TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vitendo vya uhalifu na uvunjaji wa haki za binadamu vinavyoendelea kufanyika Zanzibar, hususan kisiwani Pemba.

Kwa muda mrefu sasa hivi tokea kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na hasa baada ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa Marejeo Zanzibar tarehe 20 Machi, 2016 kumekuwapo vitendo vya uhalifu na uharibifu wa mali, ikiwemo kukata vipando mbalimbali yakiwemo mazao ya muda mrefu na mfupi. Vilevile kumefanyika vitendo vya hujuma ikiwemo kuchoma moto nyumba katika baadhi ya makazi ya watu Kisiwani Pemba.

Aidha kumekuwepo na taarifa za matukio kama vile migomo takriban maeneo mengi ya Mikoa ya Pemba na baadhi ya maeneo katika kisiwa cha Unguja, yenye kuashiria vitendo vya kubaguana, kwa maana ya kutoshirikiana katika shughuli za kijamii na huduma za kijamii. Kwa mfano baadhi ya watu wananyimwa usafiri katika magari, kususiwa harusi, maziko na nyumba za ibada. 

Vitendo vya kukata na kuharibu mali, ikiwemo kuchoma nyumba moto ni kinyume na haki za binadamu kwani kila mtu ana haki ya kumiliki mali kama ilivyoelezwa katika Ibara ya 24(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na Kifungu cha 17 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Kuwanyima watu huduma ya aina yoyote katika jamii ni kinyume na misingi ya haki za binadamu, hasa haki ya kutobaguliwa kama ilivyoelezwa katika ibara ya 12 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na Kifungu cha 11 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Vitendo vyote hivyo vinaathiri shughuli za kijamii na kiuchumi pia ni kinyume na haki za binadamu kwa mujibu wa Katiba na Sheria.

Tume pia imepata taarifa kuwa tofauti za itikadi za kisiasa zinasababisha ndoa kuvunjika kutokana na wanawake kuadhibiwa kwa kupewa talaka kutokana na kutotii amri za waume zao za kuwazuia kushiriki uchaguzi wa marejeo.

Kifungu cha 21(1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kama ilivyorekebishwa mwaka 2010 kinaeleza kuwa, “kila Mzanzibari anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kupitia wawakilishi waliochaguliwa kwa hiari”. Haki hii haitakiwi kuingiliwa na mtu yeyote, kwani ni haki inayotambua uhuru na utu wa kila mwanadamu kuamua yeye mwenyewe kushiriki au kutoshiriki katika shughuli za kisiasa, awe mwanamume au mwanamke.

Aidha Kifungu cha 21(2) cha Katiba ya Zanzibar kinatamka kuwa ”kila Mzanzibari anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu wa mambo yanayomuhusu yeye maisha yake au yanayolihusu Taifa”.

Wakati Tume ikiyasema haya, inapenda kutamka kwamba imeshangazwa na kusikitishwa  na tamko la Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar kuhusu kuwakataza Mawakili kuwawakilisha watuhumiwa katika kesi zinazotakana na uvunjifu wa amani Zanzibar, au makosa yanayoashiria kufanyika kwa msukumo wa kisiasa. Zuio hilo la mawakili ni batili,  kwani ni kinyume na misingi ya haki za binadamu, na misingi ya haki sawa, yaani (fair trial principles,) ambayo inatamka kwamba kila mtu hatotiwa hatiani mpaka ikithibitika hivyo,(presumption of  innocence until proven guilty), au kila mtu ana haki ya kuwakilishwa mahakamani (right of legal representation).

Tume inatamka kwamba matamko hayo hayaendani na dhana ya utawala wa sheria na utawala bora, ambapo kila taasisi, na kila mtu anatakiwa kutenda kazi zake kwa kuzingatia Katiba, yaani Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na Sheria ya mwenendo wa Makosa ya Jinai ya Zanzibar, Namba 7 ya mwaka 2004, pamoja na Mikataba ya Kimataifa hasa Mkataba wa haki za kisiasa na kiraia wa mwaka 1966 ambao Tanzania imeridhia.

Ibara ya 13(6) Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 na kifungu cha 12(6), ya Katiba ya Zanzibar 1984 zinaweka miongozo ya usimamizi wa haki, ambayo ni pamoja na mtu kupewa haki ya kusikilizwa kwa ukamilifu, wakati wa upelelezi na uendeshaji wa kesi za jinai, na wakati mtu anapokuwa chini ya ulinzi, utu wake utaheshimiwa, zinapiga marufuku mateso au adhabu za kinyama au zinazomtweza au kumdhalilisha mtu.

Kifungu cha 41 cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai 2004, kinampa haki Wakili aliyesajiliwa na Mahakama Kuu chini ya Sheria ya Legal Practitioners Decree Cap. 28 kumuwakilisha au kumshauri mtu yeyote anayetuhumiwa au kushtakiwa kwa kosa lolote.

 Tume inasisitiza kuwa mamlaka zote zenye kusimamia upelelezi na kuendesha mashtaka zitekeleze kazi zake kwa weledi na kuheshimu matakwa hayo ya Katiba na sheria.

Tume inapendekeza kwamba ili hali ya maelewano irudi kama ilivyokuwa hapo awali kisiwani Pemba na Zanzibar kwa ujumla, panahitajika hatua za makusudi zitakazo leta maelewano  katika jamii. Tume inashauri yafuatayo:-

(i)            Hatua za makusudi na haraka zifanyike kwa Viongozi wa Kitaifa na wa vyama vyote vya siasa vikiwemo  CUF na CCM wakae pamoja kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa suluhisho la kudumu litakalozuia matatizo ya uvunjifu wa amani  kujirejea.

(ii)          Taasisi zinazosimamia ulinzi na usalama, hususan Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola, ziwe makini katika kufanya kazi zake kwa kufuata misingi ya utawala bora, haki za binadamu na utawala wa sheria ili kuepukana na madhara yasiyotarajiwa katika jamii.

(iii)         Wananchi wote wanatakiwa kutii sheria za nchi, na kutojiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa amani na usalama.


SIGNED
Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO