Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein (wa pili kulia) akiangalia baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na wajasiliamali  wanawake wakati alipotembelea banda la Wanawake na Maendeleo (WIPE) katika Viwanja vya Maonesho ya Biashara mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Mke wa Rais wa awamu ya tatu Mama Anna Mkapa.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Tanzania ya Viwanda inawezekana hasa endapo watanzania wenyewe watathamini bidhaa zinazozalishwa humu nchini.
Akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari mara baada ya kutembelea Maonesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam leo, Dk. Shein alisema kuwa watanzania kupenda na kuthamini bidhaa za ndani ni jambo muhimu katika kufanikisha dhamira ya kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Dk. Shein alifafanua kuwa kumekuwepo na tofauti kubwa ya ubora wa bidhaa zinazozalishwa hivi sasa humu nchini ikilinganishwa na miaka iliyopita ambapo ubora wa bidhaa nyingi umeongezeka na kuwa wa kiwango cha juu.
“Tumeshuhudia kiwango cha hali ya juu cha ubunifu mkubwa katika mabanda ya Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) na Mamlaka ya Elimu ya Ufundi (VETA) ambao mashine mbalimbali zimebuniwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali” Dk. Shein alieleza.
Alitolea mfano wa mashine ya kusindika mwani katika banda la SIDO ambayo alisema ni muhimu sana kwa Zanzibar ili kuongeza thamani ya mwani na hatimae kuongeza kipato kwa kinamama ambao ndio wazalishaji wakubwa wa zao hilo la baharini Zanzibar.
Alibainisha kuwa mbali ya ubunifu wa mashine lakini hata ubora wa bidhaa za vyakula umeimarika kuanzia usindikaji hadi ufungaji wake hivyo kuweza kukidhi viwango vinavyotakiwa.
Rais wa Zanzibar na Mwenykiti wa Baraza la Mapinduzi aliongeza kuwa watanzania kutokupenda bidhaa za ndani ni tatizo kwa hivyo hawana budi kuunga mkono jitihada za ubunifu huo kwa kuzipenda na kuthamini bidhaa zinazozalishwa nchini.
Akiwa amefuatana na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Balozi Amina Salum Ali, Dk. Shein alitembelea mabanda ya Banda ya Zanzibar, SIDO, VETA, Mfuko wa Fursa Sawa Kwa Wote (EOTF) chini ya Mwenyekiti wake Mke wa Rais Mstaafu mama Anna Mkapa na mabanda ya washiriki wa nje ambayo ni Ujerumani, Afrika Kusini na Jamhuri ya Watu wa China.
Mapema Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) Edwin Rutageruka alimueleza Dk. Shein kuwa maonesho hayo yaliyoanzishwa miaka 40 iliyopita yamekuwa yakiimarika mwaka hadi mwaka.
Alifafanua kuwa katika kuimarisha maonesho hayo mamlaka imejitahidi kuyafanya kuwa ya kutengeneza biashara kati ya wafanyabiashara wa ndani na nje badala kuonekana kuwa sehemu ya wananchi kuja kununua bidhaa.
“Tumeweka vyumba maalum vya wafanyabiashara kukutana na kufikia makubaliano ya kibiashara kubwa zenye tija ili kusaidia ukuaji wa biashara” alieleza Retageruka.
Kuhusu idadi ya washiriki alieleza kuwa mwaka huu nchi 30 zimeshiriki ikilinganishwa na nchi 25 mwaka jana ambapo mwaka huu makampuni 650 ya ndani na nje yanashiriki maonesho hayo.
Alifafanua kuwa maonesho ya mwaka huu yanalenga katika kuwaunganisha wazalishaji na masoko na kuangalia mfumo mzima wa uzalishaji bidhaa tangu mali ghafi hadi ikiwa sokoni.
Sambamba na lengo hilo mamlaka inaendeleza kampeni ya “buy Tanzania” ambayo lengo lake ni kuwahamasisha watanzania kununua bidhaa zinazotengenzwa humu nchini badala ya kujiendekeza kwa kununua bidhaa za nje wakati ubora ni ule ule.


Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein  akipata maelezo toka kwa mjasiliamali juu ya vyakula vilivyosindikwa wakati alipotembelea banda la Wanawake na Maendeleo (WIPE), Viwanja vya Kimataifa vya Maonesho ya Biashara vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam mapema hii leo.

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein (kushoto), akiangalia mafuta ya kula yanayotengenezwa na wajasiliamali , wakati alipotembelea banda la Wanawake na Maendeleo (WIPE), Viwanja vya Kimataifa vya Maonesho ya Biashara vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam leo.

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein akiuliza swali kwa mjasiliamali wakati alipotembelea banda la wanawake Wajasiliamali  (WIPE), Viwanja vya Kimataifa vya Maonesho ya Biashara vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam leo.

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein akipata maelezo kuhusiana na uzazi wa mpango, wakati alipotembelea banda la Wanawake na Maendeleo (WIPE), Viwanja vya Kimataifa vya Maonesho ya Biashara vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam leo.

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein akipata maelezo toka kwa Mkurugenzi wa VETA kanda ya Dar es Salaam Bw. Habibu Bukko wakati alipotembelea banda la VETA katika  Viwanja vya Kimataifa vya Maonesho ya Biashara vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam mapema hii leo.

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein akipata maelezo toka kwa Mkurugenzi wa VETA kanda ya Dar es Salaam Bw. Habibu Bukko wakati alipotembelea banda la VETA katika  Viwanja vya Kimataifa vya Maonesho ya Biashara vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam mapema hii leo.

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein akiwa katika picha ya pamoja na Waziri  wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Zanzibar Balozi  Amina Salum Ali,wakati alipotembelea banda la Wanawake na Maendeleo (WIPE) katika  Viwanja vya Kimataifa vya Maonesho ya Biashara vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam mapema hii leo.                 
Picha na Eliphace Marwa - Maelezo

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO