Waziri Mkuu  akisalimiana na Dk Mary Mgonja viwanja vya Mwakangale


. Kwa miaka 10 imetumia dola za Marekani milioni 51 kuendeleza kilimo

TAASISI ya Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA)  imetoa wito kuwapo kwa matumizi zaidi ya teknolojia kwa wakulima wadogo ili kuwa na uhakika na usalama wa chakula huku wakiingiza ziada katika soko. 
Mtendaji wa taasisi hiyo nchini Tanzania Dk Mary Mgonja alisema hayo akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya wakulima ya nanenane katika viwanja vya John Mwakangale mjini hapa hivi karibuni. 
Katika mkutano huo taasisi zinazoshirikiana na AGRA katika kuleta mabadiliko kwa wakulima zipatazo 10 zilikuwapo.
Dk Mgonja alisema ana matumaini makubwa na hali ya baadae ya kilimo nchini Tanzania na kuongeza kwamba matumizi zaidi ya teknolojia ndio njia pekee ya kuwainua mamilioni ya wakulima wadogo kutoka katika lindi la umaskini.
“Tanzania kuanzia mwaka 2006 imekuwa ikipewa kipaumbele na AGRA na kwamba miradi 96 imepewa ruzuku inayofikia dola za Marekani milioni 51,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk Mgonja ruzuku hizo zimetoa mchango mkubwa katika kukabiliana na changamoto za wakulima wadogo katika mnyoror wa thamani wa shughuli zao kuanzia masuala ya mbegu, udongo, soko, sera hadi fedha.
Sehemu ya uwekezaji huo imezaa matunda kwa kupata aina tofauti za mbegu zilizoboreshwa kukabiliana na hali za maeneo; matumizi sahihi ya mbolea; utunzaji baada ya mavuno; teknolojia ya hifadhi za nafaka na ubunifu wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuinua kilimo.
“Ninatoa wito kwa wakulima kukumbatia njia mpya za teknolojia katika kilimo ili kupata tija zaidi ;kuanzia matumizi ya mbegu bora zilizoboreshwa  mashambani hadi kwenye matumizi ya teknolojia mpya ya kuhifadhi mavuno; Njia hizo kama zitatumika vyema zitaongeza uzalishaji na kupunguza upotevu wa mavuno. Mambo hayo ni muhimu ili wakulima wadogo wajinasue kiuchumi,” alisema Dk Mgonja.
Tangu kuingizwa kwa teknolojia ya mifuko maalumu ya kuhifadhi nafaka na bidhaa jamii ya mikunde, kampuni tatu zinashughulika na kutengeneza hifadhi hizo, huku  zikiuzwa na kuwafikia mamia kwa maelfu ya wakulima.
Aidha Dk Mgonja  aliipongeza  serikali ya Tanzania kwa kupiga hatua kwenye kuboresha sera ya kilimo yenye lengo la kukabiliana na  changamoto za wadau mbalimbali katika sekta ya kilimo.
“AGRA itaendelea kushirikiana na wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi kuhakikisha kwamba shughuli za AGRA nchini zinakwenda sambamba na juhudi za serikali ya Tanzania katika kuboresha kilimo,” alisema Dk Mgonja.
Aidha aliongeza kwamba mchango mkubwa wa AGRA umekuwepo katika Matokeo Makubwa sasa na Kilimo Kwanza.
Alisema taasisi ambazo zilisaidiana na AGRA kuleta mapinduzi ya kilimo katika kipindi cha muongo mmoja uliopita ni  pamoja na Tanzania Seeds Trade Association (TASTA), CSDI, Equity Bank, Unyiha Associates, BRITEN, RUDI, AGROZ. Nyingine  ambazo zilikuwa ni taasisi za umma ni pamoja na ARI Uyole, Chollima AGRO, ARI Mlingano  na kituo cha SAGCOT .

Dondoo za Shuhuda

Kwa muda AGRA imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na mazingira mazuri ya biashara ya mbegu kupitia mradi wa Micro Reforms for African Agribusiness (MIRA) : Mradi huu ulizaa matunda mema kwani kuanzia Juni 2016, kumekuwepo na sera mpya ya mbegu.
 Mkurugenzi Mtendaji  Tanzania Seeds Trade Association (TASTA), Bw. Baldwin Shuma. Alieleza kufurahishwa na Sera hiyo ilitengenezwa kwa namna  pekee ambapo inaruhusu sasa makampuni ya mbegu kuzalisha mbegu ambazo zilifanyiwa utafiti na taasisi za umma.
Naye Dk Matilda Kalumuna, wa Taasisi ya utafiti wa kilimo ya Mlingano –Tanga, amesema kwamba AGRA imesaidia taasisi yake kwa kuipa ruzuku ya dola za Marekani 400,000 kusaidia kuimarisha mifumo yake ya kuangalia ubora wa mbolea.
“Kupitia mradi huu taasisi ilifundisha wakaguzi wa mbolea 100; wachambuzi 15 wauzaji pembejeo wenye uelewa 338 na wadau 8000.
Kutokana na mradi huo makampuni mbalimbali na wauzaji wa pembejeo za kilimo waliamua kwa hiari yao kujisajiri na TFRA;mbolea iliyoko sokoni inasajiliwa, kukaguliwa na kuchambuliwa kwa lengo la kuona mbolea zisizokidhi viwango zinajulikana na kuondolewa sokoni.
“Benki ya Equity Tanzania imeingia ubia na AGRA kuanzisha mfuko ambao utasaidia kununuliwa kwa vifaa vya hifadhi ya nafaka. Katika mradi wa majaribio Njombe, Morogoro na Iringa, tutatoa mikopo ya sh kuanzia milioni 5 hadi 30  ili kununua mifuko maalumu ya kuhifadhia nafaka; vihenge vya chuma na vifukofuko (cocoons), kuanzia mwezi huu,“ alisema Mkuu wa biashara ya kilimo  wa benki ya  Equity, Enesto Josephat
 Mtaalamu wa viazi mviringo Owekisha Kwigizile, kutoka kituo cha utafiti wa viazi cha SAGCOT  katika mazungumzo yake alisema: “hapa nchini Tanzania tuna aina tatu viazi mviringo zinazotambuliwa kisheria pamoja na kwamba viazi mviringo ni chakula kikuu nchini. SAGCOT na wadau wengine wa AGRA tunafanya juhudi kuongeza vipando bora zaidi ambavyo vitatoa tija kubwa na kuongeza mavuno”
mwisho

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO