PRESS CONFERENCEMKUTANO KATI YA MHESHIMIWA UMMY A. MWALIMU (MB), WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA:
 TAREHE 16 JUNI, 2016

Ndugu wanahabari;
Tarehe 16 Juni, 2016 ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika. Siku hii huadhimishwa na nchi zote wanachama wa Umoja wa Afrika kwa mujibu wa Azimio lililopitishwa na nchi 51 za Umoja huo mnamo mwaka 1990. Azimio hili lilipitishwa kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya watoto wa shule yaliyofanywa na utawala wa Makaburu katika kitongoji cha Soweto, Afrika ya Kusini tarehe 16 Juni 1976. Katika tukio hilo la kusikitisha, inakadiriwa kuwa watoto wapatao 2,000 waliuwawa kikatili na utawala huo. Watoto hawa walikuwa kwenye harakati za kudai haki yao ya msingi ya kutobaguliwa kutokana na rangi yao.

Kwa waafrika na hususan Watanzania siku hii ni muhimu sana kwa kuwa inatukumbusha sisi wazazi, walezi, wanaharakati wa haki za watoto, Taasisi/Mashirika, Serikali na jamii kwa ujumla juu ya wajibu na majukumu yetu katika kuwapatia watoto haki zao za msingi.

Ndugu wanahabari;
Lengo kuu la kuadhimisha siku hii ni kuelimisha na kuwakumbusha wananchi na hasa wazazi na walezi  kuhusu Haki, Ustawi na Maendeleo ya watoto wa hali na  jinsi zote. Kadhalika, kupitia siku hii watoto hupata nafasi maalum ya kujieleza, kusikilizwa, kushiriki na kuonyesha vipaji vyao mbele ya wazazi, walezi, Serikali na jamii kwa ujumla.  Madhumuni mengine ni pamoja na:
  • Kukumbushana kuhusu kuwaendeleza watoto kielimu, kiafya, kiutamaduni na kimaadili na kuhakikisha uwepo wa ustawi wa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote;
  • Kuikumbusha na kuihamasisha jamii juu ya utoaji wa haki za msingi za watoto;
  • Kuinua kiwango cha uelewa na ufahamu wa matatizo yanayowakabili watoto wa Tanzania na  Afrika kwa ujumla;
  • Kuwahamasisha na kuwaunganisha wadau wote wa masuala ya watoto kukusanya nguvu kwa pamoja ili kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi.

Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hutumia siku hii:-
  • Kutathmini kwa kina utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2009, Sera  nyingine za kisekta zinazohusu watoto, sheria na mikakati mbalimbali inayomlenga mtoto pamoja  na mikataba ya kimataifa na kikanda kuhusu haki na ustawi wa Mtoto;
  • Kuhimiza kuwekeza rasilimali za kutosha katika afya, elimu na lishe bora ya watoto kama haki zao za msingi;
  • Kuhakikisha  kuwa watoto wanapata nafasi ya kushiriki  katika masuala yanayohusu maendeleo na ustawi wao, kupitia fursa tulizonazo ikiwa ni pamoja na kutumia vyombo vya habari.

Ndugu wanahabari;
Maadhimisho haya kila mwaka huambatana na kaulimbiu ambayo inalenga kuihamasisha jamii kuhusu changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo watoto wa Tanzania.  Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Ubakaji na Ulawiti kwa Mtoto Vinaepukika: Chukua Hatua Kumlinda Mtoto” (Child Abuse is Preventable: Take Action to Prevent a Child).  Kaulimbiu hii inatukumbusha sisi wazazi/walezi, Serikali na jamii kwa ujumla kuhusu suala zima la kuhakikisha kuwa watoto wote wanalindwa dhidi ya vitendo vyote vya ukatili ikiwepo ubakaji na ulawiti. Vitendo hivi husababisha madhara makubwa kwa mtoto kimwili, kisaikolojia, kijamii na kihisia.

Ni ukweli usiopingika kuwa katika dunia ya leo mamilioni ya watoto huathirika na vitendo vya ubakaji na ulawiti huku wengi wao wakiteseka bila ya kusema kokote kwa kukosa kujua nini wafanye katika kuyakabili mateso hayo, au wakati mwingine wanaowashtakia mateso yao hawachukui hatua zozote bali huwapuuza. Vitendo hivi vimesambaa na kuenea sehemu mbali mbali na mara nyingi hufanyika kwa vificho sana, ambapo watu ambao huwafanyia ukatili watoto wetu ni watu wa karibu ambao wanawaamini sana. Kinachohuzunisha zaidi ni kwamba yote haya hufanyika sehemu ambazo mtoto anatakiwa kujihisi salama kabisa, sehemu kama nyumbani, shuleni, na ndani ya jamii anayoishi.

Ndugu wanahabari;
Nchini Tanzania mwaka 2009 Serikali kwa kushirikiana na UNICEF, ilifanya utafiti wa kitaifa kuangalia hali halisi ya Ukatili dhidi ya watoto Tanzania. Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa Wasichana 3 kati ya 10 na mvulana 1 kati ya 7, wamefanyiwa ukatili wa kingono angalau mara moja kabla ya kutimiza miaka 18. Wasichana 4 kati ya 10 na wavulana 3 kati ya 10, wamefanyiwa ukatili zaidi ya mara tatu kabla ya kufikisha miaka 18; Wasichana 6 kati ya 10 wamefanyiwa ukatili ndani ya familia na msichana 1 kati ya 2 wamefanyiwa ukatili na walimu wao; Asilimia 49 ya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto hufanyika majumbani, wakati asilimia 23 hufanyika njiani wakati wa kwenda au kutoka shule na asilimia 15 ya unyanyasaji hufanyika shuleni. Aidha, Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Tanzania matukio ya ubakaji kwa watoto yameongezeka kutoka matukio 422 mwaka 2014 kufikia matukio 2358 mwaka 2015. Na katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2016 matukio 1,765 yameripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini.

Ndugu wanahabari;
Vitendo hivi vya Ubakaji na Ulawiti kwa watoto vina athari kubwa sana katika Ustawi wa watoto wetu.  Takwimu zinaonyesha kuwa Wasichana walioripoti kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia, kimwili na kiakili utotoni waliripoti hali mbaya zaidi ya afya kiakili na hata kimwili kuliko wasichana wengine. Na wavulana walioripoti kufanyiwa ukatili wa kiakili utotoni, waliripoti afya mbaya zaidi kiakili na kimwili kuliko wavulana wengine. Hii inathibitisha kuwa Ukatili dhidi ya watoto si suala la haki za watoto peke yake bali pia ni suala la Afya ya Jamii (Public health concern). Ambalo lisipofanyiwa kazi mapema linaweza kusababisha matatizo ya kijamii na kiafya kwa kizazi kijacho.

Kwa mantiki hiyo basi ili kukomesha ukatili huu kwa watoto tunahitaji nguvu za ziada ambapo jamii inatakiwa kubadili mtazamo mzima na kutambua kuwa watoto pia ni binadamu wenye haki na kwa hakika ndiyo waliobeba dira ya mwelekeo wa nchi yetu. Sote kwa pamoja tuna jukumu kubwa la kubuni na kutekeleza mikakati na sera za kitaifa zinazohusisha sekta mbalimbali, katika kuzuia na kukabiliana na tatizo hili na kuwalinda vizuri zaidi watoto wa Tanzania.

Ndugu wanahabari;
Serikali kwa upande wake itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kisera na kisheria katika kusimamia utekelezwaji wa haki ya mtoto ya Kuishi, Kulindwa, na Kuendelezwa. Juhudi za makusudi zimekuwa zikifanyika katika kuhakikisha kuwa Sheria ya mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 inatekelezwa ipasavyo. Sheria hii ndiyo inayotoa mwongozo wa haki za mtoto na kueleza hatua gani zichukuliwe endapo haki hizo hazitafuatwa, ikiwa ni pamoja na kumlinda kutoka katika vitendo vya ukatili. Tutahakikisha tunatoa elimu ya kutosha kuhusu ukatili dhidi ya watoto hususan watoto wa kike. Tunaamini elimu ni silaha kubwa ya kupambana na uhalifu wa aina yoyote ile.

Wizara yangu imeandaa Kitini cha Elimu ya Malezi kwa familia ambacho kimelenga kuwaelimisha wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kuwalea watoto wetu ili waje kuwa raia wema hapa nchini. Aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau inaandaa Mpango Kazi wa Taifa wa kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.  Mpango kazi huu unaandaliwa kwa kuzingatia uzoefu wa Mipango iliyotangulia ambapo pamoja na masuala mengine utahakikisha kuwa suala la uratibu na upatikanaji wa rasilimali za utekelezaji wake vinazingatiwa kwa kiasi kikubwa.  Mpango kazi huu utaweka mifumo mizuri ya kupambana na vitendo mbalimbali vya ukatili dhidi ya watoto ikiwemo suala la ubakaji na ulawiti kwa watoto na hasa mtoto wa kike. Utekelezaji wa mpango kazi huu utahusisha  Serikali, Asasi za Kiraia pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi yetu.

