Mkurugenzi
wa Huduma za Kinga wa Wizara hiyo Dk. Neema Rusimabayila akitoa ufafanuzi
kuhusu Chanjo ya Homa ya Manjano na vitendo vya baadhi ya watumishi wa afya wasiowaaminifu ambao hulipwa fedha ili waweze kuwatengenezea
wasafiri kadi za Chanjo ya Homa ya Manjano na kisha kuzitumia nje ya nchi jambo
ambalo kinyume cha sheria na hatari kwa
usalama wa Afya zao.
Aron Msigwa - Dar es Salaam.
Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewatahadharisha wananchi
wanaopanga kusafiri kwenda nje ya nchi kuhakikisha kuwa wanafika katika vituo
vya afya na kuchanjwa chanjo ya kuzuia maambukizi ya Homa ya Manjano badala ya kuwalipa
fedha baadhi ya watumishi wa afya wasio waaminifu ili wawatengenezee kadi za chanjo kinyume
cha sheria.
Mkurugenzi wa Huduma za
Kinga wa Wizara hiyo Dk. Neema Rusimabayila akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo
leo jijini Dar es salaam amesema baadhi ya wasafiri wamekuwa wakishirikiana na watumishi
wa afya wasiowaaminifu kwa kuwalipa fedha ili waweze
kuwatengenezea kadi hizo na kisha kuzitumia nje ya nchi jambo ambalo ni hatari
kwa usalama wa Afya zao.
“Kumekuwa na baadhi ya
watumishi wasio waaminifu ambao hupokea fedha na kisha kutengenezesha kadi za wasafiri
zinazoonesha kuwa wamepatiwa chanjo, Jambo hili ni hatari kwa afya ya msafiri, sasa
tunaona mlipuko wa ugonjwa huu ukitokea katika nchi za karibu ni muhimu mtu
kuchanja ili kuepuka kuwa chanzo cha kuleta ugonjwa huu” Amesisitiza Dk.Neema.
Amesema ni jambo lisilokubalika
kwa msafiri kubeba kadi ya chanjo ya Kinga ya Homa ya Manjano ili hali akijua kabisa hajachanjwa chanjo hiyo na kuongeza kuwa jambo hilo linamuweka muhusika katika hatari ya kupata
maambukizi akisafiri kwenye nchi zenye mlipuko wa ugonjwa huo.
“Napenda kusisitiza kuwa
ni muhimu sana msafiri akachanjwa chanjo hii kwa ajili ya kinga ya afya yake
mwenyewe, kupata kadi bila kuchanjwa na kwenda mahali ambapo kuna ugonjwa huu ni
kujidanganya, epuka kuwa chanzo cha kusambaza ugonjwa huu” Amesisitiza Dk.
Neema.
Kuhusu gharama za
chanjo hiyo amesema kuwa msafiri anayetaka kupata chanjo hiyo anatakiwa kulipia
gharama ya Elfu Ishirini (20,000/=) ikiwa ni malipo halali ya Serikali na
mlipaji hupatiwa stakabadhi halali.
Aidha, amesema mbali na
hatua zinazochukuliwa kudhibiti hali hiyo, Wizara inakamilisha utaratibu wa
kuwa na kadi maalum ambazo zitakuwa tofauti, zenye nembo maalum ambazo mtu hataweza
kughushi wala kufanya udanganyifu wa aina yoyote.
Post a Comment
Post a Comment