Makumbusho ya Mkoa wa Iringa inavyoonekana kwa nje baada ya mradi wa Kuendeleza Utamaduni Nyanda za Juu Kusini (Fahari Yetu) kulifanyia ukarabati jengo hilo lililokuwa boma la mjerumani miaka 116 iliyopita (Picha na Frank Leonard)

Hili ndilo jengo la makumbusho ambalo litazinduliwa kesho.
MKUU wa Chuo Kikuu cha Iringa (IUCo), Profesa Joshua Madumulla amesema Nyumba ya Makumbusho ya Mkoa wa iringa itafanya kazi kubwa ya kukusanya na kutunza vitu mbalimbali vya kale.

Vitu hivyo vya kisayansi, sanaa na historia vitatoa fursa kwa jamii ya ndani na nje ya nchi kujionea hazina ya urithi uliopo mkoani Iringa.

“Uwekezaji katika urithi wa utamaduni hauna budi kupokelewa kama sehemu muhimu ya program itakayosaidia kukuza uchumi wa jamii husika na taifa kwa ujumla,”alisema.

Ukarabati wa nyumba hiyo iliyojengwa takribani miaka 116 iliyopita na utawala wa mjerumani aliyeitumia kama boma lake kuu, umefanywa kupitia mradi wa Kuendeleza Utamaduni Nyanda za Juu Kusini (Fahari Yetu) unaofadhiliwa na umoja wa nchi za Ulaya (EU) kwa zaidi ya Sh Milioni 230.

“Fursa ya kulibadili jengo hilo la boma la kihistoria kuwa jumba la makumbusho ni msingi imara wa kukataa hatari ya kuyumbishwa na mabadiliko yasiyoleta tija katika kukuza na kuendeleza tamaduni zetu na utalii wa kiutamaduni nchini,” alisema.

Meneja msaidizi wa mradi huo unaokishirikisha chuo hicho kikuu, Jimson Sanga alisema uzinduzi wa nyumba hiyo utafanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga.

Sanga alisema  katika hafla hiyo itakayowashirikisha mawaziri wengine na viongozi mbalimbali wa serikali, siasa, mila, utamaduni na taasisi mbalimbali za ndani nan je ya nchi, utakwenda sambamba na maonesho ya rasilimali za utamaduni na historia ya mkoa wa Iringa.

 

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO