Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla akitoa neno la shukurani mara baada ya kukabidhi mifuko 150 ya saruji iliyotolewa na kampuni ya Lafarge Tanzania, kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Mahusiano na Masoko wa Lafarge Allan Chonjo, kulia ni Diwani wa kata ya Mpuguso.

Lafarge Tanzania (Mbeya Cement Company), imetoa msaada wa mifuko mia moja hamsini (150) ya saruji ya Tembo ikiwa ni msaada wake kuchangia ujenzi wa kituo cha afya cha kijiji cha Mpuguso kilichopo wilayani Rungwe mkoa wa Mbeya.
Akiongea wakati wa makabidhiano ya msaada huo, Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa Lafarge, Allan Chonjo amesema “Lafarge Tanzania inaelewa kwamba afya ndio kitu cha thamani zaidi katika maisha ya binadamu na kwa sababu hiyo tumeona ni wajibu wetu kuchangia maendeleo ya jamii hii ambayo tunayoishi. Tunasaidia ujenzi wa kituo cha afya Mpuguso kwakuwa tunaelewa kwamba afya njema ndio msingi muhimu wa jamii kuweza kupata maendeleo.”
Chonjo alisema kwamba kampuni hiyo ya saruji inaamini kuwa biashara ni kipaumbele chake lakini inaamini kwamba kusaidia jamii ni jukumu lake la msingi. Msaada huo uliopokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kijijini Mpuguso leo ni sehemu programu ya Lafarge Tanzania kusaidia jamii na umelenga kuhakikisha ujenzi wa kituo hicho kinachojengwa na wananchi unakamilika mapema ili kuboresha utoaji huduma za afya katika eneo hilo.
Akipokea msaada huo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla alielezea kufurahishwa kwake na Lafarge katika kuitikia wito wa wananchi haraka na kutoa msaada huo. Mkuu huyo wa mkoa aliwahakikishia Lafarge kwamba msaada huo utatumika ipasavyo kukamilisha mradi huo ili kuboresha maisha ya watu na kuongeza kwamba kituo hicho kitahudumia maelfu ya wakazi wa Mpuguso na maeneo ya jirani ambapo kituo cha karibu zaidi cha afya kipo umbali wa takribani kilomita 60 kutoka eneo hilo.   
Makalla alisema kwamba baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho, wakazi wa Mpuguso na maeneo ya jirani watapata huduma za msingi za afya ambazo ni pamoja na ushauri wa kitabibu, msaada wa madawa, utoaji chanjo kuzuia magonjwa mbalimbali pamoja na kutoa ushauri nasaha kuhusu afya.
MWISHO

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO