JOHANNESBURG, Afrika Kusini
 WANANCHI wa Afrika Kusini wameendelea kumkalia kooni Rais  Jacob Zuma wa Afrika Kusini baada ya Rais huyo kutangaza kuwa, anaheshimu uamuzi wa Mahakama ya Kati ya nchi hiyo dhidi yake.
Rais Zuma alitangaza juzi kwamba, anaheshimu uamuzi huo wa mahakama na kwamba, atarejesha katika hazina ya serikali kiasi cha fedha alichotakiwa kukirejesha baada ya kutumia fedha hizo katika mambo yake binafsi.

Rais Zuma amesema kuwa, hakukiuka Katiba ya nchi kwa makusudi. Rais huyo amesema kuwa, anaomba radhi yeye na kwa niaba ya serikali anawaomba radhi wananchi wa nchi hiyo na anavitaka vyama vyote vya kisiasa kuheshimu Katiba.

Hata hivyo, jana baadhi ya wananchi wa Afrika Kusini walionekana wakishinikiza Rais huyo kujiuzulu kwa kile walichosema kuwa ni kutokana na kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa uamuzi huo, Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini imemuagiza Rais Jacob Zuma kuirejeshea serikali fedha zilizotumika kukarabati makazi yake binafsi, kwenye moja ya kashfa kubwa za ufisadi zilizowahi kuripotiwa nchini humo katika miaka ya hivi karibuni.

Hatua ya Rais Zuma ya kukarabati makazi yake binafsi kwa bajeti ya serikali, ni jambo ambalo lililipua ghadhabu za wapinzani na kuwakasirisha maelfu  ya wananchi wa nchi hiyo.

Chama Kikuu cha upinzani katika Bunge la Afrika Kusini kimetangaza kuwa, kitatumia kila njia kuhakikisha Zuma anavuliwa madarakani endapo Bunge litazembea kufanya hivyo. Wabunge wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) wametangaza kuwa, wana mpango wa kuwasilisha muswada katika Bunge la nchi hiyo wa kutokuwa na imani na uwezo wa kisiasa wa Rais Zuma.

 Zuma alishika hatamu za uongozi nchini humo mwaka 2009 katika hali ambayo, kabla ya kuchukua wadhifa huo, Mahakama ilikuwa imemfutia tuhuma 700 za ufisadi wa fedha. Mwaka 2014 alifanikiwa kutetea kiti chake na hivyo kuongoza kwa muhula wa pili.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO