Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo kulia na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda Mhandisi Irene Mukoni wakisaini makubaliano ya Kikao kuhusu utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Kabaale nchini Uganda hadi Tanzania mbele ya Waandishi wa Habari katika Kikao kilichofanyika Hoima Uganda tarehe 5 Julai, 2016 ambapo walijadili maendeleo ya mpango kazi wa Bomba hilo la kusafirisha mafuta ghafi

Vikao vya utekelezaji mradiwa bomba la mafuta kutoka Kabaale nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchiniTanzania vilianza kwa wataalam wa nchi hizo mbili kufanya kikao Julai 4,2016 kabla ya kikao cha Mawaziri wa nchi husika.

Wataalam waliohudhuria kikao hicho kwa upande wa Tanzania walitoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Pia, kwa upande wa Uganda waliwakilishwa na Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini, Wadau wa sekta ya Nishati kutoka Idara mbali mbali za Serikali na Wawekezaji kampuni za Total, CNOOC na Tullow.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema kuwa vikao vya tarehe 5 Julai, 2016 vilikuwa vya mafanikio makubwa yakiwemo Kampuni ya CNOOC (China) na TULLOW (UK) kukubali kushiriki kwenye ujenzi wa Bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,443.

Alisema kuwa hapo awali Makampuni hayo yalikuwa yakiunga mkono Bomba hilo la mafuta kupita Kenya, na kueleza kuwa kwa uamuzi huo, Timu ya ujenzi wa Bomba imekamilika huku bomba hilo likipewa jina la East African Crude Oil Pipeline (EACOP).

Profesa Muhongo alisema kuwa wakiwa nchini Uganda mnamo tarehe 06 Julai, 2016 walitembelea eneo la Ziwa Albert na kujionea visima vilivyochorongwa tayari kwa uzalishaji wa mafuta ghafi (crude oil) ambapo makisio ni uwepo kwa mapipa
bilioni 6.5 (reserve) na yanayoweza kuchimbwa ni mapipa Bilioni 2 (recoverable).

“ Bomba hili la mafuta litakuwa na Gharama ya Dola za Marekani Bilioni 3.55 na litakuwa na urefu wa kilomita 1,443 ambapo litasafirisha mapipa 200,000 kwa siku,” alisema Profesa Muhongo.

Aidha, Profesa Muhongo alisema kuwa Serikali ya Uganda itajenga kiwanda cha kuchakata mafuta hayo katika eneo la Kabaale na Ujumbe kutoka Tanzania ulitembelea eneo la ujenzi huo.

Vilevile alisema kuwa Serikali ya Uganda imetoa jumla ya asilimia 40 ya hisa za kiwanda hicho cha kuchakata mafuta kwa Serikali 5 za Afrika Mashariki (kabla ya Sudan Kusini kujiunga), Hivyo, Tanzania imetengewa na kukaribishwa kununua
asilimia 8 za hisa zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 150.4. Ili kufanikisha ununuaji wa hisa hizo, Profesa Muhongo alitoa wito kwa Serikali na Sekta Binafsi kushirikiana.
SOURCE; MEM WEEKLY NEWS

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO