Mkuu wa Mkoa wa wa Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe (Kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya Nane Nane katika uwanja wa maonyesho ya kilimo Nzuguni Mkoani Dodoma


Ufunguzi wa siku kuu ya wakulima Nane nane Kanda ya kati Dodoma mwaka 2016 umefanyika leo katika Uwanja wa Maonyesho ya kilimo Nzuguni Mkoani Dodoma huku kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni "Kilimo, Ufugaji na Uvuvi ni nguzo ya maendeleo, Kijana shiriki kikamilifu (Hapa Kazi Tu).
Maonyesho haya yanahusisha shughuli za wakulima, wafugaji wa mifugo, wafugaji wa nyuki, wavuvi, wanamazingira, wasindikaji wa bidhaa za mazao ya kilimo na mifugo, wizara taasisi/makampuni ya umma, makampuni binafsi, mabenki, taasisi za umma na za binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Akizungumza katika ufunguzi huo Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe amesema kuwa sekta ya kilimo bado ni mhimili wa uchumi wa Tanzania kwa sababu inaajiri zaidi ya asilimia takribani 80 ya watanzania na kwa kuzingatia malengo ya maendeleo ya Taifa ya kuwa nchi yenye uchumi wa kati unaotegemea viwanda hivyo kilimo kikiboreshwa viwanda vitapata malighafi ya uhakika na kuimarisha masoko kwa wakulima hivyo kuwepo na ajira ya kuaminika kwa vijana na watanzania kwa ujumla.
Viongozi wa Mkoa wa Dodoma na Singida wakitembelea baadhi ya vibanda vya maonyesho wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Nane Nane

Mgeni rasmi akisikiliza kwa kina maelezo juu ya matumizi ya matrekta kwa ajili ya kilimo

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akiwasalimu wananchi wakati wa ufunguzi wa maonyesho hayo

Baadhi ya Wakuu wa Wilaya za Dodoma na Singida wakiongozwa na Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Singida Mathew Mtigumwe wakikagua eneo la maonyesho ya mboga mboga

Mgeni rasmi alipotembelea banda la dawa za kilimo, uvuvi na ufugaji Farmer Centre and Farm base

 
Baadhi ya Wakuu wa Wilaya za Dodoma na Singida wakiongozwa na Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Singida Mathew Mtigumwe wakikagua eneo la maonyesho ya bwawa la samaki lenye samaki aina ya perege, kambare na kamongo liloandaliwa na Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba

Rc Mtigumwe amesema kuwa wastani wa ukuaji wa sekta ya kilimo unabadilika mwaka hadi mwaka kutokana na kilimo kwa kiwango kikubwa kutegemea mvua ambazo zimekuwa zikinyesha kwa viwango na mtawanyiko unaotofautiana kila mwaka ambapo kwa mwaka 2010 sekta ya kilimo ilikuwa kwa asilimia 4 ikilinganishwa na asilimia 6.5 ya mwaka 2015.
"Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa kanda ya kati ina rasilimali ya maji yakutosha ya chini ya ardhi hivyo kuendelea kuitamka kama kanda kame hakuna usahihi wa jambo hilo ipo haja ya kuona kuwa rasilimali hiyo inapatikana kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji hivyo kupunguza kilimo cha kutegemea mvua" Alisema Mtigumwe
Mkuu huyo wa Mkoa wa Singida kabla ya kuwahutubia wananchi waliojitokeza katika ufunguzi huo alitembelea baadhi ya mabanda ya maonesho na kuona shughuli mbalimbali za uzalishaji wa mazao, ufugaji, uvuvi, usindikaji na wauzaji wa zana na pembejeo za kilimo ambapo amejionea matokeo ya juhudi mbalimbali zilizofanywa na serikali ya awamu ya tano katika kuinua ukuaji wa sekta ya kilimo ambapo juhudi hizo zinajumuisha uzalishaji wa mbegu mbalimbali zinazostahimili hali ya hewa ya maeneo ya kanda ya kati.
"Natoa wito maalumu kwa wakulima, wafugaji, wavuvi, wajasiriamali na wadau wa sekta zingine kuhakikisha kuwa bidhaa zenu zinafikia ubora wa hali ya juu kuanzia shambani zinakozalishwa, zinakosindikwa na kuhifadhiwa na hadi kumfikia mlaji, ikumbukwe kwamba kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu kutawezesha bidhaa zetu kuhimili ushindani wa hapa nchini na nje ya nchi na kuuzwa kwa bei nzuri" Alisema Mtigumwe
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya waandaaji wa maonyesho ya Kilimo, Mifugo na sherehe za nane nane, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Miraji Jumanne Mtaturu amesema kuwa hotuba ya Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Singida itakuwa ya mazingatio ili kurahisisha na kuendeleza kasi ya serikali ya awamu ya Tano kwa vitendo hususani katika kuakisi na kuwasaidia wananchi ambao ni wakulima na wafugaji kupata mbinu bora za kufuga na kulima kisasa ili kupata mazao kwa wingi.
Hata hivyo Dc Mtaturu amesema kuwa ana imani thabiti kuwa baada ya kumalizika kwa maonyesho hayo wakulima, wafugaji na wananchi washiriki watakuwa wamejifunza vyema mbinu bora za kukabiliana na changamoto za kilimo na ufugaji hivyo kujikita zaidi katika mbinu bora na za kisasa za kilimo na ufugaji pia.
Dc Mtaturu amesema kuwa shughuli kuu ya wakazi wa kanda ya kati inayoundwa na mikoa miwili ya Singida na Dodoma yenye jumla ya Wilaya kumi na mbili na Halmashauri 15 shughuli zao kuu ni kilimo na ufugaji.
Source: Mathias Canal, Dodoma


Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO