TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jumbe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kufuatia kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na pia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Aboud Jumbe Mwinyi kilichotokea leo tarehe 14 Agosti, 2016 Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Aboud Jumbe Mwinyi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Mwaka 1972 hadi 1984.
Kufuatia kifo hicho Rais Magufuli amesema Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye alijitoa kupigania Uhuru, Umoja, Haki na Maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika kipindi kigumu ambacho Taifa lilikipitia.
"Nimeshitushwa sana na kifo cha Mzee wetu Mhe. Aboud Jumbe, kwa hakika Tanzania imepoteza mtu muhimu ambaye katika kipindi cha uongozi wake alitoa mchango mkubwa wa kuipigania na kuijenga Tanzania tunayoiona leo" Amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli ameendelea "Kupitia kwako Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein napenda kuwapa pole familia ya Marehemu, Ndugu, Jamaa na Marafiki wote, Wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote kwa ujumla kwa kufikwa na msiba huu mkubwa"
Rais Magufuli amemuombea marehemu Aboud Jumbe Mwinyi apumzike mahali pema peponi.
Nayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza kusikitishwa kwake na kifo cha aliyekuwa rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi kilichotokea nyumbani kwake Mji mwema Dar-es-Salaama. 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waziri wa nchi Ofisi ya Makamo wa pili wa rais Mohamed Aboud , SMZ inaukumbuka mchango mkubwa wa hayati Jumbe katika kipindi cha uongozi wake wa miaka 13. 
'Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesikitishwa na kifo cha hayati Alhaji Aboud Jumbe ambaye alikuwa rais wa Zanzibar kwa muda wa miaka 13 huku mchango wake mkubwa katika kukuza na kuimarisha demokrasia ukibakia kielelezo kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla'alisema. 
Kwa mujibu wa taarifa za kutoka kwa familia ya hayati Jumbe mazishi yake yanatazamiwa kufanyika kesho mchana hapo nyumbani kwake Migombani nje kidogo ya mji wa Zanzibar eneo ambalo watoto wake watatu wamezikwa hapo. 
Jumbe alishika madaraka ya kuongoza Zanzibar katika mwaka 1972 mara baada ya kuuwawa kwa aliyekuwa rais wa kwanza wa Zanzibar hayati Abeid Amani Karume ambapo baraza la mapinduzi kwa kauli moja lilimchaguwa kushika wadhifa huo wa rais wa Zanzibar. 
Kufuatia kuchafuka kwa hali ya kisiasa Zanzibar katika mwaka 1984 Jumbe alilazimika kujiuzulu pamoja na viongozi wengine akiwemo waziri kiongozi Ramadhan Haji Faki na hivyo kupoteza nyadhfa zote ikiwemo makamo wa rais wa muungano na makamo mwenyekiti wa chama cha mapinduzi. 
Alhaji Aoud Jumbe Mwinyi atakumbukwa kwa mambo mengi akiwa ni mmoja ya viongozi walioshirikiana na baba wa taifa mwalimu Nyerere kuzaliwa kwa chama  cha mapinduzi CCM hapo mwaka 1977 katika uwanja wa Amaan Zanzibar. 
Kabla ya kuzaliwa kwa CCM Jumbe alikuwa rais wa chama cha ASP ambapo ushawishi mkubwa wa hayati Jumbe ndiyo uliosababisha kuunganishwa kwa vyama hivyo na kuzaliwa kwa CCM ikiwa ni moja ya juhudi za kuimarisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar. 
Nacho Chama cha Mapinduzi Zanzibar kimearifu kusikitishwa na kifo cha mmoja ya viongozi wake ambaye alikuwa Makamo Mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho Aboud Jumbe Mwinyi. 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na naibu katibu mkuu wa chama cha Mapinduzi Zanzibar Vuai Ali Vuai alisema mchango wa hayati Jumbe katika chama cha Mapinduzi hautosahaulika ambapo yeye kwa kushirikiana na baba wa taifa mwalimu Nyerere walihakikisha kinazaliwa chama chenye nguvu katika Jamhuri ya Muungano hapo mwaka 1977. 
'Chama cha mapinduzi kinatoa masikitiko yake makubwa kufuatia msiba mkubwa wa aliyekuwa makamo mwenyekiti wake wa kwanza hayati Aboud Jumbe Mwinyi........mchango wa Jumbe hautosahaulika katika chama cha Mapinduzi'alisema. 
Alisema Jumbe alihakikisha kinazaliwa chama kipya kitakachokuwa na nguvu pamoja na sura ya Muungano kwa ajili ya faida ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania'alisema. 
Alisema tangu kuzaliwa kwa chama hicho,kimeendelea kupata mafanikio makubwa ikiwemo kushinda katika chaguzi zote kuanzia za mfumo wa chama kimoja hadi vyama vingi. 
Aidha chama hicho kimeendelea kuwa imara bila ya kuyumba na kuendelea kushika hatamu ya kuongoza dola katika kipindi chote kuanzia mwaka 1977 hadi leo. 
'Mafanikio yote ya chama cha mapinduzi hatuna budi kukumbuka juhudi zilizofanywa na hayati Jumbe kwa sababu ndie aliyekiunganisha chama hicho kutoka ASP na TANU na kuzaliwa CCM'alisem Vuai. 
Aidha Vuai alisema katika kuimarisha demokrasia na sauti za wananchi kusikika,Jumbe alianzisha chombo cha kutunga sheria ambacho alikiita baraza la wawakilishi. 
Baraza la wawakilishi liliasisiwa katika mwaka 1979 kwa kuanzia viongozi kutoka katika wilaya za Unguja na Pemba kwa kuzishirikisha jumuiya za chama ikiwemo umoja wa vijana,wazazi ushirika na Umoja wa wanawake UWT. 
'Huo ndiyo mchango mkubwa wa hayati Jumbe katika kuanzisha chombo cha Baraza la Wawakilishi ambalo aliliita ngome ya wananchi katika kusikiliza maoni yao kusikika'alisema.
Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO