MABAKI ya ndege ya shirika la ndege la Misri Airbus 320 yenye mruko namba MS 804 yameonekana.
Ndege hiyo ilipotea katika rada za Misri na Ugiriki wakati ikipita katika anga la Mediterranea mwezi uliopita.
Wachunguzi wa Misri wamethibitisha kwamba mabaki hayo ni ya ndege hiyo.
Katika taarifa yao wamesema kwamba eneo ambalo mabaki hayo yapo limeshatambuliwa na kwamba kazi ya sasa ni kuchora mtawanyiko wa mabaki ulivyo.
Pamoja na kutoa taarifa hiyo chombo cha kina kirefu cha uchunguzi John Lethbridge ambacho kimekodiwa na serikali ya Misri kusaidia  kusaka mabaki ya ndege hiyo kimeleta picha za awali za mabaki hayo.
Ndege hiyo ilikuwa na abiria 66 wakati ilipoanguka Mei 19 ikiwa katika safari ya  kutoka Paris, Ufaransa kuelekea Cairo Misri bila kutoa ishara ya kuwapo kwa tatizo ndani ya ndege.
Hata hivyo imeelezwa kuwa ishara kutoka ndani ya ndege hiyo  ilionesha  kulikuwa na moshi katika choo na katika eneo la kuendeshea ndege kwenye chumba cha rubani.Aidha baadhi ya mabaki ya ndege hiyo yalionekana kiasi cha kilomita 290 kaskazini mwa mji wa Alexandria.
Mapema mwezi huu timu ya wataalamu wanaoshughulika na utafutaji wa mabaki hayo walisema kwamba wamefanikiwa kupokea ishara kutoka katika kisanduku cheusi ambacho hueleza mwenendo wa ndege. Ishara kutoka katika kisanduku hicho inatarajiwa kutoweka Juni 24 mwaka huu.
Sababu ya kuanguka kwa ndege hiyo bado haijajulikana lakini hakuna kundi la kigaidi lililodai kuhusika na kuanguka kwa ndege hiyo.
Wachambuzi wa mambo wamesema huenda kulikuwa na tatizo la kibinadamu au kasoro za kiufundi. Hata hivyo picha za setelaiti na takwimu zake zinaonesha kwamba  vitambua moto (moshi) vilijiwasha katika ndege hiyo muda mfupi kabla ya ishara ya ndege kupotea angani.
Kwa mujibu wa wachunguzi wa Ugiriki ndege hiyo ilitoka katika njia yake ghafla kwa digrii 90 kushoto na baadae digrii 360 kulia na kushuka kw akasi kutoka  mita 11,300 (37,000ft) hadi mita 4,600 (15,000ft) na kisha mita 3,000 (10,000ft) kabla haijapotea katika rada.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO