Wataalamu wakishangilia baada ya ripoti kufika kwamba Juno imefanikiw akuingia katika mzingo wa Jupiter
BAADA ya safari ya miaka mitano , chombo cha anga za juu , Juno, kimefanikiwa  kupita katika nguvu za mvutano na kuingia katika mzingo wa moja ya sayari kubwa katika mfumo wa jua ambamo dunia yetu imo, Jupiter.
Chombo hicho kilichorushwa na  Shirika la Utafiti wa Anga za juu la Marekani (NASA) 2011,kilitumia dakika 35 kukabiliana na nguvu za mvutano kwa kuwasha roketi ili kuipunguzia kasi na kuiweka katika nguvu za mvutano za sayari hiyo ili iweze kujiweka katika mzingo wake.
Taarifa kwamba kazi ya kuingia katika mzingo wa Jupiter imekamilika kwa ufanisi ilifikia dunia Jumatatu Julai 4,saa mbili na dakika 53 usiku kwa majira ya Marekani.
Ilikuwa ni vifijo na nderemo kubwa katika vyumba vya kuongozea safari hiyo yenye lengo la kuongeza maarifa ya dunia kuhusu sayari hiyo kubwa ambayo inaaminika kwamba imetengenezwa kwa gesi.
Mtawala wa NASA, Charlie Bolden akielezea furaha yake amesema kwamba siku ya Uhuru wa Marekani imekuwa na maana kuwa zaidi hasa baada ya kufanikiwa kufikisha chombo hicho katika eneo lililokusudiwa tena ufanisi mkubwa.
Anasema Marekani imeweza kufika eneo ambalo mwanadamu hajawahi kufika na kwamba Juno itatumika kuchunguza namna sayari hiyo ilivyoumbwa na kutokea na pia mifumo yake ya ndani.
Uthibitisho kwamba safari imefikia mwisho wake kwa ufanisi mkubwa zilifikishwa katika maabara za NASA za Jet Propulsion Laboratory (JPL) mjini Pasadena, California, katika kituo cha  Lockheed Martin huko Littleton, Colorado. Na data nyingine zilipokelewa na kituo cha kuangalia anga za juu cha  vilivyoko Goldstone, California, na Canberra, Australia.
Scott Bolton,Mtafiti mwandamizi wa Juno kutoka taasisi ya utafiti ya Southwest mjini San Antonio alisifia mwenendo wa chombo hicho na wataalamu wake na kusema kwamba Jumatatu ilikuwa siku muhimu sana kwao na kwa dunia baada ya chombo hicho kuingia katika anga la Jupiter. Awali kulikuwa na shaka kwamba kunaweza kutokea kasoro hasa wakati wa kuwasha roketi ili kupunguza kasi ya chombo hicho kukiwezesha kudakwa na  nguvu ya mvutano ya Jupiter.
Matukio ya awali  yanayohusu marekebisho katika mkito wa injini na mwelekeo wa chombo hicho kukielekeza eneo lililokusudiwa yalifanyika kwa ufanisi kama ilivyokusudiwa na chombo kilijiweka sawa katika utaratibu uliokusudiwa baada ya mapigo yake kuongezwa kutoka mzunguko wa mbili kwa dakika (RPM) hadi tano ili kuifanya iwe na mtengamano.

taswira ya chombo hicho
Hatua za marekebisho zilizoanza saa 2 na dakika 18 ili kuiwezesha kupunguza kasi yake kufikia maili 1,212 kwa saa sawa na mita 542 kwa sekunde ili kuiwezesha kuingia katika mzingo wa Jupiter. Baada ya kukamilika kwa tukio hilo Juno ilielekezwa upande wa jua kwa lengo la kuchaji betri 18,697 za jua zilizowekwa ambazo ndio chanzo cha nishati yake.
Kiongozi wa mifumo ya uendeshaji ya chombo hicho, Rick Nybakken kutoka maabara ya JPL  alisema kwamba  taratibu zilizopangwa za kudhibiti chombo hicho zimeenda salama na kwamba kitendo cha kuiweka katika mzingo wa Jupiter ni jambo la kujivunia sana.
Alisema hata hivyo kuna mambo kadhaa yanatakiwa kutekelezwa kabla ya kuruhusu wanasayansi kuanza kupokea takwimu za kuzifanyia uchambuzi.
Katika miezi michache ijayo wataalamu wa Juno na wanasayansi watafanya majaribio ya mwisho katika mifumo ya chombo hicho na kufanya makadirio mapya ya vifaa vya sayansi vilivyomo katika chombo hicho ambavyo vitasaidia kukusanya takwimu na kuzileta duniani.
Alisema kwamba ukusanyaji wa data utaanza Oktoba mwaka huu lakini kuna mengi ya kuyaangalia katika sayari hiyo kubwa kuliko zote.
Kazi kubwa ya chombo hicho ni kuelewa uasili wa sayari hiyo na mageuko yake ya muda mrefu. Ikiwa na seti 9 za vifaa vya sayansi Juno itatafiti  kiini cha sayari hiyo kama ni kigumu au gesi, kuratibu na kutengeneza ramani ya ugasumaku, kupima kiwango cha maji na gesi ya ammonia katika angahewa na kuangalia miduara ya sayari hiyo.
Pia  chombo hicho kitaweza kuleta takwimu ambazo zinaweza kuelezea namna ambavyo sayari kubwa zilivyoanza na namna zinavyosaidia kuweka mfumo wa jua pamoja kama ulivyo sasa. Pia  chombo hicho kinatarajiwa kusaidia kujua mifumo mingine ya jua inakuaje. Wataalamu wamekuwa wakiamini kwamba  mfumo wa sayari hiyo na kemia yake kutasaidia sana kujua namna gani sayari hiyo imejitengeneza takaribani miaka bilioni 4 na nusu iliyopita.
Hakuna chombo ambacho  kimewahi kupita karibu na  Jupiter kutokana na mnururisho wake ambao huharibu vifaa vyote vya kielektroniki kama hakuwekewa kinga ya kutosha.
Juno ambayo ilirushwa angani Agosti 5,2011 kutoka uwanja wa jeshi la anga la Marekani  Cape Canaveral huko Florida, mtengenezaji wake ni Lockheed Martin Space System.
Chombo hicho kilitengenezwa mithili ya tangi la maji kikihamiwa na  madini ya titanium kuzuia minururisho hiyo mikali. Ingawa wataalamu wamesema kwamba hatari bado haijaisha , kinatakiwa sasa kuanza kujiandaa kufanyakazi iliyokifikisha pale.
Kwa kuingia katika mzingo wa sayari hiyo Juno imejiweka katika duaradufu (umbo la yai) unaokamilika katika siku 53.
Uwashaji wa injini nyingine utafanyika katikati ya Oktoba na kuiweka Juno katika mzingo wa siku 14 na ni katika hali hiyo masuala ya utaalamu wa kisayansi yataanza.Mzunguko huo utafanyika mara kadhaa ikiwa ni  chini ya mawingu.
Katika kila mzunguko wa kuielekeza katika uso wa sayari Juno itatumia  vifaa  vyake pamoja na kamera kukusanya takwimu kupima joto, mwendo na mchanganyiko.Pia  kutaangaliwa kiwango cha Oksijeni katika sayari hiyo na itaonwa katika maji yaliyopo katika sayari hiyo.
"Kiwango cha maji kitatoa taarifa kuhusu sayari imejitengenezea wapi wakati wa kuundwa kwa mfumo wa jua,"  anasema mmoja wa timu ya wanasayansi Candy Hansen.
"Tunaamini kwamba Jupiter  haikutengenezwa mahali ilipo leo na kama ilitengenezwa mbali zaidi, itatupa mwanga namna mfumo wa jua ulivyojitengeneza. Hii inatokana namna tunavyoangalia mfumo mingine ya jua tunaona uwezekano."
Taasisi ya Nasa imesema chombo hicho kinatarajiwa kufanyakazi hadi Februari 2018 kama kutakuwa hakuna uharibifu wa vifaa vya elektroniki, kunakosababishwa na minururisho hatari kutoka kwenye sayari hiyo hata hivyo ufanyakazi wa kamera unatarajiwa kufa katika kipindi cha miezi michache.
Maisha ya chombo hicho yataisha wakati itakapoamriwa kujiachia moja kwa moja katika uso wa Jupiter ili kuzuia Juno kwenda kuvuruga moja ya miezi inayozunguka sayari hiyo ambapo mmoja Europa inaaminika kuna uhai.
Sifa ya sayari hii zinazojulikana ni pamoja na:
•    Jupiter ni pana mara 11 zaidi kuliko dunia na  masi (tungamo) ni mara 300 ya dunia
•    Sayari hiyo inachukua miaka 12 ya duniani kuzunguka jua na siku yake ni saa 10
•    Mchanganyiko wake wa madini ni kama Nyota (jua); sehemu kubwa ni gesi ya hydrogen na helium
•    Kwenye shinikizo kuwa kimiminika cha hydrogen , mkondo wake unapitisha umeme
•    Inaaminika kwamba  ugasumaku ya sayari hii inatokana na hydrogen  ya metali
•    Maeneo yanayoonekana katika anga hewa yanaonekana mawingu yana ammonia na hydrogen sulphide
•    Eneo kubwa Jekundu linaoonekana kama spoti ni kimbunga kikubwa kama dunia

Imeandikwa na BEDA MSIMBE kwa msaada wa taarifa za NASA na BBC


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO