Gavin Van Wijk


Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI wa Ufundi wa TBL Group na viwanda vya SABMiller Kanda ya
Afrika Mashariki, Gavin Van Wijk ambaye pia ni mtaalamu aliyebobea
katika masuala ya viwanda, amesema mkakati wa Serikali ya Awamu ya
Tano wa kuifanya Tanzania nchi ya viwanda unatekelezeka na unatarajiwa
kuleta  maendeleo makubwa kwa nchi.

Hata hivyo, alisema kinachotakiwa kufanyika kwa haraka ni kujifunza
kutoka nchi zilizofanikiwa  katika sekta ya viwanda na kutumia mifumo
ya uendeshaji viwanda  kwa tija na ufanisi inayotumika katika nchi
hizo ambayo imeziwezesha   kuwa na viwanda imara.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Wijk  alisema  kampuni ya TBL
Group imeanza kuonesha njia kuwa Tanzania ya viwanda inawezekana
kutokana na viwanda vyake vya kutengeneza bia vilivyopo nchini kuwa
miongoni mwa viwanda bora vinavyoongoza Afrika kwenye mtandao wa
viwanda vilivyopo chini ya kampuni ya SABMiller.

“Kwa miaka sita mfululizo viwanda vya bia vya Tanzania vilivyopo chini
ya TBL Group vimekuwa vikishinda tuzo mbalimbali za ubora na kuwa
tishio kwa viwanda vingine Afrika na mwaka huu rekodi ya kiwanda bora
barani Afrika inashikiliwa na kiwanda cha TBL Mbeya  wakati nafasi ya
pili inashikiliwa na kiwanda cha Mwanza pia viwanda vya Arusha navyo
viko kwenye nafasi za juu na bidhaa zinazotengenezwa na viwanda, hivi
ni tishio katika masoko ya kimataifa”.Alisema.

Alisema siri ya mafanikio hayo ni kuhakikisha mifumo ya kampuni ya
uzalishaji wenye tija inafuatwa  na  matokeo yake ni kupatikana kwa
uzalishaji wenye tija na viwango vya kimataifa.

Aliongeza kuwa, inafurahisha kuona Watanzania wapo makini kujifunza
Programu mbalimbali za kuleta ufanisi na kuzitekeleza kwa umakini
mkubwa na kuwa  viwanda vya TBL Group ambavyo vinazidi kuwa tishio kwa
ubora Afrika na sehemu nyinginezo duniani  vinaongozwa na Watanzania
na wafanyakazi katika viwanda hivyo ni Watanzania wenyewe.

Alisema mafanikio mengine kwa viwanda hivyo yanatokana pia na
uwekezaji unaofanyika kila mwaka kwenye mitambo na vitendea kazi vya
kisasa ambapo kampuni inatumia zaidi ya dola milioni 14 (sh bilioni
28), uwekezaji unaokwenda sambamba na kuwekeza kwa mafunzo ya
wafanyakazi ili waweze kuitumia kuleta ufanisi.

Pamoja na mafanikio katika uzalishaji, alisema kampuni inatekeleza
malengo ya SABMiller ya ustawishaji jamii na kuleta maendeleo endelevu
ambayo yanashabihiana na malengo ya Umoja wa Mataifa na utekelezaji
wake umeonesha kuleta manufaa katika sehemu zote ambako viwanda vya
kampuni  vipo.

Baadhi ya malengo aliyataja kuwa yamelenga kutunza mazingira na vyanzo
vya maji, kuwezesha wazalishaji wanaouzia kampuni malighafi, kuongeza
fursa za ajira za moja kwa moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

“Kampuni imepata mafanikio kwa kuwezesha wakulima wanaouzia malighafi
kupitia mpango unaojulikana kama Go Farming ambao unaendelea
kubadilisha maisha ya wakulima kuwa bora. Tumeanza na wakulima wa
Shayiri na Zabibu  na tutahakikisha mpango huu unawafikia wakulima
wengi zaidi nchini,” alisisitiza Wijk aliyeongeza kuwa, mbali ya
mafanikio hayo, anaamini TBL Group itaendelea kuwa mlipa kodi bora,
mzalishaji bora, mwajiri bora na mshirika mkubwa wa maendeleo ya
Watanzania.

Post a Comment

Find Us On Facebook

TANGAZA NASI LEO