Mwekezaji katika mgodi wa Makaa ya Nakshi wa Ntyuka mkoani Dodoma, Sweekar Nayak (kulia) akielezea namna ambavyo shughuli za uchimbaji zinavyofanyika mgodini hapo. Kushoto ni Afisa Madini Mkazi Dodoma, Mhandisi Slimu Mtigile na katikati ni Mjeolojia Edward Affa.

Imeelezwa kwamba mgodi wa madini ya ujenzi yajulikanayo kama Mawe ya Nakshi uliopo katika kijiji cha Ntyuka mkoani Dodoma unatarajia kujenga Kiwanda cha kukata na kusafisha madini hayo ili kukuza soko la ndani na nje ya nchi.
Kiwanda hicho kitajengwa katika kijiji cha Mkulabi na mgodi wa Ntyuka ambao unamilikiwa kwa ubia kati ya Kampuni ya Udbhav International Ltd ya nchini India na Israel Chunga ambaye ni Mtanzania.

Hayo yalielezwa na Mwekezaji katika mgodi huo, Sweekar Nayak wakati wa ziara mgodini hapo iliyofanywa na Afisa Madini Mkaazi Ofisi ya Dodoma, Mhandisi Slimu Mtigile ambaye aliambatana na Maafisa Habari kutoka Wizara ya Nishati na Madini lengo likiwa ni kujionea shughuli zinazofanywa na mgodi huo.

Nayak alisema kiwanda hicho kinatarajia kuajiri wafanyakazi wapatao 114 na kwamba mawe ya nakshi yatakayozalishwa kiwandani hapo yatakuwa na ubora mkubwa kumudu ushindani wa soko la kimataifa.

Alisema soko la mawe hayo kwa nchi za Ulaya, China na Japan ni kubwa na hivyo malengo na matarajio yao ni kuhakikisha wanazalisha bidhaa yenye ubora wa hali ya juu ambayo itakubalika katika nchi hizo na vilevile nchi zingine zitakazokuwa na uhitaji.

“Wazalishaji wengi wa mawe ya nakshi hapa nchini soko lao ni hapa hapa lakini sisi tumelenga kwenda hadi nje ya Tanzania; tunatarajia kuwa na uzalishaji wenye kiwango cha kimataifa,” alisema Nayak.

Alisema kiwanda hicho vilevile kitahudumia wachimbaji wadogo wa madini ya aina hiyo wa maeneo jirani ili nao waweze kupata bidhaa zenye ubora na hivyo kujiongezea kipato kutokana na shughuli husika.

“Kiwanda chetu kitapokea kazi kutoka kwa wachimbaji wadogo wa mawe ya nakshi na ili kuwasaidia kuinua kipato chao, tutatoza gharama nafuu,” alisema Nayak.

 
Afisa Madini Mkazi Dodoma, Mhandisi Slimu Mtigile (kushoto) akifafanua jambo kwa wamiliki wa mgodi wa Mawe ya Nakshi wa Ntyuka. Kulia ni Israel Chunga na katikati ni Sweekar Nayak.
Akizungumzia makadirio ya gharama za shughuli za uchimbaji wa madini hayo hadi ujenzi wa kiwanda, Nayak alisema mradi huo kwa pamoja unatarajiwa kugharimu kiasi cha Dola za Marekani milioni 5.5.

Aidha, alisema shughuli za uchimbaji wa awali wa madini katika mgodi huo zilianza mwezi Mei mwaka huu na kwamba uzalishaji rasmi unatarajiwa kuanza mwezi Oktoba mwaka huu mara baada ya kukamilika kwa vifaa vya uchimbaji ambavyo vinatarajiwa kuwasili hivi karibuni kutokea nchini India.

Naye Mhandisi Mtigile alipongeza juhudi zinazofanywa na mgodi huo katika utekelezaji wa shughuli zake na kuuasa kuhakikisha unafuata sheria za zilizopo ili kuwa na uzalishaji wenye tija.

“Ili mfanye shughuli zenu kwa ufanisi bila usumbufu, hakikisheni mnafuata sheria, taratibu na kanuni zilizopo na endapo mtakutana na vikwazo vya aina yoyote Ofisi yetu ipo wazi kutoa ushirikiano,” alisema.

Alisema uanzishwaji wa mgodi huo pamoja na ujenzi wa kiwanda husika utakuwa na mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa wananchi wa maeneo jirani na vilevile kuongeza pato la Taifa kutokana na kodi na tozo mbalimbali za Serikali.

Aidha, alitoa wito kwa wachimbaji wengine kuendesha migodi yao kitaalam ili kufaidi matunda yatokanayo na shughuli zao za uchimbaji na vilevile kutoa ushirikiano kwa Ofisi ya Madini kwa lengo la kuboresha shughuli zao.
source: Mohamed Saif


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO