WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa mkoa wa Dodoma pamoja na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kutenga eneo la b...
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa ameutaka uongozi wa mkoa wa Dodoma pamoja na Mamlaka ya Ustawishaji
Makao Makuu (CDA) kutenga eneo la bandari kavu ili mkoa huo uweze kupokea
na kuhifadhi mizigo na kurahisisha biashara kwa mikoa jirani.
Ametoa agizo hilo leo
jioni (Jumatano, Julai 20, 2016) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mkoa
wa Dodoma mara baada ya kuweka jiwe la msingi kuashiria uzinduzi wa awamu ya
kwanza ya ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dodoma.
"Ninazo taarifa kiwa
Benki ya Dunia kupitia shirika la Local Investment Climate (LIC) tayari
wametenga fedha kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kujenga
bandari kavu na tayari fedha hizo zimeshapokelewa na Mkoa wa Dod
“Uzuri wa mkoa wa Dodoma
kuna reli. Kwa hiyo makontena yanayoenda Burundi na mahali kwingine
yatashushwa hapa na kukaa kwenye bandari kavu; hivyo, wafanyabiashara
watachukua mizigo yao hapa badala ya kupata shida ya kuyafuata Dar es Salaam
kama ilivyo sasa,” amesema.
Waziri Mkuu ameitaka
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano itoe wataalam ili washirikiane na CDA
kufanikisha kazi hiyo. Amesema hatua hiyo itasaidia kurahisisha wananchi na
wafanyabiashara kupata huduma hiyo kwa urahisi na umbali mfupi tofauti na hali
ilivyo sasa.
Ameuagiza pia uongozi wa
CDA utenge eneo maalum la kituo cha biashara (commercial hub)) ili Kanda zote
zinazozunguka mkoa wa Dodoma na nchi jirani wapate bidhaa mbalimbali kutokea
Dodoma. “Kutokana na upanuzi huu na fursa zinazojitokeza, hii iende sambamba na
kuwatengea maeneo maalum wajasiriamali badala ya kuwaacha kuzagaa kila mahali,”
amesisitiza Waziri Mkuu.
Akizungumzia kuhusu
upanuzi wa uwanja huo, Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa mradi huo
kutaziwezesha ndege zenye uwezo wa kubeba abiria 90 zianze kutua kwenye kiwanja
hicho na kukuza fursa za kibiashara zinazohitaji usafiri wa haraka na salama.
“Katika Ilani ya
CCM, suala la ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya viwanja vya ndege limepewa
umuhimu mkubwa sana na ndiyo maana leo tunashuhudia utekelezaji wa ahadi za
Mheshimiwa Rais ambaye amewezesha upatikanaji wa fedha za ukarabati na fidia
kwa wananchi wa kata za Makole na Uwanja wa Ndege ambao maeneo yao yametwaliwa
na Serikali ili kufanikisha upanuzi huu,” amesema.
Amesema uzinduzi huo
ni mwanzo tu wa utekelezaji
wa miradi mingine ya kuboresha na kupanua viwanja vya ndege nchini ambapo
Serikali kwa kutumia vyanzo vyake vya mapato ya ndani na ya nje, itaendelea
kuboresha zaidi miundombinu na huduma nyingine za viwanja vya ndege kama vile
Mtwara na Mwanza ambavyo amesema vitapanuliwa kufikia hadhi ya kimataifa.
Ameitaja
miradi mingine kuwa ni viwanja vya ndege vya Kigoma na Tabora ambavyo
vinaendelea kupanuliwa kwa kujenga majengo ya abiria na maegesho ya ndege ili
kufikia viwango vya huduma za kimkoa; viwanja vya Shinyanga na Sumbawanga
vitapanuliwa kwa kuboreshwa miundombinu na majengo yake kufikia hadhi ya
viwanja vya kimkoa; huku kiwanja cha ndege cha Lindi kikiboreshwa miundombinu
yake kufikia hadhi ya kimkoa na kuweza kuhudumia viwanda vinavyotokana na
uchumi wa mafuta na gesi.
Amesema Serikali
itaendelea kukamilisha ujenzi wa jengo la tatu la abiria (Terminal 3) katika
kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) ambalo
likishakamilika Desemba 2017 litahudumia abiria wapatao milioni 6 kwa mwaka;
ilhali kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) kinapanuliwa
miundombinu yake na jengo la abiria ili kiweze kuhudumia abiria
milioni 1.2 kwa mwaka.
Akimkaribisha Waziri
Mkuu kuhutubia hadhara hiyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof.
Makame Mbarawa ameiomba Serikali iendelee kuwekeza katika ujenzi wa uwanja wa
ndege wa Msalato ili ndege za kimataifa ziweze kutua kwenye mkoa huo.
Mapema, akitoa
taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Dk. Leonard Chamuriho amesema Serikali imetoa sh. bilioni 11.8 kwa
ajili ya kazi hiyo na kwamba hadi sasa wamekamilisha asilimia 60 ya ujenzi kwa
kuweka lami umbali wa km.2.0 kati ya km.2.5 zinazohitaji kukamilishwa chini ya
mradi huo.
Amesema hivi sasa ndege zinazoweza kuruka na kutua
kwa umbali huo zinaweza kuanza kutoa huduma kwenye uwanja huo wakati
wakiendelea kukamilisha ujenzi wa mita 500 zilizobakia.
Kwa upande wake, Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Eng. George Sambali alisema ukarabati huo ulianza Juni
24, 2016 na imechukua siku 27 hadi sasa, kazi ambayo
alisema inawezesha kiwanja kutumika kwa ndege zenye uwezo wa kubeba
abiria hadi 90 na zenye mwendo wa kasi. Hata hivyo, alisema kazi iliyobakia
inatarajiwa kukamilika baada ya miezi miwili.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATANO, JULAI 20, 2016.
COMMENTS