Ofisa Nyuki wa Wilaya ya Mvomero, Oscar Kunambi (aliyechuchumaa kushoto) akisaidiana na mwanakikundi cha Dakawa Green Voices, Neema Obeid, kuweka vizuri mzinga.
Mwanahabari Judica Losai (wa pili kushoto) akimuuliza maswali Ofisa Nyuki wa Wilaya ya Mvomero, Oscar Kunambi, wakati wakiwa kwenye eneo la ufugaji wa nyuki.

Baadhi ya mizinga ya akinamama wa Dakawa Green Voices ikionekana kuning’inia kwenye miti. Mizinga hii tayari ina nyuki.

Akinamama wa Dakawa Green Voices wakisikiliza maelezo kutoka kwa mtaalam wa ufugaji nyuki, Oscar Kunambi, ambaye hayupo pichani.

Ofisa nyuki wa Wilaya ya Mvomero,, Oscar Kunambi, akiwaelekeza akinamama wa Dakawa Green Voices namna ya ufugaji bora wa nyuki.


TAKRIBAN kilometa 10 kutoka Kijiji cha Dakawa kuna kitongoji cha Magogo kilichoko msituni kabisa ambako pia kuna mashamba ya mpunga.
Msitu huu ambao bado ungali na miti mingi ya asili ambayo imenusurika kucharangwa na wachoma mkaa na wanaotafuta ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo, ndiko akinamama wapatao 30 wameamua kutundika mizinga kwa ajili ya ufugaji wa nyuki katika shamba lenye ukubwa wa ekari nne.
Licha ya kujikwatua vilivyo, lakini wanapoingia katika msitu huu akinamama hawa hawana mchezo kabisa, baadhi yao wanavaa mavazi maalum ya kujikinga na nyuki na kuanza kukagua mizinga yao kama tayari nyuki wamekwishaingia.
“Kujipamba ni jambo la kawaida, lakini tunapokuja huku tuko kikazi zaidi,” anasema Neema Obeid huku akipenya kwenye vichaka kuiendea mizinga ambayo iko juu ya miti mikubwa.
Akina mama hao wa kikundi cha Dakawa Green Voices Women Group wameamua kuingia kwenye ujasiriamali wa ufugaji wa nyuki kwa malengo makubwa mawili – kupata fedha kutokana na mazao ya nyuki pamoja na kupambana na mabadiliko ya tabinchi.
“Misitu inateketea, watu wanaendelea kuchoma mkaa na wengine wanafyeka miti ili wapate mashamba, lakini kwa kuanzisha ufugaji huu wa nyuki, kamwe hatutakubali kuona yeyote akikata hata fimbo, achilia mbali miti mikubwa,” anasema Bi. Mariam Bigambo, mshiriki kiongozi wa mradi huo.
Mariam Bigambo ni miongoni mwa akinamama 10 waliopatiwa mafunzo nchini Hispania mapema mwaka huu na wanatekeleza kwa vitendo mradi wa Green Voices, ambao unafadhiliwa na taasisi inayojihusisha na maendeleo ya wanawake wa Afrika, ijulikanayo kama Women for  Africa Foundation  inayoongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, María Teresa Fernández de la Vega. Hapa nchini, mradi huo unasimamiwa na asasi ya Environment Media Agenda (EMA) chini ya uratibu wa Bi. Secelela Balisidya
Akinamama wengine wanatekeleza miradi mbalimbali ya ujasiriamali unaoendana na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Kigoma, Kilimanjaro, Pwani na Mwanza.
Mama Bigambo anasema kwamba, ufugaji huo unahitaji kutunza mazingira ili kuwawezesha nyuki kupata chakula chao hasa nekta na maji, hivyo ni vizuri kuhakikisha mazingira yanakuwa salama.
Aidha, anasema kwamba, kwa kuwa Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine duniani, inakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi, ni vizuri kufanya shughuli za uchumi zinazohakikisha kwamba mazingira yanatunzwa na wakati huo huo shughuli hizo zikichangia kupambana na mabadiliko ya tabiachi, huku ufugaji wa nyuki ukiwa miongoni mwa shughuli hizo.
“Bila kutunza mazingira hata hao wanaokata mkaa na wanaotafuta mashamba watalia baadaye kwa kuwa miti itakwisha, tutabaki na jangwa ambao halitatoa mazao tena. Tutakufa,” anasisitiza.
Kuhusu ufugaji huo wa nyuki, Mama Bigambo anasema kwamba, ingawa zamani ilionekana kama shughuli za akina baba, lakini kama wanawake watafundishwa wanaweza kuendesha ujasiriamali huo bila shida.
“Gharama kubwa ya ufugaji wa nyuki iko mwanzoni tu – kutafuta mizinga pamoja na eneo bora linalofaa kwa ufugaji ambalo maua na maji yanapatikana kwa urahisi, baada ya hapo kazi yako ni kutembelea na kuangalia maendeleo.
“Nyuki hawachungwi kama ng’ombe, mbuzi au nguruwe wala hawaangaliwi kama kuku, hawahitaji chanjo ya ugonjwa wowote, hivyo ni rahisi kutundika mizinga yako katika eneo husika na kuendelea na shughuli zako nyingine,” anafafanua.
Akizungumzia umuhimu na faida za nyuki, Mama Bigambo anasema kuwa licha ya kusaidia kutunza mazingira, lakini nyuki ni muhimu kwa maisha ya binadamu na viumbe hai vyote, kwani ndio wanaofanya uchavushaji wa mimea.
Anazitaja faida za ufugaji nyuki kuwa ni asali na nta, mazao ambayo yana faida kubwa hata katika soko la kimataifa.
Katibu wa kikundi hicho, Amina Buteta, ana matumaini makubwa kwenye mradi huo na anasema kwamba unaweza kuwakomboa wanawake wa Dakawa na vijiji vya jirani kwa kujipatia kipato kikubwa.
“Tunakuja huku shamba kila baada ya wiki, wakati mwingine tunakuja kwa zamu kuangalia maendeleo, hivyo hatubanwi na ufugaji wa nyuki na tunaendelea na shughuli zetu nyingine,” anasema.
Amina anasema kwamba, wameanza na mizinga 30, lakini malengo yao ni kuwa na mizinga 4,000, lakini changamoto wanayokabiliana nayo ni mtaji wa kununulia mizinga hiyo.
Inaelezwa kwamba, mzinga mmoja unauzwa Shs. 70,000, lakini kutokana na uchumi kuwa mdogo, wengi wanashindwa kupata fedha za kununulia.
“Lakini ipo siku tutafanikiwa tu, hakuna shida, kwa sababu tumedhamiria,” anasema.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Dakawa, Andrea Muhando, anasema ufugaji wa nyuki siyo tu utawakomboa kiuchumi wanawake hao na jamii nzima kwa ujumla, lakini utasaidia kutunza mazingira katika eneo hilo ambalo limeshindwa kuzalisha mazao vya kutosha kutokana na mafuriko ya mara kwa mara pamoja na mvua zisizo za uhakika.
Anasema, kukosekana kwa mvua katika misimu tarajiwa kama ilivyokuwa zamani pamoja na mafuriko makubwa yanayosababisha maafa ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi, hivyo ni vyema wananchi wakaangalia miradi mingine endelevu yenye kipato lakini inayoweza kutunza mazingira.
“Kila mwaka mvua zinashindwa kunyesha kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa, na zinaponyesha zinakuja kwa nguvu na kuleta madhara hata kwa mimea kama tunavyoshuhudia katika eneo hili kila mwaka.
“Mwaka huu mafuriko yameharibu hekta 240 za mazao mbalimbali, ukiwemo mpunga ambao umekuwa mkombozi wa mkulima, na sasa tunategemea tu katika maeneo ya kondeni pekee,” anasema.
Kwa upande mwingine, Ofisa Nyuki wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Oscar Kunambi, anasema kwamba kuanzishwa kwa mradi wa akinamama hao kutachochea jamii kuingia kwenye ufugaji wa nyuki wilayani humo badala ya kutegemea kilimo na mifugo pekee.
Anasema kwamba, soko la asali ni kubwa nchini Tanzania, ambapo tayari kuna kiwanda kikubwa wilayani Kibaha kinachohitaji malighafi lakini asali inayozalishwa haitoshelezi mahitaji.
Aidha, anasema kwamba, wilaya hiyo ina maeneo mengi yenye misitu ambayo ikitumiwa kwa ufugaji wa nyuki inaweza kuleta faida kubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla.
“Unapofuga nyuki, mbali ya kupata faida kutokana na mazao yake, lakini unasaidia kuyalinda maeneo hayo kwa sababu hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kwenda kukata miti sehemu ambayo kuna nyuki, kwanza usalama wake utakuwa mdogo,” anasema.
Vyanzo vya habari vinaeleza kwamba, asali ina soko zuri kwani kilo moja inauzwa kwa Shs. 15,000 ikiwa shambani.
Kwa mujibu wa Kunambi, mzinga mkubwa wa kisasa una uwezo wa kutoa kati ya kilo 10 hadi 20 za asali baada ya miezi sita tangu nyuki kuingia kwenye mzinga.
Amewataka wananchi katika wilaya hiyo kujitokeza na kuanzisha miradi ya ufugaji nyuki, huku akiahidi kwamba yuko tayari kufanya kazi usiku na mchana kuwasaidia utaalamu na ushauri.
Mkurugenzi wa Wilaya ya Mvomero, George Mkindo, amewapongeza akinamama hao kwa jitihada zao na akasema halmashauri yake itawaunga mkono kwa kila hali.
“Nimeambiwa kwamba wanahitaji shamba, nadhani itakuwa vyema kama tukiongea na vijiji ili kutenga mashamba kwa ajili ya ufugaji wa nyuki kwa sababu inatupunguzia hata sisi kazi kubwa ya kupambana na waharibifu wa mazingira, kwa kuwa wananchi wenyewe watakuwa walinzi,” anasema.

<Mwisho>.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO