Mkhosi woMhlanga au  Zulu Reed Dance


UNAWEZA kuliita tamasha la  mafunjo . Nasema hivyo kwa kuwa ishara kuu iliyomo katika  tamasha hilo ni kitendo cha ukataji wa matete na kuyawasilisha kwa mfalme. Kila binti hufika kwa mfalme na tete lake.
Shughuli hii ambayo inalenga kuwaingiza mabinti wa kizulu katika hatua nyingine ya makuzi(ya kuwa mama ) hufanywa kwa siku kadhaa na uwasilishaji wa matete kwa mfalme ni moja tu ya tukio.
Mkhosi woMhlanga au  Zulu Reed Dance ni tamasha la kitamaduni ambapo mabinti hawa hujitoa kuheshimu utamaduni wao wenye lengo la kukamilisha maandalizi ya kuwa mama katika jamii.
Na kuna masimulizi ya kale yasemayo kwamba binti anayeenda kushiriki dansi hili wakati yeye si bikira, tete lake huvunjika.lakini pia mabinti huwa waangalifu sana wakati wa kuchagua matete, huchagua yaliyo imara na ambayo yamewapita kimo.
Shughuli nzima huchukua siku kadhaa ambamo kunakuwa na uimbaji, uchezaji ngoma na shughuli nyingine zilizolenga kumuingiza binti wa kizulu katika maisha ya umama.
Mabinti wanaofika katika shughuli hii inayoheshimika huwa katika mavazi ya asili ya Kizulu na watu wazima huwafunza mambo kadhaa yanayohusu kabila lao na namna ya kujiheshimu na kutunza miili yao hadi watakapoolewa.


Mkhosi woMhlanga au  Zulu Reed Dance,  ni utamaduni wenye miongo kadhaa na hufanyika mwezi Septemba wakati wa mwanzo wa majira ya mchepuo katika kasri la mfalme la eNyokeni huko Nongoma, Zululand.
Pamoja na kuwa tamasha lenye kurithisha utamaduni, pia hutumika kujadili masuala ya sasa kama maambukizi ya ukimwi na mimba za utotoni.
Safari ya utoaji wa mafunjo huongozwa na binti mfalme wa kabila la Zulu . Wakati wakienda huko mabinti hawa, kwa mgeni atakuwa anapendezwa na rangi mbalimbali za mavazi ya mabinti hasa shanga zao na wanaume nao hushiriki katika safari ya kumsalimia mfalme kwa aina yake wakiimba na huku wakipiga jalamba kama wako katika mapigano.
Kwa mujibu wa utamaduni wa Kizulu mababu na mabibi zao  walizaliwa kutoka katika kitanda cha mafunjo kwa hiyo kitendo chao cha kulaza matete mbele ya mfalme ni ishara ya kuheshimu utamaduni wao. Matete hayo pia hutumika kutengeneza nyumba za asili za Wazulu, mikeka, vikapu  shughuli ambazo zimewapa umaarufu mkubwa wazulu.


safari ya kwenda kwa  mfalme hujaa manjonjo

matete mtoni

Katika tamasha la mwaka huu ambalo ni la 32 Mfalme Goodwill Zwelithini  alitumia nafasi hiyo kuangalia mafanikio yaliyopatikana katika falme yake wakati anajiandaa kuadhimisha miaka 200 tangu mpiganaji Shaka Zulu kuanzisha taifa hilo.
Akihutubia  mabinti zaidi ya 30,000 na waheshimiwa wengine, Zwelithini aliapa kulinda utamaduni wa kabila hilo na kuwakumbusha watu wa Afrika Kusini kwamba hawawezi kuwa taifa wakiondoa uwapo wa kabila la Zulu na utamaduni wake uliojaa historia pana ya utaifa.
Maadhimisho ya mwaka huu kilele chake kitafanyika Septemba 24 katika uwanja wa Moses Mabhida Stadium mjini Durban . Maadhimisho haya yalishawahi kufanyika KwaDukuza, manispaa ya Ilembe katika pwani ya KwaZulu-Natal.
Akizungumza Zwelithini alisema katika kukumbuka kuundwa kwa taifa la Wazulu watu wake ni lazima warejee katika utamaduni wa taifa hilo wa kuheshimu wakubwa na kuhifadhi utamaduni.
Mfalme huyo alisema kwamba heshima kwa wakubwa ilikuwa ni msingi mkubwa wa malezi ya watoto ili kutoa taifa ambalo linaheshimu mawazo ya wakubwa wake.
 
matete hutumika kuezeka na kujenga nyumba


mabinti hucheza ngoma

Aidha mfalme huyo alisema iko shida kwa vijana wa kiume na kusema ipo haja nao kuwa katika mfumo wa mafunzo ili kuwa na taifa linaloheshimu utu na pia kuzuia magonjwa.
Alisema alipoanzisha  tamasha hilo miaka ya 1991 alikuwa amedhamiria kukabiliana na mabadiliko ya vijana katika usasa wao na kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi kwa kuhimiza kutongonoana mpaka siku ya harusi.
Alisema kelele zinazofanywa sasa na wizara ya jinsia zinaonesha pia ni kwa namna gani hawajui utamaduni wa wazulu  na pia hawajui sababu ya kuwa na  kigezo cha kuwa binti bora, ubikira. Suala la ubikira linachukulikwa na wizara hiyo kama kuingilia uhuru binafsi wa mwanamke.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO