MOTO mkubwa umeteketeza bweni linalokaliwa na wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari ya  Mwanzi iliyopo Manyoni mkoani Singida.
Moto huo ulioanza saa mbili usiku wa kuamkia leo umeteketeza kila kitu cha wanafunzi hao ambao walikuwa madarasani wakijiandaa na mitihani yao ya kawaida ya ndani.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Jane Lubasi  akizungumza kwa njia ya simu kutoka Manyoni alikiri kutokea kwa janga hili na kusema kwamba wanafunzi hao kwa sasa wanafanyiwa mpango wa kurejea nyumbani na watamaliza mitihani yao baadae.
Alisema aliitwa na mlinzi wa shule usiku wa saa mbili na juhudi za kuzima moto huo kwa kutumia maji na mchanga zilishindikana.
Aidha alisema kama gari la zimamoto lingefika mapema huenda wangefanikiwa kuokoa bweni hilo lenye sehemu tatu. Gari hilo lilifika hapo saa mbili baada ya kuitwa likitokea Singida mjini.
Alisema kwamba watoto hao kwa sasa hawana chochote na kwamba wanahitaji kusaidiwa hata nauli za kurejea kwao.
 
Mwalimu Jane
Alisema kwamba serikali imeshafikisha msaada wa magodoro na kwamba chanzo cha moto huo bado kujulikana ingawa inaaminika kwamba inatokana na hitilafu ya umeme.
" Tayari kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa imefika, tumepewa magodoro, mashuka, blanketi na vifaa vya usafi Walau vya kuanzia, wadau wengine wanaendelea kutusaidia." alisema Jane.
Alisema kutokana na mazingira yalivyokuwa, inafaa kila halmashauri ya mji wa Manyoni kuwa na gari lake na kuzima moto kwani mwendo wa gari hilo kutoka Singida hadi hapo ilikuwa moto umeshalamba kila kitu kutokana na upepo mkali ulivyokuwa ukivuma.
Jane alisema kwamba kwa siku ya leo kumekuwa na  mikutano mingi ambayo ilikuwa inaangalia mambo mengi yanayohusu kadhia hiyo.
Juhudi za kumpata kamanda wa Polisi mkoa wa Singida  kuzungumzia moto huo haikuweza kufanikiwa.Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO