Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Bahame Tom Nyanduga akitoa tamko la Tume mbele ya vyombo vya habari ...
|
TUME
YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Kitalu
Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P
2643, DAR ES SALAAM
Simu:
+255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi:
+255 22 2111281
Barua
Pepe: chragg@chragg.go.tz
Tovuti:
www.chragg.go.tz
|
Agosti 10,
2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, iliandaa mkutano leo tarehe 10/08/2016 ili
kuzungumzia tamko la Jeshi la Polisi la tarehe 07/06/2016 la kuzuia mikutano na
maandamano ya vyama vya siasa isiyo ya kiutendaji, na tamko la CHADEMA kuhusu “UKUTA”
na mikutano wanayopanga kufanya tarehe 1 Septemba, 2016.
Mkutano
huu ulihudhuriwa pia na Mhe. Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya siasa, Mhe.
Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa CHADEMA na washauri wake na Ndugu Daniel Loya, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Demokrasia
nchini (TCD).
Hivyo
mkutano wa leo ulikuwa na lengo la kuwakutanisha viongozi wa Serikali, Jeshi la
Polisi na CHADEMA na kwa pamoja kutafuta ufumbuzi wa kile Tume inachohofia kuhusu
uvunjifu wa amani, haki za binadamu na utawala bora.
Aidha
baada ya tamko la CHADEMA la kufanya maandamano nchi nzima, kumekuwa na matamko
mbalimbali kutoka kwa viongozi wa kitaifa, baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya, Makamanda
wa mikoa wa Jeshi la Polisi kukataza kufanyika kwa maandamano hayo na kwamba
watakaokiuka zuio hilo “watashughulikiwa.”
Ni
katika mazingira haya, Tume imepata wasiwasi kuwa endapo matamko haya
yataachiwa yaendelee, yana viashiria vya machafuko na uvunjifu mkubwa wa haki
za binadamu unaoweza kutokea.
Mkutano
huu kwa pamoja ulitaka kujihakikishia iwapo Tume ina mamlaka ya kujadili hoja
hizo mbili yaani kujadili zuio la maandamano na mikutano ya vyama vya siasa,
visiyokuwa vya kiutendaji na kuhusu lugha na matamshi yasiyo stahiki.
Baada
ya majadiliano Tume inapenda kutamka yafuatayo:-
1.
Wajumbe wote waliohudhuria
kikao hicho walikubaliana kuhusu umuhimu wa kudumisha amani nchini, na umuhimu
wa kuwepo majadiliano katika kutafuta maafikiano ya tofauti zozote kila mara
zinapojitokeza, na walipendekeza umuhimu wa kuendelea na majadiliano
yaliyoanzishwa na Tume.
2.
Kwamba kuhusiana na
mustakabali wa maandamano na mikutano ya vyama vya siasa ilibainika kuwa kuna
kesi mbili zilizofunguliwa na CHADEMA katika Mahakama Kuu, Masijala ya Dar es Salaam
na Mwanza na kesi zote zinaendelea. Kwa
kuzingatia Ibara ya 131 (2)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
1977, inaamini kwamba, tafsiri sahihi ya zuio lilitolewa na Polisi litapatikana
Mahakamani. Tume inaamini Mahakama itayapa
mashauri hayo kipaumbele, kama ilivyofanya wakati wa kusikiliza kesi ya mita
mia mbili hapo Oktoba, 2015 ili tafsiri yake ipatikane mapema.
3.
Pamoja na uamuzi huo wa Tume,
kwa kuzingatia mamlaka ya Tume chini ya Ibara 130 (1) (g) na (h) ya Katiba ya
nchi, kuhusu kutoa ushauri na kutafuta maelewano kati ya viongozi wa Serikali
na Jeshi la Polisi kwa upande mmoja, na uongozi wa CHADEMA, Tume inawaasa
viongozi wa pande mbili kuzingatia yafuatayo:-
(i)
Kusitisha matumizi ya lugha
au maneno yenye viashiria vya uvunjifu wa amani, haki za binadamu na utawala bora
kwani lugha hizi hazikidhi matakwa ya haki za binadamu, wala utawala wa sheria.
(ii)
Jeshi la Polisi linashauriwa lisitumie
neno “tutawashughulikia wote watakao kaidi amri”, kwa kuwa Tume inaona kuwa
maneno hayo yanaweza kusababisha matumizi mabaya ya mamlaka ya Jeshi la Polisi.
(iii)
CHADEMA warekebishe msamiati
wa mikutano wanayopanga na kuondoa neno “UDIKITETA” katika mikakati yao ya
kisiasa kwani Tanzania, ni nchi yenye taasisi za kidemokrasia na inaheshimu
utawala wa Sheria, na ndiyo sababu CHADEMA wamekwenda Mahakamani.
(iv)
Kwa kuzingatia, ukweli kwamba
kuna mashauri mawili yaliyoko Mahakamani, ambayo yatawezesha Mahakama kutoa tafsiri
ya uhalali wa zuio la Jeshi la Polisi la tarehe 7 Juni, 2016 kuhusu maandamano
na mikutano ya vyama vya siasa, Tume inashauri kwamba, pande zote mbili
ziheshimu Mahakama na ziache kutoa matamko ambayo yanaendelea kuongeza joto
kuhusu uwepo au kutokuwepo maandamano na mikutano ya tarehe 1 Septemba, 2016.
(v)
Tume inaishauri CHADEMA
kusitisha maandamano yake ili kutoa nafasi kwa Mahakama kufanya kazi yake kwa
umakini bila shinikizo la muda kati ya sasa na tarehe 1 Septemba, 2016.
Iwapo
ushauri huu hautazingatiwa, Tume inatahadharisha kwamba kuna uwezekano mkubwa wa
kuwepo na uvunjifu wa haki za binadamu na iwapo itatokea hivyo wahusika wote
pia itabidi wawajibike.
Imetolewa na:
(SIGNED)
Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Agosti 10, 2016
COMMENTS