Kuhusu rasilimali fedha, Wizara yangu itaendelea kuzihimiza na kuzihamasisha halmashauri za wilaya na miji kutenga bajeti mahususi kwa ajili ya masuala ya ulinzi wa watoto, hasa katika kupunguza vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto. Nitumie hadhara hii kuzipongeza Halmashauri 19 kwa kutenga fedha katika bajeti yao ya mwaka 2015/16 kwa ajili ya masuala ya ulinzi wa Mtoto, zikiongozwa na Halmashauri za Njombe, Magu, Mbeya, Kasulu, Mufindi na Bukoba. Ninatoa rai kwa Halmashauri nyingine kuiga mfano huu na hivyo kutenga fedha maalumu kwa ajili ya shughuli za ulinzi wa watoto.

Ndugu wanahabari;
Katika kuhakikisha kuwa watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili wanapata urahisi wa kutoa taarifa na kupata huduma stahiki, Wizara yangu imeshapewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) namba ya simu 116 kwa ajili ya kuripoti matukio/vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Nitoe rai kwa watanzania wote kutoa taarifa za matukio ya ukatili wa watoto yanayotokea katika maeneo yenu kupitia namba hii. Huduma hii ni ya bure na inapatikana kupitia mitandao yote Tanzania. Ni matarajio yangu kuwa watoto na jamii kwa ujumla wataendelea kuitumia kikamilifu namba hii ili kutoa taarifa pale tu inapotokea tukio la ubakaji, ulawiti au tendo lolote la ukatili linalofanyika kwa mtoto.

Ndugu wananchi;
Napenda kutumia hadhara hii kuisihi jamii na hasa wazazi / walezi kujenga utamaduni wa kuwa na muda na watoto, ikiwa ni pamoja na kufuatilia / kuchunguza mienendo yao, hii itasaidia kutambua mapema endapo mtoto atakuwa kafanyiwa kitendo chochote cha ukatili. Aidha ni vyema tuzipe ushirikiano mamlaka mbalimbali zinaposhughulikia kesi za watoto, hasa katika kutoa ushahidi mahakamani.

Ningependa kuweka msisitizo katika suala hili kwakuwa kuna baadhi ya wazazi / walezi na wanajamii hawatoi ushirikiano kwa vyombo vya usalama wakati wa kutoa ushahidi wa tukio la ukatili aliofanyiwa mtoto ilihali walishuhudia au kuwa na taarifa za tukio hilo. Tabia hii si njema kabisa kama kweli tunataka maendeleo na ustawi bora wa watoto wetu.

Ndugu wanahabari;
Katika kupambana na tatizo la ukatili dhidi ya watoto, sheria peke yake si suluhisho la kuondokana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Hivyo, natoa rai kwa jamii kushirikiana na Serikali hasa Wizara yangu katika kutoa Elimu endelevu kwa jamii kwa kuwa suala la kubadili tabia, mtizamo, imani, desturi au mila ni mchakato unaochukua muda mrefu. Hatuna budi kuendelea kukemea vitendo vya ubakaji na ulawiti wa watoto mpaka vitakapokoma kabisa miongoni mwa jamii yetu ya Kitanzania.

Ndugu wanahabari;
Maadhimisho haya kwa mwaka huu yataadhimishwa katika ngazi ya Mkoa ambapo kila mkoa utaadhimisha siku hii kwa kushirikisha Halmashauri za wilaya/Manispaa/Miji, kata, vijiji, mashirika na taasisi mbalimbali zilizoko katika Mkoa husika na watu binafsi. Hii itaipa mikoa nafasi nzuri ya kutafakari matatizo yanayowakabili watoto ikiwa ni pamoja na kuwapatia haki zao za msingi.  Mikoa itapata pia nafasi ya kufikiria kuweka miradi endelevu kwa ajili ya usalama wa watoto.  

Ni matarajio yangu kuwa wanahabari pamoja na wadau wengine mtatoa ushirikiano wa hali ya juu, katika kuihamasisha jamii yetu kuhusu kaulimbiu ya mwaka huu na kutoa umuhimu wa kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika kwa ujumla.  Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa chanzo kizuri cha kufichua ukiukwaji wa haki za msingi za watoto ikiwa ni pamoja na vitendo mbalimbali vya ukatili na udhalilishaji wa watoto vinavyotokea katika jamii yetu.  Ningependa kuchukua fursa hii pia kuwakumbusha kuwa tunapaswa kuhakikisha watoto wote wanapewa haki zao za msingi pasipo kujali dini, rangi, jinsi, ulemavu na hata kabila.

Mwisho nawashukuru sana kwa kushirikiana nasi katika maadhimisho haya na napenda kuwasihi muendelee kusaidiana na Serikali katika kuijenga Tanzania imfaayo mtoto.

Kwa leo naomba niishie hapa, nikisisitiza kuwa Ubakaji na Ulawiti kwa Mtoto Unaepukika: Tuchukue Hatua Kumlinda Mtoto. ASANTENI KWA KUNISIKILIZA…

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO