Serikali imeitaka kampuni ya Dodsal Hydrocarbons kuongeza kasi ya shughuli za utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia nchini ili kuendana na mipango ya Serikali ya kuhakikisha kuwa nishati hiyo inatosheleza mahitaji ya nchi kipaumbele kikiwa ni kuzalisha nishati ya umeme.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nishati na Madini na Madini, Profesa Sospeter Muhongo jijini Dar es Salaam alipokutana na Ujumbe wa kampuni hiyo ulioongozwa na mmiliki na Mwenyekiti wa kampuni husika, Dkt. Rajen Kilachand. Kampuni hiyo inatafiti mafuta na gesi kwenye eneo la nchi kavu katika Bonde la Mto Ruvu mkoani Pwani.
“ Hatutaki kuchelewa, tunataka gesi ya kutosha ya kukidhi mahitaji yetu kipaumbele kikiwa ni kuzalisha nishati ya umeme, kutumika viwandani na majumbani, na ikitoshelesha mahitaji yetu itatuwezesha pia kuzalisha umeme ambao tutauuza nje ya nchi, lakini pia baadhi ya nchi barani Afrika zimeonesha nia ya kununua gesi hii kutoka nchini,”alisema Profesa Muhongo.
Ujumbe wa kampuni hiyo ambayo mwezi Julai, 2015 ilitangaza kugundua gesi ya kiasi cha futi za ujazo trilioni 2.17 katika Bonde la mto Ruvu, ulikuja kuonana na Profesa Muhongo ili kueleza mpango kazi wa shughuli zake hapa nchini.
Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Dkt. Kilachand aliwashukuru watendaji wa Wizara na TPDC kwa kushirikiana na kampuni husika katika kuhakikisha shughuli za utafiti na uchimbaji wa gesi na mafuta zinafanikiwa na kueleza kuwa kampuni hiyo inathamini ushirikiano ulipo kati ya nchi za Tanzania na India na kuahidi kuuendeleza kwa kushirikiana katika shughuli mbalimbali.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO