Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na burudani
nchini limepiga marufuku kumbi zote za burudani zisizo na vibali kufanya maonesho ya
aina yoyote.
Aidha, BASATA linawakumbusha wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani wenye
vibali kufuata sheria, kanuni na taratibu walizopewa kwenye vibali vyao vya uendeshaji
wa kumbi.
Katika hili BASATA linawaelekeza wamiliki na mameneja wa Kumbi zote nchini
kuhakikisha wanakuwa na vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia muda
wa utumizi wa kumbi, kuepuka kelele zinazosumbua kwenye maeneo maalum hasa
makazi ya watu na kuhakikisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu.
Aidha, BASATA linawakumbusha wamiliki wote wa kumbi za burudani kwamba ni
marufuku kukusanya watoto katika kumbi zao kupitia kile kinachoitwa ‘Disko Toto’ ili
kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.
Uzoefu unaonesha kwamba, nyakati za sikukuu kama hizi za Eid El Fitr wamiliki na
mameneja hawa wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kumezwa na faida katika
biashara zao kiasi cha kuandaa madisko ya watoto hali ambayo imekuwa ikisababisha
maafa makubwa ambayo yangeweza kuepukwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.
BASATA mamlaka inayotoa vibali vya kumbi za sherehe na burudani linasisistiza
kwamba halitafumbia macho ukumbi wowote utakaokiuka maelekezo haya sambamba
na kuruhusu maonesho machafu yenye kudhalilisha utu wa binadamu hasa yale
yanayoonesha maungo ya ndani.
Hatua kali na za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maagizo haya.
BASATA linawatakia wasanii na wadau wote wa Sanaa sherehe njema ya Eid El Fitr
yenye furaha tele.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO