MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (MNEC) Livingstone Lusinde,pichani, amemshangaa aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Uchaguzi Mkuu uliopita Edward Lowassa kwa kupotosha jamii kwamba Spika wa Bunge Job Ndugai ni bora kuliko Naibu wake Dk Tulia Akson.

Aliyasema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma na kubainisha kuwa anachofanya Lowassa ni kuwaaminisha  uongo wananchi,  suala  ambalo alisema linatakiwa kukemewa.

Alisema Lowassa alikwenda kumsalimia Spika Ndugai akiwa na nia ya kumpa pole na si kumbebesha mzigo wa kushughulikia matatizo ya wabunge wa Ukawa kutoka bungeni na  kuwaaminisha wananchi kuwa kama Spika Ndugai angekuwepo kuongoza vikao vya Bunge, wapinzani wasingetoka nje.

"Ningeshauri badala ya kumtwisha kazi Ndugai wangempa pole kutokana na ugonjwa na si kumbebesha mzigo wa matatizo yao kwani walitoka bungeni kwa ridhaa yao.

"Uzushi wa Lowassa ni mbaya. Anazungumza vitu vya ajabu eti kama Spika Ndugai angekuwepo kwenye Bunge wapinzani wasingetoka nje. Wapinzani wamekuwa wakitoka nje ya vikao vya Bunge tangu Samuel Sitta akiwa Spika,” alisema.

Lusinde ambaye ni Mbunge wa Mtera (CCM) alisema siasa za kufitinisha viongozi sasa hazitakiwi na kuongeza; "Ndugai ni Spika anayetokana na CCM, tumezoea kuona Ukawa wakitoka Bungeni si mara ya kwanza kufanya hivyo."

Pia alisema ameshangazwa na kitendo cha Ukawa kutoa masharti ya kurudi Bungeni na kusema hiyo ni mbinu yao ya kuhakikisha wanaingia Bungeni katika Bunge lijalo.

"Ng'ombe zinamsubiri kule Monduli akachunge, maana  alishawahi kuhojiwa kama akishindwa urais atafanya kazi gani akasema ataenda kuchunga ng’ombe."

Alimtaka Lowassa kumuacha  Rais John Magufuli afanye kazi yake kwa utulivu kwani alishinda kwenye Uchaguzi Mkuu na kupewa ridhaa ya kutekeleza Ilani ya CCM.Alisema pia kuwa operesheni mbalimbali zinazoanzishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hazina tija yoyote.

"Miaka ya nyuma walianzisha Operesheni Sangara, baada ya kubaini haina tija wakaanzisha M4C walipogundua ina maana ya Magufuli For Change wakaamua kuiacha," alisema.

Alisema ingekuwa jambo la maana kama wangeanzisha kampeni ya msingi badala ya Ukuta na kwamba Ukuta ukijengwa bila msingi utaanguka tu.

"Wanasiasa wa matukio wananchi wasiwaunge mkono, wamuunge mkono Rais Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii," alisema.


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO