Waziri wa Nishati na Madini na  Mbunge wa Musoma Vijiini,  Profesa Sospeter Muhongo (mwenye koti la Bluu) akiwa na wananchi wa Kata ya Nyakatende wilayani  Musoma na Ujumbe wa Madaktari Bingwa kutoka China waliofika katika Zahanati ya Nyakatende   ili kutoa matibabu ya bure kwa wananchi.


Madaktari Bingwa kutoka nchini China   wametoa  huduma ya matibabu kwa wananchi mbalimbali katika Zahanati ya Nyakatende, Jimbo la Musoma Vijijini ikiwa ni mwaliko wa Mbunge wa Jimbo hilo ambaye pia ni  Waziri wa  Nishati na Madini,  Profesa Sospeter Muhongo.
Hii ni Awamu ya Tatu kwa Madaktari hao kutoa huduma hiyo ya matibabu wilayani  Musoma ambapo huduma kama hiyo ilitolewa mwezi Juni na Machi mwaka huu.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Nyakatende kabla ya kuanza kwa matibabu hayo, Profesa Muhongo alisema kuwa  matibabu na dawa hizo ni za bure hivyo wananchi wasisite kutibiwa.
“ Lengo letu ni kuhakikisha kuwa wananchi waliopo vijijini wanapata huduma bora za afya, maji, elimu,  miundombinu na umeme,  ndiyo maana hata hapa nimewaletea gari  ndogo ya wagonjwa ili iwasaidie katika kupata matibabu,” alisema Profesa Muhongo.
Madaktari hao wamebobea katika kutibu magonjwa mbalimbali kama ya Wanawake, Watoto, Meno, Vinywa, koo, macho, kisukari, presha, tumbo na kufanya upasuaji.
Aidha Ujumbe wa Madaktari hao wanaojitolea, walikabidhi vifaa kama kalamu,  vitabu vya Sayansi, Hisabati, Maarifa ya Jamii,  mipira na madafrari vyenye jumla ya shilingi milioni 4 ambavyo viligawiwa kwa shule mbalimbali za Msingi  na Sekondari wilayani humo.
Akiwa katika Zahanati hiyo Profesa Muhongo alichangia mifuko100 ya simenti na  mabati 100 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na choo cha wafanyakazi wa kituo hicho.
Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge wa  MusomaVijijini,  Profesa Sospeter Muhongo (mwenye koti la Bluui) akiwa  na Ujumbe wa Madaktari Bingwa kutoka China ambao walifika wilaya  ya Musoma  ili kutoa matibabu ya bure kwa wananchi  katika Zahanati ya Nyakatende .

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Musoma, Flora Yongolo  alimpongeza Profesa Muhongo kwa juhudi mbalimbali anazofanya katika Jimbo la Musoma vijijini  hasa katika kuboresha elimu, afya na kilimo huku akitolea mfano ugawaji wa madawati na vitabu mashuleni na kilimo cha majaribio cha zao la alizeti ambacho kimeonyesha matokeo mazuri baada ya Profesa Muhongo kugawa bure mbegu hizo za alizeti kwa wakulima.
Aidha,  Yongolo alisema atahakikisha kuwa vifaa ambavyo Profesa Muhongo amevitoa katika Jimbo hilo  kama madawati na  gari Tano za kubebea wagojwa,  vinatunzwa na kulindwa ambapo alitoa wito kwa wananchi na watendaji wa shule na vituo vya afya kuhakikisha hilo linafanikiwa.
Awali Profesa Muhongo alisema kuwa vitabu alivyogawa jimboni humo vimeletwa na Rafiki zake kutoka nchini Marekani ambapo thamani ya vitabu hivyo ni Dola za Marekani 250,000.
Kuhusu zao la alizeti, Profesa Muhongo alisema kuwa wakulima watakaolima na kuvuna zao hilo kwa mafanikio, watanunuliwa mashine ndogo za kukamua alizeti ili waweze kuuza mafuta ya alizeti na kujiongezea kipato.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO