Kiongozi wa Jumuiya ya Mabohora Duniani,Dk Seydna Mufaddal Saifuddin mwenye kilemba kichwani  akiwasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma leo ambapo anatarajia kufanya ziara ya siku 14 nchini.

KIONGOZI wa Jumuiya ya Mabohora Duniani, Dk Syedna Mufaddal Saifuddin amesema wataendelea kusaidia Tanzania kutokana na kuridhishwa na utendaji kazi wa serikali ya Awamu ya Tano ambayo inaendelea kuhakikisha nchi inakuwa na amani.
Pia alitangaza mkutano mkuu wa dunia wa jumuiya hiyo utafanyika Jijini Dar es Salaam, Oktoba mwaka huu.
Alisema hayo leo mjini hapa wakati alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Dodoma kwa ziara ya siku 14 nchini ambako alipokewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana na viongozi mbalimbali wa Jumuiya ya Waislamu Tanzania (BAKWATA) wakiongozwa na Mufti wa Tanzania, Shehe Mkuu Abubakar bin Zubeiry.
Kiongozi huyo wa Mabohora Duniani alisema Tanzania ni moja ya nchi za kujivunia kutokana na amani iliyopo na kama Jumuiya wataendelea kusaidia nchi katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu.
“Nitaendelea kuhimiza jumuiya yetu iendelee kutoa misaada kwa ajili ya kuboresha elimu nchini,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Msaidizi wa Jumuiya ya Mabohora Mkoa wa Dar es Salaam, Zainuddin Adamjee alisema wamepata faraja kubwa kuona baada ya miaka 43 Rais Magufuli anatamka serikali kuhamia Dodoma katika kutimiza azma ya Rais wa Kwanza, Julius Nyerere aliyetangaza serikali kuhamia Dodoma mwaka 1973. Alisema sasa Dodoma mpya inakwenda kujengwa.
Naye Mufti Zubeiry lisema misingi ya watanzania imejengeka katika kuwapokea wageni na kuwakirimu. Alisema ziara hiyo itakuwa ni fursa nzuri kujifunza mambo mbalimbali.
Source:  Sifa Lubasi, Dodoma

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO