SERIKALI imesema hakuna mlipuko wa kimeta katika wilaya za Chemba na Kondoa na kwamba uchunguzi unafanywa kubaini ugonjwa  ulioua watu saba  na wengine kuendelea kuumwa.
Awali watu walihisi kuwapo kwa mlipuko wa kimeta baada ya watu hao kufariki kutokana na  kula nyama ya ng’ombe.
Aidha hadi jana kulikuwa na wagonjwa wenye dalili  zinazofanana  na waliofariki 21 ambao wamelazwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema tafiti za awali zilizofanywa kwa kushirikiana na ofisi ya Mganga mkuu wa mkoa wa Dodoma zimebaini kuwa ugonjwa huo hauna uhusiano wowote na kimeta.
Alisema ugonjwa huo ulianza kujitokeza baada ya wananchi kula nyama ya ng’ombe ambaye alichinjwa kwa kuvunjika mguu katika kijiji cha Mwai Kisabe kata ya Kimaha wilaya ya Chemba mkoani Dodoma.
Hata hivyo Waziri huyo alisema kuwa watu tisa wa familia moja waliugua ugonjwa huo na  watatu walifariki huku wanakijiji wengine walikula nyama hiyo hawakuugua.
“Mpaka kufikia Juni 18 mwaka huu wagonjwa wameendelea kuongezeka siku hadi siku na kupelekea wagonjwa kufikia 21 ambao kati yao saba wamefariki na watoto 2 hali zao ni mbaya.” Alisema waziri Ummy.
Aliongeza kuwa Wizara yake imeunda kamati maalum kwa kushirikiana na ofisi ya Mganga mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kutibu dalili za ugonjwa huo ili kuzuia maambukizi mapya.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO