Balozi wa Anwani za Makazi Duniani Prof. Anna Tibaijuka akiongea akimkabidhi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa anwani ya makazi wakati wa wa hafla ya uzinduzi wa Mwongozo wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Mwogozo wa Postikodi katika ukumbi wa Pius Msekwa Bungeni Mjini Dodoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameziagiza halmashauri zote nchini kutekeleza mpango kazi wa anwani za Makazi na Postikodi kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wananchi. 
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo leo kabla ya kuzindua Mwongozo wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Mwongozo wa Postikodi uliofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa uliopo ndani ya viwanja vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dodoma.

“Nikizingatia hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali katika kuweka mazingira ya utekelezaji wa anwani za makazi, naagiza halmashauri zote nchini kuzifanyia kazi changamoto ambazo hazihitaji fedha ama ambazo hazihitaji gharama kubwa” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu amebainisha baadhi ya changamoto ambazo hazihitaji gharama kuwa ni pamoja na kuhakikisha barabara na mitaa yote inakuwa na majina yaliyorasimishwa na wananchi wenyewe, kudhibiti mipango miji dhaifu na ujenzi holela, kuwa na takwimu za idadi ya barabara na mitaa na nyumba katika kila kata na kuwa na taarifa za wakazi katika kila kata.

Changamoto nyingine zisizohitaji gharama kubwa ni kujengea uelewa wadau na wananchi kuujua na kuwa mfumo huo, kuimarisha matumizi ya daftari la wakazi ambapo taarifa za utekelezaji wa kazi hizo Waziri Mkuu ameagiza ziwasilishwe Ofisi ya Rais TAMISEMI kabla ama ifikapo mwezi Desemba, 2016.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa kufuatia nia ya Serikali kuhamia Dodoma, manispaa ya Dodoma na halmashauri ya Chamwino zipewe kipaumbele cha utekelezaji ili kuweka mazingira mazuri ya kuishi na kufanya kazi.

“Utekelezaji wa Mpango katika Manispaa ya Dodoma na Halmashauri ya Chamwino ukamilike kabla ama ifikapo mwezi Desemba, 2016 na kuhakikisha utekelezaji huo kukamilika kwa wakati” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Kwa upande mwingine Waziri Mkuu amezitaka wizara za Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Manispaa ya Dodoma, Halmashauri ya Chamwino, CDA; TCRA na TPC zishirikiane ipasavyo katika kukamilisha mpango wa anwani katika mkoa huo.

Mbali na hayo, Waziri Mkuu amezitaka taasisi za TANROADS, TBA, NHC, Mipango Mji na Mradi wa Kuboresha Miji (TSC) zinapoandaa mipango hususan mipango ya miundombinu na makazi, ziainishe pia anwani za makazi kwa kushirikiana na Halmashauri katika maeneo husika.

Katika kufanikisha hilo, Waziri Mkuu amezitaka Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Wizara ya Unjenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, TCRA na TPC kushiriki ipasavyo katika utekelezaji wa mpango hususan katika kujenga uelewa na uwezo kwa viongozi na watendaji  wa halmashauri ili waweze kutekeleza mpango huo ipasavyo.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa George Simbachawene amesema kuwa Mpango huo umefanyiwa majaribio katika majiji mawili ya Dar es salaam na Arusha pamoja na manispaa za Dodoma na Zanzibar.

Waziri Simbachawene aliongeza kuwa ili kuwa na Tanzania ya kisasa, anwani za makazi ni kigezo muhimu cha kuzingatiwa katika kundeleza majiji, manispaa, halmashauri, kata na hata mitaa ambayo ndio inajenga taswira ya nchi.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema kuwa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi una manufaa mengi ambao utarahisisha ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo mbalimbali nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema hayo leo mjini Dodoma wakati alipokuwa akizindua Mwongozo wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Mwongozo wa Postikodi ambao utatumika nchi nzima.
“Kama kila mlipa kodi tutamfahamu kwa uhakika anaishi wapi,   tutamutoza kodi stahiki na hili ni jambo muhimu la utawala bora” amefafanua Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa uwepo wa anwani ya makazi nchini utasaidia kurahisisha ukusanyaji wa mapato mbalimbali ikiwa ni jukumu muhimu la utawala bora.
Aidha, amesema kuwa mfumo huo wa anwani za makazi utaiwezesha  Serikali kuwahudumia wananchi wake kirahisi ikiwa ni pamoja na kutoa ulinzi, kurahisisha mawasiliano miongoni mwa wananchi na Serikali.
Vile vile mfumo huo utasaidia kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utoaji huduma za kijamii, huduma za kibiashara, huduma za dharura na uokoaji, kurahisisha sensa, kuboresha daftari la wapiga kura, kuboresha huduma za posta na kuwezesha utoaji wa biashara mtandao.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa katika nchi nyingi za viwanda na nchi zilizoendelea suala la miundombinu ikiwemo Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi ni muhimu na linaeleweka kwa kila mtu katika kuanzisha, kukuza na kuendeleza uchumi wa viwanda.
“Kwa kutumia mfumo huu, viwanda viwe vikubwa au vidogo vinatambulika viko wapi kwa anwani zao za makazi na hivyo kuweza  kupima kirahisi ukuaji wa viwanda” alifafanua Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amesisitiza taasisi zote za umma na zile za binafsi zianze kutumia anwani za makazi na postikodi ili kuchochea kasi ya maendeleo ya nchi ikiwa ni pamoja na kutumia katika makusanyo ya mapato.
Waziri Mkuu Majaliwa amewasisistiza wadau wote nchini kuzingatia kuwa na anwani ni haki ya kila mtu na pia kupata huduma za msingi kupitia mfumo huo ni haki ya kila mtu.

Aidha, dhana ya kuwa “dunia ni kijiji” inapaswa kuwa chachu ya kupata huduma zote mahali ulipo, inahitaji juhudi za makusudi za kuhakikisha Tanzania imekuwa sehemu ya kijiji hicho na inakuwa ni moja ya mataifa kinara wa kutoa huduma mbalimbali kwa ufanisi kwa kutumia Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi.
Kwa upande wake Balozi wa Anwani za Makazi Duniani Prof. Anna Tibaijuka amesema kuwa anajivunia mradi huo kutekelezwa nchini ambao utasaidia kuonesha watu mahali wanapoishi ambapo Tanzania imefanikiwa kuwa na anwani za makazi nchi nzima licha ya changamoto ya  kuwa na miji mingi ambayo haijapangwa.
Zao la anwani za makazi linatokana na Umoja wa Posta Dunia (UPU) iliyopitishwa katika mkutano mkuu wa 25 uliofanyika mjini Doha, Qatar mwaka 2012 ambao ulipitisha azimio la kuzitaka nchi zote duniani kuhakikisha kuwa kila mtu anakuwa na anwani.
Source:Beatrice Lyimo na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Dodoma

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO