Mhasdhamu Isuja akiwa na rais Mstaafu wakati wa sherehe za miaka 40 ya uaskofu

ASKOFU wa kwanza Mzalendo  na wa tatu kwa jimbo katoliki Dodoma, Mhashamu Mathias Isuja Joseph  ( 86) amefariki dunia akitibiwa katika hospitali ya misheni ya Mtakatifu Gaspar, Singida.
 Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Uongozi wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma,Mhashamu Isuja ambaye alistaafu kazi hiyo ya uaskofu mwaka 2005 atazikwa kanisa kuu la Jimbo katoliki Dodoma la Paulo wa Msalaba Jumatano ijayo.
 Mhashamu Isuja aliteuliwa kuwa askofu wa Dodoma Juni 26 1972 akichukua nafasi ya  Askofu Anthony Jeremiah Pesce ambaye alifariki Desemba 20 1971. Kabla ya askofu Pesce ambaye aliteuliwa Mei 10,1951 alikuwapo  askofu Stanislas dell’Addolorata ambaye aliteuliwa Juni16 1937 na kufariki 1941. 
Jimbo Katoliki Dodoma lilianzishwa mwaka Januari 28,1935.
 Jimbo hilo kwa sasa linaongozwa na Askofu Mkuu Beatus kinyaiya aliyeteuliwa Novemba  6,2014 kuchukua nafasi ya Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga ambaye alikwenda kuwa Askofu wa Mpanda. Askofu Nyasionga alichukua nafasi ya Askofu Jude Thadeus Ruwa’ichi ambaye 2010 alichaguliwa kuwa askofu wa Mwanza.
 Askofu Isuja, ambaye wengi walizoea kumwita “Babu”, amefariki dunia akiwa ametumikia utumishi wa Mungu kwa miaka 55 ya huduma ya Upadre na miaka 43 ya Uaskofu huku akibahatika kuona Jimbo Katoliki Dodoma likizaa Jimbo Katoliki la Kondoa na hatimaye, kupandishwa hadhi kuwa Jimbo kuu la Dodoma.
 Katika uhai wake Askofu Isuja tangu akiwa Padre hadi Askofu alikuwa chachu kubwa katika masuala ya elimu Jimboni Dodoma,kupambana na umasikini lakini pia alisistiza wakazi wa mikoa ya kanda ya kati kukabili umaskini kwa kujikita katika kilimo cha zabibu.
 Askofu Isuja alikuwa pia kipenzi cha watoto wa Shirika la Utoto Mtakatifu Kipapa ambapo mara nyingi alikuwa akiwasisitiza kupeleka neno kwa watoto wenzao huku akiimba sisi ni Christopher.
Askofu Isuja alizaliwa Agosti 14,1929 katika kijiji cha Haubi Kondoa,alipata daraja takatifu la Upadre Desemba 24,1960 Parokiani Kondoa na Septemba 17,1972 alipata daraja takatifu la Uaskofu Jimboni Dodoma.
Aidha mwaka 2005 Askofu Isuja alikabidhi utawala wa kichungaji kwa Ruwaichi kwa mujibu wa sheria za Kanisa pamoja na kwamba aling’atuka.
Askofu Isuja ni mtoto wa Mzee Joseph Chundu na mama Odilia Mbula alizaliwa Agosti 14, 1929 katika kijiji  cha Haubi Wilayani Kondoa.
Alisoma shule ya msingi Kondoa na Bihawana kuanzia mwaka 1942 hadi 1948, mnamo mwaka 1949 hadi 1953 alichaguliwa kujiunga na elimu ya Sekondari katika Seminari  ya Bihawana.
Mwaka 1953 hadi 1955 alijiunga na seminari ya Tosamaganga kwa elimu ya falsafa na mwaka 1956 hadi mwaka 1960 alijiunga na seminari ya Kibosho kwa elimu ya theology.
Mnamo mwaka 1960 alitunukiwa daraja la upadri katika parokia ya Kondoa mara baada ya kupewa daraja la upadri alitumwa parokia ya Kibakwe kuwa paroko mwaka 1961 hadi 1963 na mwaka 1963 hadi mwaka 1969 aliteuliwa kuwa katibu wa elimu na ilipofika mwaka 1966 hadi mwaka 1971 aliteuliwa kuwa makamu wa askofu  huku akiendele na nafasi yake ya katibu wa elimu na mwaka 1971 hadi mwaka 1972 aliteuliwa kuwa msimamizi wa kitume wa jimbo la Dodoma.Aliwekwa wakfu na Kardinali Laurean Rugambwa mwaka 1972.
Pia katika uongozi wake taasisi mbalimbali zilianzishwa ikiwemo Bihawana seminari, nyumba ya malezi ya waseminari wa jimbo Miyuji, chuo cha ufundi Mpwapwa-magogo,Chuo cha ufundi veyula, chuo cha Ufundi cha John Bosco, Seminari na chuo cha walimu cha wasalesiani, sekondari ya wasichana ya masista wa Huruma, kituo cha watoto walemavu Mlali, kituo cha watoto wenye mtindio wa akili (Cheshire Home Miyuji).
Vile vile vyuo vya kilimo Ipala na Chikopelo, Holy cross centre, hospitali ya masista wa Mtakatifu Gemma Galgani Miyuji, Kituo cha Hija Mbwanga, hosteli ya mapadri Kondoa, nyumba ya watoto yatima Kondoa, nyumba mpya ya Askofu na Ofisi ya Jimbo.
Askofu Isuja atakumbukwa pia kwa ushauri alioutoa Julai mwaka 2014 kwamba watanzania wanapaswa kuheshimu hadhi na mamlaka aliyonayo Rais wa Jamhuri ya Muunganao wa Tanzania Dk Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuthamini na kuzingatia mwongozo na ushauri mbalimbali anaoutoa kwa wananchi kwani mamlaka hayo yanatoka kwa Mungu.
Kauli hiyo  ambayo aliitoa katika mahubiri yake maalum wakati wa ibada ya misa ya jumapili katika Parokia ya Makole, Jimbo Katoliki la Dodoma, iliyokuwa na lengo la kuchangia ujenzi wa kanisa la kiaskofu  Jimbo la Kondoa, alisisitiza Watanzania waombe Mungu ajalie busara na hekima katika kutenda na kuamua mambo mbalimbali yahusuyo nchi yakiwemo malumbano yaliyokuwa yakifanyika nchini kote kuhusu mchakato wa kupata Katiba Mpya.
Askofu huyo alisema hafurahishwi na jinsi makundi mbalimbali ya Watanzania yalivyokuwa yanalumbana na kubeza hata miongozo inayotolewa na Rais Kikwete.
Wakati wa wakati wa sherehe ya miaka 40 ya Uaskofu wa Mhashamu baba Askofu  Mathias  Isuja, Septemba 18 ,2012, Rais  wa awamu ya tatu Benjamini William Mkapa  aliwataka kuachwa kwa mtazamo wa mbaya  wa kuwabeza viongozi wastaafu ambao wameitumikia nchi.
 “Kustaafu si kuchoka, sio uwe legelege lakini kwa imani unatakiwa kutoa mchango wako kwa kutumiza wajibu wako katika jamii” alisema
Alisema kuwa tatizo kubwa lililo katika jamii ni kutotaka kuheshimu mamlaka kwani kila mtu anajifanya kuwa mjuaji maishani, haambiliki.
Aidha Rais mstaafu Mkapa alishawahi kusikika akisema kwamba  anamheshimu Askofu huyo kutokana na kutosikia malumbano ya dini.
Alisema kuwa,Katika kipindi alichokuwa waziri wa mambo ya nje na hata alipokuwa rais hakuwahi kusikia malumbano yoyote ya kidini mkoani Dodoma na hilo ni jambo la kujifunza katika umoja na mshikamano wa madhehebu ya dini ya kikristo na kiislam.
“Tutamuenzi Askofu Isuja kwa kuzingatia kauli mbiu yake na ngao yake ya mapendo, haki na amani.” Alisema.
Naye Askofu Mkuu Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alisema kuwa askofu Isuja atakumbukwa kwa mchango wake kwa kuboresha huduma za afya na ujenzi wa shule na zahanati. 
Source: Sifa Lubasi, Habarileo Dodoma

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO