Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Salma Ali Hassan akisoma tamko la Tume mbele ya vyombo vya habari, ukumbi wa...
|
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P 2643, DAR ES SALAAM
Simu: +255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi: +255 22 2111281
Barua Pepe: chragg@chragg.go.tz
Tovuti: www.chragg.go.tz.
|
Juni 16, 2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tamko la Tume ya Haki za Binadamu
na Utawala Bora Wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16, 2016
Tunapoadhimisha kumbukumbu ya siku ya mtoto wa Afrika hii leo Juni 16, 2016
ikiwa ni mara ya 26 tangu uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) uizindue
siku hiyo mwaka 1991, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), inatoa
wito kwa umma, Serikali na wadau mbalimbali wa haki za watoto kuunganisha nguvu
kupinga vitendo vyote vya ukatili wanavyofanyiwa watoto mahali popote Tanzania.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inasikitishwa na kukerwa na matukio
ya ukatili wa aina mbalimbali wanayofanyiwa watoto ambayo yamekuwa yakiripotiwa
na vyombo vya habari. Matukio hayo yanajumuisha: kutupwa kwa watoto wachanga, ubakaji,
ulawiti, ukeketaji, mauaji, na watoto wa kike kuozwa katika umri mdogo, hivyo kuwanyima
haki zao, hususan haki ya kupata elimu. Matendo haya yenye kuvunja haki za
watoto yanafanywa na watu wazima wenye akili timamu.
Tume inalaani kwa nguvu zake zote ukatili wa aina yoyote wanaofanyiwa
watoto. Hivyo inawataka wananchi kuhakikisha kuwa watoto wote nchini wanapewa malezi
na makuzi stahiki katika familia na jamii. Pia wanalindwa dhidi ya vitendo vya
unyanyasaji na wanapata fursa katika maendeleo ya ustawi wao.
Hatua hii ni muhimu kwani maendeleo ya Taifa lolote duniani yanawategemea
watoto. Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 imeonyesha kuwa idadi ya watoto nchini Tanzania ni zaidi ya
asilimia 50 ya watu wote. Kwa hiyo, jukumu la kuwalinda watoto dhidi ya vitendo
vya kikatili na kuwapa fursa ya maendeleo ya ustawi wao halina mjadala. Jukumu
hili ni la kila mmoja wetu ikiwemo familia, jamii na Serikali.
Tume inasisitiza kwamba binadamu wote huzaliwa
huru, na wote ni sawa na kwamba kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na
kuthaminiwa utu wake. Haki hii ya usawa inatambuliwa katika ibara ya 12 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na mikataba ya haki za
binadamu ya Umoja wa Afrika (AU) na kimataifa.
Nchi yetu imesaini na kuridhia mikataba hii ya
kimataifa na kikanda na kutunga sheria mbalimbali za kuharamisha makosa ya
ukatili dhidi ya binadamu. Miongoni mwa sheria hizi ni Sheria ya Mtoto, Sheria
ya Kanuni za Adhabu, Sheria ya Mwenendo
wa Makosa ya Jinai na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana.
Hivyo, vitendo vya ukatili vikiwemo vitendo vya ubakaji,
ulawiti, na ndoa za utotoni, haviwezi kuendelea kutendeka huku Serikali,
wananchi na wadau wa haki za binadamu wakitazama bila kuchukua hatua.
Ni wajibu wetu sote, kuchukua hatua stahiki
kuwalinda watoto; na Serikali kupitia vyombo vyake iendelee kushughulikia kesi
za watoto kwa haraka zaidi.
Katika kuyapa kipaumbele masuala ya watoto mwaka 2007 Tume ilianzisha dawati
maalum kwa ajili ya kushughulikia masuala ya watoto nchini, yakiwemo malalamiko
mbalimbali ya uvunjwaji wa haki za watoto.
Katika kufuatilia malalamiko ya watoto hasa yanayohusu ulawiti na ubakaji,
Tume imebaini changamoto mbalimbali, zikiwemo:
upelelezi wa kesi hizi kuchukuwa muda mrefu, jamii kutokuwa na hamasa ya
kupinga vitendo vya ubakaji na ulawiti, na kutowapeleka watoto hospitali mara
inapogundulika wametendewa unyama huo, jambo ambalo hupoteza ushahidi.
Aidha, wahusika huwatishia maisha watoa taarifa, na wakati mwingine kwa
kuwa matukio mengi yanawahusisha wanafamilia au watu wa karibu, hivyo ndugu hao
hukaa na kusuluhishana nje ya mahakama.
Changamoto nyingine ni baadhi ya madaktari kutotoa ushirikiano wa kutosha
katika mashauri haya, na ucheleweshwaji katika kusikiliza kesi hizi.
Hivyo basi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora inatoa mapendekezo yafuatayo:
1.
Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto
kuyapa kipaumbele mashauri yanayohusu ubakaji na ulawiti wa Watoto, kufanya
upelelezi thabiti na kuwakamata wahusika, na kuwafikisha mahakamani kujibu
mashtaka.
2.
Madaktari katika hospitali mbalimbali kuyapa
kipaumbele matukio ya ulawiti na ubakaji na kuwasaidia wahanga wa vitendo hivyo,
hasa katika kutoa ushahidi mahakamani.
3.
Mahakama ziharakishe usikilizaji wa kesi za ubakaji na
ulawiti na kutoa hukumu kwa wakati.
4.
Wananchi, jamii, kamati za ulinzi na usalama kwa
ujumla watoe ushirikiano kwenye vyombo vya sheria kwa kutoa taarifa za matukio
ya ukatili wa watoto kama vile ndoa za utotoni, ubakaji na ulawiti wa watoto.
5.
Wazazi na walezi waache kuharibu mwenendo wa mashauri
ya ubakaji na ulawiti kwa kukubaliana na wabakaji nje ya vyombo vya sheria hivyo
kupoteza ushahidi.
6.
Wazazi watakaobainika kulinda uhalifu kwa kutotoa taarifa
wachukuliwe hatua za kisheria.
7.
Wazazi na walezi wawe makini na mienendo ya watoto ili
kubaini mabadiliko ya kitabia.
8.
Wazazi/walezi wawe karibu na watoto na kujenga urafiki
nao ili kuwafanya waweze kutoa taarifa zozote zisizo za kawaida kwa urahisi.
9.
Wazazi/walezi wachunguze mahusiano ya mtoto na jamii
ya nyumbani na nje ili kubaini viashiria vya udhalilishaji wa watoto au vitendo
vya ukatili na kuvizuia kabla havijatokea.
UBAKAJI NA
ULAWITI KWA WATOTO VINAEPUKIKA:
Chukua hatua kumlinda mtoto!
Imetolewa na:
(SIGNED)
Salma Ali Hassan (Kamishna)
Kny. Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Juni 16, 2016
COMMENTS