SERIKALI imeziagiza kila halmashauri nchini kubaini wazee walio katika maeneo yao na kuhakikisha wanapata huduma zote za msingi ikiwa ni pamoja na huduma za afya kutoka kwenye mapato yao wenyewe.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, jana wakati akizindua kampeni ya kitaifa ya “Mzee Kwanza – Toa Kipaumbele Apate Huduma”, mkoani Morogoro leo.
Alisema katika uzinduzi huo kuwa anajua  tangu serikali ipitishe maamuzi kwamba wazee watatibiwa bure katika maeneo yao, utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua katika baadhi ya maeneo hivyo kuchukua fursa hiyo kuagiza viongozi wote wa halmashauri mbalimbali kuhakikisha kuwa hilo linasimamiwa na kutekelezwa kwa ufanisi wote.
Uzinduzi huo uliofanywa kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umelenga kuikumbusha jamii ya watanzania wajibu wake wa kuwapa wazee hadhi wanayostahili katika maeneo mbalimbali ya huduma za kijamii.
“Wazee katika jamii yoyote wana nafasi muhimu sana katika ujenzi wa taifa. Wazee ndiyo hazina ya busara, hekima, amani na utulivu wa jamii yoyote. Familia isiyoheshimu wazee aghalabu itakuwa na vurugu na ugomvi kila kukicha. lakini jamii au familia inayoenzi wazee na kuwapa nafasi zao katika kushauri, kukosoa na kuelekeza utendaji wa siku hadi siku, jamii hiyo itakuwa na baraka siku zote,” alisema waziri Ummy


Alisema serikali ina matamanio mengi ya kuhakikisha wazee wote hapa nchini wanaishi maisha bora katika uzee kwa jamii kuthamini mzee na kumpa kipaumbele katika huduma.

Aidha, alisema lengo la kampeni ni kuhakikisha kuwa wazee wanapewa kipaumbele na wanahudumiwa kwanza wakati wote wanapokwenda kupata huduma mahali popote.
Aidha alisema kutokana na changamoto zilizopo sasa serikali imeanza kuchukua hatua ikiwamo ya kuandaa sera ya wazee ambayo wanaipeleka bungeni ili ipitishwe kuwa sheria kutoa haki kwa wazee na mahitaji yao ikiwemo pesheni, afya na huduma mbalimbali za jamii.

Aidha aliagiza kila mfuko wa hifadhi ya jamii kuhakikisha hakuna mzee anaenyanyasika katika kupata stahili yake tena kwa wakati.

Akifafanua zaidi kuhusu kampeni hiyo alisema kwamba imelenga kurejesha utamaduni wa zamani wa kuthamini wazee.

“Kwa kupitia kampeni hii ya mzee kwanza ni wajibu wa kila mtanzania kuona kuwa anafanya kila aweza kurejesha hadhi ya wazee na kuwapa umuhimu wa kwanza katika kupata huduma za  kijamii.”

Kwa kutambua umuhimu wa wazee katika taifa, alisema Waziri Ummy,  serikali ya awamo ya tano imeunda kitengo maalumu cha kuhudumia wazee na kukiweka chini ya wizara  Afya.

Alisema kuundwa kwa kitengo hicho kumetokana na serikali kutambua changamoto wanazokabili wazee wapatao 2,507,568 wenye miaka kati ya 60 na kuendelea sawa na asilimia 5.6 ya watanzania wote kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012.
Aidha Tanzania ina wazee takriban  474,053 wenye miaka 80 na kuendelea.
Katika tathmini inaonesha kwamba kundi la Wazee wenye umri kati ya miaka 60 – 64 wapo asilimia 31, miaka 60-69 wapo asilimia 20, kundi la miaka 70-74 wapo asilimia 19, wakati wazee wenye umri kati ya miaka 75-79 wapo asilimia 12 huku kundi la wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 80 ni asilimia 19 ya wazee wote nchini.


Waziri wa Afya Maendeleo ya  Jamii,Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizinduzi kampeni ya Wazee kwanza toa kipaumbele apate huduma leo Mkoani Morogoro

Tathmini ya ki mkoa inaonesha kuwa Mikoa inayoongoza kuwa na wazee wengi ni Kilimanjaro (6.4%), Mbeya (6.1%), Dar es Salaam (6.1%), Morogoro (5.6%), Tanga (5.6%), Dododoma (5.6%), Kagera (5%) na Mwanza (4.9%).
Alisema wazee hao wanakabiliwa na changamoto ya kipato cha matumizi ya msingi huku akiwa na ongezeko la uhitaji wa huduma za afya kutokana na kutokana na mwili kuchoka.

Ingawa mzee alikuwa mwajiriwa wa sekta rasmi, anayo nafasi ya kupata malipo ya pensheni ili kujikimu na kwa wale ambao walikuwa  wanachama wa nhif wana nafasi ya kuendele kupata huduma za bima ya afya maisha yako yote, Waziri aliuliza ni wangapi wana  fursa hizi za pensheni na bima ya afya ni asilimia ngapi ya wazee wote nchini.

“Mathalan, NHIF wametujuza hapa kwamba wanahudumia wastaafu 52,000 tu lakini pia takwimu zao zinaonesha wanahudumia wazee wapatao 244,000 kupitia huduma zao mbalimbali za bima ya afya. takwimu za mifuko mingine ya pension hazitakuwa mbali na ukweli huu kwamba hii ni asilimia ndogo ukilinganisha na idadi ya wazee nchini.

Alitaka kila Mtanzania kushiriki katika kampeni ya mzee kwanza  kwa viongozi wa halmashauri kuweka mikakati na ubunifu anuai kuhakikisha mzee popote alipo anaheshimiwa na kupewa kipaumbele.
mwisho

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO