KUGOMBEA UENYEKITI WA CHAMA CHA WANANCHI CUF.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Kutoka kwa Mwanachama mwandamizi wa Chama Cha Wananchi CUF,
Julius Sunday Mtatiro.
09 Julai 2016

Ndugu zangu,
Napenda kutumia fursa hii kuwatakia mapumziko mema baada ya sherehe za Iddi. Hata hivyo ninalo jambo muhimu ambalo ningependa kuliweka wazi. Kwa kipindi kirefu sana kumekuwa na msukumo mkubwa kutoka kwa viongozi wa chama ngazi za wilaya, wajumbe wa mkutano mkuu, wabunge, madiwani, wanachama wa kawaida, wafuasi na wapenzi wa kada mbalimbali kunitaka nishiriki katika kinyang'anyiro na hatimaye kuchukua nafasi ya Mwenyekiti wa chama. Misukumo hiyo ni mikubwa kiasi cha kutoelezeka.
Misukumo hiyo pia imetoka kwa wananchi na wanaharakati mbalimbali ambao wanaunga mkono mabadiliko. Ni jambo la kujivunia sana unapoungwa na kiaminiwa na watu wengi, ndani na nje ya chama chako, katika jambo lolote lile hasa kuwania nyadhifa za uongozi. Naahidi kuwa ntaendelea kulinda tunu zote ambazo zinawafanya wanachama na watanzania wenzangu waone kuwa ninazo sifa na vigezo vya kushikilia wadhifa mkubwa kiasi hicho.
Katika kipindi chote cha misukumo hiyo nimekuwa nikiwajibu wahusika wote kuwa "sina nia ya kuchukua uongozi wa juu wa chama" kwa sababu bado nahitaji muda wa kujiimarisha katika maeneo mbalimbali ya maisha huku nikizidi kujenga "uandamizi" katika siasa za nchi na chama changu.
Leo nitoapo taarifa hii, mbio za kuchukua fomu zimenoga na najulishwa kuwa wapo wanachama wamekwishajitokeza kwa ajili hiyo na wengine wengi wanaendelea, hilo ni jambo kubwa na la kujivunia sana.
Kwa sababu mibinyo na misukumo imekuwa mikubwa sana, kupita kiasi, siyo vema nikaendelea tu kuwajulisha wale tu wanaonifikia, kwamba sina nia ya kugombea nafasi hiyo, bali ni vema nikajulisha jamii nzima ya CUF na watanzania wote, kwamba hadi leo SIJAWA NA NIA YA KUCHUKUA MAJUKUMU YA UENYEKITI WA CHAMA CHA WANANCHI CUF na wala SOTACHUKUA FOMU KWA AJILI HIYO. Naomba tamko hili lifute misukumo, tetesi na kila aina ya taarifa kwamba ninayo nia au nitakuwa na nia hiyo.
Niliposimama hadharani kushauri kuwa Mwenyekiti Mstaafu wa CUF (namheshimu sana), Prof. Lipumba, anapaswa kupumzika uongozi na kusitisha nia yake ya kurudi kwenye nafasi aliyoondoka mwaka mmoja uliopita, wapo watu walitumia uhuru wao kueleza kuwa simtaki Prof. Lipumba kwa sababu nautaka uenyekiti wa CUF, watu hao watakumbuka niliwajulisha kwamba sina nia wala sijawahi kufikiria kugombea nafasi hiyo kubwa katika siasa za CUF na Tanzania kwa ujumla.
Huo ndiyo umeendelea kuwa msimamo wangu hadi leo, kwa mambo yote mawili, kwamba sitogombea nafasi ya UENYEKITI na siungi mkono Mwenyekiti mstaafu kurudi kwa sababu siasa za Tanzania zinakokwenda zinahitaji viongozi wapya, damu tofauti na wanaoweza kutizama mambo kisasa zaidi na kwa mahitaji ya kizazi cha sasa zaidi. Na kwa sababu Prof. Lipumba anayo heshima kubwa kwa CUF na watanzania, ni muhimu zaidi ailinde heshima na abaki kuwa mshauri mkuu wa chama.
CUF ya sasa inahitaji kuwa na mwenyekiti imara, anayeweza kukisimamia chama na kikajijenga lakini pia mwenye uwezo na ushawishi wa kufanya siasa za ushirikiano wa haki "A Fair Coalition" wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020. Hapa nina maana kuwa anahitajika mtu mwenye upeo mzuri wa kuweza kuilinda CUF lakini akiwa muwazi, mkweli na anayeamini katika ushirikiano wa vyama vya upinzani kama silaha mojawapo ya mapambano dhidi ya CCM.
Baada ya kueleza masuala haya, napenda kutumia fursa hii kuwatakia kila la heri wanachama wote ambao wanaendelea na uchukuaji fomu, bila shaka miongoni mwao tutapata mwenyekiti mzuri kwa ajili ya kukiendeleza chama miaka ijayo. Jukumu langu kama mwanachama mwandamizi ni kuendelea kukisaidia chama changu kiushauri na katika masuala yote muhimu yatakayokuwa yanahitaji "professionalism" kama ambavyo nimekuwa nikifanya.
Nitabaki kuwa mwana CUF imara, ninayejitambua na ambaye nilijiunga katika chama hiki baada ya kuvutiwa na kuamini sera na itikadi. Kamwe, sitakuwa mwanachama ambaye alijiunga na chama ili kumfuata kiongozi au mtu fulani. Katika hili naomba misimamo yangu iheshimiwe kama ambavyo mimi pia nimekuwa nikiheshimu mitizamo ya watu wengine.
"Naitakia CUF mkutano Mkuu Mwema na kila la heri kwa viongozi wote wapya".
"MUNGU IBARIKI TANZANIA, KIBARIKI CHAMA CHA WANANCHI CUF na MFUNULIE RAIS JOHN POMBE MAGUFULI KUWA KUZUIA SHUGHULI ZA VYAMA VYA SIASA NI KUJARIBU KUIINGIZA NCHI YETU KWENYE MIGAWANYIKO, MIVUTANO NA HATA MACHAFUKO"
Julius Sunday Mtatiro, Dar Es Salaam.
Jumamosi, 09 Julai 2016,
+255787536759 (Ujumbe mfupi na Whatsup tu),
juliusmtatiro@yahoo.com (Barua Pepe).

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO