Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya shilingi milioni 100 kutoka kwa Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya Caspian, Bw. Omid  Karambeck 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea msaada wa sh. milioni 121.679 ili kusaidia wananchi waliothirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera, Jumamosi, Septemba 10, 2016 na kusababisha vifo vya watu 17.
Msaada huo umetolewa leo (Ijumaa, Septemba 16, 2016) na wadau mbalimbali wakiwemo Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya Caspian, Bw. Omid Karambech aliyetoa sh. milioni 100.
 Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bordar Limited, Bw. Wu Yahui aliyetoa sh. milioni 20 pamoja na Bi. Mariam Kitembe aliyetoa sh. milioni 1.679 kwa niaba ya Wauguzi walioshiriki mafunzo ya Utafiti wa viashiria na matokeo ya ukimwi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
 Akipokea msaada huo katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma, Waziri Mkuu amewashukuru kwa michango yao ya fedha na kuwaomba wananchi wengine wajitokeze kwa wingi ili kuwasaidia watu walioathirika na tetemeko hilo ambalo ni kubwa na halijawahi kutokea nchini.
 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimshukuru, Mkurugenzi Mtendaji wa Kapuni ya Border Limited, Bw. Wu Yahui baada ya kupokea shilingi milioni 20 

 Jumapili, Septemba 11, mwaka huu, Waziri Mkuu alifanya ziara mkoani Kagera ili kuwapa pole waathirika wa tetemeko hilo pamoja na kujionea madhara yaliyojitokeza.
 Pia aliongoza maelfu ya wananchi wa Manispaa ya Bukoba kuaga miili ya watu 16 waliofariki kutokana na tetemeko hilo. Aliwaomba wananchi wawe watulivu na kuwaahidi kuwa Serikali itakuwa pamoja nao.
 Jumanne, Septemba 13 mwaka huu Waziri Mkuu aliongoza hharambee ya kuchangia waathirika wa teteme hilo na kupokea zaidi ya sh. bilioni 1.4 kutoka kwa mabalozi wa nchi za nje nchini Tanzania na Jumuia ya Wafanyabiashara wa Kitanzania.
 Mbali na kusababisha vifo, watu wengine 253 walijeruhiwa na maelfu ya wananchi walikosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264 zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA, SEPTEMBA 16, 2016

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO