wakati asilimia 32 wamewahi kutumia kondomu.”
Alisema utafiti huo ni
sehemu ya utafiti wa miaka minne ulioshirikisha Vyuo Vikuu vya Makerere cha
Uganda, Cape Town na Limpopo vya Afrika Kusini, Bergen na Oslo vya Norway,
Maastricht cha Uholanzi na Sussex cha
nchini Uingereza.
Alisema utafiti
umeonesha haja ya kutolewa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana wadogo ambao bado
hawajaanza ngono ili kuchelewesha kuanza ngono kwa mfumo wa kisaikolojia ili
waweze kujitambua na kuacha kufuata nadharia za kisayansi pekee ambazo ndizo
zinazotumika katika shule mbalimbali kuwaeleza mabadiliko ya miili yao.
Katika utekelezaji wa
utafiti huo idadi ya wanafunzi 5,099 walichaguliwa mwanzoni mwa mradi kufanyiwa
utafiti huo ambapo wanafunzi 4783 (asilimia 93.9) walifuatiliwa kwa miezi 6 na
wengine 4370 (asilimia 85.8) walifuatiliwa kwa miezi 12.
Utafiti ulionesha elimu
inayojishughulisha na masuala ya ujinsia na afya ya uzazi kwa vijana wadogo
itumie mtazamo mpana utakaoleta mabadiliko ya msingi kwenye misingi ya
virekebisho vya mabadiliko ya tabia.
Mradi huo wa PREPARE
ulitekelezwa kwenye shule 38 kutoka manispaa ya Kinondoni zilizochaguliwa kwa
kutumia taratibu sampuli mtawanyiko zilizopangwa katika makundi mawili ya shule
za mwingilio yaani ilikotolewa elimu hiyo zilizokuwa 19 na za kulinganisha zilizokuwa 19.
Ili kuweza kupata
matokeo yaliyokusudiwa mradi ulitoa mafunzo kwa walimu watano wakufunzi wa
wakufunzi; ulitoa mafunzo kwa walimu watekelezaji 76, na waelimishaji
rika wanafunzi 132 na kuelekeza watoa huduma 8 wa afya katika kliniki za huduma
rafiki kwa vijana ili kutekeleza muingiliano.
Tathmini iliyotoa majibu
ya jinsi utendaji unavyoendelea na ya matokeo ilihusisha shule zote na
wanafunzi zaidi ya 6,000 waliowekwa kwenye muingiliano, huku uchambuzi wa
tathmini ukihusisha wanafunzi wenye umri wa miaka 12-14, wenye kujua kusoma na
kuandika.
Matokeo yaliyotathminiwa ni Mabadiliko katika
masuala ya ngono (kuanza ngono) na Kutumia kondomu wakati wa kujamiiana
kwa wale waliokwisha anza ngono.
Kwa wastani mradi uliona
kwamba mwingilio wa PREPARE ulipunguza uwezekano wa vijana wadogo (wavulana
na wasichana) kuanza ngono na kuongeza uwezekanao wa kutumia kondomu kwa
wale walioanza.
Hata hivyo, katika
utekelezaji wa mradi mabadiliko katika uchukuaji wa hatua yalionekana zaidi
miongoni mwa wasichana waliopata mwingilio ukilinganisha na wale ambao
hawakupata mwingilio.
Uchukuaji wa hatua
ulisababisha tabia ya kutumia kondomu miongoni mwa wanafunzi wa kiume lakini
siyo miongoni mwa wanafunzi wa kike.
“Kimsingi tunataka
kuwaambia wanahabari kuwa miongoni mwa
mafanikio makubwa ya mradi wa PREPARE
ni kuchelewesha kuanza ngono miongoni mwa wanafunzi wa kiume na wa
kike wenye umri wa miaka 12-14 katika mkoa wa Dar es Salaam, Tanzania;
“Kuongeza uchukuaji wa hatua ulio chanya katika kutumia kondomu
kwa jinsia zote na taarifa za ongezeko la utumiaji wa kondomu miongoni mwa
vijana wa kiume. “
Mradi huu uliofadhiliwa na Umoja wa Nchi za Ulaya, Programu ya utafiti wa
afya umelenga kuangalia mwingilio ulio katika
misingi ya utamaduni na jinsia, endelevu, kijamii ili kukuza ujinsia na afya ya
uzazi miongoni mwa vijana wenye umri kati ya miaka 12-14 kwa kutumia shule kama
njia ya kufundishia.
COMMENTS