Waziri Mwijage
SERIKALI imekiri kuwa pamoja na kuingiza tani elfu 41 za sukari nchini usambazaji wake umekuwa ni tatizo kutokana na ukosefu wa ushirikiano baina ya Wakuu wa Mikoa na wasambazaji.
Sambamba na hilo, Wakuu hao wameagizwa kuwasiliana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Florens Turuka ili kuwasilisha mahitaji ya sukari kwenye maeneo yao.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya sukari nchini.
Kwa mujibu wa Mwijage alisema hesabu za wataalam kwa mwezi mtukufu wa ramadhani zinahitajika tani elfu 40 kwa mwezi na hadi kufikia tarehe 13 mwezi huu tayari tani elfu 41 zilikuwa zimewasili Bandarini. 
“Sasa tani zilizopo hizo tatizo lipo kwenye usambazaji na ni ukosefu wa ushirikiano, tulishasema sukari ipelekwe kila Mkoa kwa ujazo mkubwa kuanzia tani 300-500 ili kuthibiti uhaba wa sukari, tukiwauliza wenye sukari wanasema sukari ipo wanunuzi hakuna,”alisema Mwijage
Hata hivyo alisema Wizara hiyo imeandika dokezo kwa wahusika wenye sukari wapeleke kiasi gani kwa kila mkoa. 
“Ninachoomba watendaji wa serikali na viongozi wenye dhamana wawasiliane na Katibu mkuu ili awasiliane na wasambazaji ili waweze kupeleka sukari mikoani maana ni kweli kuna tatizo la sukari huko,”alisema Waziri huyo. 
Hata hivyo alisema namna ya kutatua tatizo hilo ni viongozi wa mikoa kufuatilia na kutoa maelekezo wanahitaji tani ngapi katika mikoa yao kama walivyofanya wakuu wa mikoa ya Mwanza na Manyara.
Katika hatua nyingine, Wizara hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania(TBS), imeandaa mkutano mkuu wa 22 wa Umoja wa Mashirika ya Viwango Afrika(ARSO) utakaofanyika kuanzia tarehe 20-24 mwezi huu Jijini Arusha.
Mwijage alisema mkutano huo utahudhuriwa na wageni kutoka nchi 37 za Afrika na Washirika wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO